MKE WA RAIS
Mwandishi Ibrahim Masimba
Phone 0743990480
*******
Hakumuona mwanaharamu, hakuwaona mabinti wawili na kingine hakumuona mwanadada aliekuwa akihudumu. Wote walitoweka katika mazingira tatanishi, lakini kule kumuona Nemisis the bastard maeneo yale akatambua kila kitu kilikuwa mikononi kwa mwanaharamu, kila kitu kilikuwa kimesimamiwa na kichaa mwanaharamu katika fani ya ujasusi. Hakuinuka kwa haraka, bali bado alikaa akiendelea kutizama mlangoni. Watu walikuwa wakiingia na wengine kutoka, katika hali ya kustaajabisha kama sio kushangaza, akamuona Bastard akiwa sambamba na mwanamke aliyekuwa akihudumu muda mfupi uliopita. Mwendo wao na hatua zao hazikuwa na urafiki kati yao. Mudy ni jasusi alieiva kisawa sawa, alitambua kile ambacho bastard amefanya. Moyoni akatabasamu akaiona safari ya kuelekea Victoria Base imefika. Akaendelea kuwasindikiza kwa macho, baada ya kupotea katika upeo wa macho yake naye akasimama kuelekea tena pale mapokezi. Tabasamu lilikuwa usoni huku mluzi ukisikika mdomoni.. Hakuwa na wasiwasi, hakuwa na hofu wala woga, alikuwa akitembea kama yupo juu ya ardhi ya Tanzania, Ardhi iliobarikiwa kuwa na vitu vingi lakini visivyo na msaada kwa watu wake kutokana na tamaa kutoka kwa viongozi wakuu. Akapokelewa tena na msichana yule, msichana ambaye hapo mwanzo hakumuonyesha ushirikiano. Hakutaka kusimama hapo zaidi ya kuchukua ufunguo na kupandisha ngazi kuelekea chumbani kwake, muda wote hakutaka kuwaza wapi alipoelekea mwanaharamu sambamba na mwanamke yule mateka. Yeye shida yake ilikuwa kwa yule mwanamke mwingine, mwanamke ambaye alikuwa akimfuatilia hapo mwanzo, mwanamke ambaye alihusika kuvamiwa kwa dereva tax kisha kuawa. Mwanamke ambaye alimuona kwa macho yake. Akazimaliza ngazi na kuifuata korido ambayo ilimfikisha mlangoni mwa chumba chake, kabla hajafungua aliupita kwanza mlango na kupitiliza mbele kana kwamba anaelekea eneo tofauti la hoteli ile. Hakuwa na wasiwasi wowote bali alitaka kujua kama yupo peke yake ama kuna watu waliokuwa wakimfuatilia kwa nyuma. Hazikupita dakika mbili akawaona watu watatu wakitembea kuelekea mlangoni mwa chumba chake, akatulia huku macho yake yakicheza kila sehemu. Akawaona mmoja kati ya watu wale akiuendea mlango na kuugusa, akatulia kwanza, muda mfupi akamuona mtu yule akichomoa kitu mfukoni, akaonekana akichomeka kwenye kitasa, mlango ukafunguka akashuhudia mtu yule akiingia huku wale wawili wakibaki pale pale wakitizama huku na huko. Muddy akaendelea kutulia hapo. Sekunde kumi na tano baadae akamuona mtu yule akitoka kisha kuufunga mlango, wakaondoka wote watatu. Baada ya watu wale kuondoka Mudy akaamua kurudi pale chumbani.
Aliufungua mlango taratibu, akaingiza uso kisha ukafuatia mwili. Macho yake yakatizama kila upande na kona ya chumba kile. Hapo macho yake yakakiona kitu, kitu ambacho kilitegwa penbeni kabisa kwa kitanda. Akaanza kuipiga hatu ya kwanza, akaipiga ya pili kukifuata kitu kile, lakini kabla hajakifikia masikio yake yakanasa kitu, kitu ambacho kiliufanya mkono wake ushuke mpaka alipoihifadhi bastola yake. Ilikuwa michakato ya miguu ya mtu nje ya mlango wa chumba. Hakutaka kudharau mawazo yake, kushuka kwa mikono yake kukaambatana na kugeuka nyuma.. akashtuliwa na mlango kusukumwa kisha mtu mmoja kuingia huku mkononi akiwa amekamatia Bastola. Hakufanikiwa kumfikia, kwani muda ule ule mtu yule akaruka hewani na kumzoa Muddy, wote wakaenda chini mithili ya mafurushi. Bastola ikamponyoka Muddy na kuangukia umbali wa hatua nne. Hapo ndipo zilipoanza kupigwa pale chini, yalikuwa mapigano makali, mapigano ambayo yalionyesha kuelemewa kwa Mohammed. Alikutana na kisiki cha mpingo, alipigwa ngumi na mateke na hata aliporusha ngumi, alihisi nguvu kumuishia huku macho yake yakiingia giza. Kila sekunde alikuwa akipoteza fahamu, hakuwa Mohammed yule, hapa alionekana kama mlevi na asie na chochote.. akatulia huku damu zikimvuja mdomoni na puani. Hakuwa na uwezo huo tena
Muda mfupi wakaingia watu wengine wanne, kila mmoja alieingia aliuadhibu mwili wa Mohamed ambao ulikuwa umelala bila kuwa na fahamu. Baada ya kuhakikisha Mudy ametokota na hakuwa na madhara tena wakamfunga kamba miguuni na mikononi kisha akatiwa kwenye mifuko maalum, baada ya hapo akabebwa begani na kutolewa kama mzigo. Walipita naye mapokezi na kutoka naye nje kabisa ya hoteli. Wakaelekea mpaka sehemu ambayo walipaki magari yao. Mlango mmoja wa gari ukafunguliwa Mudy akatupwa kama furushi, kisha mlango ukafungwa tena, muda mfupi msululu wa magari ulikuwa ukiliacha Jiji la Vancouver safari hii wakielekea ViCtoria Base. Licha ya mudy kupoteza, fahamu lakini bado majasusi wale hawakutaka kufanya ujinga. Ingawa Muddy alikuwa ndani ya mifuko maalumu ya kuwekea maiti lakini bado wanaume watatu wenye bunduki kubwa za kivita walikuwa wametulia pembeni ya mwili wake huku midomo ikielekezwa kwake.
**********
Kilikuwa chumba kidogo sana na chenye kiza kizito sana, harafu ya kifo, damu, mikojo na kinyesi ilisikika kila upande. Maji machafu yaliomwagwa chini hakikuwa kitu kigeni katika chumba kile. Chini ya sakafu ya chumba kile ulionekana mwili wa mwanamke uliolazwa pasipokuwa na hata nguo moja. Ulionekana kama mwili usiokuwa na uhai, ulionekana ni mwili wa mtu ambaye alipata mateso makali sana. Hakuonyesha kama alikuwa na Uhai, damu zilikuwa zikichuruzika mwilini kama maji, mwili wake mzuri ulikuwa umejaa majeraha kila kona, majeraha ambayo hayakumpa nafasi ya kuishi tena. Hakuwa mwingine bali Sylvia Badenshok mwanamke aliyekuwa ametekwa na Nemisis the bastard wakati alipokuwa akihudumu katika hoteli fulani. Licha ya kuteswa kwa kila njia lakini hakuinua kinywa chake kujibu maswali alioulizwa. Muda wote alikuwa akiteswa huku akiwetemea mate wetesaji. Hakufumbua mdomo juu ya wapi ilipo kambi ya victoria, hakufumbua mdomo wa kutaja ni wapi walipo viongozi waliokuwa wamepanga kufanya mapinduzi. Kikubwa alichowaambia ni kwamba Watakufa hata kabla hawajafanikisha wanachokitaka kwani Ilikuwa Vigumu kupambana na Majasusi wale kisha kurudi hai. Yalikuwa maneno ambayo hayakukubalika ndani ya Kichwa cha Mwanaharamu. Hakuwahi kushindwa kufanya kitu na kikafeli.