RIWAYA: NIACHENI NIKUFURU
MTUNZI: FAHAD MUSSA
EMAIL:
fahadmussa5@gmail.com
SEHEMU YA SITA
Nyumbani kwa Idris
Jumatatu Asubuhi
............."Roida, najua haufahamu nini lengo langu la kumtaka kimapenzi Jackline. Sijamtaka kisa ana shepu ya kuvutia, wala sijamtaka kisa ana sura nzuri yenye kuvutia, Bali ninamuhitaji Jackline kwa lengo moja tu" Idris alizungumza kidogo kisha akapumzika kidogo kumpa Roida muda wa kuyatafakari maneno yake kisha akaendelea
............"Johnson ni rafiki yangu mkubwa, ila kwenye maslahi sina budi kumsaliti, Namtumia Jackline ili amuangamize mumewe" Idris aliongea huku akimuangalia Roida ambae muda wote huo alikuwa amejilaza kitandani angali yu uchi wa mnyama.
............"Bado sijakuelewa, nieleweshe vizuri. Johnson ana kitu gani hadi unahitaji kumuangamiza?" Roida aliuliza kwa tahamaki huku akiinuka pale kitandani na kukaa kitako.
..............."Nahitaji cheo chake pale ofisini" Idris alijibu kwa kifupi
............"Ila elimu si amekuzidi, sasa utakichukua vipi cheo chake" Roida aliuliza.
.............."Kielimu tupo sawa, ufanisi wa kazi ni sawa. Hakuna nilichozidiwa na Johnson ila Bosi akaamua kumpa cheo cha 'Msimamizi mkuu wa Idara zote pale ofisini'" Idris aliongea huku akivuta pumzi ndefu
............"Kwahiyo Jackline anahusika vipi na huo mkakati wako" Roida aliuliza
.............."Ondoa shaka, utakuja kufahamu umuhimu wa Jackline baadae. Sahizi endelea kuwa mtazamaji" Idris alijibu huku akisimama na kuelekea katika kabati lake na kuchukua suruali na shati la mikono mirefu. Akazivaa tayari kwa kwenda kazini.
NASIMULIA
Hakuna siku ambayo sitakuja kuisahau katika shughuli zangu za kiofisi kama siku hii ya jumatatu. Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Jumatatu asubuhi. Siku hii niliwahi sana kufika ofisini kutokana na majukumu niliyokuwa nikiyafanya wikend. Kuna taarifa mbalimbali nilizotakiwa kuwasilisha kwa Bosi. Ninachokumbuka ni kwamba nilichukua tanakilishi (kompyuta) yangu mpakato na kuingia nayo ofisini kwangu kabla sijapeleka taarifa kwa bosi.
Jukumu langu kama mkuu wa Idara zote hapa ofisini ni kuhakikisha uwajibikaji wa wafanyakzi wote, kutatua kero mbalimbali zinazohusu idara zote hapa ofisini na mwisho kabisa kuhakikisha naweka mahusiano yaliyo bora kati ya wafanyakazi na Bosi mkuu, na pia kati ya ofisi na wateja.
Kila ninapokuja kazini, kitu cha kwanza ni kuhakikisha idara zote wafanyakazi wamehudhuria kazini na kupokea taarifa mbalimbali za kila idara. Kwahiyo nikatoka ofisini kwangu na kuelekea kwa katibu muhtasi
.............."Hello Zainabu, za asubuhi" nilimsalimia katibu muhtasi pale ofisini
............."Salama, sijui za huko kwako" aliniitikia
............"Nitokako ni wazima, vipi Godfrey ameshaingia ofisini kwake" nilimuuliza
............."Hapana bado hajaripoti hapa, hata daftari la mahudhurio hajasaini" alinijibu
............."Na Idris nae" nikamuuliza tena
............"Hata yeye bado hajafika" aliongezea
Aliponijibu hivyo sikusubiri sana nikaamua kuelekea idara mbalimbali kisha nikarudi ofisini kwangu na kusubiri niitwe na bosi mkuu ili niwasilishe nyaraka mbalimbali nilizozifanyia kazi wikendi.
Dakika ishirini baadae simu yangu iliita. niliipokea na kuiweka sikioni.
..........."Naomba uje ofisini kwangu haraka" Sauti kwenye simu ilisikika. Kabla sijajibu sim ikakatwa. Nilichukua diski mweko(Flash disk) ili niweze kunyonya nyaraka zinazohitajika ili nizipeleke ofisini kwa bosi.
Hapo ndipo kizaazaa kilipoanza. Nyaraka zote nilizozifanyia kazi wikendi na kuziweka katika tanakilishi yangu hazikuwepo. Na ni nyaraka muhimu zinazohusiana na mikataba ya miradi mbalimbali. Nakumbuka nilizihifadhi(sevu) kwa jina la "Urban projects" na nilizinakili sehemu mbali mbali katika tanakilishi yangu, ila kote huko sikuziona.
............"Mbona sizioni hizi nyaraka?, nakumbuka nilizisevu kwenye folda hili na hili, lakini kote hazipo, kwanini" nilijiongelesha mwenyewe kama kichaa huku nikijitahidi kutafuta sehem zote kwenye tanakilishi yangu ambapo zinaweza zikawepo hizi nyaraka. Ghafla simu iliita tena
............"Johnson, si nimekwambia uje haraka ofisinu kwangu?", Bosi aliniuliza kwa ukali punde nilipopokea ile simu.
............"Na na na nakuja Bosi" nilimjibu kwa kigugumizi.
............"Nakupa sekunde ishirini uwe hapa" alimalizia na kukata simu.
Hakika nilichanganyikiwa sana. Hizi nyaraka nimehangaika nazo kwa takribani wiki mbili, na wikendi ndio nilikuwa namalizia kazi, ila leo kazi yote niliyoifanya imepotea. Sikuwa na namna zaidi ya kuripoti kwa bosi pasi na nyaraka.
........."Hodi hodi" niligonga mlango wa ofisi ya bosi mara tatu na kusubiri jibu
........."Ingia" Bosi alinijibu. Nikaingia na kukaa kwenye kiti mbele ya meza ya bosi.
..........."Shi shi shikamoo Bosi" nilimuamkia kwa kitetemeshi. Kiumri alinipita zaidi ya miaka ishirini
..........."Marhaba Johnson, vipi mbona una wasiwasi What's wrong?" Bosi aliniuliza.
............"Samahani muheshimiwa, nilijitahidi sana kuifanya kazi uliyonipa kwa takribani wiki mbili na niliimaliza yote. Ila..." nilijieleza kwa bosi kisha nikanyamaza ghafla bila ya kumalizia sentensi yangu
............."Ila nini Johnson" Bosi aliniuliza kwa hamaki
............"Ma..ma..mafaili siyaoni" nilijibu kwa mkato
............"Hebu nieleweshe vizuri kijana wangu, naona unazunguka zunguka tu, huyaoni kivip?" Bosi aliongea kwa ukali.
.........."Mafaili yenye nyaraka zote niliyahifadhi kwenye tanakilishi(Kompyuta yangu) ila leo asubuhi nilipokuwa nataka kuyahamishia kwenye flashi nashangaa sijayaona kabisa. Sijui imekuwaje" nilimueleza bosi kwa unyenyekevu wa hali ya juu.
............."Be serious guy, don't mess with me, nazihitaji hizo nyaraka hapa. Inuka kaniletee hizo nyaraka haraka sana" Bosi alifoka kama mbogo.
............"Muheshimiwa, sijawahi kukuangusha katika kazi zako zote ulizowahi kunipa nikufanyie, hii leo sijui ni kipi kimetokea. Naomba unisamehe mkuu" niliongea huku nikipiga magoti mbele ya bosi.
............"Hivi unajua kwamba hii kandarasi imesimama ili kupisha tathmini zetu?, hivi unajua kwamba leo ndio siku ninayotakiwa kuonana na bodi ya wakurugenzi ili kuwasilisha makadirio yetu?. Unataka mimi niende nikawajibu nini?" Bosi aliniuliza maswali mfululizo.
Nilishindwa nimjibu nini Bosi wangu. Nikawa kimya kama bubu. Ni mchawi gani aliyeingia kwenye tanakilishi yangu na kufuta nyaraka zangu za muhimu?. Nilijiuliza bila kupata jibu. Nywira (Passwords) za hii tanakilishi yangu hakuna anayezijua zaidi ya mimi, Idris na mke wangu Jackline.
Bosi alinifokea sana. Hakuna siku niliyosemwa na kukejeliwa na bosi wangu kama siku hii. Ila nashukuru mungu hakuchukua hatua ya kunifukuza kazi wala kunisimamisha. Alipochoka kunifokea akaniruhusu niondoke.
USHAURI /PENDEKEZO
Ndugu msomaji wa kisa hiki. Katika maisha nimejifunza jambo moja. Akupepeae kwa upepo mwanana, ndie akuleteae joto kali sana. CHUNGA SANA MIENENDO YA WATU UNAOWAAMINI". Akumulikae mchana, usiku akuchoma.
tuendelee.............
Nakumbuka nilipotoka ofisini kwa Bosi, moja kwa moja nilielekea ofisini kwangu. Niliwakuta rafiki zangu Godfrey na Idris karibu na mlango wa kuingilia ofisini kwangu.
..........."Oooh papaa J J mutu muzito, nakuona umetoka kuongea na mkubwa mwenzako, sisi watoto tupo tu tunang'aza sharubu" Idris alinilaki kwa bashasha punde nilipowafikia.
............."Aaah wapi kaka, hakuna cha mkubwa wala mdogo, wote sawa tu" nilimjibu kiunyonge
.............."Vipi Broo, mbona umenyong'onyea sana leo?, sio kawaida yako kuwa mpole, nayajua makeke yako" Godfrey aliniuliza kwa hamaki mara baada ya kuniona sijachangamka kama siku nyingine.
............"Ni majanga ndugu zangu, nimetoka kutukanwa na Bosi hapa sina hamu" nilimjibu Godfrey huku nikifungua mlango ili niingie ndani. Nao walinifata kwa nyuma na mzungumzo yakaendelea.
.........."Usitupanikishe kaka, imekuwaje tena" Idris aliniuliza kwa bashasha.
Ikabidi niwaeleze ukweli wote wa kilichotokea tangu nilipokabidhiwa kazi na Bosi wiki mbili zilizopita hadi siku ya leo nilipotaka kwenda kuiwasilisha.
............"Kumbuka vizuri kaka, inawezekana umejichangaya mwenyewe ulipoweka hayo mafaili yako" Godfrey alitoa ushauri wake
............."Niko makini sana God, huwa nafanya mambo yangu kwa umakini mkubwa mno. Nakumbuka kabisa haya mafaili niliyahifadhi kwa jina la 'Urban Projects' na mara kwa mara nilikuwa nayapitia, ila leo asubuhi ndo yamepotea" nilimjibu kwa mfadhaiko
............." Au inawezekana kuna mtu aliingia ofisini mwako asubuhi na kufuta?" Idris alihoji.
............"Hapo ndo sijajua, maana funguo ya ofisi yangu ninayo mimi na katibu muhtasi tu. Sasa sijui ni kitu gani kilichotokea" niliwapa ufafanuzi.
..........."Peleleza kwanza kwa Zainabu, inawezekana aliingia ofisini kwako akachezea kompyuta yako. Ni ngumu mafaili kujifuta bila sababu. Kama ingekuwa ni virusi basi hata mafaili mengine yasingekuwa salama" Godfrey akatoa mawazo yake.
Nikaona ni kweli, ni muhimu kwenda kumuuliza katibu muhtasi kama aliingia ofisini mida ya asubuhi kipindi nimeenda kufatilia mahudhurio ya wafanyakazi katika Idara mbali mbali.
Tulitoka wote watatu na kuelekea kwa katibu muhtasi.
............"Zai nimekuja tena kwako, nina swali nahitaji unijibu" niliongea punde nilipofika mezani.
............"Uliza Bosi usijali" aliitikia
............."Ni nani aliyeingia ofisini kwangu leo kipindi nimetoka ile asubuhi" nilimuuliza
............"Aaaa..aaa asubuhi i...i....le Idris alikuja ku..." Zainabu aliongea kwa kigugumizi kisha akaka kimya.
TUKUTANE TENA KESHO PANAPO MAJAALIWA