RIWAYA: NIACHENI NIKUFURU
MTUNZI: FAHAD MUSSA
EMAIL:
fahadmussa55@gmail.com
SEHEMU YA KUMI NA TATU
Tulipoishia sehemu iliyopita...............
Sikiliza bibie, mume wako 'Johnson' ni muuaji, kwahiyo mimi lengo langu nataka askari polisi wakija kuwahoji kama ni kweli Johnson ana mienendo ya kiuhalifu mujibu ndio, tena wewe ndo inabidi useme kuwa umewahi kumuona mara kwa mara na wale wenzake aliowaua wakijadiliana kwa siri mipango yao kule kwenu, jieleze vizuri ili mukawe mashahidi kule mahakamani. Akishaadhibiwa tu kifungo cha maisha au kunyongwa basi nakufungulia biashara kubwa hapa mjini. Hakuna mwanamke atakayekufikia kwa utajiri Dodoma nzima" Mr. Hassan alizidi kupalilia maneno yake.
"Kama ni hivyo nipo tayari, mi siwezi kumsapoti mwanaume muuaji kama Johnson, kwanza namchukia sana", Jackline alijibu baada ya kusikia maneno matamu kutoka kwa Mr. Hassan.
Sasa tuendelee....................
"Mpango wetu ni huu; kesho kuna askari wa upelelezi watakuja kwenu kuwahoji. Munachotakiwa ninyi ni kukariri hizi sura za waliouawa. Chukueni hii picha yao, nyuma kuna majina ya kila mmoja. Huyu wa kushoto anaitwa Gideon, anayefuata anaitwa Oscar, anayefuata ni Daud na huyo wa mwisho ni Selemani. Kwahiyo ili uweze kuwakumbuka vizuri kariri neno 'GODS'. Yaani G=Gideon, O=Oscar, D=Daud na S=Selemani. Tumeelewana?", Mr. Hassan aliwapa maelekezo Idris na Jackline huku akiwapatia na picha.
"Hapa bado hatujaelewa muheshimiwa. Sisi tunatakiwa tuwaambie nini polisi?", Idris aliuliza.
"Wakija kuwahoji muwaambie kwamba huwa munamuona Johnson mara kwa mara na wale jamaa zake ingawa hamujui ni nini huwa wanajadiliana. Pia muwaelekeze kuwa hao waliouliwa huwa wanakuja hata nyumbani kwa Johnson. Shahidi muhimu hapa ni mke wake Johnson, huwa anawashuhudia kila wakifika. Hapo vipi?", Mr Hassan alitoa ufafanuzi.
"Hapo tumekupata, hakuna kitakachoharibika", Jackline alidakia.
"Kwahiyo malipo yetu yatafanyika lini?", Idris aliuliza.
"Kesi ikiisha tu na hukumu ya kifungo cha maisha au kunyongwa ikitoka basi ntawalipa chenu. Ila tukishindwa kesi sitoweza kuwalipa chochote", Mr Hassan alitoa ufafanuzi kuhusiana na makubaliano yao.
Baada ya majadiliano ya takribani nusu saa, Mr Hassan aliagana na wenyeji wake kisha akaondoka huku wakiwa wameahidiana kuwa mkataba wa makubaliano yao utasainiwa siku tatu zijazo.
SIKU 12 ZILIZOPITA (NYUMBANI KWA IDRIS)
"Umesema upo njiani unarudi Dodoma?, mbona hukunipa taarifa mapema ili nijiandae Roida", ilikuwa ni sauti ya kulalamika ya Idris akiongea na Roida kwa njia ya simu.
"Jamani Iddy, si nishakwambia kuwa nakuja tu kwa dharula?, kuna gari la mtu binafsi limetoka Iringa, ndo nimepewa tu lifti", Roida alijibu.
"Ok sio kesi. Karibu sana ila tambua kuwa Jack nae yuko hapa na ninalala nae", Idris aliongea huku akishusha pumzi.
"Hilo sio tatizo Iddy, nitalala hata sebuleni. Kuanzia kesho kutwa ndo nitatafuta chumba nikapange", Roida alijibu.
"Ok, karibu sana. Uko sehemu gani?", Idris aliuliza.
"Nakaribia kufika, kwenye saa tatu nitakuwa hapo", Roida alijibu.
"Poa karibu sana", Idris alijibu na kukata simu.
Roida aliumia sana baada ya kugundua kuwa kwa sasa hana chake tena kwa Idris. Alidhani kumfanyia mpango Idris wa kumshawishi Jackline usingeleta athari katika mahusiano yake. Ila leo anajuta. Neno ninge..........
.........................................................................................
Chumbani kwa Idris.
"Jack, nina ombi moja kipenzi changu, naomba leo na kesho Roida alale hapa. Alafu keshokutwa ataenda kujitafutia chumba akapange", Idris aliongea kwa unyenyekevu akiomba ruhusa kwa mpenzi wake huyu mpya (Mke wa Johnson).
"Kama ataondoka baada ya siku mbili haina shida, ila atalala sebuleni ama chumba cha wageni. Sitaki kumuona huku chumbani kwetu", Jack alijibu huku akimuangalia Idris kwa jicho lenye ishara za wivu.
"Hakuna tatizo malkia wangu, atalala chumba cha wageni. Hata yeye amekubali kulala chumba cha wageni", Idris alijibu huku akishika shika nywele za Jackline.
"Poa babe, mi nina wivu sana mwenzako. Sipendi mtu mwingine ale kwenye shamba langu", Jackline aliongea kwa sauti yake ya kudeka. Yani alishasahau kama yeye ni mvamizi tu, mwenye mali halali ni Roida. Ndio hivyo, kashafanya mapinduzi. Roida hana chake kwa sasa.
Majira ya saa tatu na robo usiku, Roida aliwasili nyumbani kwa Johnson. Alimkuta Jackline akiwa jikoni anapika chakula cha usiku. Walisalimiana salamu za kinafiki, kila mmoja alikuwa na chuki kwa mwenzake. Jack alichukia kumuona Roida kwenye miliki yake mpya na Roida nae alimchukia Jack kwa kuvamia miliki yake. Hawakuongeleshana tena jambo lolote zaidi ya salamu tu. Daaah, WANAWAKE BWANA.
Roida alipotoka jikoni alielekea chumbani kwa Idris ambapo alimkuta anasoma soma vitabu.Walisalimiana. Akaweka vitu vyake vizuri kisha akarudi tena sebuleni.
"Lazima nitimize malengo yangu leo na kesho, keshokutwa nirudi zangu Mkonze. Lazima nizijue namba za siri za 'shelf'. Pia siwezi kulala kwenye chumba cha wageni, lazima nilale chumbani kwa Idris ili nikamilishe mipango yangu", Roida alikuwa akiwaza peke ake pale sebuleni.
Baada ya dakika kumi, Idris alitoka chumbani na kuungana na Roida pale sebuleni na kuanza kupiga nae stori mpaka pale Jackline alipoleta chakula mezani wakaanza kula. Ilikuwa ni futari ya ndizi mbivu iliyochanganywa na nyama ya ng'ombe pamoja na maharagwe. Kilikuwa ni chakula kitamu.
"Jack, mimi na wewe ni marafiki. Sipendi tupishane maneno wala tugombane kisa Idris. Sijapenda leo namna ulivyonipokea. Mi keshokutwa tu naondoka. Nivumilie kwa siku mbili hizi", Roida alianzisha mazungumzo wakati wa kula.
"Roida, naomba tule. Hapa sio mahakamani", Jack alijibu kwa jeuri huku akibetua mdomo wake.
"Sawa mama yaishe. Ila wewe utabaki kuwa rafiki yangu, si adui yangu. Naomba tutabasamu kama zamani",Roida aliongeza.
Jack hakujibu kitu. Idris nae hakupenda kuingilia mazungumzo ya wake zake hao.
"Jack, mbona hujaleta maji ya kunywa, tunakulaje kama nyoka?", Idris aliuliza punde alipohitaji maji anywe.
"Hakuna tatizo, ngoja nikufatie", Roida aliongea na kuinuka kwenda kufata maji.
"Hii ndio nafasi niliyokuwa naihitaji, lazima nifanikishe lengo langu leo. Lazima Idris alie", Roida aliwaza punde alipoingia jikoni. Alilifuata friji na kutoa jagi la maji baridi. Akaingiza mkono kwenye sidiria yake na kutoa dawa ya unga kwenye mfuko. Aliimiminia dawa ya kutosha kwenye glasi na kukoroga yale maji. Aliporizika akabeba jagi na kurudi nalo sebuleni. KIZAA ZAA.
Idris alipokea jagi la maji, alimimina maji kwenye glasi na kuanza kunywa.
"Babe, nimiminie na mimi ninywe", Jackline aliongea kwa sauti ya kudeka ili amuumize Roida. Laiti kama angejua.........
Idris alimimina tena maji kwenye glasi na kumpatia Jack.
"Naomba uninyweshe, mikono yangu inauma", Jack alizidi kumdekea Idris na sauti yake nyororo ili amuumize Roida. Ameshasahau kama Roida ndie aliyemfanyia mpango wa yeye kuwa na Idris
"Usijali kipenzi changu, haya kunywa sasa", idris alijibu huku akimnywesha Jack maji. Roida alinyamaza tu huku akishuhudia hila za rafiki ake wa zamani. Aliamua kupotezea tu vile vituko vya Jackline kwa kuwa alijua nini amelenga kufanya, ingawa moyoni alikuwa akiumia.
NMP (NeuroMuscular Blocking pills) ni aina ya dawa ambayo hupoozesha viungo vya mwili kwa muda mfupi. Muathirika huwa hawezi kufanya jambo lolote pindi anapoinywa hii dawa na kukaa walau dakika kumi. Na hukaa mwilini kwa masaa yasiyozidi tisa.
Idris alianza kujihisi kuishiwa nguvu, mwili wote ulianza kumsaliti. Alipotaka kuzungumza jambo alijikuta hawezi hata kunyanyua mdomo. Jackline nae hali yake ilikuwa sawa na Idris, nae alikuwa amejilaza kwenye sofa huku akijitahidi kusimama pasipo mafanikio yoyote. Roida aliwaweza.
Roida alipoona wenyeji wake wameshazidiwa na ile dawa, aliinuka na kuelekea moja kwa moja chumbani kwa Idris. Alilifungua kabati la Idris na kutoa kiboksi cha chuma kilichokuwa na ukubwa sawa na dumu la mafuta la lita tano. Alijitahidi kulishusha hadi chini na kutaka kulifungua.
"Mungu wangu, namba ya siri ya kufungulia hili boksi siijui, ila sio mbaya, acha niondoke nalo", Roida alijiwazia moyoni na kuanza kulikokota lile boksi la chuma na kuteremka nalo hadi sebuleni. Aliwakuta Jack na Idris wakiwa bado hawajiwezi. Alifungua mlango wa kutoka nje na kulipakiza katika gari la Idris na kuondoka nalo.
"Hello Babe, sijafanikiwa kuchukua zile nyaraka. Ila nimefanikiwa kuchukua lile boksi ambalo alikuwa akitunzia hela zake", Roida alikuwa akiongea na simu na mpenzi wake aliepo Mkonze-nje ya mji wa Dodoma.
"Basi chukua taxi likulete hadi huku", sauti ya kiume ilijibu.
"Sawa, nakuja. Ndo nipo njiani", Roida alijibu na kukata simu.
MKONZE - DODOMA
Majira ya asubuhi, maiti ya mwanamke umri miaka 27-30 inagunduliwa ndani ya nyumba ya kulala wageni. Wapita njia wamekusanyika karibu na nyumba ya kulala wageni ya "Malaika Guest house" huku kila mmoja akizungumza lake.
"Huyu binti aliekufa mi namjua, anaishi mtaani kwetu, anaitwa Roida. Masikini ya mungu amekufa kifo kibaya sana daah", Mama mmoja wa makamo aliyejifunga ushungi wa kanga kichwani alikuwa akiwaeleza wenzake.
"Yani amepigwa nondo ya kisogoni, kichwa chote hakitamaniki. Alafu nasikia huyo mwanaume aliemuua ametoroka. Wanaume wabaya jamani", Mdada mwingine anayefahamika kwa jina la pendo alidakia.
"Maisha ya sahizi usikubali tu mtu anatokea huko anakwambia dada nakupenda, na wewe bila kujiuliza mara mbilimbili unakubali tu. Mwisho wa siku unakufa kifo kama cha Roida", mdada mwingine aliongea.
"Roida nae alikuwa mapepe, kila mwanaume wake. Ona sasa leo kauliwa kifo cha kinyama. Mungu amsamehe tu dhambi zake huko aliko", Mama anayefahamika kama 'Mama Juma' nae alizungumza lake.
Kila mmoja alizungumza aliloona linafaa. Roida ameuliwa na mwanaume alielala nae 'gesti'.
Je, ni mwanaume yupi huyo?, au ni yule mpenzi wake waliopanga njama za pamoja za kumtapeli Idris?
USIKOSE SEHEMU IJAYO.
TUKUTANE TENA KESHO.