SEHEMU YA 169
Watu walizidi kuponywa magonjwa yao, huduma aliyokuwa akiifanya Peter ilionyesha ni kiasi gani muinjilisti huyo alivyokuwa na upako mkubwa. Wachawi walibadilisha maisha yao na kumuabudu Mungu, waliokuwa wazinzi, wakaacha njia zao na kumfuata Mungu.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika mikutano mbalimbali ya Injili ilionyesha ni kwa jinsi gani Mungu alikuwa akitenda miujiza kutokana na huduma aliyokuwa nayo muinjilizisti Peter.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, aliendelea kumtumikia Mungu, aliyabadilisha maisha yake na katika kipindi hicho, mke wake, Lydia alikuwa mjauzito.
Huo ulikuwa mkutano wake wa pili ndani ya mwaka mmoja, Uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza ulijaza watu wengi waliohitaji ukombozi katika maisha yao. Kila siku Peter alikuwa mtu wa kukaa chumbani mwake na kuanza kuomba, hiyo ndiyo ilikuwa siri kubwa ya yale yaliyokuwa yakifanyika, hakujinyakulia utukufu, kila kitu alimuachia Mungu kwa kuamini kwamba yeye ndiye aliyekuwa akifanya yote hayo.
Baada ya siku kadhaa, akapokea wageni kutoka serikalini, walifika nyumbani hapo na kuzungumza naye kwamba alikuwa akihitajika haraka iwezekanavyo nchini Ujerumani. Aliposikia hivyo tu, alijua kwamba hiyo itakuwa ishu ya Tatiana, hakujua ni kitu gani kilichoendelea, ila alichokifanya ni kwenda huko.
Hakutaka kwenda peke yake, aliongozana na mkewe mpaka nchini Ujerumani ndani ya Jiji la Berlin, hapo, wakaunganisha mpaka hotelini ambapo gharama zote zilikuwa kwa balozi huyo. Hotelini hapo, Peter alikuwa na mawazo mno, alimkumbuka Tatiana, aliyakumbuka yote aliyofanyiwa lakini katika yote hayo, hakuonyesha chuki, yalikuwa yamepita na aliyaacha yawe hivyo.
“Usifikirie sana mume wangu kuhusu Tatiana!” alisema mkewe.
“Najua, ni muda mrefu sana, msichana huyu amekuwa kwenye matatizo mengi sana, nahisi Mungu anataka kufanya kitu kwa ajili ya maisha yake,” alisema Peter huku akiifungua Biblia na kuanza kupitia vitabu kadhaa.
“Hata mimi nakubaliana nawe, cha msingi tukamuone tu, nahisi kuna mengi Mungu atataka kufanya kwa ajili ya maisha yake,” alisema mke wake.