KISA CHA 15
ILIKUWA ni karata ya aina yake ambayo mama huyu aliamua kuicheza ikiwa hajui upande wa pili umezichanga vipi karata zake. Alifanya hivi bila wasiwasi hasahasa baada ya kugundua ule mchezo aliokuwa anashiriki uliitwa Kombolela.
Mmoja akimuwahi mwenzake nd’o mwisho wa mchezo!
Alikuwa amebeba kapu lililosheheni mchicha na mboga nyingine za majani.
Alipita mitaa kadhaa kutafuta uzoefu na kisha akamlizia Magomeni mikumi, katika nyumba ambayo alikuwa akiishi waziri wa nishati na majini bwana Mathias Obhare.
Siku hiyo alijaribu kufanya madaha ya hapa na pale ili geti liweze kufunguliwa lakini hakuna mtu aliyejitokeza kufungua.
Majirani walidai kuwa katika nyumba ile ni mara chache sana wenyewe kuonekana na haijulikani rasmi iwapo waziri huwa anaishi pale ama ni mojawapo ya samani zake.
Mama lao hakukata tamaa na siku iliyofuata kama kawaida alipitisha mboga huku akipita katika lile geti jeusi na kuita iwapo wenyewe wapo waweze kununua mboga.
Na siku ya pili hali ikawa ileile. Mama lao ambaye alikuwa akiwasiliana na Yakubu Gama ambaye alikuwa Morogoro alianza kukata tamaa lakini Gama akamsihi kamwe asikate tamaa.
Siku hii Mama lao alibahatika kuwakuta wenyeji wake.
Akabisha hodi mlango ukafunguliwa akapenya ndani na beseni lake lililosheheni mboga mboga. Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana alipoona geti likifungwa, tumbo lilimuunguruma kwa uoga lakini hakuacha kutabasamu.
Mara akatokeza msichana mrefu mweusi, akamkaribisha mama lao na kumuuliza ni mboga gani alizokuwanazo katika kapu lake.
Mama lao akazinadi mboga zote kwa ustadi huku akizipa sifa ambazo hazikuwepo hata kwa mbali.
Baada ya maneno mengi ya mama lao yule binti akaingia ndani na kurejea na ungo ambao ulionekana kuwa unatumika mara kwa mara.
“Niwekee zote!” yule binti akamweleza mama lao. Mama lao akashtushwa sana lakini hakuruhusu mshtuko ule waziwazi badala yake ili kumpoteza malikiti yule dada mrefu mweusi, mama lao akapiga magoti chini na kuanza kumshukuru yule binti.
“Kawaida tu mama yangu, imekuwa bahati yako tu maana mara kwa mara huwa naenda kuhemea sokoni mwenyewe!”
“Ubarikiwe sana mwanangu, ubarikiwe” mama lao akahitimisha kwa kunyanyua mikono juu na kumshukuru Mungu wake.
Akamwaga mboga zote kwenye ule ungo. Yule dada akampatia shilingi elfu kumi, mama lao akataka kutoa chenchi yule binti akamruhusu aondoke nayo yote.
Mama lao kwa mara nyingine tena akapiga magoti na kushukuru! Binti akamnyanyua mama lao akatii na kutoweka eneo lile.
Alipofika nje ya geti tu akajisemea kwa sauti ya juu kiasi.
Kombolela Obhare!
Akimaanisha kuwa na Obhare naye alikuwa anelekea kupatikana. Kwani kujulikana kwa nyumba ile kuishi watu ni hatua kubwa.
***
MWILI wa Yakubu Gama ulikuwa ukiimarika kadri siku zilivyokuwa zinasogea mbele, ripoti za mama lao zilikuwa zinazidi kumsisimua na kumfanya awe na kiu ya kukabiliana na wapinzani wake ambao alianza kuwajua mmoja baada ya mwingine japo kwa hisia.
Sasa hakuwa akichechemea tena na aliweza kufanya mazoezi ya kukimbia na kuruka kamba. Mazoezi ambayo yalizidi kuichangamsha damu yake.
Hatimaye yule daktari akakiri kuwa Gama ni mtu wa ajabu sana kwani alikuwa amepona upesi sana tofauti na alivyodhania awali.
Gama akaruhusiwa rasmi kuendelea na shughuli zake.
Kikosi kazi kikakamilika!
Gama akatoweka mjini Morogoro akiwa amepewa kiasi cha kutosha cha pesa na bwana Robert ili aweze kuikamilisha kazi yake.
Hatua ya kwanza kabisa alianzia pale mama lao alipokuwa ameishia.
Mama lao alikuwa ameigundua nyumba ya waziri wa nishati na madini, Mathias Obhare. Nyumba ambayo hakuwa akiishi na familia yake lakini mara moja moja alikuwa akiingia na wageni na kisha kutoka bila kujulikana iwapo aliwaacha wageni mle ndani ama vipi.
Gama akaanzia hapo na kutaka jibu la kuna nini ndani ya nyumba ile. Na kwanini mara kwa mara hakuna watu wanaoonekana kuishi pale.
KOMBOLELA ikaendelea…..
Mama lao akashauriwa na Gama apumzike kwani kazi aliyoifanmya ni kubwa na kipande kilichosalia ni kidogo sana ataweza kukimaliza peke yake upesi.
Mama lao akakubali kuwa atapumzika!!
*****
MAJIRA ya saa nne usiku katika kijiwe cha kahawa maeneo ya Magomeni Mikumi wazee walikuwa wakibishana juu ya mambo ya siasa hasahasa juu ya uchaguzi mkuu wa raisi ambao ulikuwa umebakiza miezi kadhaa tu uweze kufanyika.
Wazee waligawanyika makundi matatu, kundi moja likimuunga mkono Mathias Obhare, kundi la pili likikunga mkono chama cha upinzani na kundi la tatu likiwa haliungi mkono upande wowote.
Kati ya wote waliozunguka kile kijiwe ni mzee mmoja tu ambaye hakuwa mwingi wa maneno, yeye alikuwa akibugia kashata na kushushia kwa kahawa, kanzu yake nyeupe iling’ara vyema gizani huku kibalaghashia chake kikihifadhi kichwa chake kiunadhifu. Miguuni alikuwa amevaa makubadhi ya gharama ya kawaida.
“Eti ustadhi, wewe kwa akili ya kawaida tu unaweza kusema kuwa Obhare ana uwezo mzuri wa kutawala kuliko John Masele?” mzee mmoja akamuuliza yule bwana ambaye alikuwa mkimya.
Yule bwana akakohoa kidogo kisha akatoa jibu ambalo liliumaliza ule mzozo.
“Anayetakiwa kuzungumzwa kwa sasa si Masele tena kwa sababu hayupo kwenye kinyang’anyiro…. Jambo la msingi ni kumpokea huyo Obhare liwalo na liwe walishazoea watanzania sisi vichwa vya wendawazimu….”
Kimya kikatanda, kila mmoja akatafakari kauli ile kwa uzito na majibizano yakaishia pale.
Yule bwana akaendelea kubugia kashata na kahawa hadi kijiweni alipobaki yeye na muuzaji tu.
Alipoitazama saa yake ilimwelekeza kuwa ilikuwa ni saa tano usiku.
Wakati muafaka kabisa aliokuwa amepanga.
“Dah! Haya magari hapa hivi shilingi ngapi wanalipia kupaki…” Yule bwana mwenye kibalaghashia akamuuliza muuza kahawa.
“Dah! Halafu mlinzi alikuwa hapa muda si mrefu, yule mzee mbishi yule. Ungemuuliza sema sasa hiv atakuwa ameenda kujidunga ulabu, akirudi hapa ni kulala tu yaani…”
“Duh! Yaani anafanya lindo huku amelewa mbona balaa…”
“Tushamzoea yule na ana bahati kwa sababu Magomeni haina usiku, watu wanakesha hivyo vibaka hakuna.”
Yule bwana akaifunua kanzu yake akatoa noti akamlipa yule muuza kahawa, akapewa chenchi yake na kutoweka kuelekea alipopajua yeye mwenyewe.
Baada ya nusu saa akapita eneo lile lile kwa muuza kahawa akiwa amevaa bukta, na kofia kichwani, fulana nyeusi iliyoufanya mwili wake uonekane vyema kuwa ni wa mazoezi. Lakini akiwa gizani ilimfanya aonekane kama kivuli ama asionekane tofauti yake na giza.
Naam! Mtu yuleyule lakini muonekano mwingine.
Alikuwa ni Yakubu Gama.
Hakusimama popote na alikuwa kama mwenyeji sana eneo lile. Akatembea usawa wa magari mengi yaliyoegeshwa eneo lile.
Ukimya ulikuwa mkubwa sana hadi akaufikia ukuta ambao haukuwa mrefu sana.
Kama afanyavyo paka, Gama akaruka na katika sekunde iliyofuata bunduki yake ilikuwa kiganjani akiwa amepiga goti, macho yake ya paka yakimsubiri yeyote ajikohoze na ayapokee mauti yake.
Kimya! Hakuna aliyejitokeza.
Na yeye hakujitikisa kwa sekunde takribani nne.
Kisha akiwa amepiga goti vilevile alinyata kwa kuliruhusu goti jingine kupiga hatua na jingine kufuata.
Akaufikia mlango wa kuingilia sebuleni, alipougusa na kujaribu kuufungua akasikia dalili ya kiumbe nyuma yake.
Hakujiuliza mara mbilimbili, akafyatuka teke la punda kinyumenyume.
Kiumbe nyuma yake kikabweka kwa maumivu.
Wacha we! Mbwa mkubwa wa polisi alikuwa akitazamana na Gama huku hasira zikiwa zimemuwaka sana.
Uzuri ni kwamba Gama hakuwa mgeni na mbwa wale! Alitambua kuwa mbwa wale sio wepesi kubweka na badala yake hurarua kimya kimya. Hii ilikuwa faida kwake kutoshtukiwa na watu kuwa yupo pale.
Mara moja akafyatuka mzima mzima kisha akaunyoosha mguu wake barabara ukajikita katika shingo ya yule mbwa.
Mbwa akalainika na kutua chini kwa kishindo kikubwa kishindo ambacho kilianza kuleta harufu ya vurumai. Kishindo kikamfikia mtu mwingine aliyekuwa macho katika nyumba ile.
“Perry….. Perry…kuja kuja” sauti ya ikume ilisikika ikiita jina.
Gama akatambua kuwa lile lilikuwa jina la mbwa.
Kutokana na ukubwa wa yule mbwa Gama upesi upesi akajirusha na kujikunyata nyuma ya kule mbwa. Alifanya vile ili aweze kuipata shabaha yake vyema kama alivyokusudia wakati ule muitaji atakapofika.
Naam yule muitaji akamkuta mbwa akiwa amelala chini kiubavuubavu..
Kama alivyotaraji Gama kuwa yule bwana atafika kwa papara na kumwinamia yule mbwa ili ajue kulikoni.
Hakika ilikuwa hivyo.
Na katika ile sekunde aliyoinama naye Gama aliufyatua mguu wake ukajikita katika taya ya yule bwana, katika sekunde iliyofuata tayari alikuwa ameikaba shingo ya yule kiumbe.
Ilifurahisha kutazama utaalamu wa Gama.
“Nani wamo ndani?” aliuliza Gama.
Jamaa akajipandikiza kiburi hakujibu!
Gama akamjaza ngumi moja matata kiunoni, kisha akamziba mdomo.
“Utanijibu sasa eeh!” akakoroma Gama.
Lakini mara akausikia ubaridi ukipenya katika shingo yake. Akatambua kuwa ilikuwa ni bunduki.
Gama akafyatua teke kinyumenyume upesi ili kumwadhibu mwenye ile silaha. Lakini mara akajikuta akipiga teke nguzo ya chuma.
Na aliyeikamata ile bunduki akimtolea tabasamu la dhihaka.
“Tulia hivyo hivyo kijana lasivyo nafyatua hicho kisogo chako!” sauti ya kike ikamuamrisha.
Gama akafadhaika sana kukamatika kiulaini vile. Tena mbele ya mwanamke!!
Akasalimu amri na mikono yake akanyoosha juu huku akili ikifanya kazi kubwa sana ya namna gani kuchomoka pale.
Ghafla yule mwanamke ambaye hakuonekana kuwa na madhara zaidi ya kushika bunduki akafyatuka hewani kwa kushtukiza, na hapo Gama akapokea teke kali katika mbavu zake akalainika na kuangukia goti moja. Hakuamini kuwa yule alikuwa mwanamke.
Dada yule akatulia kama sio yeye aliyeyemsulubu Gama.
Hakufanania hakika!!
“Naitwa Suzi… ni malikia wa nyumba hii samahani we ni nani mwenzangu.” Yule dada alimuuliza Gama kwa sauti nyororo huku amelegeza macho kana kwamba ni mpenzi wake. Gama alifura kwa hasira bila kujibu chochote.
“Wewe ni nani katika ngome hii…. Elewa kwamba kunijibu ni lazima na kufa ni lazima vilevile, namaanisha utanipa jibu na utakufa vilevile.” Sauti ikasisitiza wakati huu ilikuwa ya kibabe. Gama akajaribu kuishughulisha akili yake lakini akajiona yu katika mtego mgumu sana. Aibu iliyoje kukamatika mbele ya mwanamke.
“Wewe ni nani kijana shupavu mwenye mabaka kama chura…” yule msichana akahoji huku akipuliza hewani moshi wa sigara aliyokuwa akivuta. Na ghafla tena akatokwa na teke la haja, Gama akajaribu kupangua kwa mikono lakini akatupwa mbali akaangukia tumbo.
Kimyakimya akakiri kuwa yule dada alikuwa amefuzu mafunzo fulani ambayo yaliondoka na hali yake ya usichana kiujasiri na kuvikwa uanaume wa shoka.
“Nimesema kujibu ni lazima na kufa lazima ufe…”
“Nyinyi ni nani wapumbavu nyinyi na mnajishughulisha na nini hapa…. Waoga wakubwa nyie manalinda kwa mbwa na bado mnatumia risasi“ Gama akamkejeli yule dada ili kumtia hasira aje kwa pupa. Dada yule aliyejiita Suzi wala hakubabaika.
Kama kawaida yake akaiendekeza tabia yake ya uviziaji. Akaichukua sigara yake na kufanya kama anaisigina chini kwa sekunde moja na nukta iliyofuata akapaa mzimamzima, Gama akajaribu kukwepa lakini mapigo mawili ya nguvu yalikuwa yamemuingia usoni. Na alipokaa sawa na kutaka kurusha ngumi akakutana na ubaridi katika pua yake.
Bunduki!!!
“Sogea sentimita moja mbele, nyuma, pembeni ama popote pale na niisambaze pua yako vipande vipande dume la mbegu…” alikoroma yule msichana. Na hapo yule mwanamke mwembamba mrefu akaikoki vyema bunduki yake, hakuonekana kuwa kwenye mzaha hata kidogo.
Gama akaingiwa na uoga, akayafumba macho yake kuusubiria mlio wa risasi iwapo atausikia basi atakuwa yu hai bado na endapo hatausikia atakuwa amezimishwa!!
Badala ya kusikia mlio wa risasi, mara ghafla alishangaa anaangukiwa na yule msichana huku bunduki ikiruka mbali. Gama hakutaka kujiuliza kulikoni badala yake akatokwa na ngumi kali kupita zote alizowahi kuzipiga. Ilikuwa ni ngumi na kutoka katika kifo kuja tena kwenye uhai.
Akaipenyeza katika kitovu cha yule dada, Suzi akarushwa pembeni na kuanza kulia kama mtoto mdogo.
Gama licha ya kumfyatua yule dada pigo kali ambalo lilimaanisha kuwa hawezi kuamka ndani ya muda mfupi, bado hakujua ni kitu gani kilijiri hadi yule dada akaanguka ghafla na kupoteza uelekeo.
Gama akatulia na kuangaza huku na kule, mara akaisikia sauti iliyomshtua na kumweka katika mshangao wa muda mrefu kiasi.
“KOMBOLELA YAKUBU GAMA…”
Na hapo Gama akageuka akakutana ana kwa ana na mwanamke wa shoka akiwa anatabasamu.
Alikuwa ni mama lao!!
Gama hakuamini macho yake.
“Wakati wangu wa kupumzika bado sana. Naipenda sana kombolela, na ndo kama hivi nimebutua nimekuokoa…” Mama lao akamweleza Gama, na bila kupoteza muda wakamchukua yule dada ambaye alikuwa katika maumivu makali na kumtembezea kipigo cha haja!
Akaropoka kila kitu, Gama hakutaka kufanya makosa kama ambayo adui yake aliyafanya. Mara moja akaigeuza shingo yake na kuuondoa uhai wake.
Na hapo mama lao akaitambua ile sura kuwa ni ya yule dada ambaye alinunua mboga zote za majani siku ambayo mama lao kwa mara ya kwanza aliweza kuingia ndani ya kasri ile.
Gama alitambaa tena kiubavu ubavu bunduki yake mkononi akaufikia mlango, damu ilikuwa imechemka haswa. Maana alijiona ni mzuka uliofufuka ghafla.
Akaruka teke moja matata, mlango ukatikisika na kulegea. Aliporudi nyuma ili aruke teke jingine, mama lao alijirusha na kutumia makalio yake akaumalizia mlango.
Gama akajikuta anacheka mwenyewe!
Mama lao akajibu kwa tabasamu hafifu.
Ukimya ulikuwa mkubwa ndani ya nyumba ile, ni kama hapakuwa na mtu yeyote yule. Lakini mama lao alisisitiza kuwa mle ndani lazima kuna watu maana mboga alizonunua yule dada zilikuwa nyingi sana kiasi cha kuweza kutumiwa na walaji zaidi ya ishirini ama thelathini kwa kulizika kabisa.
Gama alikuwa amempigia saluti yule mama. Hivyo aliyaamini aliyokuwa akielezwa.
Msako ukaendelea kwa tahadhari kubwa sana, vyumba vya ile nyumba havikuonekana, ilionekana kama ghala tu.
Zaidi ya sebule ndogo ambayo chini palikuwa na magodoro. Hakuna kitu kingine cha ziada kilichoonekana.
Gama alianza kukata tamaa kuwa huenda wamecheza kombolela sehemu isiyokuwa sahihi na mtu aliyejificha hayupo eneo lile.
Mama lao naye akaingiwa unyonge juu ya kilichokuwa kinatokea pale.
“Inawezekana hakuna jipya humu!” Gama akazungumza na mama lao.
Lakini badala ya kupata jibu alishtushwa kuona mama lao akirusha na kutua kwenye kochi kubwa huku akitokwa na kelele ya uoga.
Bunduki ikakakamaa katika mkono wake tayari kwa pambano lolote.
Mara kabla hajafikiria kufyatua na yeye alivamiwa.
Akajikuta akikabiliana yule mbwa mkubwa ambaye awali alikuwa amezimia baada ya kupokea pigo tata kutoka kwa Gama.
Safari hii mbwa alikuwa na hasira zaidi.
Akawa juu ya mwili wa Gama huku akijiangaa kumng’ata, Gama naye akawa ameikamata shingo ya yule mbwa. Ikawa ni vita ya nguvu kwa nguvu.
Gama alimuhesabia sekunde yule mbwa kisha kwa ghafla akamrusha ukutani.
Ebwana ee!! Mbwa kwa uzito wake akaanguka na kubomoa ule ukuta wa ajabu.
Ebo! Haukuwa ukuta! Ilikuwa ni kipande cha mbao nyepesi kabisa kilichokuwa na rangi kama ya ukuta na baada ya kufunuka pale mara zikasikika sauti za watu zikinung’unika.
Bahati iliyoje kugundua hilo dakika za mwisho kabisa.
Sasa Gama alikuwa amesisimka zaidi, yule mbwa alivyojaribu kumvamia, mama lao alijikuta akipiga kelele kwa kudhania kuwa Gama ni mtu wa kawaida na atajeruhiwa na lile jibwa.
Gama badala ya kumtazama mbwa, ghafla akampa mgongo na kisha akaikunja ngumi yake katika nukta chache na kisha ghafla akageuka na kuituma ngumi ile katika mbavu za yule mbwa.
Mbwa akatokwa na kilio cha maumivu huku akijikunja pale chini.
Gama akammalizia kwa teke kali lililoondoka na uhai wake.
Mama lao akabaki nje wakati Gama akiingia katika kile chumba ambacho ,kilikuwa kimefichwa kama ukuta.
Hakika ya wanadamu waachie wanadamu!
Ni nani angeweza kugundua siri ile kirahisi!
Chumba katika pembe za ukuta??
Gama alimwachia mama lao bunduki, na kutaka kumpa maelekezo jinsi ya kutumia. Mama lao akatabasamu na kumpiga mgongoni Gama.
“Naitambua vyema SMG ni kama unataka kunifundisha kupika mtoto wa kiume wewe…”
Gama akaduwaa akazama mle ndani!
Tochi ikamuongoza hadi akazifikia nondo zilizokuwa zikiunda chumba kile.
“Nisamehe sitarudia naapa, nionee huruma mkuu nilikosea na sitadiriki tena, mnanionea jamani mimi sihusiki!” hizi ni sauti zilizosikika wake kwa waume zikilalamika.
Gama akamurika huku na kule hakuuona funguo!
Akawamurika watu waliokuwa wa,kilalamika.
Mungu wangu!! Akashtuka walikuwa ni watu wengi afya zao zikiwa zimedhoofu, wanaume kwa wanawake walikuwa wamechanganywa pamoja.
“Naomba utulivu wenu, msipige kelele. Nipo hapa kuwaokoa… naomba muwe kimya ili wote mtoke salama humu.
“Commando Gama wa Gama….” Mara akaisikia sauti ikimtambua. Akamulika tochi akamuona mwanaume amejiinamia chini, mara baada ya kumulikwa akaunyanyua uso wake ghafla.
LAHAULA!! Gama hakuamini macho yake!!
Alikuwa ni John Masele, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na nje.
“Nilijua wapo vijana wanaoweza kupigania taifa lao. Wewe ni mmoja wapo.” Alijivuta kwa kutumia magoti, hakuwa anaweza kutembea na mikono yake ilikuwa dhaifu.
Gama hakutaka kupoteza muda akajipekua na kutoka na bunduki nyingine. Akawasihi wasipige kelele anafyatua lile kufuli.
Na pale akailenga shabaha lakini kabla hajafyatua akshtushwa na mlio wa risasi. Akasita na kukimbia hadi mlangoni huku bunduki yake ikiwa imara mkononi mwake.
Akamkuta mama lao akiwa anachokonoa meno yake kwa kijiti huku wasiwasi ukiwa mbali naye kabisa.
“Nini kimetokea..” aliuliza huku akiwa na wasiwasi.
“Hili jibwa lilijipindua kama linataka kusimama, na mimi nikajaribu kama risasi zipo…maana hukawii kunipa toi wewe.. wanaume mna maana basi..”
Gama akatikisa kichwa na kukiri kuwa yule mwanamke sio tu alikuwa na roho ya paka na kifua cha chuma kama alivyoagiza. Lakini huyu alikuwa zaidi ya alivyodhani.
Gama akatabasamu kisha akarejea na kufyatua lile kufuli! Geti dogo la chuma likafunguka.
“Gama.. mimi sitaweza kwenda popote pale, nitakuwa mzigo kwenu. Wamenipiga vibaya mno.. mno yaani, ninachokuomba kama hujaonana na yule mwandishi wa kuitwa Sam.. tafadhali kaonane naye ana mengi nimemwachia nenda akakupatie na uyafanyie kazi. Hii nchi imeoza, watawala wanatugeuza sisi watumwa wao. Pambane muupate uhuru wenu tena.” Alizungumza John Masele huku akitweta.
Gama hakuridhika na msimamo wa yule bwana lakini Masele alisisitiza vilevile.
Wale mateka wengine wapatao kumi wakatoka mmoja baada ya mwingine. Japokuwa palikuwa na giza lakini Gama alifanikiwa kukutana na sura moja ambayo haikuwa ngeni machoni pake.
Vijishimo vidogo katika mashavu yake vilimtambulisha upesi sana kwa Gama na hapa akaupigia mstari upelelezi wa jemedari mama lao. Licha ya binti yule kuwa amechakaa na kukondeana haswa lakini sura yake haikupotea.
Yule binti alikuwa ni Lilian, mpenzi wa mwisho kabisa wa Steven Marashi kabla hajapoteza uhai. Na ni huyu pekee aliyekuwa na jibu lililonyooka juu ya kifo cha Steven Marashi.
Gama akapata nguvu zaidi baada ya kumwona na hapo akaukumbuka mpangilio wa hisabati za shule ya msingi.
SWALI, KAZI, JIBU!!
Na hapo swali lilikuwa limetolewa, kazi imefanyika na lilibakia jibu tu kutoka kwa Lilian..
Mtihani ukawa mmoja tu namna ya kuwatoa watu wale nje ya geti lile salama bin salmin.
Wakati huo ilikuwa yapata saa nane usiku, Magomeni ilikuwa kimya kabisa kasoro sehemu moja tu. Lango la jiji huu ukumbi ilisikika mirindimo ya mziki wa pwani ikivuma.
Funguo ya geti ilisakwa bila mafanikio.
Gama alimwendea yule kijana ambaye alikuwa yu hai bado, yule ambaye alikuwa wa kwanza kukutana na pigo lake baada ya kuinama kumtazama mbwa aliyeanguka chini.
Gama alimmurika na kugundua bado yu hai. Akamuuliza maswali mawili matatu lakini yule kijana akaleta roho ngumu ya huko alipofundishwa kuwa na roho ngumu.
Gama aliendelea kuuliza kwa kulazimisha, yule bwana hakuwa tayari kusema. Wakati Gama akitafuta namna ya kumbana ili aweze kusema kumbe mama lao yeye alishawaza kabla yake. Akajisogeza mwanamke yule kama asiyekuwa na wazo lolote kichwani mwake huku akiyatikisa maungo yake kufuatisha mziki wa mwambao uliokuwa ukirindima. Mara ghafla kama amesetiwa akamfikia yule mwanaume pale chini. Akaupeleka mkono wake katika sehemu zake za siri akazikamata kisha akaanza kumnyanyua kuja juu.
Ebwana eeh! Jamaa akapiga yowe kubwa mno. Yowe lililomshtua hadi Gama mwenyewe. Halafu kwa kutumia ishara mama lao akamuuliza ni wapi zipo funguo.
Akalegeza kidogo mkono, jamaa akaelekeza mahali zilipo kiustadi kabisa. Gama akazichukua funguo na kuliendea geti na kufungua. Geti likaachia, wakati analifungua akamwona yule mlinzi mlevi akitembea huku anayumbayumba. Hakujua linaloendelea eneo lile.
Mama lao hakusubiri kila kitu kifanywe na mwanaume. Akaingia garini, akafungua milango na kuwaruhusu wale mateka wote kuzama garini. Wakaingia wote kwa kubanana na mlango ukafungwa.
Kabla ya kuondoka Gama alirejea tena kule chumbani na kumsihi tena John Masele waondoke wote lakini mzee alikataa, badala yake akamuita Gama na kumnong’oneza.
Gama akaelewa akatoweka!!
****