Niliua kwa Kukusudia--30-
ILIPOISHIA:
Mateso, maumivu, simanzi, huzuni na masononeko yalikuwa ni sehemu ya maisha yangu kwa wakati huo. Hakika sikujua ni kwa nini Elhakimu niliyemsheshimu na kumchukulia kama mzazi wangu alifikia hatua ya kunifanyia unyama ule bila chembe ya huruma.
"Lazima niue," nilijikuta nikitamka maneno hayo kwa sauti ya juu.
SASA ENDELEA…
Nilitamka maneno hayo nikiwa katika lindi la mawazo. Sikuona kabisa thamani ya kuwepo kwangu chini ya jua. Moyoni nikajiona ni kiumbe mwenye bahati mbaya kuliko viumbe vyote vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu.
Taratibu nikajilaza kitandani na kuendelea kuwaza juu ya maisha yangu, hadi wakati huo sikujua nini hatima yangu hapa duniani. Nikaendelea kulia kwa maumivu hadi nilipopitiwa na usingizi. Jioni nilienda bafuni na baada ya kuoga nikabadili nguo na kuandaa chakula.
Kabla ya kulala nilikunywa dawa nilizoandikiwa na daktari za kuondoa maumivu na kuzuia maambukizi zaidi. Baada ya kunywa dawa, nilimshukuru Mungu kwa kunilinda na kunipitisha salama kutwa nzima ya siku hiyo. Ingawa niliamini Mungu aliruhusu majanga yote hayo yaendelee kunizonga maishani mwangu, bado sikukata tamaa ya kumuomba kila siku na kila wakati kama marehemu mama yangu alivyokuwa akituagiza kila mara kuwa kumtegemea Mungu ni chanzo cha maarifa na ndiye nguzo muhimu maishani.
Nilichutama na kupiga magoti ambapo nilianza kuomba dua kwa Mungu ya kumtaka anilinde na malimwengu wakati wa usingizi. Nilipomaliza kuomba, nilivua nguo zote na kubakiza ya ndani tu. Nikapanda kitandani na kuchukua shuka langu zito. Kabla sijajifunika, nilipata wazo la kujikagua sehemu zangu za siri, bado kulikuwa na bandeji ambazo daktari alikuwa amenifunga pamoja na dawa. Machozi yakanitoka mfululizo, machungu niliyokuwa nayo yakaongezeka maradufu.
Haraka nikakurupuka kitandani na kukaa kitako huku nikiwa nimeshika shuka langu mkononi. Licha ya kupulizwa na kijiupepo cha feni, jasho jembamba la hasira lilikuwa nikinitoka! Hakika nilikuwa na hasira isiyoweza kusimulika kwa urahisi.
Niliendelea kukaa kitandani nikiwaza na kuwazua mambo kadha wa kadha. Mawazoni nilimuona Elhakimu amesimama mbele yangu. Hasira zikazidi kunipanda na kutaka kufanya jambo ambalo hakika sikuwahi kuliwaza maishani mwangu. Kuua!
Lakini yalikuwa ni mawazo tu ambayo hayakuwa na ukweli wowote. Moyoni nilitamani iwe kweli ili niweze kulipiza kisasi cha maumivu niliyokuwa nayo dhidi ya Elhakimu.
Nikaamua kujilaza na kujifunika kwa shuka gubigubi hadi kichwani. Sikupata usingizi kwa haraka kwani mawazo mengi yalikuwa yakikinzana ubongoni mwangu. Sikujua nililala saa ngapi kwa usiku huo lakini nilishtuka na kudamka tayari ikiwa ni saa mbili kasoro robo asubuhi.
Nikakumbuka kuwa nilitakiwa kufika kituo cha polisi kwa ajili ya mwendelezo wa kesi yangu dhidi ya Elhakimu. Moyoni nikapuuzia baada ya kukumbuka yale maneno ya kukatisha tamaa ambayo niliambiwa na yule mkuu wa kituo.
Lakini nikaamua kwenda kujua nini kitajiri ingawa moyoni nilikwishaanza kukata tamaa na kupunguza matumaini ya kumtia nguvuni Elhakimu. Maisha yakuwa yamenielemea sana.
Nikaamka kivivu na kwenda moja kwa moja kuchota maji na kuingia bafuni kwa ajili ya usafi. Nikabadili nguo na kuandaa chai pamoja na kitafunwa. Nilipomaliza kunywa chai, nikameza dawa na kuanza safari ya kuelekea kituoni.
Njiani nilitembea kwa mwendo wa taratibu licha ya maumivu kupungua lakini sikuweza kujiachia. Wakati mwingine nililazimika kupumzika ili kupunguza maumivu.
Maumivu yalipopungua nikaendelea na safari lakini kabla ya kufika kituoni, nilishtuka nikiguswa begani na nilipogeuka alikuwa ni mdogo wangu Inana. Furaha ikanijia kwa kasi na kusalimiana na Inana kwa kukumbatiana. Nikamuomba tukae mahali ili nimsimulie yaliyojiri kati yangu na Elhakimu.
"Bosi aliniambia kuwa mlikutana lakini ukiwa na hali isiyokuwa ya kawaida, kulikoni Tunu?" Inana alifungua uwanja wa mazungumzo kabla sijaanza kumjuza kisa changu.
"Ni kweli Inana, sikuwa sawa kwani nina matatizo makubwa mno mdogo wangu."
"Matatizo gani tena dada yangu jamani?" Inana aliuliza huku akinikazia macho kwa shauku kubwa ya kutaka kujua kilichonisibu.
"Elhakimu alinibaka na kunitupa mtaroni."
"Unasemaje wewe?" Inana aliuliza huku machozi yakitengeneza mifereji machoni mwake.
Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia leo jioni usikonde basi...