Jana katika hotuba yake ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi nilidhani labda rais Magufuli atautaja rasmi mshahara wake na ule wa viongozi wengine waandamizi wa umma.
Kuna wakati katika hotuba hiyo alisema hata yeye anapenda mshahara au sijui anapenda mshahara mzuri (nukuu siikumbuki vizuri).
Niliposikia anazungumzia mishahara hamu ya kusikiliza anachokiongea ikazidi kukolea. Mwishowe nikaishia kuambulia patupu.
Sasa leo ni tarehe 2 mwezi Mei. Kama sijakosea, ni mwezi sasa umepita tokea iliporipotiwa kuwa rais alitoa ahadi ya kutoa pay stubs zake akisharudi Dar kutoka mapumzikoni huko Chato.
Mpaka hivi sasa sioni hata mwelekeo wa hicho kitu kufanyika. Je, ina maana tulidanganywa? Kama tulidanganywa, tulidanganywa na nani sasa? Hao waliosema kuwa rais kaahidi hivyo ilhali labda hata hakuongea nao au tulidanganywa na rais mwenyewe?
Mimi hili suala la mishahara ya viongozi wa umma nilianza kulivalia njuga takribani miaka 9 iliyopita na nitalivalia njuga mpaka siku yangu ya mwisho au mpaka hapo kitakapoeleweka.
Ni haki yangu ya msingi kabisa kujua hao viongozi ninawalipa kiasi gani na kwa ujumla wake ni haki yangu ya msingi kujua pesa zangu za kodi zinatumikaje.