Riwaya: Hatia

Riwaya: Hatia

Adrian achomoke kwenye hili balaa.
Ila nae akome kuchepuka.

Ahsante Casuist.
 
Mkuu Casuist,tupia moja nipoze hasira maana bosi kaniaribia siku.
 
Last edited by a moderator:
Du yhe last chance kwa Matha akiipoteza hiyo atatangulia mbele ya haki.
 
Habari wakuu

Nadhani wengi wetu tunamkumbuka Ben R Mtobwa, binafsi nilimsoma shuleni na alinikosha sana. Maktaba za kishetani ni riwaya yake nyingine katika mfululizo wa harakati za Joram Kiango ambazo aliandika wakati wa uhai wake.

NB: Kitabu kitatolewa January bado kipo kwenye mchakato wa kutoka. Hapa chini ni mwanzo wake. Riwaya ya HATIA leo ni mwisho na baada ya muda ntaweka tamati yake.

attachment.php


nameless girl Khantwe davidson689 Toplady ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrangomangimezamuuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 

Attachments

  • unnamed.jpg
    unnamed.jpg
    74.7 KB · Views: 1,630
Maktaba za kishetani-harakati za Joram Kiango

ALIKUWA mwanamke! Tena mwanamke wa haja! Alisimama pale, uso wake ukiwa umeelekezwa kwangu; kama anayesubiri nifanye kazi yangu! Naapa kuwa, kwa mara ya kwanza, katika maisha yangu ya udunguaji, nilisita kubonyeza tufe la mwanangu, AK 47 ambaye nilimpenda kuliko wanangu wengine wote niliopata kuwatumia.
Alikuwa pale, kasimama, huku uso wake ukielekea kwangu mara kwa mara.
‘Ananisubiri!' Niliwaza.
Sikujua kwa nini nilisita. Maelekezo yote niliyopewa yalikuwa barabara; atakua amevaa suruali ya kitambaa, yenye rangi nyeusi na koti lake la rangi ile ile juu ya shati yenye rangi ya bendera ya taifa. Atatoka nje ya mlango wa hoteli saa nne na robo, akiwa katikati ya Rais wa Nchi kulia kwake na mgeni wake, bilionea wa viwanda na machimbo ya madini upande wa pili. Pale mlangoni watasita kidogo kuagana kabla ya kuelekea kwenye hafla maalumu. Mwondoe akiwa pale pale mlangoni.
Maelekezo yalikuwa sahihi. Muda ulikua uleule uliopangwa. Na zaidi ya yote mavazi, yalikuwa yaleyale yaliolekezwa. Wala si hayo tu, mamilioni ya dau langu lililolipwa katika fedha za kigeni tayari yalikuwa yamekwisha ingia kwenye akaunti yangu ya benki wiki moja iliyopita na kuhamishiwa katika benki mbalimbali, kwa majina tofauti, kabla ya sehemu ya pesa hizo kuja Dar es Salaam kwa matumizi yangu madogo madogo.
Purukushani za wapiga picha wa televisheni na magazeti zilikuwa nyingi. Kila mmoja alikuwa akihangaikia kupata picha bora zaidi, ama ya Rais ama ya mgeni, au wote kwa pamoja. Vichwa vyao na kamera zao zilipita mbele yao kwa namna iliyonifanya nipoteze shabaha. Lakini hilo lisingenizuia. Walengwa wangu walikuwa juu ya wapiga picha kwa ngazi moja. Isitoshe, mimi ni mtaalamu. Sekunde moja tu ya kutikisa kichwa ilitosha kabisa kumdungua muhanga wangu bila tatizo.
Hata hivyo, nilisita kumtekenya mwanangu.
Kitu gani basi kilifanya nisite kumbonyeza kidogo tu mwanangu ili nimalize kazi hiyo na kuendelea na ziara yangu ya kutembelea ziwa Tanganyika ambako nilikusudia kuwinda viboko kijiji cha Buhingu na kisha kuwashuhudia sokwe wa milima ya Kasoge? Kitu gani kiliutia uzito moyo wangu wa kishetani, ambao daima ulifurahia kuiona risasi yangu ikimpaisha mtu angani na kisha kumdondosha chini huku akiwa tayari ametokwa na uhai wake? Kitu gani? Kitu gani? Kitu ga…
Mara nikakumbuka. Zilikuwepo sababu nyingi, kubwa zikiwa mbili. Ya kwanza, ilikuwa urahisi wa kazi hii. Katika maisha yangu haya, sijapata kazi rahisi kama hii, upewe hela nyingi zaidi ya ambazo ungeomba, upewe wajihi wa mtu unayetakiwa kumwondoa, siku, saa na vazi atakalokuwa amevaa! Ilikuwa nyepesi mno. Natumaini ni wepesi huo ulionitia mchecheto kiasi cha kunifanya nisite kufanya vitu vyangu.
Sababu ya pili, mhanga wangu alikuwa mwanamke, tena mzuri! Sijapata kumuua msichana mzuri kama huyu wala kuombwa kumuondoa duniani mwanamke. Hili pia lilinikoroga kichwa.
Kulikoni? Nilijiuliza. Kisha nikajikumbusha taratibu za kazi zetu. Ukishapokea malipo yako, ukishaweka utaratibu madhubuti wa kumuondoa mhanga wako, kamwe usianze kujiuliza maswali. Hiyo ni kazi ya polisi na wapelelezi na anayewajibika kujibu ni mteja wako, sio wewe.
Wazo hilo lilinifanya nimnyanyue tena mwanangu mpenzi, kumwelekeza kule alikokusudiwa. Nikarekebisha lensi na kuzivuta nyuso zao kwangu. Ilikuwa imepita nusu dakika tu toka niliposita kuibonyeza. Walikuwa wangali palepale mlangoni. Raisi alikuwa amegeuka kusalimiana na mtu fulani. Ningeweza kumwondoa, kupitia kisogo chake kwa urahisi kabisa. Kwa bahati, sikutumwa kufanya hilo. Yule bepari wa viwanda na madini naye alikuwa pale, kaduwaaduwaa. Ningeweza kumwondoa kwa bei rahisi vile vile kupitia upande mmoja wa sikio.
Mhanga wangu alikuwa kama anayeendelea kunisubiri. Uso wake mzuri ukiwa umeelekezwa kwangu na macho yake yalikuwa na dalili za wasiwasi na vitone vya jasho jembamba katika paji lake la uso, paji ambalo nilililenga vizuri kana kwamba nipo katika mazoezi ya shabaha. Nikamtekenya mwanangu. Sekunde moja, mbili, tatu… Mara mhanga wangu alipaa kama futi moja angani na kisha kutua kama gunia miguuni mwa Rais, akiwa tayari mzoga. ‘Mkono wa Jibril haujapata kukosea' niliwaza nikicheka kimoyomoyo.
Purukushani iliyofuatia hapo haikuwa na kifani. Nilitamani sana kuitazama walao kwa dakika mbili pindi wanausalama wakicharuka kama waliopigwa ufunguo. Wanne, waliokuwa nyuma ya msafara huo; walichupa angani, mmoja akimpitia Rais kwa kumbo ambalo lilimwangusha na kumlalia kama ngao huku wenzake wakiwavuta na kurejea ndani. Wakati huohuo ving'ora vililia, polisi wakiivamia barabara na kufunga mitaa. Raia wa kawaida, waandishi na wafanyakazi wengine walikuwa taabani zaidi, huyu akianguka pale, yule akikimbilia kule kana kwamba wamepagawa. Sikuweza kujizuia kucheka.
Nilimwona mwanausalama mmoja akitazama huko na huko, kisha macho yake yakaelekea upande wa pili wa mtaa, katika jengo nililokuwepo mimi na kutoa maelekezo kwa wenzake ambao walianza kujipanga kulizingira jengo hilo.
Ulikuwa wakati wangu wa kuondoka. Nilimbusu mwanangu ambaye bado alikuwa na joto la risasi ile moja aliyotema. Nikamfungua na kumkunja taratibu na kisha kumweka katika briefcase yake vizuri. Juu yake nilirudishia vitu mbalimbali vya kudanganyia, ambavyo vingemlaghai mtu yeyote ambaye angepata wazimu wa kuikagua.
Haikuwa kazi kubwa kuliacha jengo hilo. Watu wote walikuwa wameduwaa, wakishangazwa na purukushani ambazo zilikuwa zikiendelea upande wa pili wa mtaa. Nikaipuuza lifti na kufuata ngazi ambazo zilinitoa ghorofa ya tano na kunipeleka ya nne, ya tatu, ya pili. Hapo nilipanda lifti hadi chini. Wakati nikitoka nje ya lifti hiyo watu wawili, waliovaa suti waliingia harakaharaka, mikono yao ikiwa mifukoni.
Hatukutazamana usoni, lakini sikuhitaji kuambiwa kua hao walikuwa wana usalama wakifuatilia uelekeo wa ilikotokea risasi. Nilitamani kuwapa pole. Nilitamani kuangua kicheko. Lakini yote hayo sikuyafanya. Niliondoka zangu bila kuangalia nyuma nikihisi macho yao yakilitazama umbo langu la nyuma hadi mlango wa lifti ulipojifunga.
Sikuwa na wasiwasi. Nilijua wasingenishuku kwa lolote. Nani anaweza kumshuku msichana mrembo, aliyevaa nguo fupi na viatu vya mchuchumio huku nywele zake ndefu kaziachia kama msichana wa Kihebeshi? Nani angepata muda wa kushuku wakati harufu ya marashi aliyopaka yalitawala katika chumba cha lifti alichokiacha punde?

***

Alikuwa mwanamke mzuri, zaidi ya uzuri wa haja. Picha zake katika televisheni na kurasa za kwanza za magazeti yote ya siku hiyo zilithibitisha hilo. Angeweza kushiriki urembo wa dunia na akashinda; angeweza kucheza filamu yoyote ile na akawa kivutio. Picha zilifichua uso wake mzuri uliojaa ucheshi, huku macho yake yakionyesha ung'aavu na hekima. Kiwiliwili chake chenye urefu wa kadiri, kilichojaa uhai na matumaini yote katika maisha. Hata sauti yake, pale televisheni moja iliporusha maneno yake mawili matatu enzi za uhai wake, ilithibitisha jambo moja; hakuwa mtu wa kufa.
Lakini tayari alikuwa marehemu! Mipango ya mazishi yake bila shaka ilikuwa ikiandaliwa!
Kwa jina aliitwa Cleopatra. Mumewe aliitwa Twalib. Kwasababu alizozifahamu mwenyewe, Cleopatra hakupata kulitumia jina la mumewe katika shughuli zake za kiofisi zaidi ya lile la baba yake Abeid ingawa Twalib lilikuwa jina zito katika jamii.
Magazeti yalisema na kudodosa hili na lile juu ya kifo chake. Hata hivyo, lililokuwa wazi katika kauli na maandishi yote ni utata juu ya kifo chake. Wingu zito lilitanda juu ya kifo hicho kutokana na swali zito lililokuwa likisumbua vichwa; muuaji alimkusudia yeye kweli au alikuwa amemlenga Rais?
Gazeti moja lilikwenda mbele zaidi, katika habari yao ambayo iliandikwa pia kama maoni, ilibebwa na kichwa cha habari; KWA VYOVYOTE VILE HAKUWA MTU WA KUFA.
Nani atafikiria kumuua Cleopatra? Liliandika. Hakuna hata sababu moja iliyowazi ya kupelekea mtu yeyote, awe na akili timamu au mwendawazimu kuchukua uamuzi wa kumuua kinyama tausi huyu ambaye hakupata kuwa na madhara kwa jamii wala mwanajamii yeyote.
Cleopatra alikuwa msomi, mwenye shahada ya Udaktari aliyoipata akiwa na umri usiozidi miaka thelathini na mitano. Alipata kuwa na kipindi muhimu sana cha ushauri wa kijamii katika televisheni mbili tatu nchini. Alikuwa mtumishi mwaminifu na mchapakazi hodari katika Ikulu ya Dar es Salaam. Hata kifo kimemkuta wakati akilitumikia taifa, tena mbele ya Rais aliyekuwa katika hafla nzito ya kumshawishi tajiri mkubwa wa viwanda duniani kuwekeza nchini.
Tunasema hakuwa mtu wa kufa! Bado tunaamini kuwa risasi iliyomuua haikumkusudia yeye. Ni kwa mtazamo huo ndipo tunaposisitiza haja kubwa ya uchunguzi makini wa haraka, kujua kitu gani hasa kilitokea hata mshumaa huu uliokuwa nuru kwa wanawake wote duniani na mfano kwa kila mwanaume, kuzimika ghafla…
Gazeti jingine lilizifuatilia habari hizo kwa mtindo wake. Liliwasiliana na ofisi ya Rais kutaka kujua Rais anajisikiaje kuponea tundu la sindano katika tukio hilo na iwapo anadhani risasi ilimkusudia yeye au marehemu.
No comment!
Pengine comment pekee ambayo uchunguzi wa gazeti hilo ulifanikiwa kupata ni pale walipofanikiwa kuzungumza na mume wa marehemu. Aliwashangaza, kama alivyowashangaza pia wasomaji, kwa taarifa yake kuwa yeye na Cleopatra walikuwa wametengana kwa zaidi ya miezi sita iliyopita! Kisa?
No comment.
Picha ya Twalib Khalfan ilitoka sambamba na ya marehemu mkewe katika habari hizi. Kila mmoja alikuwa akiitazama kamera huku anacheka. Mapenzi yalikuwa wazi kabisa katika macho ya tausi hawa wawili. Gazeti hilo halikuishia hapo. Lilivuka mipaka kwa kupendekeza kuwa kwa uzoefu wao, katika maswala yenye utata kama hayo yupo Mtanzania mmoja tu ambaye angeweza kuaminika katika kuyapatia ufumbuzi. Walimtaja mtu huyo kama Joram Kiango. Madai hayo yalifuatiwa na maelezo mafupi ya mikasa mingi ya kitaifa na kimataifa aliyopata kuitatua ama kwa ubongo wake ama kwa risasi ya bastola yake.
Waliyapamba maelezo hayo kwa picha ya Joram Kiango, akiwa ameketi katika bustani moja nchini, macho yake yakiwa yameinamia gazeti. Kando yake alikuwepo mwandani wake, msichana mwenye umbile nadra kwa uzuri wa ziada ambaye maelezo chini ya picha yake yalimtaja kwa ufupi ‘Bi Nuru'
Gazeti hilo lililalamika kuwa jitihada zao zote za kumpata Joram Kiango ili walao atoe maoni yake juu ya tukio hilo la aina yake, ziligonga mwaba. Kwamba walifika nyumbani kwake Ilala na kubaini kuwa hajaonekana kwa miezi. Walipita katika hoteli zote maarufu ndani na nje ya jiji na kupata jibu lilelile; hajaonekana kwa miezi.
Yuko wapi Joram Kiango?
Ilimalizia kauli ya mwandishi wa habari hiyo katika hali ya kukata tamaa.



***
Joram Kiango alizipokea habari hizo kwa njia ya mtandao wa intaneti akiwa angani. Alikuwa ndani ya ndege ya Emirates, aliyoipanda Amsterdam baada ya kushuka toka katika City Hopper ya KLM iliyomtoa Frankfurt. Alikuwa njiani toka nchini Ujerumani, katika mji wa Maizn, ambako alikuwa masomoni akipigania shahada yake ya udaktari wa falsafa. Mhadhiri wake Profesa Oed Matzke alikuwa nae sambamba kwa miezi miwili akinakili awamu ya mwisho ya kazi yake ili aweze kuvishwa hadhi ya Udaktari.
Akiwa amechoka kusoma kitabu cha Bill Clinton, The Art of Giving, aliamua kufungua kompyuta. Ndege hii ya kisasa ilikuwa na kompyuta kwa kila abiria, ambayo unaweza kuitumia kwa kutazama filamu, intaneti, kupiga simu pamoja na kuona wapi uliko katika anga hilo.
Kama kawaida yahoo ilikuwa na habari kadhaa za kimataifa; mtafaruku wa uchaguzi nchini Kenya, mauaji ya Bi Bhitto nchini Pakistan, purukushani za Hillary Clinton na Obama katika mbio za kuwania kuteuliwa kugombea Urais nchini Marekani kwa tiketi ya Democratic na kadhalika.
Habari iliyomshtua ni ile ya nyumbani, ‘RAIS ANUSURIKA KUUAWA,' ambayo ilichukua nafasi ya nne ya habari hizo za siku hiyo. Hakuitegemea. Hivyo, ilimshtua sana, kwani kwa utamaduni na hulka ya Watanzania hilo lilikuwa jambo geni.
Aliisoma habari hiyo kwa kituo mara tatu, akihariri kati ya taarifa halisi na ushabiki wa mwandishi. Haikumchukua muda kujikuta akijiuliza swali lilelile lililokuwa likisumbua vichwa vya watu wengi; walikusudia kumuua Rais?
Jibu halikuwa rahisi kiasi hicho. Aliamua kuachana na habari hizo na kufungua e-mail yake; jkiangoyahoo.com. Kama alivyotegemea alikutana na ujumbe toka kwa Nuru. "Nimekutafuta sana kwa simu hupatikani. Una habari kuwa Rais ameponea chupuchupu…" Joram alizisoma tena habari za tukio lile la Dar es Salaam kwa mtazamo wa Nuru. Alimsoma katikati ya mistari na, hivyo, kuona matarajio ya msichana huyo kumshawishi ili ajitome katika uchunguzi wa tukio hilo.
Alitabasamu.
Ili kujiepusha na blaablaa nyingi za simu ambazo zingeweza kumvurugia mkondo wa masomo yake, Joram alikuwa ametoa kadi yake ya simu ya nyumbani na kuweka ya muda. Hivyo akiwa katika anga la Kenya, kuelekea Nairobi, aliitupa kadi ile ya Ujerumani na kuirejesha ya Tanzania. Hazikupita dakika tano, simu iliita. Na hakuwa mwingine zaidi ya Nuru. "Umepata e-mail yangu?" aliuliza
"Naam" alimjibu
"Kwahiyo una maoni gani?"
"Maoni gani?" Joram aliuliza baada ya kucheka. "Nuru naona umeanza. Mimi na wewe ni nani katika nchi hiyo hata tusumbue vichwa vyetu mara kwa mara kwa matukio yasiyotuhusu? Nimesema na narudia kusema kuwa tukio la Mtambo wa mauti lilikuwa la mwisho."
Joram alimsikia Nuru akicheka upande wa pili wa simu. Kisha alisema, "Tusidanganyane Joram. Mimi nakufahamu vilivyo. Wewe si mtu wa kukaa kimya wakati Rais wa nchi yako anatishiwa kuuawa."
"Hatuna hakika kama walikusudia kumuua," joram alimkumbusha.
"Na ni hilo lililofanya kila mtu akufikirie. Hatuwezi kukaa kimya wakati kitendawili cha tukio hili hakijateguliwa," alisema kabla ya kuuliza, "Unarejea lini?"
"Leo, muda mfupi baadaye tutakuwa pamoja. Kumbuka nakuja kupumzika. Siji kufanya kazi za wavivu wanaofura matumbo na kusahau wajibu wao. Watu wanaowasahau raia na kutumia vyeo vyao kuwalinda mafisadi"
Kicheko cha Nuru kilimkatiza Joram
"Sasa unacheka nini?"
"Nimefurahi. Huyu ndiye Joram Kiango ninaemfahamu."


Nilisoma gazeti hilo na mengine yote yaliyoandika chochote juu ya kifo cha Cleopatra. Hali kadhalika, nilifuatilia habari zote katika televisheni na redio kwa makini kabisa. Kwa muda huo mfupi, kwa kupitia picha mbalimbali za magazeti na televisheni nilikwisha mfahamu vilivyo marehemu kama ninavyofahamu kiganja changu. Na kwa maelezo ya vyombo hivyo niliweza kujua mengi kuhusu maisha yake kama ninanvyomjua binamu yangu.

Katika yote niliyoyasoma au kuyasikia kitu kimoja kilikuwa dhairi, kama alivyoandika yule mwandishi kuwa "Cleopatra hakuwa mtu wa kufa" dhana ambayo ilinipa kitendawili kizito sana, hasa nikizingatia ukweli kuwa kazi ya kumuua ilikuwa nyepesi sana, kama kuua mbu ndani ya chandarua.

Kwa kawaida katika shughuli zetu hizi tunashauriwa kupanda ndege ya kwanza mara baada ya tukio kukamilika. Hivyo ingekuwa busara kuwa badala ya kuwa juu ya kitanda laini, katika hoteli murua, nikifuatilia tukio nililolianzisha mwenyewe ningestahili kuwa angani nikielekea nje ya nchi na nje ya bara. Lakini tukio hili lilinitia ushawishi mwingi, hata nijikute na hamu kubwa ya kufahamu mengi ambayo kitaaluma hatuhitajiki kuyafahamu. Nilitamani kujua mwajiri wangu ni nani na alikuwa na uwezo gani kiasi cha kunirahisishia kazi namna ile.

Hayo ndiyo yaliyoimeza kiu yangu ya kwenda kuwawinda viboko wa ziwa Tanganyika, badala yake yananizalia hamu ya kujiingiza katika utafiti wa kumpeleleza mwajiri wangu. Muuaji anapogeuka mpelelezi wa mauaji yake mwenyewe! Shit

Wakati mkondo huo wa mawazo ukichukua kasi katika ubongo wangu, nilikuwa nikimalizia kazi ya kumfumua mwanangu na kumtawanya katika sehemu mbalimbali za begi langu. Kila sehemu ilifunikwa kwa mifuko maalumu ya nailoni ambayo scanner yoyote katika viwanja vya ndege isingeweza kubaini. Hali kadhalika, ingehitaji mkaguzi mwenye ujuzi na akili za ziada kuibaini katika begi hilo maalumu hata kama angeachiwa saa nzima ya kulikagua. Hivyo, sikuwa na wasiwasi kwamba watumishi wadadisi wa hoteli hiyo wasingeweza kushuku chochote katika begi hilo.

Kazi ngumu ilikuwa ya kujibadili. Kutoka katika jinsia hii kwenda ile. Hii ilihitaji umakini na utulivu mkubwa. Aidha, ilihitaji si chini ya saa tatu hadi nne kujivua usichana na kuvaa uvulana. Yalihitajika mafuta maalumu ya kulainisha mwili ili kuitenganisha ngozi na zile plastic laini zilizofanana vilivyo na ngozi asilia. Mafuta ambayo pia yalisaidia katika kuondoa nyusi, matiti na kucha za bandia pamoja na kuvua lile wigi maalumu lenye nywele za Kihabeshi kwa kila mwanamke aliyenitazama na kushawishi kwa kila mwanaume. Jukumu la kufuta poda, rangi za midomo na kuipoteza harufu ya pafyumu mwilini ilikuwa ndogo, kama ambavyo ingekuwa rahisi kubadili mavazi yale ya kike na kuvaa ya kiume.

Hata hivyo, hayo sikuyafanya kwa sasa. Nilikodi chumba hicho kwa jina la kiume, kwa njia ya mtandao, nikitumia jina la Freddy Macbain na mke wangu Monalisa Macbain ambaye angetangulia. Nilihakikisha kupatiwa chumba hicho kwa simu, nikiitumia ile sauti yangu nzito ya kiume.

Hivyo, niko hapa kama Monalisa anayemsubiri mumewe, Dkt. Freddy Macbain, mhadhiri katika chuo kikuu kimojawapo nchini Hispania. Ili kumpa uhai Dkt. Mcbain nilipenyeza vitu fulani katika mtandao kwa kumfanya aonekane kama msomi mashuhuri aliyekuwa akifanya fukuto ili kubaini kiini cha Waafrika walio wengi kugubikwa na imani za kishirikina hadi katika karne hii ya ishirini na moja kuliko wazungu ambao wengi wao wanazipuuza. Katika hali hiyo sikuona umuhimu wa kujibadili mapema kuwa mwanaume hadi wakati utakapojiri na Macbain kuhitajika. Isitoshe huchukua siku nne hadi tano kabla ya mwili huo wa bandia kuanza uasi.

Nikaendelea kuwa Monalisa, mrembo wa haja, aliyejilaza kifudifudi, peke yake, juu ya kitanda cha kifalme, ndani ya chumba cha kimalkia, akitazama Tv na kusoma magazeti. Chumba ambacho kwa ajili ya kitanda hicho, televisheni, viyoyozi na pengine vinywaji mbalimbali katika jokofu, kilinigharimu shilingi laki nane kwa siku. Pesa ambazo, hata hivyo, niliziona kama uchafu tu katika akiba yangu iliyokuwa ikifurika kwa mamilioni ya fedha za kigeni.
Nilitabasamu peke yangu pale nilipoilinganisha starehe niliyokuwa nikiifanya na hali halisi ilivyokuwa enzi za utoto wangu, hata nikurupuke kuwa mmoja wa wadunguaji wenye hadhi ya juu duniani.
Ilikuwaje?



nameless girl Khantwe davidson689 Toplady ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrangomangimezamuuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA MWISHO

Mikono ya mwanamama illikuwa imepakata silaha hiyo ya moto. Mikono hii ilionekana kujua vyema matumizi ya hii kitu. Sekunde kadhaa zilizopita alikuwa amejirusha kutoka garini baada ya kuchezwa machale na mabadiliko ya mwendokasi wa gari iliyokuwa nyuma yao. Adrian aliyekuwa amelala hakujua lolote na hata dereva aliyekuwqa ametaharuki hakushtukia tukio hili. Sasa alikuwa amerejea tena kufanya ukombozi
"Matha!!." Aliita John. Lakini huyu hakuwa Matha aliyemtambua. Huyu alikuwa mwingine kabisa. Hakutabasamu hata kidogo.
"Ukipiga hatua mbele nasambaratisha ubongo wako." Matha naye akaunguruma. Adrian hoi akiitazama filamu hii.
"Matha unasema?" alifoka John. Matha naye akafoka kwa namna ya kipekee, namna ya kuachia risasi iliyochimba pembeni kidogo ya mguu wa John.
"Uwiiii." John akapiga kelele. Hakutegemea kitendo hicho kutoka kwa Matha.
Sasa akaingiwa na uoga wa kupoteza uhai. Akatii amri akatulia tuli akiwa ameinyanyua mikono yake juu.
"John. Uonevu wako umezidi. Nakuheshimu sana lakini kwa kuipigania roho hii isiyokuwa na HATIA naapa heshima na iishe. Au lasivyo yawepo makubaliano ya amani. Adrian abaki huru bila kusumbuliwa. Hilo ni moja. Na pili..."
"Huwezi kunipangia amri Matha..." Aliingilia kati mazungumzo Adrian.
Risasi nyingine ikafyatuka. Ikatua palepale ilipotua ya kwanza.
"Nadhani unafahamu kuwa huwa sikosei nikiamua kulenga." Alisema Matha. John akaelewa mwanamama huyu ana maanisha nini. Alimaanisha kuwa anamkosa maksudi. Akiamua anamuua ndani ya sekunde moja.
John akawa mtulivu!!.
"John, umeninyanyasa vya kutosha, umefikia wakati mimi kama mwanamke nahitaji kuwa na mtoto. Nahitaji kuwa na familia yangu. Lakini umekuwa nami kipindi hicho chote hujanieleza kama una tatizo la kuzaa na kamwe huwezi kuzaa. Haukunitendea haki hata kidogo. Sasa nimejitambua na hauwezi kunipelekesha tena.
John akajisikia aibu, siri yake i wazi sasa.
Adrian alikuwa anasikia maneno baadhi na mengine hakuyasikia kutokana na hofu!!.
"Chaguo ni lako John, aidha uiache dunia ama uniache huru nikiwa na Adrian. Mwanaume ambaye alipangwa kwa ajili yangu hapa duniani." Matha alitupa mada mezani.
John akaipokea kwa uchungu!!
Hakujibu kitu.
"John!!!" Alishtua Matha. John akashtuka kwa mara ya kwanza akakiri kuwa alikuwa amewezwa.
Huyu demu ni kiboko yao. Alijisemea huku akitafuta mbinu za kujinasua.
"Niue." Alijibu John kwa jeuri.
Alitegemea Matha angeshtuka. Haikuwa hivyo!!
"Nakuua kweli." Alimalizia Matha. Akaiweka sawa bastola yake.
Mkojo ukaanza kumpenya shujaa huyu, kamanda wa makamanda. John Mapulu.
Macho ya Matha na ya John yalipotea ghafla kuelekea kelele zilipotokea. Alikuwa ni John aliyewahi kutumia mwanya huu wa kumshangaa yule dereva aliyekuwa amezimia sasa akiwa amerejewa na fahamu. Hatua moja kubwa kisha bastola ikapigwa teke na kupotelea mbali.
Kisha akajitupa kumkabili Matha kwa hasira zote. Pigo lake likawa batili likatua katika mikono ya Matha. Akayumba kidogo kisha akajiweka sawa akarusha teke la kuzunguka, chinichini likamzoa Matha akatua kama mzigo. Akatoa yowe la uchungu. Adrian akachomoka mbio mbio kwenda kumkabili John. Akakutana na teke kali katika mbavu zake akaanguka chini na kuanza kuugulia.
John alitaka kujirusha mzimamzima ammalize Matha lakini akaingiliwa na pepo la huruma. Akasogea taratibu kwenda kumjulia hali Matha. Msichana aliyempenda kupita wote duniani.
Kosa kubwa!!
Matha aliviringika ghafla. Miguu yake ikatazamana na John aliyekuwa anakaribia kuinama.
Teke likakifumua kinywa cha John akaiachia bunduki aliyokuwa ameiokota tayari. Pigo lililofuata liliadhibu korodani za John. Yowe la sasa likawa kubwa kuliko yote aliyowahi kupiga.
Maumivu yalipokolea akajikuta tena anatazama na mdomo wa bunduki.
Matha tena alikuwa anamkabili.
"Sekunde kumi za mwisho...sekunde za kutoa maamuzi." Matha alizungumza huku akitweta.
"Matha...nisikilize tafadhali." John alijishusha na kusihi.
Mara akapiga hatua kumkabili Matha. Kwa mara nyingine Matha akamwonyesha John ujuzi wake katika kulenga shabaha.
Ni jambo hili John alikuwa analisubiri.
Akaruka pembeni baada ya ile risasi kufyatuliwa. Ghafla akatua na kumkaba Adrian.
"Bora tukose wote." Alizungumza John huku akiikaba shingo ya Adrian. Matha alivyofanya jaribio la kufyatua risasi. Hola!!

******

Michael alitokomea na Joyce kwa namna ya kujifichaficha huku wakichukua tahadhari kubwa sana. Giza liliwasaidia kutoonekana kirahisi. Hatimaye wakaifikia nyumba ya kulala wageni tofauti na ile ya kwanza iliyokuwa na gharama kubwa sana. Hii ilikuwa ya kawaida.
Wakalipia wakapewa umiliki wa chumba.
Michael alikuwa mkimya kama vile ni mgeni sana mbele ya Joyce, Joyce naye alikuwa ametawaliwa na hofu!! Hakuna aliyemsemesha mwenzake kwa kitambo kifupi.
Kila mmoja alikuwa anawaza lake!! Michael hakutaka kumuamini Joyce kwa asilimia zote. Joyce naye alihisi visa vya John Mapulu tayari vimeingia katika damu ya Michael. Huenda naye ni muuaji.


Michael alizidi kuutazama usiku ulivyokuwa unaenda, akaamua kuuvunja ukimya.
"Joyce...."
"Bee."
"Hapa Mwanza sio pa kukaa tena ujue. Unayo akiba yoyote ya pesa!!."
"Ipo pesa ya yule Defao. Lakini mi sitaki kuondoka."
"Kwanini unataka kuishi hapa Mwanza."
"Kivipi tunaondoka bila kujua hatma ya Defao." Alizungumza kwa sauti ya kujiuliza peke yake. Michael akashusha pumzi zake, akamtazama Joyce na kumchukulia kama mwanamke kama wanawake wengine!! Huruma huwatawala.
Michael alifikiria kwa sekunde kadhaa huku Joyce akisubiri jawabu.
"Joy!! Natoka kidogo. Ngoja nifuatilie walimpeleka wapi wale wajinga."
Joyce akatoa tabasamu kwa kuisikia kauli ile ya matumaini.
Michael akapiga hatua kadhaa akaufungua mlango akatoweka akimwacha Joyce ndani.

Baada ya dakika tano akarejea tena. Alikuwa ana chupa ya maji ya kunywa. Akamrushia Joyce bila kusema lolote.
"Dah! Ulijuaje kuwa nina kiu? Asante sana." Alishukuru Joyce lakini Michael hakuongezea neno.

Michael alitoka pale chumbani na kujiweka nje ya chumba kwa takribani dakika kumi. Aliporejea tena yale maji yalikuwa yamefanya kile yalichoagizwa. Joyce alikuwa amesinzia bila kupenda.
Michael akampekua joyce akakutana na kibunda cha pesa, akazitwaa zote. Akatoweka.
Safari yake ikaishia hospitali.
Akanunua ugonjwa wowote ambao ungemfaa Joyce. Daktari akaandika huku akiwa ameifadhi pesa za rushwa katika koti lake jeupe.
Michael alipofanikisha kupata kibali hicho cha kuthibitisha kuwa Joyce ni mgonjwa asiyejiweza. Alirejea hotelini.
Alikuwa na bomba la sindano na dawa katika kichupa kidogo, akamdunga Joyce.
Hapa sasa akawa na uhakika kuwa Joyce hataweza kuamka kwa masaa mengi.
"Defao ndo mdudu gani hadi aendelee kukuweka Mwanza?? Ukizinduka utajikuta upo Dar.," Michael alizungumza na mwili usiosikia wa Joyce. Kisha akajiegesha naye akasinzia.
Asubuhi sana teksi ikawachukua Michael na mgonjwa wake hadi Nyegezi kituo cha mabasi.
Wawili hawa wakaianza safari ya kuelekea jijini Dar es salaam.

*****
John alitambua uwepo wa risasi moja tu katika bastola aliyokuwa nayo na kosa alilofanya Matha ni kufyatua pembeni yake baada ya kumhadaa kwa kumsogelea.
Kile kitendo cha kujaribu kufyatua halafu risasi haikutoka. Kikabariki mikono ya John kuizungusha shingo ya Adrian kuelekea upande usiowezekana hata kwa mazoezi.
Safari yake ikamalizika kimya kimya bila kelele.
Sasa Matha akawa kama aliyechanganyikiwa. Akamrukia John kwa miguu yake miwili. Akafanikiwa kumchabaga mateke kifuani. Kabla hajainuka akamuwahi tena palepale katika korodani kwa staili ya kikondoo akamfikia. Sasa ilikuwa zamu ya mikono kufanya kazi. Mikono yote miwili ilimnyonganyonga. John akajaribu kumpiga Matha kwa kutumia viwiko vya mkono Matha akiwa anapiga kelele kubwa hakumwachia John. Cha ajabu gari zilizopita hazikuthubutu kusimama. Wimbi la ujambazi lililokuwa limetanda lilimtisha kila mtu.
Sasa John akatulia hakupiga tena viwiko. Matha naye hakuendelea kunyonga. Wote wakasalia tulivu!! Walikuwa chini.
Tofauti kati yao ilikuwa moja tu!! Matha alikuwa bado anapumua na John alikuwa maiti. Matha alikuja kusimama usiku wa manane. Eneo lilikuwa vilevile. Kasoro gari moja tu ndio haikuwepo. Dereva yule aliyezinduka alitoweka.
Matha alipohakikisha Adrian tayari ameuwawa na John naye ametangulia kwenye haki. Alijikaza akaingia katika njia za waenda kwa miguu akatoweka eneo lile.
Asubuhi alikuwa jijini Arusha!! Nafsini akiugulia maumivu ya kumpoteza Adrian, hatia ya kumuua John na kubwa zaidi kumpoteza Michael. Baba wa mimba yake.
Inauma!!!

*****


Joyce na Michael baada ya kugombana na hatimaye kupatana wakiwa jijini Dar es salaam, Michael akiwa amefanya upelelezi wa kimya kimya na kutambua kuwa hapakuwa na lolote baya lililokuwa linawakabiri walikuwa wamejifunga katika maneno watakayozungumza wakishakutana na wazaz\i ama uongozi wa shule wote wakawa na majibu ya kutekwa na mtu asiyejulikana. Hawakuthubutu kutoa majibu ambayo yangeweza kuwaweka hatiani. Mzee Keto, baba mzazi wa Joyce alidanganyika kuwa hiyo ni miujiza ya mchungaji JK. Hivyo akazidi kujikita katika dhehebu hilo. Joyce baada ya kumaliza kumlilia marehemu mama yake naye alijiunga katika dhehebu ambalo familia yao ambayo aliikuta ikiwa na umasikini wa hali ya juu yote ikiamini huko.
Michael ambaye alikuwa ametajwa kama baba wa mimba ya Joyce naye aliamua kujiunga katika dhehebu hilo kwa ajili tu!! Ya kumfurahisha Joyce na si vinginevyo.
Maisha yakaendelea!!


BAADA YA MIEZI 18


Ilikuwa siku ya ubatizo wa mtoto wa Joyce ambaye baba halisi alikuwa ni Defao ambaye sasa alikuwa anasota rumande kwa kesi ya mauaji na pia kukutwa na bunduki iliyokuwa inamkabili. Lakini siri hiyo walibaki nayo Joyce na Michael pekee. Sasa Michael Msombe alihesabika kama baba halali.
Mzee Keto alikuwa na furaha sana kwani alikuwa hana mjukuu mwingine zaidi ya huyo mtoto aliyeitwa Jackson. Pia furaha yake ilichangiwa na uwepo wa mwanaye Joyce aliyekuwa amepotea na kudhaniwa kuwa amekufa.
Sasa mwanae alikuwa hai na chuo kilikuwa kimewaruhusu kuendelea kimasomo mwaka ambao unafuata. Hilo lilikuwa jambo jema.

Ubatizo ulimalizika. Na kama ilivyo kawaida hakuna ibada bila cha kunogeshea. Sasa ulifika ule wakati wa ushuhuda.
Mchungaji JK alimwaga porojo zake nyingi huku akishangiliwa na hatimaye akaanza kuwaita watu wenye shuhuda mbalimbali wazitoe ili kuzidi kuongeza imani kwa washirika.
Kanisa lilipiga vigelegele mbinja na makofi kwa mchungaji huyu machachari. Shuhuda kuu ikatanguliwa na shuhuda ndogondogo kama za kupona upele, kupata kazi, kupata mchumba na nyinginezo.
Sasa ikafuata shuhuda kuu. Hii huwasisimua watu na ni moja kati ya vipengele ambavyo huwavuta wengi kuhudhuria ibada.
"Atajitambulisha mwenyewe kwa jina, na atawaeleza Mungu amemtendea nini."
Mchungaji alisema kwa utulivu wakati mwanamama huyu akipanda katika madhabahu. Wanawake kwa ushuhuda!!!
Vigelegele vikapigwa!!
Alikuwa amevaa mavazi yanayovaliwa na watu kutoka Naijeria, mavazi yaliukaa vyema mwili wake mnene. Na kichwani alijitanda kitambaa kilichofanana na vazi lake lile.
Aliongozana na msichana aliyebeba mtoto. Makofi yaliendelea kutawala. Alipokabidhiwa kipaza sauti makofi yakapona.
Mwanamama yule akatoa salamu!! Wapendwa wakaijibu. Akakariri vifungu kadhaa vya biblia. Akapigiwa makofi.
Sasa akaanza kujieleza jinsi Mungu alivyomtendea maajabu.
Michael Msombe alikuwa amesinzia katika namna ya kujifanya ameinama akifuatilia ushuhuda huo. Isingekuwa usumbufu wa Jackson kumfinyafinya huenda hata angekuwa katika ndoto murua. Ndoto itakayomtoa nje ya kanisa kabisa na kumrejesha katika anasa za dunia.
"Naitwa Hilder Mrosso, ni mkazi wa Arusha, neno la Mungu pekee limelita jijini Dar Es salaam. Nimeolewa na nimebarikiwa kupata mtoto mmoja mimi na mume wangu. Safari yangu hadi kufikia kuokoka haikuwa fupi. Imekumbwa na vikwazo vingi hadi hapa namshukuru Mungu kwani yeye ni mwema. Mtoto wangu anaitwa Michael. Ni huyu amenisababisha nifike mbele yenu leo." Kusikia jina la mtoto Michael akainuka. Wakatazamana na Joyce wakatabasamu.
Michael akainama tena!!
Mwanamke akaendelea kutoa ujshuhuda.
"Nikiwa na mimba ya huyu Michael, niliweza kuuona muujiza wa Mungu na huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuamini katika yeye. Nilitekwa na majambazi ambao hadi leo sijui nia yao, walinitesa walinipiga sana huku wakimuua dereva na rafiki yangu. Hawakusema kwanini wananitesa. Mungu ambaye wala sikuwa namwamini alinipa nguvu. Nikajikuta napambana nao huku tumbo langu likiwa kubwa kabisa. Mwisho nikawa mshindi lakini nilijikuta peke yangu porini. Sikuwa mwenyeji wa eneo hilo lakini maajabu yake Mungu. Niliokolewa na mtu nisiyemfahamu. Akanipa huduma zote alizoweza. Mwisho wa siku nikapona kabisa. Nikaahidi nikimzaa mwanangu lazima nimlete mbele ya Mungu. Mungu huyu ni yule Mungu wa mwanaume aliyeniokoa na kumwokoa mwanangu...:" Akasita akaanza kulia, kanisa likamuunga mkono wanawake wakawa wanalia.
Michael naye akashangaa maneno yale yanamchoma akanyanyua uso akatazama mbele akatikisa kichwa kwa huzuni.
"Mwanaume ambaye ni mume wangu sasa ndiye amenifanya nimtambue Mungu. Ni muumini mzuri wa hili kanisa na ni yeye amenifanya niwe hivi. Baba Michael.." aliita yule mwanamama.
Akasimama mwanaume mtanashati akahesabu hatua akamfikia mkewe. Kanisa likapiga kelele za shangwe. Familia hii ikakumbatiana. Mchungaji JK akafanya ishara za kuwabariki.
Picha zikapigwa!!


*****
Ibada ilipomalizika, Joyce akamsihi Michael waende kupiga picha na wajina mwenzake. Michael alileta ubishi lakini tabia ya Joyce ya kuwa king'ang'anizi ikamfanya aende japo kwa shingo upande.

"Ona kalivyokufanana ..." Joyce alimtania Michael wakati amekabeba kale katoto. Michael akatabasamu.
"Mama yake yupo wapi?" joyce aliuliza.
"Huyoo anakuja." Alijibiwa. Akageuka kumtazama.
Michael naye akageuka. Mara macho yao yakagongana. Wote wakashangaana. Joyce alikuwa amejikita katika kukabeba kale katoto. Hakupata nafasi ya kuuona uso wa Michael ulivyoshangaa.
Walikuwa wamekutana ana kwa ana na Matha ambaye amejitambulisha kama Hilder katika ushuhuda.
Matha akakwepesha macho. Kisha akaingiza mkono katika mkoba akatoa kijikaratasi. Alipomkaribia Michael akampatia kisirisiri. Hakuna aliyewaona.
Michael akauelewa mchezo. Akakipokea akakihifadhi kisha akamchukua Joyce wakaondoka.
Njia nzima Michael alikuwa tofauti kabisa. Laiti kama asingesingizia kuumwa basi hakuna ambaye angeweza kumwelewa.
Alipoachana na Joyce na mtoto wake alijaribu kupiga zile namba lakini simu iliita haikupokelewa. Akahisi labda Matha bado yupo kanisani. Akairuhusu subira ivute heri.
Usiku akampigia Matha kwa namba ileile. Sasa iliweza kupokelewa.
Alikuwa ni Matha.
"Michael siamini kama tumeonana tena."
"Yaani mimi ndio sijielewi kabisa." Maongezi yakaendelea.
Sasa Matha alimweleza Michael juu ya motto kuwa ile ilikuwa damu yake. Michael alipigwa na butwaa. Ilikuwa taarifa njema sana.
"Nitakutafuta Michael tuzungumze kwa kirefu. Acha nilale kwa sasa. Yapo mengi sana ya kuzungumza mimi na wewe." Alimaliza mazungumzo Matha. Simu ikakatwa licha ya Michael kutaka kuzungumza zaidi.
Usiku ukawatwaa!! Kila mmoja na fikra zake.


****
Matha ndiye aliyevurugwa sana na hali hii y kukutana na Michael tena. Alijikuta katika hali ngumu. Ni kweli alikuwa ameolewa lakini kitu kibaya alikuwa amemweleza mumewe kuwa baba wa huyo mtoto alikufa katika ajali. Sasa Michael ameonekana.
Huruma ya Matha kwa mtoto wake na roho yake ambayo kidogo ilikuwa imeanza kutakasika vikaisumbua nafsi yake.
Hakutaka kutangatanga tena. Hakutaka mtoto wake ateseke.
Moyoni akakiri kuwa alimpenda mtoto wake kuliko huyo Michael Msombe ambaye ni baba yake.
Asubuhi ilipofika akachukua maamuzi magumu!! Akabadilisha namba za simu kwa kumdanganya mumewe kwa maneno kadha wa kadha.


Japo ilimuuma lakini alikuwa ameamua kujiweka mbali na Michael kwa usalama wa ndoa yake. Aliamini ipo siku atakuja kukutana na Michael na atadaiwa mtoto lakini hakutaka siku hiyo iwe mapema kiasi hicho.
Ikabaki kazi ya Michael kuwa anapiga simu isiyopatikana kila siku. Matha na mumewe walikuwa wamerejea jijini Arusha tayari.

*****

Hali ilivyoendelea kuwa hivyo kila siku hatimaye Michael akazoea utumwa huu wa kulea damu isiyokuwa ya kwake. Kilichomuuma zaidi ni kuwa alipata nafasi ya kupiga picha na mwanae wa kumzaa. Hiyo picha ikabaki kumuumiza kila alipoitazama. Maskini Joyce hakujua lolote.
"Ipo siku nitairejesha damu yangu. Kwa GHARAMA YOYOTE." Aliapa Michael.

*****Huu ni mwisho wa HATIA.

Khantwe nameless girl Donatila binti kiziwi Wazo Langu Sangomwile ram Toplady Jullie Z culbby mugaru mlyn Igunga Moja nrango byb sac VAN HEIST muuza ubuyu mangimeza Mamamercy mbalu Rich Pol NYIRO Wazo Langu Honey Faith peterchoka
 
Last edited by a moderator:
asante sana mkuu casuits ... mwisho mzuri wa stori kwani wale wasio na hatia wamepona na wenye hatia wamekwenda kasoro Adrian
 
Asante mkuu Casuist,Hatia tuliipenda lakini Maktaba za Kishetani imeipenda zaidi.Lakini John kafa kizembe sana.
 
Last edited by a moderator:
Habari wakuu

Nadhani wengi wetu tunamkumbuka Ben R Mtobwa, binafsi nilimsoma shuleni na alinikosha sana. Maktaba za kishetani ni riwaya yake nyingine katika mfululizo wa harakati za Joram Kiango ambazo aliandika wakati wa uhai wake.

NB: Kitabu kitatolewa January bado kipo kwenye mchakato wa kutoka. Hapa chini ni mwanzo wake. Riwaya ya HATIA leo ni mwisho na baada ya muda ntaweka tamati yake.

attachment.php


nameless girl Khantwe davidson689 Toplady ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrangomangimezamuuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru

May the almighty God rest In Peace Ben R Mtobwa kwa kazi nzuri hata baada ya kifo chake. Tupo pamoja mwanzo mwisho. Tunomba taarifa pindi kitabu hiki kitakapotoka.
 
Last edited by a moderator:

Similar Discussions

Back
Top Bottom