Riwaya: 'Njama'

Riwaya: 'Njama'

Safi sana. Utuwekee hata mbili ikiwezekana
 
Safi sana. Utuwekee hata mbili ikiwezekana

Shukrani mkuu, story nzima ipo nina wasiwasi nikiiweka yote kwa pamoja kama itawachosha kusoma. Ila kama mtaridhia sita shindwa kuimwaga yooote mjinafasi kwa raha zenu,mna maoni gani? Nasuburi maoni yenu.
 
NJAMA
SURA YA SITA
CHIMALAMO
"Baada ya kuzungumza na wewe kwenye simu,
niliondoka kwenda New Afrika kama tulivyoagana.
Niliona hakuna sababu ya kuchukua gari, hivyo
niliondoka kwa miguu kwani nilijua dakika kumi
ningenitosha. Nilikuja moja kwa moja na barabara
ya Azania Front nikakatisha pale kwenye kanisa la
Kilutheri na kutokea barabara ya City Drive. Kama
unavyojua New Afrika inajengwa kwa mbele kwa
hivyo nilijipenyeza kwenye mwanya wa jengo la
Benki ya Taifa ya Biashara tawi la City Drive na
Azikiwe, nikawa nimetokea karibu kabisa na pale
ulipoegesha gari lako".
Ghafla nikaona watu wawili, mmoja wao akifungua
mlango wa gari lako. Mimi nikasimama na
kujibanza kwenye moja ya nguzo za jengo hili la
Benki huku giza likinisaidia. Yule wa mbele aliingia
na nyuma akaangalia huku na huko hakuona kitu
nafikiri, maana alitoa bastola mwenye joho lake
nae akaingia. Kama unavyojua gari hili lina milango
miwili tu, hivi waliinamisha kiti na kuingia nyuma
ya gari.
Mara moja nikajua nia yao; nilijua wanakusubiri
wewe ama kukuua ama kukuteka nyara. Nilipofikiri
sana niliona nia yao kukuteka nyara kwani kama ni
kukuua wasingeingia ndani ya gari, hasa nyuma, na
mahali penyewe pakiwa karibu sana na New Afrika.
Huwa naamini sana akili zangu zinavyonituma
hivyo nikaona kuwa nia yao ni kukuteka nyara.
nilifikiri nikufuate lakini sikuwa najua ofisi yako
ilipo. Hivyo nikaamua kitu kimoja, kuingia ndani ya
buti la gari kama iwazi. Kwa kuwa gari yako ina
nyavu kioo cha nyuma, nilijua watu hawa
hawataniona wala kunisikia, kwani nilijua na wao
watakuwa wamelala chini ili usije ukawaona wakati
unaingia".
Alinyamza kidogo ili kulegeza koo kwa mate,
akaniangalia akanikuta mimi naendesha taratibu
huku nikimsiliza kwa makini sana. Kisha
akaendelea, "Nikisaidia na giza la ukuta wa mabati
uliozungushiwa jengo hili la mbele la New Afrika
huku nikinyata nimeinama kimo cha buti la gari.
Kama bahati ilivyokuwa na mimi nilikuta buti lako
halikufungwa na funguo. Jihadhari sana siku
nyingine utabeba adui ndani ya gari lako".
"Nimekuwa sina aduin Tanzania, hivyo nimekuwa
nikiamini kuwa hakuna mtu wa kunifanyia ubaya,
maana hata sijawahi kugombana na mtu hapa Dar
es Salaam".
"Haya sasa lazima utambue kuwa umepata
maadui; lazima ujihadhari".
"Sawa nitajihadhari lakini vile vile kama ningekuwa
nimefunga usingeweza kuniokoa, hivyo kujiachia
mambo mara nyingine ni vizuri".
"Haya nimekubari kushindwa, lakini hata hivyo
ningepata njia nyingine. Basi taratibu nilifungua
buti la gari na kuingia ndani, kimya kimya kabisa
bila kelele yoyote. Niliwahi kusafiri ndani ya buti
wakati ninakaa na majeshi ya POLISALIO, hivyo
najua sana hali ilivyo ndani ya buti la gari kiasi
kuwa kwangu hewa ya mle ninaweza kuistahamili
ingawa ni kidogo. Unajua gari linapoanza kutembea
hewa inajaa kabisa. Basi baada ya kuingia na
kulifunga kinamna, kiasi ambacho lisingeweza
kunishinda kufungua, baada ya kuliangalia kufuli
lenyewe.
"Muda si mrefu nilisikia mlango unafunguliwa;
unajua hili gari lako lilivyoundwa ukiwa ndani ya
buti unasikia maneno yanayozungumzwa ndani ya
gari. Basi niliwasikia wakikuamrisha kuendesha
gari ndipo nikajua nilivyohisi ni sawa. Ulipopiga
honi na kusimama kama ulivyoamrishwa, nilijua
tunaingia mahali na nikajua kuna mtu anayefungua
na kufunga mlango ni wa kundi lao hivyo atakuwa
ni mlinzi mwenye silaha.
"Tulipoanza kuondoka niliinua mlango wa buti
kidogo sana na nikamuona mtu huyu nusu
amebeba bunduki. Niliendelea kuchungulia hivi hivi
nikaona njia tuliyotokea kutoka kwenye lango
mpaka gari liliposimama nikabana tena mlango.
Nikasikia wanakuamru toka kisha nikasikia sauti
zingine hapo nje halafu pakawa kimya, ndipo
nikafungua taratibu mlango na kutoka nje. nikakata
shauri lazima nipate silaha ili niweze kukuokoa.
"Hapo ndipo nilipoanza kurudi mbio kwenye lango
ili nikamnyanganye silaha yule mlinzi. Nilipokaribia
lango nilimuona yule mlinzi amesimama anavuta
sigara huku anaangalia upande wangu. Nililala
chini na kusubiri. Alipogeuka na kuangalia upande
mwingine nilianza kutambaa chini kimya kimya.
Nilikuwa nimefundishwa na wanajeshi wa Polisalio
namna ya kumnyemelea mtu kwenye giza bila yeye
kushituka. Nilipokuwa karibu nae kabisa,
nilisimama na kupiga kelele, "Yeeeeee".
"Alishituka na kuingiwa na hofu na kabla hajatokwa
na hofu nilipiga teke mikono yake bunduki
ikaanguka chini. Alipoona hivi akaanza kukimbia.
Niliruka na kumpiga teke mgongoni akaanguka
chini. Bila kuchelewa nilimrukia shingoni, ndivyo
ikawa kwaheri. Nilimvua joho nikalivaa halafu
nikatafuta kofia. Nilipoipata nikaivaa halafu
nikachukua bunduki nikakuta ni aina ambayo
wanaitumia wana mapinduzi wa Polisalio, yaani
SMG ya kichina, hii bunduki niliitumia sana wakati
nimekaa na hawa mashujaa wa Polisalio.
"Nilipoipata silaha hii, nilikimbia kurudi kwenye
kibanda mlichoingia nipokaribia nikaona watu
wawili wenye bunduki nikononi wakizunguza. Mimi
nilizunguka nyuma ya kibanda cha karibu, halafu
nikakohoa kisha nikazunguka haraka kutoka pale
nilipokoholea. Nilisikia mmoja wao akisema;
"Umesikia hicho".
"Ndio", alijibu mwenzake.
"Wewe zunguka huku na mimi nitapita huku".
"Hii ilinipa nafasi kujitayarisha, sikuwa nahitaji
kutumia bunduki maana mrio ungewashitua watu
waliokuwa ndani ya kibanda. Kwa vile nilikuwa
nimevaa nguo kama wao na kofia, nilizunguka na
kukutana na mmoja wao, yeye alinichukulia ni
mwenzake shauri ya mavazi na giza. Tulikaribiana
sana akabweteka; "Umeona nini?". Mimi niliinua
mkono kumuonyesha nyuma yake na alipogeuka tu
nikamkata karate ya shingo iitwayo ua na bila
shaka alikufa pale pale. Nilimdaka haraka haraka
na kumlaza chini bila kishindo. Kisha nikageuka
upesi upesi ili nikutane na yule aliyepita upande
mwingie sikuchukua hata hatua tatu tukawa
tumekumbana hata yeye mavazi yalimdanganya na
kufikiri mimi ni mwenzake.
"Huku hakuna kitu", aliniambia kwa sauti ya chini
chini. Nilimdanganya kwa kumuonyesha kwa ishara
aangalie nyuma yake na yeye akadanganyika. Hapo
ndipo nilipomrukia nikamtia kabali ya hali ya juu
mpaka niliposikia shingo linakatika nikamwachia.
Sina mkanda mweusi wa judo na karate bure Willy,
najua jinsi ya kuutumia".
"Zaidi ya ambavyo ningetegemea mrembo kama
wewe kuutumia", nilimjibu huku nikitoa tabasamu.
"Asante. Baada ya hapo ndipo nilikimbia na kupiga
teke mlango kwani nilisikia mlio wa bastola kabla
sijapiga teke mlango. nilipoingia nilikuona chini
hivyo nikafanya kama ulivyoona. Lo! Willy mpenzi
niliogopa niliposikia mlio wa bastola nikafikiri
wamekuua!".
"Si lahisi kuniua".
Nia yao ilikuwa nini?".
Nilimweleza yote waliyoniuliza.
Wakati namaliza kumweleza nilikuwa nataka
kutoka barabara ya Upanga na kuingia nyumbani
kwangu na kupeleka gari moja kwa moja gereji.
Tukashuka nikafunga mlango wa gereji.
Karibu ndani vero.Hapa ndipo nyumbani kwangu".
Nilifungua mlango na kuwasha taa ya sebuleni
halafu nikamkaribisha ndani akaketi kwenye
kochi.
"Asante lakini sitakaa sana, maana nasikia uchovu,
nataka kurudi hotelini nikalale".
"Hakuna haja Vero nina mengi sana ya kukusimulia,
maana hata sijakueleza yaliyotupata na Sherriff.
Halafu....... nikasita kidogo".
"Halafu nini?", aliuliza kwa shauku.
"Halafu uliniahidi tulipokuwa Siera Leone kuwa
tutafahamiana vizuri zaidi Dar es Saalaam, lazima
ujuwe kwamba ahadi ni deni".
"Haya baba umeshinda".
"Asante".
Nilichukua vinywaji ndani ya barafu, halafu
nikamkaribisha katika chumba cha kulala. Nilizima
taa sebuleni nikafunga mlango wa mbele,
nikakagua vyumba vyote vya nyumba pamoja na
madirisha na milango. Nilipoona kila kitu ni salama
nilirudi chumbani nikafungua mlango wa
maliwatoni, nikajaza maji kwenye karai la kuogea.
Nilimwita Veronika aje tuoge. Tulioga pamoja na
mtoto huyu mara moja nikasahau matatizo yangu
yote na uchovu wote wa jioni ile. Baada ya kutoka
maliwatoni tulikuwa tayari kulala.
"Haya nieleze sasa wakati tukipumzika", Veronika
alisema huku amelala karibu yangu.
Nilizima taa yenye mwanga mweupe, nikawasha
yenye mwanga wa bluu. Nikaleta chupa yenye
whiski kwenye meza ya kitanda nikammiminia Vero
ndani ya glasi nikaweka mawe ya barafu na mimi
nikatengeneza yangu.
"Na tunywe kwa usalama wa maisha yetu wote".
Tulianza kunywa huku nikimweleza yote
yaliyotupata. Baadae tukaelezana mambo yetu
binafisi ambayo yalitufanya tujishitukie
tumekumbatiana na kubusiana.
ITAENDE:LEA
 
NJAMA
SURA YA SITA
CHIMALAMO
II
"Amka", Vero alinishitua, "ni saa mbili sasa.
Nilimwangalia Vero ambae alionekana kuwa
alikuwa ameamka kitambo kwani alikuwa na sahani
ya mayai ya kukaanga na vikombe viwili vya
kahawa. Alikuwa amevaa pajama zangu; alitoa
sura ya kuchekesha, hivyo nilimcheka, maana
zilimpwaya sana.
"Unapendeza katika pajama hizo", nilimtania.
"Kwenda huko".
Mimi nikaangua kicheko, nikatoka kitandani na
kukaa.
"Mwenzangu umelala fofofo leo. Mimi nimeamka
nikafanya mazoezi kisha nimekwenda jikoni
nikatayarisha chochote. Haya tunywe kahawa utoe
usingizi", alisema huku akikaa karibu nami.
"Mimi naona nikaoge kwanza".
"Hapana. Tunywe kahawa kwanza halafu tutafanya
mazoezi ya judo na karate ili niwe katika hali nzuri,
halafu ndipo tutakwenda kuoga".
Basi tulikunywa kahawa na mayai ya kukaanga,
halafu tukatoka nje uani kufanya mazoezi.
Nyumbaq yangu ilikuwa imezungukwa na ua mzuri
wa michongoma iliyokatwa vizuri na yenye urefu
wa futi saba. Hivi ukiwa uwani kwangu mtu
anayepita nje ya ua hawezi kuona kitu chochote
kinachofanyika ndani. Basi tulifanya mazoezi ya
karate na judo ya hali ya juu sana. Hii
ilinihakikishia kuwa Veronika alikuwan na ujuzi wa
kutosha. Ilibidi tu kumwonyesha kuwa mimi najua
zaidi nilipomwingizia staili nyingine za pekee
ambazo hutumiwa na wajuzi wa hali nya juu katika
karate na kung-fu kama mimi, ambazo zilimshinda
kuzifuata.
"Ujuzi wako unatosha kabisa Veronika. Naamini
unaweza kupambana na mtu yeyote, na nina imani
ni watu wachache sana wanaweza kukushinda
katika karate na judo".
"Asante kwa pongezi laki. Lo, lakini wewe
mwenzangu ni zaidi. Mitindo mingine unayotumia
sikuwahi kuiona hata kwa walimu wetu huko
Japan. Ndio sababu wanasema ulipambana na
Inoki na kutoka nae sare. Nilivyani walikuwa
wanaongeza chumvi lakini sasa ninaamini ni kweli.
Kokote nitakapotembea na wewe hata pakiwa ni pa
hatari namna gani sitaogopa kabisa maana nina
imani kubwa katika uwezo wako kwa jambo lolote
sasa".
"Asante".
Baada ya mazoezi tuliingia pamoja maliwatoni
tukakoga.
"Mimi itabidi unipeleke hotelini nikabadili nguo.
Angalia hizi zilivgyochafuka kwa ajili ya matatizo
ya jana usiku!".
"Usiwe na taabu, lolote utakalosema".
Mimi nilibadilisha nguo, nikavaa vizuri kabisa kama
mfanyabiashara. Nilichukua silaha tulizokuwa
tumeziteka nikaziweka sehemu yangu ya siri
ambako huweka silaha zangu na ni mimi peke
yangu ninayepajua mahali hapo. Na hata ukiwa
mtu wa namna gani huwezi kupagundua.
Nilichukua silaha nyepesi kwa ajili ya siku hiyo
kama litatokea jambo lolote. Nilimpatia Veronika
bastola yenya sailensa. Nilipoona mipango yote
nimekamilisha tuliondoka kuelekea Kilimanjaro
hoteli. Ilikuwa saa tatu na robo tulipofika
Kilimanjaro.
"Nenda kajitayarishe, kabla ya saa nne mimi
nitakuwa hapa".
"Utanikuta tayari", Veronika alijibu.
Niliondoka na kuelekea ofisini. Nilimkuta Eddy nae
anaingia. Alipoona gari langu akasimama mlangoni
kunisubiri.
"Habari za leo bosi?".
"Nzuri Eddy, umelala salama kijana?".
"Ndio, bila taabu".
"Twende ofisini kwangu". Tulielekea ofisini kwangu.
Tulimkuta Linda anazungumza kwenye simu.
Alipotuona akasema, "Huyu ameingia", Akanipa
simu huku akisema "Maselina huyo.
"Halo mrembo, habari za asubuhi?".
"Nzuri tu, wasiwasi kwako ambaye unalala mpaka
saa tatu na waandishi wa habari ".
"Mwongo, nani kakuambia huyo mwandishi kalala
kwangu ?".
"Nani hakujui, danganya wengine lakini miye baba
unajua kabisa kuwa nakujua kama nyuma ya
kiganja changu".
"Haya umeshinda wewe".
"Njoo Chifu anakuhitaji, anataka kujua umefikia
wapi mpaka sasa".
"Haya nakuja, nitamweleza mpaka yeye atachoka".
"Haraka basi", alisema Maselina na kukata simu.
"Eddy jambo lolote juu ya Kiki?".
"Si nilikwambia nitakuwa na habari zote saa nne,
na saa nne bado". Eddy alijibu.
"Oke, je juu ya bohari la Mamlaka ya Pamba
umepata nini?".
"Walinzi wote wa bohari hilo wamekutwa leo
asubuhi wameuawa huko Temeke. Inaonekana
walilichukua bohari hilo kwa nguvu ili wafanyie kazi
zao kwa muda tu. Kila kitu kingine ni salama. Polisi
wanashughulikia hayo ya jana na kujaribu
kutambua maiti walizozikuta hapo. Wao wanafikilia
ni wezi. Gari walilotumia nalo lilikuwa limeibiwa".
Kisha nikamweleza yaliyokuwa yametupata na
Veronika, baada ya kuachana nae jioni ile.
"Sasa fanya uchunguzi ujuwe watu hawa
wamejiingizaje huko uwanja ya maonyesho ya Saba
Saba, maana uwanja huo unalindwa na polisi
masaa ishirini na nne!.
"Nafikiri mtindo wao ni ule ule. Wanaua walinzi na
kufanya makao ya muda. Wakimaliza shughuli zao
wanakwenda kuteka mahali pengine lakini hata
hivyo vijana watachunguza".
"Oke, ngoja mimi nikamwone Chifu halafu tutaanza
upelelezi wetu, kama kawaida utatufuata toka New
Afrika kama jana, sawa>".
"Bila wasiwasi bosi, kiijana ninayefuatana nae ni
mzuri sana nafikiri hata nyinyi mlitupoteza".
"Ndio, kazi yenu ya jana ilikuwa nzuri sana,
nilimpongeza.
"Bossi unapendeza sana leo".
"Asante sana kwa pongezi lako. Ngoja nikamwone
Chifu".
Nilimwacha akiwa anataka kuzungumza mengi na
mimi. Nilipanda ngazi na kuingia ofisini kwa chifu.
"Anatusubiri, amesema nichukue ripoti yako",
Maselina alisema.
Basi tulifungua mlango na kuingia ofisini kwa Chifu.
Chifu alikuwa amekaa kitini mwake akivuta mtemba
kama kawaida yake.
"Shikamoo Chifu".
"Marahaba, ketini chini".
"Asante...
Maselina alichukua kitabu chake cha hatimkato na
kukaa tayari kuandika mazungumzo yetu".
"Ehee, nieleze kwa kirefu mambo ambayo
umeishafanya. Maana huko makamo makuu ya
Polisi kuna kelele, mauaji ya ajabu yanatokea mjini
hapa kwa mara ya kwanza mpaka wameshindwa
mahali pa kuanzia upelelezi. Nilipopata ripoti yao
juu ya mauaji haya, nilihisi hii ni kazi ya Namba
Moja. Kwa hiyo naomba maelezo kamili ili nami
niweze kuieleza serikali maendeleo yoyote juu ya
jambo hili maana kuna wasiwasi mkubwa. Jumuia
ya Ulimwengu inaikera serikali kwa kutaka kujua
ukweli wa jambo hili, na wakati huo huo maadui
zetu wanaendelea kutupaka matope bila kupata
ukweli wa jambo hili".
Nilichukua muda huu kumweleza yote tangu
nilipotoka ofisini mwake; kwenda kwetu bandarini
na ofisi ya Kamati ya Ukombozi, barua niliyoikuta
mlangoni kwangu; mapambano dhidi ya
waliomteka nyara Sherriff na mwisho walioniteka
nyara. Nilimweleza kila kitu kwa ufasaha bila
kuacha tukio hata moja. Huenda jambo nililoacha
ni juu ya tuliyofanya nyumbani kwangu na Veronika
ambayo ni siri yetu hata nyinyi sitaki mjue.
"Kwa kutokana na maelezo ya mtu wa kikundi hiki
kinachojiita 'Wanamapinnduzi wapinga mapinduzi'
mimi naamini hawa watu ni VIBARAKA wa serikali
ya makaburu ambao wanataka kupiga vita harakati
za ukombozi dhidi ya serikali hizi dhalimu. Na mtu
huyu niliyezungumza nae nina imani ni mtanzania
kutokana na sura yake na sauti yake ingawaje
alijitahidi sana kunidanganya kwa sauti.
Mimi ninavyofikiri kuna chama kimojawapo katika
vyama vinavyopigania uhuru, ambacho makaburu
wamekidanganya kuwa kikiweza kupiga vita
harakati za mapambano ya silaha dhidi ya serikali
ya Afrika Kusini itakipa mwanya chama hicho
katika serikali ya makubaliano.
"Kwa hiyo chama hiki kimekubali kuwa kibaraka wa
Afrika Kusini na kuanza vita dhidi ya vyama vingine
vinavyoendeleza mapambano ya silaha. Kwa vile
isingekuwa rahisi chama hiki kufanya mapambano
bila msaada. Serikali ya makaburu lazima inakipa
misaada ya kila hali, yaani wagtu, silaha na fedha.
Kwa hiyo Chifu, ni imani yangu kuwa silaha hizi
hazikibwa na watu wengine ila majasusi wa
makaburu ili kutimiza lengo lao hilo'.
Chifu alikuwa ananiangalia kwa makini sana kisha
akatingisha kichwa.
"Nimekuelewa vizuri sana Namba Moja. Hata
unavyofikiri mimi naona ni sawa. Lakini tatizo letu
liko pale pale; watu hawa wamejipenyezaje nchini
humu na sasa silaha hizo ziko wapi?. Maana
silaha hizo ni za kisasa kabisa. Hatua uliyofikia
kwa siku moja inaridhisha, tafadhali kazana zaidi
katika masaa ishirini na manne yajayo tuwe na
fununu zaidi.
"Hapa tuna vyama viwili, PLF na SANP na vyama
hivi ndivyo vinaendesha mapambano ya silaha
huko Afrika Kusini. Kwa hiyo tuna chama kimoja
ambacho kiko nje ya nchi hii; ama kiko Afrika ya
Kusini ama katika nchi jirani na ndicho
kimejipenyeza kuvipiga vita hivi vyama viwili".
"Hata mimi nafiri hivyo. Kwani kuna vyama vingapi
vinavyopigana na serikali ya Afrika Kusini?".
"Viko vingi, kati ya hivyo vitatu viko Afrika Kusini
na vitano viko nchi ya nje, kwa hiyo jumla ni
vinane".
"Hili ndilo tatizo la vyama vingi. kingekuwa chama
kimoja yote haya yasingetokea", nilisema kwa
huzuni.
"Siasa kijana, wanasiasa ndio wanaleta taabu
ulimwenguni; ndio wanayumbisha vichwa vyetu.
Kila mtu na siasa yake na imani yake, na kuna
wengine hawana cha siasa wala cha nini; nia yao
kutaka ukubwa ili wale", alijibu Chifu kwa uchungu
mkubwa.
"Sawa, sisi tunaendelea na upelelezi wetu na
ushauri wako nitauweka manani".
"Asante sana Namba Moja".
"Polisi wamefikia wapi?".
"Polisi hawajafika popote. Sasa ndio
wamechanganyikiwa zaidi baada ya mauaji haya
ya usiku. Hivyo mimi nakutegemea wewe, maana
umefanya maendeleo mazuri".
Nilisimama nikampigia kope Maselina nae
akaminya midomo kuzuia tabasamu alilotaka
kunipa. Chifu alinifungulia mlango na kuniambia.
"Nakutakia mafanikio katika kazi hii kijana".
"Asante Chifu", nilijibu kisha akafungua mlango.
"Kavae upesi twende zetu Komredi", nilimwambia
Sherriff aliyetaka kubadilisha nguo.
"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka
haraka.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SEHEMU YA SITA
CHIMALAMO
III
Ilikuwa saa tano tulipofika New Afrika baada ya
kumchukua Sherriff kutoka kwa daktari akiwa
anajisikia vizuri kabisa. Veronika ndiye nilikuwa
nimewahi kumchukua kabla ya Sherriff.
"Kavae upesi, twende zetu Komredi", nilimwambia
Sherriff aliyetaka.
"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka
haraka.
Ilikuwa saa tano na dakika kumi na tano
tulipoondoka kuelekea Ofisi za PLF. Njiani
tulimweleza yote yaliyokuwa yametupata jioni ile
tukibakiza tu ile habari ya kwenda kwetu pamoja
kulala nyumbani kwangu.
Ofisi za PLF zilikuwa mtaa wa Makunganya karibu
na Achells Limited hivyo haikutuchukua muda
kufika pale kutokea New Afrika.Tulitokea barabara
ya Azikiwe, tukaingia mtaa wa Independence pale
kwenye mzunguko wa sanamu ya Askari halafu
tukakata kulia pale kwenye taa za usalama
barabarani za mtaa wa Independence na Postway,
na kuingia Postway. Tukatelemka kidogo mpaka
kwenye mtaa wa makunganya moja kwa moja
kwenye ofisi za PLF. Tuliegesha gari pale pale
mbele ya ofisi tukatelemka na kuingia mapokezi.
tulimkuta kijana mmoja akiwa mapokezi.
"Habari zako ndugu", nilimsalimu.
"Salama, sijui niwasaidie nini?".
"Tunaomba kumwona ndugu Cecil Chimalamo".
"Mna miadi naye?'.
"Hapana, lakini ukimweleza kuwa kuna waandishi
wa habari toka gazeti la Afrika natumaini anaweza
kutuona".
"Subirini hapa kwenye viti".
Tulikaa kwenye makochi mazuri sana. Cecil
Chimalamo nilikuwa ninamfahamu kwa sura na vile
vile mambo yake kwani nilikuwa nimeshasoma faili
lake mara nyingi ofisini. Kwa kifupi wanasiasa
wengi walimpenda kwa sababu ya imani zake za
kisiasa ambazo mara nyingi zilikuwa na msimamo.
Alitambulikana kama kiongozi mmojawapo
mashuhuri mpinga ubaguzi na mpenda serikali ya
wengi katika Afrika ya Kusini, makaburu
walimchukia sana.
Punde yule kijana alirudi akayakatisha mawazo
yangu juu ya Chimalamo.
"Mnaweza kumwona chumba namba tatu".
"Asante', nilishukuru kwa niaba ya wenzangu.
Tulikwenda moja kwa moja mpaka chumba namba
tatu tukabisha hodi.
"Karibu".
Nilifungua mlango tukaingia ndani tukajikuta katika
ofisi.
"Karibuni", alitukaribisha huku akisimama.
"Asante".
"Nyinyi ndio mmetoka kwenye ofisi za gazeti la
Afrika".
"Ndio".
"Twendeni mzee anawasubiri".
Alifungua mlango, tukaingia ndani na kumkuta
ndugu Chimalamo amekaa anavuta sigara.
Alipotuona alisimama.
"Karibuni, ketini chini".
Kabla hatujakaa nilichukua mwanya huu kujijulisha
mimi pamoja na wenzangu kwake.
"Mimi naitwa Willy Gamba na ni Meneja Mkuu wa
Kampuni iitwayo Afrika Internation Agencies (AIA),
na hawa ni waandishi wa gazeti la Afrika. Huyu
anaitwa Veronika Amadu na huyu ni Ahmed
Sherriff. Wote ni wananchi wa Sierra Leone",
tulishikana mikono na kusabahiana halafu tukaketi
chini.
"Imekuwaje wewe uwe pamoja nao?", aliuliza.
"Kampuni yangu ndiyo wakala wa gazeti la Afrika
hapa Tanzania kwa hivyo haja zao zote
naziwakilisha mimi.
"Aisii, nafikiri tumeshaonana mara nyingi. Wewe si
mgeni kabisa kwangu ", aliniambia na kuniangalia
kwa macho ya kudadisi.
"Bila shaka tumeonana mara nyingi hasa katika
tafrija za vyama hivi ingawaje hatujawahi
kujulishwa moja kwa moja".
"Ehe gazeti la Afrika linataka nini?", Nilishangaa
sana maana hata hakuuliza vitambulisho. Mara
moja nikajua mtu huyu aliweza kuwasoma watu na
kujua ni watu wa namna gani. Alikuwa mtu
mwenye busara nami nikaondokea kumpenda.
"Sisi tumekuja hapa mjini baada ya kupata habari
za tukio lililokikabiri chama chako na serikali ya
Tanzania kwa ujumla. Jumuia ya Ulimwengu
mpaka sasa imegawanyika katika pande mbili.
Moja inalaumu Serikali ya Tanzania kuwa ndiyo
inahusika na wizi wa silaha hizi ambazo ni za
kisasa kabisa, upande wa pili unaamini kuwa hizi
ni njama za mabeberu zinazopiga vita harakati za
ukombozi wa Afrika Kusini. Kwa hiyo gazeti la
Afrika likiwa kila siku linafuatilia kwa makini
harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kuweza
kusaidia inapowezekana, linahitaji hasa ukweli wa
tukio hili. Hii ndio sababu tuko hapa.
Tumeshawaona wakuu wengine katika OAU na
katika Serikali ya Tanzania na tumeona hatuwezi
kufika mbali bila kujua mawazo yako wewe ambaye
ndiye hasa uliyehusika na mali iliyopotea", Sherriff
alieleza kwa kinagaubaga.
"Kwa hiyo mnataka kujua mimi niko upande gani
katika mawazo hayo mawili ya Jumuia ya
Ulimwengu?".
"Hilo ndilo swali letu la kwanza", Sherriff alijibu.
"Mimi nawaunga mkono wanaoamini kuwa hizi ni
njama za mabeberu. Wale wanaosema Tanzania
inahusika wanajaribu kuongeza petrol kwenye moto
huku wakijua kuwa Tanzania ni nchi pekee katika
Afrika ambayo haiwezi kufanya jambo hili.
Nakuhakikishia kwamba tangu nikae hapa nina
miaka sita na sijaona Serikali ya kimapinduzi kama
hii. La hasha, Tanzania haiwezi kabisa kufanya
jambo hilo ila hizo ni mbinu za mabeberu za
kutugonganisha sisi na wenyeji wetu ili mambo
yaharibike kabisa. Mimi sitakubali washenzi hao
watugonganishe. nafikiri umenielewa.
"Nimekuelewa sana. Sasa unafikiri silaha hizi
zimepotea poteaje?. Hapa nataka mawazo yako
binafsi".
"Hata mimi sijui. Ni njama ya hali ya juu
iliyofanyika, hivyo nimeachia shauri hilo Serikali ya
Tanzania ambayo imeniahidi itafanya juu chini
kufichua njama hizi".
"Na isipowezekana?", Veronika aliuliza.
"Tutajua la kufanya wakati huo.
"Ilibainikaje kama wewe umekwenda Urusi kutafuta
silaha za kisasa na hali naamini jambo hili
lilifanywa kwa siri?", Sherriff aliuliza.
"Siku hizi hakuna kitu cha siri. Nafikiri hata kabla
sijaondoka hapa Dar es Salaam kwenda Moscow
ilikuwa imeshajulikana nini nafuata. Ulimwengu huu
wa teknolojia hakuna kitu cha siri. Hata mkutano
uliofanyika huko camp Davis Marekani, kati ya
Marais wa Israel, Misri na Marekani na kuweka hali
ya uficho wa hali ya juu, bado watu walijua kabla
mazungumzo hayo ya kisiri ya hali ya pekee
hayajatangazwa rasmi. ili kujibu swali lako hata
sisi hatukutegemea tutajulikana.
"Watu wanafikiri kuwa, silaha hizo zimefanyiwa
njama za kuibiwa kwa sababu ni silaha za kisasa
kabisa na za hali ya juu. Ndio sababu watu
wanasema Tanzania isingeweza kuziona
zinakwenda hivi hivi. Sasa swali langu ni kwamba
kwa nini uliamua kuomba silaha za kisasa za jinsi
hii wakati vita havijafikia hali ya juu sana kuhitaji
silaha za namna hiyo.
"Ahaa, swali lako zuri sana. Ili mwelewe kwa nini
nilichukua hatua hiyo ni lazima niwape maelezo
kamili, juu ya hali ya silaha alizonazo adui
tunayepigana naye", alinyamaza kidogo
akaegemeza mikono yake mezani.
"Maana mtu hawezi kupigana kwa rungu dhidi ya
mtu mwenye bunduki. Kwa hiyo hamtajali naona
nikiwaeleza kwa kirefu jinsi wapinzani wetu
walivyojidhatiti kijeshi na ndipo tu mnaweza kuona
kwa nini niliagiza silaha za kisasa".
"Sisi tutafurahi sana kupata fursa ya kusikia
maelezo hayo", nilijibu kwa niaba ya wenzangu.
"Katika miaka 15 iliyopita", alieleza Chimalamo.
"Makampuni ya kimataifa yamezidisha rasilimali
zao ili kuimalisha uchumi wa Afrika Kusini.
Makampuni makubwa ya Marekani na Ujerumani
Magharibi yamepanua rasilimali zao katika sehemu
muhimu za utawala wa Makaburu. Na makampuni
haya yana ushirikiano mzuri sana na utawala wa
Makaburu.
"Miaka michache iliyopita mabenki ya kigeni
yameikopesha afrika Kusini mamilioni ya fedha ili
kuwezesha kukabili migogoro ya kiuchumi
iliyosababishwa na kulegalega kwa uchumi wa nchi
za magharibi na kuendelea kukua kwa mapambano
ya wazalendo wanaokandamizwa na utawala wa
Makaburu.
"Mabenki ya kigeni yametoa mtaji mkubwa kwa
utawala wa Makaburu kwa mahitaji ya fedha kwa
ajili ya mambo ya kijeshi na kiuchumi, katika miaka
michache iliyopita deni la kigeni la Afrika Kusini
limeongezeka haraka kufidia gharama za mafuta
yake, kupanua ununuzi wa silaha na gharama za
mipango ya kuuwezesha utawala huo dhalimu
ujitegemee. Kwa taarifa yenu mpaka kufikia
mwishoni mwa mwaka 1976 utawala wa Makaburu
ulikuwa na deni lipatalo Shs.72 bilion, lakini idadi
inaweza kuwa kubwa kuzidi hapo maana mikopo
kwa Afrika Kusini ni siri. Sijui mnanielewa?".
"Tunakuelewa sana", tulijibu kwa pamoja, huku
Veronika akiwa anaandika maelezo hayo.
"Kuna ukweli unaoonysha jinsi biashara ya
makampuni ya kigeni na rasilimali zao zilivyosaidia
kuimarisha viwanda vya kijeshi vya Afrika Kusini
hata kuuwezesha utawala wa Makaburu kuwa na
kiburi na kupuuza maoni ya dunia na kuendelea
kudumisha udhalimu wake na kuwakandamiza
wananchi walio wengi wa Afrika Kusini.
Makampuni ya kigeni yamejihusisha moja kwa
moja katika kuimarisha kijeshi Afrika Kusini.
Kumbukumbu za kampuni moja inayoshughulika na
utengenezaji wa silaha katika nchi zinazoendelea
zinaonyesha kuwa makampuni ya kigeni yametoa
liseni kwa makampuni ya Afrika Kusini kutengeneza
zana za kijeshi za aina mbali mbali, pamoja na
ndege za kijeshi, mabomu, risasi na bunduki. Vile
vile kuna makampuni yanayotengeneza vipuri na
vifaa vingine kwa madhumuni ya kijeshi. Shirika la
Baruti na madawa la Afrika Kusini 'AECI' linatajwa
kuwa linamiliki viwanda vitatu vinavyotengeneza
silaha na linashirikiana na kampuni moja ya
viwanda vya madawa ya Uingereza. "Imperial
Chemical Industries", Kampuni hiyo ya Uingereza.,
imetoa utaalamu na vifaa vinavyotumiwa na Shirika
la AECI la Afrika Kusini. Na wakati huo huo
kampuni ya Darman Long ya Afrika Kusini iliyounda
manowari moja yenye uzito wa tani 220
inashirikiana na Shirika la vyuma linalomilikiwa na
serikali ya Uingereza katika shughuli za
utengenezaji silaha".
Alinyamaza kidogo, akachukua sigara akaiwasha
kisha akavuta mara tatu hivi halafu akaendelea.
"Kutokana na misaada hii toka nchi za Magharibi,
Afrika Kusini imejiimarisha sana kijeshi. Utaona
kuwa miaka ya sitini, matumizi ya kijeshi ya Afrika
Kusini yameongezeka mara sita kutoka Shg 520
milioni hadi mwaka 1977/78 matumizi ya kijeshi
yalikuwa yameongezeka tena na kufikia kiasi cha
Shg 16,450/- milioni kwa mwaka. Nimetoa maelezo
hayo pamoja na tarakimu ili kuwaonyesha kimsingi
kuwa Afrika Kusini ina uwezo kifedha kutengeneza
au kununua silaha za kisasa kabisa.
Alitua tena ili kuvuta sigara yake kisha akaendelea
huku sisi tukimsikiliza kwa makini kama wanafunzi
wanavyomsikiliza mwalimu katika somo
wanalolipenda.
"Vijana lazima mtu ujue nguvu za adui yako kabla
hujamkabili, la sivyo, utakuwa unafanya
mapambano yasiyo ya kimsingi. Ili kuwapa ukweli
hasa uliopo, jeshi la Afrika Kusini limekuwa
likitumia zana za kisasa zilizoko duniani tangu
mwaka 1970. Matumizi ya kijeshi kwa ajili ya
kununulia silaha na vifaa maalumu vya kisasa vya
kijeshi badala ya vya zamani yaliongezeka kwa
asilimia 32 mwaka 1971 kufikia asilimia 53 mwaka
1973. Kati ya mwaka 1970 na 1979 Shg 2,240
milioni zilitumika kwa mambo ya ndege za kijeshi,
shs 1,000/- milioni kwa ajili ya kununua radio,
mitambo ya kutazama ndege angani (radar) na
vifaa vingine vya kisasa. Kama nilivyokwisha
kuwaeleza hapo awali, wakati huo huo utawala wa
Afrika Kusini umekuwa ukichukua hatua kuimarisha
utengenezaji wa zana humo humo nchini kadiri
vipuli na vifaa vya mahitaji yake ya kijeshi
yanavyozidi kuongenzeka.
"Kwa mjibu wa toleo moja la kijeshi la Marekani,
tangu tangu mapema mwaka 1971 makaburu
walikuwa wanaweza kutengeneza mabumu na
baruti kiasi cha kujitosheleza na wanaweza kuuza
nchi za nje. Juu ya risasi Afrika Kusini
inatengeneza aina 100 za risasi. Kwa bunduki
inajitosheleza kabisa. Kwa silaha za jeshi la nchi
kavu, ama imejitosheleza ama imefikia hatua za
utoaji, na itajitosheleza hivi karibuni kwa zana za
jeshi la maji na sasa inatoa zana zote za moto
inazohitaji. Bunduki za kisasa kama vile Rifle na
Machine-gun vile vile zinatengenezwa. Hivi
utengenezaji wa mizinga unaanza, na kuna huduma
ya kuweza kutengeneza karibu kila aina ya magari
ya kijeshi. Radio za ndege, vifaa vya kutegulia
mabomu na vifaa vingine vya kisasa vya kijeshi
vinabuniwa na kutengenezwa huko huko Afrika
Kusini.
Alinyamaza na kuwasha sigara nyingine na kwa
nguvu zile zile akaendelea kueleza.
"Hivi karibuni ilidokezwa kuwa Afrika Kusini
inaunda aina fulani za bunduki, mabomu ya
kudondoshwa na ndege yenye uzito wa kufikia ratili
1,000 kila moja na inaendelea na utengenezaji wa
makombora ya kuangusha ndege. Mabomu hayo
inasemekana yalifanyiwa majaribio mwezi
Septemba 1977 kwa kutumia ndege za aina ya
'Mirage'. ndege hizi za mirage zilianza kuundwa
huko Afrika Kusini chini ya liseni ya kampuni ya
ufaransa ya Sessoult mnamo mwaka 1974. Kama
hatua ya mwanzo. Afrika Kusini ilinunua vipande 50
vya ndege za aina hiyo na kuunda yenyewe ndege
za mirage".
"Wakati huo vile vile ilikuwa tayari imeanza kuunda
ndege za kijeshi aina ya Impala za muundo wa
Italia-Armachi MB-326, magari ya kijeshi aina
nyingi ya silaha ndogo ndogo pamoja na bunduki
za aina ya rifle muundo wa Ubelgiji. Na kwa mjibu
wa Waziri wa Uliniz wa Makaburu. Afrika Kusini
ilitegemewa ianze kutengeneza vifaru vyake. Vile
vile Afrika Kusini inasemekana imeanza kuendeleza
utengenezaji wa mizinga ya kutungulia ndege aina
ya CAC-TUS, ikisaidiwa na kampuni moja ya
Ufaransa".
Alipofika hapa aliinua simu na kumwamru
mwandishi wake mahsusi atuletee vinywaji baridi
na sambusa kisha akaendelea.
"Naona nitawachosha lakini kwa sababu nyie
wenyewe mmeuliza mimi nitawapa hali halisi ilivyo
na mkiwa kama waandishi wa habari ni vizuri kujua
hali ya kijeshi ya huyu adui wetu mkubwa katika
Afrika. Kwa kutumia gazeti lenu mnaweza kujulisha
jumuia ya ulimwengu ukweli wa nguvu za adui yetu
huyu zilivyo, hivyo msitahimili karibu nitamaliza.
Mwandishi wake alileta vinywaji barudi na
sambusa.
"Habari unazotueleza ni za kusisimua mno kwani
kwetu sisi wengine ni habari mpya, hivyo hata
ukiendelea mpaka usiku tutakuwa tayari kabisa
kukusikiliza", nilimhakikishia.
"Kama hivyo basi nitaendelea. Magari ni muhimu
sana katika mambo ya kijeshi. Kuna makampuni
kadha wa kadha ya kigeni ambayo yamekuwa
yakiisaidia Afrika Kusini kijeshi katika mambo ya
magari. Makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya
Marekani ya General MOtors (GM), kampuni kubwa
duniani inayotoa magari kwa wingi baada ya Vita
Kuu ya kwanza. Hivi sasa ina mtambo wa
kuunganisha na kuunda magari huko Port Elizabeth,
na mtambo wa kutengeneza injini za magari nje
kidogo ya mji huo.
"Kampuni nyingine ya magari ni ile ya Ujerumani
inayotengeneza magari ya aina ya 'Benz'. Magari
ya kijeshi ya aina hii ndiyo yanatumiwa sana na
majeshi ya Afrika Kusini. Msemaji mmoja wa
kampuni ya magari ya Benz na BMW, alijigamba
hivi karibuni kwamba kampuni yake inatengeneza
magari hayo Ujerumani kwenyewe na Afrika Kusini
na inakusudia kutumia Afrika Kusini kama kituo cha
kuuzia magari hayo kwa nchi za nje zilizoko Kusini
kwa Ikweta. Hii inaonyesha dhahiri kuwa Afrika
Kusini inayo magari haya zaidi ya mahitaji yake ya
kijeshi".
Alinyamaza tena akachukua glasi yake iliyojaa
Coca-cola akainywa kwa mara moja kisha akainua
macho yake na sura yake ikageuka kuwa nzito
kisha akaendelea.
"Na mwisho napenda kuwaeleza jambo la mwisho
lakini muhimu si kwa sisi wapigania uhuru tu bali
kwa Afrika nzima. Katika mwaka 1974 Shirika la
Nyuklia la Marekani lililoko Oak Ridge lilipeleka kilo
45 za madini ya 'Uranium' kwa mtambo wa utafiti
wa nyuklia uliopo Palandaba huko Afrika Kusini
baada ya Tume ya Nyuklia, chombo pekee cha
Marekani kinachotoa liseni za usafirishaji nje vifaa
vya nyuklia kukubaliana na Afrika Kusini kwamba
haitaruhusu madini hayo yapelekwe pengine au
kutumiwa vinginevyo. Marekani vile vile mwaka
1975 na 1976 iliipa Afrika Kusini madini hayo
yanayotumiwa kutengeneza zana za nyuklia na
kuahidi kuuza zaidi madini hayo kwa mtambo wa
pamoja na nguvu za nyuklia wa Marekani na
Ufarasa unaotazamiwa kujengwa Afrika Kusini
mwaka 1984. Kwa jumla Marekani imeiuzia au
imeahidi kuiuzia Afrika Kusini ratili 300 za madini
hayo kwa ajili ya mtambo wa utafiti wa nyuklia
uliopo Palandaba. Kwa taarifa yenu ratili 300 za
Uranium zinawza kutengeneza mabomu 15 ya
Atomiki".
Kila mmoja alipiga mluzi wa mshangao.
"Nafikiri ndugu Willy nimejibu swali lako kwa kirefu,
kwa hiyo utaona sisi wapigania uhuru hatuna budi
kuomba silaha za kisasa zinazoweza kukabili
nguvu hizi kubwa ya kijeshi za adui yetu. Kwa hiyo
tukio hili lililotokea linaonyesha dhahiri kuwa hawa
makaburu wameona hatari inayowajia hivyo kuiba
silaha hizi ni mbinu moja ya kujihami. Na mimi
nimeapa sitarudi nyuma nitaondoka tena karibuni
kwenda kutafuta silaha za kisasa na kali toka nchi
rafiki ambazo naamini zitaamini kuwa tukio hili ni
njama za mabeberu. Hivyo njama zao zinazidisha
tu moto katika wapigania uhuru na ndugu zao
wanaowasaidia. Huu si mwisho wa mapambano.
Ila ni matayarisho tu ya mapambano - historia
itanihukumu. Mna swali zaidi?".
Tuliangalia na kukawa hakuna mtu mwenye swali
kwani risala yake ilituchoma mioyoni kama miali ya
moto wa umeme.
"Asante, tumetosheka", nilijibu kwa niaba ya
wenzangu.
"Oke mnakaribishwa tena siku yoyote kwani katika
kuzungumza nanyi ndipo tunapoweza kujua hali
halisi ya Kusini mwa Afrika. Asante sana vijana wa
Afrika kuja kunitembelea". Alitupa mkono wa
kuagana.
"Asante sana", tulijibu na kuondoka ofisini mwake
kimya kimya.
Tulipofika kwenye gari langu niliona ni saa saba u-
nusu, kweli tulikuwa tumekaa sana ndani. Tuliingia
ndani ya gari.
"Sasa twende tukaonane na Ray Sikazwe. Rais wa
Chama za SANP
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA SITA
CHIMALAMO
IV
Ofisi za SANP zilikuwa barabara ya Umoja wa
Mataifa baada ya kuvuka barabara inayoingia
Hospitali ya Muhimbili. Hivyo niliendesha moja kwa
moja na kuingia barabara ya Morogoro kutokea
mtaa wa Makunganya. Tulipofika kwenye taa za
usalama barabara za Jangwani, nilikata kulia na
kuingia barabara ya Umoja wa Mataifa.
Nilisimamisha gari karibu na mlango wa ofisi kwani
kwa upande mwingine wa barabara kuna gereji na
magari yalikuwa yamejaa kibao.
Tuliingia mapokezi na kumkuta binti mmoja
anajipaka poda usoni. Alipotuona akaweka mkebe
wa poda kando, alijifuta vizuri usoni halafu
akatutolea tabasamu.
"Karibuni".
"Asante. Hujambo Binti?".
"Mimi sijambo, sijui niwasaidie nini?".
"Tunaomba kuonana na Ndugu Sikazwe.
"Mna miadi naye?".
"Hapana".
"Basi hawezi kuwaona, ana kazi nyingi sana.
Huenda mnaweza kumwona ndugu Amos Shumka
ambaye naye ni ofisa katika ofisi hii".
"Wewe ni Mtanzania?".
"Ndio".
"Basi dada sisi hatutaki kumwona mtu mwingine ila
ndugu Sikazwe".
"Basi kaka yangu, ndio huwezi kumwona leo.
Amesema hawezi kumwona mtu yeyote hata awe
nani kama hana miadi naye. Mimi ninatii amri ya
wakubwa wangu kwa hiyo siwezi kufanya
vinginevyo".
"Jaribu kumpigia simu umwambie sisi tunataka
kumwona tunatoka gazeti la Afrika, mwache yeye
aamue".
"Hata kama mnatoka katika gazeti la dunia,
siwezi", alichukua rangi ya midomo na kuanza
kujipaka.
"Naona tumenoa", alisema Veronika.
"Basi, tutajipeleka wenyewe, twendeni", niliwaambia
wenzangu.
Yule msichana alisimama na kututangulia haraka
haraka na kuelekea kwenye ofisi moja huku uso
wake umejaa hasira. Na sisi tukamfuata mbio mbio
nyuma. Alipofungua mlango wa ofisi hiyo tu na sisi
tukaingia.
Hawa watu nimewakatalia kumwona mzee lakini
wamekuja kwa mabavu", alimweleza msichana
mwingine aliyekuwa anapiga taipu. Kabla yule
msichana hajajibu mimi nilipita mbele na kufungua
mlango wa ofisi ya ndugu Sikazwe kwani bila huyu
msichana kujua alikuwa ametuelekeza mwenyewe.
Wasichana wote wawili walibaki wameshikwa na
butwaa na kushika midomo yao. Mimi nilifungua
mlango na wote watatu tukaingia ndani. Tulimkuta
Ndugu Sikazwe anazungumza kwenye simu, na
alipotuona tunaingia mara moja alikata simu na
sura yake ikawa na hasira.
"Nani amewaruhusu kuingia ofisini mwangu kwa
kikuku namna hii?".
"Samahani ndugu Sikazwe. Sisi tunatoka kwenye
ofisi za gazeti la Afrika na tumekuja kukuona kwa
jambo la maana sana kuhusu wewe na Afrika
nzima. Sasa tulipofika hapa ofisini kwako mzee,
msichana wa mapokezi akatukatalia tusikuone.
Kwa sababu sisi tuna uhakika kuwa ungeturuhusu
tuonane nawe, tumeona hatuna budi kufanya jambo
lililo la busara, ambalo ni kujileta sisi wenyewe
tukiwa na imani kubwa kuwa utatuona. Naamini
umeelewa kwa nini tumechukua hatua hii, na ukiwa
kiongozi mmojawapo mwenye busara kati ya
viongozi wa vyama vya wapigania uhuru wa Afrika
Kusini tuna imani utatupokea kwa mikono miwili.
Jambo lililotuleta si jambo la kitoto", nilimweleza
kwa utaratibu sana.
Ghafla uso wake ukabadilika. Tabasamu kubwa
likaonekana usoni mwake naye akasimama.
"Samahani sana ndugu zangu katika jina la Afrika
huru. naamini mtawasamehe hao wasichana
pamoja na mimi, kwani ilibidi kutoa amri hiyo kwa
sababu sasa hivi nashughulikia tukio ambalo
limetokea hivi karibuni ambalo limevuruga vichwa
vyetu. Msiwe na wasiwasi jioneni kama halikutokea
jambo la kuwaudhi. Karibuni tuendelee na shughuli
zilizowaleta".
Baada ya maelezo haya tulipeana mikono
tukajulishana kisha tukaketi chini tayari kwa
mazungumzo.
"Nafikiri ndugu Gamba tumewahi kuonana?",
aliuliza.
"Ndio tumewahi kuonana kwenye tafrija nyingi".
"Umesema kampuni yako ndio wakala wa gazeti la
Afrika hapa Tanzania?".
"Ndio".
"Aisee, haya mimi niko tayari tuendelee na
mazungumzo yaliyowaleta".
Veronika alikohoa kuliweka koo lake vizuri kabla
hajaanza kusema. Alipokuwa tayari alichukua
uwanja.
"Gazeti la Afrika ni gazeti ambalo limekuwa na
litazidi kutetea mapambano ya Kusini mwa Afrika.
Hivi majuzi tumesikia tukio lililotokea hapa mjini,
ambalo sisi tumelichukua kama pigo kubwa sana
kwenye harakati za ukombozi wa Kusini mwa
Afrika. Ndio sababu tuko hapa ili tuweze
kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Tanzania
na Maraisi wa vyama vya wapigania Uhuru walioko
hapa nchini hivyo tuweze kupata mwanga wa
jambo hili. Kumekuwa na uvumi wa kutatanisha
ulimwengu mzima juu ya tukio hili.
"Kuna mambo mawili yanazungumziwa. Jambo la
kwanza ni kwamba tukio hili limetokana na njama
za mabeberu za kutaka kuzima harakati za
ukomboni Afrika Kusini na ndiyo sababu silaha hizi
zimeibiwa. Wengine wanalaumu serikali ya
Tanzania kuwa ndiyo iliyofanya njama hizi kwani
silaha zilizokuwa zimekuja. Serikali yoyote hata iwe
ya kimapinduzi namna gani ingeweza kupata
kishawishi cha kuchukua silaha hizi kwa manufaa
yake. Sijui wewe una mawazo gani juu ya jambo
hili", Veronika aliuliza baada ya kutoa maelezo
haya marefu.
"Kusema kweli mimi bado nimechanganyikiwa juu
ya tukio hili. Mambo yote haya mawili nimeyasikia
lakini bado mimi sijasikia uamuzi jambo lipi ni
sawa. Kama mlivyonikuta hata mimi najaribu
kuzungumza na maofisa mbali mbali wa serikali ya
Tanzania na Ofisi ya ukombozi ya OAU ili na mimi
nipate msimamo wangu. Tukio hili si la kukimbilia
kuamua".
"Kwa hiyo tuseme una wasiwasi kuwa huenda
ikawa kweli Serikali ya Tanzania ikawa inahusika?",
aliuliza Veronika huku macho yake yakimwuliza
Sikazwe.
"Sikazwe alisita kidogo akajaribu kukwepa macho
ya Veronika.
"Sina wasiwasi na Serikali ya Tanzania kuhusika
na tukio hili, lakini ili niwe na uhakika vile vile ni
lazima nichunguze upande huo vile vile. Msinielewe
vibaya, mimi ni mtu ambaye mara kwa mara
hupenda kuchunguza mambo na nipatapo ukweli
nang'ang'ania kwenye ukweli. Sijui mumenielewa?".
"Mimi nimekuelewa kuwa utakuwa na uhakika tu
kuwa Tanzania haijahusika utakapopata ukweli wa
jambo lilivyo", Veronika alijibu.
Sikazwe alisita tena.
"Kitu kama hicho. Mnajua sisi wapigania Uhuru
tuko katika hali ya kutatanisha sana. Kwa sababu
serikali za nchi huru za Kiafrika unakuta moja
inapendelea chama hiki nyingine chama kile maana
sisi tuko vyama vingi. Hivyo ili kuamua jambo hili
ni lazima uangalie mambo mengi", alijibu.
"Kama nimekuelewa vizuri unatupa tena hali ya
tatu kuwa huenda si Tanzania wala mabeberu
waliohusika katika njama hizi ila inaweza kuwa
nchi mojawapo katika nchi huru za Kiafrika",
nilisema.
"Nafikiri sasa umenipata".
Sisi tuliangaliana kwa mshangao kwani fikra hii
ilikuwa haijaingia vichwani mwetu.
"Vizuri tumejua msimamo wako", nilijibu.
"Kwa hiyo ili niweze kuwapa msimamo wangu
kamili mnipe muda ili niweze kutuliza mawazo
yangu baada ya kuzungumza na watu fulani".
"Unamjua kijana mmmoja aitwae George Kiki",
Sherriff aliuliza.
Sura ya Sikazwe ilionyesha mshituko ambao ni mtu
kama mimi tu ambaye angeweza kuona.
"Ndio ninamkumbuka aliwahi kuja hapa ofisini
kwangu akiwa mkimbizi kutoka Afrika Kusini baada
ya matatizo ya Soweto. Na sisi huwa ni wajibu
wetu kama chama cha wapigania uhuru
kuwasaidia. Tokea siku hiyo mpaka leo sijapata
kumwona tena. Je ana nini?".
"Amekutwa ameuawa nyumbani kwake", Sherriff
alimjibu.
Sikazwe alionyesha hali ya mshangao.
"Nimesikitishwa sana; alionekana kijana mzuri".
Simu ililia Sikazwe akaichukua.
"Sikazwe hapa".
Akaisikiliza kwa muda halafu akajibu. "Sawa,
nakuja sasa hivi".
Akakata simu.
"Sijui mna maswali zaidi maana nahitajiwa ofisi za
Ubalozi wa Botswana kwani kesho kutwa nina
safari ya kwenda huko kuonana na wanachama na
wanajeshi wangu walioko huko".
Tulitazamana tukaona hakuna zaidi.
"Nafikiri inatosha, tukikuhitaji naamini utakuwa
tayari kutuona kabla hujaondoka".
"Bila shaka".
Tulisimama, tukapeana mikono na tukaagana.
Tulitoka na kuingia ndani ya ofisi ya mwandishi
wake.
"Hujambo mrembo, maana hatukusalimiana wakati
tunaingia kwani tulikuwa katika haraka",
nilimsalimu.
"Mimi sijambo", alijibu huku bado anatuangalia kwa
macho ya kushangaa.
Tulimwacha ashangae tukatoka nje ya ofisi na
kuelekea mapokezi. Hapo tulimkuta yule msichana.
"Siku nyingine ukitukatalia utafukuzwa kazi.
Angalia vizuri sana sura hizi maana sidhani
utapata kazi mahali pengine wanakochukua muda
kujirembua wakati wa kazi. Hivyo chunga kazi
yako", nilimshauri.
"Si nikikosa kazi kwa sababu yako nitakutafuta".
"Nani atataka msichana wa kujirembua huku
chungu jikoni kinaungua nyumbani kwake?".
Msichana yule alivimba, tukaona tuondoke kabla
hajapasuka. Tulipotoka nje tulielekea moja kwa
moja kwenye gari letu tayari kwa safari ya mjini.
Ghafla nikasikia sauti.
"Bosi, rukeni ua".
Kama umeme tuliruka na kuanguka chini upande
mwingine wa ua wakati ambapo risasi zilimiminika
pale pale tulipokuwa tumesimama.
"Nenda ofisini", tulisikia sauti ya Eddy ikiamru.
Kama umeme tuliruka na kuangukia mapokezi
wakati tuliposikia mlipuko mkubwa wa bomu
uliotingisha hata ofisi za SANP.
Baada ya dakika-mbili hivi Eddy alisimamisha gari
lake mbele ya mlango na kuamru twende. Kama
risasi tuliingia ndani ya gari na kuondoka kasi na
kuacha gari langu likiwa limesambazwa vipande
vipande.
ITAENDEEEEEEEEEEEa
 
NJAMA
SURA YA SABA
BINTI TANZANIA
"Lo, hiyo ilkuwa alimanusura", veronika alisema
huku jasho likimtoka na akihema.
"Nakuambia", Sherriff naye huku akihema.
"Eddy, moja kwa moja nyumbani kwangu, akili
yangu imevurugika", nilimwambia Eddy aliyekuwa
akiendesha kwa kasi sana.
"Huyu Eddy ni nani na katokea wapi?, maana bila
yeye sasa hivi sote tungekuwa maiti", aliuliza
Sherriff.
"Katika kazi hizi Komred Sherriff lazima uwe na
plani bila plani huenda mimi ningekuwa nimeuawa
siku nyingi. Huyu kijana ni mfanyakazi mwenzetu,
na toka asubuhi yuko pamoja nasi lakini kazi yake
ilikuwa ni kutulinda sisi. Na kwa jumla ndivyo hivyo
tunavyofanya kazi".
Eddy alisimamisha gari mbele ya nyumba yangu.
Tulitelemka ndani ya gari, nikafungua mlango
tukaingia sebuleni wote na kuketi. Nilikwenda
katika barafu na kutoa chupa ya whiski na chupa
za soda kali. Nilitenga glasi, wote wanne tukaanza
kunywa. Nilipoangalia saa ilikuwa saa tisa kasoro
robo.
"Eddy nafikiri hatuna muda wa kupika hapa
nyumbani, hivyo nenda Palm Beach Hoteli
wakakufungie chakula cha watu wanne",
nilimwambia Eddy".
"Sawa".
Eddy aliondoka kwenda kutafuta chakula.
"Willy, watu hawa wamepania sana", Sherriff
alisema kwa sauti nzito.
"Mimi nilijua watapania, ndio sababu nikaweka
tahadhari yote hii. Ngoja Eddy arudi atueleze
ilikuwaje mpaka wakaweza kutufuata mpaka pale
walipotushambulia. Ni bahati nzuri sana kwamba
wote mna mafunzo ya kijeshi hivi mlitii amri za
Eddy bila hata kufikiri. Jambo hili limenifurahisha
sana maana kama mtu angesita, sasa hivi
tungekuwa tunamuombolezea".
"Naona wote tumejenga silika ya hali ya juu kwa
wakati wa namna hii", Sherriff alijibu.
"Tukimsubiri Eddy, sijui mmewaonaje hawa Maraisi
wa vyama hivi vile vile", Veronika aliuliza.
"Mimi moja kwa moja nimempenda Chimalamo
maana ni mtu aliye wazi. Nafikiri ni kiongozi
mwenye busara. Kutokana na maelezo aliyotupa
nafikiri anajua anafanya nini, na mtu kama huyu
anaweza kabisa kuendesha harakati za ukombozi
dhidi ya Makaburu maana anawajua nje na ndani.
Ukikumbuka mazungumzo yetu siku ile huko
Freetown juu ya Afrika Kusini sasa ukiongeza haya
aliyotupasha ndugu Chimalamo hata wewe unazidi
kupata mwanga mkubwa juu ya Afrika Kusini. Kwa
ujumla nafikiri Chimalamo ni kiongozi mzuri na
halisi. Juu ya Sikazwe nina dukuduku nae moyoni,
maana sikumwelewa sawasawa sababu si mtu
wazi. Hata nidhamu ya ofisi yake ilivyo kabla
hujaonana naye, inaonyesha kasoro fulani. Nafikiri
bila Willy kuwa mtu anayejua mbinu nyingi
tusingemwona maana mbinu aliyotumia mimi
mwenyewe mkufu. Halafu kuna kitu fulani ndani ya
Ndugu Sikazwe ambacho sijui ni nini lakini
kinanidundadunda sijui wenzangu mmemuonaje?",
Sherriff alieleza.
"Nafikiri mawazo yako na ya kwangu hayako mbali.
Nakubaliana na wewe kuwa Ndugu Chimalamo ni
kiongozi mzuri. Na vile vile kuhusu Sikazwe hata
mimi kuna kitu fulani ambacho sikukielewa ni nini
kilicho ndani yake, lakini huenda nitakijua nikipata
muda mrefu kufikiri. Lakini huenda ni mtu wa tabia
ya namna hiyo, na kwa namna yake hiyo anaweza
kuwa ni kiongozi mzuri zaidi kuliko hata
Chimalamo. Huenda kila kitu kilicho ndani yake ni
uongozi bora", nilieleza.
"Mimi sina la kuongeza, naona mawazo yetu
yameoana", Veronika alijibu.
"Kusema kweli jamani sijastuka kama leo, kweli
tumeponea chupu chupu, asante sana Willy kwa
kuweka tahadhari".
"Bila asante Vero, maana ni kazi yangu kuhakikisha
usalama wenu na wangu, hivyo uwe na amani
kuwa nitafanya kila jitihada kuhakikisha usalama
wetu, kama nikishindwa itakuwa nje tu ya uwezo
wangu".
"Naomba sigara", Sherriff aliniambia.
"Hapa mimi nina aina ya sigara iitwayo Tropicana,
sijui kama itakufaa".
"Wewe nipe tu, sigara zangu ziko hotelini. Baada
ya kashikashi nahitaji sigara kama kufa".
"Nilitoa pakiti ya Tropicana nikaiweka mezani
tukaanza kuivuta.
"Lo, mbona sigara safi kabisa, ni sawa sawa tu na
555, zinatengenezwa wapi?", Sherriff aliuliza.
"Hapa hapa nchini kwetu".
"Lo, mmeendelea sana, mnaziuza na nje?", aliuliza
Veronika ambaye naye alichukua moja akavuta
ingawaje hakuwa mvutaji sana.
"Sijui maana wameanza kuzitengeneza hivi
karibuni, lakini naamini watafanya hivyo".
Mara Eddy akawa amerudi tukapata chakula
ambacho tulikishambulia vizuri sana maana njaa
zilituuma vibaya.
ITAENDELEA...
 
NJAMA
SURA YA SABA
BINTI TANZANIA
II
Baada ya kula chakula cha mchana tulikaa kitako
kumsikiliza Eddy, akitusimulia jinsi mambo
yalivyotokea pale SANP.
"Baada ya nyinyi kuondoka kwenye ofisi za PLF,
nilingoja hadi nikaona gari Peogeot 504 namba TZ
311251 likijitokeza kwa upande mwingine na dereva
wake akichungulia kwenye kioo cha kuendeshea
baada nafikiri ya kuona hakuna gari zaidi lililokuwa
nyuma yake; liliongoza kufuata njia mliyofuata.
Mimi nililitilia mashaka nikalifuata nyuma baada ya
magari kama mawili hivi kuwa kati yangu na gari
hilo. Gari hilo pia lilikuwa limeacha magari matatu
kati yake na gari lenu. Tulifuatana hivyo hivyo
mpaka kwenye taa za usalama barabarani za
Jangwani.
"Hapo ndipo nilihakikisha kuwa huenda gari hili
lilikuwa na jambo. Mlipoingia barabara ya Umoja
wa Mataifa gari hili lilisita kidogo mpaka gari
zingine zikalipigia honi kwani taa zingebadili kabla
hatujapita. Inaonekana kulikuwa na ubishi. Baada
ya hapo gari hili liliingia barabara ya Umoja wa
Mataifa nami nikalifuata. Niliona nyinyi
mnasimamisha gari kwenye ofisi za SANP.
Nilitelemka na kufungua boneti ya gari langu
kwamba limeharibika, huku nikifikilia kuwa lile gari
litarudi.
"Nilichukua spana na kuanza kujifanya
ninalishughulikia gari langu. Gari lile halikurudi.
Mimi niliendelea kujishughulisha hivi kiasi cha nusu
saa, wakati nyinyi bado mko ndani ya ofisi. Mara
nilistukia gari moja linaingia pale gereji, kwa bahati
lilisimama karibu tu na mimi. Ndani ya lile gari
mlikuwa na watu wanne. Dereva wa gari hili
alitoka na kuingia ndani ya ofisi ya gereji hii.
Alikuwa amevalia vizuri sana. Nilimwangalia kwani
alikwenda akazungumza na mfanyakazi aliyekuwa
amekaa mezani akiandika risti na simu iko upande
wake. Alizungumza na mtu huyu wakabishana
kidogo kisha nikaona anatoa kitu kama shilingi
moja akampa yule mfanyakazi. Halafu yule
mfanyakazi akachukua funguo na kufungua kufuli la
kwenye simu. Yule mtu akapewa simu akaanza
kupiga. Mambo yote haya niliyaangalia kwa chati
huku nikiendelea kujishughulisha na gari langu".
Eddy alitua akachukua sigara nikamwashia,
akavuta kidogo kisha akaendelea.
"Sura za wale watu wengine ndani ya gari
hazikuwa za kawaidana vile vile walikuwa na
wasiwasi. Kila mara walikuwa wakigeuka kuangalia
upande wa SANP. Yule mwingine alipomaliza
kuzungumza na simu alikuja moja kwa moja
akaingia ndani ya gari na kulizungusha. Mimi pale
pale nikafunga boneti ya gari langu, maana tayari
akili yangu ilikuwa imeshakuwa katika hali ya
tahadhari nami nikageuza gari langu kuangalia
barabarani. Hapo ndipo niliona mnatoka nje ya
ofisi. Nikaona mmoja wa watu wale katika gari
anainua "machine gun" kutoka chini na kabla
hajaweka sawa nyinyi mlikuwa mmefika kwenye
gari. Niliruka toka ndani langu na kuwapigia kelele.
Nashukru kuwa mlinitii mara moja, kwani wakati
ule ule mliporuka alimimina risasi pale pale
mliposimama nikajua alikuwa mtu mwenye shabaha
ya hali ya juu kwani gari lilikuwa likienda polepole.
"Mliporuka tu niliona mtu mwingine anatoa bomu la
mkono na kuuma kifungo chake. Hapo ndipo
nilipopiga kelele ya pili kisha nikarukia ndani ya
gari wakati yule mtu anatupa hilo bomu na gari lao
linaondoka kwa kasi. Ndipo na mimi nikaja na
kusimamisha gari langu pale mlangoni baada ya
ule mlipuko wa lile bomu. Pole sana bosi gari lako
zuri sana limeteketea".
"Siku Eddy, nitapata jingine aina hiyo hiyo,
nimetokea kupenda sana aina hiyo ya magari.
"Lo, inaonekana watu hawa wamejitayarisha vizuri
sana", Veronika alisema kwa mshangao.
"Toka niliposikia jinsi walivyoiba zile silaha sikuwa
na hamu nao tena. Nilijua ni watu wanaojua
wanafanya nini. Ndio sababu niliwaasa hatari
zitakazotokea toka mwanzo. Nafikiri sasa
mnaamini mawazo yangu", hakuna aliyejibu; wote
walinyamaza tu. Nafikiri walikuwa wakijutia kwa
nini wamejiingiza katika janga hili.
"Vipi Eddy umepata habari zozote juu ya Kiki?",
nilimwuliza.
"Kama nilivyokuahidi nimepata habari za kutosha".
Sisi wote tukawa tena tayari kumsikiliza huyu
kijana na kusahau yote yaliyopita.
"Ehee hebu lete habari", nilimwambia.
"Nitaanzia toka ripoti nilizopata toka kwa
makomredi wetu wa Soweto. Makomredi wetu huko
wanakataa katakata kuwa hakukuwa na mtu
mwenye jina au wa sura kama nilivyowaeleza huko
Soweto. Wanasema mtu aliyetoroka gerezani kati
ya wale waliokamatwa na kutiwa ndani, yuko huko
huko Soweto na wanaye sasa hivi. Hivyo ni uongo
mkubwa kuwa huyu mtu alihusika na matatizo ya
Soweto. Inasemekana kuwa mara ya kwanza mtu
huyu kuonekana Tanzania ni wakati alipofika Mbeya
akiwa na hiyo hadithi yake kuwa ametoroka
gerezani huko Afrika Kusini baada ya kutiwa ndani
kutokana na machafuko ya Soweto. Habari hii
aliitoa kwa ofisi ya Chama huko Mbeya na ofisi
hiyo ndiyo iliyomleta Dar es Salaam baada ya
kusema kuwa yeye ni mwanachama wa SANP.
Hivyo alipofikishwa hapa alipelekwa kwenye ofisi
za SANP ambako inasemekana aliwaonyesha kadi
yake, hivyo katika hali ya kumsaidia wakampeleka
kwenye Kamati ya Ukombozi ya OAU.
"Je umepata habari zozote kuhusu maisha yake
hapa mjini".
"Ndiyo, vijana wetu wamefanya kazi nzuri sana.
Wameweza kupata habari kuwa Kiki alikuwa mtu
asiye na rafiki. Ila alikuwa na rafiki mmoja wa kike
Mtanzania anayeitwa Zabibu Abeid. Wanasema
msichana huyu aliingia hapa mjini toka Tanga miezi
minne iliyopita kwani alikuwa amepatiwa kazi na
Meneja wa Kampuni iitwayo Twiga Safari ambayo
inashughulikia mambo ya watalii. Msichana huyu
amesoma mpaka kidato cha Nne alichomaliza
mwaka jana. Anasemekana kuwa na uuzuri wa
pekee. Katika ripoti yao wanasema kuwa kama
hujamwona msichana huyo basi hujamwona binti
Tanzania. Hivyo baada ya Kiki kufanya urafiki na
msichana huyu mrembo, muda wake na maisha
yake aliyatoa kwa msichana huyu.
"Zababu anakaa mtaa wa Jamhuri, kwenye orofa
karibu ya mzunguko wa mtaa wa Zanaki na
Jamhuri. Yuko mwenye nyumba ya orofa ya Msajili
wa Majumba. Jengo Nambari K orofa ya tatu,
nyumba nambari 7a. Nyumba hii amepewa na
waajiri wake. Inasemekana kuwa fanicha yote ya
mle ndani imenunuliwa na Kiki pamoja na gari moja
zuri aina ya Ford Mustang"
"Na huku Kiki alikuwa tarishi tu... nilimkata kauli
Eddy.
"Ofisini alikuwa tarishi, lakini nje alikuwa na fedha
nyingi za kutosha. Hivyo kwa nje alikuwa ofisa wa
mkubwa katika Kamati ya Ukombozi ya OAU".
"Na ndio sababu aliweza kumpata msichana
mrembo kiasi hicho?", Sherriff aliuliza.
"Bila shaka maana sura ya Kiki ilikuwa ya
kupendeza sana hivyo sioni ajabu kumpata
msichana mrembo kiasi hicho".
"Kwa hivyo zaidi ya msichana huyu maisha ya Kiki
hapa mjini hayaeleweki".
"Ndiyo, Kiki hakuwa na rafiki mwingine zaidi ya
Zabaibu, lakini muda mwingi alikuwa kwa Zabibu.
Tumejaribu sana kupata habari nyingine zozote juu
yake lakini tunashindwa. Huenda Zabibu anaweza
kujua".
"Okejamani nafikiri nyinyi mnaweza kurudi
matotelini kwenu. Ila mjihadhari sana maana hali
ya sasa ni ya hatari, nitakuja kuwaona baadaye
msitoke mpaka nimekuja. Eddy atawapeleka
mkapumzike. Mimi nitakwenda kumwona Zabibu
sasa hivi, nafikiri atakuwa ametoka kazini",
niliwaeleza.
"Nafikiri atakuwa amerudi maana anatoka kazini
saa kumi kamili", Eddy alinieleza.
"Twende wote", Veronika alinieleza huku
akiniangalia kwa macho ya wizi.
"Hapana wewe nenda ukapumzike, kazi uliyofanya
mpaka sasa inatosha. Usiwe na wasiwasi
nitajiangalia".
Veronika alikuwa haamini kwenda kuonana na
msichana mrembo namna hiyo peke yangu. Hiyo
ndiyo ya kazi na dawa.
Waliondoka wakaniacha mimi nikienda maliwatoni.
Baada ya kukoga na kubadili nguo, niliangalia saa
yangu nikaona ni saa kumi na moja na nusu.
Nilichukua bastola yangu nikaiweka ndani ya jaketi
nililovaa, nikajiona nilikuwa tayari kupita kiasi
kuonana na Binti Tanzania. Nilitoka nje nikafungua
mlango, nikaenda mpaka Palm Beach ambako
nilichukua teksi kunipeleka kwa Binti Tanzania.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA SABA
BINTI TANZANIA
III
Ilikuwa yapata saa kumi na mbili wakati dereva wa
teksi aliponishusha hatua chache kabla ya kufika
kwenye mzunguko wa Mtaa wa Jamhuri na Zanaki.
"Hapo hapo pananitosha", nilimweleza huku
nikimpa shilingi ishirini kisha nikatelemka.
Niliangalia kwenye maegesho ya mtaa huu wa
Jamhuri nikaiona gari ya Zabibu. Ilikuwa gari ya
rangi ya kijani ambayo haikuiva sana, na ilikuwa ni
aina ya Ford Mustang muundo wa kisasa. Kama
umeshaiona Ford Mustang zilizoundwa vizuri basi
hii ilikuwa mojawapo. Hata mimi niliipenda kwa
umbo lake maana ilikuwa na milango miwili. Yaani
'Ford Mustang Sports Car', kama wanavyoiita
wenyewe walioitengeneza.
Kule kuona gari hii kulinihakikishia kuwa Zabibu
alikuwepo nyumbani, niliangalia jengo, nikaangaza
huku na huku kuona kama kuna mtu ananifuata,
nikaona hakuna. Kila mtu alionekana kuwa na
hamsini zake. Basi mimi Willy nilijipenyeza kwenye
lango linaloelekea kwenye ngazi za jengo hili.
Nilipofikia ngazi nilianza kupanda taratibu kama
mtu anayejua anapokwenda. Nilipanda mpaka orofa
ya tatu, na nyumba iliyokuwa inatazamana na
ngazi hizi ilikuwa namba 1a na nikajua 7a itakuwa
mkono wa kulia hivyo nikafuatia taratibu.
Kwa sababu giza lilikuwa linaingia nyumba zingine
zilikuwa zimewasha taa na zingine zikiwa giza
kuonyesha wenye nyumba walikuwa bado
hawajafika. Nyumba namba 5a na 6a zilikuwa giza
ila 7a ilikuwa inawaka taa sebuleni. Nilitembea
taratibu bila kupiga kelele mpaka kwenye mwisho
wa namba 6a, niliposikia sauti ya msichana inapiga
kelele ndani ya namba 7a. Harafu nikasikia sauti
ya mwanaume.
"Mimi nisingependa kukuua Zabibu maana mimi
nafurahia uumbaji wa Mungu mzuri aliokuumba
lakini mimi nimeamriwa nikuue hivyo sina njia.
Nisipokuua wewe, mimi nitauawa. Hivyo huna haja
ya kupiga kelele, kufa hakika utakufa".
"Kwani mimi nimekosa nini masikini?", msichana
aliuliza.
"Hata mimi sijui, haya kwa...".
Mimi nilikuwa nimejivuta na kuwa sawasawa na
mlango wa hii nyumba, hivyo nilisikia mazungumzo
haya. Niliona nikichelewa msichana huyu anaweza
kuuawa. Basi nilitudi nyuma, bastola mkononi,
niliurukia ule mlango na kuupiga teke ukafunguka.
Hapo hapo mimi nikatumbukia ndani nikitanguliza
kichwa chini lakini nikafyatua bastola na kumpata
yule kijana niliyemuona ameshika kisu chenye
mpini mwekundu. Ile risasi ilikuwa haikumpata
vizuri hivi alisimama wakati na mimi
nimeshasimama yakaanza masumbwi. Alitupa
konde moja likanikosa mimi nikampa shoto langu
lililompata shingoni akaenda chini na hakusimama
tena.
Mambo haya yalitokea kwa muda mfupi sana.
Zabibu alikuwa amepigwa na butwaa kiasi cha
kwamba yule mtu alipoanguka chini na yeye
akaanguka juu ya kochi na kuzirai. Nilienda
kumwangalia yule mtu pale chini, sikuwa na haja
hata ya kumgusa ili nijue kama amekufa. Niliona
kulikuwa na barafu pale sebuleni, nikaifungua
nikatoa chupa ya maji baridi nikammiminia Zabibu
naye akashituka.
"Kweli huyu Zazibu alikuwa ndiye Binti Tanzania.
Mimi nimeona warembo katika nchi hii, lakini huyu
alikuwa ni zaidi. Ukiwa unaamini kuwa kuna
binadamu wengine hushushwa moja kwa moja toka
mbinguni, basi Zabibu alikuwa mmoja wao, kwani
mpaka sasa siamini kama msichana huyu alizaliwa
na binadamu. Ingawaje haiwezekani kuamini kuwa
mtu anaweza kutelemshwa toka mbinguni, lakini
ukimwona Zabibu wewe mwenyewe utaona
uwezekano. Maana hata mimi niliona inawezekana
kwa huyu kiumbe wa binadamu alikuwa ameumbwa
bila kasoro. Palipo ukweli lazima tuseme;
mwenzetu alikuwa na uzuri sio kifani. Mcho yake
manene ya mviringo yaliyozungukwa na nyusi
zenye rutuba yalifunguka na kuniangalia mimi.
"Umetoka wapi?", aliuliza kwa sauti nyororo
iliyotoboa rohoni mwangu kama miali ya moto.
"Nimekuja kukuokoa".
"Kama wewe si mmoja wao umejuaje kuwa
amekuja kuniua?".
"Kama mimi ni mmoja wao kwa nini nimwue wakati
anataka kukuua?".
"Ndicho kinachonishangaza".
"Basi mimi si mmoja wao, mimi ni rafiki yako.
Kama una akili timamu tuondoke hapa chumbani
kwako maana kinanuka mauti".
"Sijui kwa nini naona kama ninakuamini".
"Kwa sababu ndio jambo la busara".
"Haya nichukue, nitoe hapa, yule mtu kweli
angeniua. Huenda lazima nikushukuru, asante
sana?".
"Bila asante, msichana kama wewe una haki ya
kuokolewa, huna haja ya kushukuru, hiyo ni haki
yako".
"Na huyu mtu tutamwacha humu?".
"Nitafanya mipango aondolewe, simu iko wapi?".
"Chumbani".
Aliniongoza chumbani, nikapigaa simu ofisini
nikamkuta Eddy nikamweleza kwa kifupi, kisha
nikamwambia afanye mpango mtu huyu aondolewe
hapa. Eddy akasema atatekeleza.
"Wewe ni polisi?", Zabibu aliuliza.
"Hapana".
'Sasa wewe ni nani?".
"Mimi ni mtu ninayesaidia warembo kama wewe".
Nilimjengea tabasamu babu kubwa kisha nilimshika
mkono tukazima taa, nakurudisha mlango, halafu
tukaondoka. Nilipata teksi pale chini, tukapanda na
kumwelekeza dereva nyumbani kwangu.
"Tunakwenda wapi?", Zabibu aliuliza.
"Nyumbani kwangu, unaonaje?".
"Nakuona wewe ni mtu wa ajabu ajabu tu,
usingekuwa umeniokoa nisingekuamini hata
chembe!.
Nilikuwa nimeingia na mashaka makubwa kwenda
moja kwa moja nyumbani kwangu. Nilikuwa sijui
kwa nini, hivyo nikabadili mawazo na kumwelekeza
teksi dereva twende Ocean Road ambako ndiko
Eddy alikuwa akikaa. Nilikuwa nina ufunguo mmoja
wa nyumba yake kwa ajili ya nyakati kama hizi.
Tulikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa
Eddy baada ya kumwelekeza dereva nyumba.
Nilimlipa dereva teksi pesa zake, halafu
tukatelemka. Nilifungua mlango kisha nikawasha
taa.
"Karibu ndani bibie".
Asante sana".
Nilikwenda kwenye barafu nikaifungua.
"Sijui utakunywa nini?".
"Baada ya vituko vilivyotokea nafikiri whiski na
soda kali vitanifaa".
Nilichukua chupa ya whiski na soda kali halafu
nikaendea glasi na kumimina kwenye glasi mbili ya
Zabibu na ya kwangu halafu tukainua glasi zetu.
"Na tunywe kwa maisha yako marefu mrembo",
nilisema.
"Na tunywe", alijibu kisha akanywa whiski ile
haraka haraka.
Mimi nilikwenda kwenye simu nikapiga tena ofisini
nikampata Eddy. Nilimpasha habari kuwa mimi na
huyu mrembo Zabibu tulikuwa nyumbani kwake. Na
yeye vile vile akanieleza juu ya kazi niliyokuwa
nimemuagiza; vijana walikuwa wamempigia simu
kuwa tayari walikuwa wameshaifanya.
Nilimpongeza kwa jinsi kazi yake alivyokuwa
anaifanya haraka kwa juhudi na maarifa.
"Nafikiri kwanza itabidi tufahamiane", nilimweleza
Zabibu.
"Hasa ndilo litakuwa jambo la maana", alijibu.
"Mimi naitwa Willya Gamba, sijui wewe mwenzangu
unaitwa nani?".
"Mimi naitwa Zabibu Abeid".
"Lo kweli aliyekuwa jina la Zabibu alijua kweli,
kwani mimi naamini umtamu kama Zabibu".
"Ndio unataka kusemaje?".
"Nataka kusema wewe ni msichana mrembo
ambaye sijawahi kumwona, na bila shaka aliyekuwa
jina la Zabibu alijua utakuwa mtamu kama Zabibu".
"Usinivike kilemba cha ukoka. Kijana nadhifu
mwenye sura nzuri na vituko vingi namna hii,
haiwezekani kuwa haujamwona msichana mrembo
kunizidi".
"Amini usiamini".
"Asante, lakini hata mimi leo nimemwona mvulana
wa kipimo changu, sijui ulikuwa umejificha wapi mji
huu hata nisikuone?".
"Mimi nilikuwepo nimejaa tele hapa mjini, lakini
najua ingekuwa vigumu kuniona maana George Kiki
alikuwa amekuganda kama kupe".
Pale pale sura yake iligeuka akainua macho yake
marembo kunitazama machoni. Mimi nikamjengea
tabasamu la sheria yake, Zabibu alionekana
alikuwa amechanganyikiwa mawazo.
"Unajua nini juu ya George?".
"Hakuna haja ya kuzungushana sana, nafikiri
inabidi sasa tuelezane ukweli. Na kabla
hatujaendelea mbali ningependa kukuuliza lini
umeonana na Kiki kwa mara ya mwisho".
Kwa kutokana na uzito wa sura yangu, Zabibu
alilegeza sura yake kisha akajibu kwa sauti
nyororo.
"Siku nne zilizopita, alisema atakwenda safari
Botswana na atarudi baada ya wiki tatu".
"Na hauna habari nyingine yoyote kuhusu yeye?".
"Sina, kwani kumetokea nini?".
"Kwani yule mtu aliyetaka kukuua alikuwa
amekueleza nini?".
"Hata, alinieleza tu kuwa alikuwa ametumwa kuja
kuniua ingawaje yeye hakutaka lakini alikuwa
amelazimishwa. Hakunieleza kabisa sababu.
"Nakuomba uwe na roho ngumu, rafiki yako George
Kiki ameuawa jana. Maiti yake ilikutwa chumbani
mwake ikiwa imechomwa kisu chenye mpini
mwekundu".
Nilitoa kisu nilichokuwa nimekiokota nyumbani kwa
Zabibu kabla hatujaondoka.
"Na watu wale wale waliomwua ndio walikuwa
wanakuja kukumalizia wewe".
Zabibu alibubujikwa machozi na kidogo azirai tena.
"Lazima ujitulize kwa sababu mimi niko hapa
kupeleleza mauaji ya mpenzi wako".
"Mimi nilijua tu wewe ni Polisi. Sura yako na
namna ulivyoingia chumbani kwangu sijapata
kuona kwa macho ila ndani ya sinema tu. Zile
sinema za kijasusi".
"Mimi si polisi bali ni mpelelezi. Huenda polisi nao
wakaja kufanya upelelezi wao, lakini mimi bahati
nimewahi na kukuokoa huenda wao wangefika
wakati wewe umekwisha kuwa maiti".
"Una maana gani kusema wewe ni mpelelezi wala
si polisi?".
"Mimi ni mpelelezi wa siri kama umewahi kusikia
watu kama hao".
Macho ya Zabibu yakapanuka.
"Usije ukawa wewe ndiye mtu ambaye huwa
tunasoma habari zake kwenye magazeti
akipambana na majasusi mbali mbali wanaofanya
maovu dhidi ya Afrika".
"Ndio mimi".
Zabibu aliruka pale alipokaa akaja katibu na mimi.
"Ooh! Mungu ni bahati gani kuonana na mtu kama
wewe maana mimi nilikuwa nafikiri ni maneno ya
uzushi tu ya magazeti maana walikuwa hata
hawatoi jina. Kila mara ukisoma unaona tu vijana
wa Afrika wakiongozwa na mpelelezi mashuhuri
kutoka Tanzania wamefaulu katika kuwateketeza
majasusi ya mabeberu yaliyokuwa yanatenda
mambo maovu dhidi ya Afrika. Nitawaeleza rafiki
zangu kuwa ni kweli huyu mtu yupo na mimi
nimeonana naye".
"Halitakuwa jambo la busara, tafadhali fanya hii
iwe siri kati yangu na wewe, nimekueleza tu kwa
sababu unaweza kunisaidia katika upelelezi wangu
juu ya tukio la kutisha lililotokea hapa mjini siku
chache zilizopita".
"Ahaa nimeelewa tumesikia kwenye maredio ya
nchi za nje, kuwa silaha kali za wapigania uhuru
zimeibiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam".
"Basi umebashiri sawa".
"Sasa George ana uhusiano gani na tukio hili?".
"Ndio sababu tumekuja kukuona, huenda ukajibu
maswali yangu nitaweza kuambulia jambo lolote
linalomwunganisha Kiki na tukio hili".
"Niko tayari kukusadia, kwanza kwa sababu
umeniokoa, pili kwa sababu unapeleleza kifo cha
mpenzi wangu na tatu nafikiri wewe ni kijana
mwenye kupendeka".
"Asante, swali langu la kwanza nilitaka kujua kama
ulikuwa unajua Kiki ni mtu wa Afrika Kusini?".
"Nilikuwa najua".
"Alikwambia alikuwa akifanya kazi gani?".
"Alisema yeye ni mwakilishi wa chama cha SANP
katika Kamati ya Ukombozi ya OAU".
Nilishangazwa na jibu hili lakini sikuonyesha.
"Kwa hiyo mara nyingi alipokuwa anakuja kwako
alikuwa akiandamana na wanachama wenzake wa
SANP?".
"Hapana, George alikuwa mtu wa pekee, huenda
ndio sababu nilimpenda. Alikuwa kila siku
ananiambia kama ninataka kuepukana na matatizo
nisizoeane na watu wengi. Na yeye kweli alikuwa
hakuzoeana na watu. ila alikuwa na marafiki wawili
tu. Ndugu Ray Sikazwe, rais wa SANP na Patlako
Shuta ambaye ni ofisa mkubwa katika SANP.
Sikumwona na mtu mwingine. Oh, kidogo nisahau,
vile vile walikuwa na rafikio yao mwingine Mzungu
ambaye George alifahamishwa kwake na Sembuche
na mwenzake Shuta. Na hata gari nililo nalo,
George aliuziwa na Mzungu huyu. Kwa vile yeye
alikuwa hapendelei gari kwani alikuwa anatumia
gari la ofisini alinipa mimi".
Kwa mara ya kwanza niliona mwanga kwa mbali,
na nikajua kwa nini msichana huyu alitakiwa
auawe. Nilijivunia bahati yangu kuwahi kabla
hajauawa.
"Unaweza kujua Mzungu huyu anafanya kazi
gani?".
"Lo! hawa ndio wenye lile kampuni kubwa lililo na
makampuni kadha wa kadha katika nchi nyingi za
kiafrika yaani EUROAFRO Limited. Na huyu Mzungu
ndiye mwakilishi wa kampuni hilo hapa akiangalia
akiangalia makampuni yake madogomadogo
yaliyoko hapa".
Kapuni hili EUROAFRO Limited lilikuwa kampuni
kubwa la kibepari lililokuwa na hisa nyingi katika
makampuni katika nchi nyingi za Afrika. Kirefu
chake kilikuwa EUROPE - AFRIKA COMPANY.
Uhusiano huu kati ya wanachama wa chahama cha
wapigania uhuru na kampuni ya kibepari ulinishinda
kuelewa.
"Kwa hiyo unasema huyu Sikazwe na Shuta
walikuwa marafiki wa karibu sana wa Kiki
"Ndiyo, hao ndio alikuwa anatembea nao mara kwa
mara na vile vile walikuwa wanajuja kumwona au
kumchukua pale kwangu mara kwa mara. Lakini
zaidi ya watu hawa wawili na yule Mzungu, George
hakuwa na rafiki mwingine".
"Huyu Mzungu unaweza kumkumbuka jina?".
"Ndiyo anaitwa Tony Harrison".
"Hawa marafiki wa Kiki uliweza kuzoeana nao?".
"Kusema kweli, Shuta na yule Mzungu walikuwa
wananiheshimu kiasi cha kutosha lakini Sikazwe
alikuwa wa ovyo sana. Amewahi kunitongoza mara
nyingi na kunitaka nimwache George. Kwanza
alikuwa anajivuna kuwa yeye ni Rais wa Chama na
George alikuwa mtu mdogo tu, na kwamba
msichana kama mimi sikufaa kutembea na George
ila mtu kama yeye. Mimi nilimponda na
kumwambia cheo na pesa havileti mapenzi, ila mtu
anampenda mtu kwa vile alivyo, maana mtu na mtu
ndio wanapendana".
Lakini nakwambia uso wa msichana huyu
unapoonyesha sura ya haya ndipo uzuri wake
unapozidi. Ingekuwa wewe usingevumilia lakini mie
nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi. Nilifikiria
swali jingine nikaona nimepata maelezo ya kutosha
ila nikaamua nimweke zabibu chini ya ulinzi wangu
mpaka hapo baadaye.
Nilikuwa bado nafikiri hivi wakati tuliposikia gari
linapiga breki mbele ya nyumba. Nilitoa bastola
yangu tayari. Mlango ulipofunguliwa na Eddy
akakingia.
"Bosi, twende haraka Veronika amenipigia simu
anasema yuko katika matatizo. Nimekuja sababu
nilijua huna gari", Eddy alisema huku akitweta.
"Oke Zabibu, subiri hapa tutarudi sasa hivi".
Nilifungua mlango kabla Zabibu hajasema neno
lolote.
ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom