ZIMWI LETU!!

ZIMWI LETU!!

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2014
Posts
3,456
Reaction score
4,736
MUHTASARI

Faraja zote walizozitegemea baada ya ujio wa uongozi mpya, zilipotea. Maisha kupanda, mfumuko wa bei ya vitu, ufisadi, ukosefu wa ajira, rushwa ya kila namna. Watu walimlaani Rais mpya, waliapa kutokuja kumpigia kampeni mwanasiasa yeyote. ajabu alipotatua matatizo aliyoyaweka wapo walikuja kuandamana kupongeza na kusahau viapo vyao. hili ndiyo ZIMWI LETU. Riwaya iliyoangaza mengi sana kuhusu maisha ya waafrika, na namna wanavyojipambania.

ZIMWI.jpg


Riwaya hii inahusu maisha halisi ya Mwafrika na siasa na harakati zake zilizopo kwenye nchi za bara hili.

Kutana na Aidan Kibwana kiongozi wa Tanzania ambaye alitumainiwa kuwapeleka watanzania pazuri. Ila aliposhika nchi mambo yalibadilika, mafuta yalipanda bei ghafla, kodi nayo ilipaa, ajira hakuna, maisha magumu huku mawaziri wake wakifanya vitu kiholela.

Waliyompigia kura na kuvaa nguo kipindi cha kampeni waliingia majuto makuu, wapo ambao waliapa hawatohusika na wanasiasa. Ila baadaye alipokuja kulegeza mambo walimpongeza na kuunga naye. Ndiyo ZIMWI LETU lenyewe hilo.

---

Ndani kuna dereva tukutuku (bajaji) aitwae Zumo, huyo anamlaani sana Aidan Kibwana kabla ya ujio wake maisha yalikuwa safi hadi alifanikiwa kununua kiwanja na kujenga hakumalizia, ila alipoingia mambo ni mabovu sana.

Zumo alijali maisha yake tu na hakutaka kusikia kuhusu siasa ni apate hela tu. Yaani hadi aliposikia wanachuo wanataka kuandamana si akapanga kununua maji ya chupa mengi, akauze kwa bei juu. Wao wakiendelea kuhaha juani, yeye apige hela.

Nyumbani ni baba wa familia anayekumbana na malezi na mahutaji mengine muhimu. Kiasi kwamba akipata hela akifurahi ila akija kukumbuka ana majukumu, tabasamu linapotea.

Anakumbana na suala la petroli kuwa bei juu hadi ananunua ya kinyemela atumie. Bado nishati ya kupikia wanasiasa walivuruga mkaa na kuni usipatikane, wakipigia debe kesi aliishia kuleta samadi itumike kupikia.

Mwisho wa majanga yote kunyooshwa mambo na yule ambaye alisababisha. Alimwona mkewe aliyeapa hatokuja kuhusika na wanasiasa ndiyo mstari wa mbele kuelekea kushangilia. Aliishia kusema ni ZIMWI LETU.

----

Aidan Kibwana alijulikana kama kiongozi aliyefanya mengi ili apate madaraka. Alikuwa na mkono mpana kwenye mambo mbalimbali, hadi wanasiasa wenyewe wa upinzani walimhofu hasa. Siasa zao walifanya mambo ambayo hayawezi kumchukiza.

Aliruhusu mawazidi wake wapige dili, ila wasije kuingilia maslahi yake. Basi mawaziri wawili mmoja wa kike, mwingine wa kiume. Waliyokuwa watu wake wa karibu, waliishia kuandaa mpango wa kuchota pesa za mikopo ya wanafunzi. Jambo ambalo ni kinyume na maslahi yake, alipanga kuwajali wanafunzi aje kuwatumia baadaye.

Walikuja kumwomba radhi, na aliishia kuonesha hana kinyongo nao. Ila walipoondoka kumbe alishaweka hukumu yao, waziri wa kiume alifariki ghafla na wa kike alikumbwa na aibu picba zake kuvuja. Akaja kuomba msaada kwake na akijiuzulu mafasi zake zote.

Aidan alionesha kumwonea huruma kama ahusiki, akaridhia kujiyzulu. Kumbe huo ndiyo mshahara wa usaliti wake aliyempa.

---

Ndani kuna kijana aliyeamua kujitumbukiza kwenye biashara ya uuzaji karanga mjini. Alipoona mambo yamekuwa magumu mtaani. Ajira kakosa na amehitimu shahada kwa ufaulu wa juu. Rushwa imetamalaki kila alipoenda kwenda kuomba ajira.

Akaishia kuuza karanga akitumia ubunifu na ucheshi, akiongea lugha ya kingereza kwenye kujinadi. Mwishowe akawa maarufu mjini, video zake zikasambaa. Akapata matangazo ya udhamini, kapu likawekwa nembo atangaze. Pesa nayo aliipata hadi ndugu wa marehemu baba yake alikuja akijifanya anataka kumpa fursa kumbe aliongozwa na wivu.

----

Kijana mmoja mwenye ushawishi mkubwa kwa wanafunzi wenzake wa chuo, mpaka alifikia kuteuliwa kuwa Rais wa chuo. Aliandaa mgomo baada ya pesa za mikopo kukwama kisa wale mawaziri.

Alipanga waandamane, hata aliposhauriwa na wahadhiri asirishe hakutaka. Alipoelezwa ni agizo la Rais toka ikulu. Aliishia kusema kama hata na yeye ni rais labda aje kuonana na mwenzake wajadili.

Akaja kuchukuliwa kweli akakutanishwa na Rais kwenye nyumba ya siri, jeuri yote ilimuisha alipotoka hapo baada ya kupewa kifinyo, akasitisha mgomo mara. Huku pesa nazo zikiachiwa kwani Aidan Kibwana hakuridhia zichukuliwe.

---

Bosi mmoja wa idara alijulikana sana kupenda mabinti warembo, ilihali nyumbani ana mke. Basi ofisini akaja mmoja anavutia hakutaka kumuacha. Akamuundia kosa na kumtisha akifikishkwa mkubwa wap angefukuzwa.

Binti akaombwa aje mahali baada ya kutoka ofisini. Aliishia kwenda na aliishia kutoa ngono bila kupenda. Bosi akaona amefanikiwa kutembea na binti aliyeumbika.
Kumbe ni mwathirika akaja kuokota VVU, aliyokuja kumwambukiza mkewe. Asijue aliyempa nani miongoni mwa wengi aliyotembea nao. Mke alimlaumu ila alishindwa kuondoka na ameshaambukizwa akaamua abaki naye tu.

-----
Demokrasi hamna!

FB_IMG_1783889924902.jpg

FB_IMG_1783889930577.jpg


----
UNAFIKI WA NDUGU!

Mmojawapo kati ya waliyoshuhudia tukio lile ni Shaibu, akiwa kwenye harakati zake za kusambaza karanga. Ndiyo aliingia mtaa ule akajionea wazi kilichotokea, kuanzia kugombana kwao hadi kila mmoja kumpiga mwenzake. Mwishowe akaja askari ambaye alipendelea upande mmoja. Hakujali kuchunguza tukio lile. Wala kukagua leseni zao wote wawili, alifikia kuhukumu kutaka kuandikia faini.

Alisikitishwa sana na tukio lile ila hakuwa na la kufanya. Aliishi kuondoka zake aendelee kutafuta shilingi ya siku. Alitambua fika nchini hakukuwepo na usawa, wala kujali haki ya mtu. Ikitokea mmoja akawa na pesa basi ilimaanisha ndiyo mwenye haki. Aonee au aonewe haikuangaliwa, labda suala lije kushika vichwa vingi ndiyo sheria kama yenyewe ingeangaliwa hapo.

Aliamua kuendelea uuzaji karanga kama kawaida. Akitumia ubunifu wake aliyouzoea wa kumletea umaarufu. Akizungumza hadi mitaa ya jiji pasipo kusumbuliwa na Mgambo. Kisa alijulikana wazi ni mwenye udhamini wa wafanyabiashara kadhaa, ambao wasingekaa kimya kumwona akionewa. Ndiyo maana walimwacha aendelee kuuza kwa amani. Waliishia kumpiga picha mara kwa mara, hakuwajali sababu alishachagua kujifanya haoni kitu.

Mchana wa kuelekea saa tisa alishamaliza mzigo wake. Ikambidi kuondoka hapo mjini akapitie sokoni anunue mzigo wa kutayarishwa usiku wa manane kama ilivyo kawaida yake. ilimbidi kukata mitaa hadi alipofika Kariakoo sokoni. Aliponunua kilo kadha za karanga ndiyo alipanda daladala kurudi nyumbani kwao. Kipindi hicho akiwa ameacha utaratibu wake wa kutembea baada ya pesa kuzidi. Toka alipoanza kulamba mipango ya udhamini.

Alasiri ikielekea jioni aliwasili nyumbani kwao. Siku hiyo alikuta kukiwa na ugeni wa mwanaume mtu mzima aliyevaa vyema. Huyo alimkuta akiwa amekaa kwenye stuli akiongea na mama yake aliyeonesha hana raha. Hadi alijikuta akisimama na kumtazama kwa umakini mgeni yule. Kisha alishusha pumzi na kupiga hatua akamsogelea.

Si kwamba hakumfahamu, la hasha kumbukumbu dhidi yake haikumtoka kabisa. Alikumbuka vyema aliyepo hapo, aliyevaa shati jekundu la kuteleza, suruali nyeusi na kiatu cha gharama cha ngozi. Mkononi mwake akiwa ameshika funguo ya gari akichezea. Alimjua vyema ni kaka wa baba yake mzazi, ambaye alimtambua kama mtoto wa nduguye kipindi akiwa hai tu. Ila hakuonesha kumjali baada ya kufariki. Kiasi cha kufikia alimkataza asije nyumbani kwake, huku akimpa ruhusa mlinzi wake amfukuze kama akimwona mlangoni.

Bado hakusahau kama alitoa wazo la kwenda kuifanyia arobaini ya baba yake kijijini. Baada ya kukamilisha shughuli aliwatelekeza pasipo kuwasaidia usafiri, ilihali hawakuwa sawa kifedha. Wakaishia kurudi mjini kwa msaada wa lori la nyanya. Lililokuja kuwacha soko kuu la mabibo, walipofikia. Walipofanikiwa kupata msaada mwingine wa gari la mchanga lililokuja kuwashusha nyumbani kwao. Tangu hapo ndiyo hakuwahi kuwaza kama ni mtoto wa ndugu yake. ila ghafla alikuja kuibuka nyumbani kwao.

Hasira yenyewe ilimjaa ila aliishia kujikaza asijulikane akamsalimia. Baada ya hapo alienda kukaa kwenye msingi wa boma lao upande ambao haujamaliziwa. Alibaki mita chache tu toka walipo wakubwa zake hao, akitaka kusikia kuna kitu gani kipya. Ujio huo aliamini wazi alikuja na jambo, si kwamba alifika hapo kwa lengo la kuwajulia hali pekee.

“Shaibu naona siku hizi umekua mkubwa sana, ila bado hujajua kujitambua. Unajua ni aibu sana ukoo wa Msanje kuja kuuza karanga mjini. Hadi watu wanakuja kukufanyia vituko na kukuona huna akili. Kwanini umechagua kazi hii?”, alianza kulaumu utadhani aliwahi kumsaidia hapo kabla.

“sasa shemeji ulitaka afanye kitu gani? Kazunguka na vyeti ofisi zote hakuwahi hata kuitwa kazini. Bado anafaulu hizo sahili, ila hakuna anayemchukua. Heri aendelee kuuza tu amejiweza sasa na kunisaidia sana. hata nikiumwa sina wasiwasi wa kupatikana chakula nyumbani”, Mama yake alimtetea.

“Shemeji na wewe unaona ni sawa hii? Yaani huyu mwanao anahojiwa kwenye TV anakuja kujisema kama ana digrii ila kachagua kuuza karanga. Muulize kama hajapigiwa simu akatakiwa aende kazini kwa elimu yake. kajibu vipi”, aliendelea kuangusha lawama.

Shaibu aliposikia hivyo aliishia kusema, “ulitaka nifanye nini? Kama hiyo ofisi niliwahi kwenda ila waliishia kunifukuza wakisema sina uzoefu. Hebu niambie huo uzoefu niliupata mpaka wafikie kuniita tena wanipe kazi. Kazi ninayoifanya ninaipenda sana na inanisaidia sitakuja kuiacha hata mara moja”

“Ah! Shemeji unamsikia mwanao mwenyewe”

“Baba mkubwa hivi toka baba yetu afariki ulikuwa na msaada gani? Si uliwahi kunifukuza kwako nilipotaka msaada. Saidi alipoumwa hadi mama alienda kupiga magoti getini kwako umsaidie hukutaka hata kumwona. Ona mama yangu huyu kapambana hadi mikono ina alama za ajabu ili atuletee na kafanikisha hilo. Nimesoma kwa mkopo kuna muda ilibidi nitoe hela kidogo nimpe mama akiwa mgonjwa mimi nikishindia mihogo au mikate shuleni. Hukuwahi kumpa hata shilingi. Leo hii nauza karanga na nimeweza kumudu tunabadili mlo hapa nyumbani ndiyo uje kusema ninajiaibisha”, aliongea kwa uchungu hasa.

Hakuishia hapo aliendelea, “ukiwa kama ndugu wa baba yangu ulinisaidia nini wewe? Kwenye arobaini kwenyewe ulitutelekeza hadi tumerudi na lori ya nyanya hapa. naanza biashara hii nakimbizana na mgambo, naamka usiku wa manane. Natembea kwenda na kurudi kwa miguu, sikuwahi kukuona ukija kunisaidia chochote. Sasa hadi nimedhaminiwa na ninalipwa kutangaza biashara za watu. Ndiyo uje kusema ninajiaibisha”

“Ona sasa mwanao siku hizi amekosa adabu”, alijikuta akimshutumu alipoona ameguswa panapo ukweli.

“bora huyu unayemwona asiye na adabu, kuliko Jamali wako aliyewahi kuja kunitukana matusi aliponiona mtaani. Ila hakuona hana adabu, haya mtoto kaamua kukwambia ukweli ndiyo unaona hana adabu. Nikwambie ukweli tu shemeji, sihesabu kama mwanangu ana mkubwa kama wewe. Eti wale wengine ni ndugu zake. Ndugu pekee aliyembakiza ni Saidi, ambaye amekuwa akimsaidia kuandaa magazeti ya biashara zake. Tunakula na kuishi vizuri hadi nyumba ina umeme sasa, kazi hiyohiyo unayoona inamdhalilisha. Bado ana mpango wa kumaliza nyumba yetu na kanza kununua vifaa. Wiki ijayo anaezeka kulipobakia. Kazi hiyohiyo unayoona wewe ni aibu ndiyo imeleta hayo. Kiukweli hata akidhalilika huko mjini, ilimradi asivuliwe utu nakaa kimya. Sababu imemfanya akaishi vizuri. Ninachoomba utuache na maisha yetu”, Mama yake naye aligongelea msumari.

Mwenyewe alikimbilia kuingiwa na mshangao huku akisema, “Hawa!”

“ndiyo jina langu hilo. Nilitaka nikustahi tu kwa kuona mwanangu angekuwekea heshima. Ila kwakuwa naye ameshakuchoka na mambo yako. Nikwambie tu hatuhitaji msaada wako, wala kukuona ukitushauri kuhusu maisha yetu wakati hujawahi kutupigania. Shamba lenye la kijijini ambalo ni sehemu ya urithi wa mdogo wako, uliishia kutupora baada ya arobaini ukisema ni mali yako. Tena ukome kukanyaga hapa, utuache na maisha yetu kwa amani”, mengine yaliongezewa yaliyomfanya asione umuhimu wa kubaki, aliishia kuondoka zake akiwacha mama na mwana.

Hawa ndiyo aliongezea, “eti kijana hatakiwi kufanya mambo mwenyewe asikilize wakubwa zake. Wakubwa gani ambao walimdhulumu urithi wake, waliyotaka kupora hadi hii nyumbani wakashindwa sababu si mali ya kurithi kama lile shamba. Haya huna”. Maneno hayo alimsindikizia akiwa yupo mlango akitoka. Msemaji alitaka amfuate na kumwongeza mengine, Shaibu ndiyo alikimbilia kumzuia akimwambia, “mama yatosha basi, haina haja ya kuongelea nje. Bora umemwambia ukweli hatarudi tena hapa. nilikushangaa sana siku zote kuonekana mpole kila ukikutana nao”.

“sikutaka uje kunifikiria vibaya mwanangu. Ila kwakuwa nawe unajitambua nimeona waziwazi nisikae kimya tena haitokuwa na maana tena mwanangu. Huyu baba yako mkubwa ana roho mbaya sana yeye na mkewe”

“Mama mimi sina baba mkubwa wala wadogo kama hao wengine. Ndugu pekee niliyokuwa nao ni wewe na Saidi pekee. Jamali si alinitemea mate yule na alikaa kimya. Mkubwa wangu gani huyo sasa... naenda kupumzika Mama, usiku nitakuja kuamka nile nianze kuandaa karanga”, Shaibu alisema huku akiingia zake chumbani kwake.

-----

RUSHWA!

“Unasema huna kosa, hivi unajua sheria kunizidi? Basi ungekuwa Askari na mimi nije kuwa dereva bajaji kama wewe. Usingekuwa unaendesha kidude hichi kilichochoka. Wala kupauka na kuzeeka mapema hivyo kisa hizi kazi. Ungekuwa unavaa nguo kama zangu”

Yalikuwa maneno ya Askari wa usalama barabarani, aliye mfupi, mweusi na mwenye kitambi. Huyo alisimamisha Zumo na kuanza kumtajia makosa ambayo hayapo. Alipobisha kidogo tu alikutana na maneno yasiyopendeza kiasi cha kumfanya ajawe na hasira. Asiwe na chochote cha kumfanya aliishia kuingiza mkono mfukoni.

Alitoa noti ya shilingi elfu tano, aliyoibana na vidole. Akiipanga kutomruhusu aendelee kusema maneno mengine. Machache aliyotoa yalimuumiza na alijua wazi ni uonevu pekee aliyofanyiwa. Hivyo alitaka kukata mzizi wa fitina, aende kuchukua abiria aliyempigia simu akimtaka afike alipo.

Mkono ule alijifanya kama alitaka kusalimiana naye. akampatia pesa huku akiachia tabasamu usoni mwake. Mpaka Afande yule alionesha kufurahishwa na jambo hilo. Aliishia kusema, “siku nyingine jua kujiongeza usisubiri muda upotee. Msalimie shemeji huko nyumbani”. Alipomaliza kutamka hayo alimruhusu kuendelea na safari huku akimpungia mkono kama alifahamiana naye kumbe katoka kuvujisha kipato cha mtu cha siku.

SHIDA ZA WANAOLIA BILA YA KUMPATA WA KUMLILIA, NDANI YA RIWAYA HII

ZIMWI LETU
 

Attachments

  • FB_IMG_1783889930577.jpg
    FB_IMG_1783889930577.jpg
    115.8 KB · Views: 1
Riwaya hii unaweza kuisoma kwenye mtandao wa Everand, ambao hata App yake ipo playstore. Unaweza kuchagua kutumia browser au App, kote inafunguka.

Everand ni mtandao wa malipo unalipia kwa mwezi na unasoma riwaya au kuaikilza Audio book uzitakazo kwa mwezi mzima. Ikiwa utajiunga tu aanakupa mwezi mmoja mmoja. Yaani ndani ya siku 30 unasoma riwaya uzitakazo kulingana na kasi yako tena bure.

Baada ya 30 ndiyo wanaanza kuchukua malipo na unaweza kucancel subscription muda wowote ule kama uliridhia malipo.

Bofya hapa ukajisomee ZIMWI LETU

Riwaya huko zipo za kutosha nimeweka, unaweza kuziona zingine kwenye orodha

GUSA HAPA kufungua ukurasa wa mwandisji wenye orodha ya riwaya zote ndani ya Everand
 
Back
Top Bottom