NJAMA
SURA YA TATU
Niiegesha gari langu kwenye maegesho ya Hoteli
ya New Afrika. Nikatelemka na kuzunguka ili
nimfungulie Veronika. Tuliingia New Afrika Hoteli
katika sehemu iitwayo duka la Kahawa tukatafuta
meza tukaa.
"Ulishastafutahi?", nilimuuliza Veronika.
"Kawaida yangu huwa ninastafutahi kabla ya
kufanya mazoezi kila siku, ili kujiweka katika hali
nzuri".
"Ndio sababu umbo lako linapendeza namna hiyo".
"Asante".
Mtumishi wa hoteli alifika na kutuuliza mahitaji
yetu.
"Mimi nitakunywa maji ya machungwa kama
yapo".Veronika alisema.
"Mimi niletee maji ya ndimu". niliagiza.
Alipoondoka mtumishi huyo nilimweleza Veronika
kuwa mimi nitakwenda mapokezi kumwita Sherriff,
ambaye niliamini alikuwa bado chumbani.
"Habari za leo Tom?", nilimsalimia kijana wa
mapokezi ambaye tunafahamiana vizuri sana.
"Aha mzee, shikamoo", alinisalimia.
"Marahaba", nilimjibu.
"Sijui nikusaidie nini mzee?".
"Kuna mgeni wangu hapa anaitwa Ahmed Sherriff,
alifika usiku".
"Ndio ndio, yuko yuko namba 406, unahitaji
kwenda huko au nimpigie simu".
"Mpigie simu nizungumze nae".
Alimpigia simu na alipompata akanipa.
"Hallo Sherriff habari za leo?".
"Ohoo, Willy salama?, nilikuwa ninakusubiri kwa
hamu".
"Oke, telemka chini. Tuko hapa duka la kahawa
pamoja na Veronika".
Oh, amekwisha wahi namna hii?".
"Sana tena".
"Oke nakuja sasa hivi".
"Haya tunakusubiri", nilimjibu na kukata simu.
"Oke Tom asante sana", nilimwambia kijana wa
mapokezi.
"Asante mzee karibu", alijibu Tom.
"Asante niko hapa duka la kahawa".
Niliporudi nilikuta vinywaji tayari.
"Yupo?", aliuliza Veronika.
"Yupo, anakuja sasa hivi", nilimjibu.
Haukupita muda Sherriff alitokea na kuja moja kwa moja mezani kwetu. Tulisalimiana akavuta
kiti na kuketi. Mtumishi aliyekuwa anatuhudumia alipomuona alikuja mara moja.
"Mzee nikusaidie nini?," alimuuliza Sherriff.
"Kuna maji ya nanasi?".
"Ndio, yapo".
"Haya niletee hayo, lakini weka barafu nyingi, maana si joto hili".
"Bila ya wasiwasi mzee".
Mtumishi alipoondoka tulikaa kimya tunatazamana kwanza kila mtu anashindwa kuanza
mazungumzo. Veronika aipoona hivi akatabasamu kisha akasema. Sherriff wewe kidogo uko nyuma
ya habari, lakini nitakueleza kwa kifupi ili kukuweka pamoja nasi katika habari zinazotuhusu
wote".
"Nitakushukuru", alijibu Sherriff.
"Willy nimemweleza yote tunayojua juu yake, na jambo la kushangaza ni kwamba na yeye
anatufahamu sisi huenda kuliko tunavyojifahamu wenyewe".
"Usitie chumvi", nilimuasa.
"Ala!", Sherriff alitamka kwa mshangao mkubwa. "Kama ni hivyo basi ni vizuri sana. Kwani
wote sasa tunafahamiana misimamo yetu. Unajua mimi nilishangaa sana usiku pale uwanja wa
ndege. Waandishi wote wengine wa magazeti mbali mbali ulimwenguni tuliokuja nao wamekataliwa
kuingia hapa nchini, na tumewaacha uwanja wa ndege wakilalamika vibaya sana wakiomba kuonana
na mabalozi wao, lakini sisi tumeruhusiwa kwa urahisi sana, kitu hiki kilinishangaza sana
nikahisi lazima huu utakuwa mpango wa Willy. Sasa nimeamini kabisa. Uongo au kweli".
Sherriff aliuliza huku akiniangalia.
"Bila shaka niliwaahidi toka tukiwa Freetown kuwa mnakaribishwa kwa dhati Tanzania, sasa
nimetimiza ahadi yangu".
"Asante sasa", Sherriff alijibu.
"Mimi naamini unajua tumekuja kwa ajili gani, na vile vile naamini likizo yako imekatishwa
kwa ajili sababu hiyo hiyo tuliyoijia sisi", Veronika aieleza huku macho yake yaking'aa
kuonesha kuwa sasa tulikuwa tunazungumza kikazi.
"Sawa, endelea", nilimjibu.
"Mimi naonelea tungeliungana na wewe, kwani wewe ukiwa mwenyeji itakuwa kazi rahisi kwetu
kuweza kupata habari. Sijui wewe unaonaje?".
"Kwa taarifa yenu lazima niwaeleze kuwa tukio hili lililotokea si la kawaida. Mnaweza kuwa
mmeshiriki katika mambo ya hatari sana kama vile mambo ya vita, lakini lazima
niwatahadharishe kuwa kutafuta habari za aina yoyote zinazoweza kufichua kundi lililofanya
ujahiri wa hari ya juu ni hatari sana kwa maisha yenu kuliko hatari yoyote mliyokwisaha
kuikabiri. Nadhani mmenielewa. Ningewaomba ili kuponya maisha yenu muwe watoto wazuri,
muachane kabisa na kuuliza uliza habari za tukio hili".
"Kabla hatujatoka ofisini kwetu London, tumetahadharishwa kama unavyotutahadharisha sasa,
lakini tulikaa tukaamua kuwa tutaendelea; Lolote baya litakalotupata tutakuwa tumetoa damu
yetu kwa ajili ya ndugu zetu. Kwani sisi tunaamini watu waliofanya kitendo hiki si watu
wengine bali ni mabeberu wapinga ukomboni wa kusini mwa Afrika", alijibu Sherriff kwa nia
moja.
"Kama uamuzi wenu ni huo basi tutashirikiana kwa kadiri tutakavyoweza".
"Mlikuwa na nia ya kuanza kutafuta habari tokea lini?".
"Tokea sasa hivi kama unaweza kutupa fununu tuanzie wapi!", Sherriff alijibu.
Kwa vile katika mpango wangu wa upelelezi nilikuwa nimepanga kuwatumia ndugu hawa. niifurahi
sana kuona kuwa mambo yaikuwa yanakwenda kama nilivyopanga. Hivyo niliamua kuwaeleza kwa
kirefu maelezo aliyokuwa amenieleza Chifu.
"Ili kuwaweka sawasawa ninyi katika picha ya tukio hili mtakuwa wageni wa kampuni yangu. Kwa
hiyo mimi naona tangia sasa nitakuwa ni wakala wa gazeti lenu, kwa kufanya hivi nitapata
kisingizio cha kutembea na kupeleleza na nyinyi mkiwa kama wateja wangu; nafikiri
mmenielewa?".
Wote walitingisha vichwa kuonesha kuwa wamenielewa. Kutokana na mipango yangu ilivyokuwa
nilionelea tokea wakati huo tuanze kazi bila kupoteza muda.
Nilitoa onyo tena "Kukubali kwenu kushiriki na mimi katika upelelezi wa tukio hili mjue
kabisa mmejiwekea sahihi ya kifo. Natoa natoa muda wa mwisho kama kuna mtu anaona wasiwasi
katika moyo wake nampa nafasi aache shughuli hii", niliwaasa na kuwaangalia kwa makini sana.
Mwisho Veronika akasema
"Unajuwa Willy dakika ile mtu anapozaliwa pale pale anapewa huku ya kifo. Nina maana ya
kusema kuwa binadamu hata aishi vipi kufa lazima atakufa. Kule kuishi baada ya kuzaliwa ina
maana kuwa ile hukumu ya kifo inaahirishwa kutekelezwa. ..
ITAENDELEA