Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliua kwa Kukusudia--31-

ILIPOISHIA KWENYE IJUMAA:
"Ni kweli Inana, sikuwa sawa kwani nina matatizo makubwa mno mdogo wangu."
"Matatizo gani tena dada yangu jamani?" Inana aliuliza huku akinikazia macho kwa shauku kubwa ya kutaka kujua kilichonisibu.
"Elhakimu alinibaka na kunitupa mtaroni."
"Unasemaje wewe?" Inana aliuliza huku machozi yakitengeneza mifereji machoni mwake.
SASA ENDELEA…



Kufumba na kufumbua machozi yakaanza kumtiririka Inana. Nilipoona hivyo, machungu yakanishika nami nikajikuta nikianza kulia. Tulilia kwa uchungu mkubwa huku tukimuuliza Mungu kulikoni aendelee kuruhusu matatizo yazidi kutuandama.
"Kwa nini sisi Mungu, kwa nini jamani?" Inana alilia huku akitamka maneno hayo.
"Hapana usiseme hivyo Inana, huenda Mungu ana mpango wake kwetu," nilimtia moyo mdogo wangu Inana huku nikiendelea kulia kwa uchungu na maumivu makali yasiyokuwa na kipimo wala kusimulika kwa namna yoyote ile.

Moyoni niliendelea kuwachukia mno wanaume. Nikaona si viumbe wema hata kidogo. Wakati tukiendelea kulia, ghafla kuna jambo lilinishitua mno na kujikuta nikisitisha kidogo kulia. Kilichonishitua ni kiwango cha kulia alichokuwa akikionesha Inana. Kwani alilia kwa sauti kubwa na kwa muda mrefu mno. Hakika alionesha uchungu mwingi kuliko hata mimi ambaye nilikuwa nimekumbwa na tatizo hilo.
Ikabidi ninyamaze na kuanza kumbembeleza kwa kumtaka aache kulia kwani kama ni kubakwa tayari nilishabakwa. Na kwa wakati huo nilikuwa nikielekea polisi kudai haki yangu.

"Hapana dada, kuna jambo limeniuma zaidi," alianza kusimulia Inana kwa sauti ya kitetemeshi iliyoambatana na kwikwi ya hasira.
"Jambo gani tena Inana zaidi ya hili la kwangu la kubakwa na Elhakimu?," nilimuuliza nikitaka kujua ni jambo gani lililomuumiza zaidi Inana kama alivyokuwa akidai.
"Samahani kwa kuwa nilikuficha dada, hata mimi huyo Elhakimu alinibaka nyumbani kwa mdogo wake ninapofanya kazi."

Nilikuwa kama niko ndotoni. Maneno ya Inana nikayachukulia kama ndoto ndefu ambayo kwa hakika niliamini kama ingekoma muda si mrefu na kubaki katika hali yangu ya kihalisia.
"Ni kweli kabisa dada, Bosi wako Elhakimu alinibaka mwezi mmoja uliopita sasa, lakini niliogopa kukuambia kwani ni jambo la aibu na udhalilishaji wa hali ya juu mno," alisema Inana huku nikizidi kumshangaa kwani sikuwa tayari kabisa kuyaamini maneno yake.

Kabla sijasonga mbele na simulizi hii, hapa naomba niweke wazi jambo moja muhimu sana.Ukweli ni kwamba hadi sasa nikiwa nasimulia hivi, sijawahi kuisahau siku hiyo kwani ilibadili kabisa mfumo mzima wa maisha yangu. Moyoni nikaanza kujiona kama nimebadilika na kuwa na roho chafu ya kinyama. Nilianza kuhisi harufu ya damu ikinukia kutoka kila pande ya dunia na ulimwengu kwa ujumla.
Basi ngoja niendelee. Inana akanisimulia mkasa mzima kwa jinsi alivyobakwa na Elhakimu kabla hajanibaka mimi. Akasema siku ya tukio Elhakimu alienda nyumbani kwa mdogo wake aitwaye Ashraf mahali ambako mdogo wangu alikuwa akifanya kazi. Kama utakumbuka ni Elhakimu ndiye alinipa wazo la kumtafutia mfanyakazi Ashraf na kulazimika kumfuata Inana huko Chalinze nilikokuwa nimemuacha akihangaika na vibarua vya kujitafutia riziki.
Haya ngoja niendelee. Inana alisema kuwa siku hiyo alikuwa peke yake nyumbani ndipo Elhakimu akafika na kuanza kuzungumza naye. Katika mazungumzo yao, Inana alikuwa akishangaa kuona Elhakimu akimsogelea kila sekunde iliyokuwa ikiondoka.
Inana akaendele kusimulia kuwa, Elhakimu alianza kumshika pasipo ridhaa yake na kuanza kumvua nguo kwa nguvu huku akimwambia maneno ya kimapenzi. Pamoja na kukataa huku akitoa upinzani mkubwa wa kujinasua mikononi mwake, Elhakimua alizidi kutumia nguvu nyingi na hatimaye kufanikisha kumvua nguo zote na kuanza kumwingilia mwilini bila huruma!
Akaweka wazi kuwa, baada ya tukio hilo Elhakimu aliondoka na kumuacha akiwa hajitambui na damu nyingi zikimtoka lakini alipozinduka na kukuta hakuna mtu, aliamua kujikanda kwa kutumia majani ya mtapei yalitokuwa nyuma ya nyumba hiyo ambapo aliyachemsha. Hata alipokuja bosi wake hakuthubutu kumweleza chochote.
Akaendelea kuishi kwa taabu na kujifichaficha hadi alipopona kabisa.

Hadi Inana anamalizia kusimulia mkasa huo wa kubakwa na Elhakimu, sikumbuki vyema machozi yalikuwa yamefika wapi kwani hata macho yalikuwa hayawezi kufumbua vizuri kutokana na kuzidiwa na wingi wa machozi. Haraka nikajikuta nikigairi kwenda kituo cha polisi kuendelea na kesi na kujikuta nikiamua kuchukua uamuzi hatari mno.

Je, ni uamuzi gani huo? Itakuwaje? Kufuatilia leo jioni Usikonde tu

 
Huyu Elhakimu si zinaa tu lilomsumbua bali ana pepo mbaya wa uuaji. Ni hadithi tu lakini yanatukia haya ktk jamii ndiyo maana MziziMkavu kayaona. Asante sana.
 
Last edited by a moderator:
Niliuwa kwa kukusudia--32-

ILIPOISHIA:
Hadi Inana anamalizia kusimulia mkasa huo wa kubakwa na Elhakimu, sikumbuki vyema machozi yalikuwa yamefika wapi kwani hata macho yalikuwa hayawezi kufumbua vizuri kutokana na kuzidiwa na wingi wa machozi.

Haraka nikajikuta nikigairi kwenda kituo cha polisi kuendelea na kesi, nikaamua kuchukua uamuzi hatari mno. SASA ENDELEA…

Ulikuwa ni uamuzi wa kuua! Kwa dhati kabisa nilikuwa nimedhamiria kuua. Ndiyo, kumuua Elhakimu. Moyo wangu ulijawa na chuki kali mno dhidi yake na hakika sikuona adhabu au kisasi kingine alichostahili mwanaume huyo zaidi ya kifo.

Nikamwambia Inana turudi nyumbani kwani nahitaji zaidi muda wa kupumzika. Akili yangu ikawa inawaza ni kwa jinsi gani nitaweza kuikamilisha kazi iliyokuwa mbele yangu. Kazi ya kumwaga damu. Damu ya Elhakimu.

Tulirudi na Inana hadi nyumbani kwangu. Tulipofika nikajilaza kitandani kwangu huku machozi yakinitiririka kimyakimya. Hata Inana alikuwa akilia japo awamu hii si kwa sauti ya juu kama alivyoanza mwanzo. Tulikuwa katika wakati mgumu mno maishani. Maumivu na mateso yalishakuwa sehemu kubwa ya maisha yetu na kamwe hatukuona kama kuna siku tutakuja kupata faraja na kuyafurahia maisha kama wengine.


"Dada, mimi naamini haya ni majaribu na mapito ya muda tu. Kwa sasa Tunapita kwenye tabu na mateso lakini yote ni kwa sababu Mungu ana mpango maalum na sisi," alisema Inana huku akiniangalia machoni kwa uso uliomaanisha kile alichokuwa akikisema.
Kauli yake ikanifanya ninyamaze. Inana alikuwa akizungumza kwa busara na hekima ya hali ya juu mno ukilinganisha na umri aliokuwa nao.


"Kwani baada ya tukio la kukubaka uliendelea kufanya kazi hotelini kwake?" Inana aliniuliza.
"Hapana, tangu siku hiyo sijarudi tena hotelini kwake na sitaki kabisa, kama ni kufa na njaa nitakufa lakini kwa sasa ninachofikiria ni kumwaga damu yake."
"Haaa! Wewe dada Tunu wewe!" Inana alihamaki kwani sikuwahi kumtamkia kuwa nilikuwa na mpango wa kumuua Elhakimu.

"Mbona unashtuka sana Inana?"
"Si ulivyosema kuwa unatamani kumwaga damu ya Elhakimu."
"Ndiyo, lazima nimuue huyu mwanaharamu."
"Siyo vizuri dada," Inana alianza kunisihi nisiendelee na mpango wa kuua.

Pamoja na jitihada zote za Inana, hakuweza kufanikisha kuondoa mpango uliokuwa umeota mizizi moyoni mwangu kwa wakati huo. Moyo wangu ungefurahi endapo nigeona damu ya Elhakimu ikimwagika kupitia mikononi mwangu.
Inana alikaa nyumbani kwangu hadi jioni ambapo aliondoka na kuniacha nikiwa nimejilaza. Akasema angerudi baada ya siku mbili ili kuja kunijulia hali japo na yeye alikuwa hajapona sana.
****

Majuma machache baadaye, hali yangu ilikuwa imeimarika kwa kiwango cha kuridhisha. Moyoni nilikuwa bado na maumivu makali mno dhidi ya kitendo cha kinyama nilichofanyiwa na Elhakimu.
"Lazima nitimize nilichodhamiria, lazima kesho nimwage damu ya Elhakimu," nilikuwa nikiwaza usiku huo wakati nikiwa kitandani nikiusaka usingizi kwa nguvu. Mpango wa kuondoa roho ya Elhakimu sasa ulikuwa unaelekea kutimia.


Nililala hadi asubuhi ambapo nilijiandaa kwa kuoga. Nikavaa nguo nzuri. Nilipita sokoni ambapo nilinunua kisu kikali, kirefu na chenye ncha kali sana huku kikimeremeta. Nikakiweka kwenye mfuko maalum na kukibeba kwa uangalifu wa hali ya juu.


Nikatembea hadi mahali walipokuwa wakipaki bodaboda. Nikakodisha mojawapo na kumwambia mwendeshaji anipeleke Mikocheni, mahali alipokuwa akiishi Elhakimu. Moyoni nilikuwa nikiwaza mambo ambayo hakika yalikuwa yakimchukiza Mungu kwa kiwango cha juu mno.

Njiani nilikuwa nikimhimiza mara kwa mara dereva bodaboda aongeze mwendo kwani nilikuwa na haraka isiyokuwa na kifani. Mahali palipokuwa na msongamano mwingi na foleni ndefu ya magari na pikipiki, nilichukia mno.


Tulipofika, nikamlipa bodaboda ujira wake. Akaondoka nami nikatembea hadi nyumbani kwa Elhakimu. Kwa kuwa haikuwa mara yangu ya kwanza kufika, mlinzi wake hakunitilia shaka. Aliponiruhusu nikaenda moja kwa moja hadi sebuleni na kumkuta Elhakimu akiwa amekaa kwenye kochi huku akisinzia.


Mbele yake kulikuwa na meza ndogo ambayo kwa juu kulikuwa na bastola ambayo aliwahi kunionesha ofisini kwake. Nikiwa na hasira kali huku mikono na midomo ikinitetemeka, niliichukua ile bastola na kumwangalizia Elhakimu. Nikaanza kuhesabu moja, mbili hadi tatu.

ITAENDELEA TENA
 
je tunu alifanikiwa kumuua mwarabu??? usikose ahahahaaaaa mzizi unatutia presha
 
Back
Top Bottom