NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 088
Usingizi ukaichukua nafasi na kumfanya asisikie kingine tena. Masimba akarudi kwenye usingizi mzito, usingizi ambao ulikuwa ndio tiba kwake.
*****
Giza lilimpokea Teddy ndani ya bagamoyo, hakutaka kuchelewa kuelekea kule alikopanga kuelekea. Ilikuwa ni lazima afike sehemu hiyo katika usiku ule ule. Wana usalama waliosambaa sambamba na Askari Kanzu (CID) hakumshtua wala kumfanya aache kile alichotaka kukifanya. Mkoba begani kwa mwendo wa Twiga akaliacha eneo aliloshukia, sasa alikuwa akiitafuta na hata kuifuata Njia iliyo sahihi ya kumpeleka Huko. Kiunoni alikuwa na bastola sambamba na sehemu nyingine tatu za siri. Moyo wake ulikuwa katika vita nzito ya kumtafuta Mtekaji na hata mtekwaji. Hakutaka kusikia Masimba yupo hai. Alitaka kusikia kifo chake. Hii ilikuwa ni vita ya kuipigania Roho yake. Vita ambayo aliianzisha yeye na pia ataimaliza yeye. Muda huu tayari alikuwa amefika katika maeneo ya kambi ile ya Siri ya mafunzo kwa Majasusi wa Usalama wa Taifa. Akapokewa na macho ya watu wanaomjua na wasiomjua. Hakuongea na yeyote zaidi ya kupita na kuingia Ndani Zaidi. Alitembea ndani ya kambi ile mawazo yakimpeleka moja kwa moja katika namna ya kutoroshwa kwa Masimba ndani ya kambi hiyo. Camera na mitambo mingine ya usalama ilikuwa kila mahali huku mingine ikiwa katika Usiri mkubwa. Ni nani aliyemtorosha Masimba? Ni swali ambalo alijiuliza wakati Akiufungua mlango wa chimba alichokuwa amewekwa Masimba kabla ya kutoroshwa. Ugumu wa chumba hiki kwa muonekano asingeweza kutoroshwa na mtu asiyeijua Idara. Aliyemtorosha Masimba alikuwa ni jasusi mwandamizi na mtu wa ndani sana. Haiwezekani mitambo na Camera za usalama zisinase chochote. Kuna sehemu itakuwa imechezewa tu. Lakini atakuwa nani aliyemtoa humu ndani? Lilikuwa swali ambalo lilimfanya atoke hapo ndani. Sasa alikuwa akielekea chumba kinachoongoza mitambo na camera zote. Aliufungua mlango na kuingia ndani. Macho yake yakaenda moja kwa moja kwa vijana watatu waliokuwa wakihangaika huku na huko kuliangalia hilo tatizo. Teddy akawaangalia kwa muda mrefu huku macho yake yakitizama Huku na kule. Aliyazungusha macho yake kila kuta ya chumba kile. Shida yake ilikuwa ni kugundua kile ambacho alitaka kugundua. Hakuona chochote katika kutizama huko. Akaamua kusogea mpaka pale walipokaa Vijana wale. Hakutoa salama bali alichofanya ni kuwauliza. "Nini kinaendelea Hapa?. Vijana wale wakamuangalia kwa muda pasipo kumjibu kitu. Akili zao zilikuwa zimechoka kwa kazi hii. Hakuna aliyetayari kumjibu. Wakamuangalia Kwa Muda Wa dakika moja bila kuongea wala kujibu walichoulizwa. "Hii ni Order kutoka Ikulu mnahitaji kunijibu sio kukaa kimya." Akaendelea kunguruma Teddy. Lakini bado watu hawa waliendelea kumtizama Usoni. Bado watu hawa hawakumjibu. Mmoja akampa ishara ya kusogea pale kwenye mitambo. Teddy akasogea mpaka sehemu Husika. Mmoja kati ya wale vijana akarudisha nyuma mfumo wa matukio ya Jana kuanzia mapema. Teddy akaanza kutizama kwa umakini Zaidi matukio yote ya Awali. Matukio ambayo yalichukuliwa na mifumo ya Kiusalama mle ndani. Licha ya kuangalia kwa Muda Mrefu na kwa Umakini mkubwa bado hakufanikiwa kuona chochote. Harafu Cha ajabu camera hazikuzimwa wala kuchokonolewa popote. Anaonekana aliyeingia alikuwa Jasusi Zaidi Yao, pia alikuwa fundi mkubwa katika masuala yote nyeti. Mtu achukuliwe Ndani ya kambi ya siri ya Idara ya usalama. Harafu hapo hapo mitambo ya usalama isimuone? Lilikuwa ni swali lililomchosha na kumpa wasiwasi. "Huyu ni Zaidi ya Jasusi, huyu ni zaidi yetu. Nimefanya kazi hii kwa miaka kumi na tano lakini sijawahi kukutana na tukio kama hili. Inawezekana Mossad ndio wamekuja kumchukua Kiongozi." Aliongea kijana mmoja Huku akizunguka ndani ya chumba kile. Kila mmoja alikuwa ameshindwa kugundua chochote.
Teddy akatoka hapo muda huu akielekea kwenye vyumba ambavyo walikuwa wakiishi walinzi waliouawa usiku huo. Akiwa amechanganyikiwa huku kichwa chake kikishindwa kufanya kazi vizuri, akalifikia eneo lile. Wakati anataka kuingia ndani ya moja kati ya vyumba hivyo, akaona alama ya kiatu kwenye mchanga. Hakuchanganywa na ile alama tu ya kiatu, kilichomchanganya ni kile alichokiona katikati ya soli zile za kiatu. Hakutaka kuamini kama wana usalama walishindwa kugundua hilo. Katikati ya soli za kiatu kile kulionekana alama zenye ncha mfano wa kisu. Ilikuwa imechimba Ardhini. Moja kwa moja akatambua nini ambacho kilifanyika kwa walinzi. Hawakuchinjwa kwa mkono bali kwa kisu maalum kilichotengenezwa katika viatu maalum Hapo akachuchumaa na kuangalia kwa umakini zaidi. Ni kile kile alichokuwa akikiona. Akawaita vijana watatu wengine waliokuwa karibu. Baada ya kuwaita na kuwaonyesha. Akaongea nao mambo kadhaa wa kadhaa, akaondoka katika viunga vile akielekea sehemu nyingine Kabisa.
*******
Aliuhisi mwanga wa jua ukimmulika Usoni. Taratibu akafumbua macho yake ili kuweza kuliona jua. Macho yakapokewa na Nuru ya mwanga wa Juu la Asubuhi. Jua ambalo lilimpa Joto. Joto ambayo haikuwa kama zile joto nyingine. Kufanikiwa kufumbua macho na kupokelewa na mwanga wa Jua. Kulimpa uwezo zaidi wa kuzungusha macho yake taratibu. Macho yake yakatua kwenye udongo ambao ulionekana kukandikia kijumba hicho. Paa la bati likikuwa karibu kabisa kuonyesha kuwa alikuwa sehemu ya kijijini. Sauti za ndege na wanyama ndizo zilizomuaminisha kuwa alikuwa shamba, alikuwa kijijini ama alikuwa shamba. Akainua macho yake zaidi na zaidi huku akiigeuza Shingo yake. Macho yake yakatua kwenye Bastola. Bastola ambayo ilikuwa Pembeni Mwa Kitanda alicholala. Bastola aina ya MM9. Hilo likamfanya ainuke zaidi huku akiiangalia kwa umakini. Kushtuka kutoka usingizini, kisha kuikuta bastola pembeni take ni kitu ambacho hakikutegemea. Licha ya kutokukitegemea lakini ni kitendo ambacho kilimrudisha kwenye kumbukumbu ya kilichotojea. Akalikumbuka Tukio kuanzia ubalozi wa Marekani na hata kwenda kuwekwanda ndani ya chumba ambacho baadae alikuja Teddy kwa dhamira ya kumuua. Kumbukumbu yake iliishia pale alipochomwa kitu mfano wa Sindano na kupoteza fahamu. Kama ni Hivyo ni kwa nini sasa ameshtuka na kujikuta amelazwa hapa huku pembeni kukiwa na Bastola. Je yupo wapi hapa? Kwa nini ameamka na kujikuta huku? Nani amemuokoa kutoka mikononi kwa Teddy na serikali? Hayo yalikuwa maswali tata. Bado hakuwa na kumbukumbu kama kuna mtu anaitwa Veronica. Mtu ambaye aliamua kuwasaliti wenzake kwa Ajili yake. Mtu ambaye ameisaliti mafia kwa sababu yake. Bado kumbukumbu ya kile kilichofanywa na Teddy kilikuwa kikimuumiza. Teddy huyu ambaye muda wote alihubiri mapenzi. Mapenzi Dhidi ya Masimba. Lakini leo amekuwa Teddy Huyu, teddy ambaye simu yake kwa sasa Inashinda na mwanaume. Mwanaume ambaye hapo mwanzo alisema hamhusu. Jimmy Lambert. Akajitizama na kuitizama bastola tena. Wakati akiliwaza Hilo akamuona Mtu akiingia akitembelea Mkongoja Akionekana kama Babu. Licha ya Masimba kurudiwa na kumbukumbu katika muda ule, bado kumbukumbu zake hazikupotea. Macho yake yalipotua Usoni kwa Babu huyu. Tabasamu na mshangaa pamoja Vikatamalaki. Alikuwa akitizamana na mtu ambaye alimfahamu. Mtu ambaye hapo awali hakujua kama atakuwa yupo katika eneo. Mtu ambaye alimjua. Lakini amefikaje Hapa? Na kwa nini yupo katika mabadiliko haya? Amenipata wapi ama kuniokota wapi? Yalikuwa Maswali, yalikuwa maswali ambayo hakuyapatia Majibu. Wakati akishangazwa na uingiaji wa Huyu Mtu, safari hii akaingia mtu mwingine. Huyu ndiye aliyeufanya Moyo wake uchanue kwa tabasamu. Uchanue kwa furaha na hata uzizime kwa Mapenzi kama sio hisia za Mapenzi. Alikuwa akitizamana na Veronica. Alikuwa akimuangalia mwanamke huyu ambaye ameonyesha kumpigania katika hatari. Furaha iliyoikuwa ikizizima moyoni mwake ilisababisha Ainuke pale Alipolala huku akumita Veronica. Akimuita Veronica kwa sauti ya Kutokuamini. Haikuchukua sekunde moja wakajikuta wamekumbatiana. Veronica alikuwa amelala kwenye kifua cha mwanaume huyu. Walikuwa wakiangaliana kwa macho ya kuitana na hata kuvutana. Macho ya ulegevu na hata macho ya mapenzi. Nyuso zao zikasogeleana huku Kila mmoja akitabasamu. Sekunde hii ya tatu walikuwa wakinyonyana ndimi zao. Ikawa hivyo na hivyo zaidi ya hivyo. Bado babu huyu aliyesimama na mkongojo pembeni alikuwa akiwaangalia. Aliuona Upendo na Hata mapenzi katika nyuso za watu hawa.. "sio wakati wa mapenzi, sio wakati wa kulia katika hili. Mnatakiwa kusimama ili kulimaliza hili. Tayari betri ipo mikononi mwa Rais wa Tanzania. Tayari betri inaendaa kuuwasha mtambo wa kutengenezea Kemikali za kuwaharibu Vijana Taifa hili. Ni wakati wetu kujaribu kulizuia hili." Aliongea Veronica Akijiondoa Mwili kwa masimba. Kujiondoa akimuacha masimba akishangazwa na Taarifa hiyo. Taarifa ya betri kurudi mikononi mwa Serikali. "TEDDY NITAKUPATA TU. NA NITAKUUA KWA MIKONO YANGU." Aliongea masimba sasa akimfuata yule Babu. "The Bastard hutakiwi kujificha katika uzee. Njoo katika Ujana tuifanye hii kazi." Bado masimba alizungumza huku akitembea. Wote wakatabasamu kwa pamoja kisha wakakumbatiana. Utatu Mtakatifu Ukazaliwa. Utatu ambao ulikuwa tayari kwa kulipigania Taifa la Tanzania. Taifa ambalo limekuwa shamba la kuchumwa mali kwa muda mrefu.
******
Walikuwa Watatu katika chumba hiki cha hoteli katika jiji la Dar es salaam. Alikuwa veronica, Masimba sambamba na Mwanaharamu. Masimba na Veronica walikuwa wakimtizama huyu Mwanaharamu usoni kwake. Mipango juu ya kuipata hii betri ilikuwa ikipangwa katika aina ambayo isingekuwa rahisi kugundulika. Lakini kabla ya mkakati wa kuipata Betri, ulifikiwa muafaka wa kuwapata watoto wa Masimba sambamba na Mzee Raymond ambaye anaonekana kulijua sana hili suala. Kazi hii ya hatari ilipangwa kufanya kwa siku hii. Kwa sababu ya hali ya Masimba kutokutengeamaa, Veronica na Mwanaharamu ndiyo ambao waliipanga kuifanyakazi hii. Veronica hakuonyesha woga, woga wakulisaliti kundi kubwa na hatari sana Duniani. Kundi ambalo liliweka Mizizi duniani kote. Kundi la Mafia. Moyo wake ulikuwa tayari kuingia katika uhatari. Aliamua kuasi katika kundi ambalo miko yake unaposaliti ni kifo. Kifo cha kinyama ama kutekwa na kufungiwa sehemu maalum ambayo hutumika kama Jela. Veronica hakuiona hiyo Hatari, aliamua kwa moyo wake kuingia rasmi katika kazi hii. Ilikuwa kazi Ya kifo, kazi ambayo ni lazima wajitoe kafara. Walikuwa tayari kwa kazi hiyo, walikuwa tayari kupambana katika mapambano ya aina yoyote.
*******
Ulikuwa usiku tulivu, usiku ambao ulimkuta mtu huyu katika eneo ambalo mara nyingi sana hupatikani watu fulani fulani. Alitulia hapo kwa utulivu wa Hali ya Juu. Mkononi alikuwa na kikombe kidogo cha Kahawa sambamba na kashata. Alikuwa akipiga fumbo taratibu huku macho yake yakitizama kila mtu ambaye alikuwa akipita karibu na kijiwe hicho. Hakuwa hapo kwa makusudi bali alikuwa hapo kwa kazi maalum. Aliambiwa mtoto wa kwanza wa Rais wa Nchi alikuwa akifikaga hapo kupata kahawa akiwa na marafiki na hata Walinzi wake. Alitulia hapo kanakwamba hakuwa na sababu ya msingi ya kufanya. Punde gari aina ya Land cruiser V8 ikaonekana ikitokea kwa mbali kwa mwendo wa Taratibu ikisogea maeneo yale. Mtu huyu aliyekuwa akimimina kahawa mdomoni akaendelea kufanya hivyo kanakwamba hakuliona tukio la gari hiyo kusogea. Baada ya Gari kusogea Zaidi na Zaidi kisha kuegeshwa. Mlango ukafunguliwa kisha mtoto wa Rais akashuka akiwa sambamba na Walinzi wake pamoja na Marafiki. Baada ya mtoto wa Rais kushuka sambamba na Watu wake. Wakasogea mpaka sehemu fulani ambayo ilionekana kupangwa kwa Ajili Yake. Kabla ya kupelekewa kahawa uchunguzi Ukafanywa kisha ndipo mtoto huyu wa Rais akaruhusiwa. Muda wote mtu huyu alikuwa akitizama kwa hila bila kujulikana. Alikuwa akiwaangalia na walinzi wengine ambao walikuwa wamesimama Barabarani wakionekana kutofuatilia kile kilichokuwa kikiendelea hapo. Mtu huyu hakuwa hapa kwa bahati mbaya, alikuwa hapa kwa kazi moja. Kazi ambayo waliona ndio sahihi kwa wakati huo. Ilikuwa ni Lazima Wampate Mtoto wa Rais Ili kulazimisha waipate betri Hiyo. Aliendelea kunywa kahawa taratibu. Hata mtoto wa Rais alipoingia ndani ya gari, Bado mtu huyu aliendelea kunywa. Hakuwa na Haraka Yakuinuka kwa kuwa Alijua kuna macho yapo sehemu yatizama ENEO HILO.