Riwaya: Mkono Wa Chuma

Riwaya: Mkono Wa Chuma

RIWAYA : MKONO WA CHUMA

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA KUMI NA NANE.

_____________
ENDELEA....
_____________
Mswahili aliendelea na shughuli zake ndogo ndogo, huku kila muda akijipongeza kwa kutumia muda alioachwa peke yake kwa kumchoma sindano ya sumu yule mwanamke ambaye kwa maelezo yake alionekana anamjua fika yule mwanamke,

"alafu huyu BQ mbona amebadilika sana, au huyu sio yule mwenyewe, kwa maana mwenyewe alishakufa Katika ajali ya ndege" Mswahili alijiuliza mwenyewe bila kupata jibu kamili.

Baada ya saa moja, Dokta Smith alirejea na mizizi yake aliyotoka kuichimba, alipofika alimkuta yule bwana mswahili akiwa nje akikata nyama ya mnyama pori,

"wewe bwege ina maana hujatoka tangu muda ule?" Dokta Smith alimuuliza yule bwana Mswahili ambaye muda huo alikuwa akikinoa kisu kwa kukipitisha katika jiwe gumu la mlimani,

"ningetoka angekupikia mama yako? Mwendawazimu wewe" Mswahili alijibu na kumfanya Dokta Smith atabasamu, walishazoea kuishi katika maisha ya namna hiyo, utani, mizaa na matusi ya hapa na pale bila kuleteana kero.

Wakati Dokta Smith akiingia ndani ya hema, huku huyu Mswahili alikuwa hajiamini kabisa, alijua fika kuwa msala wa kifo cha yule binti ni lazima atapewa yeye,

"shauri yake bwana, hata nikisema nimemuua mimi atanipeleka wapi?" Mswahili aliongea mwenyewe huku akibinua midomo yake.

Wakati Mswahili akiwa katika mawazo hayo, uko ndani Dokta Smith aliingia na kumpima joto la mwili mgonjwa wake, akagundua joto lipo juu kiasi. Dokta Smith akachukua kitambaa na kukiloweka ndani ya sufuria yenye maji, kisha akaanza kumkanda BQ maeneo ya kichwani, alifanya hilo zoezi kwa dakika chache, kisha akaichukua ile mizizi aliyokuja nayo na kuichemsha. Ilipochemka katika kiwango anachotaka yeye, aliipua sufuria, kisha akamimina maji ya ile mizizi katika bakuri, akayapooza yale maji na kumnywesha BQ, kisha akatoka nje na kuungana na jamaa yake Mswahili.

"vipi hali ya mgonjwa?" Mswahili aliuliza,

"kidogo imeimarika, maana hata joto la mwili limeongezeka, tofauti na mwanzo, maana mwanzo alikuwa amepoa kabisa" Dokta Smith alijibu na kumfanya Mswahili ashangae, tena mshangao wa wazi kabisa, kwa maana alijiandaa kupokea habari za kifo, ila sasa anapokea habari tofauti,

"kwanini hafi jamani?" Mswahili aliuliza kwa jazba na kumfanya Dokta Smith amshangae,

"wewe mbona sikuelewi? tangu umezisoma zile katatasi za mikataba ya huyu dada, umeonekana kubadilika sana. Kwanini unamjuaje huyu dada?" Dokta Smith aliuliza huku akimuangalia rafiki yake huyo,

"ujue nini? yule Dada ndio BQ" Mswahili aliongea na kumtupia jicho Dokta Smith ambaye alikuwa bado hajamuelewa mwenzake,

"BQ? BQ ndo nini?" Dokta Smith aliuliza kwa mshangao,

"sio ndio nini, sema ndio nani?" Mswahili alimrekebisha mwenzake kisha akachukua chumvi katika kopo na kuipaka nyama aliyokuwa akiiandaa kwa ajili ya chakula,

"sawa, BQ ndio nani?" Dokta Smith ikabidi aulize kama alivyofundishwa,

"BQ alikuwa ni mlinzi binafsi wa rais aliyeondolewa madarakani, yaani Rais aliyepita kabla ya huyu, na ndio maana kama umesoma vyema ile mikataba, unaona walifanya na mtu aliyeitwa Tammy Semmy, ambaye ndiye huyo Rais aliyepita, ila wakati wakifanya hiyo mikataba, huyo Tammy Semmy alikuwa ni makamo wa Rais" Mswahili aliongea na kumuachia mwenzake nafasi ya kuuliza swali,
"sasa kwa maelezo yako hayo, ubaya wa huyu dada ni upi? maana hapo hawali ulisema huyu mwanamke ni mtu mbaya sana" Dokta Smith aliuliza,

"huyu dada ni elite killer, yaani muuaji wa kulipwa, kabla ya Tammy Semmy kulikuwa na Rais mwingine ambaye aliuawa, na aliyemuua ni huyu dada, ukimuondoa huyo Rais, pia Kuna watu wengi sana aliwaua" Mswahili aliongea na kumfanya Dokta Smith sasa ashtuke,

"kwa hiyo hafai ee?'' Dokta Smith aliuliza kwa hofu,

"hafai kabisa, sio mtu wa kumuachia aendelee kuishi, ndio maana nakushangaa kwa namna unavyoangaika kumtibu" Mswahili aliongea kwa uchungu,

"acha tu tumtibu, huwezi jua, huenda amebadilika au huenda hapendi kuua ila ni katika utafutaji tu wa ridhiki" Dokta Smith aliongea,

"endelea kumtetea, mpaka aje akuue wewe ndio utaona ubaya wake" Mswahili aliongea huku akiwasha moto katika kuni zilizokuwa katikati ya mafiga ya mawe,

"yote kheri, kama ataniua basi ujue ilipangwa iwe hivyo" Dokta Smith aliongea huku akiingia katika hema,

"shauri yako. Ukitoka utoke na wavu wa kuchomea nyama" Mswahili aliongea huku akiweka mafiga vuzuri, na muda huo jua lilikuwa limeshazama, giza ndio lilikuwa linaanza kutawala ndani ya msitu huo wa kutisha.

****************

Wakati hayo yakiwa yanajili, tunamuona yule kijana anayetumiwa na Rais akiwa na gari, alikuwa akielekea ikulu muda huo.

Alikuwa makini na barabara, sterling ya gari aliishikiria kwa nidhamu na mikono yake miwili ambayo ilikuwa ndani ya gloves, na katika kioo cha gari upande alikuwepo, alibandika picha ndogo iliyokuwa ikimuonesha mwanamke mmoja akiwa sura ya furaha akitembea na mtoto mdogo wa kike ambaye nae pia alikuwa na sura ya furaha. Yule kijana akapeleka mkono wa kulia katika ile picha na kuifuta kidogo, kisha akapeleka mkono machoni na kujifuta chozi lililokuwa likitiririka katika jicho lake la mkono wa kulia.

Na muda huo gari yake ilikuwa mbele ya geti la ikulu, walinzi wakamfungulia geti, akaipitisha gari na kulipeleka moja kwa moja katika eneo la maegesho, akatelemka na kuelekea moja kwa moja katika ofisi ya Rais,

"vipi mambo?" Rais alimsalimia kijana, na wakati huo Rais alikuwa anajiangalia katika kioo huku akijifuta futa usoni na kitambaa,

"safi mkuu" Kijana alijibu,

"nilisikia umeshindwa kumuua yule askari?" Rais aliuliza,

"sikufanikiwa mkuu, nisamehe sana" Kijana alijibu,

"siku hizi misheni zako zinafeli sana, yule dada ulichukua muda mrefu sana kumkamata na kumuua, ingawa sina uhakika kama amekufa kweli. Huyo Askari wa jana umeshindwa tena kumuua" Rais aliongea huku akiwa hamuangalii yule kijana,

"ni kweli mkuu, ila nadhani ni makosa madogo tu niliyafanya mpaka yule Askari akapata upenyo wa kunitoroka" Kijana aliongea,

"sawa, nina kikao muda huu na wawekezaji, ngoja nikaongee nao, wewe tutaongea baadae" Rais aliongea huku akitengeneza kora ya shati lake la bluu bahari lililokuwa ndani ya koti la suti ya rangi nyeusi.

"sawa mkuu" Kijana alijibu kikakamavu,

"muda huu unaenda wapi?" Rais alimuuliza,

"nataka niingie karakana" Kijana alijibu na kumfanya Rais amuangalie kwa umakini kidogo,

"umepata tatizo?" Rais aliuliza,

"hapana, nataka nikakae tu" kijana alijibu na muda huo mlango wa ofisi ya Rais ulikuwa ukigongwa,

"ingia" Rais aliitikia ile hodi, ataingia binti mmoja mfanyakazi wa mule ikulu,

"Mkuu, muda umefika wa kwenda katika chumba cha mkutano, zimebaki dakika tatu tu" Binti aliongea huku akiwa amesimama kwa heshima mbele ya Rais. Rais akamgeukia kijana wake,

"baadae" Rais aliongea na kutoka nje, kisha yule kijana akafuatia kwa nyuma, ila yeye alitoka moja kwa moja mpaka nje, ataingia ndani ya gari lake, akaliondoa gari.

Alishika barabara mpaka katika nyumba moja kubwa iliyokuwa na uzio mrefu wa ukuta. Gari ilipofika katika geti, geti lilifunguka lenyewe, akaingiza gari kisha geti likajifunga lenyewe. Akatelemka katika gari na kuingia ndani ya nyumba yake, akapitiliza mpaka nyuma ya nyumba ambapo kulikuwa na nyumba nyingine ndogo ndogo. Akaingia ndani ya nyumba hiyo, ambayo ilikuwa na vyuma vingi vipya. Kijana akaenda katika mlango wa chumba kimoja na kuufungua, kisha akaingia. Katika kile chumba kulikuwa na kitanda kidogo cha chuma, na ukutani kulikuwa na kioo.

Kijana akaelekea katika kioo na kujiangalia, kisha akaziondoa gloves zake mikononi, cha ajabu mikono yake ilikuwa ya chuma, kisha akavua shati lake, ajabu nyingine ni kuwa kuanzia chini ya shingo, mwili wake wote ulikuwa chuma, alikuwa kama roboti, kijana akajiangalia kwa muda kisha akasikitika kwa huzuni, akachukua kifaa cha kufungulia nati na kupachika waya wa kile kifaa katika umeme, kisha akakaa chini na kukipeleka kile kifaa katika nati zilizokuwa ubavuni, akaanza kujifungua.

*************

Siku iliyofuata, muda wa saa mbili asubuhi, Sajenti Minja alikuwa hotelin pamoja Tom. Sajenti Minja alimuita Tom hilo eneo kwa lengo moja tu, kuja kuangalia mchoro wa taswira wa mtu anayedaiwa alimvamia Sajenti Minja, pia huyo huyo mtu ndio anadaiwa alimuua BQ.

Tom alikuwa makini akiiangalia ile picha,

"huyu ndiye yeye kabisa, mchoraji ana kipaji kikubwa sana" Tom aliongea huku akiendelea kuuangalia ule mchoro,

"kama na wewe umeridhika na huo mchoro, basi nadhani acha niende kituoni sasa, nikamuoneshe mkuu huu mchoro, maana yeye ndiye aliyetoa maagizo huu mchoro uchorwe jana, kisha leo nimpelekee" Sajenti Minja aliongea,

"basi sawa braza, wewe nenda tu, alafu ukipata muda tuwasiliane" Tom aliongea,

"tuwasiliane?, una habari mpya?! " Sajenti Minja alimuuliza Tom,

"kwani kuwasiliana mimi na wewe ni mpaka niwe na habari mpya bro?" Tom aliuliza huku akitabasamu,

"sawa basi. Hivi si bado hujapata kazi?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,

"bado braza" Tom alijibu,

"sawa basi, tutaongea baadae hilo suala, maana kukaa mjini bila kazi ni mtihani" Sajenti Minja aliongea,

"ila mshahara wangu unaingia, kwa maana kule wilayani nahesabika bado mfanyakazi" Tom aliongea,

"aah, kwa hiyo wewe ni mfanyakazi hewa?" Sajenti Minja aliuliza kwa utani huku akicheka,

"baadae bwana braza, nakuchelewesha tu hapa" Tom aliongea huku akitoka nje, kisha Sajenti Minja nae akatoka na kufunga mlango wa chumba hicho cha hotel. Sajenti Minja akatoka na kuchukua bajaj iliyomfikisha mpaka kituoni, kisha akashuka na kuelekea katika ofisi ya mkuu wake, alipoingia alitoa heshima,

"kaa chini" Mkuu wa polisi alimwambia Sajenti Minja, kisha Sajenti Minja akakaa katika kiti,

"mchoro unao?"Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja,

"ndio mkuu" Sajenti Minja alijibu huku akiutoa ule mchoro kutoka katika bahasha kubwa ya kaki, mkuu wa polisi akaupokea na kuukunjua ule mchoro, akauangalia kwa sekunde tu, akashtuka,

"huyu ndio huyo mtu aliyekushambulia juzi?" Mkuu wa polisi aliuliza kwa mshtuko,

"ndio huyu, pia ndiye aliyemuua yule dada mtuhumiwa wa mauaji" Sajenti Minja alijibu,

"haiwezekani" Mkuu wa polisi aliongea huku akitoa tabasamu la taharuki na kumfanya Sajenti Minja hasielewe ni kitu gani kinaendelea,

"kwanini isiwezekane mkuu?" Sajenti Minja aliuliza kwa mshangao,

"unamjua huyu?" Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja,

"hapana, ni nani kwani?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya mkuu wake ajikune kichwa huku akiwa bado ahamini kitu anachokiona katika ule mchoro, hapo Sajenti Minja akahisi kuchanganyikiwa zaidi baada ya kumuona mkuu wake akiwa hajihamini kabisa, kwa maana tangu ameanza kazi hapo, hiyo ni mara ya kwanza anashuhudia mkuu wa polisi akiwa amekosa amani kabisa.

"Minja, muda wowote nakuondoa kazini, naona hauna makini tena, huo mchoro sio wa mtu aliye hai, ni mchoro wa marehemu" Mkuu wa polisi aliongea kwa hasira na kuitupa ile picha mezani, Sajenti Minja akatoa macho ya mshangao, alikuwa bado ahamini kile anachokisikia kutoka kwa mkuu wake, ilikuwa ni habari mpya kwake, yaani mtu waliyepambana naye siku mbili nyuma, leo anaambiwa yule mtu ni marehemu, Sajenti Minja hakuamini, na wala hakutaka kuamini, ila ukweli ulikuwa ni ule alioushikiria mkuu wa polisi, kuwa yule mtu alishakufa siku nyingi tu, alikufa miaka mitatu iliyopita......

**********ITAENDELEA**********

the Legend☆
 
RIWAYA : MKONO WA CHUMA

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KUMI NA TISA.

__________________
SONGESHA...
__________________

"hivi we mzee ni mwendawazimu? yaani mtu amenishambulia juzi tu usiku alau unasema alishakufaga mtu mrefu'' Sajenti Minja aliongea ndani ya nafsi bila kutoa sauti, hakutaka kabisa kuamini maneno ya mkubwa wake huyo.

"ujue Minja kama hii kazi inakuwa ngumu kidogo kwako, ni bora useme mapema, ila mimi siamini kama kazi hii itakushinda. Ila vielelelezo unavyoniletea ndio vinapunguza imani yangu kwako" Mkuu wa polisi aliongea huku akimtazama Sajenti Minja,

"samahani mkuu kama nitakuhudhi kwa swali langu. Hivi huyu mtu amekufa lini? jana au leo?! " Sajenti Minja aliuliza huku akimuangalia mkuu wake kwa mshangao,

" jana au leo? Ulianza alikufa miaka mingapi iliyopita" Mkuu wa polisi alijibu huku akikunja ndita katika paji la uso wake,

"miaka tena?, kwanza umemjuaje na alikuwa ni nani?" Sajenti Minja aliuliza,

"anaitwa Ray Charles" Mkuu wa polisi alijibu,

"alikuwa ni nani?" Sajenti Minja alimuuliza mkuu wake, ila mkuu hakutaka kuendelea na maswali muda huo,

"sihitaji maswali zaidi, wewe kaendelee na kazi zako, ila kumbuka kuwa hiyo kazi unayoifuatilia ni kwa ajili ya manufaa ya serikali yako, sasa endapo utaendelea na upuuzi huo wa kuniletea picha za watu waliokufaga miaka mingi iliyopita na kuwabebesha tuhuma, tambua kazi utaiweka ajira yako hatarini" Mkuu wa polisi aliongea na kumfanya Sajenti Minja ainuke katika kiti, hakutaka kujibu kitu, alikuwa na mshangao ulioambatana na viulizo vingi visivyokuwa na idadi. Sajenti Minja baada ya kuinuka, alitoka nje bila kuaga.

Kama Kuna siku alivurugwa, basi hiyo siku ni leo. Sajenti Minja akaingia katika gari yake na kuondoka huku akiwaza ampe taarifa Tom au akae kimya kwa muda afanye uchunguzi wake?

"kwa kuwa jina nimeshalijua, haitonisumbua?" Sajenti Minja aliongea mwenyewe huku akifikicha jicho lake ambalo ni chongo.

Ilimchukua dakika chache tu Sajenti Minja kufika katika hoteli anayoishi kwa muda huo, alishuka katika gari na kupitia funguo yake mapokezi, kisha akaelekea katika lifti.
Dakika chache tu alikuwa nje ya mlango wa chumba chake, akafungua na kuingia, alipoingia alivua shati na kulitupa katika kochi, kisha yeye akajitupa kitandani, akaitoa simu mfukoni na kuelekea katika application iliyoandikwa "GOOGLE" akabonyeza na kwenda katika sehemu iliyoandikwa "SEARCH" hapo akaandika RAY CHARLES, hilo ndilo jina aliloambiwa na mkuu wake, hilo ndio jina la yule kijana aliyemvamia siku chache nyuma.

Matokeo yaliyokuja baada ya kuandika jina lile, Ray Charles aliyeonekana ni yule mwanamumziki wa kimarekani aliyekuwa na ngozi nyeusi, yaani mmarekani mweusi, aliyezaliwa 1930, na kufariki mwezi wa sita wa mwaka 2004.

Historia ya huyo Ray Charles, ilionesha kuwa alianza kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitano, na alipofikisha miaka saba alikuwa kipofu kamili, yaani hakuwa na uwezo wa kuona kabisa. Na mwisho Ray Charles alikufa akiwa na miaka 73, hiyo ni mwaka 2004, na kilichomuua ni ugonjwa wa ini.

Sajenti Minja akatoka katika habari hiyo, kwa maana huyo Ray Charles mmarekani alikuwa anazifahamu habari zake, alikuwa ni mtu maarufu sana.

Akaendelea kupekua habari za watu wengine ambao wana jina hilo hilo la Ray Charles, ndipo alipokutana na kichwa cha habari "WANAJESHI WA TANZANIA WAMEKUFA BAADA KUVAMIWA NA AL SHABAB" hicho kichwa cha habari kikamvutia, kwa maana mmoja wa hao wanajeshi waliouawa, jina aliitwa Raymond Charles.

Sajenti Minja akaifungua ile habari na kuisoma kwa umakini,

"wanajeshi watatu wamekufa baada ya kukamatwa na kundi la kigaidi la AL shabab, inadaiwa wanajeshi hao walikuwa wameingia nchini Somalia kwa lengo la kwenda kumkamata na kumpeleka katika vyombo via sheria mmoja kati ya viongozi wa juu wa AL shabab, ila waligundulika na kukamatwa, kisha wakapewa mateso makali kabla hawajafa, na baadae inasemekana walipigwa risasi na kutangazwa katika vyombo vya habari huku nyuma ya miili yao wakiwa wamesimama wanamgambo wa AL shabab wakiwa wameshika bunduki na kujifunika usoni kwa kutumia vitambaa.
Majina ya wanajeshi hao, ni Luteni Said Sedan, kanali Raymond Charles, na kanali Mdendu Kidufu.

Jeshi la Tanzania limethibitisha kuwa hao ni watu wao, ila wamekanusha vikali kuwa walienda Somalia kwa ajili ya kwenda kumkamata kiongozi wa AL shabab, wanachodai wao ni kuwa wanajeshi hao walikuwa katika Jeshi la umoja wa Africa, lililokuwa Somalia kwa ajili ya kulinda amani" Habari ilisomeka hivyo, Sajenti Minja akajikuna kichwa, ila bado hakuamini huyo mtu ndio huyo aliyeambiwa amekufa au lah! Akaamua atafute na picha za hao wanajeshi, hapo ndipo alipata mshangao, kwa maana kwenye jina la Raymond Charles, ndipo kulikuwa na picha ya yule kijana anaemtafuta,

"kweli amekufa, sasa kwanini yupo hai? ni mzimu?" Sajenti Minja alijiuliza huku akiwa ameikazia macho ile picha ya yule mwanajeshi aliyekufa, ila ndio huyo huyo ambaye alitaka kumuua siku chache zilizopita.

"hii ni ngumu kukubalika, haiwezekani kwa kweli" Sajenti Minja aliongea huku akiinuka kitandani, akasimama na kuvaa shati, akavua tena, alikuwa kama kachanganyikiwa,

Akaiangalia simu yake, kisha akatafuta namba ya Tom na kumpigia, simu ikaanza kuita,

"Tom vipi?" Sajenti Minja aliongea mara baada ya upande wa pili kupokea simu,

"poa bro, nambie" Tom alijibu katika hali ya uchangamfu,

"una kazi muda huu?! " Sajenti Minja aliuliza,

"nipo tu, nasoma soma habari mitandaoni" Tom alijibu,

"njoo hapa hotelini, chukua bajaj" Sajenti Minja aliongea,

"sawa bro, ila unanitisha" Tom aliongea huku akicheka kwa utani,

"njoo ili uje uogope zaidi" Sajenti Minja alijibu na kumfanya Tom aanze kupata wasiwasi wa kweli,

"Kuna nini kwani?" Tom aliuliza, safari hakuwa akicheka kama mwanzo,

"bwana njoo, utayajua huku huku" Sajenti Minja aliongea na kukata simu, kisha akajitupa kitandani, macho yakaangalia pangaboi namna linavyozunguka, ila akili haikuliwaza pangaboi hilo, akili iliwaza juu ya Ray Charles, hilo ndio jina lililomvuruga kwa wakati huo.

**************

Upande wa msituni, anaonekana Dokta Smith na yule bwana mswahili wakiwa wamekaa pembeni mwa BQ, Dokta Smith alikuwa akimnyesha dawa BQ ambaye alikuwa bado fahamu hazijamrudia, na wala kulikuwa hakuna dalili za fahamu kumrudia.

Baada ya Dokta Smith kumaliza kunywesha BQ dawa, alifungua sanduku lake na kukitoa kile kukichukua kile kichupa kilichoandikwa "POISON", yule bwana mswahili akakikumbuka kile kichupa, kuwa alishawahigi kukichukua na kufyonza dawa ile kwa sindano na kumchoma BQ.

"mbona hii dawa imepungua sana, imemwagika nini?" Dokta Smith aliuliza huku akikagua katika sanduku aone kama ile dawa imemwagika kweli, lakini hakuona kitu, Dokta Smith akapuuza, akachukua bomba la sindano na kufyonza ile dawa ya kwenye kichupa, kisha akamchoma BQ katika mkono, bwana mswahili akajifanya ameshtuka,

"wewe mbona unamchoma sindano ya sumu?" Mswahili aliuliza huku akijifanya amepaniki,

"wewe si ulikuwa unataka afe? basi acha afe" Dokta Smith aliongea huku akitabasamu, ila kitu ambacho hakukijua, ni kuwa tayari yule mswahili alishawahi kumchoma BQ ile dawa, na BQ hakufa, kwa hiyo alichokuwa akikifanya yule bwana mswahili, ni kumdadisi tu Dokta Smith bila Dokta Smith kujua kitu,

"acha ujinga wewe, yaani unamchoma mtu sindano ya sumu alafu unacheka?" Mswahili aliinuka kwa hasira sasa, hata sura yake ilionesha amepaniki,

''subiri wewe punguani, unafikiri mimi nina akili za kijinga kiasi hicho? Hii sio sumu, bado haijakamilika kuwa sumu, ili iwe sumu, ni lazima hii dawa ichanganywe na mkojo, ila bila kuchanganya na mkojo, inakuwa inaongeza joto tu mwilini" Dokta Smith aliongea huku akirudishia ile dawa katika sanduku lake,

"siamini mpaka nione matokeo yake" mswahili aliongea huku akiwa amesimama, ila kwa upande mwingine alishajua namna ya kuichanganya ile dawa na kuwa sumu.

"wewe pumbavu kweli, kwa hiyo unabishana na mimi mtaalamu wa dawa? hii ingekuwa sumu, huyu angeshakufa kitambo tu, ebu ngoja niibebe kidogo alafu tuingie msituni uone" Dokta Smith aliongea huku akifungua sanduku lake na kukitoa tena kile kichupa cha ile dawa, kisha akaipunguzia ile dawa katika kichupa kingine kidogo, kisha akachukua na bomba la sindano,

"haya, twende nikakuoneshe sasa" Dokta Smith aliongea huku akielekea nje, mswahili nae akabeba camera yake na kumfuata Dokta Smith, alidhamiria haswa kujua undani wa ile sumu.

Wakatoka na kufunga ngome yao, kisha wakaingia msituni, lengo lilikuwa ni Dokta Smith kumuonesha yule bwana mswahili kazi ya ile sumu.

Wakafanikiwa kukamata kima wawili, uwa wanamitego yao ambayo hutegea wanyama wa kitoweo chao, na pia mitego mingine uwa kwa ajili ya kukamata wanyama kwa ajili ya utafiti wao.

Dokta Smith akawasogelea wale kima huku mswahili akiangalia kwa umakini. Dokta Smith akatoa kile kichupa, kisha akatoa bomba la sindano, akafyonza dawa katika kichupa na kumchoma kima wa kwanza,

"unaona, bado kima yupo vizuri tu. Chukua hiki kichupa, kojolea kidogo tu, alafu tuangalie zoezi linalofuata" Dokta Smith aliongea huku akimpatia yule mswahili kile kichupa ili aweke mkojo wake,

"Sasa si ungekojolea hata wewe?" Mswahili aliongea huku akikichukua kile kichupa na kusogea pembeni kidogo, kisha akakojolea kidogo kile kichupa, alafu akamrudishia Dokta Smith. Dokta Smith akakipokea kisha akafyonza dawa iliyochanganywa na mkojo ambayo ipo ndani ya kile kichupa, akamchoma yule kima mwingine, sekunde mbili tu baada ya yule kima kuchomwa ile sindano, akaanza kushtuka kama ana kifafa, alifanya hivyo kwa sekunde thelathini, kisha akaanguka na kufa,

"umeona sasa, hii ndio sumu, ila kabla Haijachanganywa na mkojo inakuwa sio sumu. Kwa hiyo yule dada hawezi kufa, nilimchoma hii dawa ikiwa haina mkojo" Dokta Smith aliongea huku akimuonesha kile kichupa yule mswahili, mswahili akakikwapua kile kichupa mikononi mwa Dokta Smith,

"lete ni kusikia. Hivi kama nikitaka nimuwahi ili hasife, natakiwa nimpe dawa gani? au maziwa?" Mswahili aliuliza huku akikitia mfukoni kile kichupa,

"akishafikia hatua ya kupapalika hivo, ujue ndio basi hawezi kupona tena, ni wa kufa tu, hata aje nabii mwenye miujiza kiasi gani, hawezi kumuepusha na kifo kiumbe aliyechomwa hiyo sumu" Dokta Smith alijibu,

"duh, ni hatari sana" Mswahili aliongea huku akijipiga piga katika mfuko wake wa suruali alioweka kile kichupa cha ile sumu,

"kitupe tu, cha nini sasa?" Dokta Smith aliuliza wakati huo mswahili alijifanya hasikii, akageukia upande wa pili kabisa, na akatoa camera yake na kujifanya anapiga picha huku akitembea kuelekea mbele, Dokta Smith akatabasamu, kisha akamuachia yule ambaye alikuwa mzima, na yule aliyekufa, alimtupa, kisha akageuka kumtazama yule mswahili, akamuona kwa mbali akiendelea kupiga picha, Dokta Smith akatabasamu huku akitikisa kichwa kwa masikitiko.

Upande wa pili, huyu mswahili, hakuwa akipiga picha kama Dokta Smith anavyodhani, huyu mswahili alichokuwa akifanya ni kuzuga anapiga picha huku akitembea, lengo lake lilikuwa ni kumtoroka Dokta Smith na kurudi katika hema, ili akammalize BQ.

Baada ya dakika ishirini za kujifanya anapiga picha, alifanikiwa kumtoroka Dokta Smith, kisha akarudi mpaka katika ngome, akafungua kufuri na kufunga kwa ndani katika ile "cage" kisha akanyoosha mpaka katika hema, akaingia, akafungua sanduku na kutoa bomba la sindano, akatoa mfukoni kile kichupa cha ile dawa kilichochanganywa na mkojo, akanyonya ile dawa kwa ile sindano, kisha akamchoma BQ mkononi, kisha mswahili akainua kichwa kutazama mlangoni mara baada ya kuhisi Kuna mtu kasimama, ndipo alipokutanisha macho yake na Dokta Smith akiwa anamuangalia huku machozi yakimtoka, na muda huo BQ alianza kushtuka kama mtu mwenye kifafa, Dokta Smith akatoka nje na kukalia katika jiwe, akawa analia kwa uchungu, atafanyaje sasa na alishamwambua yule mswahili kuwa mtu akifikia katika hali ile ya kushtuka vile, hawezi kupona tena, ni lazima afe tu. Dokta Smith alilia kwa uchungu sana, wakati ndani yule mswahili alikuwa anashangaa namna BQ anavyopapalika pale chini, kwa namna alivyokuwa akipapalika, roho ya huruma ikamuingia yule mswahili, alitamani kumsaidia ila hakuwa na njia ya kutoa msaada, na kipindi hicho BQ alikuwa anatulia na mwili ukanyooka, yule mswahili akatupa lile bomba la sindano, akaanza kulia, alijilaumu kwa kile alichofanya, na upande wa nje, Dokta Smith alikuwa akilia kwa sauti nzito na uchungu mkuu, ngome iligubikwa na machozi...

*********ITAENDELEA*********

the Legend☆
 
RIWAYA : MKONO WA CHUMA.

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA ISHIRINI.
_________
TEMBEA...
_____________
Yule bwana akajitupa chini kabisa, nguvu zilikuwa kama zinataka kumuishia, mara akainuka na kutoka nje, akamkuta Dokta Smith akiwa amekaa huku akilia,

"naona umetimiza hadhma yako" Dokta Smith aliongea huku akijifuta machozi, ila yule bwana mswahili alishindwa kujibu, alikuwa akilia tu.

Dokta Smith akainuka taratibu na kuingia ndani ya hema, huku machozi yakiendelea kumtoka, baada ya kuingia ndani, alifungua sanduku lake na kutoa kichupa kidogo sana kilichokuwa na dawa ya maji iliyokuwa na rangi ya ugoro pembeni iliandikwa antibiotic, kisha akamkamulia BQ mdomoni maji ya kile kichupa, alafu akamuondoa shuka mwilini na kumuacha akiwa amelala mtupu.
Alafu akachukua chupa ya maji safi, akaijaza maji aliyoyachanganya na mizizi iliyotwangwa, akamtundikia kama drip, kisha Dokta Smith akatoka nje huku akijifuta machozi, akaenda kukaa na yule mswahili,

"kile kichupa cha sumu ulichotumia kumuua huyo mwanamke umekiweka wapi?" Dokta Smith aliuliza huku akiwa na hasira,

"nisamehe sana rafiki yangu, roho inaniuma sana kufanya kitendo hiki" Mswahili aliongea huku akifuta kamasi kutokana na kilio,

"Ile sumu upo wapi?" Dokta Smith aliuliza kwa kufoka kiasi kwamba mate yakamtoka, lakini yule bwana mswahili hakujibu kitu aliendelea kulia tu.

Dokta Smith akaona kama anadharauliwa vile, akampiga yule bwana mswahili ngumi kali ya kichwani,

"Ile sumu ipo wapi?" Dokta Smith aliuliza kwa hasira huku akimkwida shati,, yule bwana Mswahili akaona ni vyema aitoe ile chupa ya sumu, akaitoa mfukoni na kumpatia Dokta Smith,

"mpumbavu wewe" Dokta Smith aliongea huku akiikwapua ile chupa, kisha akamsukuma yule Bwana Mswahili, kisha Dokta Smith akakifungua kile kichupa, akamkata jicho kali yule Mswahili, kisha akaigida dawa yote iliyokuwa katika kile kichupa. Kuona hivyo yule Mswahili akahamaki, akabaki amepigwa na bumbuwazi,

"unafanya nini wewe?" Mswahili aliuliza huku akijaribu kumpora ile dawa, ila alikuwa amechelewa, alifanikiwa kumpora ila chupa ilikuwa tupu, tayari dawa yote aliinywa Dokta Smith.

Mswahili akapiga hatua moja nyuma na kubaki akishangaa, ghafla Dokta Smith akaanza kupapalika kwa kurusha miguu huku na uko kama anakata roho, kisha akanyooka na kutulia.

Mswahili akajishika kichwa na hasiamini anachokiona, kulia alishindwa, kucheka alishindwa, alibaki mdomo wazi huku nguvu zikimuishia mwilini.

*******************

Sajenti Minja alikuwa yupo kitandani muda huo akimsubiri Tom, bado kichwa chake kilikuwa kikimuwaza yule kijana aitwaye Ray Charles, yaani alikuwa hajielewi kabisa, yaani kwanza alikuwa ahamini maelezo ya habari aliyoisoma mtandaoni kuhusu mtu yule kufa, na pia aliilalazimisha akili yake ijaribu kutofautisha kati ya picha ya mtu yule aliyesoma habari zake kwenye gazeti na mtu yule aliyemvamia siku chache zilizopita, lakini ilishindikana, kwa maana mtu ndiye yule yule mmoja.

Wakati akiwa katika tafakari nzito, alisikia mlango ukigongwa kwa nguvu, akainuka na kuchukua bastola yake, hakuwa akijiamini kabisa, alishamuogopa Ray Charles baada ya kusoma habari zake, alihisi ni mzimu au mtu hasiye wa kawaida.

Sajenti Minja alisogea mlangoni kwa umakini mkubwa, huku nako mgongaji alizidisha nguvu ya kugonga mlango. Sajenti Minja aliufikia mlango na kufungua kwa nguvu, kisha akaelekeza bastola mlangoni,

"we we we bastola hiyo!" Tom aliongea kwa uoga huku akijiziba uso wake kwa mikono, Sajenti Minja akacheka,

"we lazy kweli, yaani unaizuia risasi kwa mkono?" Sajenti Minja aliongea huku akiendelea kucheka,

"mambo gani hayo ya kutishiana bastola hivyo?" Tom aliongea kwa kulalamika huku akiingia ndani,

"sio nakutishia, najihami tu kutokana na kitu nilichokigundua leo" Sajenti Minja aliongea huku akikaa katika kochi,

"ni nini tena?" Tom aliuliza,

"si unakumbuka ule mchoro niliokuonesha siku iliyopita?" Sajenti Minja aliuliza huku akiiweka bastola yake pembeni,

"ndio, si ya yule jamaa aliyekuvamia?" Tom alijibu kwa mtindo wa kuuliza,

"swadakta, ndio huyo huyo" Sajenti Minja alijibu,

"amefanyaje sasa?" Tom aliuliza,

"Yule bwana, ni mtu aliyekufa. Yaani inasemekana amekufa muda mrefu tu" Sajenti Minja aliongea na kumtazama Tom usoni, uso wa Tom ulionekana kutaharuki kabisa,

"sijakuelewa bro" Tom aliongea huku akiwa bado kataharuki,

"ni somo gumu sana kulielewa, ila shika hii simu na uangalie hii habari" Sajenti Minja aliongea huku akimpatia Tom simu yake.

Tom akaanza kuipitia ile habari, alisoma mpaka akaimaliza, akarudia tena, akaisoma mpaka akaimaliza.

"tayari nimeimaliza, sasa hii habari inahusiana vipi na yule jamaa aliyekuvamia?" Tom aliuliza huku akitaka kumrejeshea Sajenti Minja simu,

"umeangalia na picha ya huyo mwanajeshi uliyesoma habari zake?" Sajenti Minja alimuuliza Tom huku akiwa hataki kupokea simu,

"picha zipo kwa wapi?" Tom aliuliza,

"chini kabisa ya hiyo habari" Sajenti Minja alijibu, kisha Tom akashuka mpaka chini katika ile habari, hapo ndipo alipopigwa na butwaa, ni kweli kabisa, picha ya mtu ambaye habari zake inasemekana alikufa, ndiye yule yule Tom aliyemshuhudia nyumbani kwa Sajenti Minja siku chache nyuma.

"hii haiwezekani" Tom aliongea kwa kupaniki,

"ndio imeshawezekana sasa" Sajenti Minja aliongea,

"haya mambo mbona kama ya Sudy Bakari? au amerudi?" Tom aliuliza huku akimuangalia Sajenti Minja,

"sijui, ebu chekecha kichwa ili tupate kitu" Sajenti Minja aliongea kivivu,

"Sasa mimi nitachekechaje kichwa? sijui pa kuanzia" Tom aliongea huku akiitupia kitandani simu ya Sajenti Minja,

"lazy sana wewe, hivi taaluma yako ni nini?" Sajenti Minja aliuliza huku akiinua kichwa chake kumtazama Tom,

"mimi ni muandishi wa habari" Tom alijibu huku akimtazama Sajenti Minja,
"tumia taaluma yako kupata ukweli, usikae kizembe" Sajenti Minja aliongea,

"Sasa mbona sina ajira, nitatumiaje taaluma yangu kupata ukweli? si bora Ningekuwa naandika gazeti au natangaza " Tom alijibu,

"unajua ulimwengu ni kama kijiji? Ebu tafuta maneno ya kujaribu kuchimbua hii habari ya huyu mtu, ukiyapata you jaribu kupost mtandaoni ili tuone ni nini kitafuata" Sajenti Minja alimuelekeza Tom,

"bro hukumbuki kipindi kile nilifanya hivyo kwa lile tukio la waziri wa ulinzi? nilikutana na kashkash nyingi sana. Kwa hiyo bro hilo wazo lako siliungi mikono, naogopa" Tom aliongea,

"wewe fanya kama inawezekana, nakuhakikishia, mimi na vyombo vya usalama tutakuwa nyuma yako" Sajenti Minja aliongea,

"bro usiseme hivyo, mimi najua kwa namna nilivyoteseka" Tom aliongea kwa huruma,

"mbona huniamini wewe, amini mimi nipo nyuma yako" Sajenti Minja alijaribu kumshawishi Tom,

"ujue bro wasiwasi wangu ni kama huyo mtu atajua na mimi nafuatilia mambo yao, ndo hatari itapoanzia, nadhani sasa hivi hana mpango na mimi kwa kuwa anajua simfuatilii" Tom aliongea,

"unakuwa kama mtoto wa kike bwana, watoto wa kiume uwa hatuogopi kupambana Tom" Sajenti Minja aliongea kwa kusihi,

"sawa bro, ngoja nifikirie cha kuandika" Tom aliongea kiunyonge huku akisikitika,

"huo ndio uanaume sasa, basi wewe endelea kufikiria, ngoja nikalete chakula nje" Sajenti Minja aliongea huku akiinuka kitandani na kuvaa shati yake, kisha akaelekea nje na kumuacha Tom akiwa peke yake ndani.

Tom baada ya kufikiri kwa muda mchache kidogo, akaitoa simu yake mfukoni na kuingia "Facebook" akaenda katika account yake na kuandika "UNAMJUA RAYMOND CHARLES? ASKARI WA TANZANIA ALIYEKUFA MIAKA MITATU ILIYOPITA, ILA AMEONEKANA TENA AKIWA HAI. BAADA YA SIKU MBILI NITAKUJA NA HABARI KAMILI" Tom alindika na kurudia kusoma alichoandika, kisha akapost ule ujumbe, akatoka Facebook.

Baada ya dakika mbili, Sajenti Minja alirudi ndani akiwa na chipsi na soda,

"dogo umeshapata cha kuandika au bado unafikiria?" Sajenti Minja alimuuliza Tom,

"nimeshaandika na kutupia Facebook kama dakika mbili zilizopita" Tom alijibu,

"safi, safi sana, tusubiri majibu" Sajenti Minja aliongea kwa furaha huku akimpa Tom mfukn mmoja uliokuwa na chipsi na soda,

"sasa bro mimi niache niende, hizi chipsi nitaenda kula na shemeji yako" Tom aliongea huku akiinuka katika kiti,

"sawa, we wahi, chukua hii utapanda bajaj" Sajenti Minja aliongea huku akimpa Tom noti ya shilingi elfu kumi, Tom akaipokea na kuiweka mfukoni,

"ngoja nikutoe basi" Sajenti Minja aliongea huku akisimama,

"hapana, hapana, we endelea kula tu" Tom aliongea,

"sio vizuri bwana, ngoja nikufikishe hata hapo mapokezi" Sajenti Minja aliongea kwa kusihi,

"we kula bwana, kwani mimi mgeni bwana?!" Tom aliuliza na Sajenti akabaki anatabasamu,

"usiku mwema basi" Sajenti Minja alimuaga Tom,

"poa bro, na kwako pia" Tom aliongea kisha akaondoka, akatoka nje ya geti la hotel, na kuingia barabarani, safari ya kurudi kwake ilianza usiku ule, hakuchukua bajaj, aliamua atembee tu kwa kuwa hakuwa na haraka ya kuwahi kurudi.

***************

Mida Ile ile ya usiku, anaonekana Ray Charles akiwa ameegesha gari yake nyeusi pembezoni mwa barabara, na upande wa pili wa barabara kulikuwa na nyumba nzuri ya Kisasa yenye geti jeusi.

Ray Charles alikuwa akiitazama ile nyumba huku akionekana ana huzuni, alipeleka mkono wake katika picha ndogo aliyoibandika katika kioo cha gari yake, akaipapasa ile picha ambayo alionekana yeye akiwa na mwanamke mrembo, pamoja na mtoto wa kiume wa miaka minne.

Ray aliipapasa ile picha huku akiuma meno yake kwa hisia kali, wakati akiendelea kuwa katika hali hiyo, alishuhudia gari ikasimama mbele ya ile nyumba, kisha akatelemka yule mwanamke mrembo aliyekuwa katika picha ya Ray Charles, baada ya hapo yule mwanamke akasogea mlango wa nyuma na kumchukua mtoto, ambaye huyo mtoto nae yupo katika picha ya Ray Charles. Kisha ile gari ikaondoka, yule mwanamke akagonga geti, mlango ukafunguliwa, yule mwanamke akaingia ndani, Ray Charles akatabasamu, ila tabasamu halikubeba furaha.

Simu yake ikaanza kuita, akaiangalia na kupokea,.
"naam mheshimiwa" Ray Charles aliongea baada ya kupokea simu,

"wewe umeona habari zinazozagaa mitandaoni muda huu?" Rais aliuliza kwa ukali,

"hapana mheshimiwa" Ray Charles alijibu huku akijiuliza ni habari gani?

"Kuna mpumbavu mmoja amepost habari zako Facebook, na watu wengi wameonekana kuvutiwa na habari, ile, ebu ingia uitafute hiyo habari, aliyepost anaitwa Thomas Anthony" Rais aliongea na kukata simu, Ray Charles akaingia mtandaoni na kutafuta jina aliloambiwa, kweli akaikuta ile habari, akaipitia muda mfupi tu, kisha akabonyeza katika jina la huyo aliyeandika habari, shida yake ilikuwa kuiona picha tu ya huyo aliyeandika hiyo habari. Alipofungua picha, akakutana na picha za Tom, Ray Charles akatabasamu kwa hasira, maana huyu mtu anamjua, na kipindi hicho simu yake ilikuwa ikiita, aliyepiga alikuwa Rais.

"umeshaiona hiyo habari?" Rais aliuliza baada ya ray Charles kupokea simu,.
"ndio mkuu" Ray Charles alijibu,

"huyo mtu mtafute siku mbili kabla hajapost habari kamili, na umuue" Rais aliongea kwa mamlaka,

"sawa mkuu, huyu atapatikana leo hii hii" Ray charles alijibu,

"unamjua?! " Rais aliuliza,

"ndio, ni rafiki yake na yule Askari amayefuatilia kesi ya yule dada niliyemuua baharini" Ray Charles alijibu,

"basi uwa, uwa wote" Rais aliongea na kukata simu.

***********

Tom aliendelea kukata mitaa usiku ule. Akaona kama ataendelea kufuata barabara atachelewa vile, alichoamua ni kuingia njia za vichororoni. Alipita kichochoro cha kwanza, kikafuata cha pili, ila kichochoro cha tatu alipofika, alihisi kuna mtu alikuwa akija huku akikimbia, Tom akataka kujikaza asimame, ila akakumbuka mkaa huo una vibaka sana, Tom akaamua akimbie tu. Tom alipoanza kukimbia, yule mtu akaongeza kasi, Tom akakunja kona, yule mtu nae akamfuata huko huko, Tom alikimbia dakika tano tu, akachoka, akaamua asimame huku akihema kwa nguvu, vichomi vilimshika,

"sina hela, nina simu tu, hii hapa" Tom aliongea huku akihema, alishaamini huyo anayemkimbiza ni kibaka. Yule mtu akaichukua ile simu, kisha akaiwasha huku sura yake ikiwa karibu na kile kioo, hapo Tom ndipo aliiona vizuri sura ya yule mtu, alikuwa ni Ray Charles, Tom akashtuka, akaanza kukimbia tena, ila alishangaa akipigwa risasi ya bega na kutupwa chini, Tom akaanguka chali huku akihisi maumivu makali sana begani,

"wewe ndiye unayejifanya unanijua sana?" Ray Charles aliuliza huku akiwa ameelekeza mdomo wa bastola katika kichwa cha Tom,

"nisamehe, mimi nilitumwa tu" Tom aliongea huku akilia, na pembeni ya kichwa chake kulikuwa na mfuko chipsi uliopasuka baada ya kuutupa chini,

"msamaha utasaidia nini kwa jambo ambalo limeshasambaa nchi nzima?" Ray Charles aliuliza huku akiikoki bastola yake, Tom mkojo ukamtoka, Ray Charles akaruhusu risasi usawa wa kichwa cha Tom, Tom akakumbwa na giza nene kichwani, hakuona kitu tena, hisia zake hazikuwa tena duniani, mwili wake ulilegea na hakutambua tena kitu chochote kinachoendelea duniani......

**********ITAENDELEA**********

the Legend☆
 
acha wivu jina tu hilo
Sio wivu...

huyu jamaa kazuka tu kiaina...lakini ni kama sio mgeni humu...

Na hii je maana yake ni nini... niambie na mie nikajaribu kuitumia ...

Asituletee za kichaga...
hapa sambusa kuita baga! Allah !

Wenzie tunakula kwa macho hapa kwani wajinga??


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Sio wivu...

huyu jamaa kazuka tu kiaina...lakini ni kama sio mgeni humu...

Na hii je maana yake ni nini... niambie na mie nikajaribu kuitumia ...

Asituletee za kichaga...
hapa sambusa kuita baga! Allah !

Wenzie tunakula kwa macho hapa kwani wajinga??


Sent using Jamii Forums mobile app
Hahahahahaa, sitii neno hapa

the Legend☆
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom