RIWAYA: NIACHENI NIKUFURU
MTUNZI: FAHAD MUSSA
EMAIL:
fahadmussa@gmail.com
SEHEMU YA KUMI NA SITA
Ilipoishia...............
Aflo hakupenda kupita njia anayopitaga kila siku kuelekea kwake. Alipita njia tofauti kabisa na anayoitumiaga siku zote.
Akiwa anatembea kwa kuvizia na kubakiza chini ya mita mia kufikia nyumba aliyopanga, alishangaa akipigwa na kitu kizito maeneo ya kisogoni pasipo kutarajia. Fahamu zilianza kumpotea taratibu. Giza nene lilitanda usoni mwake. Hakujua kilichoendelea.
Sasa tuendelee...............
"Daah, Tafu bwana, yani mtu uliyekuwa unasema amekuchimba biti kule chooni ndo huyu boya?", mbona mlaini sana?, Benja aliuliza kwa dhihaka baada ya kufanikiwa kumzimisha Aflo baada ya kumpiga ngumi nzito maeneo ya chini ya kisogo.
"Mi nilishamsoma tangu alipokuwa akinichimba mkwara ila nilimstahi tu", Tafu alijibu huku akimtemea mate Aflo kwa kejeli.
Benja alimuacha Tafu akimlinda mateka wao kisha yeye alielekea kwenye kichaka cha mtaa wa pili kuchukua pikipiki waliyoificha pindi walipofika kumteka Aflo.
STENDI KUU YA MKOA- NANENANE
Ahmed Jabir, Kachero wa polisi kutoka mkoani Morogoro akiambatana na makachero wawili Aneth na Julius kutoka kituo kikuu cha polisi Dodoma, wapo ndani ya stendi kuu ya mabasi ya mkoa- Dodoma (NANENANE) tangu saa kumi na nusu jioni wakimsubiri mgeni wao 'mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya nchini' anayefahamika kwa jina la Onesmo Bageni. Inasemekana, mfanyabiashara huyo baada ya kuukimbia mkono wa Dola mkoani Morogoro, alivaa Baibui na kujitanda nikabu ili kuficha utambulisho wake kisha alipanda Basi maeneo ya Gairo(Morogoro) na kuja Dodoma.
Majira ya saa mbili kasoro usiku wakati Kachero Ahmed akiwa ametulia sehemu, ndani ya stendi hiyo, ndipo alipomuona rafiki yake kipenzi 'Alexander Florence' (Aflo) waliepotezana takribani miaka kumi na mbili iliyopita wakiwa ni wafanyakazi katika ofisi za makao makuu ya polisi nchini yaliyopo Dar-es-salaam.
"Mungu wangu, hivi ni macho yangu kweli ama naota?, huyu si Alex huyu?, au?", alijiuliza pasipo kupata jibu baada ya kumuona Aflo akiwa anaipakiza familia yake kwenye gari.
Aliinuka pale alipoketi na kusogea sehemu ya karibu zaidi ili athibitishe kama akionacho ni kweli ama laa.
"Ni kweli, ni yeye. Daah, mungu wa ajabu sana. Sikutarajia kama ningeonana na mtu kama huyu huku ugenini kutoka Dareslam", Ahmedy alizidi kumkazia macho Aflo. Ila hakuthubutu kumsogelea.
Kanuni za kiusalama zinasema, ukiwa ndani ya 'mission' eneo flani, kisha ukamuona mtu uliyepotezana nae au hata mtu unayefahamiana nae, hata kama ni mama yako hutakiwi kujionesha kwake, kwa maana unaweza kuharibu 'mission' iliyokuleta mahala husika. Hiyo ni moja ya sababu iliyomfanya Ahmed kutokumsogelea Alex (Aflo).
Pia ukiachana na sababu za ki-mission, pia mazingira aliyokuwa nayo Alex yalimuacha Ahmed na maswali mengi. Kwa macho ya mtu wa kawaida asiye na mafunzo ya kishushushu au kisaikolojia, angeweza kumuona Alex(Aflo) kama mu asiye na hofu wala mashaka. Ila kwa macho ya Kachero aliebobea kama Ahmed, Alex alionekana ni mtu mwenye wasiwasi mwingi sana pindi alipokuwa anaagana na yule mwanamke mwenye mtoto(Mama Betty), alikuwa akirusha rusha macho sehemu mbalimbali za eneo la stendi. Hii ilimpa wasiwasi Ahmedy.
"Aneth, endelea kufatilia windo. Kuna dharula imetokea. Nakuja mda si mrefu. Msisitize na Julius ili muwe makini", Ahmed alitoa maelekezo kwa Kachero mwenzake kisha akaanza kumfatilia Alex nyuma nyuma tangu alipokuwa akitoka pale stendi.
Ahmed alishangaa sana kumuona Alex akitembea kwa wasiwasi huku akigeuka nyuma mara kwa mara kuangalia usalama wake. Alishajua kuwa rafii yake hayuko katika hali ya kawaida, kuna jambo analificha. Ni jambo gani hilo?. Hii ndio sababu ya Ahmed kumfuatilia Alex.
Alex alitembea haraka haraka huku akigeuka nyuma mara kwa mara ili kuangalia usalama. Ahmed alikuwa akijificha kila Alex alipogeuka nyuma.
Alex aliifikia barabara ya lami na kukodi pikipiki ambayo ilimfikisha mtaa anaoishi- Kata ya Makulu. Ahmed nae hakuwa nyuma. Alikodi pikipiki na kumpatia maelekezo dereva kwamba aifatilie pikipiki aliyoipanda Alex bila kugundulika. Dereva alitii maagizo na kuanza kuifatilia pikipiki aliyoipanda Alex. Pikipiki aliyopanda Ahmed ilisimama mbali kidogo na pale aliposhukia Alex, alimlipa Dereva nauli yake na kuendelea na zoezi lake la kumfuatilia Alex.
Wakiwa wametenganishwa na umbali wa mita sabini, ndipo Ahmed alishtuka baada ya kumuona mtu mwingine akimvamia Alex na kumpiga ngumi iliyompeleka alex chini. Mwanga hafifu wa mbalamwezi ulitosha kabisa kushuhudia tukio lile. Alex hakuinuka tena, ndipo hapo Ahmed alipogundua kwamba Alex amezimishwa na ile ngumi. Je, aende kumsaidia rafiki ake au atulie?, Hakufanya papara ya kutaka kwenda kumsaidia Alex, bali alijificha
sehemu na kushuhudia kinachoendelea. Kumbe hisia zake za kutaka kumfatilia Alex zimezaa matunda.
Alisogea taratibu eneo la tukio huku akitumia kuta za nyumba jirani kujificha. Alisikia namna yule jamaa aliempiga Alex akimuita mwenzake. Hapo akagundua kuwa yule jamaa hakuwa peke yake, bali yuko na mwenzake. Kama angeingia kichwa kichwa kupambana na yule jamaa basi angeishia pabaya. Uvumilivu wake ulimsaidia. Alisikia maongezi yote waliyokuwa wakiongea wale jamaa. Alisubiri tu dakika chache zijazo ili aanzishe varangati.
Benja alipomuaga Tafu kwamba anaelekea kuichukua pikipiki waliyoificha mtaa wa pili, ndio nafasi hiyo Ahmed aliitumia kumuokoa Alex(Aflo).
Tafu akiwa amesimama wima huku akimpigapiga mateke Aflo, alishtuka baada ya kuhisi kuna kitu mfano wa kopo limetupwa eneo lile. Alilisogelea lile kopo na kuinama ili aliangalie, Daah, hakupata muda wa kulitathmini lile kopo. Alishtuka akipigwa teke la mdomo ambalo lilimpeleka chini moja kwa moja. Aliinuka haraka na kuangalia kule teke lilipotokea, hakuona kitu. Akajidanganya ageuze uso wake upande wa pili kama atamuona adui.
La-haula, alishtukia akipigwa kichwa cha mdomo, meno mawili ya mbele yalimng'oka. Kitendo cha kupigwa kwa kushtukizwa kilimkera sana na kumtia hasira, hakujua kwamba hasira hasara. Alijipanga upya sasa kwa mapambano baada ya kumuona adui yake alipo. Alirusha ngumi mfululizo huku akisindikiza na mateke ili kumchanganya adui yake. Hakujua anapigana na mtu wa aina gani, laiti kama angejua mapema, basi angepata muda wa kukimbia kuliko kujitia ujuzi wa kupambana. Ngumi zote pamoja na mateke aliyokua akirusha kwa kasi yalipanguliwa vyema na Ahmed. Hakuna ngumi iliyogusa sehemu muhimu za mwili wa Ahmed.
Ahmed alitumia janja ya kujifanya anarudi nyuma ili ampumbaze Tafu, na kweli, tafu akasahau jukumu lake la kujilinda, aliwaza kushambulia tu, hilo ndilo kosa kubwa alilolifanya. Alishtuka akipigwa ngumi tatu za uso zilizomuangusha chini, kabla hata hajainuka alishtuka akipigwa mateke mfululizo ya mbavu. Nguvu zikamuisha. Ngumi moja nzito iliyopigwa chini ya kidevu ilitosha kabisa kumzimisha Tafu. Ahmed alimsogeza Tafu kwenye kichaka kilicho karibu na pale kisha akatulia kwa lengo la kumsubiri Benja, aliyeenda kufata pikipiki.
Zilipita takribani dakika saba ndipo Benja alirejea na pikipiki. Alikuwa akiikokota bila kuiwasha. Hakujua kilichokuwa kikiendelea.
"Oy Tafu, uburuze huo mzigo hadi hapa tuupakize tusepe", Benja aliongea kwa sauti ya chini punde alipowasili.
Ahmed, kutokana na urefu wake na wembamba kushabihiana na Tafu, ilikuwa ni ng'umu kwa Benja kung'amua mapema. Ahmed aliushika mwili wa tafu huku akijifanya kuuburuza.
"Unazingua mshikaji wangu, yani kushika mkono tu na kuburuza huo mzigo unasumbuka hivyo, acha kumbwela kamanda wangu, Rich anatusubiri kule", Benja aliongea kwa kulaumu huku akiisimamisha pikipiki yake na kuelekea kumsaidia Tafu. Alipokaribia kumsogelea Ahmed ndipo machale yalimcheza. Aliiona sura ngeni kabisa machoni mwake. Alitaka kuupeleka mkono mfukoni ili aitoe bastola, ila spidi yake ilikuwa nyuma sana. Ahmedy alishaigundua janja ya benja. Aliilenga bastola yake yenye kiwambo cha kuzuia sauti aliyoificha nyuma ya mgongo wake kuelekea kwenye kiganja cha mkono wa kulia wa Benja. Risasi yenye spidi kali ilipenya kiganja cha Benja na kumfanya Benja apige yowe la maumivu. Ahmed alimsogelea Benja kwa wepesi wa hali ya juu na kumpiga mtama uliomuangusha Benja chini. Kisha akamlalia kwa juu huku akimuelekezea bastola yake kichwani.
"We kenge, naomba unijibu maswali yangu kabla sijapitisha risasi ya pili kwenye kichwa chako. Kwanini mnataka kumteka huyu muliemfuata", Ahmed alihoji kwa ukali huku amemgandamiza Benja pale chini. Benja hakujibu kitu, bali alikuwa akitweta tu.
"Watu viburi kama nyie ninawapenda sana", Ahmed aliongea huku akichukua kisu kidogo kilichokuwa kwenye mfuko wa mbele wa suruali yake na kukishindilia kwenye kiganja kilekile cha mkono wa Benja kilichojeruhiwa kwa risasi. Benja alitaka kupiga kelele ya yowe ila ngumi nzito ya Ahmed aliyompiga nayo kwenye shavu la kulia ilimnyamazisha. Damu zilikuwa zikimtiririka Benja kwa wingi. Ahmed alichana shati la benja na kumfunga kwenye viganja vyote viwili ili kuzuia damu kisha mahojiano yaliendelea.
"Haya nijibu haraka kabla sijabadili zoezi", Ahmed aliongea kwa ukali.
"Tu...tu...tumetu...mwa na Rich kuja ku...ku...kumteka....Aflo", Benja alijibu kwa shida kutokana na maumivu ya mdomo yaliyosababishwa na ngumi ya Ahmed. Ahmed alitafakari alipotajiwa jina la Aflo ndipo alipong'amua kwamba Aflo ni Alexander Florence.
"Kwanini munataka kumteka?", Ahmed aliuliza.
"Sijui", Benja alijibu kwa mkato. Ahmed hakuwa na muda wa kubembeleza muharifu. Alichukua kisu na kukichomeka kwa nguvu kwenye kiganja cha pili cha mkono wa Benja.
"Haya, niambie sasa kwanini munataka kumteka", Ahmed aliuliza tena.
"A....a...aliingilia dili lisilo muhusu", Benja alijibu.
"Alafu wewe, mimi sio babu yako, ninapokuuliza jambo naomba unijibu kiurefu na kwa ufasaha, umenielewa?", Ahmed aliongea kwa ukali huku akimshindilia Benja ngumi ya pua.
"Nisamehe Broo, utaniua bure. Nakuambia kila kitu, Rich ni kiongozi wetu,na ni askari mpelelezi kituo kikuu cha polisi Dodoma. Kuna wenzetu waliuliwa na Aflo, kwahiyo Rich alituagiza tuje kumteka Aflo kisha tumpeleke kwa Bosi Rich tukamtese hadi kufa", Benja alieleza kwa ufasaha.
"Kwahiyo ninyi ni polisi alafu pia munahusika na uhalifu", Ahmed aliuliza na Benja alitikisa kichwa kuonesha isjara ya kukubali.
Ahmed hakuwa na muda wa kupoteza. Alimpigia simu Aneth.
"Vipi, Aneth, kifurushi chetu kimeingia?", Ahmed aliuliza.
"Kishawekwa kwenye mikono salama.
Haikua kazi ngumu. Kiliposhuka tu tukakidaka", Aneth alijibu.
"Ok, kuna vifurushi vingine ninavyo hapa ila nahitaji nilale navyo usiku huu nikavihoji usiku kucha kabla sijavipeleka kituoni. Huwezi kunisaidia eneo la kwenda kujadiliana nao?", Ahmed aliuliza.
"Uko sehemu gani nikufate", Aneth aliuliza. Ahmed alimuuliza Benja mahala pale panaitwaje, kisha akamuelekeza Aneth.
Baada ya dakika zisizozidi kumi, gari la Aneth lilisogea pale.
"Koplo Benja, imekuwaje?", Aneth alipigwa na butwaa baada ya kugundua kwamba kifurushi alichotajiwa na Ahmed ni askari mwenzake.
Je, nini kitafuata?
USIKOSE SEHEMU IJAYO