SIMULIZI: UHAI WA MWANANGU
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: mwandishi.phiri
SEHEMU: 10
David alikosa majibu ya maswali yake, alibaki kamtolea macho Aman aliyekuwa mbele yake. Aman alielewa hali ya David akaamua kufafanua zaidi ili kumuweka David karibu na mawazo yake
"Kundi la wauza madawa ya kulevya tunalotaka kukuingiza kila siku linafanya mawasiliano na kundi letu mama lililo Afrika Kusini pasipo wao kujua kama kundi hilo na kundi hili ni kitu kimoja"
Aman aliendelea kuona mshangao wa David usoni kwake, mshangao uliomaanisha alikuwa haelewi chochote zaidi ya kusikia sauti inayoelezea. Amani alifafanua zaidi
"Baada ya kundi hilo lililo chini ya binti mwenye asili ya Uarabuni kufanikiwa kuchukua kila kitu toka mikononi kwetu, sisi tuliandaa mpango wa kulipiza kisasi na kuliteketeza kabisa kundi lake. Kuna mzee na vijana wangu waliopo Afrika Kusini ambao ndiyo huratibu biashara yetu toka huko mpaka hapa Tanzania. Vijana hao pamoja na mzee huyo waliweza kumuingiza mtegoni binti wa kiarabu akaanza kufanya nao biashara pia, ilikuwa rahisi kwa sababu binti wa kiarabu alikuwa akichukua mzigo wake toka nchi hiyo na jinsi mtego ulivyosukwa haikuwa rahisi kushituka".
David alikuwa makini sana kumsikiliza Aman, muda wote akiwa amepiga magoti. Aman aliona umuhimu wa David kuinuka, alimwambia ainuke kisha akae kwenye kiti cha plastiki kilichokuwa ndani ya eneo hilo. David akatimiza maagizo ya bosi wake. Aman akaendelea
"Japokuwa ilikuwa rahisi lakini haikuwa rahisi sana kumuaminisha binti wa kiarabu kukubali kufanya biashara na watu aliokuwa hawajui wala kuwafahamu awali. Hakika tuliandaa mpango wa kumuaminisha binti huyu jeuri. Tulifatilia nyendo za biashara zake tukagundua ratiba yake ya kuendea mzigo Afrika Kusini. Tuliandaa mpango wa watu wake watakaoenda kuchukua mzigo wa madawa ya kulevya Afrika Kusini wakamatwe na polisi. Tuliandaa polisi feki waliofanikiwa kuwakamata watu wa kundi lake wakiwa na mzigo wa madawa ya kulevya tayari kwa kuondoka kuelekea Tanzania.
Kitendo kile kilimaanisha jela tena ughaibuni, vijana wale walifadhaika sana. Walifungwa pingu kisha wakaingizwa kwenye gari la polisi feki tuliowaandaa lakini kabda gari lile halijaondoka mahala pale pa maficho ambapo hutumika kufanyia mambo ya kijangili na uuzaji wa madawa ya kulevya ghafla gari tatu zikiwa na mwendo kasi zilivamia eneo lile, zikafanikiwa kulizuia gari la polisi lililowateka vijana wa binti wa kiarabu. Walishuka vijana zaidi ya nane wakiwa na silaha za moto za kisasa. Polisi walishurutishwa kushuka ndani ya gari lile, polisi hawakuwa na jinsi walishuka kama walivyoamuriwa wakaambiwa wachague kufa au kutimua mbio. Hakuna polisi aliyejibu, muda huo walikuwa wakitimua mbio.
Vijana waliokamatwa na polisi awali wakawa mikononi mwa vijana walioenda kutoa msaada. Makundi yote mawili yalikuwa hayafahamiani kabisa kwa sura lakini vijana walioenda kutoa msaada walikuwa na taarifa za kutosha kuhusu vijana waliotoka nchini Tanzania. Mmoja wa vijana walioenda kutoa msaada akaongea
"Hakuna haja ya kujiuliza mara mbili, hamtufahamu hata kidogo lakini sisi tunafahamu kuwa ninyi ni Watanzania mnaojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya. Msihofu, hiyo ni biashara yetu pia"
Akapumzika kidogo akawatazama wenzake waliokuwa kimya huku wamevaa sura za kazi. Kijana yule akaendelea kutoa maelekezo kwa vijana waliookolewa toka mikononi mwa polisi
"Mpo kwenye mikono salama kabisa, wala msiwe na hofu yoyote. Nyie ni mwenzetu. Wote tuonafanya biashara za madawa ya kulevya tuna uaduni na polisi na Serikali kwa ujumla. Tuligundua polisi walifahamu nyendo zenu tukaamua kufatilia ili tutoe msaada endapo ukihitajika. Hakika tumefanikiwa kwa asilimia mia moja"
Japokuwa ufafanuzi uliendelea lakini vijana waliosaidiwa toka mikononi mwa polisi hawakuwaamini waliotoa msaada kwa sababu hawakupewa sababu za msingi za kusaidiwa na watu wasio wafahamu, vile vile hawakuachwa huru waondoke zao bali walichukuliwa wakapelekwa kwenye ngome ya waokoaji, ngome iliyo kama Casino kwa muonekano lakini ina siri nzito ndani yake. Ilikuwa ni ngome ya kitajiri yenye kila aina ya ufuska. Wacheza kamari, wasagaji, wanawake malaya wachezea fimbo pamoja na mambo mengine ya anasa yaliendelea kama kawaida.
Waliingizwa ndani ya Casino hiyo kisha wakaingizwa kwenye chumba cha siri, hata baadhi ya wafanyakazi wa Casino hiyo hawafahamu uwepo wa chumba hicho. Chumba hicho kinafahamika kwa watu wachache sana ndani ya kundi, watu ambao wanafahamu uwepo wa gwiji wa madawa ya kulevya ndani ya Casino hiyo. Chumba hicho kipo chini ya jengo la Casino, chumba cha chini. Mlango wa siri wa kuingilia chumbani humo unapatikana kwenye choo kimojawapo kati ya vyoo vya Casino hiyo. Sio rahisi mtu kufahamu uwepo wa mlango huo wa siri.
Chumbani humo walikutanishwa na mzee wenye umri zaidi ya miaka sabini, mzee alijitambulisha mbele yao kwa jina Masiya akimaanisha kuwa yeye ni mkombozi aliyeletwa duniani makusudi kuwatetea watu wanyonge na masikini. Aliwaeleza kuwa yeye ndiyo msambazaji nguli wa madawa ya kulevya barani Afrika. Hakika aliweza kujielezea kwa vijana wale. Mwisho wa siku, mzee Masiya aliwahakikishia ulinzi na usalama.
Siku iliyofuata aliwasafirisha kwa njia za panya zaidi ya njia walizokiwa wakizifahamu wakafanikiwa kufika Tanzania pasipo kipingamizi chochote. Hakika wakijihakikishia kuwa mzee yule ni nguli katika biashara ya madawa ya kulevya. Kilichowashangaza zaidi hawakuporwa mzigo wao wa madawa ya kulevya wala fedha nyingi walizokuwa nazo bali waliongezewa ulinzi na usalama wa safari yao.
Mzee yule alikuwa wa ajabu sana vichwani mwao. Walijiuliza
"Inakuwaje muuza madawa ya kulevya akuache uondoke na madawa pamoja na pesa nyingi kiasi hiki?"
Lakini walipoufikiria utajiri wa mzee yule waliamini aliamua kuwaachia tu kwa sababu alijiita mtetezi wa wanyonge na masikini. Taarifa za mzee yule walimfikishia bosi wao, binti wa kiarabu. Zilikuwa taarifa za kumshitusha lakini baada ya kuwasiliana na mzee Masiya kupitia mawasiliano aliyowapa vijana wake hofu ya binti wa kiarabu iliisha kabisa. Hapo ndipo urafiki wa kazi kati ya binti wa kiarabu na mzee Masiya ulipoanza, walifanya biashara ya kuaminiana sana, biashara isiyokuwa na mambo ya kiswahili. Mzee Masiya alimuhakikishia binti wa kiarabu kuwa anamjali kama mwanae wa kumzaa, hakika kauli hiyo aliidhibitisha kupitia uhusiano wao. Japokuwa wapo mbali na hawajawahi kuonana lakini wanawasiliana sana kama watu walio ndani ya mkoa mmoja. Binti wa kiarabu alifungiwa mzigo wake, ukapewa na ulinzi na kukwepa vipingamizi vyote kwa nguvu ya mzee Masiya.
Biashara ilileta hali ya uaminifu zaidi ya undugu, uaminifu huo ulijengwa na binti wa kiarabu dhidi ya mzee Masiya, akahitaji kufahamiana zaidi. Binti wa kiarabu alimuomba mzee Masiya waweze kuonana nchini Tanzania, aende maana amemuandalia zawadi anayohisi itamfaa lakini mzee yule alimsisitizia binti wa kiarabu kuwa umri wake ni mkubwa sana, hashauriwi kusafiri safiri ovyo maana akifanya hivyo anahatarisha afya yake. Lakini mzee Masiya akamwambia binti wa kiarabu kuwa atamtuma kijana wake aende kumpokelea zawadi hiyo.
Kauli hiyo ilikuwa nzuri katika masikio ya binti wa kiarabu lakini aliomba kitu kingine zaidi, binti yule alimwambia mzee Masiya
"Ningependa mwanao angebakia ndani ya kundi langu ili tukafanya biashara vizuri zaidi, uwepo wake kwangu utarahisisha mambo mengi ambayo yatakuhitaji wewe"
Kauli hiyo ilimaanisha kijana wa mzee Masiya aende nchini Tanzania kuchukua zawadi ya baba yake kisha arudi nchini Tanzania kujiunga na kundi la binti wa kiarabu ili wafanye kazi kwa ukaribu zaidi. Kauli hiyo ilikuwa tamu sana masikioni mwa mzee Masiya, aliona amepata mwaya wa kumuingiza kijana wetu katika himaya ya binti wa kiarabu. Mzee Masiya alinielezea kila kitu, akaniambia nimuingize kijana makini katika himaya ya binti wa kiarabu ili tuweze kumsambaratisha. Kijana huyo amepatikana, kijana huyo ni wewe David. Lazima uingie kwenye himaya ya binti wa kiarabu kama mtoto wa mzee Masiya. Hakika Nasra alikuwa hajui alikuwa akisukiwa mtego siku nyingi, mtego ulioandaliwa ili kumsambaratisha yeye na kundi lake. Sasa amenasa mtegoni"
Baada ya Aman kumaliza kutoa ufafanuzi, sasa David alilitambua jina la binti wa kiarabu kuwa ni Nasra lakini utambuzi wa jina hilo haukumsaidia chochote wakati huo, yeye aliufikiria mpango ulioandaliwa, mpango wa kumuingiza kwenye imaya ya Nasra kama mpelelezi kisha akafikiria kazi aliyopewa na Nasra, kazi aliyomuweka mtoto wake dhamana. David alibaki njia panda.
Upande wa pili Nasra alikuwa akimsubiria kwa hamu mtoto wa mzee Masiya, aliamini akimpata mtoto huyo utakuwa ni mwanzo mzuri wa safari yake ya matumaini. Akatabasamu baada ya kuona anaweza kuua ndege wawili kwa wakati mmoja.
ITAENDELEA