Mawaziri watetea safari za Kikwete
Ramadhan Semtawa na Elizabeth Mjata
MAWAZIRI wawili wa serikali ya awamu ya nne waliokuwa wameongozana na Rais Jakaya Kikwete katika nchi za mashariki ya mbali, wamezitetea ziara za Rais nje ya nchi, wakisema zina manufaa makubwa kwa taifa.
Wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro alisema ziara hizo zina manufaa makubwa kiuchumi na kidiplomasia, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Basil Mramba, aliwabeza wanaopinga ziara hizo.Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na wingi wa ziara hizo, Dk Migiro, alisema Rais hawezi kufungwa miguu kwa kukaa Ikulu.Alifafanua kwamba Rais Kikwete alishinda uchaguzi kwa kutumia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo lazima aende nje kutafuta njia za kutekeleza ilani hiyo.
Waziri Migiro aliongeza kwamba, hadi sasa haionyeshi kwamba Rais Kikwete amefanya ziara nyingi, ikilinganishwa na umuhimu zaidi wa kufanya ziara hizo."Kwanza labda niseme, hadi sasa Rais hajasafiri sana nje, bado anapaswa kusafiri zaidi ajitambulishe na pia kueleza sera na msimamo wa serikali yake, ikilinganishwa na zilizopita," alisema Dk Migiro na kuongeza:
"Lakini pia Rais hawezi kufungwa miguu kukaa Ikulu, amechaguliwa na wananchi kwa kutumia ilani ya chama, hivyo lazima angalie njia za jinsi ya kuitekeleza."Dk Migiro alisema kila nchi duniani inapoona kuna mabadiliko ya uongozi katika nchi fulani, huwa inataka kujua msimamo wa serikali mpya iliyoingia madarakani.
Akifafanua zaidi, Dk Migiro alisema Tanzania nayo imekuwa ikiongozwa na serikali tofuati tangu uhuru na imekuwa ikitekeleza mambo tofauti, hivyo ni lazima Rais Kikwete azihakikishie nchi rafiki kwamba atadumisha uhusiano uliokuwepo tangu uhuru.Katika kuelezea mafanikio ya ziara ya Rais kuanzia Oktoba 19, Dk Migiro alisema imekuwa na manufaa makubwa kuanzia Japan, China, Korea Kusini, Dubai na Falme za Kiarabu.
Kwa upande wake, kwa wakati tofauti, Waziri Mramba alitumia nafasi ya kuelezea mafanikio ya ziara hiyo, kumtetea Rais Kikwete kuwa amekuwa akitumia fedha nyingi katika ziara badala ya kutatua matatizo ya ndani, aliwashangaa wanaotoa shutuma hizo."Nawashangaa watu hawa, Rais Kikwete ana haki ya kwenda nje ili kuzungumzia masuala ya uchumi wa nchi yake na ikiwezekana apate wafadhili ambao watasaidia uchumi wa Tanzania kukua," alisema Mramba.
Mawaziri hao wametoa kauli hizo ikiwa ni miezi kadhaa baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuutangazia umma wa Watanzania kuwa ziara za Rais Kikwete ni za manufaa kwa Watanzania, kwani amekuwa akipata misaada ya kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu.Hatua ya mawaziri hao inafuatia kauli za Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, aliyesema Rais Kikwete amekuwa akisafiri zaidi nje kuliko kuangalia matatizo ya ndani.
Akizungumzia baadhi ya mafanikio hayo, Dk Migiro alisema ni pamoja na China kukubali ksaidia ujenzi wa barabara Maangaka-Masasi yenye urefu wa kilomita 54 ambao utaanza rasmi mwaka 2008.Alisema manufaa mengine kutoka China ni mkopo nafuu wa dola za Marekani 20 milioni (Sh25 bilioni) kwa ajili ya kusaidia bajeti ya maendeleo katika Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta) na fedha za ujenzi wa barabara ya Arusha-Namanga.
Kwa upande wa Dubai na Falme za Kiarabu, alisema zimeonyesha nia hasa kwa wafanyabiashara wake kuja kufanyabiashara nchini na Japan imeonyesha nia ya kusaidia miradi ya maji mijini na vijijini, hasa Zanzibar.Kwa upande wake, Mramba alisema Wafanyabiashara wa Urusi wanashindwa kuja kuwekeza nchini kutokana na kukosekana kwa hoteli za kutosha na vyakula vya Kirusi.Alisema kutokana na hali hiyo, wizara yake imejitolea kuwasaidia wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kuwekeza katika sekta ya hoteli kujitokeza kwa ajili ya kuunganishwa na wawekezaji kutoka nchi hizo.
"Wafanyabiashara wa Urusi na wengine wengi wanataka kuja hapa, lakini wanakumbana na kikwazo cha makazi na vyakula," alisema Mramba.Waziri Mramba alisema akiwa Japan, pia alipata malalamiko ya aina hiyo, kwani baadhi ya wafanyabiashara walikuja kama watalii na kushika nafasi kwenye hoteli moja nchini, lakini mwezi mmoja kabla ya safari yao, walitumiwa taarifa kwamba hoteli haina nafasi.
Alisema katika ziara hiyo, wamekutana na wafanyabiashara mbalimbali ambao wana uwezo wa kuwekeza katika sekta mbalimbali, lakini tatizo Tanzania imeshindwa kufikia vigezo wanavyotaka, ikiwamo miuondombinu.Aliwataka Watanzania watakaotaka kufanya biashara na wenzao wa Urusi kufika wizarani kwake, ili kuwaelekeza jinsi wanavyoweza kukuza biashara ya Tanzania na pato la nchi.Mramba, alisema wamebaini China walivyo na uwezo mkubwa wa kutengeneza umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kikiwemo upepo. Tanzania ina sehemu nyingi ambazo zina upepo mkali.