Rais Samia amechagua njia sahihi kushusha bei mafuta

Ferruccio Lamborghini

JF-Expert Member
Apr 15, 2020
1,664
2,517
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameamua kulikabili sakata la mgogoro wa mafuta kwa kutoa maelekezo ya kujibana katika matumizi ya ndani ya Serikali. Kwa nini hii ndio njia sahihi? Nitaeleza;

Wapo waliopendekeza kuondoa tozo mbalimbali kwenye mafuta ili bei ipungue. Ni mawazo lakini msaada wake upo wapi?

Tozo ambazo zinaongelewa nyingi zipo kwenye mfumo wa bajeti. Hivyo kuziondoa ni kuathiri moja kwa moja fedha za Serikali.

Mapato ya Serikali yanapata athari hasi, maumivu yanakwenda kwenye miradi ya maendeleo.

Uamuzi wa Rais Samia unamaanisha kuwa tozo hazitolewi. Zinabaki. Miradi ya maendeleo iendelee kuhudumiwa vizuri. Na bei ya mafuta inaweza kupungua. Hapa ndipl Rais Samia amecheza vizuri na mwisho atachomoza shujaa wa hili sakata.

Ameamua kucheza na mgawanyo wa bajeti ya Serikali. Miradi ya maendeleo haiguswi kabisa. Eneo linalopaswa kufanyiwa kazi inavyotakiwa ni lile la matumizi ya kawaida.

Bajeti ya Tanzania, matumizi yake hugawanywa katika mafungu mawili; matumizi ya kawaida (recurrent expenditure) na matumizi ya maendeleo (development expenditure).

Mathalan, bajeti ya nchi inayofanyiwa kazi hivi sasa ambayo ukomo wake ni Juni 30, mwaka huu ni Sh37.98 trilioni. Asilimia 63 ya fedha hizo ni matumizi ya kawaida, halafu asilimia 37 ndio miradi ya maendeleo.

Mwaka ujao wa fedha, matarajio ni kuwa na bajeti ya Sh41 trilioni. Kama ilivyo katika mwaka huu unaoelekea ukingoni, fedha nyingi zitaelekezwa kwenye matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo itapata mgao wa chini.

Rais ameshaamua; sehemu ya miradi ya maendeleo haiguswi kabisa. Hivyo, tujielekeze kwenye matumizi ya kawaida.

Tunapoelekea; fungu la matumizi ya kawaida, nalo mishahara haiguwi. Hata fedha za malipo ya madeni nazo bila shaka hazitaguswa.

Kazi ianze kwenye mgawanyo wa fedha za wizara na idara zake, kuanzia uendeshaji wa kila idara mpaka ununuzi wa viburudisho. Hapo ndipo inaweza kuwa rahisi kupata pesa za kushusha bei ya mafuta.

Madereva wa magari ya viongozi wanatumia mafuta vibaya. Gari linaunguruma saa mbili mpaka tatu, dereva yupo ndani ya gari amejiwashia kiyoyozi. Eti anasubiriwa kiongozi aamke, ajiandae ndipo apande gari.

Wakati mwingine ni kwenye mikutano. Dereva anampeleka kiongozi mkutanoni. Wakati anamsubiri, gari linawaka kwa ajili ya kiyoyozi. Mafuta yanateketea.

Ukipiga hesabu, utagundua kuwa kama gari la kiongozi lilikuwa linawekewa mafuta ya Sh1,000,000 kwa wiki, kumbe mafuta ya Sh400,000 yanamtosha kabisa. Inaweza kupungua kadiri inavyowezekana.

Dereva ajue kuwa akimpeleka kiongozi kwenye mkutano, wakati anasubiri, gari lizimwe. Akimfuata kiongozi nyumbani kumpeleka kazini, asiache gari linaunguruma wakati kiongozi yupo kitandani. Akifika azime. Akishaingia kwenye gari ndio awashe safari ianze.

Mfumo wa recurrent budget ni kwamba husemi matumizi ili upewe fedha za kutumia, la! Unapewa fedha, unatumia, halafu baada ya kutumia ndio unaeleza ulivyotumia.

Aina hii ya bajeti imekuwa ikitumiwa vibaya serikalini. Kuna matumizi yasiyo ya lazima hufanyika ili kuhakikisha fedha ambazo taasisi ya Serikali imepangiwa katika mwaka wa fedha, inatumika yote.

Mfano ni sasa hivi, mwaka wa fedha 2021-2022 upo jirani. Unaweza kupatia ukisema kuwa kuna watu kwenye ofisi za Serikali, wapo ‘busy’ kutumia fedha ili ziishe kabla ya Juni 30, kuliko kufanya kazi walizoajiriwa kuzifanya.

Lingine muhimu ni kupunguza safari na ikiwezekana kuzifuta kabisa mpaka taifa livuke kipindi hiki dunia ipo kwenye mgogoro wa mafuta.

Tatizo la matumizi mabaya ya mafungu ya serikali ni la kihistoria. Unaweza kukuta bei ya maji inayoripotiwa na wizara hii ni tofauti na nyingine. Ingawa maji ni yaleyale, kutoka kampuni ileile na ujazo uleule.

Ndani ya wizara moja, idara hii inajaza bei yake na nyingine ya kwake tofauti kwa manunuzi kitu kilekile.

Kwa vile fedha wanapewa ndio wanatumia, suluhu ni kupunguza ukubwa wa fungu. Wapewe kidogo ili watumie kwa uangalifu.

Kuna idara ya Serikali, unakuta mashine ya kahawa, mgeni anaambiwa achague aina anayotaka. Nyeupe, nyeusi, cappuccino na kadhalika. Jumlisha korosho na viburudisho vingine.

Nyakati hizi za mkwamo wa bei ya mafuta, kupanda kwa bidhaa na huduma mbalimbali, anasa za nini serikalini?
Baada ya Vita ya Kagera, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alilitangazia taifa kipindi cha kufunga mkanda. Kila mwananchi akawa tayari.

Taifa lilishapoteza fedha nyingi kwenye ‘misheni’ ya kumwondoa Nduli Idi Amin, hivyo kutibu majeraha ya kiuchumi baada ya vita ilihitaji watu wajifunge mkanda.

Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani mwaka 1995, aliwaambia Watanzania kuwa ilikuwa lazima kufunga mkanda kwa ajili ya kuhudumia madeni ili nchi iondoke kwenye mstari wa kutokopesheka.

Na sasa, Rais Samia ametangaza ni kujigunga mkanda serikalini. Bajeti ikatwe. Iekezwe kwenye kupunguza bei ya mafuta.

Hili si la kwanza. Mwaka 2006, Bajeti ya Wizara ya Miundombinu ilikuwa finyu mno. Fedha zilizotengwa hazikuwa zinatosheleza ujenzi wa miundombinu yenye tija kwa nchi.

Kilichoinusuru Wizara ya Miundombinu ni recurrent budget. Matumizi ya kawaida yalipunguzwa na fedha Sh360 bilioni zilipatikana, zikaongezwa Wizara ya Miundombinu.

Kwa wenye kufuatilia Bunge na historia yake, watakuwa wanafahamu kuwa vitabu vya bajeti mwaka 2006 ilibidi visahihishwe na kuchapwa upya ili kupunguza fedha kwenye recurrent budget na kuongeza Sh360 bilioni kwenye miradi ya maendeleo, Wizara ya Miundombinu.

Ushauri huu wa kunyofoa fedha kwenye recurrent budget, ulitolewa na Kamati ya Miundombinu iliyokuwa na wajumbe kama mzee Paul Kimiti, Peter Serukamba na wengine. Hoja ikapelekwa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Abdallah Kigoda, Zitto Kabwe na wengine.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliposikia ushauri wa akina Serukamba uliokubaliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi, aliwaita wajumbe wote wa Kamati ya Miundombinu. Lowassa alipoielewa hoja, alimshirikisha Rais Jakaya Kikwete. Vitabu vya bajeti vikachapwa upya.

Kama serikali itafanya mapitio mazuri kwenye recurrent budget, kuna uwezekano wa kuokoa hata Sh3 trilioni. Hizo fedha ziende bika shaka zitatumika kushusha bei ya mafuta.

Na endapo bei ya mafuta itashuka kwa udhibiti mzuri wa fedha za matumizi ya kawaida, Rais Samia ataibuka shujaa wa kipindi hiki nchi inateswa na ongezeko la bei za bidhaa. Chanzo kikiwa kupaa kwa bei ya mafuta. Na ataweka historia.


credit:Luqman MALOTO
 
Umeandika kwa ureeefu ilhali mistari mitatu tu ingetosha kumsifia kutimiza nia yako.

Sijasoma yote, ila hakuna uhalisia. Serikali hii itoe pesa kwaajili ya wananchi? Labda kama wanagawana wenyewe tu. Kaulize kwenye taasisi na idara za serikali, mpaka mwaka wa fedha unaisha wanalalama hawajapata kasma yao, mambo hayaendi!

Achilia mbali kutokuwa wawazi kuhusu hata tozo wanazotupiga kuwa zinafanyiwa nini, mpaka sasa waliishia kusema 48bn tu, madarasa, msaada madarasa, mkopo na wenyewe unasingizia madarasa! Yako wapi hayo madarasa?

Kaangalie taasisi na idara za serikali ambazo hazijapewa mgawo wao kutoka kwenye bajeti iliyopita KISHA uje kusahihisha hili pambio.
 
Matumizi yapi ya serikali yanayobana? Wanaweza kuainisha? Unafahamu posho ya mafuta ya gari kwa mbunge kwa kila lita amekuwa akilipwa sh 2,500 tangu na tangu? Fuatilia kwa sasa ujue imepandishwa kufikia wapi kisha uje useme kuwa wanabana matumizi.

Unajua ni kwa kiasi gani sheria ya manunuzi inavyoligharimu taifa? Unajua mnufaika ni nani? Bidhaa ya sh 1,000 kwenye soko la kawaida, serikali inanunua kwa sh 100,000 unafahamu hilo?

Unayafahamu MADOKEZO? POSHO, MADARAJA YA MSHAHARA? NYONGEZA ZA MSHAHARA? Yote hayo hayajali kama kunakuwa na tija kwa taifa au ni kwa kiki za mtaji wa kisiasa!

TTCL ilifeli, ikamegwa celtel, inaendeshea bila sheria za kipumbavu za manunuzi au nyongeza za mshahara na madaraja bila tija, angalia walipo leo!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom