RIWAYA : MKONO WA CHUMA.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA TISA.
_____________
ENDELEA...
_____________
Tom alifungua macho na kuhisi baridi kali likishambulia mwili wake, na pia alihisi maumivu ya kichwa, akavuta kumbukumbu na kukumbuka ni tukio gani alikutana nalo, sasa wasiwasi ukamuingia, akahisi kabisa atakuwa chini ya uangalizi wa polisi, akaanza kujilaumu kwa kumfuatilia yule Dada kichaa, akawaza endapo yeye ndio atashtakiwa kwa vifo vya Askari waliouawa kwenye nyumba ya waziri wa katiba na sheria, atajibu nini Wakati ni yeye ndiye aliyekutwa yupo ndani ya geti la Ile nyumba? Tom akaanza kujuta huku machozi yakimtoka, mara akasikia sauti ya gari likipita, akashtuka na kuinuka kwa haraka, akashangaa, kumbe alikuwa pembezoni mwa barabara, akapepesa macho huku hasiamini kinachomtokea,
"au polisi walinipiga risasi wakajua nimekufa? Kisha wakanitupa hapa? " Tom alijiuliza huku akijiangalia mwilini kama atajikuta na jeraha la risasi, lakini alijikuta yupo sawa tu, akajisachi mifukoni, maana alikumbuka kabla ya tukio alikuwa na pesa kidogo mfukoni, akaingiza mikono mfukoni na kuzikuta, akakumbuka pia alikuwa na simu, akaitoa mfukoni na kuiangalia, akakuta amepigiwa zaidi ya mara 50, mpigaji alikuwa ni mpenzi wake, akatabasamu, akataka ampigie ila akaghairi, akaangalia sehemu ya ujumbe mfupi wa maneno, akakuta sms zaidi ya kumi, akafungua na kukuta zote zimetoka kwa mpenzi wake na alikuwa akimuuliza yupo wapi? Akairudisha simu mfukoni na kusogea mpaka barabarani, ilikuwa yapata saa kumi na moja alfajili.
Akatembea kwa dakika kadhaa, bahati nzuri ilitokea bajaj, akaisimamisha na kuingia, akamuelekeza dereva ni wapi anaenda.
Ilichukua takriban dakika kumi na tano bodaboda kufika nyumbani kwa mpenzi wa Tom, Tom akatelemka na kumlipa dereva bodaboda, bodaboda ikaondoka.
Tom akasimama kwa muda huku akifikiria atamwambia nini mpenzi wake? Wakati akitafakari, mlango ulifunguliwa, akatoka mpenzi wake,
"haya nieleze ulikuwa wapi!?"Mpenzi wake Tom aliuliza huku machozi yakiwa jirani kabisa na macho,
"ebu kwanza tuingie ndani, nitakueleza" Tom aliongea kwa kumbembeleza mpenzi wake,
"Tom tokea umekuja safari hii sikuelewi kabisa, Kama una mwanamke mwingine si uniambie?" Mpenzi wake Tom aliuliza, na safari hii alikuwa analia kabisa,
"wewe unatanguliza wivu tu, hufikirii labda nilikuwa na tatizo?" Tom aliuliza,
"tatizo gani? Ungekuwa na tatizo si ungepiga simu? Mbona hukupokea simu?" Mpenzi wake alimuuliza kwa ukali,
"bwana ngoja nilale, kukisha pambazuka vizuri tutaongea" Tom alijibu huku akiingia ndani, mpenzi wake akamfuata kwa nyuma,
"umekalia umalaya tu, kama umenichoka bora uniambie tu, maana utaniletea maradhi" Mpenzi wake alizidi kulalama Ila Tom hakutaka kuongea tena, akavua shati, akajihisi ana maumivu mgongoni, akapeleka mkono eneo alilohisi maumivu, akashtuka alipouangalia mkono wake, ulikuwa na damu za kutosha.
"ebu niangalie mgongoni" Tom aliongea huku akimpa mgongo mpenzi wake aliyekuwa amekaa kitandani.
"eh!!!!!!" mpenzi wake alishtuka baada ya kumuangalia, lilikuwa jeraha kubwa kiasi, ni kama mkwaruzo chuma au kisu,
"nini?" Tom aliuliza kwa uoga,
"kidonda kikubwa, umefanyaje?" Mpenzi wake aliuliza kwa uoga, hapo tena wivu ulipungua,
"chukua maji ya moto nisafishe, nitakusimulia pakikucha" Tom aliongea huku pia akishukuru kuwa na kidonda hicho, alipanga namna ya kumdanganya mpenzi wake, na Wakati huo mpenzi wake alichukua sufuria ndogo na kuinjika kwenye jiko la gesi, Tom akatabasamu.
*****************
Mkuu wa polisi alikuwa amekaa kwenye kiti chake ofisini akitafakari, na kilichomfanya atafakari ni asubuhi Ile kuamshwa na habari za kuuawa kwa baadhi ya Askari waliokuwa wakilinda nyumba ya waziri, lakini pia taarifa zilikuwa zikikinzana, wakati waziri wa nishati na madini akidai aliyevamia na kuua polisi ni mwanamke, Wakati polisi walioenda baada ya tukio wanadai aliyeua polisi ni mwanaume, Ila pia polisi wanadai walimdhibiti yule mwanaume waliyemkuta pale, cha ajabu akaja kuokolewa na mwanamke mwenye mikono miwili, tofauti na yule wa kwanza mwenye mkono mmoja aliyeongea na waziri.
"kwa maana hiyo wapo watatu? Mwanaume, mwanamke mwenye mkono mmoja na huyo mwanamke mwingine mzima?" Mkuu wa polisi alijiuliza mwenyewe huku mawazo yakizidi.
"hapa ni lazima apatikane mtu mmoja makini wa kufuatilia hili kasheshe" Mkuu wa polisi aliongea, kisha Akachukua miwani yake na kuipachika machoni, akatoa simu yake kwenye droo na kwenda upende wa majina na kutafuta jina analolitaka, akapiga,
"upo wapi?" Mkuu wa polisi aliuliza mara baada ya mtu wa upande wa pili kupokea simu,
"nipo ofisini mkuu" Mtu wa upande wa pili alijibu,
"njoo ofisini kwangu" Mkuu wa polisi aliongea na kukata simu, kisha akavua miwani yake na kuwasha computer yake.
Baada ya dakika mbili mlango wa ofisini kwake uligongwa, akaingia kijana mrefu kidogo na miwani mieusi machoni, kijana akapiga salute,
"kaa" Mkuu wa polisi aliongea kisha kijana akaa, Mkuu wa polisi akaendelea kubonyeza vitufe vya computer yake, kisha akashusha pumzi ndefu,
"si umesikia hii hali inayoendelea nchini? Polisi wanauawa hovyo, viongozi wa nchi wanakufa pia" Mkuu wa polisi aliongea na kutulia kidogo,
"sasa bwana, kuanzia sasa hiyo hii kazi unatakiwa kuifuatilia wewe, sijaona mtu mwingine wa kuifanya zaidi yako" Mkuu wa polisi aliongea na kumtupia jicho yule kijana aliyekuwa ametulia akisikiliza kwa umakini.
"kumbuka, unatakiwa uifuatilie kwa uangalifu na usiri mkubwa sana, nakuamini katika hilo" Mkuu wa polisi aliongea,
"sawa Mkuu, nitafanya kama unavyotaka" Kijana alijibu,
"leo hii saa nne asubuhi, mtuhumiwa atakuwa ofisini kwa waziri, Kuna askari kadhaa tumewaweka kwa ajili ya kumkamata huyo Dada, sasa na wewe ni vizuri ungekuwepo eneo hilo ili upate chochote" Mkuu wa polisi aliendelelea kuongea,
"Ila kwa nilivyosikia ni kuwa waziri hataki mtu yoyote wa usalama afike eneo lile" Kijana aliongea,
"ni sawa, Ila hata hao Askari wataokuwepo eneo hilo pia watakuwa wamevaa kiraia, kwa hiyo ni ngumu kugundulika" Mkuu wa polisi aliongea,
"mimi nadhani ni vyema kufuata maelekezo ya mtuhumiwa, endapo mtuhumiwa atagundua Kuna mtego, itakuwa mbaya sana kwa waziri" kijana aliongea kwa upole,
"kijana nenda kama nilivyokuagiza, sikukuita unipangie kazi wala sikukuita tujadiliane, nimekuita kukupa amri" Mkuu wa polisi aliongea,
"sawa mkuu" kijana alijibu kikakamavu kisha akageuka na kuondoka, huku nyuma Mkuu wa polisi alimuangalia huku akitafakari maneno ya yule kijana.
"litalokuwa na liwe" Mkuu wa polisi aliongea na kuipachika miwani yake machoni.
************
Ndani ya ofisi ya waziri wa katiba na sheria, alikuwa waziri peke yake, na Muda wote alikuwa na wasiwasi, alikuwa akisimama kila muda na kwenda dirishani, anachungulia nje kwa muda na kisha anarudi kukaa kwenye kiti chake na kutupia macho kwenye runinga kubwa iliyobandikwa ukutani ambayo ilionganishwa na camera zilizopo mapokezi, kwa maana hiyo kila mtu aliyeingia na kutoka ndani ya jengo, waziri alimuona.
Pia waziri alikuwa makini kuangalia watu wa usalama kama wapo ofisini kwake, hakutaka kabisa mtu wa usalama kuwepo eneo lile, alichotaka ni kuongea na yule Dada kisha aone kama ni kweli ana haki au analazimisha tu.
Waziri aliendelelea kusubiri huku Muda ukiendelea kukatika, ilianza kupotea dakika, ikafuata saa, kisha masaa. Waziri akajiuliza kwanini huyu binti hajaja, maana alisema atafika saa nne.
Waziri hakukata tamaa, aliendelelea kusubiri, mwisho saa kumi jioni ikamkuta ofisini, na huo ndio ulikuwa Muda wake wa kutoka kazini.
Akachukua koti Lake la suti alilolitundika nyuma ya kiti, kisha akalivaa, akatoka na kuhakikisha mlango wake ameufunga vizuri, alatelemka mpaka ghorofa ya chini, akakukuta gari yake ikiwa na dereva, alikuwa akisubiriwa yeye, akaingia katika gari,
"nipeleke nyumbani" waziri wa katiba na sheria aliongea na kisha dereva akaiondoa gari, nje ya geti walimpita kijana mmoja aliyekuwa amevaa miwani mieusi, huyu ndiye yule kijana aliyetumwa amtafute mtuhumiwa wa mauaji yanayotokea hovyo. Kijana baada ya kupitwa na gari ya waziri, aliangalia saa yake, kisha akatoka kwa mwendo wa kawaida, alielekea uelekeo tofauti kabisa na lilipoelekea gari la waziri.
*************
Mishale ya saba usiku, waziri bado alikuwa sebuleni akimfikiria yule Dada, na siku hiyo hakutaka kuwe na ulinzi nyumbani kwake, aliwatimua walinzi wote, na Muda huo alikuwa sebuleni, alikaa peke yake, familia ilikuwa ndani, wamelala.
Ilipofika saa nane kasoro, waziri alianza kusinzia, Ila akahisi mlango ukisukumwa, akanyanyua kichwa haraka, macho yake yakagongana na macho ya yule Dada kichaa,
"karibu, nilijua utakuja tu" Waziri aliongea huku akijiweka vizuri juu ya kiti,
"ulijua ntakuja, ulijuaje?" Dada kichaa aliuliza huku akikaa chini,
"kwa sababu asubuhi hujatokea" waziri alijibu kwa utulivu,
"kweli, ilishindikana mimi kuja uko kwa sababu ofisi yako yote ilizungukwa na watu wa usalama, kwa hiyo sikutaka kuja kwa maana ningeua tena, na mimi sipendi kuua" Dada kichaa alijibu,
"usalama!? Lakini mimi nilizuia mtu yoyote wa usalama asisogee eneo la ofisi yangu" Waziri aliongea,
"ni kweli, Ila mipango ya kuwaweka watu wa usalama, ilifanywa na Mkuu wa polisi" Dada kichaa aliongea,
"kwanini wanaingilia mambo yangu? Nilitaka nikutane mimi na wewe na wala sio wao" waziri aliongea kwa hasira,
"usijali, kama haki ipo, ipo tu" Dada kichaa aliongea,
"alafu mpo mapacha?" Waziri aliuliza,
"kwanini mheshimiwa?" Dada kichaa aliuliza,
"maana aliyekuja jana alikuwa ana mkono mmoja, Ila wewe umekuja ukiwa na mikono miwili" Waziri aliongea, ila Dada kichaa hakutaka kujibu, alitabasamu tu,
"kilichonileta hapa ni kwamba, kampe onyo Mkuu wa polisi, mwambie ahache kunifuatilia, kama ataendelea kunifuatilia, basi vijana wake wataendelea kufa kwa sababu yake, yeye asubiri tu mpaka muda wake wa kuonana na mimi utapofika, Ila akiharakisha kuonana na mimi ni sawa na kuharakisha kifo chake" Dada kichaa aliongea na kumfanya waziri akae kimya kwa muda,
"sawa, je umekuja na mikataba ili niione?" Waziri aliuliza,
"hapana, hapa sio sehemu sahihi ya kuoneshana mikataba, nitakuja nayo ofisini kwako siku yoyote" Dada kichaa alijibu,
"Hilo nalo ni jambo zuri, Ila utaingiaje ofisini kwangu ingalikuwa kuna polisi kila kona?" Waziri aliuliza,
"hakuna wa kunizuia, mimi sio mtu kama unavyodhani wewe, sipo kawaida kabisa na watu" Dada kichaa alijibu,
"jina lako unaitwa nani?" Waziri aliuliza na kumfanya yule Dada kichaa atabasamu, kisha akainama kidogo na kurudisha nyuma kichwa kwa nguvu na kufanya nywele zake ndefu zirudi nyuma, sura yake ikaonekana vizuri,
"niite BQ, jina halisi utaliona kwenye mikataba" Dada kichaa alijibu na kutulia kidogo kama mtu aliyesikia kitu, kisha akasimama,
"vipi?!" waziri akauliza,
"Kuna mtu nje" Dada kichaa aliongea,
"hakuna mtu, mbona Askari wote niliwaondoa?" Waziri aliuliza,
"mzee acha mimi niende, funga milango yako" BQ aliongea huku akielekea nje na waziri alimfuata kwa nyuma, walitoka na kuangaza, hawakuona mtu.
"mzee funga geti, mimi naondoka " BQ aliongea huku akiondoka, waziri hakutaka kuongea tena, alifunga geti na kuingia ndani.
Dada kichaa alipiga hatua chache, akahisi Kuna mtu nyuma, BQ akasimama na kugeuka, akakukuta Kuna kijana mmoja akiwa amesimama na machoni alikuwa na miwani mieusi, ni yule kijana aliyetumwa na Mkuu wa polisi.
BQ akageuka na kuendelea kutembea huku akiamini huyo kijana atakuwa anamfuatilia yeye.
"simama wewe" kijana aliongea kwa amri na kumfanya BQ asimame na kugeuka,
"Kuna tatizo?" BQ aliuliza,
"upo chini ya ulinzi" Kijana aliongea huku akimfuata BQ, hilo lilikuwa kosa kubwa, kwani wakiwa wameachana hatua mbili tu, BQ alizungusha kwa nguvu nywele zake na kupiga uso wa yule kijana, kijana akajishika kwa maumivu, pasipo kutegemea BQ aliachia ngumi kali ya mkono wa kushoto, kijana akaiona akaiepa, ile ngumi ikapiga ukuta, ukuta ukapasuka, ukatengeneza ufa, kijana akashtuka, kwa maana haikuwa ngumi ya kawaida.
Kijana akaogopa akarudi nyuma, BQ akatabasamu. Kijana akahisi huenda leo anapambana na mtu hasiye mtu. Kijana akaokota kipande cha jiwe gumu kilichokuwa chini, akamrushia kwa nguvu, BQ kwa mkono ule ule wa kushoto akapiga ngumi kile kipande cha tofali na kusambaratika. Kijana akaona atumie mbinu za ziada kumuingia, akamfuata kwa kasi, lakini iliachiwa ngumi kali tena ya mkono wa kushoto, kijana akaiona, akakwepesha kichwa kidogo, ile ngumi ikapasua kioo cha miwani cha jicho la kulia, kijana akarudi nyuma na kuvua miwani kabisa, naaam, sasa kijana alionekana vyema, jicho lake la kushoto lilikuwa limetoboka, lilionekana vizuri kabisa, alikuwa na chongo.
Naam, baada ya kumjua BQ, sasa nadhan hata anayepambana nae mtakuwa mmeshamjua...
********ITAENDELEA********
the Legend☆