RIWAYA : MKONO WA CHUMA.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA KUMI NA SABA.
___________
ENDELEA...
_____________
Wakati wakiendelea kutazama namna mamba wanavyogawana ridhiki yao, huku yule bwana mwingine akiwa bize na camera yake kuchukua matukio, ghafla aliiondoa camera machoni na kutupa macho pembezoni mwa mto, akapata mshangao,
"Dokta Smith, yule sio mtu kweli?" Yule bwana mswahili alimuuliza yule mzungu huku akionesha kwa kidole upande ule ambapo aliuona mwili wa mtu. Yule mzungu aitwae Dokta Smith, akatupa macho upande ule, akaweza kuuona mwili wa mwanamke ukiwa ufukweni katika mto, Dokta Smith ikabidi asogee mpaka lile eneo, maana sio rahisi kuwe na mtu wa kawaida eneo lile, tena mwanamke kuwepo katikati ya ule msitu wa kutisha.
Dokta Smith alipomsogelea, alimkuta yule binti akiwa amelalia tumbo, pua na mdomo vilikuwa chini, kwa hiyo hakuwa na uwezo wa kupumua, Dokta Smith akamgeuza kwa haraka, akaona ana tundu la risasi kichwani, akashtuka, ila haikumzuia kupeleka mkono wake katika kifua cha binti ili aangalie mapigo ya moyo ya yule dada, hakubahatika kusikia kitu, ikambidi aichane fulana aliyoivaa yule mdada na kumfanya kubaki maziwa yakiwa nje, aligundua kuwa kifuani kwa yule binti Kuna tundu jingine la risasi,
"huyu ni jangili nini amepigwa na Askari wa msituni?" Dokta Smith alijiuliza huku akipapasa tundu la risasi lililopo kifuani kwa yule dada,
"we mzungu unataka kufanya nini hapo? Mbona unampapasa maziwa huyo maiti?" Yule mswahili aliuliza huku akiwa mbali na eneo alilokuwa Dokta Smith,
"sogea ili uone ninachokifanya, huyu dada amepigwa risasi" Dokta Smith aliongea huku akipekeka sikio lake katika kifua cha yule dada, tena upande ambapo moyo unasadikiwa unakaa. Baada ya kupeleka sikio na kulikandamiza kwa nguvu kifuani kwa yule dada, aliweza kusikia mapigo ya moyo ya yule dada yakipiga kwa mbali, Dokta Smith akafungua begi lake na kutoa dawa ya maji na kumnywesha yule binti, kisha akambeba na kumuweka begani,
"beba yale mabegi, yatakuwa ni mabegi yake tu" Dokta Smith alimwambia mwenzake ambaye muda wote alikuwa na camera akichukua kila tukio na kisha alitumia muda mdogo kuandika katika karatasi yake.
"mhmmmm, huyu mzungu nae kwa kujipa majukumu, sasa ameokota mtu anamatundu ya risasi, yeye anabeba tu, hata kama Dokta sio kwa dizaini hii" Mswahili aliongea huku akielekea ule upande ambapo mabegi yalikuwepo, alipoyafikia aliinama na kuyabeba, kisha akafuata ile ile njia aliyoelekea Dokta Smith.
Alitembea kwa mwendo wa dakika kumi mpaka alipofika katika sehemu moja ambapo kulikuwa na uzio wa wavu ulioshikiliwa na vyuma vilivyochimbiwa chini, ule uzio wa wavu ulikuwa umezunguka hema moja kubwa lililokuwa katikati ya uzio ule.
Yule bwana Mswahili alipofika pale alifungua komeo na kisha akaingia ndani ya uzio, alafu akafunga mlango wa uzio kwa kutumia kufuri kabisa, kisha akaelekea katika hema na kumkuta Dokta Smith akiwa amemlaza yule binti ambaye hakuwa na mkono mmoja, na pia Dokta Smith alikuwa akitwanga mizizi ya miti, ambayo ile mizizi ilitoa maji ambayo aliyajaza katika kikombe na kumnywesha yule dada.
"huyo mzima kweli?" Mswahili aliuliza huku akimtupia jicho yule dada ambaye alikuwa hajitambui,
"anapumua kwa mbali, nadhani alizamishwa na maji, maana nilimkamua tumbo na ametapika maji mengi tu, sasa hapa nampa dawa ya kumuongezea nguvu, ili baadae nimuondoe hizo risasi" Dokta Smith aliongea huku akijaribu kumvua suruali yule dada,
"wewe bwana wewe, usimvue" Mswahili aliongea huku akimtazama yule dada kwa uchu,
"mwili wake unahitaji hewa ya kutosha kwa ajili ya kurejesha fahamu yake. Kama hutoweza kuvumilia nenda kakae nje tu" Dokta Smith aliongea huku akiwa ameshaitoa mwilini ile suruali ya dada, kisha akamtoa na nguo ya ndani, na kumuacha hapo, akatoka nje kuendelea na shughuli zake,
"na wewe toka uko ndani, huyo ni nusu mtu nusu mfu, usije ukaendekeza tamaa zako ukamuua bure binti wa watu" Dokta Smith alimwambia yule Mswahili,
"nenda uko, mimi sio mtu wa hivyo" Mswahili aliongea huku akitoka ndani ya hema.
**************
Asubuhi hii ilimkuta Sajenti Minja akiwa njiani akielekea kituo cha polisi, alipanga kuonana na mkuu wake, alitaka kumpa taarifa juu ya upelelezi wake ulipofikia.
Sajenti Minja alifika kituoni na kuelekea moja kwa moja mpaka katika ofisi ya mkuu wa polisi, akagonga mlango na kukaribishwa, akaingia na kutoa heshima kwa ukakamavu,
"kaa" Mkuu wa polisi aliongea kisha Sajenti Minja akakaa katika kiti,
"jana baada ya yule mwanamke mtuhumiwa kukamatwa, nasikia gari ya polisi ilipata ajali na kisha yule mwanamke akatoroka. Je ulifika eneo la tukio?" Mkuu wa polisi alimuuliza Sajenti Minja, Sajenti Minja akakaa kimya kidogo kisha akamuangalia mkuu wa polisi, akakuta yupo bize na makabrasha yake yaliyopo juu ya meza,
"nilifika muda ule ule wakati ajali imetokea, ila nilichogundua ni kuwa ile ajali sio ya bahati mbaya, ni ajali iliyosababishwa na mtu" Sajenti Minja aliongea na kumfanya mkuu wa polisi amtupie jicho,
"kivipi?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"mimi nilifika wakati ajali ikitokea, ila baada ya ajali niliweza kumuona mwanaume mmoja akikimbia na yule dada mtuhumiwa, walikimbia mpaka eneo la ufukweni upande wa juu, mimi nilikuwa nawafuatilia tu. Walipofika pale ufukweni, walisimama na kuanza kuongea, sikuweza kuwasikia kwa kuwa nilikuwa mbali kidogo. Ila ghafla nilishuhudia yule kijana akichomoa bastola na kumuelekezea yule dada mtuhumiwa, nikiwa katika hali ya taharuki, niliweza kumshuhudia yule mwanaume akimpiga risasi ya kifua yule binti, papo hapo tena akampiga risasi ya kichwa, yule binti akaangukia baharini, na mimi nikajitokeza na kumtaka yule kijana ajisalimishe, lakini hakujisalimisha, akaanza kunishambulia, nikajificha nyuma ya mwamba, nilipoona milio ya risasi imepoa, nikachungulia, ila sijakuta mtu, nikatoka mbio mpaka katika eneo alipoangukia yule dada mtuhumiwa, nikamuona akielea ndani zaidi ya maji, ikabidi niingie baharini ili nimuokoe, ila sikufanikiwa, yule dada alizamishwa na maji, baada ya muda liliibuka hili begi tu" Sajenti Minja aliongea huku akilinyanyua lile begi la BQ,
"umelikagua hilo begi?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Kuna nguo tu, sijabahatika kupata kitu kingine" Sajenti Minja alijibu,
"kwa hiyo huyo dada alikutoroka kwa mbinu hiyo?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"hapana hakunitoroka, ila atakuwa amekufa na amesombwa na maji, ni ngumu sana mtu kupigwa risasi ya kichwa na kupona" Sajenti Minja alijitetea,
"utasemaje amekufa wakati mwili bado haujapatikana? Kupigwa risasi ya kichwa sio sababu ya kufa. Unamfahamu 50 cent yule msanii wa marekani, alishawahi kupigwa risasi tisa, na nyingine zilimpiga kichwani, ila mpaka leo anaishi" Mkuu wa polisi aliongea,
"ni bahati sana kwa mtu kupigwa risasi na kuishi, ila siwezi kukataa husemi wako, kuwa nisiseme amekufa mpaka mwili wake upatikane" Sajenti Minja aliongea,
"sio husemi wangu, hiyo ndiyo kanuni ya kipelelezi" Mkuu wa polisi aliongea,
"sawa mkuu" Sajenti Minja aliongea,
"pia jana nimesikia umevamiwa usiku, na ulirushiana risasi na mtu" Mkuu wa polisi aliongea,
"ni kweli, na aliyenivamia ndio yule yule kijana aliyempiga risasi yule binti mtuhumiwa" Sajenti Minja alijibu na kumfanya mkuu wa polisi avue miwani na kumtazama,
"kwanini alikuvamia, hakukupa sababu?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"hakunipa, nadhani alikuja kuniua tu, hakuja kujadiliana" Sajenti Minja alijibu,
"pia nimesikia ulitumia risasi nyingi sana kupambana na huyo mtu, imekuwaje risasi zote zimemkosa?" Mkuu wa polisi aliendelea kuuliza,
"sio zote zimemkosa, asilimia themanini ya risasi nilizomrushia zilimpiga" Sajenti Minja alijibu na kumfanya mkuu wake ashangae,
"kama umempiga mbona hakupata jeraha na wala hakufa" Mkuu wa polisi aliuliza,
"Yule sio mtu wa kawaida" Sajenti Minja alijibu,
"ni mchawi? kumbuka sisi hatuamini katika hizo imani" Mkuu wa polisi aliuliza huku akiendelea kupekua makabrasha yake,
"sijasema ni mchawi, ila katika risasi zote nilizompiga, hakuna hata moja iliyopenya katika mwili wake" Sajenti Minja aliongea,
"kwa hiyo unataka kusemaje sasa?" Mkuu wa polisi alihoji,
"kwa sasa sina cha kasema, ila nitapofanikiwa kukutana nae tena, nitakuwa nimepata jibu" Sajenti Minja aliongea,
"ila sura ya huyo mwanaume si umeikariri?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"ndio, ingawa sio kwa asilimia mia" Sajenti Minja alijibu,
"ukitoka hapa pitia ofisi namba nane, utakutana na mchoraji, mpe maelezo ili amchore huyo mtu" Mkuu wa polisi aliongea,
"sawa mkuu" Sajenti Minja alijibu,
"vipi kuhusu kifo cha waziri wa katiba na sheria, umefikia wapi?" Mkuu wa polisi aliuliza,
"na hilo pia nilitaka kulizungumzia, nilichogundua pia, kuwa kifo cha waziri wa katiba na sheria sio kazi ya yule dada mtuhumiwa, itakuwa ni kazi ya yule mwanaume aliyenivamia, kwa kuwa katika mwili wa waziri kulikuwa na matundu ya risasi, tena risasi zenyewe ni kama zile zilizofyatuliwa na yule jamaa aliyenivamia jana" Sajenti Minja aliongea,
"hiyo sio sababu ya kumuondoa huyo mwanamke mtuhumiwa katika katika kifo cha waziri, au labda kama ipo sababu nyungine" Mkuu wa polisi aliongea,
"ni hiyo tu, kwa maana nilifuatilia kuanzia kifo cha mkuu wa wilaya, kifo cha msaidizi wa mkuu wa wilaya, kifo cha mkuu wa mkoa na kifo cha naibu waziri, hakuna hata mmoja aliyepigwa risasi, wote wameuawa eidha kwa kukabwa au kushambuliwa kwa mkono tu" Sajenti Minja aliongea na kumfanya mkuu wake amuangalie huku akionesha hilo neno limemuingia,
"nenda katoe maelezo ya mchoro, kesho mapema ulete huo mchoro" Mkuu polisi aliongea na kumfanya Sajenti Minja ainuke na kutoka nje,
"huyu mzee bwana, mimi naongea yeye anapinga. Ananifundisha kazi??? sasa akaifanye yeye" Sajenti Minja aliongea huku akielekea katika ofisi namba nane, ofisi inayohusiana na mambo ya michoro.
************
Kule msituni, baada ya nusu saa ya kumuacha BQ dawa ifanye kazi mwilini, Dokta Smith alirudi ndani ya hema na kukagua yale matundu ya risasi, kisha akaenda mpaka katika sanduku lake kubwa lililotengenezwa kwa bati, akafungua na kutoa vifaa vipya kabisa via upasuaji, vilikuwa vifaa vya kisasa. Dokta Smith akavaa mipira mkononi, na kuusogelea mwili wa BQ, kisha akapeleka kisu katika kifua upande wa kushoto kabisa, na kupasua kidogo katika eneo ambalo risasi iliingia, kisha akaingiza kifaa kidogo chenye umbo kama la bikali, ila chenyewe hakikuwa na ncha kali.
Baada ya kuingiza kifaa kile, akakivuta juu, kikatoka na risasi, Dokta Smith akaiweka ile risasi katika mfuko mdogo wa nailoni, kisha akamshona BQ katika jeraha.
"umeshaanaza kumtoa risasi kumbe?" Mswahili aliongea huku akiingia ndani,
"ndio, nimeanza na hii ya kifuani kwa kuwa haikuwa eneo baya sana, ingawa ilichimba sana ila ilipita mbali na moyo" Dokta Smith aliongea huku akimalizia kushona jeraha la kifuani kwa BQ,
"sasa hiyo iliyoingia kichwani si ni hatari zaidi?" Mswahili alihoji huku akimtazana BQ ambaye alikuwa amelala bila fahamu,
"hii hatari kweli, ila haijaingia sana, huenda imepasua kidogo fuvu la kichwa, angekuwa mjini angefanyiwa x-ray ili kujua kama imeingia sana" Dokta Smith aliongea,
"sasa si tupeleke tu mjini?! " Mswahili alitoa pendekezo,
"hii risasi kuendelea kukaa kichwani ni hatari zaidi, kwa maana kuna risasi nyingine zina sumu, inavyozidi kukaa mwilini ndivyo inavyozidi kuhatarisha maisha" Dokta Smith aliongea,
"alafu katika mabegi yake hatukukagua" Mswahili aliongea huku akivuta begi moja na kulifungua, akakuta vipande vya vyuma vilivyotengenezwa katika umbo la mkono,
"huo ni mkono wake wa kutumia, si unaona hapa hana mkono mmoja?" Dokta Smith aliongea huku akimpora yule Mswahili ule mkono na kuanza kuuangalia yeye,
"sasa ndio unipore, we mzungu gani una mambo ya kiswahili" Mswahili aliongea kwa jazba huku akilichukua lile begi jingine na kulifungua, akatoa laptop ndogo na kuikagua kwa kuigeuza geuza, kisha akaweka pembeni na kuingiza tena mkono ndani ya begi, akatoa mfuko wa Rambo uliokuwa na karatasi ndani yake, akazitoa zile karatasi,
"hii mikataba" Mswahili aliongea huku akianza kuisoma,
"mikataba inahusu nini?" Dokta Smith aliuliza,
"sasa si ungoje nimalize kuisoma" Mswahili aliongea kisha akaendelea kuisoma, akashtuka baada ya kusoma jina la huyo mwanamke, kisha akasimama na kwenda kumuangalia vizuri,
"vipi?" Dokta Smith aliuliza baada ya kumuona mwenzake akimtazama kwa mashaka binti yule,
"ah hakuna kitu" Mswahili alijibu huku akiendelea kutazama, hata furaha aliyokuwa nayo hapo hawali ilipotea,
"Kuna nini kwani?" Dokta Smith aliuliza huku akiinyakua ile mikataba na kuanza kuisoma yeye, aliisoma kwa muda mchache tu,
"kumbe huyu mwanamke ana utajiri mkubwa? ndio maana umehamaki" Dokta Smith aliongea huku akiendekea kuisoma ile mikataba,
"tatizo sio utajiri, huyo mwanamke namjua vizuri, tena vizuri sana" Mswahili aliongea huku akielekea nje, hakuwa tena na amani kuanzia muda huo.
Dokta Smith akaamua amuache tu, akaona atamuuliza baadae kuwa amemjuaje huyo mwanamke.
Dokta Smith akaendelea na kazi, muda huu alikuwa anamtoa ile risasi ya kwenye kichwa, hii ilimchukua muda wa saa na nusu mpaka alipofanikiwa kumtoa ile risasi, kisha akamfunga bandeji.
Baada ya hapo Dokta Smith aliingia msituni kuendelea kutafuta mizizi na miti kwa ajili ya utafiti anaoufanya wa kutengeneza dawa.
*************
Mswahili tangu asome ile mikataba na kulijua jina la yule dada, alijikuta akiwaza sana, kwani anamfahamu vizuri yule dada, na isitoshe anajua kuwa yule dada alishakufa muda tu kutokana na ajali ya ndege, na mbaya zaidi anamfahamu fika ukatili wa huyo dada.
"huyu sio wa kuishi, ni wa kufa tu" Mswahili aliongea huku akiingia ndani ya hema, akapekua sanduku la Dokta Smith na kuchukua bomba la sindano, kisha akachukua kichupa kidogo cha dawa, kilichoandikwa pembeni "POISON" akaingiza sindano katika kile kichupa na kuivuta ile sumu, kisha akamsogelea BQ aliyekuwa amelala hajitambui, akamchoma ile sindano mkononi katika mshipa, na kuiminya ile dawa, kisha akalitupa lile bomba la sindano na kuirudisha ile sumu katika sanduku la Dokta Smith.
Baada ya hapo Mswahili akachukua camera yake na kuelekea msituni, alishatimiza adhma yake, sasa angalau alipata amani, maana tayari alishaua, aliamini amemuua mtu mbaya kabisa, amemuua kiumbe ambaye hastahili kuishi.
Ni kweli, BQ hakustahili kuishi tena.
**********ITAENDELEA************
the Legend☆