Kila mmoja katika nafasi yake, japo kwa viwango tofauti, amewahi kufanya kosa.
Umadhubuti wa kiongozi haupo katika kutofanya kosa bali katika kutafuta suluhisho sahihi baada ya kufanya kosa.
Hatua ya kwanza ya kupata suluhisho sahihi la kosa, ni kukiri umefanya kosa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema,
"..... kukiri upungufu siyo kujidhalilisha bali ni kitendo cha kujiimarisha"
Rais Magufuli, ninaamini amefanya makosa mengi katika kukabiliana na corona. Lakini Watanzania tulikuwa tayari kumsamehe maana corona imekuja kwa mara ya kwanza, na hakuna aliye na uzoefu wa kukabiliana nayo.
Mimi ni mmoja wa wahanga wa corona, mtoto wa kaka yangu katika umri wake wa ujana, amepoteza maisha ya Duniani, na kwa dalili alizopitia, tuna hakika ni corona. Lakini kuna rafiki yangu amepoteza ndugu zake 4 na marafiki wa familia 3. Leo baada ya Rais kumpoteza msaidizi wake wa karibu, kwa dalili zinazoonesha, kwa tatizo la corona, tulitarajia kupata neno la faraja kutoka kwa Rais.
Kuna mambo tuliyatarajia kutoka kwa Rais:
1) Watanzania wote kwa umoja wetu, kukiri kuwa tumepatwa na janga la corona
2) Kukiri kuwa hatujawa na jitihada za dhati kukabiliana na corona
3) Kukiri kuwa tumeishi kimbumbumbu bila hata ya kuwa na jitihada za tafiti za kujua ukubwa wa tatizo
Kisha Serikali ingetangaza hatua za pamoja tunazozichukua kama Taifa.
Badala yake Rais ametaka kuonesha kuwa yeye ni mwenye imani kubwa kwa Mungu kuliko hata maaskofu wetu na mashekhe, na labda kumzidi hata Papa. Yaani tuishi kwa kutegemea miujiza ya Mungu. Mimi ni muumini mkristo mkatoliki, ninatamka kuwa Rais ana upotofu mkubwa wa neno la Mungu. Ni kweli Kristo Yesu alipokuja Duniani aliponya, alifufua na kutenda miujiza mingi. Lakini kama waumini tunatakiwa kujua kwa nini Yesu alitenda miujiza ile? Yesu hakuja kubadilisha mpango wa Mungu, hakuna kuleta mwisho wa magonjwa, mwisho wa vifo vya miili au mwisho wa njaa ya mwili. Bali miujiza ile ililenga kuonesha ukuu wa Mungu, kwamba Mungu akitaka hakuna anachoshindwa. Lakini mpango wake juu ya maisha ya mwanadamu uliachwa vile vile.
Mungu anamshirikisha mwanadamu katika uumbaji, katika kukuza watoto na hata katika uponyaji. Maana yake katika jambo ambalo Mungu anatenda, ameweka ushiriki wa mwanadamu. Usipotaka kushiriki usimjaribu Mungu.
Rais usiwapotoshe watu, wala usipotoshe neno la Mungu.
Yaani sisi tunaowategemea Polisi na wakurugenzi kupora kura, sisi tunaoruhusu wasiojulikana wapoteze na kuua watu wanaotukosoa, sisi tunaowabambikia watu kesi za uhujumu uchumi, leo ndio tuwe na imani kuwazidi Maaskofu na Maimamu na hata Papa, maajabu makuu! Tusimtanie Mungu, tusimchezee Mungu. Mungu anatuvumilia katika uovu wetu kwa sababu anataka kutoa nafasi ya kwetu ya kutubu, badala ya kutubu, tunamjaribu?
Tumwombe Mungu awajalie watawala japo hekima ndogo ya kukabiliana na janga hili la corona. Na wala wasimtumie Mungu kuficha udhaifu wao wa wajibu kama viongozi.
Watawala adhabu yenu mbele za Mungu ni kubwa mnapowapotosha wasio na uelewa. "Ole wao wanaowapoteza wadogo hawa, wanastahili kufungiwa jiwe la kusagie shingoni na kutumbukizwa majini", asema Bwana.