Riwaya: Hatia

Riwaya: Hatia

RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

Sasa kilikuwa ni kifurushi kingine lakini hiki cha sasa hakikuwa kikipanda na kushuka. Kilikuwa kimetulia tuli, huku kikiwa kina rangirangi nyekundu zisizokuwa rasmi.
Kifurushi hiki kilifanana na jamaa yao na John , aliyeitwa Bruno.
Walipokiita kwa jina hilo hakikuitika wala kutetemeka.
Bruno alikuwa maiti!!!
Kifua chake kilikuwa kimeruhusu risasi kupita katikati yake.
Hofu ikatawala!!! John akapandwa na hasira. Akakitazama kifurushi kilichokwenda kwa jina la Monica. Akaiweka bunduki yake katika kiwambo cha kuzuia sauti.
Akafyatua!!! Monica akaungana na Bruno katika safari hiyo!!!!!
Michael na John wakatoweka. Huku wakiamini kuwa vita ndiyo imeanza.
Kwa miungu yote aliyoiamini Michael alikuwa akiomba Joyce aendelee kuwa salama. John Mapulu yeye alikuwa akimlaani Adrian kwa kuianzisha vita hiyo.

****

Adrian alikuwa kama anayekaribia kuchanganyikiwa, suala la Stallone kupoteza uhai akiwa katika kutekeleza alichomuagiza kulimtia katika hofu kuu. Aliamini alikuwa katika kuwindwa na muuaji, muuaji aliyeihalalisha roho ya Stallone kuingia peponi.
Hata ule mpango wake wa kumvisha pete Monica aliuona kuwa ni batili sasa. Upesi upesi Adrian aliichukua simu yake na kuandika ujumbe mfupi wa kuhairisha shughuli hiyo kisha akautuma kwa wahusika wote.

Baada ya zoezi hilo akaamua kuizima simu yake huku akiweka namba ambayo ni Monica na watu wengine wachache muhimu waliokuwa wanaitambua.
Baada ya hapo aliingia katika mgahawa mmoja akaagiza kinywaji chenye kilevi. Alifanya hivyo kwa kurudia chupa hadi zikafike nne, alikuwa anakunywa kwa mfumo wa kupiga tarumbeta, hakutumia glasi iliyowekwa mbele yake. Mfululizo huu uliendelea hadi alipoanza kuona glasi iliyokuwa mezani ikizaa nyingine na kuwa mbili. Mara miujiza mingine na meza zikawa mbili na hata wahudumu wakaanza kuja wawili wawili kumuhudumia.
Adrian akatabasamu!!!
"We malaya..kuna vyumba hapo." Aliuliza kwa sauti ya kilevi.
"Vipo shilingi elfu kumi na tano!." Alijibu yule mwanamke bila kujali alikuwa ametukan wa kabla ya kuulizwa. Hata kama angekataa kutoa huduma, angekuja mwingine angeitwa jina hilo hilo na angetoa huduma kama kawaida bila kinyongo.
Akili ya Adrian bado ilikuwa na uwezo wa kufanya kazi. Akampatia yule msichana shilingi elfu ishirini kwa ajili ya chumba.
Chumba kikalipiwa, chenchi haikurudishwa.
Ningeitoa wapi kama ningekataa kuitwa malaya??? Alijiuliza yule muhudumu huku akiitia vyema katika pochi yake.
Adrian alikuwa amejiweza kwa dozi ya pombe aliyojipatia kwani alipoingia tu alipitiwa na usingizi murua. Hakukumbuka hata kuvua viatu.
Adrian alipoteza kumbukumbu majira ya saa tano asubuhi na sasa ilikuwa imetimu saa nne usiku, kumbukumbu zikarejea. Masaa kumi na mbili ya kuwa mbali na dunia.

****

Suala la kumshirikisha kila jambo Michael Matha alianza kuliona kuwa ni la kipumbavu. Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu akifikia maamuzi yake ya kimya kimya si Michael wala John aliyepatwa na wasiwasi baada ya Matha kuwaeleza kuwa hataweza kuandama nao kwenda kumuadabisha Adrian.
Michael alisikitika sana kwani alijua ni kipi kinamsumbua Matha. Michael alidhani Matha anasumbuliwa na utata wa mimba yake, lakini haikuwa hivyo wakati huu.
Matha alikuwa katika mgongano wa nafsi yake akijifikiria jinsi ya kumwokoa Adrian katika kifo kisichomuhusu hata kidogo.
Baada ya kuhakikisha kuwa John na timu yake wametoweka, harakaharaka Matha alimpigia simu Adrian. Simu iliita mara ya kwanza haikupokelewa, mara ya pili ikapokelewa.
Sauti ya Adrian ilisikika ikiwa imetawalia na uoga. Matha aliligundua hilo lakini hakumuuliza.
"Adrian mambo vipi mpenzi wangu?" Matha alizungumza kwa utulivu huku akiwa amezibana pumzi zake asiweze kusikika kama anahema kwa kasi.
"Matha...hebu ngoja kidogo nitakupigia baadaye." Alijibu Adrian kisha akakata simu. Matha alitaka kuongezea neno lakini tayari simu ilikuwa imekatwa.
Haraka haraka Matha akabonyeza tena kitufe ili ampigie Adrian.
Hakuwa anapatikana tena na tayari ilikuwa saa tatu usiku!!!!

Matha alichanganyikiwa, alijiuliza ni kipi kinamsibu Adrian huko alipo. Wasiwasi wake ukawa kwamba Adrian anaweza akawa ameingia katika mikono hatari ya John Mapulu.

Mwanaharakati huyu wa kike akaamua kucheza pata potea. Upesiupesi akavaa bukta ngumu na viatu vya michezo. Akabeba pochi yake ambayo kwa wanawake wa kawaida ungeweza kukuta wameweka vipodozi, kanga ya dharula, na simu zao. Lakini Matha hakuwa mwanamke wa kawaida sasa!!! Yeye alikuwa amehifadhi, visu viwili vyenye sumu kali katika ncha ya mbele. Bastola ndogo kabisa na unga unga mweupe usiokuwa kwa matumizi ya kawaida kwa watu wa kawaida.

Kama mwanajeshi kamili aliyefuzu mafunzo kambini, Matha alilifunga geti akatoka nje. Giza lilikuwa nene lakini halikumtisha hata kidogo, ni yeye aliyelitisha giza hilo. Hatua kwa hatua, akakutana na dereva wa pikipiki. Akamsimamisha akapanda. Alivyokaa kwenye kiti, ile pensi yake ikapanda juu zaidi mapaja yakawa nje akafanana na wale machangudoa ambao huo ndio ulikuwa muda wao wa kutoka.
"Wapi hiyo dada!!."
"Isamilo fasta." Alijibu Matha.
"Buku saba ipo hiyo." Matha hakujibu kitu, pikipiki ikawashwa na kuanza kukata upepo kuitafuta Isamilo.
"Niache hapahapa." Matha walipoikaribia nyumba ya Adrian alimsihi mwendesha pikipiki. Naye akatii. Matha akatoa shilingi elfu kumi.
"Nenda tu usijali." Matha alimweleza yule mwenye pikipiki baada ya kumuona akihangaika kusaka chenchi. Dereva akashukuru akapanda pikipiki akatoweka kwa mwendo wa kawaida.

Matha hakupiga hatua yoyote mbele badala yake alitulia tuli na kufanana na mti mkavu usio na matawi. Kuna jambo alikuwa analingojea. Tano...nne....tatu....mbili....puuu!! kilisikika kishindo kidogo, Matha akageuka na kutimua mbio kuelekea kishindo kilipotokea.
Alijuakilichokuwa kinaendelea!!!
Alimkuta yule mwendesha pikipiki akiugombania uhai wake, alikuwa amejikita kumkabili israeli ili asiweze kuondoka na roho yake. Lakini Israeli alikuwa yupo katika kushinda na aliyejua hayo alikuwa ni Matha mtoto wa Mwakipesile. Dereva hakujua kama alitoa shukurani yake ya mwisho duniani. Matha alikuwa ameandaa ile noti ya shilingi elfu kumi kwa ajili ya kuondoa uhai wa dereva huyu. Matha alikuwa na shida na pikipiki. Hakuwa na njia zaidi ya kuua.
Mwendesha pikipiki akaiaga dunia na kuiacha pikipiki yake ikiwa hai.
Matha akatoa ‘glovus' akavaa mikononi. Akainyanyua pikipiki akaufunga mkoba wake kwa nyuma akakaa juu yake. Akaipiga stata ikaitika, akapepea nayo.
Akafunga breki katika baa moja ambayo hadi wakati huo ilikwa haijafungwa bado.
"Samahani babu..aah!! shkamoo." Matha alitoa salamu zake. Mzee aliyekuwa na mvi lakini akionekana kuupenda bado ujana alijibu kinyonge. Huenda hakupenda kusalimiwa.
Matha alimnyenyekea yule mzee ambaye alikuwa ni mlinzi katika baa ile. Akamsihi amlindie pikipiki yake kwa ujira maalumu. Yule mzee akachangamka. Akakubali biashara, Matha akapaki pikipiki yake ya wizi. Akampatia shilingi elfu tano kama kianzio cha biashara. Kisha akatoweka kwa mwendo wa kawaida kama asiyekuwa na haraka, alipofika katika uchochoro akaanza kutimua mbio. Aliupita ule mwili wa mwendesha pikipiki kwa kuuruka kama vile gogo.
Bunduki mkononi, Matha akawa ananyata sasa. Macho yake makali yaliweza kung'amua baadhi ya vitu gizani. Alisubiri kwa muda na sasa alichokingojea alikiona. Alishuhudia, viwiliwili viwili vikiwa katika hali tofauti. Kimoja kilikuwa cha kiume kikiwa wima na kingine cha kike kikiwa katika mateso makali, kilikuwa kimefungwa kamba.
Baadaye kidogo kiwiliwili cha kiume kikaanza kunyata kuelekea gizani, Matha naye alianza kunyata kwa kutembelea vidole. Hakuweza kusikika. Alipoweza kukiona kiwiliwili kile tena sasa kilikuwa kimemkaba koo mwanaume. Huyu alikuwa ni Adrian na kiwiliwili kiliitwa Bruno. Mwanga hafifu ulimuwezesha kutambua hilo.
Matha alishukuru kwa kumkuta Adrian akiwa hai, sakata la kukabwa na Bruno hata halikumshtua. Aliiweka bastola yake sawasawa, huku akihakikisha kuwa ipo katika kiwambo cha kuzuia sauti.
Matha alitabasamu baada ya kumwona Adrian akiwa ametulia tuli kwahofu. Ni hivyo alitaka iwe, ili aweze kuipata shabaha yake vyema.
Bastola ilinyanyuliwa, kisha ikakohoa kimyakimya, kama vile gunia Bruno akatua chini. Akiwa hana taarifa yoyote Adrian, katika taharuki kubwa alipitiwa kwa kasi kama vile mwewe anavyonyakua kifaranga, alikuwa amezibwa mdomo huku akilazimishwa kukimbia.
Hakuamini kwa yule ni Matha!!!
Haukuwa muda wa kuulizana maswali wala kutoa majibu. Adrian alilazimika kufuata amri.
Matha alimsihi Adrian amsubiri mahali kwa dakika mbili. Adrian akaulia Matha akatoweka.
Mzee alikuwa ameanza kusinzia Matha alipofika pale. Matha alimshtua naye akashtuka huku akizuga kuwa alikuwa hajalala.
Matha alitaka kumtokomeza naye duniani lakini huruma ikamshika. Akamsamehe. Akamwongeza elfu tano nyingine,biashara ikaishia hapo!!!
Pikipiki ikafunga breki miguuni mwa Adrian. Akatoa ukelele wa hofu.
"Panda!!!." Sauti ya kike iliamrisha. Ady akapanda.
Kwa kasi kubwa mwanadada akaindoa ile pikipiki kutoka eneo lile.
Walipoufikia mji, Matha akasimamisha ile pikipiki eneo ambalo halikuwa na watu wengi. Adrian akashuka, wakaanza kuelekea mahali alipopajua Matha na halmashauri ya kichwa chake.
Wakaitelekeza pikipiki. Wakaenda nyumba ya kulala wageni. Kila aliyewatazama alijua kuwa Adrian alikuwa ameopoa changudoa mshamba anayekubali kuingizwa gesti hovyo.
Haikuwa kama walivyodhani.!!!

****

Jitihada za John na Michael kumsaka adui yao ambaye amemuua Bruno hazikuzaa matunda.
"Adui katuzidi ujanja...hapafai hapa." John alimtahadharisha Michael. Michael akakubali kwa kichwa. Wakatoweka eneo lile!!! Kwa tahadhari kubwa sana.
Raundi ya kwanza John Mapulu na Michael Hoi!!!
Mwili wa Bruno uliachwa palepale. Michael na John. Usiku ule ndio ulikuwa wa mwisho kuingia katika nyumba yao ya Mecco.
Njia nzima walikuwa wakifikiria jambo moja tu. Kumchukua Matha na kutafuta hifadhi nyingine ya siri kwa muda wakati mapambano haya yakiendelea.
Geti lilikuwa limefungwa kama ilivyo ada. Walifika na kutaka kugonga ili Matha awafungulie kwani simu yake haikuwa ikipokelewa kwa muda mrefu.
Ilikuwa saa tisa kasorobo za usiku!!! Palikuwa kimya huku mbwa wakishindana kubweka pasipo sababu za msingi.
Michael alijaribu kusukuma geti. Maajabu!!!! Likafunguka bila kikwazo chochote
Tahadhari!! Kwa wote John na Michael.
Hali ya hatari!!!
John akachomoa bastola akaiweka makini kabisa kiwambo cha kuzuia sauti kikiwa katika utendaji kazi.
Michael akalikanyaga geti. Likafunguka. Waaa!!!
John akaingia upesi bunduki mbele, macho huku na kule.
Hakuna kitu!!
Michael naye akiwa katika hali ambayo hajapata kuwa nayo hapo kabla alihaha huku na kule huku John akiwa anamlinda na bunduki mkononi. Jitokeze ewe kiumbe hai na ubadilishwe kuwa maiti!!!
Hakuna aliyejitokeza. Zama mpaka ndani, msako wa chumba kwa chumba. Hakuna kiumbe hai aliyejitokeza.
Hofu kwa wote wawili.
Hata Matha hakuwepo!!1
Matha ametekwa!! Wote waliwaza hivyo. John akahisi kuchanganyikiwa. Kile alichokuwa anakipigania sasa kimetoweka pia.
Adrian ameniwahi!! Alijisemea John. Michael akaguna.
Hakika Matha hakuwepo eneo hilo. Wala vyumbani hakuwepo.
Ameenda wapi? Wamempeleka wapi? Hayo yakawa maswali magumu kujibika. Mtihani!!!
Hawakupata majibu. John akatoa maamuzi. Wakatoweka eneo lile. Tayari halikufaa tena kukalika. Walifunga kwa nje kufuri imara kabisa. Wakachukua vifaa walivyovihitaji kwa mapambano.
Wakatoweka kwa uangalifu wa kufungiwa tela na maadui.
Nyumba ya kulala wageni ndio ikawa makazi yao usiku huo.
Michael akiwa katika mtihani mgumu sana. Joyce Keto, msichana aliyempenda kwa mara ya kwanza katika maisha yake sasa alikuwa amepotea kwa mara ya pili baada ya kuwa amepatikana tena. Mwingine ni Matha, msichana ambaye ni mali ya John Mapulu, msichana ambaye sasa amembebea mtoto katika tumbo lake ikiwa imebakia miezi kadhaa aweze kujifungua. Naye alikuwa ametoweka. Tena ghafla katika mazingira ya kutatanisha.
Adrian!! Jina hilo lilivagaa kichwa chake na kumshtua moyo wake. Ni Adrian alikuwa anahusika na utekaji wa wawili hawa. Bahati mbaya iliyoje, Michael hakuwa amewahi kuonana na Adrian.
Wakati Michael akiumizwa kichwa na mawazo haya, John ambaye alionekana kama amesinzia alikuwa hoi akishambuliwa na mzimu wa Adrian. Hakuwa na jingine la kufanya zaidi ya kuulaani mzimu huu. Mzimu unaomkosesha raha.
Nikimpata nitamuua!!! Alinuia John.
Hilo lilikuwa wazo lake la mwisho kabla ya kupitiwa na usingizi. Wakati anasinzia Michael alikuwa anakoroma.

******

Hapakuwa na ushahidi wowote ulioweza kumtia Defao hatiani. Baada ya kusota rumande siku tano aliachiwa huru. Hakuwa na kesi yoyote ya kujibu. Maelezo yake yalikuwa yamenyooka na kwa kiasi kikubwa yalichangia yeye kuikwepa hatia.
Siku tano rumande na tatu za kukaa hospitali zilitosha kumkongoroa haswa kijana huyu wa Singida aliyeponzwa na tamaa ya kupata mali nyingi na sasa alikuwa matatani.
Ilikuwa ni bahati ya kipekee kwa Defao kuukwepa mtihani huu. Au labda tuseme ni Mungu aliegemea upande wake kwa kiasi kikubwa. Kwa hali halisi kesi kama hiyo isingeweza kumwacha lofa kama Defao arejee mtaani tena kuvuta hewa safi bure.
HATIA ikamuangukia Joyce, ambaye alitoroka hospitali!!!


Defao akafanya ishara ya msalaba na kisha kufanya majuto kidogo kwa kuilaani ardhi ya Mwanza kwa dhahama iliyompatia.
Baada ya kukabidhiwa vifaa vyake vichache alivyokutwa navyo baada ya kutiwa hatiani Defao alitoweka. Alikuwa na noti kadhaa. Akataka kupanda daladala lakini akagundua kuwa mwili wake ulikuwa unatoa harufu sana. Akataka kupanda teksi napo akagundua pesa yake haikuwa ya kutosha sana.
Alipofikiria juu ya pesa kutotosha, akakumbuka pesa zake nyingi alizoziacha chini ya kitanda katika hoteli aliyolala mara ya mwisho kabla ya kukumbwa na haya yaliyomkuta.
Moyo ukashtuka na kusukuma damu upesi. Ilikuwa taarifa ya kushtua sana. Defao akajiwekea imani kuwa huenda ile pesa bado ipo mahali alipoiacha. Japo imani hiyo hakuipa nafasi kubwa sana.
Defao akachukua maamuzi. Akaingia vyoo vya kulipia kwa ajili ya kujipatia huduma ya kuoga. Akalipia akaipata huduma hiyo. Akapaka mafuta mengi ili aweze kung'aa. Mafuta yalizidi usoni na kumfanya kwa namna moja awe kichekesho mbele ya watu.
Hakujali!!!
Sasa aliweza kupanda daladala. Akashukia mahali ilipokuwa hoteli aliyofikia mwanzo. Awali alikuwa anajiamini sana kurejea hotelini pale lakini mara akaanza kujihisi uoga na hofu baada ya kulitazama bango la hoteli ile.
Hofu yake ililetwa na muonekano wake. Na mapokezi atakayoyapata katika hoteli hiyo, pia alijiuliza ni vipi asipozikuta zile pesa zake alizozificha pale. Siku yake inayofuata itakuwa vipi na maisha yake Mwanza yataendaje. Hana ndugu wala rafiki.
Mungu saidia nikute walau nauli tu!! Ya kwenda Singida. Defao aliomba kwa Mungu wake.
Kisha akaanza kutambaa gizani akiambaa pembezoni mwa barabara hadi akafikia sehemu ya mapokezi. Sura iliyokuwa pale mapokezi ilikuwa ngeni kabisa machoni mwake. Haikuwa sura aliyokutana nayo siku alipokuwa analipia chumba kimadaha. Huyu alikuwa mwingine!! Defao akashukuru kimoyomoyo kwani angekutana na sura anayoifahamu lazima angekumbana na maswali mengi ambayo yangembughuzi na kumwongezea hofu.
"Kuna vyumba?." Defao aliuliza kwa sauti iliyokuwa inatetemeka.
"Mh!! Yah!! Vipo." Yule dada alimjibu kwa mashaka kidogo huku akimtathmini hadhi yake ya kuwa hapo. Alikuwa akijiuliza iwapo kaka huyo mbele yake hajaziona nyumba nyingine za kulala wageni zenye hadhi sawa na yeye.
"Vyumba vipi vipo wazi..." Swali hili kutoka kwa Defao likamdhihirishia yule dada kuwa mtu aliyeko mbele yake hakuwa mgeni wa eneo hilo. Imani ikarejea!!
Badala ya kujibu kwa maneno, yule dada akampatia Defao orodha ya vyumba.
Moja kwa moja akatazama chumba namba 18. Kilikuwa na mtu!! Na hakuwa wa kutoka siku hiyo.
Shit!!! Alilaumu Defao. Akategemea yule mwanadada atamuuliza kitu. Hola!! Hakuulizwa.
Nipe namba 25!! Hatimaye alitaja chumba alichokichagua. Akatoa pesa akalipia. Akaandikiwa chumba hicho kisha akapewa kijana maalum kwa ajili ya kumsindikiza.
Hakuwa na mizigo!!
"Ukitaka kuwasha taa unatumia kikadi hichi, ukitaka kutumia simu......"
"Najua kila kitu toka njea!!!" Alitoa karipio kali Defao. Yule kijana akakoma kuzungumza kisha bila kuaga akatoweka.
"Njoo ufunge mlango pumbavu wewe!!!" Defao akabwatuka baada ya kugundua kuwa mlango umeachwa wazi. Maneno hayo hayakumfikia yule kijana. Defao akasonya kisha akainuka na kwenda kuufunga mlango.
Akarejea na kujirusha kitandani!! Akatua kama ambaye anaangukia mayai. Aliona aibu uchafu wa nguo zake kulalia mashuka meupe!!!
Hasira zilikuwa zimemkaba kooni. Yule Defao aliyekuwa na mamilioni ya shilingi siku kadhaa nyuma. Leo hii hana hata senti tano mfukoni. Tumbo likaunguruma akatanabahi kuwa ni njaa. Hasira ikazidi.
Yote haya kisa ni Pesa. Pesa ya bwelele. Pesa kutoka kwa John Mapulu na mpenzi wake. Matha Mwakipesile.
"Hivi nimemuua John?." Ghafla Defao alijiuliza!!!
kujiuliza huko kukamfanya atetemeke na kutoamini ke imemteketeza John Mapulu!!

*****



****MATHA mwanaharakati wa kike amengia rasmi katika gemu dhidi ya JOHN MAPULU...Nini hatma ya mchezo huu ambapo MATHA hataki maadui zake wamtambue...amemuangusha BRUNO na Dereva wa pikipiki....


DEFAO amerejea katika hoteli ambayo ana kumbukumbu ya kuacha pesa zake haramu.....kibaya zaidi chumba kimekodiwa na mtu mwingine......ATAFANYA NINI.....aweze kulikimbia jiji.


***JOYCE keto alifanikiwa kurejea DAR????


Wazo Langu Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO


Nipe namba 25!! Hatimaye alitaja chumba alichokichagua. Akatoa pesa akalipia. Akaandikiwa chumba hicho kisha akapewa kijana maalum kwa ajili ya kumsindikiza.
Hakuwa na mizigo!!
"Ukitaka kuwasha taa unatumia kikadi hichi, ukitaka kutumia simu......"
"Najua kila kitu toka nje!!!" Alitoa karipio kali Defao. Yule kijana akakoma kuzungumza kisha bila kuaga akatoweka.
"Njoo ufunge mlango pumbavu wewe!!!" Defao akabwatuka baada ya kugundua kuwa mlango umeachwa wazi. Maneno hayo hayakumfikia yule kijana. Defao akasonya kisha akainuka na kwenda kuufunga mlango.
Akarejea na kujirusha kitandani!! Akatua kama ambaye anaangukia mayai. Aliona aibu uchafu wa nguo zake kulalia mashuka meupe!!!
Hasira zilikuwa zimemkaba kooni. Yule Defao aliyekuwa na mamilioni ya shilingi siku kadhaa nyuma. Leo hii hana hata senti tano mfukoni. Tumbo likaunguruma akatanabahi kuwa ni njaa. Hasira ikazidi.
Yote haya kisa ni Pesa. Pesa ya bwelele. Pesa kutoka kwa John Mapulu na mpenzi wake. Matha Mwakipesile.
"Hivi nimemuua John?." Ghafla Defao alijiuliza!!!


*****


John Mapulu hakuwa amekufa kama Defao alivyoweza kufikiria. Lakini alikuwa kama mfu. Kila mpango wake ulikuwa batili. Alijaribu kumuwinda Adrian bila mafanikio yoyote yale. Michael alikuwa anaogopa kumsemesha jambo lolote kiumbe huyu kwani majibu aliyokuwa anayatoa yalikuwa yanasikitisha sana na wakati mwingine yalikuwa yanatia kero.
John alikuwa katika majuto makubwa. Licha ya kuwa mbabe katika matukio makubwa makubwa. Mbele ya hili la kutekwa kwa Matha na Joyce alikuwa kiumbe dhaifu aliyeamini kuwa ameshindwa kumsaidia chochote Matha na pia aliamini kuwa amemfadhaisha Michael kwa kukaa kimya muda mrefu bila kumueleza juu ya uwepo wa Joyce Keto.
Yaani Matha naye kweli ameshindwa kabisa kufanya lolote kujiokoa na huyu jamaa? John alijiuliza huku akiwa ameyafumba macho yake. Alimjengea picha Matha kama mwanamke aliye na chembe za mwanaume jasiri na makini ndani yake. Hakuwa mtu wa kukubali kushindwa kirahisi.
Au jamaa walimpiga risasi? Alijiuliza tena. Katika hili hakutaka kuumiza kichwa chake kufikiria kuuona mwili wa Matha ukiwa umepasuka kifuani baada ya kushindiliwa risasi mfululizo alipojaribu kujitetea kwa kurusha mateke kadhaa aliyomfunza.
Zilikuwa zimepita siku kadhaa na hakuwa amepata taarifa zozote zile juu ya kifo cha matha na Joyce au walau simu kutoka kwa mtekaji kumfahamisha alikuwa na shida gani hadi amewateka wawili hao.
Timu anayoshirikiana nayo imejipanga!! Alikiri kwa sauti ya juu kiasi John. Michael Msombe akasikia lakini hakuchangia chochote.
Tayari walikuwa wamehama nyumba za kulala wageni zaidi ya nne. Na sasa walikuwa Kisesa nje kidogo ya jiji la Mwanza.
Michael akiwa msikilizaji na John mtendaji.
Simu ya John ilipotoa mlio. Iliwafanya wawili hawa kushirikiana kuitazama simu ile kisha bila kutegemea wakatazamana.
"Nani anapiga?." Michael alimuuliza John. Hakujibiwa!!!
John akaitazama simu iliyokuwa inaendelea kuita kisha akaipokea. Akaunguruma kwa sauti yake iliyojaa shari kama kawaida.
"Mambo vipi mzee!! Umelala?."
"Aaah! Nipo tu!! Uchovu, vipi nambie."
"Aaah! Umenitupa mzee mzima vipi?."
John hakujibu!!
"Vipi lakini dadangu mzima."
"Mzima tu kwani vipi?." Alihoji John. Swali kutoka kwa mmoja wa waliokuwa kaka zake na Matha lilimtia mashaka.
"Ah! Hamna nilimfananisha tu. Ndio maana nikataka nimjulie hali huenda nimemkumbuka tu!!."
"Wapi tena? Lini?."
"Huku Nyegezi, kwenye magari ya kwenda Arusha kitu kama hicho!!."
"Mh!! Arusha. Ujue nini, mimi nimesafiri kidogo. Sina taarifa zake halafu tulikuwa tumegombana kidogo si unamjua tena dadako. Ehee!! Ni gari gani hiyo." John aliufuma uongo upesiupesi akaurusha kwa mzungumzaji upande wa pili.
"Sijui ni basi gani lile sikutilia maanani, limeondoka kama saa mbili na nusu hivi."
John akatazama saa yake ilikuwa saa tatu na dakika tano.
"Ahaa!! Huenda wamefanana tu!! Ngoja nipige simu nyumbani, nitakujulisha."
"Haya shemeji yangu, si unajua tena tunakulindia maana alikuwa na kidume yule kamganda kama nini. Sijui ni yeye ama vipi."
Akaendelea kuchombeza. John akawa anamsikiliza.
"Basi poa Kelvin. Namba yako si ina huduma zile za kupokea pesa eeh!!."
Kelvin akakubaliana na John. Simu ikakatwa.
John alikuwa anautambua usumbufu wa Kelvin akiwa hana pesa. Akamtumia kiasi cha pesa muda uleule kisha akajikita katika kuitumia ile taarifa aliyopewa na Kelvin.
"Adrian anamtorosha Matha kuelekea Arusha." John alimweleza Michael.
"Vipi kuhusu Joyce?." Michael aliuliza. John akakosa la kujibu.
"Naondoka sasa hivi kuelekea huko wanapoenda. Itakubidi uhame hii hoteli.....eeh!! tutaondoka wote." John alimweleza Michael huku akijiweka sawa. Michael naye akaendelea kuwa msikilizaji kama kawaida yake.
Baada ya nusu saa walikuwa ndani ya teksi. Safari ya kwenda Nyegezi stendi.
John alikuwa makini kabisa asiweze kukutana na Kelvin. Na hakumpa taarifa yoyote baada ya kumtumia ile pesa. Michael naye alikuwa akifuata yote yaliyotamkwa na John.
Kwa kuwatumia watu wake walioko maeneo ya stendi ya Nyegezi ilimchukua nusu saa nyingine kupata jawabu kuwa hakuna abiria aliyesafiri siku hiyo akiwa na jina la Adrian lakini Matha alikuwepo.
"Huyu amekata tiketi peke yake, hakuwa na mtu!!!." Alipewa maelekezo hayo. Akashusha pumzi kwa fujo sana. Alianza kupoteza matumaini.
John hakubarikiwa akili ya darasani lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri katika mambo mengine. Na alikuwa mwepesi wa maamuzi katika mambo magumu.
Alipiga simu mara tatu. Kwa watu tofauti tofauti. Baada ya robo saa, akakabidhiwa gari aina ya Landcruiser na mmoja kati ya watu aliofahamiana nao.
"Michael. We baki huku Mwanza. Nitahitaji sana msaada wako nikiwa huko niendako." John alimnong'oneza Michael. Michael akaiona hofu iliyotanda katika uso wa John. Hakuleta ubishi wowote.
Akapatiwa fungu la pesa!! John akazama garini.
Akatoweka!!!
Michael akaondoka akiwa ameinamisha kichwa chini. Miwani nyeusi ikiwa imehifadhi macho yake. Alikuwa amekata tamaa.
Aliponyanyua kichwa chake kukabiliana na barabara ndefu ya kutoka stendi ndio hapo alipomuona!!!
Mapigo ya moyo yakajitahidi kuongeza kasi. Akaivua miwani yake. Akatazama zaidi ni hapo alikuwa amemuona!!!
Amuite ama asubiri!! Asubiri kitu gani sasa.
Hakuwa peke yake.
Macho hayakuwa yakimdanganya ni yeye!!!
Ni yeye!!!

****

Defao hakuweza kuupata usingizi kabisa. Hata hivyo hakuhitaji kupitiwa na usingizi.
Wa nini sasa huo usingizi?
Alikuwa akiwaza na kuwazua juu ya siku yake ya kesho na nyingine zilizosalia hapo Mwanza ataishi vipi? Alitamani sana kuingia katika kile chumba. Lakini bahati mbaya kilikuwa kina mteja. Usingizi huwa hauna hodi. Hatimaye ukamtwaa. Akalala!! Uso wake ukiwa na majonzi tele.
Asubuhi ikafika!! Alitakiwa kulipia chumba upya tena!!
Pesa haikuwepo tena!!!
Hakuwa na budi kukiachia chumba. Defao akaingia kujichanganya mtaani. Kwa mavazi aliyokuwa amevaa alifanania na mlevi wa pombe za kienyeji asiyejielewa kabisa.
Aanzie wapi? Hilo lilikuwa swali.
Defao akaikumbuka simu yake. Aliyoinunua kwa bei ghali kipindi kile ana pesa. Akawaza kuiweka rehani aweze kupata senti kadhaa. Wazo hilo likapita katika kichwa chake.
Ilikuwa saa nane mchana na njaa ilikuwa imemtafuna haswaa!!
Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza.
Haikuchukua muda akawa ameiuza kabisa maana hakuwa na mahali popote pa kuiweka rehani. Pesa aliyoipata si haba!! Ilimtosha kupata chakula kizuri na pia aliweza kulipia tena nyumba ya kulala wageni.
Ileile ambayo aliamini kuna pesa zake. Sasa Defao alikuwa ameamua litakalokuwa na liwe.
Usiku huu akiwa katika chumba kilekile alicholala usiku uliopita. Aliijiwa na wazo hilo la liwalo na liwe.
Alijongea kutoka chumba chake. Hatua kwa hatua hadi chumba namba 18. Hofu ikamtwaa akahisi hatakuta chochote ndani ya chumba hicho ama anaweza kukumbana na ugumu kutoka kwa mteja aliyepanga katika chumba hicho.
Eeh!! Mwenyezi Mungu saidia wasiwe wawili!! Defao alifanya sala fupi kwani alijua kabisa wakiwa mwanaume na mwanamke watakuwa na biashara zao nyingine ambazo kuwakatisha itakuwa ngumu sana na pia inaweza kumwekea matatizo kwani muhudumu wa mapokezi tayari alikwishamwekea mashaka tangu siku alipoingia mara ya kwanza tangu atoke rumande.
Akapiga moyo konde!! Akaunganisha kiganja chake akagonda mlango!!
Mara ya kwanza!! Kimya...akagonga tena. Kimya!!
Mara ya tatu akasikia kitanda kikilalamika. Aah!! Wanafanya mambo yao hawa!! Aliwaza Defao huku akijilazimisha kujiweka katika hali ya kutokuwa na wasiwasi.
"Nani?." Sauti ya kike kutoka ndani iliuliza.
Mh!! Kamtuma mwanamke ndo aje kufungua au?
"Mimi....mimi." alijiumauma.
"Nani?."
"Muhudumu." Alijikuta akijibu hatimaye.
Mlango ukafunguliwa taratibu. Ndani palikuwa giza.
"Nini?." Aliuliza mwanadada kutoka ndani. Alikuwa katika mavazi yake ya kulalia, laini kabisa kuweza kumtamanisha yeyote atakayepata fursa ya kumwona akiwa katika mwanga. Defao hakumwona katika mwanga.
"Samahani dada..kuna mteja anadai kuna kitu chake anaweza kuwa aidha alikisahau humu ndani. Siku kadhaa nyuma. Samahani sana kwa usumbufu wowote utakaojitokeza." Defao akiigiza kama muhudumu wa hoteli hiyo alijieleza.
"Aaah! Usumbufu huo sasa. Kwanini msije wakati wa usafi asubuhi." Alilalamika huyu mteja.
Defao hakujibu kitu!!
"Subiri kidogo." Alisema yule dada huku akiufunga mlango. Baada ya dakika tano akaufungua tena. Alikuwa amejifunga kanga.
"Ingia..."
Defao akapiga hatua akaingia katika chumba hicho.
"Ila nisamehe sana..." Alisihi defao huku akielekea kilipo kitanda.
"Samahani nataka kuinua hili godoro unaweza kutoa hii.." Defao alimweleza kiaibuaibu huku akiinyooshea kidole ile chupi ambayo kwa kila hali ilikuwa mali ya yule dada.
Mara wakatazamana!!! Defao akaruka pembeni!! Akaziba midomo yake.
Yule binti akatulia kama aliyepigwa shoti. Alikuwa amekumbvana na kiumbe cha ajabu katika maisha yake. Kiumbe ambacho alikiri kabisa akilini mwake kuwa kam we hakutaka kukutana na kitu kama hicho. Mara ya mwisho kukiona alijikuta anapoteza fahamu. Sasa alikuwa anayerembua macho yake.
Taratibu Joyce Keto akalegea na kuanguka chini. Bila kupata msaada wowote kutoka kwa Defao kwa jina halisi Gervas.
Defao alibaki katika mshtuko huo kwa sekunde kadhaa. Alikuwa haamini kama mbele yake amesimama Joyce Keto na kisha amelegea na kuanguka chini.
Akili ikamkaa sawa akamsogelea na kuanza kumpepea, kisha akawasha kiyoyozi, hali ikawa ya ubaridi na bado hakuacha kumpepea.
Joyce aliyeangukia mgongo, akarejewa na fahamu zake nusu saa baadaye. Alikuwa chumbani na mwanamme aliyembaka miezi kadhaa iliyopita na sasa alikuwa mjamzito. Defao!!
"Gervas!!!." Aliita Joyce.
"Joyce!!." Alijibu Defao. Kisha wakakumbatiana. Zile chuki na hasira ambazo Joyce alikuwa amezitunza kwa miaka mingi ziliyeyukia kifuani mwa Defao.
"Umejuaje nipo humu Gervas." Joyce alimuuliza Defao.
Defao akapiga kimya kwa sekunde kadhaa akatazama darini kama mchunguzi fulani huku akiwa ameibana midomo yake na kuyauma meno yake.
Kisha akajieleza. Maelezo yote yalimshangaza Joy, sasa wakafikia maelezo kuhusu pesa. Hapo sasa wote wakatazama lile godoro. Halafu wakalivamia na kuliinua.
Huku na huko!! MAAJABU Pesa ilikuwepo!!
Kama alivyoiacha Defao mara ya mwisho.

Defao alipagawa kumkuta Joyce akiwa bado ana mimba aliyompatia katika njia ya kumbaka. Hali hiyo ikamfanya kuisahau kabisa ile pesa waliyoikuta pale ndani.
Joyce naye akasahau kisasi cha kubakwa. Wawili hawa wakawa kitu kimoja. Defao akahamishia makazi katika chumba cha Joyce. Kile kitoto ndani ya tumbo la Joyce kikaleta pendo jipya.
Japo mimba ilipatikana kwa kitendo cha ubakaji lakini mimba ilibakia kuwa mimba.

Jiji la Mwanza halikuwa na usalama wowote kwa wawili hawa. Baada ya kuwa wamesimuliana kila mmoja nini kimemsibu sasa waliamua kwa sauti moja kutoweka katika jiji hilo. Jiji lililobadilisha historia ya kila mmoja.
Mpango ukasukwa usiku huohuo. Na kesho yake wakaongozana kuelekea stendi kukata tiketi.
Nyegezi!!! ni huku waliweza kuonwa na Michael bila wao kujua.
Michael akawa amemuona Joyce. Pagumu hapa!! Mpambano mpya.



****DEFAO na JOYCE ndani ya mpango mmoja wa kuondoka jijini Mwanza....MICHAEL amewaona!!! Nini kitatokea.


JOHN ameipata taarifa kuwa MATHA amekimbilia ARUSHA ameamua kufuatilia...JE ATAMPATA??? Kumbuka yu pamoja na ADRIAN!!!!


ITAENDELEA!!!


Wazo Langu Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom