RIWAYA: NIACHENI NIKUFURU
MTUNZI: FAHAD MUSSA
EMAIL:
fahadmussa55@gmail.com
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Ilipoishia sehemu iliyopita......
Johnson alipanick, alishajua sasa mwisho wake umefika, amevamiwa na majambazi. Kabla hata hajakata simu, ghafla mlango wa chumbani kwake unavunjwa na wanaume watatu waliovalia mask wanaingia ndani.
......"Paaa, paaa,paaa, paaa,paaaa", sauti za risasi zinasikika ghafla mule chumbani na wale majambazi watatu wanaanguka chini hata kabla hawajapata muda wa kujitetea. Johnson anashangaa imekuwaje tena wale majambazi wamepigwa risasi, nani amewaua?.
Sasa tuendelee......
Johnson akiwa bado ameduwaa kwa kitendo cha wale majambazi kuanguka chini huku wakiwa hawana uhai, ghafla akashtuka kumuona jamaa mmoja mrefu, mweusi na mwenye mwili mwembamba ila umejengeka kimazoezi akiingia ndani huku ameshikilia bastola yake mkononi aina ya 'DB 380 CALIBER'.
Hata kabla ya kuzungumza chochote na Johnson, akaanza kuzipiga mateke zile maiti huku akiimba kwa sauti ya kilevi;
"Mama mimi sio mkorofi, wamenianza wenyewe.
Mama mimi ni mtu safi, wamenichokoza wenyewe.
Mama nimewapiga makofi, wamejifia wenyewe.
Nielewe mama sofi, wamejiua wenyewe.",
yule jamaa aliendelea kuimba kwa sauti yake ya kilevi huku kashika bastola mkononi. Hahahaha, ungefurahi sana kama ungemuona jinsi alivyokuwa anacheza kiduku huku akijipigia vigeregere na kuzizunguka zunguka zile maiti.
Wakati wote huo yule mlevi alipokuwa akiimba, Johnson alishindwa kuelewa afanye nini. Akimbie au abaki?. Kama akiamua kukimbia atapita wapi, pale mlangoni yupo yule mlevi na bastola yake anaimba imba huku akizizunguka zunguka zile maiti.Au abaki ametulia tu palepale?, ila hajui huyu mlevi akimaliza kuimba nyimbo zake atafanya nini. Je, akiuliwa?. HAKIKA NI HEKAHEKA.
Zilipita takribani dakika mbili tangu yule mlevi aanza kuimba nyimbo zake ndipo akanyamaza na kumgeukia Johnson.
"Dogo, una bahati sana. Hawa wanaume walikuja kukuposa hapa, shukuru mungu mahari yao ilipelea, la sivyo ungeolewa usiku huu", yule mlevi aliongea huku akimuangalia Johnson kwa macho ya kivivu.
"U...u....u...si...si..niue tafadhali, nisamehe. Nitakupa chochote ukitakacho", Johnson alipayuka huku akipiga magoti chini kuomba aonewe huruma.
"Lione hili, eti unasema utanipa chochote ili nikuache hai, basi nipatie Sodoma na Gomola nikuache hai", yule mlevi alijibu huku akikaa kitandani na bastola yake mkononi.
"Si....si...si..sijakuelewa broo", Johnson aliongea tena.
"Acha wenge mtoto wa kiume, yani upo tayari kunipa chochote kisa uhai?, Laana-tu-llah, daaah, kweli wanaume tupo wachache sana hapa duniani", yule mlevi aliongea kwa masikitiko kisha akaishusha silaha yake chini.
"Mimi si mtu m'baya, si umeona mwenyewe nimekusaidia hapa?, kosa mimi ulikuwa unaolewa leo", yule mlevi aliongea huku akijilaza pale kitandani na kujifunika shuka.
"Huyu jamaa vipi, mbona simuelewi. Yani kanisaidia alafu sahizi anapanda kitandani kulala,ngoja nitoke alafu nipige simu polisi", Johnson aliwaza kisha akaanza kunyanyua mguu wake ili atoke nje.
"Najua unachowaza Braza wangu, si unataka kupiga simu polisi?, ngoja niondoke alafu upige hiyo simu yako", yule mlevi aliongea huku akijifunua shuka na kuteremka pale kitandani.
"Hili ni Jini ama?, amejuaje kama nataka kupiga simu polisi", Johnson alijiuliza pasipo kupata jibu.
"Sikiliza kijana, mi nilikuwa napita tu hapo nje. Nikaona kuna wahuni wamevamia nyumba yako, ndo nikaamua kuja kutoa msaada. Vipi lakini, si umetega kamera humu ndani mwako?", mlevi aliuliza.
"Ndio, zipo. Zinafanya kazi saa 24", Johnson alijibu. Sasa hakuwa na wasiwasi sana baada ya kumzoea huyu mlevi.
"Vizuri sana, sasa naomba uwapigie simu polisi uwaambie kuwa ulivamiwa. Wakija alafu wakikubana maswali basi uwaoneshe kumbukumbu za CCTV camera waone jinsi tukio lilivyokuwa. Mi naondoka!!!!", yule mlevi alimpa maelekezo Johnson kisha akafungua mlango na kutaka kutoka nje.
"Nimekumbuka, nipatie na mimi hizo kumbukumbu za CCTV kamera, naweza nikazihitaji siku moja".
Johnson alielekea kwenye kona ya chumba chake ambapo kulikuwa na tanakilishi mpakato iliyounganishwa na CCTV kamera za nyumba nzima. Alipekua faili la video ya siku husika na kumtumia yule mlevi kwenye simu yake. Yule mlevi aliaga na kuondoka. Johnson alipiga simu polisi, na ndani ya robo saa, polisi wakawa wamefika eneo la tukio.
NYUMBANI KWA Mr. HASSAN MSANGI (BOSI WA JOHNSON)
"Mkuu, imepigwa simu hapa kituoni mda si mrefu kwamba kuna tukio la ujambazi limefanyika maeneo ya "Area A" kwa Mkorea, nyumba namba 109. Bila shaka itakuwa ni kule ulipowatuma wale vijana wako", sauti ilisikika kwenye simu ya Mr Hassan aliyoipokea muda mfupi baada ya kuita.
"Gooood, very nice. Mungu kajibu maombi. Yule mshenzi itakuwa wameshamuua. Sasa wewe nenda kahakikishe, ukimkuta bado roho haijamtoka vizuri naomba um'malizie, kanitia hasara kubwa shetani huyu", Mr. Hassan alifurahi sana baada ya kusikia kwamba kuna tukio la ujambazi nyumbani kwa Johnson.
Taarifa hii alipewa na polisi asiyemuaminifu katika kituo kikuu cha polisi Dodoma mjini. Sio siri, Serikali ina jukumu kubwa na zito la kupandikiza mashushu kwenye hizi idara nyeti zinazohusika na usalama wa raia na mali zao. Askari wengi sio waadilifu, wanavaa tu mavazi ya kiaskari ila moyoni ni majambazi sugu.
Mr.Hassan alikaa kwenye sofa huku akiiangalia simu yake mara mbili mbili kama atapigiwa tena ama la. Ilitimia saa kumi na mbili na nusu asubuhi ndipo akapigiwa tena.
"Bosi, sijui nikueleze vipi, tulichokikuta huko ni hatari tupu", yule askari aliongea mara tu simu ilipopokelewa.
"Hahahahaha, mumekuta hatamaniki kwa risasi alizopigwa?, usihuzunike, hivyo ndo safi sana, hiyo ndo dawa ya wajinga wanaoharibu kazi zangu. Muache akaozee kaburini", Mr.Hassan aliongea kama chiriku huku akifurahi sana. Hakuijua hali halisi.
"Bosi, simaanishi kwamba tumemkuta ameharibiwa kwa risasi. Bali wale uliowatuma ndo wameuliwa wote. Na Johnson ni mzima wa afya", yule askari alifafanua.
"Unasemaje Richard?, ina maana vijana wangu wameuliwa?, nani kawauwa?", Mr Hassan alinyong'onyea aliposikia kuwa vijana aliowatuma wameuliwa wote.
"Bado tunachunguza, ila kwa maelezo ya awali tuliyoyapata eneo la tukio ni kwamba kuna mtu alimsaidia Johnson. Huyo ndie aliyewaua vijana wako", Richard alijibu.
"Daah, sasa mbona huu ni mtihani. huoni kama upelelezi ukifanyika naweza kukamatwa?", Mr. Hassan aliuliza huku akiwa anahema kwa nguvu. Hakutarajia kusikia kwamba vijana wake aliowaamini na anaowatumiaga kwenye madili haramu wameshindwa kazi, tena cha kusikitisha zaidi ni kwamba wameuliwa. Haiingii akilini.
"Kuhusu hilo usijali bosi, niachie kazi. Kila kitu kitaenda vizuri", Richard alijibu kwa kujitapa.
"Fanya uwezavyo, hii aibu iniepuke. Kuna mzigo wako mwingi sana nimekuandalia ukifanikisha hilo. Kumbuka huyo alikuwa ni mfanyakazi wangu na huku mwishoni nilimfuta kazi. Hakikisha wapelelezi hawaungi doti", Mr. Hassan alimpa maelekezo Richard.
Hakika maji yalimfika shingoni. Vijana aliowaamini katika ulengaji wa shabaha na mapambano, leo wanauliwa kirahisi kama kondoo. Yeye alidhani kwamba hakuna mtu mwenye uwezo wa kupambana na vijana wake. Alisahau kuwa "kila m'babe ana m'babe wake".
KITUO KIKUU CHA POLISI DODOMA(CENTRAL)
"Naona tunaleteana utani kijana, sema ukweli. Wale majambazi wenzako uliowaua kule kwako ni kina nani?", na mumedhurumiana nini hadi uwauwe?, Afande Richard, polisi anayesifika kwa kutesa majambazi sugu wakati wamahojiano ndie aliyekuwa akimuhoji Johnson.
"Unanionea afande, mimi sio jambazi, na wale waliokufa nyumbani kwangu hata siwajui. Si nimewapa 'flash disk' yenye tukio zima muangalie, sasa kwa nini munazidi kunitesa?", Johnson alikuwa akiongea huku akilia kwenye chumba cha mahojiano. Yani yeye ndie alievamiwa na majambazi, na ni yeye ndie aliepiga simu polisi. Alafu sahizi anaambiwa kuwa wale majambazi waliofariki ni wenzake, na yeye ndie aliyewaua. MAAJABU.
"Sikiliza bwana mdogo, umejifanya kutugea 'flash disk' ambayo haina chochote ndani ili sisi tukuachie, si ndio?", Afande Richard aliuliza kwa ukali huku akimpiga Johnson kibao cha usoni.
"Flash haina kitu?, haiwezekani, kabla sijawapa tulihakikisha wote zile video na wale maafande wenzako, ndo wakaondoka nayo", Johnson aliongea huku jicho moja likiwa limevimba kwa kipigo alichokipata kutoka kwa afande Richard
"Naona unataka kulitukana jeshi tukufu la polisi, kwahiyo sisi ndo tumefuta hizo video zako?, acha uhuni we boya. Nitakuua humu, sema ukweli, kwanini umeua wenzako", Afande Richard bado alikuwa mkali kama mbogo aliyejeruhiwa. Hakutaka kusikiliza porojo yoyote kutoka kwa Johnson.
"Afande utaniua bure, mi sina kosa. Na wale majambazi siwajui na wala sio wen....", Kabla Johnson hajamalizia sentensi yake alijikuta anapigwa ngumi la tumbo, kabla hajatulia akapigwa kofi la sikioni.
"Sasa sikiliza, mda huu naondoka, ila nikirejea naomba uniorodheshee kwenye hiyo karatasi majina ya majambazi wenzako uliowaua. Na utaje sababu zilizokufanya uwaue. Kuwa makini",Afande Richard alimkabidhi Johnson peni na
karatasi nyeupe isiyoandikwa chochote kisha akafungua mlango na kutoka nje.
.....NYUMBANI KWA IDRIS (Baada ya siku 10)
"Karibu sana Bosi, naona leo umeamua kunitembelea nyumbani kwangu", Idris alimkaribisha Bosi wake huku akimtaka akae pale kwenye sofa, sebuleni.
"Nimeshakaribia, ahsante sana Idris", Mr. Hassan aliitikia karibu ya Idris huku akikaa kwenye sofa.
"Jack, nenda kwenye friji kalete maji ya baridi Bosi wangu apunguze joto", Idris aliongea huku akimuangalia Jackline.
Jackline nae bila hiyana akaamka pale kwenye sofa na kuelekea jikoni kuchukua maji.
"Wewe Iddy, huyu si mke wa rafiki yako Johnson, mbona yuko hapa. Nakumbuka alikuwa anaambatana sana na muwewe kwenye tafrija za kiofisi",Mr. Hassan alizungumza kwa sauti ya chini punde Jackline alipotoka pale sebuleni.
"Aaah Bosi, haya mambo ya kawaida tu. Si unajua tangu kipindi kile walivyogombanaga na mumewe ndo akahamia hapa kwangu mazima, mi nifanyeje sasa, siwezi kumtimua", Idris alijibu kwa kujibaraguza.
"Sasa itakuwaje kuhusu mazungumzo yetu, si inabidi atupishe kwanza tuongee alafu tukimaliza tutamuita", Mr. Hassan aliuliza kwa tahamaki.
"Hakuna tatizo bosi, huyu ni mke wangu kwa sasa. Kwahiyo ongea tu hata akiwe....", Idris alimtuliza Bosi wake ila kabla hajamaliza kuongea, Jackline alikuwa tayari ameshawasili na Chupa ya maji na glass. Alisogeza stuli karibu na Mr. Hassan, akammiminia maji kwenye glass. Alipomaliza akamkaribisha na kutaka kuaga ili awapishe wazungumze vizuri.
"Usiondoke Jack, kaa hapa kuna maongezi kidogo", Idris alizungumza na Jack akatafuta sehemu nzuri ya kukaa ili asikilize hayo maongezi.
"Kama nilivyokuelekeza Iddy kwenye simu. Nataka munisaidie ili Johnson afungwe, Baada ya hapo nitakupa cheo kikubwa sana pale ofisini. Pia hata huyu mke wako, 'Jack' nataka nae nimfungulie biashara yoyote kubwa anayoipenda mwenyewe. Au nyie mnasemaje?", Mr. Hassan alizungumza kisha akanyamaza kidogo kusikilizia majibu.
"Aaah, Bosi hilo sio la kutuuliza, tupo tayari hata sahizi, cha msingi ni mkataba tu", Idris alijibu haraka haraka.
"Naomba na mimi niulize, kwahiyo hii kesi ya mauaji anayoshitakiwa Johnson ni kweli aliua au?", Jackline aliuliza.
"Sasa huamini nini, mume wako ni muuaji. Ametapeliana na majambazi wenzake, akaamua kuwaua", Idris alidakia na kuongea kwa jazba baada ya Jackline kuhoji.
"Sikiliza bibie, mume wako 'Johnson' ni muuaji, kwahiyo mimi lengo langu nataka askari polisi wakija kuwahoji kama ni kweli Johnson ana mienendo ya kiuhalifu mujibu ndio, tena wewe ndo inabidi useme kuwa umewahi kumuona mara kwa mara na wale wenzake aliowaua wakijadiliana kwa siri mipango yao kule kwenu, jieleze vizuri ili mukawe mashahidi kule mahakamani. Akishaadhibiwa tu kifungo cha maisha au kunyongwa basi nakufungulia biashara kubwa hapa mjini. Hakuna mwanamke atakayekufikia kwa utajiri Dodoma nzima" Mr. Hassan alizidi kupalilia maneno yake.
"Kama ni hivyo nipo tayari, mi siwezi kumsapoti mwanaume muuaji kama Johnson, kwanza namchukia sana", Jackline alijibu baada ya kusikia maneno matamu kutoka kwa Mr. Hassan.
USIKOSE SEHEMU IJAYO.
TUKUTANE TENA KESHO