Riwaya - Balaa

Riwaya - Balaa

SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY.
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA NANE

Kundi la Six killers walikuwa wamejipanga vizuri sana huko Kilwa Kivinje. Kutokana na kutokuwepo kwa Tano, ratiba zao zilibadirika kidogo. Kazi ya kumuwinda Dokta Yusha sasa alipewa Sita. Huku waliobaki walikuwa wanalinda eneo la chumba cha kuhifadhia maiti ili operesheni yao ya kutoa mioyo iliyotarajia kufanyika usiku wa siku hiyo iende vizuri. Kwa bahati nzuri siku hiyo ilitokea ajari ya basi katika kijiji cha Somanga. Ajari ilioua watu thelathini na kujeruhi saba, Six killers walikuwa na uhakika wa kupata mioyo thelathini ambayo, mara mbili ya oda yao, bahati ilioje?

Saa moja usiku Dokta Yusha alielekea Kilwa Kivinje. Kwenda kuwaangalia watu aliowapenda sana. Ambao sasa walikuwa wagonjwa, Mkewe kipenzi Nasra, rafiki wa mkewe, Hasina na mkwe wake. Njiani roho ilikuwa inamdunda sana, bila kujua kwanini hali ile ilimtokea. Laiti Dokta Yusha angejua anayoenda kukutana nayo huko basi angeusikiliza moyo wake, Dokta Yusha alikuwa anaenda kwenye balaa kubwa sana!
Na moyo wake uliligundua hilo mapema sana. Lakini hakuusiliza moyo wake, au labda hakuuelewa moyo wake unamaanisha nini?

Nusu saa ilitosha kumfikisha Dokta Yusha Kilwa Kivinje. Na moja kwa moja alienda katika wodi waliolazwa wakina Nasra. Hali ya wagonjwa wale wawili ilikuwa vilevile. Mkewe kipenzi Nasra na rafiki wa mkewe
Hasina walikuwa wamelala katika usingizi ule mbaya, usingizi nzito usiojulikana mwisho wake. Huku Mzee Mpaukha naye akiwa kalala kwa kujifunika nusu shuka safi ya hospitali, shuka iliiyoiashia kifuani, uso ukiwa wazi. Dereva alikuwa amejifunika shuka la hospitali gubigubi sawa na mgonjwa mwengine aliyelala kitanda cha pili toka pale alikolala dereva.

Kumbe jirani yule alikuwa ni Sita wa Six killers, akiwa amejificha kwa kujifunika gubigubi katika kitanda kimoja katika wodi ile. akiwa amepania kummaliza Dokta Yusha kabla hajaenda katika jukumu lake lengine la usiku ule.

Dokta Yusha kama kawaida yake alienda kwenye kitanda alicholala mkewe kipenzi, Nasra, alimwangalia kwa muda mkewe, bado alikuwa katika hali ya kutia shaka. Alipiga hatua chache na kukisogelea kitanda cha Hasina, nae alikuwa taabani kwa ajari ile. Alisogea tena hadi kitanda alicholazwa Mzee Mpaukha, Mzee Mpaukha alikuwa amelala, hakutaka kumsumbua, alimshuhudia akipumua vizuri. Alikiangalia kitanda alicholazwa dereva wa Mzee Mpaukha, alimwona amejifunika gubigubi. Alikisogelea taratibu kile kitanda, alikuwa anasogea Huku akiiona kuwa kitanda cha pili kutoka kitanda cha dereva Musa nacho kulikuwa na mgonjwa aliyejifunika gubigubi kama Musa, alipanga kwenda kumwangalia nae, bila kujua dhamira mbaya ya mgonjwa aliyelala kitanda kile. Kitanda kililaliwa na Sita wa Six killers. Na lengo lake kuu ni kumuuangamiza Dokta Yusha...

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY

SEHEMU YA THELATHINI NA TISA

Dokta Yusha alifika kitanda alicholazwa dereva Musa. Aliifunua lile shuka na kumwangalia Musa usoni. Alistuka sana!
Alikuwa daktari, na hakuhitaji kifaa chochote kile kutumia ili kumpima dereva Musa, macho ya kidaktari yalitosha kumwambia kwamba alikuwa anatazamana na mtu ambaye ameshafariki !
Nguvu zilimuisha Dokta Yusha. Kwa hali aliyomuacha nayo dereva Musa, haikumuingia akilini hata kidogo kama Musa angefariki, moja kwa moja alijua kwamba ameuliwa!
Kwa jinsi hali aliyoiacha, angeamini kama mkewe Nasra ama Hasina wangekuwa wamefariki, maana ndio ambao walikuwa katika hali ngumu, lakini siyo dereva Musa. Dokta Yusha Alijua kwa vyovyote vile kuna mchezo mbaya ulikuwa unaendelea mle wodini.
Kwa mwendo wake uleule wa taratibu alikuwa anakisogelea kile kitanda alicholazwa mgonjwa mwengine, ambaye nae alijifunika gubigubi, au pengine alifunikwa gubigubi baada ya kuuwawa kama dereva Musa. Bila kujua kitanda alichokuwa anakisogelea ndio kitanda alicholala Sita. Muuaji hatari toka kundi la Six killers, ambaye ndiye alimuua dereva Musa kwa kumnyonga shingo muda mfupi uliopita.

Dokta Yusha alikifia kile kitanda ambacho alilala mtu hatari sana. Aliishika ile ncha ya shuka taratibu na kuanza kumfunua yule mgonjwa.
Hamadi!
Dokta Yusha alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola. Moyo wa Dokta Yusha ulipiga kwa kasi sana. Kilikuwa ni kitendo cha ghafla ambacho hakukitegemea kabisa. Sita wa Six killers alinyanyuka pale kitandani na kukaa kitako.

"Hongera sana Dokta Yusha, uko vizuri sana, tumeona ulichomfanyia Tano, hongera Dokta Yusha" Sita alikuwa anaongea huku akiipangusa vumbi bastola yake kwa kutumia shuka la hospitali.
"Mwisho wako umefika Dokta Yusha, nakuuwa!
Ndio nitakuuwa baada ya mateso kidogo lakini" Sita aliongea kwa kujiamini sana.

Dokta Yusha aliamua kutulia, alijua kuwa na wasiwasi hakutomsaidia, aliamua kuwa makini ili ajue anatoka vipi katika kisanga kile kipya.

"Unaona wagonjwa wako wote wamelala, sipendi tuwasumbue, tutoke humu ndani kimyakimya nikakusulubu huko nje, sitaki niwamalize hawa kwa ujinga wako" Sita alimtahadharisha Dokta Yusha.

Dokta Yusha hakuwa na jinsi, aliongoza mwenyewe mlangoni, huku akifuatwa na Sita wa Six killers na bastola yake. Wakiwa wameongozana walifika nje, Dokta Yusha alisimama akisubiri maelekezo toka kwa Sita.

"Elekea chumba cha kuhifadhia maiti" Sita alitoa maelekezo kwa sauti ya chini....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI

Bila kujishauri Dokta Yusha alielekea katika chumba cha kuhifadhia maiti, huku akifuatwa nyuma na Sita. Dokta Yusha hakuwa anajua balaa alilokuwa anaenda kulishuhudia katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Waulikuta mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti upo wazi. Waliingia ndani.
Hali aliyoikuta Dokta Yusha mle ndani yalimstua sana!
Aliona maiti zimelazwa bila mpangilio mle ndani, tena sakafuni. Maiti zenye majeraha ya kutisha sana, ambayo ni ngumu kutazamwa na macho ya kawaida. Aliangalia watu aliowakuta mle ndani, wote wakiwa makini na shughuli zao za kinyama, walikuwa hawamwangalii kabisa yeye. Macho ya Dokta Yusha yalitua kwa Dokta Sharifa, daktari wa kike alikuwa makini bila wasiwasi wowote, akiishughulikia maiti iliyolazwa juu ya meza mbele yake. Dokta Yusha aliitazama kwa makini ile maiti akitaka kujua Dokta Sharifa alikuwa anaifanyia kitu gani. Bila wasiwasi wowote Dokta Sharifa alichomeka kisu kwa nguvu kidogo kifuani kwa yule maiti aliyekuwa amelazwa katika kitanda kilichokuwa mbele yake. Mwili wa Dokta Yusha ulimsisimka kwa hofu na woga, alifumba macho ili asiushuhudie unyama ule. Alipofumbua macho aliona moyo wa yule maiti ukiwa mkononi mwa Dokta Sharifa !
E bwana eee!
Nesi mmoja alienda pale kwenye meza iliyolazwa maiti akiwa na deli jekundu, ule moyo ukawekwa humo. Na Dokta Sharifa alianza kuushona ule mwili.
Dokta Yusha sasa alikumbuka, alikumbuka kuhusu kile kidonda alichokutwa nacho mama Mpaukha kifuani. Kumbe mama Mpaukha alifanyiwa mchezo huu mbaya, mama Mpaukha naye alitolewa Moyo!
Hasira zilimpanda Dokta Yusha, mishipa ya kichwa ilimsimama huku machozi yalikuwa yanamtiririka bila kupenda. Alitamani awauwe watu wote waliokuwemo mle ndani, lakini hakuweza, atawauwa vipi ilhali yeye ndiye aliyekuwa katika hatari zaidi ya kuuwawa!
Chozi la Dokta Yusha lilimsha shangwe mle ndani. Watu wote walikuwa wanamcheka Dokta Yusha alivyokuwa analia. Dokta Yusha alijiona kama yupo katikati ya mashetani wenye roho mbaya. Alipangusa machozi kwa kutumia kiganja chake cha mkono wa kushoto. Aliwaona manesi wawili wakichagua maiti pale chini, ilikuwa mithili ya wanunuzi wakichagua nguo katika soko la Tandika. Wakaipata maiti wakiyoitaka. Wakaibeba na kuipeleka kwenye ile meza iliyokuwa mbele ya Dokta Sharifa. Dokta Sharifa aliendelea na kazi yake huku akitabasamu...

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA MOJA

Kwa mara nyingine tena, daktari katiri wa kike Sharifa Juma alichomeka kile kisu chake kifuani mwa yule maiti mwengine. Aliifanyia kama alivyoifanyia ile maiti ya awali. Safari hii Dokta Yusha alithubutu kuangalia, aliangalia kila hatua ya kikatili iliyofanywa na mabaradhuli wale. Alibaki anatikisa kichwa tu kwa masikitiko. Hakutegemea kabisa kama kitendo kile cha kikatili kinafanywa na daktari wa kike anayeheshimika zaidi wilayani Kilwa, Dokta Sharifa. Hali ilikuwa ya kusikitisha sana.

Dokta Yusha aliangalia upande wake wa kulia, alimwona Dokta Zaidi Kilumba akiwa ametulia tuli kitini. Akitabasamu huku akimwangalia Dokta Yusha kwa dharau.

"Una dhamana kubwa sana Dokta Kilumba, umeaminiwa na Taifa kuingoza hospitali hii, kuwahudumia wananchi maskini, tena wagonjwa. Kinachofanyika hapa siyo haki Dokta Kilumba. Ndio! Hii siyo haki kabisa Dokta, kwanini unafanya hivi vitu ? Kumbuka maadili ya kazi udaktari, Kumbuka kiapo ulichoapa Dokta, kinafanana na kinachofanyika hapa Dokta?" Dokta Yusha alisema kwa hisia na uchungu mkubwa sana.
"Hahaha eti maadili ya kazi, hahaha eti kiapo cha udaktari, kiapo cha udaktari nd'o nini, kwa taarifa yako hii kazi tumelipwa hela nyingi sana! Tofauti na hizo zinazowafanya madaktari wagome kila siku. Unazungumzia maadili ya kazi, hivi kuna maadili mbele ya pesa?" Dokta Kilumba alikuwa anaongea akiwa amekaa palepale katika kiti, anaongea bila wasiwasi wowote.
"Mtalipa Dokta kwa huu unyama mnaofanya hapa, naapa mtalipa!. Hata mkiniua mimi kizazi kijacho kitalipa damu za hawa watu!" Dokta Yusha munkari ulianza kumpanda.
"Tulipe damu gani Dokta Yusha wakati hawa wameshakufa, hizi ni maiti Dokta?"
"Usibishane nae, yeye tunamtoa moyo leo akiwa anajiona. Ili tulipe vizuri hizo damu anaozisema huko mbinguni kama kupo!"
"Mletee hapa!"

Sita akamshika mkono na kumvuta. Kumpeleka pale alipo Dokta Kilumba. Alipofikishwa pale ndipo Dokta Yusha alimuona mtu mwengine kabisa, ambaye hakuwa amemuona pindi alipoingizwa mle ndani. Na hakuwa amemuona kabisa katika maisha yake. Mzee mwenye sura ya kikorofi, alikuwa na sharubu mithili ya Karl Peter's 'mkono wa damu'. Mzee mwenye mwili uliojengeka kimazoezi, mrefu sana, kwa majina alikuwa anaitwa Don Genge. Dokta Yusha alidhani ile sauti ya kuitwa imetoka kwa Dokta Kilumba, la hasha. Haikuwa hivyo, kumbe alikuwa ni jasusi Don Genge mwenyewe....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA MBILI.

"Hahaha hiki ndio kifaranga wasumbua?" Don Genge aliuliza kwa kejeri huku akiubinua kwa juu mdomo wake mpana.
"Ama kweli maajabu hayatofika mwisho duniani. Wewe ndio umemvunja goti komando Tano? Kwa nguvu gani ulizonazo mpumbavu wewe, kwa akili gani ulizonazo mjinga wewe? Don Genge alikuwa anauliza maswali bila ya kusubiri majibu toka kwa Dokta Yusha.
Kamtie kwenye gari tuondoke nae kambini tukaone uwezo wake mpaka Komando Tano ashindwe kumkamata na kuambulia kuvunjwa goti." Kwa haraka Sita alimsukasuka Dokta Yusha na kumpeleka kwenye gari.

Gari aliloingizwa dokta Yusha ni yale magari yenye bodi zenye visanduku nyuma. Mara nyingi hutumika katika mahospitali kusafirishia dawa. Kundi la Six killers nao walikuwa wanautumia gari aina hiyo kusafirishia mioyo. Na leo hii gari hiyohiyo ilitumika kama mahabusu inayotembea kwa Dokta Yusha. Ndani ya kile kisanduku kulikuwa na giza totoro, pia kulikuwa na joto sana, maana hakukuwa na uwazi wa kupitisha mwanga wowote katika kisanduku hiko. Kilikuwa kisanduku kidogo sana kilichompa shida sana Dokta Yusha. Ilimbidi ajikunje sana ili akae vizuri mle ndani ya gari. Hakukaa vizuri lakini alikaa.

Baada ya nusu saa alisikia kelele za miguu ya watu ikielekea pale kwenye gari aliyokuwa ndani yake. Mara alisikia mlango wa ile bodi ukifunguliwa.
Ulifunguka.
Yule jamaa aliyetambulika kwa jina la komando Sita aliingia na kuweka deli, deli la kuhifadhia mioyo ya maiti. Baada ya kuweka lile deli jekundu yule jamaa alitoka nje. Kile kisanduku kikafungwa tena. Giza likarejea kwa kasi!

Akiwa kule nyuma ya gari alisikia gari likiwashwa. Na safari ya kuelekea kusikojulikana ilianza. Gari lilitembea sana, takribani saa sita lilikuwa halijafika lilikokuwa linaenda. Dokta Yusha aliamini safari ile ilikuwa ni nje ya wilaya ya kilwa, au nje ya mkoa kabisa. Maana hakukuwa na sehemu ndani ya kilwa ya kutembea saa nyingi namna ile. Sasa alianza kulizoea giza, na kuyaona vizuri mandhari ya kule nyuma kwenye kisanduku. Kwenye sakafu ya gari ile, aliyaona madeli matatu yakiwa yamewekwa pamoja. Hakujua ni madeli ya nini, ingawa alihisi yatakuwa ya mioyo. Dokta Yusha hakutamani hata kuhangaika kuyafungua. Aliangazaangaza mle ndani ya gari, hakuona kitu kingine zaidi ya yale madeli mekundu.
Mara gari lilisimama, ishara kuwa lilikuwa limefika ilikokuwa inaelekea. Saa zaidi ya nane walizitumia barabarani.
Ilichukua kama robo saa ndipo akaja kufunguliwa kule nyuma....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
Sorry wadau mambo ya kijamii yalinibana tupo pamoja tukutane kesho
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA TATU

Dokta Yusha akaona tena mwanga halisi wa dunia. Alishuka mwenyewe bila kuambiwa. Alikuwa amechoka sana kukaa mle ndani ya kisanduki. Joto kali ndani ya kisanduku na kukosa hewa kulimuadhibu barabara Dokta Yusha.
Alishuka chini, alikutana na nyumba ndogo ya kisasa. Nyumba iliyonakshiwa kwa rangi ya bluu bahari. Huku chini kukiwa na michirizi ya rangi nyeusi. Juu iliezekwa na bati za vigae toka Afrika ya Kusini. Nyumba hiyo ilikuwa imezungukwa na ukuta mkubwa sana wenye rangi ya bluu bahari pia. Ulikuwa ukuta mrefu ulioipita hadi nyumba yenyewe. Yaani kama mtu akiwa kwa nje ataishia kuuona ukuta tu. Hatuiona nyumba ile. Dokta Yusha aliingalia kwa makini nyumba ile huku akiangalia mandhari ya sehemu ile. Alikiri kuwa hakuwahi kufika hata siku moja mahali pale. Hakujua kabisa nyumba ile ilikuwa mahali gani ndani ya nchi ya Tanzania?

Sita wa Six killers alimshika mkono Dokta Yusha na kuizunguka nyumba ile kuelekea nyuma kwa kupitia mkono wa kushoto. Walipofika uwani Dokta Yusha macho yake yalitazamana na kibanda kidogo mithili ya stoo. Sita alifungua kile kibanda kwa funguo na kumsukumia Dokta Yusha mle ndani.

Kilikuwa ni kibanda kidogo kwa nje, na ndani pia. Dokta Yusha alisimama hatua kama mbili toka katika mlango wa kile chumba na kuanza kukiangalia. Kilikuwa ni chumba ambacho hakukuwa na kitu chochote zaidi ya kiti kimoja tu cha chuma. Kuta yake ilipakwa rangi nyekundu ambayo ilikuwa inaumiza macho ukiitazama muda mrefu.
Dokta Yusha alipiga hatua za taratibu kuelekea katika kile kiti. Alikuwa na lengo la kwenda kukikalia kiti kile. Maana hakukuwa na sehemu nyingine ya kukaa zaidi ya kwenye kile kiti. Alikikaribia kabisa kile kiti, alitaka kukaa lakini aligairi. Alikitilia mashaka kile kiti. Kwanini kile kiti cha bati kiwekwe katika chumba kile, ni kweli kimewekwa kwa lengo la kukalia tu? Au kuna lengo lengine, siku zote wasiwasi akili. Dokta Yusha hakukaa, alirudi kinyumenyume hadi ukutani. Akakaa chini taratibu huku akikiangalia kwa makini kile kiti cha chuma......

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA NNE

Dokta Yusha alikaa pale chini sakafuni huku akitafakari mustakabari wa maisha yake. Aliona mambo yamebadirika kwa kasi sana, tena yakianzia siku ya sherehe ya ndoa yake.
Aliwakumbuka wagonjwa aliowaacha hospitali. Mkewe kipenzi Nasra, rafiki wa mkewe, Hasina na mzee Mpaukha, alijua watakuwa katika hali ngumu sana kwa kutokuwepo yeye, pia alijua jinsi walivyoikaribia hatari ya kutolewa mioyo na wale mabaradhuli. Alimfikiria dereva wa Mzee Mpaukha, Musa akijua kwa vyovyote kwa sasa atakuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, akisubiri kutolewa moyo .

"Kwanini moyo? Itakuwa wanafanyia nini hiyo mioyo? Tena bila shaka mioyo ya maiti ndiyo inayohitajika ndio maana wameweka kambi hospitali tena katika chumba cha kuhifadhia maiti. Lazima nijue undani wa sakata lile, na Lazima nihakikishe watu hawa wenye nia mbaya wanafikishwa katika vyombo vya sheria" Dokta Yusha aliwaza hayo bila ya kujua yupo sehemu hatari kiasi gani, bila kujua atatoka vipi ili akawafikishe katika vyombo vya sheria ilihal alikuwa tunduni akisubiri adhabu yake, bila shaka adhabu ya kifo!

Wakati akiwaza hayo alisikia mlango ukifunguliwa kwa nje. Ukafunguka kidogo na mtu mpya alisukumwa kwa nguvu kuingizwa mle ndani. Dokta Yusha alimwangalia vizuri mtu yule walitambuana.

"Wamekuleta huku Dokta"
"Nawe wamekuleta huku"

Ilikuwa ni kushangaana tu. Mtu yule alikuwa ni mmoja wa askari wa kituo cha Polisi Masoko. Tena ndiye askari aliyemhoji dokta Yusha alipoenda Polisi .....

"Eeh imekuwaje ukafika huku" Dokta Yusha aliuliza kwa wahka mkubwa.
Huku akiwa amesimama yule askari alianza kuelezea.
"Ulivyoomba kutoka pale Polisi ili kwenda kwenye mazishi ya Mwanasheria tulikukubalia, lakini ulivyotoka tu tulikubaliana tukufuate kwa nyuma, na ni mimi ndiye niliyepewa jukumu hilo. Nilikufuata kwa nyuma kila ulikoenda. Mpaka wanakuingiza kwenye gari mimi nilikuwa nashuhudia. Lakini nikiwa nimejibanza nyuma ya wodi moja nikisubiri muda muafaka wa kuja kukuokoa, nikiwa pale nyuma ya wodi nilipojificha nilistukia nimepigwa na kitu kizito kisogoni. Toka hapo sikujua nini kiliendelea. Nimeamka toka ndani ya gari dakika kama sita zilizopita na wakanileta moja kwa moja humu"
"Hivi tuko wapi hapa Afande?"
"Hata sifahamu, maana nilizimia kabisa, nimezinduka nimejikuta nipo humu"
"Itakuwa tuko mbali sana Afande, saa nane tumetumia mpaka kufika hapa"
"Saa nane?"
"Ndio, Afande"

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA TANO

"Mh itakuwa wametuleta wapi washenzi hawa" Yule askari alikuwa anaongea huku anapiga hatua kuelekea kukaa katika kile kiti pekee cha chuma mle ndani. Alikikaribia kile kiti na kusema.

"Sijui watakuwa wana mpango gani hawa wanaharamu"
"Nooooo afande usikae hapooooo!" Dokta Yusha alipiga kelele kali kumuonya yule askari asikalie kile kiti chuma, lakini alikuwa amechelewa sana.

Jamaa alikaa kwenye kiti kilichotokea...........Dokta Yusha alifumba macho!
Kiti kilibadirika rangi na kuwa chekundu sana, askari hakutoa hata ukelele mdogo, rangi nyekundu ya kiti ilienda sambamba na rangi ya askari yule. Kumbe kiti kile kilikuwa na shoti ajabu ya umeme!
Dokta Yusha alithubutu kufumbua macho, macho yalimtoka pima! hakutegemea kabisa kitendo kile. Ingawa alikuwa anahisi kiti kile sio kizuri tangu alivyoingia katika chumba kile, lakini hakudhani wala kufikiria kwamba kina madhara namna ile. Yule askari alianza kubadirika rangi tena, akawa mweusi tii huku akikakamaa ilhali kiti kilibaki na rangi yake ileile nyekundu. Dokta Yusha aliyaangalia yote huku huku akitetemeka, mikono yake ikiwa kauziba mdomo wake. Alikuwa anaangalia picha mbaya sana!
Huku akitetemeka dokta Yusha alisimama, kwa kiasi kikubwa akisaidiwa na ukuta katika kumsaidia kunyanyuka pale chini. Alivyosimama tu alikaribishwa na kitu kingine, harufu, ule mwili uliokakamaa pale chini ulianza kutoa harufu kali sana!
Dokta Yusha alijitahidi kubana pumzi ili harufu ile isiyoeleweka isiingie puani mwake, ilikuwa ngumu sana, maana kuendelea kubana pumzi kulimaanisha anakiita kifo chake mwenyewe. Hata hivyo hakutaka kabisa kuvuta harufu ile, aliendea kuziba pumzi huku anaachia mara chache chache, akiwa katika hali hiyo ngumu sana katika maisha yake, mara alisikia kelele za mlango, ishara kuwa mlango ulikuwa unafunguliwa. Mlango ukafunguliwa, aliingia Sita wa Six killers kwa majigambo makubwa sana. Alienda hadi pale ukutani ambako Dokta Yusha alikuwa amesimama.

"Hahaha Dokta nawe unahisi harufu, siamini. Wewe ni daktari bwana unakutana na harufu mbaya zaidi ya hii. Hebu simama" Sita alisema kwa urafiki zaidi.

Dokta Yusha alimwangalia Sita huku akionesha sura ya upole sana. Lakini sura yake ya upole haikusaidia kitu. 'Maji aliyavulia nguo..............'

"Haya toka nje" Sita wa Six killers alimwambia huku akionesha kwa kidole cha shahada mahali mlango ulipo...

ITAENDELEA JIONI MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA SITA

Dokta Yusha alitoka nje ya chumba kile huku akifuatiwa na Sita. Alipotoka tu nje, alikutana na jamaa mmoja akiwa amekaa katika kiti cha plastiki huku anavuta kiko. Jamaa yuleyule aliyekuwa anaongea kwa majivuno na kujiamini kule katika chumba cha kuhifadhia maiti. Alikuwa anaitwa Don Genge.
Dokta Yusha alisimamishwa mbele ya Don Genge huku nyuma yake akiwa amesimama imara Sita. Pembeni ya Don Genge upande wa kushoto walikuwa wamesimama watu wawili, na upande wa kushoto walikuwa wamesimama watu wawili. Don Genge alikuwa kati mithili ya Mfalme.

"Naitwa Don Genge, umeshawahi kulisikia hilo jina" Don Genge aliuliza punde tu Dokta Yusha alivyowasiri pale.
Dokta Yusha alikataa kwa kutingisha kichwa.
"Wewe ni bubu?"
"Hapana"
"Kwanini unapenda sana kufatilia mambo ya watu?" Don Genge aliachana na mwendelezo wa swali la awali na kuuliza swali jipya.
Dokta Yusha alikaa kimya, kimya ambacho kilimkasirisha sana Don Genge.
Don Genge alinyanyuka, akamsogelea Dokta Yusha huku akitabasamu. Ghafla, Don Genge alirusha kibao kilichotua sawia katika shavu la kushoto la Dokta Yusha. Dokta Yusha aliyumba kidogo, kisha akasimama tena wima. Alijishika shavu lake la kushoto kwa mkono wake wa kulia.

"Kwanini unapenda kufatilia mambo ya watu?" Sasa Don Genge aliuuliza uso wake ukiwa karibu sana na uso wa Dokta Yusha.
"Nisamehee sirudii tena" Dokta Yusha aliamua kuomba msamaha bila ya kujielewa.
"Hakuna mtu aliyewahi kuingia katika nyumba hii, akatoka hai, wote wameuwawa, tena kikatili sana! Ila wewe utakufa kifo cha tofauti....." Don Genge aliacha kuongea, aliacha maneno yale yamuuingie vizuri Dokta Yusha. Akavuta kiko kidogo, halafu akampulizia moshi Dokta Yusha. Dokta Yusha alikohoa kutokana na ule moshi.
".........Utakufa kifo cha tofauti sana, utakufa kwa njaa!
Siku nyingi nilikuwa najiuliza hivi binadamu anaweza kukaa siku ngapi bila kula? Lakini nitapata jibu la hilo swali kupitia wewe" Don Genge alikuwa anaongea wakati Dokta Yusha alikuwa anaendelea kukohoa kutokana na ule moshi. Lakini Don Genge hakujari kama kasikia ama hajasikia.
"Hebu mrudishe ndani kule"
"Hapana, musinipeleke katika kile chumba" Dokta Yusha alikuwa anakataa kurudi tena katika chumba kile chenye harufu ya mbaya na ya kuchukiza.
"Kile ndio chumba chako, lile ndio kaburi lako, usilikatae, ulipende Dokta, peleka huyo!"

Sita alimshika suruali kwa nyuma Dokta Yusha mithili ya kibaka ashikwavo na askari na kumrudisha katika kile chumba chenye harufu kali sana...

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
Unatupa kiduchu hata kwenye koo haifiki ladha ishapotea
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA AROBAINI NA SABA

Hali ilikuwa ngumu sana katika chumba kile, ambacho nd'o ilikuwa selo ya Dokta Yusha, au kubali la Dokta Yusha kama alivyosema Don Genge. Lakini Dokta Yusha ilimbidi akae katika selo ile, hakuwa na jinsi. Aliishi mule kwa hofu kubwa sana, kila kitu alichoongea Don Genge bado kilikuwa kinarindima katika kichwa chake, kwamba kile kitakuwa chumba chake, pia litakuwa nd'o kaburi lake.

"Nakubari kitakuwa chumba changu, tena kwa muda bila shaka, lakini haliwezi kuwa kaburi langu kamwe" Dokta Yusha alijisemea mwenyewe kwa ujasiri.
Sasa alikuwa anaivuta harufu yote ya chumbani, hakuwa anaziba tena pua, aliamua liwalo na liwe, harufu yoyote iingie puani mwake, lakini lazima atoke mle ndani.

Usiku uliingia, usiku ambao Dokta Yusha alipanga nd'o uwe kilele cha yeye kuishi katika selo ile, lazima atoke mle ndani. Ndani ya chumba kile kulikuwa na giza kubwa sana. Dokta Yusha alinyanyuka kwenye sakafu alipokaa na kuusogelea mlango. Alishika komea la mlango na kujaribu kulizungusha taratibu.
Mlango ulikuwa umefungwa!

Dokta Yusha ilimpasa kutafuta njia nyingine mbadala ya kumuwezesha kutoka katika chumba kile cha kifo. Ilimpasa kutumia akili za ziada kutoka katika chumba kile cha mauti.

'Lazima nitoke humu, siwezi kufa kikondoo humu'

Dokta Yusha aliangalia juu ya kile chumba, alikutana na vigae vilivyowezekwa vizuri sana kule juu. Hakuna mjanja atakayeweza kufanya chochote ili kupita katika vigae vile. Ilikuwa ngumu sana!
Dokta Yusha alirudi nyuma, akarejea tena ukutani, akauangalia ukuta, akautomasa ule ukuta kwa kidole, ulikuwa ukuta mgumu sana!

Mlango, ukuta, bati vyote havikumruhusu kabisa Dokta Yusha kutoka katika chumba kile cha hatari....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA
 
Back
Top Bottom