Niliuwa kwa kukusudia--35-
ILIPOISHIA:
Nikiwa gerezani, nilijiuliza yule msichana aliyeamua kujitwika kesi yangu alitokea wapi na lengo lake lilikuwa ni nini? Sikupata majibu.
ENDELEA...
SIKU hiyo ilikuwa ndefu sana kwangu kwa sababu kila nilipojitahidi kuyafumba macho ili kuutafuta usingizi nilishindwa.
Bado sehemu ndogo ya moyo wangu haikufurahia hata kidogo na wazo la mimi kutokuwa mtu pekee niliyemuua Elhakim. Nadhani hiyo ilitokana na kisasi kikubwa nilichokuwa nacho kwa muda mrefu dhidi ya Elhakim aliyetubaka mimi na mdogo wangu.
Siku iliyofuata kabla ya kupandishwa kizimbani, wakili wangu alinifuata kwa ukali akijaribu
kunionya hasa baada kutofuata ushauri wake alionipa kuwa nisikubali mbele ya Jaji Athumani kuwa nilimuua Elhakim.
"Una bahati sana! Kama asingekuwa yule msichana usingeniona tena nikikusaidia katika kesi yako," alisema wakili wangu kwa ukali, akaendelea: Ripoti ya vidhibiti na uchunguzi wa maiti ya Elhakim (postmortem) imetoka leo asubuhi.
Nilipewa ruhusa maalumu ya kuvipitia, unajua nini nilichokigundua?" Wakili wangu aliniuliza swali ambalo nilijua halikuwa lazima kulijibu japo nilikuwa nikitamani kujua nini alichokiona.
"Umegundua nini?"
"Ripoti ya alama za vidole katika ile bastola zinaendana kwa asilimia mia moja na vyako. Pia bastola ile ilionekana kutumika dakika chache mara baada ya wewe kukamatwa hivyo kwa mambo hayo mawili wewe ndiye mtuhumiwa namba moja. Siamini hata kidogo kama yule dada aliyejiita muuaji, aliua."
Kabla sijazungumza chochote, karani mmoja wa mahakama alikuja mpaka nje ya chumba nilichowekwa akiwa na askari wa mahakama na kututaarifu kuwa muda wa kesi yangu ulikuwa umewadia.
Wakili wangu aliondoka mara moja na mimi nilichukuliwa na askari yule na kupelekwa moja kwa moja hadi kwenye chumba cha mahakama nikisubiri hatma yangu.
Tofauti na siku nyingine, siku hiyo niliweza kumuona mke wa Elhakim ambaye ni mtu pekee aliyeongezeka katika orodha ya ndugu wa Elhakim waliofika hapo.
Kwa upande mwingine nilimuona mdogo wangu akiwa ameketi viti vya mbali akinitazama kwa huruma dada yake nikiwa kizimbani.
Kama kawaida, kesi ikaanza kusikilizwa.
Maswali yakaulizwa; upande huu ukiulenga upande ule na upande ule ukiulenga upande huu, hatimaye ilifika zamu ya Jamila, yule msichana aliyedai kumuua Elhakim kupanda kizimbani na kueleza mbele ya mahakama jinsi gani alikuwa akihusika na kifo cha Elhakim.
Kwa kujiamini, Jamila alisimama kwenye kizimba kile na kuanza kuelezea:
"Kama nilivyosema jana, jina langu ni Jamila Msuya. Mimi ndiye muuaji wa Elhakim. Mnamo mwezi Julai, mwaka juzi, nikiwa mkoani Iringa, dada mmoja alikuja nyumbani kwetu akisema kuwa anamtafutia rafiki yake aishiye Dar mfanyakazi wa ndani.
"Kwa kuwa sikuwa na shughuli yoyote ya kuniingizia kipato, niliamua kumwambia dada huyo kuwa ningependa kwenda Dar kuifanya kazi hiyo.
"Baada ya kuwaaga wazazi wangu na taratibu zote kukamilika, nilisafiri na yule dada hadi hapa Dar. Sikujua hata kidogo kuwa nyumba ambayo ningefikia ingekuwa ni ya Elhakim, laiti kama ningelijua hilo hata nisingethubutu kuikubali kazi hiyo.
"Nikiwa nyumbani kwa Elhakim, siku za kwanza nilifanya kazi kwa furaha na niliishi vizuri sana na mkewe pamoja na ndugu zake ambao wengi wao wapo hapa mahakamani leo hii.
"Nilianza kujua tabia mbaya za Elhakim, siku chache baada ya mkewe niliyezoea kumuita dada kusafiri. Kwa mara ya kwanza nilishangaa kumuona Elhakim akiwa na mazoea ya kuingia ghafla chumbani kwangu.
"Mara nyingine alikuja akiwa na nguo za kulalia na kama hiyo haitoshi alikuwa akitaka kulala na mimi kwa kunilazimisha, jambo ambalo nilikataa na kuamua kutoka chumbani na kuwa nalala sebuleni ambako aliogopa kunifuata kwa kuwa watoto wake wangemsikia kama tu ningepiga kelele.
"Nafahamu kuwa marehemu hasemwi kwa ubaya lakini siyo kwa Elhakim ambaye kila siku alikuwa akibuni njia ya kuninasa katika mtego wake. Hakujali hata pale nilipotishia kumwambia mkewe.
"Nikiwa katika maisha hayo ya kupambana, siku moja baada ya mlo wa mchana nilihisi kupoteza nguvu zangu jambo nililokuja kulifahamu baadaye kuwa aliniwekea dawa za kulevya katika maji ya kunywa kwani kabla sijapoteza fahamu nilimuona Elhakim akinibeba na kunipeleka chumbani kwake.
"Nikiwa sina nguvu hata ya kuniwezesha kunyanyua midomo yangu kupiga makelele kuomba msaada, Elhakim alinivua nguo zangu zote na kuniacha kama nilivyozaliwa kisha akaniingilia kimwili na mbaya zaidi aliniingilia hadi kinyume na maumbile.
"Kwa kuwa nilikuwa na uchungu sana, nilipoteza fahamu na kuzinduka siku iliyofuata ambapo mwili wote ulikuwa ukiniuma. Nilipomfuata na kumueleza kwa nini alinifanyia kitendo kile, alinidhihaki na kunitaka niondoke nyumbani kwake.
"Kwa kweli, kwa siku hiyo sikuweza kufanya jambo lolote zaidi ya kuondoka nyumbani kwake, nikiapa kuwa lazima siku moja nitamshikisha adabu kwa kitendo alichonifanyia," alisema Jamila huku macho yaliyojaa ujasiri mkubwa yakianza kulengwalengwa machozi.
FAINALI YA MWISHO USIKOSE KUFUATILIA USIKU MWINGI....