NYEMO CHILONGANI
DILI LA DOLA BILIONI 4
Sehemu ya Kumi na tatu
Mara baada ya kuzipata picha ambazo Oyoyo na watu wake walikuwa wakilingia nazo, Robinson na Robert wakarudi mjini Mombasa na kukaa katika hoteli ya kawaida ambapo huko wakaanza kupanga mipango yao.
Ilikuwa ni lazima wazitumie picha hizo kupata pesa nyingi kutoka kwa watu hao, ilikuwa ni lazima waionyeshe Afrika kwamba wao walikuwa watu hatari, waliopaswa kuogopwa, watu ambao walikuwa na uwezo wa kufanya mambo magumu ambayo yalishindikana kabisa.
Kitu cha kwanza kilikuwa ni kutafuta namba ya Rais Kimoni kwa lengo la kuzungumza naye na kumwambia kuhusu picha hizo.
Haikuwa kazi nyepesi kuipata namba ya mwanaume huyo hivyo walichotakiwa kufanya ni kutafuta namba za watu wengine ambao waliamini kabisa kupitia wao wangeweza kufanikiwa kuipata namba yake.
Hilo halikuwa tatizo, wakapewa namba ya Waziri wa Fedha, Bwana Machali na kuanza kuzungumza naye. Walimwambia kwamba walikuwa na ishu walitaka kuzungumza na rais.
Waziri huyo hakutaka kuwapa, alihisi kabisa kulikuwa na jambo la hatari na hata hivyo halikuwa jambo jepesi kumpa mtu asiyemjua namba ya rais wake, hivyo akawaambia kwamba hakuwa nayo.
“Unajua sisi tuna jambo muhimu sana tunataka kuzungumza naye, hebu mpigie simu, mwambie kijana mwenye zile picha za Kimeta na yule Jesca anataka kuzungumza na wewe,” alisema Robinson kwenye simu.
Machali hakujua Robinson alimaanisha nini lakini hakuwa na jinsi, alipokata simu tu, akampigia Rais Kimoni na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia kama alivyoambiwa kwamba kulikuwa na kijana ambaye alikuwa na picha za rafiki yake, Kimeta ambaye alipiga na msichana Jesca wakati wakiwa hotelini akimbaka.
Rais alivyoambiwa hivyo hakutaka kuchelewa, haraka sana akaomba hiyo namba, akapewa na kumpigia Robinson, alihitaji kuzungumza naye kuhusu jambo hilo kwa kuwa alichokiamini ni kwamba picha hizo zilikuwa kwa Oyoyo na Jesca, sasa ilikuwaje ziwe kwa mtu mwingine?
Akampigia na kuanza kuzungumza naye. Robinson alimwambia ukweli kwamba picha alizichukua kimazingaombwe tu kutoka katika simu ya Jesca ambapo zilikuwa zimefichwa na kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angeziona tofauti na yeye.
“Kwa maana hiyo wao hawana picha hizo ama?” aliuliza rais huku akionekana kuchanganyikiwa kwa furaha.
“Pigia mstari mzee baba! Yaani mimi ndiye mwenye picha hizo na si mwingine,” alijibu Robinson kwa sauti ya kujiamini sana.
Rais hakutaka kuamini, alihitaji kuziona hizo picha, hilo halikuwa na tatizo, Robinson akamtumia picha moja. Rais alipoipata, akashtuka, hakuamini alichokuwa akikiona.
Ni kweli ilikuwa picha ikimuonyesha rafiki yake, Kimeta akimbaka Jesca chumbani. Yeye mwenyewe ndiyo kwanza ilikuwa mara ya kwanza kuziona picha hizo, hakuamini alichokuwa akikiona.
Akampigia simu Robinson na kumwambia kwamba alikuwa tayari kumlipa kiasi chochote cha pesa lakini alihitaji picha hizo zifutwe na zisionekane tena kwenye dunia hii.
“Sawa! Ninahitaji dola milioni mbili, fanya haraka,” alisema Robinson kiasi ambacho kilimshtua mno rais.
“Unasemaje?”
“Nadhani umenisikia, utanipa ama?” aliuliza Robinson.
“Naomba nijifikirie!”
“Dau linaongezeka zaidi kila baada ya saa moja, ukizidi kuchelewa ndivyo ambavyo pesa itaongezeka zaidi,” alisema Robinson.
Ukimya ukasikika kwa sekunde kadhaa, kiasi alichokitaja kilikuwa ni milioni mia mbili kwa shilingi ya Kikenya na bilioni nne kwa shilingi ya Kitanzania.
Kilikuwa ni kikubwa mno lakini ili kumsaidia rafiki yake kuepuka kifungo ilikuwa ni lazima akilipe kiasi hicho cha pesa kwa sababu bila kufanya hivyo basi mtu wake wa karibu afungwe gerezani.
Akazungumza naye na kumwambia kwamba angempigia muda si mrefu kwani alihitaji kujifikiria zaidi kuhusu malipo hayo.
Mtu ambaye alikuja kichwani mwake alikuwa ni jaji, Ibrahim Kifathi ambaye ndiye aliyechaguliwa kuisimamia kesi hiyo mpaka siku ya hukumu. Akampigia simu na kumwambia kuhusu kilichokuwa kikiendelea, kulikuwa na watu waliokuwa na picha za ushahidi, kama lingekuwa jambo jema basi wazinunue ili kesi hiyo washinde pasipo tatizo lolote lile kwa sababu ushahidi ungekuwa umepotea.
Alichokisema Kifathi ni kwamba hawakutakiwa kuzinunua picha hizo kwa sababu yeye mwenyewe tayari aliseti mipango yake ili kuonekane hakuna kesi yoyote ile hivyo piga ua ilikuwa ni lazima huyo kimoni ashinde kesi hiyo.
“Kwa hiyo nisinunue hizo picha?” aliuliza rais.
“Wala usinunue! Kimeta anashinda kesi bila tatizo,” alisema Kifathi kwenye simu.
Hiyo ikaonekana kuwa nafuu kwa rais, hakutakiwa kununua picha hizo kwa kuwa alihakikishiwa kwamba kesi wangeshinda hata kama picha zilikuwepo. Hakutaka kumwambia Robinson, akaamua kumpotezea kwa kuwa aliamini jaji Kifathi alikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile.
***
Kitendo cha rais kumpigia simu Robinson lilikuwa kosa kubwa, simu ilipokatwa, alichokifanya Robinson ni kuanza kuidukua simu hiyo ili aanze kufuatilia kila simu iliyokuwa ikiingia na kutoka, siyo hiyo tu bali hata meseji ambazo zilikuwa zikiingia na kutoka.
Hilo alifanikiwa pasipo rais wala usalama wa taifa wa Kenya kuligundua. Mpaka kipindi ambacho Rais Kimoni anampigia simu Kifathi na kuanza kuzungumza naye, Robinson na Robert walikuwa wakisikia mazungumzo yao, alikasirika kwa kuwa aliamini kwamba ni kweli Kifathi alikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile.
“Tumefeli,” alisema Robert huku akionekana kukata tamaa, mazungumzo aliyokuwa ameyasikia, yalimvunja nguvu.
“Sijawahi kufeli tangu nizaliwe, na sitoweza kufeli! Hapa bado tutafanikiwa na kupata kiasi hicho ch pesa,” alisema Robinson.
Kitu ambacho kilikuja kichwani mwake ni kuhusu huyo Jaji Kifathi, alichokiamini ni kwamba kulikuwa na mambo mengi ambayo majaji walikuwa wakiyafanya ili kuwanyanyasa watu fulani mahakamani na hata kutoa hukumu ambazo hazikuwa sawa.
Aliamini hilo kwa sababu ndiyo ilikuwa hulka ya baadhi ya majaji barani Afrika. Alitaka kuzijua siri hizo na kwa sababu aliipata namba ya Kifathi, aliamini kuwa iliunganishwa na akaunti yake ya barua pepe hivyo alihitaji kuingia huko.
Kwa uwezo wake mkubwa wa kudukua, akafanikiwa kuingia kwenye barua pepe ya Kifathi na kuanza kuangalia zile zilizokuwa zimeingia na kutoka. Humo hakukutana na yoyote mbaya, zilikuwa ni zile za kawaida.
Hakutaka kuishia hapo, alichokigundua ni kwamba hakukuwa na mtu aliyeiacha barua pepe mbaya sehemu ya wazi, kama kulikuwa na mchezo aliucheza na kushirikishwa humo, ilikuwa ni lazima aifute.
Alichokifanya ni kwenda kwenye sehemu ya kufutwa barua pepe, huko alikutana na baadhi, hakuridhika, kwa kutumia programu yake ya Undelete email, aliyoiweka kwenye kompyuta zake, akaanza kuzitafuta zile barua pepe zote ambazo zilikuwa zimefutwa kabisa na hazikuwepo, ilikuwa ni sawa na kurestore vitu ambavyo vilipotea.
Hapohapo barua pepe nyingi zikaanza kujirudisha huku nyingine zikiwa na picha nyingi. Alizirudisha barua pepe zaidi ya mia moja na kuanza kuzipitia.
Huko ndipo alipokutana na vitu alivyokuwa akivitaka mno, aliweza kuziona barua pepe ambazo mwanaume huyo aliwasiliana na watu wengi waliokuwa na kesi mbalimbali na kuambiwa kwamba angepewa kiasi kikubwa cha pesa kama tu angewasaidia kushinda kesi zao.
Mwanaume wa kwanza ambaye aliwasiliana naye aliitwa Brown Williams. Huyo alikuwa mwekezaji kutoka nchini Uongereza ambaye alifika Kenya mwaka 1990 na kuwekeza katika kilimo cha kahawa.
Alipofika hapo, kutokana na matendo yake ya udhalilishaji wa wanawake waliokuwa wakimfanyia kazi ikiwemo kuwabaka na kuwapiga, akafikishwa mahakamani na jaji ambaye alisimamia kesi hiyo alikuwa Kifathi.
Baada ya kuona kwamba angeshindwa kesi hiyo na kufungwa miaka mingi, akawasiliana na mwanaume huyo na kumwambia kuhusu lile lililokuwa likiendelea.
Kwanza akamwambia angemlipa dola milioni moja na nusu kama tu angemsaidia kushinda kesi hiyo.
Walizungumza mengi kwenye barua pepe na huyo Kifathi kumwambia awamalize mashahidi wote watatu ili kusiwe na kesi yoyote na barua pepe ambayo ilifuata kutoka kwa Brown ilimwambia Kifathi kwamba tayari mashahidi waliuawa na hivyo kushinda kesi iliyomalizika mwaka 2011.
Ukiachana na hiyo pia kulikuwa na mambo mengine mengi. Robinson mwenyewe alipokuwa akiyaona, alishindwa kuamini kama kweli yule Kifathi alikuwa mtu muovu kiasi hicho.
Alizichukua zote hizo, alikuwa na ushahidi wa barua pepe na hivyo kupanga kumtafuta Kifathi ili amwambie kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea.
“Kumbe kuna watu waovu sana. Aisee yule mzee ukimwangalia unaweza kupiga magoti akuongoze sala ya toba, kumbe mshenzi tu,” alisema Robert.
“Hii ndiyo dunia! Ngoja nimtafute,” alisema Robinson na hapohapo kumpigia simu Kifathi.
Simu haikuita kwa muda mrefu, ikapokelewa na kuanza kuzungumza naye. Alijitambulisha kwa jina la The Ghost ambaye alikuwa akijua mambo mengi kwenye dunia hii ambayo yalijificha, hata yale yaliyokuwa chini ya kapeti aliyafahamu vilivyo kabisa.
“Sijajua unamaanisha nini! Unataka nikusaidie nini wewe The Ghost?” aliuliza Kifathi, kwa jinsi alivyomsikiliza Robinson, aliona kama mwanaume aliyejisifu sana.
“Unamkumbuka Brown Williams?” aliuliza Robinson.
Baada ya kulisikia jina hilo, moyo wa Kifathi ukapiga paa! Hakutarajia kulisikia, lilimshtua kupita kawaida. Robinson akabaki kimya huku akiendelea kumsikilizia mwanaume huyo, alihitaji kusikia kama angezungumza kitu chochote kile.
Alipoona amebaki kimya, akaanza kumwambia kuhusu kilichotokea kati yake na Muingereza hiyo, jinsi alivyopokea rushwa kutoka kwake, alivyomsaidia kushinda kesi yake na kuwamaliza mashahidi watatu ambao waliwekwa kwa ajili ya kesi hiyo.
Hakuishia hapo tu, alimwambia mambo mengi, kesi nyingine ambazo alizisimamia na kujifanya mtuhumiwa kushinda na wakati ushahidi ulionyesha wazi kwamba alishindwa kesi hiyo.
Kwa jinsi alivyokuwa akiambiwa kwa data, Kifathi akabaki akitetemeka, mwili ukaanza kutoa jasho jingi, hakuamini kama siri zake zingejulikana. Hakujua huyo ghost alizijuaje na wakati hata kuwasiliana na Brown alifanya kwa barua pepe tu kwa kuamini mawasiliano ya simu yangeweza kudakwa.
“How do you know all of this?” (umejuaje yote haya?) aliuliza Kifathi swali ambalo alijua wazi kabisa hakutakiwa kuuliza.
“I told you...I am the Ghost...” (nilikwambia...mimi ni mzimu) alisema Robinson na kukata simu.