RIWAYA : MKONO WA CHUMA
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE.
_______________
ENDELEA.....
_______________
Edward Sambo akapigwa na butwaa, maana mtu aliyeamini amekufa, au mtu ambaye alifanya majaribio mengi ya kumuua, leo hii alikuwa mbele yake wakitazamana uso kwa uso,
"naona vyombo vya habari kila siku vinakuongelea wewe kama shujaa, kwa ushujaa gani uliofanya?" BQ aliuliza huku akiwa amesimama jirani kabisa na Edward Sambo ambaye alikuwa akitetemeka tu,
"sijaja kukupa onyo hapa, nimekuja kujionesha kwako kuwa bado nipo, Mungu amenipa nafasi ya tatu ya kuishi, aliniokoa nilipotaka kulipuliwa na ndege kule katika hifadhi ya wanyama, nikapona. Nafasi ya pili ni ile nilipopigwa risasi baharini, na nafasi ya tatu ni ya wewe kujaribu kuniua kwa sumu, ila bado naishi, nitakufa nikishapata haki yangu" BQ aliongea huku akiiweka bastola yake katika kichwa cha Edward Sambo,
"ondoka, polisi watakuja sasa hivi" Edward Sambo aliongea bila kutegemea,
"Polisi, polisi ndio wakina nani? mimi ni zaidi ya polisi, na uwape ujumbe, waambie kuwa ule unyama nilioufanya hawali, nitauongeza mara mbili, maana wameshindwa kuniua kwa kunitumia mwanajeshi wa kukodi" BQ aliongea huku akiikoki bastola yake, hapo Edward Sambo ushuzi ukamtoka akajikuta anabana miguu bila kutegemea.
Wakati BQ akiendelea kuongea na Edward Sambo, honi za gari zilisikika kutokea getini, BQ akasogea mpaka dirishani na kuchungulia, walikuwa ni polisi, BQ akarudi mpaka aliposimama Edward Sambo,
"ebu ngoja nione kama na wewe unaweza kupewa nafasi ya pili ya kuishi kama mimi, nitafanya jaribio la kukuua" BQ aliongea huku akiiweka bastola yake katika paji la uso wa Edward Sambo,
"nina mengi sana ya kuongea na wewe, ila tutaongea kama utapata nafasi ya kuishi tena" BQ aliongea huku akiikoki bastola yake na wakati huo Edward Sambo alikuwa akiomba polisi waingie ndani tu wamuokoe.
Uko nje polisi waliendelea kupiga honi,
"mbona hatoki?" Dereva wa ile gari ya polisi alimuuliza mwenzake waliyekuwa nae upande wa mbele,
"alafu sio kawaida yake, kila siku uwa tunamkuta getini anatusubiri, leo sijui imekuwaje? au alizidisha kilevi jana?" Yule Polisi mwingine alihoji,
"kwani anakunywaga yule mzee?" Polisi dereva aliuliza huku akicheka,
"anapiga vyombo huyo, tena zile pombe kali kali" Yule polisi mwingine alijibu, kisha akatoa shingo kwa dirishani na kuangalia katika upande wa nyuma wa gari ambao kulikuwa na Askari katika bodi ya gari,
"mmoja ashuke akamuangalie ndani" Askari alipaza sauti kuwaambia wenzake, wakati askari mmoja akishuka ili aingie ndani, walisikia mlio wa risasi, wote wakaruka chini na kulala, walijua kabisa mlio ule umetokea ndani ya nyumba ya Edward Sambo.
Wakiwa bado wanajipanga namna ya kuingia ndani, walisikia mlio mwingine wa risasi, Askari mmoja mwenye nyota mbili, akainua mkono na kutoa ishara watu wawili waingie ndani, kisha yule Askari mwenye nyota akasogea getini na kufungua, Askari wawili wakaingia ndani kwa mtindo wa kutambaa ardhini, kisha wale wa nje wakasubiri sekunde thelathini, hawakusikia shambulio jingine lolote. Askari yule mwenye nyota mbili akatoa ishara kuonesha Askari wengine watatu waingie ndani, Askari watatu wakasogea na kuingia ndani ya geti, kisha yule Askari akaingia na yeye, akatambaa mpaka katika mlango wa kuingilia sebuleni wa nyumba ile, akawaita vijana wake kwa ishara, wakasogea mpaka karibu yake kwa tahadhari kubwa,
"tunavamia sasa, mmoja atafungua mlango, alafu sisi tutaingia kwa kasi ndani na kutawanyika ili kumchanganya adui, sawa?" Askari mwenye nyota mbili aliuliza na wenzake wakajibu kwa kutikisa kichwa kuonesha kukubaliana nae, kisha yule Askari akahesabu kwa vidole mpaka tatu, mmoja wao akafungua mlango kwa kasi, na wengine wakarukia ndani huku silaha zikiwa mkononi, wakamkuta Edward Sambo akiwa amekaa katikati ya dimbwi la mkojo huku akihema haraka haraka,
"mzee Kuna usalama?" Askari mmoja alimuuliza, Edward Sambo akaitikia kwa kichwa kukataa,
"nini tatizo?, maana tumesikia mlio wa risasi" Askari aliuliza,
"BQ" Edward Sambo aliongea,
"ndio nini?" Askari aliuliza,
"sio ndio nini, sema ndio nani?" Edward Sambo aliongea huku akimtazama yule askari usoni,
"sawa, BQ ndio nani?" Askari aliuliza,
"Yule mwanamke muuaji tunayemtafuta" Edward Sambo alijibu na kuwafanya Askari washangae na waweke vizuri silaha zao,
"kafanyaje?" Askari aliuliza,
"ndio aliyepiga zile risasi, alinivamia" Edward Sambo alijibu
"Yupo wapi sasa" Askari aliuliza,
"atakuwa ameshaondoka, alielekea katika chumba changu, kisha kama mlisikia ule mlio wa risasi wa mara ya pili, nadhani alitumia kuvunja kioo cha dirisha, maana alipiga ile risasi akiwa ndani" Edward Sambo aliongea,
"lakini dirishani si Kuna nondo?" Askari aliuliza,
"ndio zipo, kwa hiyo inawezekana bado yupo ndani?" Edward Sambo aliuliza huku akipata nguvu ya kuamka baada ya kugundua kuwa hata kama yule mwanamke amevunja kioo, basi nondo zitamshinda,
"Twendeni" Askari mwenye nyota mbili aliwaambia wenzake huku akiongoza kuelekea katika vyumba, kulikuwa na vyumba viwili tu, kimoja uwa kinafungwa muda wote, kwa hiyo wao walienda moja kwa moja katika chumba cha Edward Sambo, wakapigwa na mshangao mara baada ya kuliona dirisha, ndio kioo kilivunjwa, ila nondo za dirisha hazikukunjwa, ila zilikatwa kabisa, tena sio na machine, inaonesha zilikunjwa kunjwa mpaka zikakatika.
"huyo mwanamke ni mwanaume?! " Askari mmoja aliuliza baada ya kuona hilo tukio,
"acha maswali ya kipumbavu" Mkubwa wake aliongea huku akisogea dirishani.
"ameshaondoka, hakika BQ bado ana uwezo mkubwa sana" Edward Sambo aliongea na kufanya Askari wamtazame,
"unamjua muda mrefu kwani?" Askari alimuuliza,
"sana, tena sana" Edward Sambo alijibu,
"twende ukatoe taarifa ya kuvamiwa kituoni, na hayo maelezo mengine utayatoa mzee wangu" Askari mwenye nyota mbili alimwambia Edward Sambo,
"ngoja nikaoge wadogo zangu, si mnaona hali niliyonayo?" Edward Sambo aliongea huku akiwaonesha eneo la mbele la suruali yake, lilikuwa limelowana mkojo.
Ilibidi polisi wamsubirie Edward Sambo aoge, safari ya msituni haikuwepo tena, maana mtu waliyekuwa wanaenda kumtafuta, waliambiwa ametoka muda sio mrefu.
Baada ya nusu saa, Edward Sambo alikuwa ameshamaliza kuoga, wakatoka pamoja mpaka nje, wakaingia katika gari, safari ya kituoni ikaanza.
Iliwachukua muda mchache tu kufika kituoni, wakatelemka na moja kwa moja walimpeleka Edward Sambo katika ofisi ya mkuu wa polisi, alitakiwa akaeleze alichokutana nacho kutoka kwa BQ.
***************
Baada ya mahojiano kati ya mkuu wa polisi na Edward Sambo kuisha, habari ya kuonekana kwa dada muuaji ilienea kwa haraka sana, safari hii mpaka jina liliwekwa wazi, jina lake halisi, Maria Zyachenko.
Mishale ya saa moja usiku, mkuu wa polisi alipigiwa simu kutoka ikulu, alihitajika na Rais kwa haraka sana.
Mkuu wa polisi alishangaa huo uito, maana tangu alivyoapishwa ndani ya ikulu, hajawahi kufika tena eneo hilo.
Mkuu wa polisi alifika mpaka Ikulu, akakaguliwa mlangoni na kuruhusiwa aingie, akaingiza gari na kuiegesha katika sehemu maalum za maegesho, kisha akatelemka na kuanza kuelekea ndani, ila alisimamishwa na mlinzi mmoja wa Ikulu, akampa heshima yake,
"mheshimiwa Rais yupo upande wa nyuma katika bustani, anakusubiri wewe, naomba nikupeleke" Mlinzi aliongea, kisha mkuu wa polisi akamfuata mpaka nyuma ya nyumba. Walimkuta Rais akiwa amevaa kaptula, laptop ilikuwa mezani, na pembeni ya laptop kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo, na kulikuwa na bilauri mbili, moja ilikuwa na kinywaji, inaelekea Rais alikuwa akinywa, na nyingine ilikuwa tupu.
Mkuu wa polisi alipofika karibu na Rais, alimpigia saluti,
"kaa hapo" Rais alimwambia mkuu wa polisi, na wakati huo yule mlinzi aliyemleta mkuu wa polisi alikuwa akiondoka.
Rais akachukua chupa ya mvinyo na kumimina katika ile bilauri tupu, kisha akamsogezea mkuu wa polisi, mkuu wa polisi akaipokea kwa heshima na kuigida kiasi, kisha akaishusha mezani.
"za siku bwana" Rais alimsalimia mkuu wa polisi,
"nzuri mheshimiwa" Mkuu wa polisi aliitikia kwa uoga,
"nataka kujua haya mambo wewe unayaendeshaje, maana sioni matokeo yoyote mpaka sasa?" Rais aliuliza huku akiifunga laptop yake na kumuangalia mkuu wa polisi,
"mambo gani mheshimiwa?" Mkuu wa polisi aliuliza huku mapigo ya moyo yakiongezeka kasi, maana mpaka Rais akuulize hivyo, ujue kuna jambo hujalifanya kwa ufanisi,
"Habari ya huyo mwanamke muuaji, wewe unaichukuliaje?" Rais aliuliza na kumfanya sasa mkuu wa polisi afikirie kwa muda,
"ni jambo zito kwa kweli, ila kama unavyosikia kupitia vyombo vya habari, huyu mwanamke baada ya ukimya kidogo, aligundulika alikuwa msituni, tena alikuwa na hali mbaya, tukatuma vijana waende wakamkamate uko, ila hatukufanikiwa kumpata mpaka leo tena tulivyosikia ameonekana asubuhi kwa Edward Sambo" Mkuu wa polisi alieleza,
"hii kesi nyie mnaifuatiliaje?" Rais aliuliza,
"samahani mheshimiwa, sijaelewa swali" Mkuu wa polisi aliongea kwa utulivu,
"yaani nyie kama polisi, kuna mtu yoyote mmemteua aifuatilie hii kesi au mnasubiri mletewe taarifa na wasamalia wema tu?" Rais aliuliza kisha akagida kidogo mvinyo,
"Kuna mtu maalum nilimteua aifuatilie hii kesi kwa siri" Mkuu wa polisi alijibu,
"amefikia wapi katika upelelezi wake?" Rais aliuliza,
"mmmh, kwa maelezo ya yule mpelelezi, anadai hili jambo, kuna vita nyingine ya mtu mwingine dhidi ya yule dada, na mtu ambaye anadai alimshuhudia akimpiga yule dada baharini na ikasemekana yule dada amekufa, ni Ray Charles" Mkuu wa polisi aliongea huku akimtazama Rais, Rais akatabasamu,
"huyo kijana wako mpelelezi anaitwa nani?" Rais aliuliza huku akitabasamu,
"anaitwa Joel Minja" Mkuu wa polisi alijibu,
"mwambie awe makini sana" Rais aliongea huku akitabasamu, ila hiyo kauli haikueleweka kwa mkuu wa polisi,
"sawa mheshimiwa" Mkuu wa polisi aliongea,
"au kama vipi, nitakupigia simu, nataka nionane na huyo kijana. Siku mbili hizi nitakupigia simu,. Kingine cha ziada, ongeza ufanisi uhakikishe huyo dada anakamatwa, na ikiwezekana afe kabisa, vinginevyo hiyo nafasi uliyonayo utaiweka mashakani" Rais aliongea kwa umakini mkubwa,
"sawa mkuu" Mkuu wa polisi alijibu kinyenyekevu,
"unaweza kwenda" Rais aliongea na kisha mkuu wa polisi aliamka na kuanza kuondoka, alipopotea tu machoni kwa Rais, alitokea Ray Charles, alikuwa amejificha, hakutaka mkuu wa polisi amuone.
"inaelekea wameshajua uwepo wako katika hii kesi, ila huyu mkuu wa polisi hana uhakika na uwepo wako" Rais aliongea lakini Ray Charles hakujibu kitu.
Wakati mkuu wa polisi akitoka, alipishana na mtu mwingine ambaye alimjua kupitia vyombo vya habari tu, hakuwahi kukutana nae, hivyo walipishana kimya kimya tu.
Yule mtu alielekea moja kwa moja mpaka upande wa nyuma wa Ikulu na kwenda alipo Rais, wakasalimiana kwa bashasha, kwa kukumbatiana, kisha yule mtu akakaa katika kiti, ila yule mtu alipotupa macho nyuma ya Rais, alimuona Ray Charles, yule mtu akashtuka, Rais akaligundua hilo,
"usiogope, kwanini unaogopa?" Rais alimuuliza yule mtu,
"huyu si Ray Charles huyu" Yule mtu aliuliza huku akimuoneshea kidole Ray Charles ambaye aliangalia chini,
"ndiye yeye" Rais alijibu huku akitabasamu,
"imekuwaje kuwaje anaishi wakati alishakufa, familia ilishazika mabaki ya mwili wake?" Yule mtu aliuliza,
"unataka kujua imekuwa Ray anaishi tena?" Rais aliuliza huku akitabasamu,
"ndio, nataka kujua kwa kweli, maana huu ni muujiza" Yule bwana alijibu huku akiwa bado akimtazama Ray Charles,
"lakini hicho sicho nilichokuitia hapa?!" Rais aliongea huku akimimina mvinyo katika bilauri yake,
"ulichoniitia utaniambia baadae, nataka kujua kwanini Ray Charles yupo hai" Yule bwana aliongea,
"sawa, Ray, ebu nenda katembee kidogo" Rais aliongea huku akimgeukia Ray Charles, ambaye taratibu aligeuka na kuondoka eneo hilo, yule bwana alikuwa bado anamuangalia tu Ray Charles, hakuwahi kuamini hata siku moja kuwa Ray Charles anaishi,
"huyo utakuwa unamuona kila siku, hata usijali" Rais aliongea huku akimtazama yule bwana,
"aisee, dunia ina maajabu. Haya nieleze ilikuwaje?" Yule bwana alimuuliza Rais,
"ni story ya kusisimua kidogo'' Rais aliongea huku akiweka sura ya umakini,
"nieleze tu" Yule bwana alionesha kiu yake ya kutaka kuujua ukweli,
"sawa, ngoja nikupe ukweli, ila hakuna anayejua ukweli zaidi yangu na yeye, wewe utakuwa wa Tatu" Rais alianza namna hiyo, kisha akaendelea..
"Huyu Ray Charles sio mzimu wala sio robot " Rais aliongea na kumfanya yule bwana awe makini zaidi..........
**********ITAENDELEA**********
*kwani Kuna mtu hataki kujua habari za Ray Charles humu?
Tutamjua zaidi katika episode inayokuja
the Legend☆