Rais John Magufuli amempa miezi miwili mtoto wa dada yake, ambaye ni Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoa wa Pwani, Mhandisi Martin Madulu, kuhakikisha umeme unafika kwenye kiwanda cha kusindika matunda cha kampuni ya Bakhresa kilichomo ndani ya mkoa wake, vinginevyo atamtumbua.
Rais alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo Vikindu wilayani Mkuranga mkoani humo, agizo ambalo limekumbusha jinsi alivyomtumbua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliyekuwa anadaiwa kuwa rafiki yake wa karibu.
Uteuzi wa Kitwanga kwenye Baraza la Mawaziri ulitenguliwa na Magufuli Mei 20, mwaka huu baada ya Mbunge huyo wa Misungwi (CCM) kuingia bungeni akiwa amelewa na kujibu swali lililoelekezwa kwenye wizara yake.
Na katika uzinduzi wa kiwanda hicho jana, Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi, alilazimika kutoa agizo hilo kwa mpwa wake mara tu baada ya kuelezwa na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Aboubakar Bakhresa, kuwa wanalazimika kutumia jenereta kukiendesha kutokana na kutokuwapo kwa nishati ya umeme wa Tanesco.
Aboubakar alimweleza Rais kuwa upatikanaji wa umeme bado ni changamoto katika kiwanda hicho na kwamba wanahitaji umeme wa megawati 10 ili kukiendesha.
“Meneja wa Tanesco mkoa wa Pwani, wewe Madulu, tena ni mtoto wa dada yangu, nitakutumbua wewe!" Alisema Rais Magufuli na kufanya umati uliohudhuria halfa hiyo uangue kicheko.
"Ulifanya kazi nzuri ulipokuwa Kagera na Tanga, sasa fanya kazi na hapa. "Nataka ndani ya miezi miwili umeme uwe umefika hapa, mimi huwa sibembelezi mtu, mkono wangu ni mwepesi sana kutumbua.”
Rais Magufuli alimtaka meneja huyo kushirikiana na meneja wa Tanesco wilaya ya Mkuranga, Dar es Salaam na Pwani kuhakikisha umeme unafika kwa haraka katika kiwanda hicho.
Alisema ni jambo la kushangaza kwa Tanesco kutopeleka umeme katika kiwanda hicho wakati nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.
Rais alisema ni jambo ambalo haliingii akilini tangu upimaji wa kiwanja ulipoanza hadi kiwanda kinajengwa na kukamilika, umeme haujafika katika kiwanda hicho wakati makao makuu ya Tanesco yako kilomita chache kutoka kilipo.
Alisema kutokana na kiwanda kutumia jenereta kujiendesha, gharama za uzalishaji zinakua juu, hali itakayosababisha hata wafanyakazi kulipwa mishahara midogo.
“Leo (jana) ni Oktoba 6, kabla ya mwezi wa 12 (Desemba), nataka umeme uwe umefika hapa," alisema Rais Magufuli. "Tena ninatamka kwa dhati kutoka moyoni mwangu; kama mnataka kazi, basi umeme uwe umeshafika hapa. Nyie Tanesco ni watu wa ajabu sana, sijawahi kuona... ila Madulu fanya kazi usiogope sikutumbui leo,” alisema Magufuli na kufanya umati uangue kicheko kwa mara nyingine.
Alisema Tanesco inapaswa kujipanga kwa kuangalia maeneo ya kipaumbele ya kupata umeme na "ikiwezekana wasipeleke umeme katika magereza ya wafungwa, lakini uzalishaji viwandani ni lazima umeme upewe kipaumbele".
Source:Nipashe.