Tumeandika mara nyingi kuhusu sababu za wznz kutaka muungano uvunjike. Tumekuwa tukipewa sababu nyepesi nyepesi na wengine tumeeleza kuwa kujitenga ni haki yao na wafanye hivyo haraka kuelekea nchi ya kanaani yenye mito ya asali na maziwa.
Nimewahi kuandika kuwa wenzetu wa mzalendo forum sababu yao moja kubwa ni kutaka kufutiwa visa za Oman kwasababu wao wanaamini ni sehemu ya uarabuni, nikazogolewa!
Nimewahi kusema hakuna kisiwa chenye wakazi wa asili bali wote ni wahamiaji, nikajibiwa znz ilikuwepo kabla ya pori la Tanganyika, kwa maana ni nchi pekee iliyowahi kuwepo kabla ya zingine.
Nilisema wznz wapo wa kipilipili na kimanga, nikijabiwa hapana wao ni dugu moja.
Soma hii kitu kutoka raia mwema.
TEMBELEA mji wa Durban nchini Afrika Kusini, utakuta wakazi wanaojulikana kama "Wazanzibari"; kwa maana ile ile ya Uzanzibari wa Visiwa vya Unguja na Pemba, ingawa hawaishi Zanzibar wala si raia wa Tanzania.
Inawezekana usiamini hili na kujiuliza maswali mengi: "Je, Wazanzibari hawa ni wazawa wa masetla wa Kiislam karne zilizopita nchini Afrika Kusini kama walivyo Makaburu nchini humo? Kwanza mji wa Durban wenyewe si mji wa kale kiasi hicho; kwani ulianza mwaka 1834, vipi hii iwe kweli?
Kwa hiyo, Wazanzibari hawa ni kina nani? Walitoka wapi? Walifikaje Durban? Serikali ya Mapinduzi Zanzibar [SMZ] inawafahamu? Ni kina nani? Ni watoro/wakimbizi kutoka Zanzibar au jina hilo ni ngano tu za historia iliyosahaulika? Maswali haya yanataka utafiti makini kuelewa Wazanzibari hawa ni kina nani, na walifikaje huko.
Jamii inayojulikana jijini Durban na Chatsworth kama "Wazanzibari" nchini Afrika Kusini, ilionekana kwa mara ya kwanza katika eneo hilo mwaka 1873. Hawa ni wa vizazi vya watumwa wa kabila la Wamakua waliokombolewa na meli za vita za Waingereza katika Pwani ya Afrika Mashariki na bahari ya Sham; kisha wakapewa makao Zanzibar.
Wakati wakiishi hapo Zanzibar sambamba na Waswahili na Waislamu wa Kiarabu, waliweza kusilimishwa. Hata hivyo, chini ya mpango maalumu uliofikiwa kati ya Serikali ya Uingereza nchini Zanzibar na Gavana wa Jimbo la Natal nchini Afrika Kusini, ilionekana vyema watumwa hao huru wapelekwe Natal badala ya kubakia katika himaya ya Sultan wa Zanzibar kwa kuhofia kukamatwa na wafanyabiashara ya utumwa; licha ya kuwapa mkataba kati ya Uingereza na Sultan huyo mwaka 1873 kupiga marufuku biashara ya utumwa katika himaya yake.
Hiyo ni sababu moja; lakini kubwa zaidi ilikuwa ni upungufu wa nguvu kazi huko Natal kiasi cha kuhitaji wafanyakazi wa mashambani kutoka sehemu zingine. Kwa hiyo, watumwa hao huru walipelekwa huko kupunguza utegemezi wa nguvu kazi mashambani kutoka India ulioanza mwaka 1860.
Walipofika Natal waligundua kuwapo kwa Waislamu wenzao miongoni mwa Wahindi manamba waliofika kabla yao. Mikataba ya kazi ya Wazanzibari na Wahindi ilitofautiana kidogo. Wakati Wahindi walitakiwa kuchukua kitambulisho [kipande] kila waendako, Wazanzibari walikuwa huru kwenda wapendako.
Mikataba ya kazi ilikuwa ya miaka mitano mitano kwa Wahindi; kwa Wazanzibari ilikuwa mitatu. Hata hivyo, makundi yote mawili yalinyanyaswa vikali na watawala weupe.
Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba makundi haya mawili yaliyofanyishwa kazi kwa pamoja chini ya msimamizi mmoja, yalijenga udugu na kushabihiana katika kunyanyaswa kwao. Mikataba yao ilipomalizika, Wazanzibari hao walifanya makao ya kudumu Durban na kuishi kama Waswahili.
Katika jamii za Kiswahili, kijiji ndicho kitovu cha jamii na ufuasi wa dini. Hivyo, utamaduni wa Kiswahili na dini ya Uislamu uliwajengea mshikamano wa kijamii kuwawezesha kujenga jamii yao pekee eneo la Kingsrest mjini Durban. Hapa walijishughulisha na kilimo cha bustani na ajira za majumbani kwa matajiri.
Kutokana na asili yao, yaani Zanzibar, iliyokuwa chini ya himaya ya Sultani, "Wazanzibari" hawa waliwekwa katika daraja la kijamii la "Kiasia" [Asiatic], na zaidi ya yote, imani yao ya Kiislamu iliwatofautisha na Wabantu wengine. Juhudi zilikuwa zikifanywa na Serikali ya Durban kutunga sheria watambuliwe kama Wabantu.
Jamii hii ya "Wazanzibari" iliendelea kujitambua kwa dhehebu la Ki-Sunni likizingatia "Shariah", kama njia ya kujichanganya na kujumuika na jamii zingine zilizotupwa nje ya utamaduni asilia.
"Wazanzibari" hawa, hata hivyo, waliendelea kupinga kuwekwa daraja moja na Wabantu kwa madai kwamba nchi yao ya asili - Zanzibar, kilikuwa kisiwa nje ya mpaka wa maji wa bara la Afrika. Na katika mkutano wa 1958 ulioandaliwa na Mfuko wa Juma Masjid Trust, hatimaye ilikubaliwa jamii hiyo ya Wazanzibari ipewe daraja la "Wenye rangi mbali mbali.
Baada ya mazungumzo marefu na Serikali kufuatia Sheria ya Uandikishaji watu Na. 30 ya 1950, mwaka 1961, ilikubaliwa daraja la Wazanzibari hao chini ya "rangi mbalimbali", lifafanuliwe kumaanisha "Waasia wengineo" [Other Asiatics].
Ni muhimu kufahamu kuwa "Wazanzibari" hawa walijitambua zaidi na asili ya Uarabu; licha ya rangi yao nyeusi. Hali hii iliwaepushia adha ya ukandamizaji na unyanyasaji waliofanyiwa Wabantu chini ya Serikali ya ubaguzi wa Makaburu.
Tishio lingine lililowakabili "Wazanzibari" juu ya kuwapo kwao Durban, ni lile kufuatia kutangazwa kwa Sheria ya Maeneo ya Vikundi [Groups Areas Act] ya mwaka 1957 ambapo eneo la Kingsrest walitengewa watu weupe. Hapa tena Mfuko wa Juma Masjid Trust uliingilia kati kuwatetea "Wazanzibari" na juhudi za kutaka wahamishiwe eneo la Zeekoevalleei zilishindwa.
Uhusiano wa mwanzo uliojengeka kati yao na Wahindi ulizidi kuimarika kwa vile waliabudu pamoja, walisherehekea Maulid pamoja, na walijumuika pamoja katika sherehe na vilio, na walitumia makaburi ya pamoja eneo la Kingsrest. Wakati mwingine "Wazanzibari" waliswali kwenye msikiti mkuu mtaa wa Grey, uliojengwa na Waislamu wa Kihindi waliofika hapo miaka ya 1860; na kufikia miaka ya 1880, walikuwa wafanyabiashara mahiri, ndipo wakaanzisha Mfuko wa Juma Masjid Trust.
Mwishoni mwa muongo, Waislamu wenzao wa Kihindi waliwapiga jeki "Wazanzibari" hao kwa kuwapatia mwalimu wa dini, Mustafa Osman, kutoka Visiwa vya Komoro ili akae nao na kuwasaidia kwa mambo ya kiroho.
Mwaka 1899 wafanyabiashara wa jamii ya Kihindi walianzisha mfuko mwingine wa Mohammedan Trust uliowawezesha kuwanunulia "Wazanzibari" hao ardhi eneo la Kingsrest na kuwahakikishia makazi ya kudumu. Mfuko huo uliweza pia kuwalipia kodi zote za serikali, kutunza msikiti, kuendesha madrassa, hivyo kuwahakikishia "Wazanzibari" hali ya usalama wa maisha.
Itakumbukwa pia kwamba jamii ya Kihindi ya Durban ndiyo iliyompokea mwanaharakati mashuhuri wa ukombozi wa India, hayati Mahatma Gandhi alipokimbilia na kukaa huko baada ya kuona India hakukaliki kutokana na harakati zake. Ni kutoka Afrika Kusini Mahatma Gandhi alirejea India akiwa na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya na akaweza kuleta uhuru wa India.
Hata hivyo, mambo yaliwageuka mwaka 1938 ilipotungwa sheria iliyowatambua kama Waafrika na hivyo kutakiwa kulipa kodi ya kichwa kama Wabantu wengine na kubeba vitambulisho kila walikokwenda. Hata hivyo, kwa msaada wa Mfuko huo, "Wazanzibari" hao waliweza kupatiwa ardhi katika eneo la Wahindi la Chatsworth mwaka 1961, kwa sababu tu makundi haya yalishabihiana kidini.
Wazanzibari hawa walianza kuhamia Chastworth mwaka 1962 ambako wanaishi mpaka sasa. Utawatambua kwa tabia zao za ki-Makua, na wakati huo huo alama yao ya Uzanzibari kwa mivao kama vile kanzu, kikoyi, kofia, kimau, na kanga na kwamba wanazungumza Kiswahili fasaha cha kimwambao.
"Wazanzibari" hawa wanaheshimu swala tano za kila siku, na wanaitukuza na kuisherehekea siku ya Maulid katika nchi ambayo zaidi ya asilimia 90 ya raia wake ni Wakristo wenye mawazo kwamba Uislamu ni dini ya Kiarabu.
"Wazanzibari" wa Durban ni Wazanzibari wa asili ya Visiwa vya Zanzibari, kwa sababu hapo ndipo walipoanzia makazi kama watu huru. Na ndivyo ilivyokuwa kwa Wa-Creole wa Freetown huko Siera Leone waliopewa makao huko baada ya kukombolewa kutoka utumwani kuanzia mwaka 1808.
Idadi ya "Wazanzibari" wa Durban si kubwa sana katika nchi yenye Waislamu wanaounda asilimia moja tu ya wananchi wa Afrika Kusini na idadi ya waumini isiyoongezeka. Wameishi maisha ya kubaguliwa na utawala wa Makaburu [weupe], wakiumia bila uchungu kwa miaka mingi ya sera za kibaguzi wa rangi na ubaguzi wa kidini, kama walivyofanyia Wamarekani wenye asili ya Kiafrika kwa karne nyingi nchini Marekani.
Ubaguzi huu haukufichika miongoni mwa Makaburu. Mapema mwaka 1971, Mkuu wa Kanisa la Makaburu (The Dutch Reformed Church – DRC) Dakta Benjamin Vorster, nduguye aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Vorster, aliulizwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza [BBC], kama kulikuwa na uhalalisho wowote wa ki-Biblia juu ya ubaguzi huo, naye haraka haraka akajibu akisema: "Torati 32:8", inayoeleza kwamba, Mungu alipowagawia mataifa wana wa Israeli, alitaka wajitenge na wasioamini ili kutimiza mpango wake, na kwamba ubaguzi wa rangi kati ya weupe na wasio weupe ndio mfumo bora unaotakiwa na Mungu Afrika Kusini; na zaidi kwamba, Uislamu ni dini batili inayohatarisha Ukristo Afrika Kusini, Afrika na dunia nzima.
Vorster alitaja wazi wazi kuwa, "Wazanzibari" wa Durban ni hatari zaidi kuliko wahamiaji wa Kihindi [Wahindu] nchini Afrika Kusini.
Wazungu hawa [Makaburu] wanafananisha safari yao ndefu kutoka Kusini [Natal], kwa misafara, kuingia ndani ya Afrika Kusini karne ya 19, na safari ndefu [miaka 40] ya Waisraeli kutoka Misri kwenda nchi ya ahadi [Kanaani] yenye mito iliyofurika maziwa na asali.
Kitabu chao kikuu walichosoma kila siku ni Biblia, ni Agano la Kale, na mtazamo wao wa dunia umejengeka kwa misingi ya maandiko hayo. Hotuba zao mara nyingi ni kama unasikiliza manabii wa Agano la Kale. Waliamini kwamba kupinga ubaguzi wa rangi ni kupinga mpango wa Mungu, na hivyo ni kushindana na Mungu.
Msimamo mkali wa kidini wa "Wazanzibari" uliukera utawala wa kibaguzi wakaonekana kuwa watu wasiotakiwa na utawala huo katika nchi yenye idadi kubwa ya Wakristo kama hii. Mpaka sasa "Wazanzibari" wa Afrika Kusini ni watu baridi wanaoishi kwa kukumbuka asili yao daima – "Zanzibar".
Lakini mtu hapotezi asili yake kwa maana kufanya hivyo ni kupoteza utamaduni. Utamaduni ndio unaomfanya mtu aweze kuishi alivyo. Mtu asiyekuwa na utamaduni si kitu, bali ni sawa na mti usio na mizizi.
Huko Ethiopia ilibainika kuwa baadhi ya raia wa nchi hiyo walikuwa wa asili ya Kiyahudi wakijulikana kwa jina la kabila la "Wafalasha", nao hawakupenda kupoteza au kusahau asili yao; licha ya kukaa huko kwa karne nyingi. Na kwa sababu hiyo, Serikali ya Israeli ilichukua hatua za makusudi za kuwarejesha Uyahudi Wayahudi hao, chini ya mpango maalumu uliopewa jina la "Operation Moses", mwishoni mwa miaka ya 1970, na kuungana na Wayahudi wenzao.
Kwa kuwa "Wazanzibari" wa Durban wanainua macho kutazama na kuwakumbuka ndugu zao Wazanzibari wa Unguja na Pemba; na kwa kuwa damu ni nzito kuliko maji, tutarajie "Operesheni Zanzibar", mithili ya ya "Operation Moses" ya Mafalasha kurejea kwao Zanzibar?
Pengine ni vyema ikawa hivyo ili "Wazanzibari" hao wa Afrika Kusini wajumuike na ndugu zao wa Pemba na Unguja katika siasa za "ngangari na ngunguri", Visiwani humo; kwani ardhi yao bado inatosheleza kupokea wageni - "Wazanzibari" kwa "Wazanzibara".