Kufuatia kusambaa kwa picha mjongeo zikimuonesha kijana mmoja akiwa amenasa kwenye kibanda cha biashara katika eneo la Chadulu jijini Dodoma, Jambo TV imefika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya mashuhuda ili kupata undani wa tukio hilo.
Kijana huyo anayetambulika kwa jina la Festo, anadaiwa kunasa kwenye kibanda hicho kwa tuhuma za kujaribu kufanya wizi.Mama mwenye nyumba, anayefahamika kwa jina la Jesca Hennry, amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alimpigia simu mpangaji wake na kumueleza kuhusu kijana huyo, ambapo alijibiwa kuwa huenda mtuhumiwa huyo alikuwa mwizi na kumshauri asihusike naye.
Jesca amesema baadaye waliwasiliana na polisi ili mtuhumiwa huyo aweze kutolewa katika kibanda hicho, lakini juhudi hizo zilishindikana hadi pale mmiliki wa kibanda hicho alipomtuma mdogo wake kufika eneo la tukio na kumtoa kijana huyo, ambaye baadaye aliondoka akiwa ameambatana na jeshi la polisi.
Aidha, Jesca amewataka vijana kuachana na vitendo vya wizi na badala yake kufanya kazi halali zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha yao.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Nobert Pangaselo, amesema mtuhumiwa huyo amepelekwa kituo cha polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, huku akiwataka vijana kuachana na tabia za udokozi na vitendo vingine vya uhalifu