Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliuwa kwa kukusudia-33-

ILIPOISHIA JANA
Mbele yake kulikuwa na meza ndogo ambayo kwa juu kulikuwa na bastola ambayo aliwahi kunionesha ofisini kwake. Nikiwa na hasira iliyopita kiwango huku mikono na midomo ikinitetemeka, niliichukua ile bastola na kuielekeza kwa Elhakimu. Lengo lilikuwa ni kumuua hivyo nikaanza kuhesabu; mojaaa...mbilii...tatu.... SASA ENDELEA...

ila kusita nikammiminia kwa hasira risasi kadhaa mwilini mwake. Risasi ya kwanza nilihakikisha inapenya na kuharibu sehemu zake za siri kama adhabu ya kuzitumia sehemu hizo vibaya kutunyanyasa kijinsia mimi na mdogo wangu Inana. Risasi ya pili nilihakikisha inatua katika paji la uso wake nikilenga kuuadabisha ubongo wake kwa kuthubutu kuwaza kutubaka. Baada ya kutekeleza unyama huo, ghafla hasira zangu ziliyeyuka.

Nikaanza kuingiwa na hofu kuu kutokana na mauaji niliyoyafanya ambayo sikuwahi kuyafikiria. Kuna wakati nikiwa nimeishika ile bastola baada ya kumpiga risasi mbili, nilihisi nimefanya maamuzi sahihi hasa baada ya kukumbuka unyama alionifanyia lakini baada ya muda tena nikajiwa na mawazo kwamba nimechukua uamuzi mbaya ambao utaniharibia kabisa maisha yangu. "Potelea mbali," nilijikuta nikitamka maneno hayo na kuitupa ile bastola chini.

Bila kuangalia chini, nilitoka kwa kukimbia kuelekea nje ya nyumba ya Elhakimu ambaye kwa wakati huo nilikuwa na uhakika kuwa tayari ni mmoja kati ya wafu waliopokelewa kuzimu siku hiyo. Kabla sijafika mlangoni, nilijikuta nikiwekwa chini ya ulinzi na askari polisi wakiongozwa na yule mlinzi wa Elhakimu ambaye nilikuwa na uhakika alisikia milio ya risasi wakati namuua bosi wake hivyo kuamua kuniitia polisi.


Kutokana na idadi ya polisi waliofika, sikuwa na ujanja, nilikuwa mpole nikijua fika kuwa hakuna cha kunifanya niwe huru kutokana na tukio lile la mauaji. Siku hiyo kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilipelekwa kituo cha polisi kama mtuhumiwa, mikononi mwangu nikiwa na pingu huku askari wakiwa pembeni na nyuma yangu, wawili wakiwa wameshikilia bastola.


Baada ya kufika kituoni nilichukuliwa maelezo kuhusiana na tukio hilo ambapo nilikataa katakata kuwa sikuua jambo ambalo liliwachukiza polisi wale waliokuwa na uhakika kuwa nilihusika kwa asilimia mia moja na mauaji ya Elhakimu. Bila kupoteza muda waliniingiza ndani ya selo nikiwa navuja jasho huku nikionekana kama niliyechanganyikiwa.


Nililala mpaka siku iliyofuata ambapo mdogo wangu Inana alikuja kuniona na kuniletea chakula. Sikuwahi kumuona Inana akiwa katika hali hiyo kabla kwani uso wake ulikuwa mwekundu ajabu. Macho yake yalikuwa na rangi ya manjano kuonyonesha kwamba alilia kwa muda mrefu kabla ya machozi kukauka.


"Dada, hata siamini! Siyo wewe wamekusingizia tu. Wewe siyo muuaji dada, niamini haya nisemayo," aliniambia mdogo wangu Inana huku akiangua kilio kikubwa palepale kituoni. Bila kujali kwa pamoja tukaanza kulia wote huku nafsi yangu ikinisuta kwa maneno ya mdogo wangu ambaye kwa wakati huo hakuamini kabisa kama ningeweza kufanya unyama ule.


Kilio chetu kilibadilika na kuanza kuwakera mahabusu wenzangu, ikabidi polisi wamtake mdogo wangu aondoke mara moja kituoni hapo jambo ambalo alilifanya japo kwa uzito. Siku moja kabla ya kesi yangu kutajwa, kaka mmoja aliyejitambulisha kama wakili wangu alikuja kunitembelea gerezani na kunitaka nimsimulie kila kitu kilichotokea na uhusika wangu katika mauaji ya Elhakimu.


Kwa kuwa nafsi yangu ilikuwa imeanza kujutia yote niliyoyafanya, nikamuelezea mwanzo hadi mwisho bila kuficha jambo lolote ili yeye ajue kama ni kunisaidia, ananisaidiaje. "Pole sana kwa yaliyokukuta, lakini naomba nikuambie kwamba, usije ukathubutu kukubali kuwa umeua na kusimulia ukweli wote huo mbele ya

hakimu," aliniambia wakili huyo kwa msisitizo na kuahidi kuwa atatumia taaluma yake ya sheria kuhakikisha kuwa siingii hatiani.

"Sawa kaka," nilimjibu wakili huyo, tukaagana na kurudishwa selo. Nikiwa mle selo watuhumiwa wenzangu walikuwa na shauku ya kujua nilikuwa nimefanya kosa gani hadi kufikishwa pale kituoni huku nikiwa binti mdogo. Mmoja wao ambaye alionekana alikuwa na cheo mle selo, aliniita na kuniuliza nilifanya kosa gani lililonifanya niwe pale. Je, alijibu nini?

Usikose kufuatilia simulizi hii kesho jioni .....


 
dah ,inatia huzuni sana.Ila kwamimi nimejifunza jambo kupitia story hii.PONGEZI MWENDESHA STORY
 
Niliuwa kwa kukusudia---34-

ILIPOISHIA KWENYE IJUMAA:

Nikiwa mle selo watuhumiwa wenzangu walikuwa na shauku ya kujua nilikuwa nimefanya kosa gani hadi kufikishwa pale kituoni huku nikiwa binti mdogo.
Mmoja wao ambaye alionekana kuwa na cheo, aliniita na kuniuliza nilifanya kosa gani lililonifanya niwe pale? SASA ENDELEA...


We binti kwani umefanya kosa gani?" aliniuliza mama huyo huku wafungwa wengine wakinisogelea kwa shauku ya kutaka kujua kilichonikuta mpaka nikawa pale.
"Nimeua!" nilijikuta nikisema maneno hayo kwa kukaza meno, lakini kilichonishangaza ni kitendo cha kila mmoja kuanza kucheka kwa dharau wakiamini kuwa kwa muonekano wangu nisingeweza kuua hata panya sembuse kuua mtu!

Kwa vicheko vile, moyo wangu ulizidi kupata simanzi. Nilitambua fika kuwa kweli sikupaswa kuwa mahali pale, tena kama muuaji kwa kuwa hata muonekano wa sura yangu ulikuwa ni wa upole mno.
Niliinamisha uso wangu kwa muda kidogo kisha nikainua macho yangu na kuanza kuwasimulia bila kuficha mkasa mzima uliosababisha mimi kuua.

Nilipomaliza kusimulia kila mmoja alinionea huruma na kuniunga mkono kwa kitendo nilichokifanya japo wengine walipinga na kusema kuwa nilifanya jambo hilo kwa kukurupuka na kuwa ningelijutia baadaye.
"Ndiyo hivyo tena umeshakuwa mfungwa, sasa ndo umepata nini? Binti mdogo umejiharibia maisha yako yote kwa hasira za mkizi.

"
Tulaleni jamani kila siku stori mpya leo huyu kesho atakuja mwingine utasikia kamuua mume wake kisa mali," alisema mfungwa mmoja kati ya wafungwa wale walionizunguka kisha kila mmoja akatawanyika na kwenda kulala kwenye kigunia chake alichokitandika sakafuni.

Yule mfungwa aliyeonekana kuwa na cheo zaidi pale ndani alinitupia kipande cha gunia na kunionesha kisehemu cha kulala pale sakafuni. Huwezi amini kwa jumla tulikuwa kama watu kumi na sita hivi sote tukiwa tumelala chini tena kwa kubanana sana kiasi kwamba ukilala upande mmoja basi ni huohuo mpaka asubuhi.

Usiku mzima nilikesha nikifikiria juu ya hatima yangu kwa kuwa hata kama nitakwepa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, basi sitaepuka kifungo cha maisha.
***
Kwa kuwa uchunguzi wa kesi yangu ulimalizika mapema, siku chache tu zilizofuatia mimi na mahabusu wachache niliowakuta gerezani, tulipandishwa kwenye gari la magereza na kupelekwa mahakamani kusomewa mashitaka yetu na wengine kusikiliza hukumu zao.

Njiani niliwaza mambo mengi sana hadi kichwa kikaniuma. Ukweli ni kwamba japokuwa nilimuua Elhakim, lakini bado kila nilipofumba macho nikijitahidi kufuta kumbukumbu ya ile siku aliyonibaka, nilishindwa kabisa.
Kuna wakati nilihisi huenda adhabu ya kifo niliyompa Elhakimu ilikuwa haitoshi hata kidogo. Nikajiapiza kuwa hata kama nitafungwa lakini nilitaka kesi yangu iwe somo kwa wanaume wote wenye tabia kama za Elhakim, nikaona ni vyema nisikanushe mashitaka yangu kama nilivyoambiwa na wakili wangu.
Dhamira yangu ilinituma kukubali kuwa niliua.

Gari letu lilipofika mahakamani tulishushwa harakaharaka na kupelekwa moja kwa moja kwenye chumba maalum huku mmoja baada ya mwingine alikuwa akiitwa na kesi yake kusikilizwa.
Tukiwa katika chumba hicho tuliweza kusikia sauti za wenzetu wachache wakifurahi na ndugu zao kwa kuachiwa huru baada ya hukumu huku mara kadhaa tukisikia vilio ambavyo mara moja tulitambua kuwa kuna mwenzetu alihukumiwa jambo ambalo lilinitia woga.

"
Tunu Ramadhani!" liliitwa jina langu na askari mmoja wa kike ambaye alikuja kufungua chumba tulichokuwemo na kunifungua pingu kisha kunipeleka kwenye chumba cha mahakama kila kona nikiwa nimezungukwa na askari.

Nikiwa kizimbani niliweza kumuona mdogo wangu Inana ambaye machozi yalikuwa yakimtiririka kama mvua. Kwa upande mwingine niliwaona ndugu wa Elhakim walioonesha chuki ya wazi juu yangu jambo ambalo lilizidi kunitia hofu. Kwa kifupi, chumba cha mahakama kilikuwa kimejaa watu wengi sana ambao wote walivutika kujua nini hatima yangu.
Nikiwa nimezama katika ulimwengu wa majuto, sikuwa na nafasi ya kutazama kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Nilijikuta nikishtuliwa na wakili wangu aliyenitaka nisimame ili jaji aingie mahakamani jambo ambalo nililifanya.
Bila kupoteza muda, jaji alichukua faili langu na kulisoma kwa muda kisha akaniuliza huku akinitazama kupitia sehemu ya juu ya miwani yake aliyoishusha mpaka puani.
"Tunu, mnamo tarehe 2, Machi ulimuua kwa bastola bwana Elhakim, unakubali au unakataa?"
Niliinua macho yangu na kumtazama wakili wangu ambaye kwa wakati huo alikuwa akiniminyia jicho kunikumbusha nikatae kwa kusema sikuua ili kesi iaharishwe kama tulivyopanga jana yake.

Tofauti na tulivyokubaliana, nilijikuta nikikubali huku machozi yakinitoka kwa hofu na aibu kiasi kwamba nilishindwa hata kumtazama mdogo wangu.
"Nakubali," nilipomaliza kusema hivyo ghafla nilishuhudia mdogo wangu akidondoka kama gunia palepale alipokaa, lakini kabla jaji hajachukua hatua yoyote msichana mmoja alisimama.
"Hapana jaji huyo hakuhusika na mauaji yoyote, mimi ndiye niliyemuua Elhakim," alisema msichana huyo kwa kujiamini huku akisogelea kizimba.


Je, nini kitaendelea? Fuatilia leo jioni.....

 
Back
Top Bottom