SEHEMU YA 92
“Lakini Peter....”
“Lydia, nina moyo wa nyama, ninaumia kama wengine wanavyoumia, nisingeweza kuvumilia na ndiyo maana nimetoka Dar mpaka hapa kwa ajili yako tu, si mwingine, nimekuja kwa ajili yako, sikutaka kuona nikiendelea kuumia zaidi,” alisema Peter huku kwa mbali machozi yakianza kumlenga.
Maneno hayo aliyozungumza peter yaliuchoma moyo wa Lydia, akabaki akimwangalia tu pale kochini alipokuwa amekaa. Kwa mbali, hata naye machozi yakaanza kumlenga. Hapo ndipo alipogundua kwamba Peter alikuwa na upendo wa dhati kwake, hakuwa kama watu wengine ambao walitamani kuwa na mwanamke ili mradi, kwa Peter, alionekana kuwa tayari kufanya lolote lile lakini mwisho wa siku ampate.
“Naomba unisamehe Peter, nilihisi tofauti na ulivyofanya,” alisema Lydia huku akianza kububujikwa na machozi.
“Ooppss...! Lydia, nimefanya hivi kwa kuwa ninakupenda, sitaki kukutania katika hili. Nimekuwa nikikufikiria sana na nisingekuwa tayari kukuacha ukiondoka, nilihitaji kukuonyeshea mapenzi ya dhati Lydia, hakukuwa na kingine zaidi ya hicho, ninakupenda mno,” alisema Peter huku akisimama na kuanza kumsogelea msichana huyo.
Lydia naye hakubaki pale alipokuwa, akapiga hatua kumsogelea Peter alipomfikia, wote wawili wakakumbatiana na kuanza kulia, upendo wa dhati ukaanza kuchipua moyoni mwa msichana Lydia, machozi yao yakaanza kulowanisha migongo yao. Huku wakiwa kwenye hisia kali za kimapenzi, mara mchungaji Marcus na mkewe wakatokea sebuleni hapo, kile walichokiona, kikawashtua.