SEHEMU YA 66...
Mtu wa kwanza kabisakumuona mbele yake alikuwa Dk. Buffet. Alivalia koti refu jeupe huku shingoni mwake akiwa ameipitisha mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo. Kwa kumwangalia tu, alikuwa mwanaume mzuri wa sura ambaye kila alipokuwa akitabasamu, uzuri wake uliongezeka zaidi.
Tatiana alipomuona Dk. Buffet, akausikia moyo wake ukimripuka kwa furaha, hakuamini kama duniani kulikuwa na watu wenye sura nzuri kama alivyokuwa daktari huyo. Hapohapo, akauhisi moyo wake ukimuingiza daktari huyo na kumpenda kwa mapenzi ya dhati.
Hakujua Smith alionekanaje, hakujua sura yake ilikuwa vipi lakini kitu alichokuwa akikiamini ni kwamba mwanaume huyo hakuwa na sura nzuri kama aliyokuwa nayo Smith. Dk. Buffet alipokuwa akitabasamu, Tatiana alijiona kama anamwangalia malaika.
Kuna wakati alitamani kumvutia kwake, ambusu kwani hakukuwa na kitu alichokuwa na hamu kukifanya kwa daktari huyo kama hicho. Kila wakati alipokuwa akimwangalia, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimdunda tu huku akihisi damu yake ikizunguka kwa kasi kubwa mishipani mwake.
“Vipi?” aliuliza Dk. Buffet kwani hata macho aliyokuwa akimwangalia yalionekana tofauti.
“Poa, nafurahi kuona,” alisema Tatina kwa sauti iliyojaza mahaba tele, sauti ndogo ambayo hakutaka manesi waliokuwa chumbani humo kuisikia.
Huo ndiyo ulikuwa wakati wake wa kuangukia katika penzi la mtu mwingine kabisa ambaye hakuwa amemtegemea kabisa maishani mwake. Hata Smith alipokuja hospitalini hapo na kumwangalia, hakuvutiwa naye kama alivyokuwa Dk. Buffet ambaye kila alipokuwa akitabasamu tu, moyo wake ulikuwa hoi.
Siku hiyo ambayo alitakiwa kubaki hospitalini hapo alitaka kuitumia vilivyo, hakutaka kuona akiendelea kuteseka mapenzini na wakati mtu ambaye alimuweka katika hali hiyo alikuwa na uwezekano mkubwa wa kumpata.
Alichokifanya usiku alipokuwa kitandani akichati na Smith ni kumuomba nesi amuitie Dk. Buffet ambaye pasipo kuhisi chochote kile alifika haraka chumbani hapo.
“Naomba manesi watoke, kuna kitu nataka kukwambia,” alisema Tatiana kwa sauti ndogo, hilo halikuwa tatizo, Dk. Buffet akafanya hivyo na kubaki wawili chumbani.