Papa anasema sehemu ambayo huzungumzia vishawishi ilitafsiriwa vibaya.
Habari SATURDAY, DECEMBER 9, 2017
Papa ashauri sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni ifanyiwe marekebisho
0
Vatican City, Vatican. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito akitaka sala maarufu ya Kikristo ya Baba Yetu Uliye Mbinguni ifanyiwe marekebisho kwa vile tafsiri yake haiendani na ukweli wa mambo.
Katika wito wake, Papa anasema sehemu ambayo huzungumzia vishawishi ilitafsiriwa vibaya.
Amesema tafsiri kwamba "usitutie katika vishawishi (majaribu/majaribuni)" itazamwe upya kwa vile ilifanywa vibaya kwa sababu Mungu huwa hawaongozi binadamu kutenda dhambi.
"Usiniache nikaingia kwenye vishawishi kwa sababu ni mimi nitakayeanguka, si Mungu anayetutia katika vishawishi na kisha kutazama nilivyoanguka. Baba hawezi kufanya hivyo, baba hukusaidia uinuke upesi,” amesema Papa Francis
alipozungumza na televisheni ya TV2000 inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Italia.
Kiongozi huyo ambaye amekamilisha ziara yake hivi karibuni katika mataifa ya Mynmar na Bangladesh amependekeza watu watumie "usituache tukaingia katika vishawishi” kama neno mbadala la lile la sasa.
Sala ya Baba Yetu ndilo linalofahamika vyema zaidi miongoni mwa maombi ya Kikristo.Papa Francis amesema Kanisa Katoliki nchini Ufaransa sasa linatumia tafsiri hiyo ya "usituache tukaingia katika vishawishi" kama mbadala na kwamba jambo kama hilo linafaa kufanywa kote duniani.
Maneno hayo ni tafsiri kutoka kwa tafsiri ya biblia ya Kilatini ya karne ya nne ambayo iliidhinishwa rasmi na kanisa Katoliki karne ya 16, ambayo ilitafsiriwa kutoka kwa maandiko ya kale ya Kigiriki, Kiebrania na Kiaramaic.