Riwaya: Hatia

Riwaya: Hatia

john mkamate tena defaooo....mi simpendi na misifa yakeee
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI


Joyce alizidi kukimbia gizani akitafuta mwanga ulipo. Siku hiyo ndio aligundua kuwa alikuwa mgeni sana wa eneo lililoizunguka nyumba hiyo aliyoamini kuwa ni mali ya John Mapulu. Joyce alijikuta akifanya jitihada za kupanda na kushuka katika matuta. Alikuwa katika shamba!!!


Uoga ukazidi nguvu ujasiri, sasa akawa anatapatapa asijue pa kwenda. Akiwa katika mahangaiko hayo ya kutafuta njia ya kutokea alisikia kwa mbali dalili za uwepo wa kiumbe hai eneo lililozunguka, Mbwa!, Paka!! Alijiuliza Joyce ambaye aliwahofia paka kuliko mnyama yoyote maishani mwake. Akiwa katika kunyata nyata alishtuka ghafla, machale yakamcheza akayaheshimu akageuka nyuma, ana kwa ana akakutana na kitu kama mtu si mtu mnyama si mnyama akiwa hoi sana na akiwa anahema juu juu, Joyce alitaka kupiga kelele lakini mikono ikauzidi mdomo ujanja ikawahi kuuziba. Usiseme neno!!!!
Hofu ilizidi kuchukua nafasi macho ya Joyce yalivyokitazama kiumbe kile cha maajabu. Uso wake ulikuwa umevimbiana hovyo hovyo huku ukitawaliwa na mabonge mabonge ya damu hapa na pale. Kwa mtazamo wa haraka kiumbe huyu ni kama alikuwa ametoka kufyonza damu ya kiumbe mwingine na sasa ilikuwa zamu ya Joyce. Miguu ikasahau wajibu wake wa kuubeba mwili, fahamu nazo zikakimbia majukumu yake, Joyce akalegea, giza likatanda akajikuta katika safari nyingine.
Alikuwa amezimia.

*****

Adrian Mhina alikuwa amepanga mikakati na sasa aliamini ilikuwa imepangika. Mikakati ya kulipiza kisasi kwa John Mapulu kwa vitendo kadhaa vya kinyama alivyomtendea zamani na sasa. Kitendo cha kupokonywa mdomoni mpenzi wake wa kwanza (Matha), pili kubakwa kwa mpenzi na mchumba wa sasa Monica, kisha kama hiyo haitoshi suala la kuchezewa mchezo mchafu na kujikuta katika mkono wa dola kwa kesi ya kukutwa na risasi. Mambo hayo yote Adrian aliamini kuwa muhusika alikuwa ni John Mapulu.
Roho ya kisasi ikachukua nafasi, Adrian kwa kutumia pesa za miradi ya baba yake na ya kwake anaamua kulipiza kisasi. Wakati huu alikuwa anajiamini zaidi na hakutegemea kufanya kosa la aina yoyote ile. Huku akimtumia kijana wa mjini Stallone, aliyekuwa maarufu kwa jina la Rambo kutokana na umahiri wake katika mapigano ya ana kwa ana na pia matumizi ya silaha .

Stallone alikuwa akijulikana sana kwa jina lake lakini sio sura yake, ni watu wachache sana waliofanikiwa kuiona sura hii, Adrian alikuwa mmoja kati ya watu hao wachache. Haikuwa mara ya kwanza kufanya kazi na Stallone, kazi ya kwanza ilikuwa kumuadabisha Mark yule kijana ambaye Adrian alikuwa naye siku ile alipokamatwa na risasi katika mkoba wake. Zoezi hilo lilichukua siku tatu, na ukweli kuthibitika kuwa Mark hakuwa akijua lolote juu ya John Mapulu wala risasi zilizokutwa katika mkoba.
Sura ya Stallone pekee ilimshawishi Adrian kutoa pesa iliyohitajika, Stallone alikuwa na misuli kila upande wa mwili wake, kichwa chake cha mviringo kisichokuwa na nywele kilikuwa na majeraha mengi ambayo sasa yalibakiza makovu tu. Hakuwa na dalili ya kutabasamu, na jicho lake lilikuwa tiba tosha kwa watoto wadogo wanaopenda kulia lia.
Adrian aliondoka akiwa na matumaini makubwa sana ya kumkomesha John Mapulu.
Katika kipindi hicho cha kusubiri majibu Adrian alijiweka mbali sana na Matha, alihofia Matha anaweza kutibua mipango yake yote iwapo John atagundua kuwa wanawasiliana hivyo Matha alivyokuwa anapiga simu haikuwa ikipokelewa.
Na baadaye aliamua kubadili namba kwa muda!!!

******

Michael Msombe na Matha walikuwa katika maandalizi ya mwisho kabisa ya kutoroka, hali ilikuwa imezidi kuwa tete. Mimba ya Matha ilikuwa imeanza kuonyesha dalili za waziwazi kuwa muda wowote ule itachungulia. Michael kwa upendo ulioanza kujengeka kwa Matha, kutokana na kumbebea kiumbe tumboni mwake alikubali kwa roho safi kutoroka ili kukaa mbali na John Mapulu. Kukaa mbali na HATIA.

Yalikuwa yamesalia masaa arobaini na nane tu mkakati kabambe wa kutoroka uweze kutimia. Matha alikuwa tayari na pesa za kutosha kuwawezesha kufika jijini Arusha ambapo Matha alimwambia Michael kuna ndugu yake atawapokea huko na kuwahifadhi kwa muda kabla ya kuamua ni wapi wanaelekea.

Michael hakuwa na kipingamizi alikubaliana na Matha. Kichwani alikuwa jasiri sana ujasiri uliotokana na penzi kwa Matha na mtoto.
Usiku huu majira ya saa nane na dakika kadhaa, Michael akiwa katika pumziko kitandani lakini akiwa hajapitiwa na usingizi. Alishtushwa na mlango wake kugongwa kwa nguvu sana, alisimama wima haraka akakitwaa kisu chake akakiweka tayari kisha akaufungua mlango na kumkabili mgongaji.
Akaghairi na kukishusha kile kisu chini baada ya kukabiliana na John Mapulu. John akaunda mfano wa tabasamu kabla ya kuingia chumbani mle bila hodi.
John hakuchelewa kuyaanzisha maongezi. Yalikuwa ni maongezi yaliyotangaza hali ya hatari, hatari kubwa.
"Kuna ----- anatuwinda!!!" alianza kujieleza John huku Michael akimsikiliza, "Ni wale mafala waliomuua Joram, wamevamia anga zangu na kuondoka na watu wangu wawili halafu mmoja wamemuua pale pale na maiti yake wameyaweka katika mlango wa kuingilia…"
"Wapi?? Mbona mi sijaona???" aliuliza kwa hamaki, Michael Msombe.
"Sio hapa ni maskani ya kule Nyasaka niliwahi kukwambia…"
"Kwa hiyo sasa inakuwaje hapa kaka…"
"Wameanzisha…lazima tuyamalize…", "Inatulazimu kuwafunza adabu" alisisitiza John, macho yake yakiwa yanang'aa sana, ikiwa ishara za hasira kali.
Michael akabaki kutetemeka asijue la kufanya, John akaisoma hali hiyo akaongezea neno.
"Wametoroka na Joyce, wale mabwege wanaweza wakamfanyia mambo ya kinyama sana…"
"Joyce yupi tena??..nadhani nitakuwa simjui.."
"Unamfahamu vyema kabisa ni Joyce…..K…Keto…yeah!! Joyce Keto.." Alizungumza kwa kusita sita Mapulu. Michael aliyakodoa macho yake kumtazama John, jina hilo lilikuwa limeanza kusahaulika katika masikio yake, ni jina la msichana aliyemsababishia kuwa hapo alipokuwa, sasa anasikia kuwa na yeye yupo katika kutekwa na wapinzani wa John.
Ilikuwa ngumu sana kuelewa hadi John alivyomsimulia kila kitu kilivyokuwa kuanzia awali mpaka hapo walipofikia lakini neno moja tu ambalo John hakulisema, sio kwa kusahau bali kwa kuhofia urafiki wake na Michael.
Suala la mimba!!!! Mimba ya Joyce Keto!!!!
Somo likamwingia Michael ipasavyo sasa akawa tayari kukamata mtutu wa bunduki kwenda kumkomboa Joyce, msichana pekee aliyeamini kuwa aliwahi kumpenda hadi akapitiliza.
"Lazima nimpate Joyce, nimweleze kuwa nampenda!!!" alijiapiza Michael huku akiagana na John Mapulu.
Suala la kutoroka likaanza kuyeyuka kichwani mwake, kutoroka na Matha ni sawa sawa na kumuua Joyce, Michael hakuwa tayari kushuhudia damu ya Joyce ikimlilia.
"Joyce mmoja alikufa mikononi mwangu sikufanya lolote la kuweza kumwokoa, na huyu wa pili akifa wakati uwezo ninao, ni LAANA!!!" alizidi kujipandisha mori, Michael.

Michael hakuwa kwenye utulivu kabisa baada ya kupewa taarifa hiyo ya kushtukiza na John Mapulu, akiwa amebaki peke yake alikuwa akijiuliza mara mbili mbili. Alitaka asimuamini John na kuamini kuwa huenda ile ni mbinu tu lakini nafsi ilisita maana John alionekana kumjua Joyce vizuri.
Hapana hakuna mbinu hapa!!! Alijihakikishia Msombe kabla simu yake haijaunguruma; akasimama akaiendea. Alikuwa ni Matha anapiga, yalikuwa yamebaki masaa machache kabla ya uamuzi wao wa kutoroka kutimizwa. Michael alijifikiria kuipokea simu ile kwa takribani sekunde thelathini, kisha akaipokea huku akiongea kwa hadhari kubwa sana.
"Michael…Michael…tunatakiwa asubuhi tuondoke…."
"Kwanini?? Mbona tumepunguza masaa Ma…" akajibu kwa wasiwasi huku akisita kumalizia jina la aliyempigia simu, kwa tahadhari ya kusikiwa na John.
"----- ametuundia mbinu, sijui machale yamemcheza!!!", alianza kujieleza Matha kwa utulivu kisha akaendelea, "Anataka tuingie kwenye mapambano fulani hivi, nahisi yatakuwa ya kutengeneza tu!!!" Matha alimaliza tuo ya kwanza na kumsikiliza Michael atasema nini.
"Mh!! We kakwambia lini??" aliuliza Michael kama vile hajui chochote.
"Usiku huu huu, na wewe anaweza kukwambia asubuhi."
"Ma….hebu ngoja asubuhi tutazungumza…." Alisema Michael bila papara.
"Michael asubuhi ni mbali atatuzidi ujanja huyu na tutashindwa kuondoka, Michael pleeeease." Alisihi Matha huku akiwa na dalili ya kulia.
"Hapana naniii…haraka haraka haina baraka, subiri nimsikie kwanza halafu tutajua cha kufanya."
"Michael mpenzi wangu, mtoto Michael mtoto wetu, babangu nielewe tafadhali, atatulaani huyu mtoto, tukiingia kwenye mapambano tutamuua, Michael nakuomba Michael" Matha alizidi kulalamika. Maneno yake yakawa kama yana ncha kali kwa mbele, cha ajabu hayakulishambulia na kulijeruhi sikio badala yake yalienda na kuutekenya moyo wake katika namna ya kushangaza, akajisikia uchungu mkali.
"Tutaongea baadae…" Michael Msombe akajibu bila kuelewa maana halisi kwa Matha juu ya hiyo baadaye kisha akakata simu bila kutilia maanani kilio cha kwikwi kilichosikika na kutoa mwangwi kwenye simu. Michael alizimisha simu yake, mapigo ya moyo yakawa juu sana, alikuwa hoi kimawazo akazihisi dalili zote za kuzimia. Huku Matha analilia kiumbe aliyeko tumboni mwake, huku kuna taarifa kuwa Joyce Keto yupo matatani.
Michael akaibana misuli ya kichwa chake kilichokuwa kinaanza kuuma kisha akajiongoza hadi sebuleni akaliendea jokofu akatoa maji ya kunywa akayagida kiasi cha glasi mbili. Akapata ahueni akajilaza kitandani.
Amsikilize nani na asimsikilize nani, nani mwenye umuhimu kati ya Matha na Joyce, kilio cha nani akisikilize!!!! Michael Msombe matatani.


******
Jopo la Stallone baada ya utafiti wa hali ya juu sasa walikuwa wakimjua vyema John Mapulu, walimtazama kwa jicho la nje kama ----- mmoja aliyekuwa akimsumbua Adrian kwa kuwa tu ni dhaifu zaidi yake. Wafuasi wa Stallone hawakushtuka siku walivyomwona kwa mara ya kwanza.
John Mapulu hakuwa na dalili zozote za kutisha!!!
Baada ya Adrian Mhina kufanya malipo yale yaliyohitajika sasa ni utekelezaji uliokuwa unahitajika.
Jopo la Stallone aliyejulikana zaidi kwa jina la Rambo, lilikuwa limeipanga siku maalum ya kwenda kumchukua John Mapulu na kumuadabisha na kisha kumfikisha mbele ya Adrian Mhina akiwa hai. Kwa udhaifu waliouona kwa John, Rambo hakuwa na haja ya kuandamana na vijana wengi, isingekuwa msaidizi wake wa karibu kulazimisha kwenda naye basi angeenda mwenyewe kumkabili John.
Majira ya usiku wa saa nne bila hadhari kubwa sana, Rambo na mwenzake walikuwa katika geti kubwa la kuingilia nyumbani kwa John Mapulu maeneo ya Nyasaka. Hali ilikuwa shwari sana na tulivu kiasi cha kuwaruhusu ndege warukao angani kuitawala anga watakavyo kwa sauti zao nzuri zisizohitaji ala nyingine kuzipendezesha. Rambo akiwa anajiamini kabisa alitangulia mbele akiwa na silaha yake ndogo ya kisu mkononi huku bunduki ikiwa imehifadhiwa mbali kidogo. Lakini ambapo panafikika kirahisi.
Geti lilikuwa limeegeshwa kidogo tu, Rambo akamtanguliza mwenzake aliyekuwa ameshika bunduki tayari kwa kumpasua yeyote atakayeleta kipingamizi katika zoezi hili.
Walifanikiwa kuingia mpaka ndani, hapakuwa na dalili yoyote ile ya kuwepo mlinzi wala kiumbe hai. Rambo akaichomoa bunduki yake ndogo, msako ukaanza mara moja, ni kule kule walipoanzia ndipo walikifikia chumba kilichokuwa na kiumbe hai akiwa hajitambui. Rambo alimnyanyua juu juu akamtazama, hakuwa ameadhibiwa sana lakini ni kama aliangushwa vibaya, hakuwa anaweza kuongea. Rambo akachukizwa na hali hiyo, akaikamata shingo yake na kuizungusha kisha akamkokota kama gunia akamlaza getini.
Ukafuata msako wa ndani ya nyumba, Rambo alikuwa mwepesi sana akazunguka huku na huko kila chumba, hapakuwa na dalili yoyote ya mtu. Rambo akajisikia hasira kwa mbali, ni kama John Mapulu alikuwa anamcheleweshea muda wa kufanya masuala mengine.
Sasa walikuwa wamesimama nje ya nyumba hiyo karibu na mwili wa aliyekuwa mlinzi.
"Tumsubiri au tuje siku nyingine???" Rambo alimuuliza mshirika wake. Hakupata jibu!!!
Mshirika wake hakuwa na lolote la kujibu, badala yake alihifadhi silaha yake kisha akatoa pakiti ya sigara akachomoa moja na kuchomoa kiberiti akaiwasha. Akauvuta moshi mwingi ndani kisha akaupuliza hewani kwa mara ya kwanza, akauvuta tena na kuupuliza hewani huku akiusindikiza kwa macho. Akaonekana kuufurahia mchezo huu badala ya kuwa makini na nini kilichomleta pale. Rambo naye ambaye hakuwa mtumiaji mzuri wa sigara akawa anautazama ule moshi jinsi unavyopaa hewani katika namna ya kuvutia. Rambo naye akajisahau kuwa yupo eneo ambalo sio la kushangaa shangaa, lakini huenda dharau yao dhidi ya John Mapulu iliwapa viburi. Mshirika akazidi kuvuta sigara kwa juhudi kubwa ili mchezo ule uendelee kuwaburudisha.
Huku zoezi la kutazama ule moshi angani likiendelea, mara jitu kubwa jitu lililokuwa linatisha sana kulitazama, lilikuwa kama limezidiwa na harufu ya ule moshi sasa lilikuwa limelewa ghafla na kuanguka chini kisha kikatoka kishindo cha namna yake. Rambo alikuwa chini, mshirika alipokuwa akijiuliza kulikoni, mara alishtushwa na pigo la kitu kizito katika mbavu zake, akaegemea upande mmoja kama anayeokota kitu ama anayesumbuliwa na kichomi. Kabla hajapata uwezo mzuri wa kusimama wima, alipokea zawadi nyingine tena safari hii ilikuwa katika paji la uso wake, na alipojaribu kufungua macho yake alikutana na yule jamaa ----- ----- waliyemuona siku kadhaa zilizopita sasa alikuwa sio ----- tena, bali tahira maana alikuwa anatabasamu wakati jitu zito likiwa linavuja damu likiwa limeikumbatia ardhi. Yule mshirika akathubutu kufanya kitendo cha haraka kuitoa silaha yake, mara akajisikia kama yupo katika anga safi ya kuvutia halafu baada ya sekunde chache akatua chini katika ile sakafu maumivu makali yakafuatia.
"Amekutuma nani hapa!!"
"Ady…Ady…" ndio neno la mwisho aliloweza kulisikia likitoka kinywani mwake kabla ya kunyamaza milele. John akasonya lakini tayari alikuwa ameupata mwanga.
Kesho yake majira ya mchana vyombo vya habari vikatangaza kukutwa mwili wa aliyekuwa jambazi anayetafutwa siku nyingi, pembezoni mwa ziwa Viktoria ukiwa maiti. Hakuna aliyeamini kuwa Stallone Rambo hatimaye ameuwawa. Kifo cha mshirika wake hakikumgusa mtu yeyote zaidi ya ndugu zake. Hata jina kufahamika kuwa aliitwa Chriss ni baada ya wazazi wake kuomboleza.
Taarifa ya kifo cha Rambo ilimshtua John Mapulu, hakuamini kama alikuwa amepambana na mtu hatari kama yule, japokuwa alikuwa ni mtukutu na jasiri alikuwa anamheshimu sana Rambo japo hawakuwahi kuonana hapo kabla. Sasa alikuwa amemuua.

*****

Adrian naye alizipokea habari hizi akiwa katika gari la baba yake akiwa anaelekea mahali ambapo Rambo alimwahidi kuwa siku hiyo mwili wa John ambao upo hoi kabisa utakuwepo, Adrian alikuwa mwenye furaha sana, katika akili yake alikuwa anaiona taswira ya Matha, alimtazama jinsi atakavyofurahi akimpigia simu siku hiyo baada ya kukaa kimya siku nyingi. Adrian aliamini kuwa kwa onyo atakalompa John hakika hatathubutu kuendelea kuwa na Matha.
"Akileta ubishi mi naua kwani nini bwana!!" Adrian aliongea peke yake.
Baada ya taarifa ile Adrian aliyumba kidogo aipeleke gari mtaloni kabla ya kuiweka sawa akapunguza mwendo na kuegesha pembeni. Habari ile ilisomwa kwa kirefu sana na ilikuwa na hadhi ya kuitwa habari kubwa. Adrian sasa akaisikia njaa ambayo tangu asubuhi ilikuwa ikimsumbua ikitoweka na kutwaliwa na hofu kuu moyoni.
Mungu wangu!!! Kama Rambo alinitaja kuwa ni mimi nilimtuma itakuwaje…au sio John aliyemuua???....eeh!! Mungu saidia asiwe John maana…..Aliwaza Adrian huku akisikia kabisa mapigo yake ya moyo yakiwa juu sana.
Ni siku hiyo aliyotegemea kabisa kuwa Rambo atamletea majibu juu ya John na ilikuwa ni hiyo safari aliyokuwa anaelekea huko kwa Stallone Rambo, sasa anasikia Rambo ni marehemu!!!!!!
Mshtuko!!!!

******

Mzee Keto baada ya kuyamaliza masharti yote aliyopewa na yule mganga wa kienyeji sasa lilikuwa bado sharti moja tu ambalo lilikuwa kuu kabisa. Mzee Keto akiwa anamwamini kabisa mganga huyu maarufu kabisa katika jiji la Dar Es Salaam, sasa alikuwa anaenda kumkomesha mchungaji JK ambaye aliamini kuwa ni yeye aliyemtenda mama yake na Joyce hadi akafikia uamuzi wa kujinyonga.
Jumapili hii ilikuwa zaidi ya jumapili nyingine, waumini walikuwa wengi sana, kulikuwa na wageni kutoka nchi za nje ya bara la Afrika waliokuwa wametembelea kanisa la Jacob Komanya, wageni wengine walikuwa wakitokea nchini Naijeria, nchi ambayo alichukua shahada yake.
Kwaya mbali mbali zilitumbuiza na hatimaye ukaja ule wakati wa maajabu, maajabu ambayo yalikuwa kwa nia moja ya kushawishi waumini kutoa sadaka kubwa na kuwavuta wengi ambao bado walikuwa hawajajiunga na kanisa hilo.
Mchungaji JK, alikuwa anatoa neno akikemea mapepo na sasa alianza kutetemeka.
"Kuna shetani amemuingilia mpendwa mwenzetu…Hatutakubali hata kidogo aondoke hivi hivi, aleluyah!!!....shetani shetani…kwa nini shetani anatutawala kwanini lakini…" aliendelea kulalamika mchungaji JK, wakati huo waumini wengine walikuwa wakinena kwa lugha.
Mzee mmoja naye siku hii hakuwa mgeni hata kidogo. Naye alijumuika kwa bidii zote kunena kwa lugha, alifanana na waumini wengine kwa kila kitu.
"Mungu amenijalia talanta…talanta ya kulihubiri neno lake lakini akaniongezea uwezo wa kumtambua adui yangu, leo kuna shetani anataka kunitoa uhai…mtumishi wa Mungu natakiwa kuuwawa nikiwa katika himaya yangu, nikiwa katika hekalu la bwana, madhabahu yaliyobarikiwa!!!" alizungumza kwa hisia kali huku mkalimali akitafsiri kwenda katika lugha ya kiingereza. Wageni wale walioitambua lugha ya kiingereza wakapatwa na majonzi huku imani yao ikiendelea kuimalika kwa mchungaji huyu anayemiliki kanisa peke yake akiwa na vyeo mbali mbali kikiwemo cha uweka hazina.
Mchungaji JK alizidi kuzungumza kwa kufokafoka mithili ya mpiga debe wa daladala za Dar es salaam, alikuwa akirudia maneno kadhaa kama mtu anayeyakariri, na sasa alikuwa anapiga hatua kulizunguka kanisa.
Mzee Keto akaanza kutetemeka, maneno yale makali ni kama yalikuwa yakisemwa kuelekea kwake, alikuwa anatamani akimbie lakini hakuweza kunyanyua mguu wake kupenya umati huu mkubwa. Ile hatia ya kuingia katika kanisa hilo akiwa na dawa za kienyeji alizoambiwa kuwa zitamkomesha mchungaji JK ikaanza kumshambulia, Hatia ilikuwa inamsuta, akaanza kukiri kuwa mchungaji JK ni mtumishi wa Mungu na kwa vyovyote vile Mungu wake wa kweli atamuumbua mzee Keto hadharani.
Hofu ikazidi na sasa mchungaji JK alizidi kumkaribia mzee Keto, mchungaji alikuwa anavuja jasho, wafuasi wake walikuwa bize wakimfuta kwa kutumia vitambaa vyeupe na vyekundu.
"Nasikia nguvu za giza eneo hili..nasikia nguvu za giza eneo hili….Mungu ni mkubwa Mungu ni mkubwa!!! Nguvu za giza hazina nafasi katika himaya yake!!! Ooooh!!! Haleluyaaah!!" Alinena kwa fujo mchungaji, mzee Keto akajifanya amefumba macho, mikono yake ilikuwa inatetemeka.
"Ni nani alinituma kwa Manyaunyau!!!" alijiuliza huku akiiomba mizimu ya mababu zake imwepushe na aibu iliyo mbele yake.

Umati ukazidi kumfuata kwa macho mchungaji JK wakati akiwa ameweka kituo kidogo jirani na mahali ambapo mzee Keto alikuwa amesimama na waumini wengine.
Mzee Keto aliyakumbuka masharti aliyopewa na mganga Manyaunyau na sasa alikuwa akishuhudia yale aliyoelezwa yakitokea mbele yake mchungaji JK alikuwa pembeni yake.
"Akisogea tu angusha kitambaa chini…pale utakuwa umemaliza kila kitu.." maneno ya mganga yalikuwa yanajirudia rudia katika mfumo wa mwangwi kichwani mwa mzee Keto. Akajivika ujasiri huku akiwa anatetemeka akakichomoa kitambaa na kutaka kukidondosha chini. Ilikuwa ni kama mchungaji JK alikuwa akilisubiri tendo alilotaka kufanya mzee Keto na yeye aweze kugeuka, kile kitendo cha mzee Keto kudondosha kitambaa, kitambaa chekundu akakumbana na macho makali mithili ya Simba jike katika mawindo yalikuwa ni macho mawili ya mchungaji JK. Mzee Keto akaanza kutetemeka akataka kukimbia lakini mlango wa kutokea ulikuwa mbali sana, akafadhaika, sasa mchungaji JK alikuwa anapiga hatua katika namna ya majivuno, kanisa zima lilikuwa kimya, kiatu chake cha bei ghali kilikuwa kinasalimiana na ile ardhi yenye marumaru na kutoa mlio ambao haukuleta bughudha katika masikio ya waumini.
Mzee Keto akazidi kutetemeka na sasa bila ridhaa yake alijikuta anakaa chini.


****


***MICHAEL katika wakati mgumu sana wa kufanya maamuzi aidhaaaa amfuate MATHA na penzi la wizi ama amuokoe JOYCE KETO kutokena na penzi la dhati!!

***MZEE KETO anashangaa dawa zake hzifanyi kazi mbele ya mchungaji huyu....Je? ni kipi kimesababisha iwe hivi...ina maana JK ni mtumishi wa Mungu kweli!!!!!

***ADRIAN katika majuto ya kunzisha vita na JOHN MAPULU!!!

***JOYCE KETO yu wapi???


Wazo Langu Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila


 
Imetulia sana.... leta nyingine
 
Ikipita siku bila hatia sina raha. Asante so casuits
 
Duh maskini Rambo ameenda hivi hivi. Haya adrian kazi kwako ila nitamtext ajiandae John is on the way.
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU


Umati ukazidi kumfuata kwa macho mchungaji JK wakati akiwa ameweka kituo kidogo jirani na mahali ambapo mzee Keto alikuwa amesimama na waumini wengine.
Mzee Keto aliyakumbuka masharti aliyopewa na mganga Manyaunyau na sasa alikuwa akishuhudia yale aliyoelezwa yakitokea mbele yake mchungaji JK alikuwa pembeni yake.
"Akisogea tu angusha kitambaa chini…pale utakuwa umemaliza kila kitu.." maneno ya mganga yalikuwa yanajirudia rudia katika mfumo wa mwangwi kichwani mwa mzee Keto. Akajivika ujasiri huku akiwa anatetemeka akakichomoa kitambaa na kutaka kukidondosha chini. Ilikuwa ni kama mchungaji JK alikuwa akilisubiri tendo alilotaka kufanya mzee Keto na yeye aweze kugeuka, kile kitendo cha mzee Keto kudondosha kitambaa, kitambaa chekundu akakumbana na macho makali mithili ya Simba jike katika mawindo yalikuwa ni macho mawili ya mchungaji JK. Mzee Keto akaanza kutetemeka akataka kukimbia lakini mlango wa kutokea ulikuwa mbali sana, akafadhaika, sasa mchungaji JK alikuwa anapiga hatua katika namna ya majivuno, kanisa zima lilikuwa kimya, kiatu chake cha bei ghali kilikuwa kinasalimiana na ile ardhi yenye marumaru na kutoa mlio ambao haukuleta bughudha katika masikio ya waumini.
Mzee Keto akazidi kutetemeka na sasa bila ridhaa yake alijikuta anakaa chini.
Mchungaji akamfikia mzee Keto. Akaunyanyua mkono wake akauweka katika kichwa cha mzee Keto. Zamani mzee Keto hakuwahi kuwa na imani ya muumini kuguswa kichwani kisha anaangulka chini na kuanza kugaagaa, sasa leo ilikuwa zamu yake kuhakikishiwa kuwa hilo linawezekana. Mkono mmoja wenye nguvu wa JK ulianza kumhangaisha mzee Keto huku na kule, mzee Keto kwa kujitambua kuwa alikuwa na hatia akawa ametulia tuli bila kuleta fujo, waliokuwa wanamsukuma waliongezeka sasa akawa anasukumwa kwa fujo zaidi. Baada ya zoezi la kusukumwa huku sauti zinenazo kwa lugha ambazo hakuzitambua zikiendelea kubwabwaja maneno ambayo hakuelewa maana yake, mara mchungaji JK hakumshika kichwa tena, safari hii alimkamata hadi usoni, bado alikuwa akinena lugha zake kwa kufoka sana.
Taratibu mzee Keto akanza kuandamwa na usingizi mzito, usingizi huu ulileta kero kubwa katika nuru ya mzee Keto, giza likawa kubwa, akatamani kufanya jaribio la mwisho la kujinasua kutoka katika mikono hiyo. Jaribio likashindikana akili ilitoa ushirikiano mdogo lakini viungo vikamsaliti, macho pekee ndio yalijitahidi hadi dakika ya mwisho, lakini baada ya viungo vingine kulala na yenyewe yakalala.
Macho yalivyokuja kufunguka alijikuta katika chumba ambacho kilikuwa na hewa safi kabisa na mbele yake walikuwepo wanaume wanne,
"Haleluya…bwana apewe sifaa!!!" Sauti moja ilisema halafu nyingine zikaanza kunong'ona bila mpangilio. Kila mmoja alikuwa kwenye kunena.
Mbele ya mahali alipokuwa palikuwa na kitu mfano wa nyoka lakini alikuwa hatembei tena, huenda alikufa kwa maradhi aliyojua mwenyewe lakini hakuwa amepondwa kichwa chake. Hali ilivyomrejea vizuri akaelezwa kuwa yule nyoka alikuwa katika mwili wake. Yule nyoka alikuwa ni shetani.
Mzee Keto almanusura aruke kutoka mahali alipokuwa, hakuamini kuwa alikuwa na kiumbe yule ndani yake. Lakini wale wanaume pale ndani ni kama walikuwa kwenye akili yake waliwahi wakamshikilia, mzee Keto akaelezwa kila kitu kuwa shetani alikuwa amemtuma kwa ajili ya kumuangamiza mtumishi wa Mungu. Lakini sasa huyo shetani alikuwa ameangamizwa. Hayupo tena!!!
Mzee Keto hakuwa na la kujibu zaidi ya kuisikia HATIA ikimtia aibu mbele ya wanaume hawa, ile hatia ya kutaka kufanya mauaji alitegemea kinachofuata ni sheria kuuchukua mkondo lakini ilikuwa ajabu mchungaji JK alipomshika mkono akamnyanyua na kumkumbatia kisha akamwambia maneno haya.
"Mungu baba amekusamehe na upo huru tangu sasa….mambo ya kidunia hayana mamlaka juu ya mwili na roho yako…okoka, tubu na umfuate yeye aliyekusamehe…" maneno yale yalipenya na kufanya ubaridi katika moyo wa mzee Keto, kisha yakazaa kitu kama upendo na kuanza kutambaa huku na kule katika mwili wake kwa kasi ya ajabu, laiti kama asingekuwa anamjua Mungu basi angekiri kuwa JK ni Mungu. Mzee Keto akamkumbatia kwa nguvu mchungaji JK.
Tangu siku hiyo akawa mtumishi hai wa kanisa hilo. Akatoa ushuhuda na kuzidi kuwavuta waumini.
Laiti kama angejua kuwa mchungaji JK na Manyaunyau yule mganga jambo lao ni moja, asingekubali kupelekwa na mkondo huu. Mzee Keto hakujua kuwa lile gari aliloliona likitoka kwa kasi kule kwa mganga Manyaunyau lilikuwa limempakiza mchungaji JK ndani yake. Manyaunyau alikuwa katika biashara moja na wachungaji feki wengi jijini Dar es salaam. Aliwapatia habari juu ya watu wanaoenda kuhitaji huduma zake kwa lengo la kuwakomoa watumishi hawa feki, mmoja wao alikuwa ni mzee Keto ambaye aliishia kuambulia aibu kubwa na baadaye kuwa mfuasi.
Mfuasi wa shetani!!!!!
Umaskini ukabisha hodi nyumbani kwa mzee Keto, kila wiki alilazimika kuuza kifaa cha ndani aweze kutoa sadaka kama shukrani kwa mchungaji JK na Mungu wake.
Hakujua kuwa alikuwa anaibiwa!!!!! Alikuwa ni kipofu aliyedhani anajua njia!!

*******

Katika Hospitali ya mkoa ya Bugando jijini Mwanza, madaktari walikuwa bize katika kuokoa maisha ya mgonjwa aliyekuwa amefikishwa hospitali hapo na wananchi. Hali ya mgonjwa huyu ilionekana kuwa mbaya sana tofauti na hali ya mgonjwa mwingine. Alikuwa amepoteza damu na maji mengi mwilini. Dripu zilikuwa zinapishana katika mishipa yake kwa kasi, alikuwa anapumua kwa kutumia mashine. Kwa kuwa tatizo lilikuwa halijajulikana bado aliwekewa dripu za glucose ambazo hazikuonekana kumsaidia kitu, sasa walibadilisha na kumwekea ‘normal saline' hii huwa haizidi chupa mbili kabla ya mgonjwa kurudiwa na fahamu lakini sasa ilikuwa chupa ya tatu ya normal saline huku mipira ikiendelea kutumika katika kumsaidia kupumua kiumbe huyu.
Ni kama alikuwa amekata tamaa ya kuishi tena, uso wake na sehemu nyingine za mwili zilikuwa zimechubuka na kuvimba sana. Alionekana kama kibaka aliyenusurika kifo baada ya kupigwa sana na wananchi. Hakufahamika jina lake mara moja, lakini hivyo hivyo madaktari walilazimika kumshughulikia huku taarifa ikitolewa polisi juu ya tukio hilo.
"Akizinduka yule mwenzake atatusaidia yeye hana majeraha kabisa!!" daktari mmoja aliwaambia wenzake. Wakakubaliana.
Ndani ya masaa mawili punde tu baada ya ile dripu ya glucose kumalizika aliyetegemewa alizinduka, alikuwa na afya njema licha ya kupepesuka huku na kule kama anayetaka kuzimia tena. Hiyo ilikuwa hali ya kawaida sana kwa wagonjwa hivyo alisubiriwa hadi akakaa sawa. Alikuwa imara licha ya kuonekana amelegea. Aliendelea kushangaa shangaa kabla ya kumuuliza muuguzi wa kike aliyekuwa jirani yake juu ya ni wapi alikuwa. Alijibiwa yupo hospitali ya mkoa ya Bugando. Hakuuliza maswali mengi akabaki kama zezeta, kisha akafumba macho na kuvutia kasi ya matukio ya mwisho aliyoyapitia kabla ya kuwa katika hali hiyo.
"Mimi ni nani??"
"Nesi"
"Na huyu??"
"Simjui"
"Unaitwa nani??"
"Joy.."
"Joy nani"
"Naitwa Joyce….Joyce Keto" alijibu maswali yote kwa ufasaha, mwanadada Joyce kuthibitisha kwamba alikuwa anajitambua kweli kweli.
Daftari la maelezo ya mgonjwa lililetwa ili maelezo juu ya Joyce na mwenzake yaweze kuandikwa kwa kumbukumbu iwapo litatokea lolote linalohitaji maelezo yakinifu. Baada ya maelezo kutimia daktari aliondoka akiongozana na nesi na baada ya muda alirejea nesi akiwa peke yake. Joyce akaanzisha mazungumzo ambayo yaliwapelekea kuzungumza juu ya ujio wake pale hospitali.
"Yule uliyekuwanaye ni nani hivi maana ameumizwa huyo.." nesi alimwambia Joyce.
"Hata simjui…" alijibu Joyce.
"Kuna watatu wamekufa basi hapa polisi watatuuliza maswali weee!!" nesi aliendelea kupiga soga na Joyce ambaye hakuwa muongeaji sana bali msikilizaji.
Neno ‘Polisi' likamwingia katika akili yake akaanza kuiona hatari ikimnyemelea. Akavikumbuka vitisho vya John Mapulu, kisha akamkumbuka Michael. Aliamini kuwa Michael alikamatwa kwa kesi ya mauaji na polisi walikuwa wakimsaka yeye (Joyce) kwa ajili ya kusaidia upelelezi. Joyce aliwaogopa askari na usumbufu wao lakini aliiogopa zaidi milango ya gereza.
Mawazo ya kutoroka yakaanza kumjia lakini hakumpa nafasi yule muuguzi kuelewa lolote linalosafiri katika kichwa chake. Muuguzi yule bila kujua kuwa Joyce yupo katika kumdadisi alitoa ushirikiano wa kutosha, ushirikiano uliomwezesha Joyce kukiacha kitanda chake na kutoroka usiku huo.

*****

Asubuhi Matha alikuwa wa kwanza kuikanyaga sebule ya John Mapulu maeneo ya Mecco Mwanza, John aliyekuwa amelala aliamshwa na vishindo vya Matha. Akajiweka sawa kisha akanyata na kumkuta sebuleni. Sasa Michael aliamshwa pia akakaa sawa halafu Bruno akakamilisha idadi.
"Akuanzaye…." John alianzisha maongezi. Hakuna aliyejibu, hakujali kuhusu hilo.
"Tunaenda kwa pamoja kumnyamazisha milele yule -----", "kuna watu yupo nao ni watu hatari kiasi fulani lazima kuwa makini…..kuna watu amewashikilia ni wa msingi sana kwangu siwezi kumwacha hivi hivi…."
"Saa ngapi??" aliuliza kiujasiri Matha.
"Nne usiku wa leo tunamaliza kazi…halafu pia hakuna mtu kwenda kule Nyasaka patakuwa katika hali mbaya" alitoa maelekezo John Mapulu kila mtu akawa anamsikiliza.
Baada ya maelezo Matha alipewa jukumu la kumpa Michael somo la haraka haraka juu ya tukio walilokusudia kulifanya.
Matha aliutumia huo mwanya kumshawishi tena Michael juu ya kutoroka kwao. Lakini kinyume na matarajio yake Michael aliweka ngumu, huku akimtaja John Mapulu kuwa alikuwa msaada wake mkubwa tangu akiwa rumande na amemuhifadhi kwa siku zote bila ubaya wowote.
"Ndo umemlipa kwa kumjaza mimba mpenzi wake eti?." Aliuliza kwa kejeli Matha, hasira zilikuwa zimemzidia kutokana na ubishi wa Michael. Michael aliwahi akamziba mdomo Matha na kumsihi asizungumze maneno kama hayo. Matha akatulia, Michael naye akaanza kuzungumza akamlaghai Matha lakini bado Matha hakuonyesha kukubaliana na Michael.
"Lakini kwani huyo Adrian yeye ana jeshi kubwa kiasi gani??" Michael alimuuliza Matha katika lugha ya maelewano makubwa.
"Adrian ndo nani?"
"Si huyo ambaye John anamwita -----??" Michael akajibu bila wasiwasi, ikawa zamu ya Matha kukaa kimya na kuduwaa bila kumruhusu Michael kugundua hali hiyo. Jina la Adrian likawa limemshtua Matha. Japokuwa majina huwa yanafanana lakini hili jina lilimpeleka moja kwa moja kwa Adrian Mhina mpenzi wake wa kwanza kabisa kabla ya John Mapulu. Japokuwa ni muda mrefu ulikuwa umepita lakini penzi hili halikuweza kusahaulika, na mara ya pili walivyokutana ukubwani ni kama walikuwa wamelianza upya penzi lao. Kukutana kwao ukawa muda muafaka wa wao kuliendeleza penzi lao. Matha kimyakimya akakiri kuwa alifanya makosa makubwa sana kumkimbia Adrian na kuingia katika uhusiano na John Mapulu. Hatia iliyokuwa inamfuata akaamua kuitua kwa kumrudia Adrian kwa usiku mmoja, usiku uliowazaa wawili hawa upya wakalitamani lile penzi walilolipoteza. Matha aliamini kuwa John hakumtendea haki mwanaume mwenzake lakini alibaki kimya hakusema neno, leo hii John anataka kumuondoa duniani Adrian, hapana!!! Alikataa Matha ndani ya moyo wake. huruma ikamwingia alivyoijenga picha ya sura ya upole ya Adrian Mhina ikiwa katika mikono iliyokomaa ya John Mapulu, mikono isiyokuwa na huruma katika kuzigeuza shingo za maadui, mikono iliyozoea damu. Mikono ya mauti!!!
Lile wazo la kutoroka likayeyuka upesi mithili ya barafu ndani ya maji ya moto. Akaisahau ile mimba na mmiliki wake kwa muda akaweka mbele huruma, akajiona ni muhusika wa kumweka Adrian matatani. Hakuwa tayari kusikia Adrian amekutwa ufukweni akiwa amekufa kwa kupigwa risasi. Hakutaka kabisa kumsikia John Mapulu akijitamba kuwa amemuua adui wake kirahisi sana.
Matha akaamua kumtetea Adrian, hakumwambia tena Michael kuhusu kutoroka na pia hakuwa na uwezo wa kumwambia Michael juu ya Adrian Mhina maana aliutambua wivu wa Michael. Matha akatulia tuli akitafakari nini cha kufanya.
Walijikuta wameelekezeana migongo, Michael akiwaza juu ya kumkomboa Joyce Keto kutoka katika mikono ya mtu ambaye John alimwita ----- (Adrian Mhina) huku Matha alikuwa katika kizungumkuti cha kutafakari anamzunguka vipi John Mapulu na Michael Msombe ili aweze kumwokoa Adrian Mhina katika janga hili. Yalikuwa yamebaki masaa machache, wawili hawa walikuwa wamesahau juu ya MIMBA!!!!

******

Wazo la Matha juu ya kutoroka sasa halikuwepo tena, alikuwa katika mtihani mwingine mkubwa mno ambao ulikuja ghafla bila yeye kuutegemea. Alikuwa katika nafasi ya kufanya maamuzi mazito, maamuzi ambayo aidha yanaweza kumweka huru ama kumuingiza katika matatizo mengine mapya. Matha alikitazama kitumbo chake ambacho ni yeye binafsi aliweza kukisikia kikiwa kinaanza kuwa kigumu kigumu katika dalili zote za kiumbe kuanza kukomaa. Matha alifikiria juu ya mambo mengi sana ambayo ameyapitia na hatimaye akafikia katika kuwafikiria John Mapulu na Adrian Mhina.
Matha alizifikiria fadhila alizotendewa na Adrian Mhina enzi hizo za penzi lao la utotoni, akakumbuka jinsi alivyokuwa akimjali na kumsikiliza bila kuwaza juu ya kebehi mbalimbali kutoka kwa jamaa na marafiki. Adrian alikuwa mwema sana kwa Matha na hakika alimpenda kupindukia. Matha alilitambua hilo na sasa lilikuwa likimtesa nafsi yake alijihisi ana hatia ya waziwazi, hatia ya kumsaliti Adrian na kuwa katika mahusiano na John Mapulu licha ya mema yote aliyomtendea wakiwa katika mahusiano ya siri, na sasa baada ya kukutana ukubwani na kukumbushia uhusiano wao Matha akidhani kuwa ni njia mojawapo ya kuifuta ile hatia iliyokuwa inamfuata kwa nyuma kila alipoenda tangu amkimbie Adrian kumbe alikuwa anajiingiza katika hatia kubwa zaidi. Na hii ilikuwa ni roho ya Adrian, roho iliyokuwa katika kila dalili ya kutolewa na jitu baya, jitu lisilokuwa na huruma wala nafasi ya kujiuliza mara mbilimbili iwapo liue ama lisiue.

******

Msichana mrembo wa haja alikuwa peke yake chumbani akiyafikiria mambo kadha wa kadha yaliyomjengea tabasamu hafifu na aina fulani ya mshawasha katika mwili wake, alirusha miguu huku na huko na kukipa tabu kitanda kilichobeba godoro la futi sita kwa tano pamoja na yeye kujikaza ili kisimwangushe. Ni kama kuna kitu alikitegemea muda wowote ule ambacho kingempatia furaha na faraja ya pekee, ndio alikuwa na kila sababu ya kutabasamu hasahasa alipokuwa akivitazama vidole vya mikono yake. Vidole hivi vilitegemea kuongeza mzigo usiokera usiku huo. Mzigo wa pete. Pete ya uchumba!!!
Huyu alikuwa ni Monica hakika furaha aliyokuwanayo aliijua yeye mwenyewe na nafsi yake. Ulikuwa ni usiku wa kipekee alioungojea kwa siku nyingi na sasa ulikuwa umefika!!!! Adrian alikuwa ameamua kumvisha pete ya uchumba zikIwa ni dalili za mwishomwisho za kumuoa.
Feni ya juu aina ya ‘panga boi' ilikuwa inazunguka kwa kasi sana ili kukipa kile chumba hali nzuri ya hewa. Monica hakuutambua msaada wa pangaboi ile hadi ilipoanza kupunguza kasi na kukoma kuzunguka. Monica akawalaani wafanyakazi wote wa shirika hili la umeme akiwemo mama yake mzazi ambaye alikuwa ni muhasibu wala hakuhusika na huu mchezo wa zima washa. Zile laana zikaanza kukosa maana baada ya macho ya Monica kushuhudia nyumba za jirani pakimeremeta vyema.
"Mh!! Mbona tuko ‘line' moja??" alijiuliza kwa sauti ya juu kidogo. Alipogundua kuwa hakuwa na haja sana na huo umeme, akajirudisha kwa kasi kitandani akapokelewa na godoro lililokidhi haja ya kuitwa godoro.
Mawazo juu ya usiku huo wa aina yake yakarudi tena. Monica akiwa amefumba macho akaileta picha ya Adrian akiwa na rafiki zake watano aliowaalika katika tafrija hiyo fupi ya kuvishana pete halafu akawafikiria pia shoga zake aliowaalika, alijua kuwa wataumizwa sana na kitendo hicho cha kuvishwa pete na hilo hasa ndilo lilikuwa lengo lake ‘Kuwakomoa' waliosema kuwa hataolewa na Adrian.
"Watanunaje!!!!!!!" Monica akajikuta akisema kwa sauti ya juu kisha kikafuatia kicheko kikali sana kilichokoma ghafla baada ya kubaini kuwa hakuwa akicheka peke yake. Mbele yake kulikuwa na mfano wa kundi dogo la watu lisilokuwa na habari naye. Kundi hili ni kama lilikuwa likimngojea amalize kwanza kuwaza ndo liombe ruksa ya kuwa pale chumbani.
Monica alitaka kujiaminisha kuwa wale ndo rafiki zake Adrian ambao aliwaalika kwa ajili ya kushiriki naye katika tafrija ya usiku huo. Lakini wageni hadi chumbani kwangu!!! Alijiuliza Monica, na mbona hawajachangamka kabisa.
Hawawezi kuwa wageni hawa!!!! Aliendelea kuwaza na kuwazua.
Jibu lilipokuwa gumu huku akiwa bado kaduwaa, jibu la uhakika lilitolewa. Mmoja kati ya wanaume waliokuwa hapo chumbani akachomoa kitu mfano wa mti uliochongwa vyema. Lakini mbele kilikuwa ni kijicho cha aina yake.
Bunduki!!!.
Monica akaanza kutetemeka, jicho likafunguka hadi hatua ya mwisho. Sura zote zilikuwa katika hali ya ukatili. Dalili ya urafiki haikuwepo kabisa.
"Yupo wapi hawara yako??" sauti kali ya kiume ilimuuliza mwanamama huyu.
"Si…si..siju..i" alijiumauma wakati akijibu swali hilo. Kiganja kilichotua kwa nguvu katika uso wake mweupe kiliacha alama za vidole vitano katika paji la uso wake na kisha kufuatiwa na kilio kikali.
"Shhhh!!!!!!!" Kidole cha shahada katikati ya mdomo wa John mapulu kilimnyamazisha Monica akabaki kulia kwa kwikwi.
"Yupo wapi Adrian….." safari hii John aliuliza kwa utulivu. Monica naye akajaribu kuulazimisha utulivu, lakini bado alikuwa anatetemeka.
"Sijui alipo…ila alisema kuwa atakuja" alijaribu kuzungumza japo kwa kutetemeka.
"Hujui eeh!!" alizungumza kwa sanifu John. Kisha akawaamuru Michael na Bruno kumchukua Monica. Kama walivyoambiwa palepale wakamtwaa mzegamzega na kuanza kutoka naye nje.
"Michael mwache Bruno amchunge huyo we njoo huku" aliamuru John, Michael akatii.
Monica akabaki katika mikono ya Bruno. Michael na John wakaanza kuikagua vyema nyumba kama kuna uwezekano wa mabaki yoyote yanayoweza kuwasaidia kujua wapi Adrian yupo. Hawakupata chochote kile!!!

Kishindo kilichosikika kwa nje kikawawekawawili hawa katika tahadhari kila mmoja akatoka akiwa ameiweka sawa silaha yake.
Kitu kama furushi kilichomoza gizani, Michael akiwa ameitanguliza bunduki yake mbele alikimulika kwa tochi yenye mwangaza hafifu huku akikisogelea. John alikuwa anaelekea upande mwingine.
"John!!" Michael aliita kwa sauti ya chini lakini iliyomfikia John. John hakuitika bali akarejea katika namna ya tahadhari kuu. Alipomfikia Michael alilitazama lile furushi, lilikuwa linapanda juu na kushuka chini. Halikuwa furushi bali alikuwa ni Monica mchumba wa Adrian akiwa amefungwa kamba vyema mikononi.
"Bruno yuko wapi??" John aliuliza swali hilo, lakini aliamini kuwa hatapata jibu lolote kutoka kwa Michael kwani wote walikuwa wametokea ndani na walikuwa wamemwacha Bruno nje.
Monica aliachwa hivyo hivyo akiwa amefungwa kamba. Michael na John wakaanza kumtafuta Bruno.
"John!!!" Michael aliita, safari hii sauti ilikuwa ya juu mno. John akakurupuka kutoka alipokuwa akakimbilia sauti ilipotokea.
Sasa kilikuwa ni kifurushi kingine lakini hiki cha sasa hakikuwa kikipanda na kushuka. Kilikuwa kimetulia tuli, huku kikiwa kina rangirangi nyekundu zisizokuwa rasmi.
Kifurushi hiki kilifanana na jamaa yao na John , aliyeitwa Bruno.
Walipokiita kwa jina hilo hakikuitika wala kutetemeka.
Bruno alikuwa maiti!!!
Kifua chake kilikuwa kimeruhusu risasi kupita katikati yake.
Hofu ikatawala!!! John akapandwa na hasira. Akakitazama kifurushi kilichokwenda kwa jina la Monica. Akaiweka bunduki yake katika kiwambo cha kuzuia sauti.
Akafyatua!!! Monica akaungana na Bruno katika safari hiyo!!!!!
Michael na John wakatoweka. Huku wakiamini kuwa vita ndiyo imeanza.
Kwa miungu yote aliyoiamini Michael alikuwa akiomba Joyce aendelee kuwa salama. John Mapulu yeye alikuwa akimlaani Adrian kwa kuianzisha vita hiyo.

****


***MATHA ameechukua maamuzi magumu ya kupambana na JOHN MAPULU ili amuokoe ADRIAN....MICHAEL hajui lolote juu ya uhusiano wa MATHA na ADRIAN.

***MATHA naye hajui lolote kuhusu JOYCE KETO na MICHAEL.

***MZEE KETO naye amekuwa mfuasi wa JK.

***JOHN MAPULU akiwa na MICHAEL wanashuhudia maiti ya BRUNO......nani amemuua???


Wazo Langu Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 
Leo ijumaa ungeweka na nyingine, manake.....mmh!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom