nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
Reli hii hakika itakuwa mkombozi wetu kiuchumi Thursday, 17 March 2011 20:18
Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete jana alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wawekezaji wa Reli inayotazamiwa kujengwa kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali, nchini Rwanda na Keza hadi Musongati, nchini Burundi. Mradi huo utagharimu kati ya Sh5.2 trilioni na Sh7.6 trilioni.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na mabalozi wa nchi wahisani, mawaziri wanaosimamia masuala ya usafiri wa reli nchini Tanzania, Rwanda na Burundi na wawakilishi wa benki za biashara za ndani na nchi za nje, lilijadili jinsi ya kupata fedha za ujenzi wa reli hiyo inayotegemewa kusafirisha tani milioni 35 ifikapo mwaka 2030. Inatia moyo kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), tayari imetoa Sh18 bilioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa mradi huo.
Hapana shaka kuwa reli hiyo ikikamilika itakuwa chachu kubwa ya maendeleo na mkombozi kiuchumi wa nchi hizo tatu za Afrika Mashariki. Pengine wakati tukifurahia ujio wa mradi huo wa reli na kuzungumzia maendeleo ambayo nchi zetu hizo zitapata kutokana na kusafirisha mizigo na abiria kwa kutumia reli hiyo, ingekuwa vyema tujiulize kwa nini imechukua muda mrefu kiasi hicho kabla ya viongozi wetu kubuni mradi huo.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa nchi wahisani zilikuwa tayari kuufadhili siku nyingi tu na nchi zetu zilikuwa na uwezo wa kuunganisha nguvu na kupata fedha za mradi.
Imetolewa hoja na baadhi ya watu kwamba mradi kama huo usingewezekana siku za nyuma kwa sababu Rwanda na Burundi zilikuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Lakini tunadhani kuwa tatizo hasa halikutokana na vita, bali lilitokana na viongozi wetu kukosa ubunifu pamoja na kushindwa kuvua mbeleko za ukoloni mamboleo, Tanzania ikiwa imetawaliwa na Uingereza na Rwanda na Burundi zikiwa na uchovu uliotokana na utawala wa Ubelgiji.
Siyo siri kwamba, ingawa Rwanda ilipata uhuru mwaka 1960 ikifuatiwa na Burundi mwaka 1962, nchi mbili hizo zilikuwa hazina vita katika miongo mitatu ya kwanza baada ya kupata uhuru kutoka Ubelgiji.
Rwanda ilikumbwa na vita mwaka 1990 hadi 1994 yalipotokea mauaji ya kimbali na Burundi ilikumbwa na vita mwaka 1992. Tanzania imekuwa na amani wakati wote tangu ipate uhuru 1961.
Tunachojaribu kusema hapa ni kwamba viongozi wengi katika Bara la Afrika wamechelewa sana kutambua umuhimu wa usafiri wa reli katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Tuangalie jinsi viongozi wa Tanzania na Zambia walivyoitelekeza Reli ya Tazara (mashuhuri kama Reli ya Uhuru), hadi ikafikia katika hali ya kusikitisha iliyomo hivi sasa.
Viongozi wenye dira na mwelekeo wangehakikisha reli hiyo inapasua kupitia Zambia na kutokezea Bahari ya Atlantic kupitia Angola. Leo hii bidhaa za Afrika Mashariki zingekuwa zinafika Bara la Amerika kwa gharama ndogo mno.
Tunataka viongozi wetu watambue kuwa usafiri wa reli katika nchi yetu ndilo jibu pekee kwa changamoto nyingi za usafiri zinazotukabili. Licha ya usafiri huo kuwa wa gharama ndogo sana, husafirisha abiria wengi na mizigo mingi mizito kwa mara moja. Nchi nyingi duniani hutumia reli, badala ya barabara kusafirisha mizigo mizito kwani, kama tunavyoshuhudia uharibifu wa barabara zetu kwa kiasi kikubwa unatokana na sababu hiyo.
Tunapendekeza kuwa Serikali isifanye mzaha kwa ujenzi wa reli hii. Inawezekana kabisa kuwa inaweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kwa maana ya kuhakikisha kuwa reli hii ikifika Isaka, Shinyanga, Serikali inaunganisha reli ili ifike mjini Mwanza.
Kwa kufanya hivyo, hata bei za bidhaa kama sementi, sukari, vifaa vya ujenzi na kadhalika zitapungua kwa kiasi kikubwa. Serikali itafute wawekezaji ili zijengwe reli nyingine kwenda katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha na pia iangalie uwezekano wa kuijenga katika mikoa mingine, hasa ya kusini.