MATATA MATATANI
MZEE MATATA kama ilivyokuwa kawaida yake, kila mambo yanapoharibika alikuwa anajipooza hasira zake kwa kumwadhibu Tina ambaye alikuwa mateka wake. Alikuwa akifanya hivyo kwa kuamini kuwa mchumba wa Tina ndiye aliyekuwa nyuma ya haya yote.
Na hata baada ya kuuwawa wazungu wanne ambapo mzee Matata aliamini kuwa mkono wa Sam unahusika, alikivamia chumba cha Tina kwa lengo la kumwadhibu. Na adhabu aliyoipanga siku ile ilikuwa kubwa zaidi, alipanga kuuondoa uhai wa Tina.
Lakini kabla ya kuuondoa uhai wa binti yule aliwaza kuzimalizia hasira zake kwa kumbaka na baada ya hapo amuue kwa namna yoyote ile.
Kitu ambacho alisahau ni kwamba siku ile alivyoitwa na raisi ghafla huku akiwa amechanganywa na simu kutoka uholanzi, aliondoka na kusahau kufunga kile chumba.
Na ni upenyo huo ambao Tina aliutumia vyema ili aweze kujikomboa. Nafasi ambayo ilibadili kila kitu.
Mzee Matata alifika na mkanda na kuanza kumchapa Tina huku akimuuliza maswali yasiyojibika.
Kisha akamuamuru avue nguo zake zote.
Amri hii ilimtisha Tina na kuona kama mpango wake unataka kuharibika. Hakuwa tayari kuvua nguo kirahisi namna ile kama Matata alivyotaka. Na hapo akaamua kucheza na hisia za Matata.
Mwanamke mwanamke tu!
Tina akaitoa nguo yake ya juu.
Matiti yakabaki kumtazama mzee Matata. Tina akalitazama koo ya mzee Matata akaliona linapanda juu na kushuka.
Mate ya tamaa yamemezwa! Akajisemea huku moyo wake ukitabasamu kwa jinsi mzungu yule alivyokuwa akienda kuuvaa mkenge.
Hapohapo Tina akamvamia mzee Matata, kwa maksudi kabisa akayaruhusu matiti yake kukichoma kifua wazi cha yule mzee.
Mzee Matata akatokwa na neno tamu la kimahaba kwa lugha ya kiingereza. Wakati mzee Matata anaanza kupagawa, Tina alikuwa kwenye akili zake timamu kabisa na alitambua kuwa zile zilikuwa dakika zake za mwisho za kujitetea.
“Mkeo hawezi kuja kuchungulia jamani…” Tina akahoji kwa sauti nyororo katika masikio ya mzee Matata.
Mzee yule akacheka kama bwege!
“Nipo na mlinzi tu hapa, yupo getini huko… vua basi mpenzi… yaani ukinipa vizuri nakuachia uondoke…” Matata akabubujikwa na maneno, joto la mtoto wa kingoni lilikuwa limeondoka na utimamu wake.
Naam kama alivyoamriwa kuvua nguo, Tina akaingiza mkono katika nguo yake ya ndani, akaibetua kama anayetaka kuivua, wakati huo mzee Matata akiwa amejikita katika kulambalamba matiti ya Tina.
Mkono wa kuume wa Tina ukaendelea kuhangaika katika chupi, wakati ule mwingine ukiwa unampapasa na kumfinyafinya mzee Matata.
Mkono wa kuume ukaibuka na kisu kidogo ambacho Tina alikipata ndani ya ile nyumba siku ambayo mlango ulisahauliwa wazi.
“Mzee Matata… I love you sana baby wangu!” Tina akamdhihaki mzee Matata, kisha akauzamisha ulimi wake katika sikio baridi la mzee Matata.
Pumzi za yule mzee zikapanda juu, wakati zinashuka Tina naye akaushusha mkono wake katika tumbo la yule mzee.
Uchovu wa tamaa za kimwili, na makali ya kisu kikali, mzee Matata akashindwa kupiga kelele akaanguka chini. Tina akamrukia na kuzamisha tena na tena katika tumbo lile kubwa. Damu ikamrukia usoni lakini hakujali.
Alikuwa na roho ya kinyama!
Naam! Na alikuwa sahihi, maana hata yeye alitendewa unyama haswa.
Mzee yule akatokwa na kelele hafifu kisha akaanguka chini huku akifanya jitihada za kuzuia utumbo wake usimwagike chini.
Tina alibaki akiwa amekishikilia kisu kile huku akingoja yeyote yule atakayejitokeza mbele yake na amwangamize.
Hakuna aliyejitokeza!!
Akiwa vilevile alitoka hadi nje, akamwona mlinzi getini akiwa ameshika kirungu tu. Muonekano wa Tina ulikuwa kama mzimu tu, alikuwa ametapakaa damu na nywele zake zilikuwa zimetimka hovyo.
Na kwa jinsia livyokuwa amekonda, mlinzi alikuwa na haki ya kukimbia.
Tina akatoka mbio huku akikitupa kile kisu, barabara nzima alionekana kama kichaa kwa jinsi alivyokuwa. Lakini ni nani wa kujali jijini Dar kila mtu akaendelea na mihangaiko yake.
Tina akazidi kuambaa na kupotelea mbali huku mapigo yake ya moyo yakiwa yanadunda sana. Kadri alivyozidi kukimbia alikuwa akizidi kuona watu wakipungua, hilo lilimfurahisha sana lakini hakujua ni wapi anapoelekea ikiwa ni salama ama la!
Aliyakumbuka yote aliyowahi kushuhudia katika jumba lile.
Aliwahi kumwona raisi wa nchi katika jumba lile. Hili nd’o jambo lililomsisimua zaidi. Na pia kumfanya ahofie kukutana na polisi. Maana ikiwa raisi alikuwa akifika katika jumba lile basi bila shaka anafurahia vitendo vilivyokuwa vikifanyika pale ndani.
Kwa kukamatwa na polisi angeishia kurejeshwa kulekule alipokuwa ametoroka.
Alipenya asijue anapoelekea hadi pale aliposikia akiamrishwa kusimama. Mkojo ukataka kumtoka Tina.
Akatamani kukimbia lakini akahofia kuzua jambo jingie, kwanza mwili wake ulikuwa dhaifu bado. Na kitendo cha kukimbia ilikuwa kuhalalisha kuwa yeye ni mkosefu.
___
UOGA ulimvaa IGP baada ya kuikaribia nyumba ya mzee mazoea ya kumtetemekea mzee huyu yalikuwa yanamtafuna. Ilikuwa heri kuikaribia ikulu kuliko kulikaribia jumba lile la tajiri yule kutoka magharibi.
IGP alijiuliza ataanza kumuuliza maswali gani ili walau aweze kuupata mwanga juu ya nini kinachoendelea kati yake na raisi wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
Uoga wake ulienda kando baada ya kukumbuka kuwa alitakiwa kuujua ukweli ili kuuokoa uhai wa mtoto wake pekee wa kike ambaye kutoweka kwake kulikuwa kumeipoteza amani ndani ya nyumba yake.
Wakati akiwaza haya IGP alimtilia maanani msichana aliyekuwa akitembea upesiupesi huku akionekana mwenye hofu. IGP alitaka kujishughulisha naye lakini akatambua kuwa hilo halikuwa la msingi sana kwake kwa wakati ule badala yake alitakiwa kutilia maanani upelelezi wake.
Akatelemka garini na kulifikia geti ambalo nusu lilikuwa wazi na nusu likiwa limefungwa.
Akalisukuma huku akitarajia kukutana na mlinzi ambaye atamweleza ikiwa mzee Matata yupo ndani ama la kwa sababu awali alikuwa amempigia simu na haikupokelewa.
Pale mahali anapoketi mlinzi hakukuta mtu! Akatembeza macho yake huku na kule bado hakuambulia kitu, akashusha pumzi na kutazama chini. Na ghafla akayakodoa macho yake katika marumaru iliyokuwa imetapakaa katika ua wa nyumba ile.
Akainama na kutazama kwa makini. Akajihakikishia kuwa ile ilikuwa ni damu. Akajaribu kutazama ni wapi ilikuwa imetokea, akayaona madoa kadhaa kuelekea ama kutokea kwenye nyumba ya mzee Matata.
IGP akaichomoa bastola yake kiunoni upesi na kuishika kwa umakini kabisa kisha akanyata kufuata alama zile zilizoachwa na damu.
Akafika hadi mlangoni, kabla ya kuingia akachukua simu yake ya upepo na kutoa taarifa za hali ya hatari kwenye nyumba anayoishi mzee Matata.
Kisha akaupiga teke mlango uliokuwa wazi, akataraji kukutana na kiumbe hai lakini haikuwa hivyo, akazidi kuifuatilia ile damu.
Naam! Akakifikia chumba ambacho hakikuwa na michirizi bali dimbwi la damu.
Na aliyekuwa anaogelea katika dimbwi lile alikuwa mzee Matata ambaye ulimi ulikuwa umemtoka nje.
IGP akapiga simu ya dharula na kuhimiza kikosi cha huduma ya kwanza kifike upesi. Na hata kabla hajakata simu alizisikia gari za polisi zikifunga breki nje ya geti. Akakumbuka kuwa alipiga simu kabla hajaingia ndani kuhitaji msaada wa dharula.
Mwili wa Matata ukachukuliwa na kupelekwa hospitali upesi huku ile nyumba ikiwekewa ulinzi mkali na upelelezi ukiwa unashika hatamu juu ya nani aliyeshiriki katika tendo lile.
IGP alikuwa amepagawa zaidi kwa sababu hakuwa amefanikisha kusudi lake la kumtambua mzee Matata kiundani hasahasa mahusiano yake na raisi wa nchi. Kitu ambacho kilimaanisha alikuwa anamsogeza mwanaye mpenzi hatua moja zaidi katika umauti. Hakujua atajitetea vipi ili aeleweke na kupewa muda zaidi wa kuutafuta ukweli.
Hofu yake ikamtisha mkewe na mdogo wake wa kike ambaye alikuwa akiishi nyumbani kwake.
Akaanza mkewe kilio cha kwikwi, mdogo wake naye akafuatia. Kisha kikawa kilio kikubwa. Wakawa wanaomboleza kifo cha Suzan.
IGP alijaribu kuwakanya lakini hakuweza kuzimisha kilio chao, simu zikapigwa kwa ndugu na jamaa. Ni kama walikuwa wanaalikwa pale ili kusaidia kupaza sauti za vilio.
Mkewe akaenda mbali zaidi na kumpigia simu raisi wa nchi ambaye walikuwa na mawasiliano ya karibu. Akamweleza kuwa Suzan amekufa lakini IGP hataki kusema ukweli kwa sababu anamjua mtekaji wa mwanaye.
IGP alichukizwa na tabia ya mkewe ya kutokuwa mvumilivu, lakini kwa hali aliyokuwanayo asingeweza kumrekebisha.
Akiwa yu chumbani mara simu yake ikaita, akatambua moja kwa moja kuwa atakuwa ni raisi anataka kupata uhakika iwapo ni kweli maneno aliyoelezwa na mke wake. IGP alijifikiria sana maswali ya mitego atakayokutana nayo huku akilikumbuka na onyo la Sam kuwa asije akathubutu kumshirikisha raisi juu ya jambo lile. Akaipuuzia simu ile hadi ikakatika.
IGP akataka kuizimisha simu yake lakini akahofia kuzua jambo jingine kubwa kuliko hili ambalo lilikuwa linatoke.
Simu yake ikaita tena.
Akaipokea kwa utulivu huku akijiahidi kuwa hatazungumza lolote la maana na raisi zaidi ya kumwambia kuwa ampe muda.
“IGP…..” akataka kujitambulisha lakini sauti ya upande wa pili ikamkatisha.
“Nakutambua mkuu, tunakuhitaji Makongo jeshini. Kuna tukio linakuhitaji wewe, ni sasa hivi tunakuomba tafadhali. Kijana wetu yupo nje ya nyumba yako unaondoka naye sasa hivi mkuu. Luteni K” Upande wa pili ukazungumza na kisha simu ikakatwa.
IGP akaghafirishwa na amri ile aliyopewa lakini amri za jeshi zote ni sahihi hivyo alijiandaa na kuondoka akiacha kilio nyuma yake huku mkewe akisisitiza kuwa anataka kuiona sura ya mwanaye kwa mara ya mwisho walau aweze kuaga.
IGP hakujibu kitu!
Akatoka nje na kupokelewa na mwanajeshi ambaye alikuwa katika magwanda yake rasmi.
Wakaondoka kwa kutumia gari alilokujanalo yule mwanajeshi.
Punde tu baada ya kuingia ndani ya ile gari, walitokea mafichoni wanajeshi wengine wawili vijana. Wakamshurutisha IGP kuwapatia simu zake zote, akatii bila kuleta ubishi. Na hakuzungumza lolote hadi walipofika Makongo jeshini. Akaingizwa katika chumba ambacho kilikuwa na viti vine, akaamriwa kuketi katika kiti kimojawapo.
LUTENI K :IGP unamfahamu vipi mzee Matata….” Alikumbana na swali kutoka kwa mjeshi aliyeitwa Luteni K.
IGP:Mwekezaji kutoka nje.” Alijibu kwa ufupi.
LUTENI K: Ni hilo tu unalofahamu…”
IGP:Mengine nimeryasikia kama tetesi tu hivyo siwezi kuyatumia kama majibu.”
LUTENI K :Mfano wa hizo tetesi…”
IGP:Mzee Matata ni mojawapo wa mafisadi na mnyonyaji katika nchi hii…”
LUTENI K :”Baada ya kusikia hizo tetesi umewahi kuzifanyia kazi.”
IGP:N’do nilikuwa naanza kufuatilia nikakutana na tukio la Mzee Matata kujeruhiwa ama kujijeruhi bado sijaelewa.”
LUTENI K:Unamfahamu binti anayeitwa Tina…”
IGP:Wapo wengi sijui Tina yupi
Luteni K hakujibu kitu badala yake alitoa amri kisha mbele yake akaletwa binti ambaye awali akiwa ndani ya gari lake wakati akienda kwa mzee Matata alimuona akiwa anahangaika mtaani huku akiwa na hofu.
Alikuwa ni Tina!
“Umewahi kumwona binti huyu…” Luteni akampiga swali IGP, hakika haikuwa mara ya kwanza wala ya pili kumuona. Akakiri kumwona masaa machache kabla ya kushuhudia tukio la kujeruhiwa kwa mzee Matata.
“Nimewahi kumwona… lakini sijui iwapo anaitwa Tina.”
“IGP huyu anaitwa Tina, na anadai anao ushahidi kuwa raisi wa nchi ni msaliti. Na kama yeye ni msaliti basi wewe lazima utakuwa kibaraka wake. Jeshi limekasirika sana, na halijaanza kukasirika sasa hivi, miaka hii mitano ya mwisho ya utawala wenu imekuwa migumu sana kwa jeshi. Chakula ni cha shida na hakuna ile hali ya kujaliwa zaidi ya kutuchukua na kutubwaga nchi zenye vita na kwenda kufia huko kwa kigezo kuwa tunasaidia kurejesha amani. Baada ya kufa familia zetu zinateseka na kuishia kuyalaumu makaburi yetu.
Sasa nimekuita hapa baada ya mawasiliano ya dharula na wenzangu.. tunach….” Kabla hajaendelea simu ya IGP iliyokuwa mikononi mwa mwanajeshi aliyeenda kumchukua iliita.
_____
MAKAMBAKO, NJOMBE.
SAM alikuwa katika mfadhaiko wa hali ya juu sana, alimwona IGP kama mpumbavu asiyejijua kama yeye ni mpumbavu. Kitendo cha kusikia kuwa mzee Matata yu mahututi baada ya kujeruhiwa kwa visu tumboni akiwa nyumbani kwake ilimaanisha kuwa ule ulikuwa mpango madhubuti uliosimamiwa na Raisi ambaye amegundua kuwa mambo yanaenda mrama.
Na angejuaje ikiwa IGP hajamweleza juu yake?
Alijiuliza na hapo akakumbwa na pepo mchafu ambaye awali alimfanya kama utani lakini sasa alimaanisha.
Sam akajifikiria kumuua Suzan kisha ikiwezekana na yeye ajiue akaungane na Tina wake ambaye hadi wakati ule aliamini kuwa amekufa.
Sam akaingia katika nyumba ambayo aliijenga kijijini kwa baba yake, ambayo ndani yake alikuwa amemuhifadhi Suzan. Kabla ya kufanya lolote alichukua pombe kali na kuigida katika kipimo alichoona kimemtosha.
Baada ya hapo akachukua panga ambalo lilikuwa linang’ara kutoka na upya wake.
Nakata kiungo kimoja baada ya kingine, kisha napiga picha nawatumia waandishi… lazima niwatese kama walivyonitesa wao! Alijisemea Sam huku uoga ukiwa mbali naye.
Alitaka kutimiza dhambi ile kisha ajiue lakini alitamani kuisikia sauti ya IGP ikilia kwa uchungu wakati atakapokuwa anamsikiliza mwanaye akilia wakati kiungo kimoja baada ya kingine kikitolewa.
Sam akajiapiza kuwa hatasikiliza uongo wowote kutoka kwa IGP badala yake yupo tayari kukisikiliza kilio chake tu.
Akatoka tena nje akalitazama jua lilivyokuwa linaanz akuchomoza lakini lisiweze kushindana na baridi.
“Nisamehe baba… nakuja kwa Tina wangu…” alizungumza na anga, kisha akajihisi kama amebarikiwa kufanya vile.
Akaingia na kulichukua panga kali katika mkono wake, akamvamia Suzan na kumziba mdomo.
Kisha akamfunga kamba imara kabisa!
Kitu kizuri ni kwamba nyumba ile ilikuwa imejitenga mbali sana kutoka kwa wanakijiji wengine hivyo hakuwa na mashaka yoyote endapo Suzan atapiga kelele.
Baada ya kumfunga vyema, akachukua simu yake na kuiwasha kisha akampigia IGP.
Simu ikaita muda mrefu na hatimaye ikapokelewa.
”Picha za mtoto wako … aah sorry picha za viungo vya mtoto wako nimeamua sitavisambaza Tanzania nzima badala yake nitawatumia waandishi wa habari ili waweze kujaza katika kurasa za mbele za magazeti yao. Na nimekupigia simu hii ili uwe unamsikia mwanao kila hatua yake ya kukaribia umauti, sikupi nafasi ya kuzungumza naye lakini nakupa nafasi ya upendeleo kumsikia akiwa analia kilio cha mwisho… pumbavu mkubwa wewe. Ni shauri lako sasa iwapo utakata simu ama la…..”
Sam hakusubiri IGP ajibu kitu chochote akaiweka ile simu kando, na kisha akalichukua panga lake kali. Akamtazama Suzan kisha akamsogelea na ghafla akaliachia panga kwa kasi kubwa likamfikia.
Suzan akatokwa na yowe kubwa lenye mchanganyiko wa hofu na kila aina ya uchungu.
Sam akamtukania mama yake. Akalinyanyua tena, awali alimpiga kwa kutumia ubapa lakini sasa aliyaweka makali katikati. Akaushika mkono wa yule binti na kuutandaza vyema wakati huo alisikia simu yake IGP akilalamika maneno ambayo hakuyasikia.
Sam akalinyanyua panga ili aweze kufyeka vidole vya Suzan mara akagutushwa na kitu.
Hakuamini macho na masikio yake!
****
IGP alikosa uvumilivu baada ya tamko lile la Sam, alikuwa kama mwehu akamrukia Luten K bila kujua kwa nini amemrukia.
“Anamuua mtoto wangu… luteni nisaidie anamuua.. luteni sina mtoto mwingine wa kike… luteni sijui lolote kuhusu maasi ya raisi. Mimi si kibaraka luteni natii amri za jeshi. Mkubwa hakosei!! Wajua Luteni wajua….” Alilalamika IGP huku akilia kama mtoto na kamasi zikimtoka.
Luteni K alibaki katika mshangao asijue nini cha kufanya. Anamsaidia vipi wakati iliyopo mbele yake ni simu na si mtu.
Alijaribu kumtuliza lakini IGP alikuwa kama mwendawazimu, mara akimbie huku mara ajikune hapa mara pale.
Hakika alikuwa amechanganyikiwa!!
Akiwa na simu yake hana hili wala lile zaidi ya kukisikia kilio cha mtoto wake ambaye alikuwa anaugulia kipigo kutoka kwa Sam.
Mara ghafla alishtuka akikwapuliwa ile simu na binti ambaye haikuwa mara ya kwanza kumuona. Alikuwa ni binti ambaye alimuona akihaha huku na kule barabarani wakati anafika kwa mzee Matata kisha akamchukulia kuwa ni mwendawazimu na kumpuuzia.
Sasa binti yule alikuwa ameishika simu yake huku kila mtu pale ukumbini akimkodolea macho.
“Sam…. Sam kama unanisikia please acha unachotaka kukifanya… kiache na unisikilize mimi Sam…. Saaam!!” alizungumza yule dada kwenye simu kwa sauti ya juu.
MAKAMBAKO, NJOMBE TANZANIA.
Sam akaisikia ile sauti iliyokuwa na maana kubwa kwake, sauti ambayo kwa mara ya mwisho aliisikia ikilalamika kwa wivu kabla hajatoweka na maaskari na hakuwahi kumuona tena. Upesi akasita kile alichokuwa anakifanya, akaikwapua ile simu na kusikiliza kwa makini.
“Tina….. Tina ni wewe mpenzi wangu… Tina nihakikishie kuwa ni wewe… nihakikishie Tina.” Sam alizungumza huku akiwa katika mgawanyiko wa taharuki mbaya.
Na hapo akaisikia sauti kutoka upande wa pili ikijibu. Wakati inajibu wakajikuta wote kwa pamoja wakizungumza.
“Moyo wangu ukatua kwako, nafsi ikakiri kukuhitaji. Nitaziheshimu hisia zako, nitakupa penzi langu lote. Na Mungu atulinde hadi kesho itakapokosa kesho nyingine”
Hakika alikuwa ni Tina na Sam. Maneno hayo hakuyafahamu mtu mwingine bali wawili hawa tu.
Naam! Machozi yaliyotiririka Njombe yakatiririka katika jiji la Dar es salaam pia.
Sam na Tina walibubujikwa machozi ya furaha!
“Naomba usifanye lolote ulilotaka kulifanya…”
“IGP nd’o alikuwa amekuteka?” Sam aliuliza, Tina akakanusha. Na kumsihi afanye hima kurejea jijini Dar es salaam kwani kuna mambo anatakiwa kuyajua upesi sana.
“Kesho nakuja! Nitakuja na Suzan ikiwa tu utaniambia wewe bila kushurutishwa kuwa nije.”
“Sam sijashurutishwa na mtu yeyote. Njoo Dar es salaam.” Tina akasisitiza.
Baada ya hapo simu ikakatwa!
Luteni K akabaki kumshangaa Tina bila kusema chochote. IGP alitamani kusema neno lakini akakosa la kusema mbele ya Tina, akamsogelea na kupiga magoti mbele yake ili amshukuru.
IGP akiwa analia kama mtoto mdogo, Tina akajisikia fadhaa sana. Na yeye machozi yakamtoka, akapiga magoti na kumkumbatia IGP.
KIKOSI KAZI KAMILI.
UWANJA wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Nyerere ulikuwa umetapaa mamia ya watu, kila mmoja akitambua ni jambo gani lililompeleka pale. Wengine kupokea wageni wao na wengine kusafiri lakini wapo pia ambao hawakuwa na kazi bali walienda kuketi na kuvuta hewa safi inayopatikana maeneo yale.
Muda ulizidi kusonga huku hekaheka zikiongezeka na kupungua. Ndege ilipotua pirika ziliongezeka na pia wakati anakaribia kupaa.
Ndege ya shirika la kimataifa ilitua majira ya saa kumi alasiri. Pirika pirika hazikuwa nyingi sana kama ambavyo ilikuwa kwa mashirika ambayo yanafanya safari za ndani pekee.
Abiria waliowasili hawakuwa wengi sana. Hivyo iliwapa wepesi hata watu waliokuja kuwapokea kuwapata kirahisi.
Baada ya muda kidogo alitoka mgeni ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu na makundi matatu pale uwanjani.
Wa kwanza ni wale walioenda kumpokea kwa ajili ya kumfikisha ikulu ambapo alikuwa na mazungumzo na raisi, hawa walikuwa watu watatu na mmoja kati ya hao alikuwa ni kijana kutoka usalama wa taifa.
Kundi la pili lilikuwa jeshi la mtu mmoja tu, huyu hakuwa makini katika macho yake lakini akili yake ilifanya kazi maradufu. Baada ya wageni wale kupokelewa ndipo akatambua kuwa yawezekana mtu anayemuhisi akawa ndiye yule aliyepokelewa.
Huyu alikuwa ni Yakubu Gama, hakuwa akiijua sura ya BvB lakini uwepo kijana kutoka usalama wa taifa ambaye aliwahi kufanya naye kazi kabla hajakumbwa na dhahama na kisha kutangazwa kuwa alipoteza uhai.
Alizifuatilia nyendo za kijana yule hadi pale walipompokea mzungu aliyekuwa amejivika kofia ya pana huku akiwa hana mzigo wowote zaidi ya bahasha ndogo mkononi mwake. Hawakupoteza muda wakatoweka na kuingia katika gari.
Gama hakuwa na papara alingoja waondoke kwanza ndipo aanze kuwafuatilia ili ajue ni wapi wanaelekea na iwapo itabidi aweze kuzusha vurumai na kuupata muafaka. Kitu ambacho aliombea sana kisitokee ni mgeni yule kupelekwa ikulu moja kwa moja. Kwani kwa kufanya vile alijua asingeweza kuipenya ngome na kuingia na hata kama angefanikiwa basi mwisho wake ingekuwa umauti.
Gama aliingia katika gari aliyokuwa amekuja nayo, lakini kabla hajaanza kuwafuatilia aliona kundi jingine ambalo lilikuwa na watu wawili. Walikuwa wakipeana maelekezo fulani ambayo hakuyasikia lakini walikuwa wakinyooshea mkono gari lililokuwa linatoweka.
Gama akatulia kidogo, akatoa sigara yake na kuanza kuvuta akiwategea watu wale waanze kuondoka kwanza.
Walipoingia katika gari yao naye akawasha na kuwafuata kwa tahadhari kubwa huku akiyaruhusu magari mengine mawili yamtangulie ili kuondoa dhahania kuwa anawafungia tela watu wale.
Uwepo wa yule kijana makini wa usalama wa taifa ulimfanya Gama aongeze umakini ili asiweze kushtukiwa.
_____