Nusu Siku Ndani ya Jeneza -19-
ILIPOISHIA JANA.
Baadhi ya viongozi duniani waliwahi kupinduliwa na watu wenye nyota ya Simba kwa sababu wao hawakuwa na nyota hiyo. Waliwatawala wakiwa na nyota dhaifu sana.
Tukiachana na yote, namaliza na nyota ya Simba kwa kusema kuwa wengi wenye nyota hii ni wanamichezo, masonara, wanamitindo, wacheza sinema na kazi zinazohusiana na mambo ya vijana.
SASA ENDELEA
Kabla sijaendelea mbele na lile darasa nililolikuta kule kwa viumbe napenda kuwajulisha kwamba, kila binadamu ana nyota yake inayoambatana na maisha yake ya kila siku.
Nasema hivi kwa sababu nilimsikia yule kiumbe akisema hivi:
Unajua kama binadamu wote kule duniani wangejua uwezo wa nyota zao wangekuwa wanafanya makubwa sana. Lakini hamna kitu kwa sababu hawajui lolote lile. Kila binadamu anayezaliwa na mwanamke ana nyota yake inayomwangazia, hata yule nabii wenu (Yesu) naye alizaliwa akiwa na nyota yake ndiyo maana kwenye maandiko yenu mmeandika kwamba nyota yake ilionekana kutoka upande wa Mashariki.
Ile yenyewe inadhihirisha kwamba kila binadamu ana nyota yake. Na nyota kwa kawaida inaonesha tabia ya mtu, karama yake au kule duniani mnasema kipaji au kwa nini binadamu alizaliwa.
Lakini wapo binadamu ambao nyota zao huchukuliwa na inapotokea hivyo yale yote yanayohusu nyota yake yanakuwa hayapo tena katika maisha yake.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya elimu ya kawaida na nyota kila kukicha, suala la elimu si la nyota na nyota ya binadamu haipatikani shuleni au vyuoni ndiyo sababu wapo binadamu hawana elimu kabisa lakini wana mafanikio makubwa katika maisha.
Nyota pekee ndiyo inayoweza kumfanya binadamu kuwa mzuri au mtaalam wa jambo fulani, kama wanamuziki, wacheza mpira, madereva au mambo mengine mengi yenye kutaka kufanywa na watu mbalimbali.
Nyota huweza kumpa akili ya ziada ndani ya akili yake akaweza kufanya jambo ambalo wengine walilishindwa kwa kutokuwa na akili hiyo.
Lakini nyota hiyohiyo ndiyo inayoweza kumfanya mtu angae na kuonekana zaidi mbele ya watu, au tuseme mtu anakuwa na mvuto.
Siku hizi binadamu wengi kule duniani wanahangaika kuanzisha biashara mbalimbali tena kubwa tu, wanakopa mikopo mikubwa tu, lakini hawaoni maendeleo yoyote zaidi ya kudidimia kwa sababu nyota zao zinazowaongoza zimezolewa na wabaya wao ili wateseke au ili wakawape watu wengine.
Wapo binadamu wenye utaalam wa kumpoka mtu nyota yake yenye mafanikio ya kibiashara na kwenda kuwapa watu wengine ambao wanateseka kusaka maisha mazuri yenye mafanikio.
Kuna mwenye swali kabla sijaendelea? aliuliza yule kiumbe. Mimi nilinyoosha mkono, akaniuliza wewe unasemaje? Halafu unajua kule duniani wanadamu, nduguzo bado wanaomboleza kifo chako?
Sijui, nilimjibu.
Ndiyo hivyo nilivyokwambia. Leo mchana wa kule jeneza lako linaandaliwa ili ukazikwe.
Mimi?
Wewe ndiyo. Lakini sidhani kama utazikwa kwa muda huu tunaouendea wa nusu siku. Haya uliza swali.
Nilibabaika kidogo kutokana na mazingira ya kauli ya yule kiumbe, lakini nikajitutumua na kuuliza:
Sasa binadamu atajuaje kuwa nyota yake imechukuliwa na wabaya wake?
Aliniangalia kwa macho yaliyoonesha kuwa swali langu lilikuwa na umakini wa hali ya juu, akasema: Binadamu akiwa hana nyota inayomwangazia maisha yake hata kama atakuwa ana elimu ya juu ya vyuo vikuu lazima atakosa dira ya maisha yake. Kama ni mfanyabiashara haitakwenda vizuri, atakuwa anadaiwa na mabenki na taasisi za fedha.
Au angalia mtu anayefanya kazi kubwa, muda mwingi yupo kazini analipwa mshahara mkubwa tu lakini hana msingi wa maisha kwa kuwa nyota yake imepokwa na wabaya wake.
Katika hili kazi ipo, siwezi kushauri hasa nini cha kufanya kwani nafasi hainiruhusu hapa lakini kuna kitu cha kufanya.
Basi, yule kiumbe akaendelea kufundisha kuhusu nyota sasa.
Nyota nyingine ni ya sita, inaitwa Mashuke au lugha ya kigeni inaitwa Virgo. Binadamu kama nyota yake haijapokwa na wabaya wake, mwenye nyota hii ambayo inamhusu aliyezaliwa Agosti 23 hadi Septemba 22, mafanikio yao makubwa ni kwenye kazi ya uchapishaji, uongozi wa mahali, kazi ya afya, biashara mbalimbali na ukatibu (secretary).
Nyota hii haina watu maarufu sana kama ya simba kwa sababu mashuka huweza kufunikwa na nyota nyingine mbalimbali nyingi, haina nguvu kubwa ya kupambana.
Nyota nyingine ni ya saba ambayo ni Mizani au kwa lugha ya kigeni ni Libra. Watu wa Libra walizaliwa Septemba 23 mpaka Oktoba 23, hawa ndiyo wanahusika.
Kazi zao zenye kuwapa mafanikio ni uhusiano katika jamii, ushauri wa masuala ya ndoa. Wengi waliotaka kupeana talaka waliposuluhishwa na wenye nyota hii walirudiana na ndoa kudumu.
Pia ni wafanyabishara wakubwa sana hasa ya mambo ya sanaa, mambo ya sheria au uhakimu. Mtu mwenye nyota hii akiwa wakili anashinda sana kesi na wateja kwake hawapungui. Kama atakuwa hakimu atakuwa anatoa hukumu ya haki kwenye kesi ngumu.
Je, nini kiliendelea? Kesho wakati kama huu.