NYEMO CHILONGANI.
DILI LA DOLA BILIONI 4
Sehemu ya Ishirini na Tano
Kazi ilifanyika kikamilifu, Hernandez alichukuliwa na kutolewa gerezani, hakukuwa na mtu aliyejua lolote lile, wale askari wa gerezani waliendelea kuwazuia wafungwa pasipo kugundua kulikuwa na mtu muhimu sana alichukuliwa kutoka hapo gerezani.
Kila mmoja alijua kwamba hernandez alikufa na kuzikwa katika makaburi yaliyokuwa ndani ya eneo la gereza hilo, hakukuwa na yeyote aliyejua kama mwanaume huyo alichukuliwa na vijana wale watatu ambao walijifanya kutoka katika kampuni iliyokuwa ikihusika na uzikaji wa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini Marekani.
Safari ilikuwa ikiendelea, walipofika jijini Texas wakawasiliana na Kamacho na kumwambia kuhusu kile kilichotokea, walikuwa na ndugu yake mikononi mwao, walihitaji awamalizie kiasi kilichobaki ili waweze kumruhusu kumchukua mtu huyo.
Kamacho hakutaka kukubaliana nao, kwake, hilo lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo, kwa gereza kama lile alilofungwa ndugu yake, kwa jinsi lilivyokuwa na ulinzi mkubwa, jinsi alivyopambana kumtoa gerezani na kushindwa, kwake ilikuwa ni vigumu kukubaliana nao kwamba walifanikiwa kumtoa mtu huyo humo.
Hawakutaka kupoteza muda kuongea naye sana, walichokifanya ni kumpiga picha na kumtumia. Kamacho alipoziona picha hizo, hakuamini, alitamani kushangilia lakini hakutaka kufanya hivyo mpaka pale ambapo angekuwa na uhakika kwamba kweli mtu yule aliyekuwa akimuona alikuwa hernandez.
Aliwaambia kwamba alitaka kumuona ndugu yake huyo, lilikuwa jambo gumu kumruhusu mpak pale ambapo angewatumia kiasi hicho cha pesa kwani kwenye mambo makubwa na ya kibiashara kama hayo, hawakutakiwa kumuamini mtu yeyote yule.
Kwa Kamacho, japokuwa alikuwa mtu katili, lakini kwa jinsi watu wale aliozungumza nao walionekana kujiamini na bila kuwa na hofu yoyote ile, akawaambia ni lazima waondoke na kwenda Mexico, wakutane huko na kuzungumza vizuri huku wakiwa na huyo Hernandez.
Ugumu ulikuwa ni mpakani El Paso. Hawakujua kama wangevuka salama lakini kwa sababu walizungumza naye na kuwaambia kwamba kusingekuwa na tatizo, wakakubali na kuanza kuondoka kuelekea huko.
Walipofika njiani, yaani sehemu ambayo ilikuwa na janga kubwa, wakakutana na gari moja la kifahari, Audi nyeusi ambapo wakasimamishwa, wanaume wawili wakateremka huku wakiwa na bastola, kwa kuwaangalia isingekuwa tatizo kugundua kama walikuwa Wamexico, waliwasimamisha kwa kuwa walitumwa na Kamacho kuhusu mtu waliyekuwa wamembeba.
“Hatuwezi kuwaruhusu muondoke naye bila sisi,” alisema Robinson huku akiwaangalia.
“Kwa nini?”
“Kwa sababu tunahitaji kuonana naye, lakini bado hajatumalizia pesa yetu,” alijibu Robinson.
Japokuwa kwa kila mtu waliyekuwa wakimfuata na kugundua kama walitumwa na Kamacho alionekana kuogopa lakini kwa watu hao hali ilikuwa ni tofauti kabisa, hakukuwa na yeyote aliyekuwa na hofu, walijiamini kana kwamba nao walikuwa wakimiliki watu waliokuwa na bunduki na mabomu.
Hapohapo simu ikapigwa mpaka kwa Kamacho, wakazungumza naye na kumpa Robinso kuongea naye. Yeye alimwambia kwamba walifurahi kufanya naye kazi na ndiyo maana waliifanya kazi hiyo hata kabla ya kupewa pesa zote kama malipo, hivyo hakutakiwa kuwa na hofu nao hata kidogo.
“Sawa. Hao watawalete huku. Msijali kuhusu mpakani, kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Kamacho.
Kama alivyowaambia ndivyo ilivyotokea, hapo mpakani, El Paso hakukuwa na tatizo lolote lile, walivuka na kuingia nchini Mexico.
Gari liliendelea kwenda mpaka katikati ya Jiji la New Mexico ambapo hapo likaingia ndani ya jumba moja kubwa na la kifahari ambapo huko wakakutana na Kamacho aliyewapokea huku akionekana kuwa na furaha tele.
Kitu cha kwanza kabisa alihitaji kumuona kaka yake, hilo halikuwa tatizo, mlango ukafunguliwa na Hernandez kutolewa.
Alipomuona, akamsogelea, hakuwa ameamka, bado alilala kutokana na dawa ile kuendelea kuwepo mwilini mwake. Akaagiza achukuliwe na kupelekwa ndani ambapo huko akalazwa kwenye kitanda na kurudi sebuleni kuongea na vijana hao.
“Mliweza vipi kumtoa gerezani?” lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa Kamacho, hakuwa akiamini kile kilichotokea, kama vijana wake walifanya kila liwezekanalo, alitumia pesa lakini bado akashindwa, alijiuliza mno kuhusu vijana hao, walitumia njia gani mpaka kumuondoa Herandez kule gerezani?
Hawakuwa radhi kumwambia, walichokijibu ni kwamba kulikuwa na mipango ambayo waliifanya na mwisho wa siku kufanikiwa. Kwa jinsi walivyoongea, kwao, kwa kile walichokifanya kilionekana kuwa kitu cha kawaida mno ambacho wangekifanya kwa mtu yeyote yule.
Kamacho alichanganyikiwa, akagundua kwamba watu hao walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kitu chochote kile, hivyo kama lingekuwa jambo zuri basi awape kazi nyingine ya kufanya ambayo ingekuwa na malipo makubwa zaidi.
“Kazi gani?” aliuliza Robinson.
“Ni ya hatari sana, ila ina malipo makubwa,” alisema Kamacho huku akiwaangalia wote.
“Itatuingizia kiasi gani cha pesa?”
“Dola milioni hamsini kila mmoja,” alijibu huku akiwaangalia.
Robinson, Robert na Richard wakaangaliana, kwao lilionekana kuwa jambo la ajabu sana kwa mtu kama huyo kuwapa kiasi kikubwa kama hicho. Kwa maana hiyo, kwa kazi hiyo ambayo hawakuijua ingekuwa ni ipi wangelipwa sawa na kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mia moja kwa kila mmoja kwa pesa za Kitanzania.
Zilikuwa pesa nyingi sana ambazo hawakuzitarajia lakini pia hazikuwa pesa ambazo walitaka kuingiza, walichokiitaji kilikuwa ni dola bilioni nne ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni nane za Kitanzania ili kila mmoja achukue shilingi trilioni moja.
“Kazi gani?” aliuliza Robinson ambaye alikuwa muongeaji mzuri.
“Kuna watu watatu ninawahitaji mikononi mwangu,” alisema huku akiwaangalia.
“Watu gani?”
“Ni mabilionea wakubwa sana. Ni kwamba tulikuwa tukifanya biashara kwa kushirikiana kwa kipindi kirefu sana lakini baada ya kuona ninatafutwa na Marekani, wakaamua kunizika na kuchukua kiasi changu cha pesa, dola bilioni tano, wakanidhulumu, waliona kabisa siwezi kuwapata kwa kuwa siwezi kutoka ndani ya Mexico, nilikasirika sana, ninachohitaji ni kuwaona watu hao mbele yangu, niwaue kwa mkono wangu,” alisema Kamacho huku akiwaangalia vijana hao ambao muda wote vichwa vyao vilifikiria pesa tu.
“Sawa. Ila ulitapeliwa kiasi cha dola bilioni tano, si ndiyo?” aliuliza Robert.
“Ndiyo!”
“Kwa maana hiyo baada ya kuwapata, bila shaka utawaambia wakurudishie kiasi hicho cha pesa, si ndiyo?” aliuliza Robert.
“Ndiyo!”
“Sasa kama wakikurudishia dola bilioni tano, utatupa dola milioni mia moja na hamsini, yaani sisi tukuingizie dola bilioni tano halafu wewe utuingizie dola milioni mia moja na hamsini, huu ni utani Kamacho,” alisema Robert.
“Naomba mnisaidie!”
“Hilo si tatizo. Hiyo ni kazi ngumu sana, hatuwezi kukuingizia kiasi hicho na sisi kutulipa kiasi kidogo cha pesa,” alisema Robert.
Alichokisema kilikuwa kweli kabisa, kazi ambayo walitakiwa kuianza ilikuwa kubwa mno, ni ya hatari ambayo ingeweza hata kuwafanya kukamatwa, hivyo kama ilikuwa ni ya hatari sana ilikuwa ni lazima walipwe pesa nyingi pia.
Mzee Kamacho aliwabembeleza na mwisho wa siku wakakubaliana naye kufanya kazi hiyo kwa kuingiza kiasi cha dola bilioni moja kwenye akaunti yao ambacho kilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni mbili.
Hilo likawafurahisha, wakainuka na kumpa mkono wa pongezi Kamacho na kumwambia kwamba kazi ile ingefanywa katika utaalamu mkubwa, walitoka barani Afrika na kwenda Marekani mpaka hapo Mexico kwa kuwa walikua na uhitaji wa kutafuta pesa, na kama hizo zilikuwa mbele yao basi waliona ni jambo jema kama wangeziingiza kwenye akaunti zao haraka sana.
Kilichofanyika, zile pesa ambazo walikuwa wakimdai, akawaingizia kwenye akaunti yao na hivyo kuanza kazi ya kuwaambia ni kitu gani kilitakiwa kufanya.
Kulikuwa na mabilionea watatu, mmoja aliitwa Ryan Godlove, huyu alikuwa akiishi nchini Australia. Alikuwa na hoteli nyingi na za kifahari, alikuwa na hisa kubwa katika Shirika la Ndege la Orange Airline lakini pia alikuwa akimiliki ardhi ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa.
Utajiri wake ulikuwa mkubwa, alikuwa ni mwanaume mwenye pesa ambaye kwenye akaunti yake alikuwa na utajiri wa dola bilioni kumi na sita, alikuwa bilionea namba moja nchini Australia.
Ukiachana na huyo kulikuwa na mwingine aliyeitwa Scott Anderson, huyu alikuwa bilionea mkubwa nchini Ukraine. Alikuwa akimiliki hoteli nyingi, majengo makubwa na alikuwa na hisa nyingi katika makampuni mengi nchini humo.
Pamoja na kuwa na utajiri huo lakini alishirikiana na Kamacho katika biashara haramu na hakukuwa na yeyote ambaye alilifahamu hilo na utajiri wake kwenye akaunti yake ilikuwa ni dola bilioni kumi na tatu.
Ukiachana na huyo, wa mwisho alikuwa Hussein Abdoulaziz. Huyu alikuwa Mwarabu aliyekuwa akiishi Dubai. Alikuwa mmoja wa watu wenye pesa ndefu ambao walikuwa msaada mkubwa kwa nchi hiyo. Alipenda kula bata, alikuwa amewekeza katika biashara nyingi na kwenye akaunti yake alikuwa na kiasi cha dola bilioni ishirini na mbili, alikuwa ni tajiri namba sita hapo Dubai, na pesa yake ilikuwa ikiingia kupitia biashara ya mafuta aliyokuwa akiyachukua kutoka hapo Dubai na huko Kuwait.
Hao ndiyo watu ambao Kamacho alitaka kuwaona mbele ya macho yake. Hakujua alikuwa na ulinzi kiasi gani, alichokuwa akihitaji ni kuona watu hao wakiwa mbele yao. Alikuwa na hamu nao kwa sababu waliuumiza moyo wake na aliamini kabisa kwamba watu hao walikuwa na uwezo mkubwa wa kumfanya kupata alichokuwa akikitaka.
“Sawa. Dili la dola bilioni moja lipo sawa?” aliuliza Robinson.
“Hakuna tatizo! Ila nitawapata?”
“Hilo ondoa shaka. Tutaifanya kazi hiyo kama CIA. Tutafanikiwa ila utatakiwa kutupa dola milioni tano kama pesa ya kutumia katika mishemishe zetu!” alisema Robert.
“Na hizo zitakuwa ndani ya hiyo dola bilioni moja?”
“Hapana! Hiyo ni nje kabisa. Hatuna pesa kabisa, kwa hiyo tupe hiyo tuanze nayo!” aliingilia Richard.
“Basi sawa. Nitawapa pesa hiyo. Naomba sana kazi ifanyike!”
“Hakuna tatizo!”
Baada ya kukubaliana hawakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana wakaondoka kuelekea hotelini na siku mbili mbele ambapo Hernandez alirudiwa na fahamu, wakaondoka kurudi Marekani huku wakimwambia Kamacho kwamba ile kazi ambayo aliitaka ifanyike, ingefanyika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutaka kufuatilia kuhusu hao matajiri, walikuwa wakiishi maisha gani? Biashara zipi walikuwa nazo na ni kwa namna gani wangeweza kuwapata? Hiyo yote ilikuwa ni ya kufuatilia.
***
Robinson, Richard na Robert walikutana ndani ya chumba cha hoteli na kuanza kuzungumza kile kilichokuwa kikiendelea. Kulikuwa na pesa nyingi zilizokuwa mbele yao ambapo walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanazipata.
Kiasi cha dola bilioni moja ambazo kilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa pesa za Kitanzania kilikuwa kiasi kikubwa kupita maelezo, kama wangefanikiwa kupata kiasi hicho ha pesa kilimaanisha kwamba wasingekuwa na shida yoyote ile maisha yao yote na hata kama wangetumia kwa fujo bado pesa hizo zingekuwa nyingi sana mpaka kuzimaliza.
Katika kikao chao hicho wakaanza kukumbushana kuhusu maisha yao ya nyuma, jinsi walivyokuwa wamepigika lakini ghafla tu wakaanza kufanikiwa kwa kufanya mambo ya kijanja na hatimaye kuwa matajiri wakubwa wanaochipukia. Kwao ilikuwa kama ndoto, kila kitu kilichokuwa kimetokea nchini Tanzania, Kenya na mpaka hapo Marekani bado walihisi kama walikuwa wakipita katika maisha fulani hivi ya maigizo na baadaye kuambiwa picha limeishia hapo.
Pesa waliyotangaziwa na Kamacho ilikuwa nyingi sana, pesa hiyo ingetoka yote baada ya kukamilisha kazi hiyo, ilikuwa ni lazima waifanye hata kama ilikuwa ngumu kiasi gani. Walijipanga, ilikuwa ni lazima kupambana kwa asilimia mia moja na kufanikisha suala hilo zima.
Kabla ya kufanya kitu chochote kile ilikuwa ni lazima kuangalia mafaili ya watu hao, wajue walikuwa wakiishi maisha gani huko, familia zao na mambo mengine. Mtu wa kwanza kabisa ambaye walihitaji kumfanyia kazi alikuwa bilionea Ryan Godlove.
Wakaanza kumwangalia mwanaume huyo. Walisoma sifa zake nyingi lakini lililowatisha ni kuwa mwanaume huyo alisomea masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard hapohapo Marekani kabla ya kuamua kuondoka kurudi nyumbani kwao huko Australia.
Alikulia maisha ya kitajiri, mwanzo walifikiri kwamba alikuwa na akili sana mpaka kusoma katika chuo hicho kumbe haikuwa hivyo, ni kwa sababu baba yake alikuwa na pesa hivyo aliamua kumsomesha katika chuo hicho.
Kipindi hicho alikuwa na miaka arobaini na moja, alikuwa akiishi na familia yake jijini Melbourne hapohapo Australia huku akiendelea kufanya biashara zake kama kawaida. Kila mtu nchini humo alikuwa akimuheshimu, alimsikiliza na alikuwa huru kufanya kitu chochote kile kwa ajili ya watu wengine.
Hakuwa mtu wa starehe, alikuwa mtu wa kushinda nyumbani kwake na ofisini tu, alipenda kufanya kazi kuliko kitu chochote kile katika maisha yake. Kwa jinsi walivyosoma faili lake waligundua ilikuwa ni vigumu sana kumpata mwanaume huyo kwa sababu hakuwa mtu wa klabu au sehemu nyingine yoyote ile, kazi yake kubwa ilikuwa ni kukaa nyumbani na familia yake huku muda mwingine ofisini kwake.
“Hii kazi naiona kama ngumu hivi,” alisema Richard huku akiwaangalia wenzake.
“Na ndiyo maana ina pesa nyingi sana. Lakini wakati mwingine hatutakiwi kuiona kazi ngumu mpaka tuondoke na kwenda sehemu ya tukio. Hebu tuondokeni kwanza, tukifika huko ndiyo tutajua kama kazi ni ngumu ama si ngumu,” alisema Robinson.
Hilo ndilo walilotakiwa kulifanya, hakukuwa na sababu ya kupoteza muda nchini Marekani, haraka sana wakaomba viza katika ubalozi wa Australia na walipopata tu wakaondoka nchini humo kuelekea huko.
Ndani ya Ndege ya Shirika la Alliance Airlines kila mmoja alikuwa na mawazo yake, hakukuwa na mtu aliyeuona urahisi wa kazi hiyo, kila mmoja aliona kabisa mbele yao kulikuwa na ugumu mno hivyo walitakiwa kupambana mpaka kuhakikisha wanampata mwanaume huyo na wenzake na kuchukua pesa walizokuwa wameahidiwa.
Ndege ilichukua saa kumi na mbili ikaanza kutua katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Melbourne ambapo wakateremka na kwenda nje ambapo wakaingia ndani ya gari la wateja waliokuwa wakifikia katika Hoteli ya nyota tano ya Bayview Eden iliyokuwa pembeni kidogo mwa jiji hilo.
Walipofika, wakachukua vyumba vitatu ambavyo waliweka oda na kabla ya kulala ilikuwa ni lazima kukutana na kuzungumza kile kilichokuwa kikiendelea. Mipango ilitakiwa kusukwa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufahamu mahali mzee huyo alipokuwa akiishi, baada ya kujua huko ndipo wangeanza kufikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya.
Hapo, wakajifanya kama wageni waliofika kwa lengo la utalii, siku iliyofuatwa wakaanza kutembezwa sehemu mbalimbali huku wakijifanya kupiga picha kila kitu kilichoonekana kuwa kigeni. Walizungumza na watu wengi, waliwaambia kwamba wao walikuwa Wamarekani ambao walifika hapo kwa lengo la kuitazama Australia kwani hawakuwahi kufika.
Kuamini kama hawakuwa Wamarekani weusi ilikuwa vigumu mno kwani kwa jinsi walivyokuwa wakiongea kwa slang, ilikuwa ni lazima kuamini kila kitu walichokuwa wakikizungumza.
Kutokana na ucheshi wao mkubwa wakapata marafiki wengi ambao waliwatembeza sehemu mbalimbali lakini lengo lao kubwa lilikuwa ni kutaka kujua mahali alipokuwa akiishi Godlove.
Siku hiyo hawakutaka kuwa na presha yoyote ile, ilikuwa ni lazima kujifanya wageni wakubwa na siku zinazofuata ndiyo ambazo wangetumia kuuliza mambo mengi kuhusu mwanaume huyo.
Hapo Melbourne mtu ambaye walimpata kwa ajili ya kuwatembea huku na kule alikuwa kijana mdogo wa makamo yao aliyeitwa Pegg Ball. Kijana huyo ndiye alichukua jukumu la kuzunguka naye huku wakimwambia kwamba wangemlipa kiasi cha dola elfu mbili kila siku huku kula na vitu vingine vikiwa ni juu yao.
Ilikuwa pesa nyingi kwake ambayo ingemfanya kuwafanyia kitu chochote kile ambacho watu hao wangekihitaji. Walihitaji kumzoea kwa siku kadhaa, kama mbili hivi ndipo wakaanza kumuuliza kuhusu bilionea Godlove.
“Ryan Godlove! Kuna watu wana pesa bwana!” alisema Ball huku akiwaangalia.
“Huwa anaishi wapi?”
“Mh! Anaishi wapi?”
“Seacombe Grove upo katika mji mdogo wa Brighton,” alijibu Ball.
“Mtaa huo upo vipi?”
“Ni wa kitajiri sana! Sisi walalahoi huwa haturuhusiwi kufika huko,” alijibu.
“Kwa nini?”
“Utaanzaje kufika huko? Umesahau kitu gani? Kuna ulinzi wa kila aina! Mnamuulizia sana, kuna lolote mnahitaji?” aliuliza Ball huku akiwaangalia.
“Yeah! Tunahitaji kufungua kampuni ya utalii! Sasa tunahitaji kukutana naye,” alijibu Richard.
“Sasa si muwasiliane naye?”
“Sasa tutawasiliana naye vipi?”
“Kwani hamna namba yake?”
“Hatuna. Wewe unayo?”
“Hapana!”
“Hata sehemu ambayo tunaweza kuipata?”
“Hapana! Sijui sehemu yoyote ile,” alijibu Ball kikawaida pasipo kugundua watu hao walikuwa na mpango gani kwa huyo bilionea.
Ball hakuonekana kuwa na msaada wowote ule zaidi ya kuwatisha kwamba mtaa aliokuwa akiishi Godlove haukuwa ukiingilika na watu wengine kwa sababu kulikuwa na ulinzi mkubwa mno.
Hawakutaka kukata tamaa, walifika nchini Australia kwa ajili ya mwanaume huyo na ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha wanampata na kuondoka naye kwenda kumficha sehemu fulani.
Waliendelea kukaa nchini humo kwa siku kadhaa huku kila siku wakawa wanaonana na kuzungumza kama namna mojawapo ya kuona kama kulikuwa na njia nyingine ambayo waliipata kuitumia kumuingiza mwanaume huyo katika mikono yake.
Baada ya kukaa kwa wiki moja huku Kamacho akiwapigia simu na kuwauliza walipofikia ndipo wakapata wazo la kwenda ofisini kwake. Hawakupajua lakini waliamini kama wangemuuliza Ball angewaambia mahali alipokuwa akifanyia kazi.
Haraka sana wakamuuliza, alichowajibu ni kuwa hakufahamu ofisi yake ilipokuwa ila angeweza kuuliza na kuwaambia, hivyo walitakiwa kusubiri kwa siku moja mpaka atakapokutana na marafiki zake.
“Hivi nyie huyu Ball mnamuonaje? Mimi naona kama anatuzingua. Manake kila kitu hafahamu, sasa wa kazi gani?” aliuliza Robert huku akionekana kuwa na hasira.
“Kama vipi tumteme!”
“Hapana! Tumeanza naye mbali, amesema kwamba atawauliza marafiki zake, tumpeni muda, tutajua tu,” alisema Robinson.
Hilo ndilo walilolifanya, kwa sababu kijana huyo alihitaji muda, akapewa na siku iliyofuata akawapa majibu kwamba mwanaume huyo alikuwa akifanya kazi katika jengo kubwa la Richmond lililokuwa na ghorofa ishirini na nne na ofisi yake ilikuwa ni kuanzia ghorofa ya kumi na nane kwenda juu.
Kulikuwa na wafanyakazi wengi humo na kampuni hiyo ilikuwa ikijihusisha na mambo ya majengo. Wakapanga na hivyo kumtuma Richard kuelekea huko. Alitakiwa kujua kila kitu kilichokuwa kikiendelea, ofisi ilikuwaje na kulikuwa na ulinzi gani mpaka kumuona bosi huyo, yaani kwa kifupi alitakiwa kujua kila kitu.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema Richard akaondoka kuelekea huko. Hakuchukua muda mrefu akafika na kuhitaji kuonana na meneja wa ofisi hiyo ambapo akasaini na kupewa kitambulisho maalumu na kuanza kupandisha juu kwa kutumia lifti.
Kwa jinsi alivyovaa, alipendeza, alivalia na miwani iliyomfanya kupendeza kupita kawaida na kwa jinsi alivyokuwa na sura nzuri, kila msichana aliyekuwa akimuona, alichanganyikiwa, alipendeza na wengi walitaka japo kuisikia sauti yake.
Hakuzungumza na mtu yeyote mpaka alipofika katika ghorofa husika, akateremka na kwenda sehemu ambapo akapewa kitambulisho kingine na kuruhusiwa kuingia ndani. Kila alipopita, kulikuwa na kamera, alikuwa makini, aliziangalia huku akiwaza ni kwa namna gani wangefanikiwa kuingia humo na kuondoka na mtu huyo.
“Ninahitaji kuonana na meneja wa ofisi hii,” alisema Richard sehemu ya mapokezi.
“Una miadi naye?”
“Hapana!”
“Huwezi kuonana naye!”
“Kabisa?”
“Kabisa!”
“Hata mkurugenzi?” aliuliza.
Wasichana waliokuwa hapo mapokezi waliangaliana, wakaanza kutoa tabasamu. Hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angefika mahali hapo na kumuulizia mkurugenzi. Kumuona Godlove lilikuwa jambo gumu sana, si kwa watu wengine, hata kwao pia, kama wafanyakazi hawakuwa na uwezo wa kuusogelea mlango wa ofisi yake na kuzungumza naye.
Godlove alikuwa mtu wa kazi nyingi, hakuwa na muda wa kuzungumza na watu humo, alipenda kukaa peke yake akifanya mambo yake kivyakevyake na taarifa zote kuhusu ofisi alikuwa akipelekewa na meneja wake, ilikuwaje Richard afike mahali hapo na kutaka kuonana na mkurugenzi wao.
“Mbona mnanicheka?” aliuliza Richard huku akitabasamu.
“Hatukucheki! Bali tumeshangaa!”
“Mmeshangaa nini?”
“Kumuulizia mkurugenzi. Hivi unamjua Godlove kweli?” aliuliza msichana mmoja.
“Na ndiyo maana nilihitaji kuzungumza naye.”
“Samahani! Huwezi kumuona.”
“Hata nyumbani kwake?”
“Yaani huko ndiyo kabisaaaa.”
“Kwa hiyo huwa haonekani?”
“Inawezekana!” alijibu msichana mmoja.
***
Richard hakuzungumza kitu, alibaki akiwaangalia wasichana wale, walimjibu kwa nyodo kiasi kwamba mpaka akasikia hasira moyoni mwake. Hakutaka kuona akiendelea kudharauliwa vile, alichowaambia ni kwamba alihitaji kuondoka na angerudi siku nyingine.
Wakati akiondoka, wasichana wale walibaki wakimwangalia. Walishangaa, mtu ambaye alisimama mbele yao sekunde chache zilizopita alikuwa mzuri wa sura na waliamua kumzingua makusudi ili waweze kupata kile walichokuwa wakikihitaji.
Haraka sana msichana mmoja akasimama na kumuagiza mlinzi aliyekuwa humo amsimamishe na kumwambia arudi. Mlinzi huyo alifanya kama alivyoambiwa, huku akiendelea kuwa humo ofisini, akasimamishwa na kuambiwa kwamba alikuwa akihitajika, hivyo akarudi.
Kwa muonekano ambao walionekana wasichana hao kipindi hicho hakuwa na maswali mengi kwamba ni kitu gani walikuwa wakihitaji, macho yao yalionyesha kila kitu, akatoa tabasamu kidogo kitu kilichowachanganya wasichana hao.
“Umekasirika?” aliuliza msichana mmoja, swali la kipumbavu kabisa kwa Richard, akakosa jibu, akabaki akiwaangalia kwa zamu tu.
“Tulikuwa tunataka kuuona msimamo wako. Naitwa Rose,” alisema msichana mmoja huku akimpa mkono.
Richard akashusha pumzi ndefu, hakuamini alichokuwa akikiona mahali hapo, wasichana haohao walimjibu kidharau huku wakimwambia lingekuwa jambo gumu kuonana na Godlove lakini mwisho wa siku akashangaa kuona akiitwa na kuulizwa swali hilo.
“Jamani naomba tusamehe. Mimi naitwa Gwen,” alisema msichana mwingine, naye akampa mkono.
Kwa kuwa lengo lake halikuwa limefanikiwa ndani ya ofisi hiyo, Richard akatoa tabasamu pana na kuanza kuzungumza naye. Kitu walichokihitaji ni kwamba walitaka kula naye chakula cha mchana katika mgahawa wa ofisi hiyo na huko wangeongea mengi kuhusu Godlove lakini pia wangemsaidia kuonana naye.
“Ila mliniambia kwamba haiwezekani!” alisema Richard.
“Tulisema, ila nahisi inaweza kuwezekana,” alisema Rose.
Yeye ndiye alikuwa na shida ya kuonana na Godlove hivyo hakuwa na jinsi, alihitaji kuwasikiliza wasichana hao kujua ni kitu gani walikuwa wakihitaji. Alibaki humo huku akizungumza nao mambo mengi, walifahamiana kwa mengi lakini kwenye yote ambayo aliyazungumza, hakutaka kuwaambia ukweli alikuwa nani hasa na alitoka wapi.
Ilipofika majira ya saa sita mchana, wakatoka na kwenda mgahawani. Kila mtu alikuwa akimwangalia Richard, alikuwa mwanaume mzuri, mpole ambaye hata kutembea kwake ilikuwa ni rahisi kugundua kama alikuwa mtu aliyejiheshimu.
Wakaelekea mpaka kwenye mgahawa huo na kuanza kula chakula. Muda wote Richard alionekana kuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria huyo Godlove, japokuwa kimwili alikuwa mahali hapo lakini mawazo yake yalikuwa sehemu nyingine kabisa.
Walizungumza mambo mengi, wasichana wale walijisikia raha kuzungumza naye. Uzuri wake wa sura uliwafanya mpaka wengine kuja pale na kuwasalimia, walichokihitaji ni kumsikia Richard akiongea, sauti yake ilifananaje? Alikuwaje kwa karibu?
“Unamfahamu Godlove?” aliuliza Gwen.
“Kwa kumuona kwenye picha, ila si uso kwa uso,” alijibu Richard.
“Kwa hiyo ulikuwa unakuja kumuona mtu ambaye hukuwahi kumuona ana kwa ana?”
“Ndiyo! Kuna biashara ningependa kufanya naye, hivyo nilihitaji ushauri wake kidogo!”
“Biasharara gani?”
“Kuchuna watu ngozi!” alijibu Richard huku akitabasamu, tabasamu lililowafanya wasichana wote hao kuanza kucheka kwani walijua alidanganya na hakutaka kuwaambia ukweli.
Hawakujua jinsi ya kumsaidia, na hawakuwa na uwezo huo ila ilikuwa ni lazima waonyeshe kwamba wangemsaidia ili wamtie katika mikono yao. Walichomwambia ni kuwaachia namba ya simu, wao wangezungumza na Godlove na kupanga siku ya kuonana kwani walimwaminisha kwamba kwao asingeweza kupindua hata kidogo.
Richard hakuwa na jinsi, akafanya hivyo, akawapa namba yake na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulikuwa na uhakika kama angefanikiwa na hata alipofika kwa wenzake aliwaambia kazi ilikamilika na ni kitu kidogo tu ndicho kilikuwa kimebaki.
“Kwa hiyo wamesema watakupigia simu?” aliuliza Robinson.
“Ndiyo! Watanipigia!”
“Una uhakika?”
“Kabisa! Hawawezi kunidanganya. Hivi unaweza kweli kumdanganya handsome kama mimi?” aliuliza Richard huku akiwaangalia wenzake.
Hawakumjibu swali lake, walibaki wakiangaliana tu na kuendelea na mambo yao. Wakati hayo yote yakitokea huku akiendelea kusubiri simu kutoka kwa Rose na Gwen ndipo akaanza kuyafikiria maisha yake.
Suala la Upendo lilimuumiza kichwa chake, bado alimfikiria msichana huyo mno, alimwambia kwamba alikuwa na mimba yake, alichokikumbuka ni kwamba siku zote amekuwa mtu wa kutumia kinga na hakukumbuka kama kuna siku aliwahi kufanya bila kinga.
Aliambiwa kwamba siku ile ambayo mpia ulipasuka ndipo mimba hiyo ilipoingia, hakukubaliana na hilo kwa sababu siku hiyo aliikumbuka vilivyo. Alihisi kabisa kulikuwa na jambo nyuma ya pazia, moyo wake ulimwambia asubiri mpaka pale ambapo mtoto angezaliwa ili aone kama kweli alikuwa wake ama la.
“Nitapima DNA,” alisema Richard.
Hilo ndilo lilimjia kichwani mwake lakini bado alikuwa na mambo mengine mengi ambayo yalimsumbua. Hofu aliyokuwanayo kuhusu ujauzito huo ilikuwa kubwa kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe akabaki akishangaa.
Alichokifanya ni kuwashirikisha wenzake, ilikuwa ni lazima wajue kile kilichokuwa kichwani mwake, aombe msaada ili kujua ni kitu gani wangemshauri katika suala hilo.
“Hofu yako nini?” aliuliza Robert.
“Hiyo mimba jinsi ilivyoingia!”
“Sasa wewe unaogopa nini?”
“Yaani nina hofu kubwa sana. Mimi sijawahi ndani, sasa hiyo mimba imeingiaje mazee?’ aliuliza Richard.
Marafiki zake hao wakaangaliana na kuanza kucheka. Walijua ni kwa jinsi gani aliumia, waliujua ukweli kwamba Richard hakumpenda Upendo hata kidogo, alifanya mambo yote yale kwa sababu tu kulikuwa na sababu ya hayo yote.
Richard alikuwa siriazi kuwaambia wenzake kuhusu mambo yake yaliyokuwa yakimsumbua lakini wenzake ndiyo kwanza walikuwa wakicheka na kumwambia kwamba mimba ni yake na alitakiwa kumlea mtoto, asikimbie majukumu hata kidogo.
“Mtoto wako huyo, litakuwa bonge la handsome?”
“Naomba tusikilizane! Tuacheni utani, naomba mnisaidie, tufanye nini katika hili!” alisema Richard huku akionekana kukasirika.
“Hakuna cha kushauriana. Tusubiri mtoto azaliwe kwanza!”
“Nyie hamuoni kama nitakuwa nimeuziwa mbuzi kwenye gunia?”
“Kwamba ulipiga lakini mtoto siyo wako au kuna jamaa mwingine alimfuata Upendo na kupiga kisha akapata mimba? Richard! Come down. Hivi kuna jamaa gani hapa anaweza kutembea na Upendo zaidi yako?” aliuliza Robert huku akimwangalia Richard ambaye alionekana kuwa na hasira zaidi.
Richard hakuzungumza kitu, akaachana na suala hilo akaendelea na mambo yake kama kawaida. Siku iliyofuata akapokea simu kutoka kwa namba ngeni, alipoichukua na kuipokea, akagundua kwamba ilitoka kwa Rose hivyo akaanza kuzungumza naye.
Msichana huyo alimwambia kuhusu kuonana naye, alikuwa na mengi ya kumwambia hivyo ilikuwa ni lazima kukaa sehemu na kuzungumza naye kwa kirefu kuhusu huyo Godlove aliyekuwa akihitaji kuonana naye.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akawaambia wenzake kwamba mambo yalitiki na hivyo alitakiwa kuondoka kwenda kuonana na msichana huyo mahali na kuzungumza kile alichokuwa akihitaji.
Akaondoka na kwenda kwenye mgawa wa Marrybrown uliokuwa hapohapo Melbourne. Waliponana, wakatafuta kiti na kutulia, wakaanza kuzungumza, kitu alichotaka Rose kumwambia Richard ni kuhusu moyo wake, jinsi alivyompenda mwanaume huyo lakini kichwa cha Richard muda huo kilikuwa kikifikiria kuhusu Godlove, mwanaume ambaye aliamini kwamba kama angebahatika kuonana naye, basi kila kitu kingekwenda kama kilivyotakiwa.
***
Upendo alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Richard, hakujua ni kitu gani ambacho kingetokea kama siku moja mwanaume huyo angekuja kugundua kile kilichotokea.
Hakutaka kuona hilo likitokea, alichokifanya kilikuwa siri kubwa na ndiyo maana hata wahusika ambao alishirikiana nao walikuwa ni Wazungu, watu waliosafiri kutoka mbali kabisa na kwenda kuifanya kazi hiyo.
Hakuwa na amani, moyo wake ulikuwa na mawazo tele, alichokifanya alijua kabisa hakikuwa sawa lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kitokee kile kilichotokea kwa sababu tu mwanaume huyo hakuwahi kukubali kufanya naye mapenzi bila kutumia kinga.
Aliendelea kwenda hospitalini, alihitaji kujua kuhusu afya yake, aliwasiliana na baba yake na kumwambia ukweli kuhusu mimba hiyo, mzee wake alifurahi sana, aliwapigia simu marafiki zake na kuwaambia kwamba hatimaye binti yake alipata mimba.
Mzee mwenyewe alijua jinsi binti yake alivyokuwa mbaya, hakuwahi kuhisi kama kungetokea mwanaume yeyote ambaye angemfuata na kumwambia nakupenda, hivyo hakuwa na uhakika kama kuna siku Upendo angekuja kufanya mapenzi na mwanaume, mtu huyo ambaye angejitolea kufanya naye basi alikuwa na moyo wa kishujaa sana.
Alimuuliza mara mbili mbili kama kile alichokizungumza kilikuwa kweli ama la, alimhakikishia kwamba ni kweli alikuwa mjauzito, akaona hiyo haitoshi, akamuonyeshea mpaka vipimo alivyokwenda kupima hospitalini, aone jinsi majibu yalivyokuwa.
Mzee Massawe alichanganyikiwa mno kiasi cha kuanza kulengwa na machozi machoni mwake. Hakutegemea kupata majibu hayo kwamba binti yake alipata mimba, hakutaka kujua ni mwanaume gani alimpa hiyo mimba, yeye alichokifurahia ni kile kilichokuwa tumboni mwa Upendo tu.
Hakutaka kuwasiliana tena na Richard, alijua kabisa mwanaume huyo hakuwa akimpenda, alifahamu kabisa kama alikuwa na ugumu wa kuikubali mimba hiyo, alimwaha aendelee na maisha yake lakini alichokuwa akikiangalia ni kwa jinsi gani mtoto wake huyo angeishi baada ya kuzaliwa.
Wiki ya pili baada ya Richard kuondoka na wenzake kuelekea nchini Marekani ndipo akapokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakumfahamu. Simu ile ilitoka kwa namba ambayo ilipigwa kutoka nchini Tanzania na mtu aliyekuwa akisikika alikuwa ni mwanamke ambaye alikuwa na kitu cha kumwambia.
“Kitu gani?” aliuliza Upendo huku akionekana kuwa na wasiwasi kwani kwa jinsi alivyokuwa akiongea, ilionyesha kulikuwa na jambo kubwa mno lililokuwa likiendelea.
“Nasikia una mimba ya Richard!” alisema msichana huyo. Alishtuka, suala la yeye kuwa na mimba alilifanya siri, hakutaka mtu mwingine yeyote afahamu zaidi yake na Richard tu, akahisi kwamba mwanaume huyo ndiye aliyekuwa amemwambia mtu aliyekuwa akiongea naye.
“Haikuhusu dada!” alisema.
“Najua! Ila ni afadhali hata ungeipata kwa kupitia ile kitu, yaani yenyewe. Kumbe mimba yenyewe ni ya kutengeneza! Yaani mwanamke mtu mzima unafanya Surrogation. Na Richard hajui, ila ni lazima nitamwambia,” alisikika mwanamke huyo kutoka kwenye simu.
Moyo wa Upendo ukapiga paaa! Hakuamini alichokuwa amekisikia kutoka kwa msichana huyo. Hakuwa na la kusema, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kile alichokisikia kilikuwa kama ndoto.
“Unasemaje?” aliuliza kwa hofu lakini hapohapo simu ikakatwa.
Akasimama pale kwenye kitanda na kuanza kuzunguka huku akiita lakini hakukuwa na majibu yoyote yale kwenye simu. Hilo lilimchanganya mno, kile alichokifanya kilikuwa ni siri kubwa, ni yeye na Manka tu ndiyo waliokuwa wakijua kuhusu mimba ile.
Mwili wake ulikuwa ukitetemeka mno, alitamani kumfahamu mtu huyo, ampe pesa ili asiweze kutoa siri hiyo. Alijua kungekuwa na tatizo kubwa endapo angethubutu kuufumbua mdomo wake na kumwambia Richard kwamba ile mimba aliyokuwanayo ilikuwa ni ya kutengeneza, aliiona kabisa aibu kubwa ikija mbele yake.
“Haiwezekani!” alijisema Upendo, hakutulia hapo chumbani, alikuwa akihangaika, na kilichomchanganya zaidi ni kwamba kila alijaribu kumpigia simu mwanamke huyo, hakupatikana.
Upendo alizidi kuchanganyikiwa, siri ambayo aliamini ingedumu milele katika maisha yake kumbe upande wa pili kulikuwa na mtu ambaye alifahamu kila kitu, hiyo ilimuuma sana na muda mwingine alihisi kabisa kungetokea tatizo fulani kama tu asingemnyamazisha mtu huyo kuufumba mdomo wake.
Hakuwa na raha tena, muda wote alikuwa na mawazo tele, alihitaji mimba ya Richard, aliipata lakini hakuwa na amani hata kidogo. Moyo wake ulimuuma, alitamani kuonana na mwanamke huyo na kumuomba sana, asimwambie Richard kwani endapo angejifanya mjanja basi kusingekuwa na siri tena.
Alichokipanga ni kumtafuta mtu huyo, ilikuwa ni lazima afanye hivyo kwani hakutaka kuona akipata aibu kubwa. Alikuwa na pesa, aliamini katika jambo lolote lile, kama angetumia pesa basi lisingekuwa tatizo lolote lile, kusingekuwa na kitu chochote ambacho kingeharibika.
Alikuwa na mawazo, hakumwambia mtu yeyote yule, aliendelea kuwa hivyohivyo na hata wazazi wake walipomuuliza juu ya kile kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kuwaambia lolote lile zaidi ya kujifanya hakukuwa na kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea.
Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, ya pili ikaingia, siku ya tatu akapigiwa simu na namba ileile na kuanza kuzungumza naye. Kitu cha kwanza, Upendo akaanza kumuomba sana asimwambie Richard kwani alijua endapo angefanya hivyo mwanaume huyo angeweza kumfunga.
“Hakuna shida. Utatakiwa kuulipia mdomo wangu usitoe siri,” alisema mwanamke huyo kwenye simu.
“Niambie kiasi chochote kile,” alisema Upendo.
“Ninahitaji bilioni moja kuunyamazisha mdomo wangu,” alisema msichana huyo.
Upendo akashtuka, hakuamini kama mtu huyo angehitaji kiasi kikubwa cha pesa namna hiyo, alichohisi ni kwamba angehitaji milioni kumi ama ishirini.
Alibaki akitetemeka, akaishiwa pozi la kuongea, simu ilikuwa sikioni mwake lakini alikuwa kimya kabisa.
“Kwa heri,” alisema mwanamke huyo baada ya kuona ukimya umekuwa mkubwa.
“No! Naomba usikate simu!” alisema Upendo.
“Sasa mbona huongei?”
“Umeniambia kiasi kikubwa sana. Bilioni moja?”
“Kwa hiyo hiyo unaiona nyingi sana? Hivi hujui kesi ikifika mahakamani Richard anaweza kuhitaji kiasi gani? Hujui waandishi wa habari wakiiandika habari yako utapata aibu kiasi gani? Jamii itakuonaje? Upendo! Baba yako ana pesa sana, fanya unitumie hiyo pesa, vinginevyo, nitamwambia Richard akirudi kutoka alipokwenda,” alisema mwanamke huyo.
“Naomba unisaidie mwanamke mwenzako!”
“Niambie kitu kimoja! Utatoa pesa hiyo au hautotoa?” aliuliza msichana aliyesikika kwenye simu, alionekana kuchoshwa na vilio vya Upendo, alihitaji kusikia jibu moja tu.
“Naomba unionee huruma!”
“Hilo si jibu ninalolitaka. Niambie! Utatoa au hutotoa?” aliuliza tena.
Upendo hakujua ni kwa namna gani angelijibu swali hilo, jibu lake lilikuwa jepesi mno, yaani ni ‘ndiyo’ au ‘hapana’ lakini hakuwa radhi kutoa jibu lolote lile.
Aliendelea kuomba sana lakini mwanamke huyo hakumuelewa hata kidogo. Alisisitiza kwamba ni lazima amwambie Richard kilichofanyika kama tu hakutaka kutoa kiasi cha pesa alichokuwa amekitaka.
Upendo akafikiria biashara zake, akamfikiria baba yake na mwisho wa siku akamwambia mwanamke huyo kwamba alikuwa tayari kutoa kiasi hicho cha pesa, ila alihitaji kupewa mwezi mmoja mpaka kukamilisha mpango huo.
“Sawa. Haina shida. Leo ni tarehe kumi, inamaana mpaka tarehe kumi ijayo nataka pesa iwekwe kwenye akaunti hii, 01J2030341600,” alisema mwanamke huyo.
“Sawa.”
Simu ikakatwa.
Kwa sababu ya maombi ya watu ya kuihitaji hadithi hii kuwa kwenye mfumo wa kitabu, maombi yao yanafanyiwa kazi kwa maana hiyo sasa humu ninaikata na kuahidi kuitolea kitabu mwaka kesho. Kitabu kitakuwa na kurasa zaidi ya 300, kitakuwa kimeshiba na mambo mengi yatasimuliwa huko mbeleni.
Ila sitowaacha hivihivi bali nitawaletea simulizi ndefu pia iitwayo SEX ADDICTED Yaani Muathirika wa Ngono. Itakuwa ni hadithi inayohusu maisha ya msichana aitwaye Cindy ambaye alizaliwa na mwanamke kahaba, alilelewa huko, ila watu wakataka kuutumia mwili wake kuwakamilishia mambo yao wakiwemo wachungaji na mabilionea.
Hutakiwi kuikosa hii. Hiyo itaanza na kuisha humuhumu..
Ahsanteni.
Ahsanteni sana.