Niliwahi kusoma makala moja ktk gazeti la raia mwema iliyoandikwa na mjengwa, akisimulia kisa cha mfalme mmoja mwaminifu kwa nchi yake, ni kisa cha kuwasha na kuzima mishumaa. Kwamba mfalme huyo alitembelewa na mgeni nyumbani kwake, bila shaka mgeni huyo alikuwa ni mwandishi wa habari, hivyo alikuwa akimhoji mfalme maswali mbalimbali. Wakati mfalme akihojiwa maswali hayo alikuwa akiwasha mshumaa fulani, mara anauzima na kuwasha mshumaa mwingine kwa kipindi chote cha mahojiano. Kitendo hicho kilimshangaza sana yule mgeni, kwa kuwa hakuwa ameelewa mantiki ya mfalme yule kuwasha na kuzima mara mshumaa ule mara huu, na hatimaye swali la mwisho alimuuliza mfalme yule ni kwanini katika muda wote wa mahojiano alikuwa anawasha na kuzima mishumaa, kwamba ni kwanini baada ya kuwasha mshumaa wa kwanza hakusubiri uishe ndio awashe mshumaa mwingine. Mfalme yule alimjibu kwamba alikuwa akiwasha na kuzima mishumaa ile kulingana na maswali aliyokuwa akiulizwa na mgeni yule, kwamba alikuwa akiulizwa maswali ya kiofisi kama mfalme anawasha mshumaa wa serikali, na pale alipokuwa akiulizwa masuala binafsi yaani yasiyo ya kiofisi kama vile idadi ya watoto wake, wake zake na mifugo yake alikuwa akizima mshumaa wa serikali na kuwasha mshumaa wake, kwa kuwa haikuwa maadili kwake kutumia mali ya serikali kwa mambo yake binafsi.
Baada ya kueleza kisa cha mfalme huyo, sasa ngoja nieleze ni kwa vipi Waziri mkuu Pinda ni fisadi kama walivyo mafisadi wengine nchini. Nilitembelea wilaya ya Mpanda Mkoa mpya wa Katavi mwezi August mwishoni mwaka huu. Nikiwa huko nilishangaa kukuta magari mengi makubwa ya JWTZ yakibeba matofali kutoka Mpanda mjini kuyapeleka Mpimbwe kibaoni nyumbani kwa waziri mkuu. Nikamuuliza dereva mmoja wa magari hayo kama walikuwa wakijenga kambi ya jeshi huko.Akanijibu hapana, hawajengi kambi, wao wapo kule kwa ajili ya kubeba mahindi ya serikali toka Sumbawanga kuyapeleka Mpanda ambapo yanapandishwa kwenye garimoshi kwenda kwenye maghala ya akiba ya taifa kanda ya ziwa. Kwa hiyo wakifika mpanda wakishusha mahindi wanapakia matofari ya kuchoma ya waziri mkuu na kuyasusha kibaoni kwa waziri mkuu umbali wa kama km 100 toka mpanda mjini kisha kuendelea hadi sumbawanga kupakia mahindi, na wanaendelea hivyohivyo. Nilishangaa sana, na nikauliza kwanini basi hakufyatulia matofali hayo hukohuko kibaoni badala ya kufyatulia mjini na kuyabeba kuyapeleka kijijini, akanijibu kwamba kule kibaoni haikuwa rahisi rahisi kwake waziri mkuu kupata wafungwa wa kumfyatulia matofari yale. Hapo nikaelewa kwamba kumbe licha ya kutumia magari ya JWTZ kubeba matofali yake hata hayo matofari katumia rasilimali ya serikali kuyafyatua, na huu ni ufisadi mkubwa uliopitiliza. Kutumia wafungwa kufyatua matofali ya mtu binafsi ni ufisadi, na kutumia magari ya JWTZ kubeba matofali hayo ni ufisadi pia kwa kuwa hata kama magari yale yanapita pale kwa waziri mkuu, lakini bado yanakuwa yametumia muda mwingi wa kupakia na kushusha matofali yale na hivyo zoezi la kubeba mahindi litachukua muda mrefu zaidi kwa sababu yake. Kitendo hicho ni ufisadi mkubwa, na hamna namna yoyote ya waziri mkuu kujitetea kwa hili, na kama ingekuwa ni nchi ya maadili kama nchi za wenzetu hili pekee linatosha kwa waziri mkuu kujiuzulu kwa ufisadi.