Hebu onja kidogo hii kitu..
UCHU
KAZI IMEANZA
IV
Ndege ya Chama Cha Msalaba Mwekundu
ilitua kwenye uwanja wa ndege wa
Kayibanda mjini Kigali yapata saa nne
kamili. Willy Gamba alichukua mkoba
wake na kutelemka.
"Asante", Willy alimshukuru rubani na
kumpa dola mia za kimarekani.
"Asante sana mzee", yule rubani
alishukuru na kufunga mlango tayari kwa
kuruka tena.
Willy alikwenda moja kwa moja kwenye
jengo la uwanja wa ndege na kuelekea
Uhamiaji. Ulinzi uwanjani ulikuwa bado
mkali lakini kwa sababu alikuja kwa
ndege ya Chama Cha Msalaba Mwekundu
na alikuwa amefanyiwa mpango na rafiki
yake Dar es Salaam aje apokelewe na
mmoja wa maafisa wa Msalaba
Mwekundu walioko Kigali, yeye akiwa
kama Afisa wa habari wa Msalaba
Mwekundu kimataifa na ndivyo Chifu
alivyomtayarishia pasipoti aliyoikuta
nyumbani, taratibu zake pale uwanja wa
ndege zilikwenda haraka bila kipingamizi
chochote.
Katika pasipoti yake hii jina lake lilikuwa
George Mambo.
Alipojitokeza tu nje, alimkuta mwenyeji
wake aliyekuwa amevaa beji ya Msalaba
Mwekundu na kwa vile na yeye toka
alipotua tu aliweka beji aliyokuwa
amepewa na Msalaba Mwekundu
wakatambuana mara moja.
"Bwana George Mambo natumai", yule
mwenyeji wake alisema huku akitoa
mkono wa salamu.
"Ndio mimi. Habari zako", Willy alijibu na
kusalimu.
"Nzuri, mimi naitwa Vicent Nyemazi, ni
afisa wa habari hapa, na mimi ni Mhutu
ila mimi siyo Mhutu mwenye siasa kali",
Vicent alijibu huku akitabasamu.
"Vizuri sana na pole kwa yote yaliyotokea
hapa nchini kwenu".
"Asante sana, ndio hali ya dunia. Gari
nimeegesha hapo mbele", Vicent alieleza.
"Mkahawa wa hapa umefunguliwa?", Willy
aliuliza.
"Ndio, uko wazi".
"Unajuwa nimeondoka asubuhi sana,
sijanywa hata chai na ndege zetu kama
unavyojuwa si kama ndege za abiria,
hamna chochote hata kikombe cha chai",
Willy alijibu huku akiangalia saa yake.
"Sawa, twende hapa kuna mkahawa
mzuri, na hali imeanza kurudi kama
zamani, hivyo vitu vingi vinaendelea
kama kawaida.
Walipanda juu kwenye mkahawa na willy
aliagiza kahawa na kipande cha mkate na
Vicent akaagiza kahawa peke yake. Willy
aliangalia saa yake kwa chati kabisa,
akajuwa ile ndege ya Tanzanair ilikuwa
karibu kutua, na alitaka tu kuona kama
kungeweza kuwa na fununu za kuja
kwake. Hii ilikuwa hadhari tu kwani
aliamini hakuna mtu ambaye angeweza
kujua kuwa anakuja kwa jinsi alivyokuwa
ameondoka Dar es Salaam kisirisiri.
"Ah, vipi hali ya huko Ngara, nasikia hali
ya wakimbizi ni mbaya sana, yaani
chakula, maji na madawa ni taabu",
Vicent aliuliza.
"Ni kweli hali ni mbaya, jumuiya ya
kimataifa inajaribu kusaidia lakini
wakimbizi ni wengi mno. Fikiria watu
kama wa mji huu mnamo wiki moja
watengeneze mji mwingine ambao
haukuwepo kabisa, ambako ni porini tu
hakuna huduma za kijamii za aina...".
Kabla Willy hajamaliza kueleza mlio
mkubwa ulitokea na mara ukatokea
mlipuko. Willy na Vicent walikimbilia
dirishani kuangalia kwenye uwanja wa
ndege ambako ndiko mlipuko ulikotokea.
Kwenye barabara zinakoondokea na kutua
ndege wakaona vipande vya ndege
vimesambaa na kuwaka moto.
"Kazi imeanza", Willy alisema na kumvuta
Vicent mkono. Wakakimbilia chini
kuangalia kwani vishindo vya kukimbia
uwanjani vilisikika kutoka kila pahala.
Walipofika chini na kuelekea uwanjani
walikuta magari ya jeshi aina ya
Landrover yakiwa yamejaa askari
yakielekea pale mabaki ya ndege
yalipoangukia na wengine wakija huku
kwenye jengo la uwanja ili kuzuia watu
wasiende kule uwanjani.
Vicent na Willy walionyesha beji zao za
Msalaba Mwekundu wakiomba wafike
kwenye tukio lakini walikataliwa na askari
ambao kwa sasa walikuwa
wamechachamaa. Willy aligundua kuwa
kumbe walishajua atafika na maskini yule
rubani na afisa wa Msalaba Mwekundu
waliuawa kwa kufikiri ni yeye. Willy
alimshukuru Mungu kwa kumfanya afikiri
na kufanya kama alivyofanya.
Kweli kama Msoke alivyosema, kazi hii
tayari ilionyesha kuwa ni ya hatari. Ila
kilichomshangaza Willy ni jinsi yule mtu
aliyeshambulia ndege ya Tanzanair
alivyojuwa kuwa yeye angekuwemo mle
ndani ya ile ndege. Hii ilionyesha kuwa
kati ya wale maafisa wa PAM miongoni
mwao kulikuwa na msaliti, lakini kwa
sasa hakukuwa na haja ya kufikiria hicho
ila kufanya kilichomleta Kigali. Huyu
msaliti angetafutwa baadaye. Jinsi ile
ndege ilivyokuwa imepigwa na kombora.
Willy alijua kabisa kuwa hakuna mabaki
ya binadamu ambayo yangeweza
kutambuliwa, kwani kombora lililotumika
lilikuwa kubwa wakati ndege yenyewe
ilikuwa ndogo.
"Twende zetu, nipeleke hotelini, acha
wanajeshi wafanye kazi yao", Willy
alimvuta Vicent wakaondoka huku
wakisesera kuelekea kwenye gari la
Vicent.
"Kwanini wameipiga ile ndege?", Vicent
aliuliza huku akifungua mlango wa gari.
"Huenda ilikuwa na hatari, bado unajuwa
mambo hayajatengamaa hapa", Willy
alijibu.
"Unafikia hoteli gani?".
"Nafikiri jaribu Meridian Hotel kama kuna
nafasi", Willy alijibu na kuikacha Hotel
Des Mille Collines aliyokuwa amepangiwa
na rafiki za Musoke, kwani sasa
hakukuwa tena na kumwamini mtu yeyote
kwa vile hakujuwa nani alikuwa ametoa
amri ya kupigwa kombora ndege
aliyopaswa kuwemo na huyo mtu alikuwa
anajuwa habari kiasi gani kumhusu yeye
Willy.
"Sawa, pale hotelini wanatua na watu
wetu kutoka mataifa ya nje wako pale. Na
vilevile pana usalama maana ofisi zingine
za jeshi ziko pale, na maafisa wengine wa
jeshi wanakaa pale", Vicent alimweleza
Willy. Wakati wakielekea Meridian Hotel
walikutana na magari madogo ya jeshi,
kama matatu, yakielekea uwanja wa
ndege. Willy aliona wengi walikuwa
maofisa wa vyeo vya juu na akahisi
walikuwa wanakwenda kutathimini tukio
lililotokea.
Walipofika Meridian walikuwa watu wako
vikundi vikundi wakizungumza, bila saka
walikuwa wamepata habari za tukio la
uwanja wa ndege. Vicent likwenda
mapokezi na kuzungumza na mmoja wa
wafanyakazi wa pale ambaye alionekana
kumfahamu sana, na baada ya muda
kidogo Willy aliitwa kujaza fomu za
kupatiwa chumba. Baada ya kupewa
funguo alichukua mkoba wake na vicent
akamweleza kuwa atamsubiri kwenye
mkahawa wa hoteli.
"Si utataka twende ofisini?", Vicent
aliuliza.
"Bila shaka", Willy alijibu.
"Basi utanikuta hapo kwenye mkahawa".
"Asante", Willy alijibu na kuelekea kwenye
ngazi kwani alikuwa ameelezwa lifti
zilikuwa hazifanyi kazi. Alikuwa amepewa
chumba namba 412, ghorofa ya nne.
V
Baada ya Col. Gatabazi kuhakikisha kuwa
hakuna kitu kilichobaki ndani ya ndege na
ndege yenyewe, alielekea nyumbani
kwake ili akampashe habari Jean.
Alipompata Jean alimweleza. "Kazi tayari,
mtu wako hata mfupa haukuonekana,
kawa hewa".
"Safi sana, hakika mimi hupenda mtu wa
vitendo na siyo maneno", Jean alijibu.
"Lililobaki ni la kujieleza kwanini
tumeipiga hiyo ndege, lakini tayari mkuu
nimemwandikia taarifa safi ambayo
hawezi kuwa na mashaka nayo. Wasiwasi
wangu Tanzania tu", Col. Gatabazi
alieleza.
"Nilikwambia Tanzania niachie mimi.
Tuongee jioni. Kama kawaida mzigo
mwingine unatua leo, na ni shehena
kubwa", Jean alijibu na kabla Col.
Gatabazi hajajibu alikata simu.
Baada ya kukata simu ya Col. Gatabazi.
Jean alimpigia simu JKS, Dar es Salaam.
JKS, aliyekuwa na wasiwasi mkubwa
aliipokea simu haraka ilipolia. "Nani".
"Jean hapa. Kigali Bingo!!, mambo safi".