KIDOKEZO
Si kazi yangu kujishughulisha na makosa ya jinai.Nilishangaa kidogo Chief aliponiamuru nifuatilie tatizo la upungufu wa almasi.Isingekuwa kwa sura aliyoonesha,nilitaka kumwambia apeleke malalamiko yake kwa kamishna wa polisi au anipe uhamisho kwenda huko kama alikuwa hanihitaji katika idara yake.
Siku hiyo alivaa sura ya kutisha na sikuwa na la kufanya ila kukukubali.Kulikuwa na ushahidi kwamba almasi zilizouzwa katika Masoko ya nje zilikuwa chache sana Kulinganisha na kiasi kilichochimbwa,kwa nini?
Idara ya upelelezi ya makosa ya jinai imejitahidi bila mafanikio.Askari polis Joel amegusa chanzo cha uhalifu,akafa katika ajali ya ndege siku chache kabla ya kufunga ndoa na mchumba wake Amanda,na uhalifu ukaendelea.
Chifu alimtuma Jack Mbwile,mpelelezi wa kawaida,lakini maiti yake ikaokotwa ikielea katika ziwa Victoria na uzito wa jambo zima ukawa umetambuliwa.Ndipo nikatumwa mimi,Willy Gamba
Lahaula!Kama ungetumwa wewe nina hakika ungekimbia na kupotea Kabisa!Lakini mimi sio wewe.Safari yangu ilinichukua katika miji ya Mwanza,Shinyanga,Maganzo na Songwa na uvundo nilioufichua ulisababisha umwagaji mkubwa wa damu na kuteketeza maisha ya watu wengi.
Yalikuwa mapambano makali na kila mmoja wetu alishangaa kuona ni nani alikuwa anaongoza uhalifu huo.
Ama kweli kikulacho ki nguoni mwako.