Ni Jukumu la Kila Mmoja Kuhakikisha Watoto Wote Wanaishi Salama Katika Jamii

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
UKATILI DHIDI YA WATOTO.png


Ukatili unaotekelezwa dhidi ya watoto unaweza kuwa wa aina nyingi. Unaweza kuwa wa kimwili, kihisia au kingono. Unaweza kufanyika katika mazingira yoyote kama vile nyumbani, katika jamii, shule na mtandaoni.

Ukatili dhidi ya watoto unajumuisha aina zote za ukatili dhidi ya watu walio chini ya umri wa miaka 18. Wavulana na wasichana wako katika hatari sawa ya kufanyiwa ukatili wa kimwili na kihisia na kutelekezwa, na wasichana wako katika hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia, kwa mujibu wa WHO.

Watoto wadogo pia wamo hatarini zaidi kwakuwa hawawezi kuzungumza na kutafuta usaidizi na hivyo kusababishiwa uharibifu usioweza kurekebishwa katika ukuaji wao.

Umoja wa Mataifa pia unasema Watoto bilioni moja duniani kote hupitia aina fulani ya unyanyasaji wa kihisia, kimwili au kingono kila mwaka; na mtoto mmoja hufa kutokana na ukatili kila baada ya dakika tano. Inaelezwa pia kuwa mara nyingi ukatili huu hutekelezwa na watu ambao watoto/waathirika wanawaamini – yaani wazazi, walezi, walimu, wenzao/marafiki na majirani.

Hata hivyo, ubaya ni kwamba matendo haya mara nyingi hayaonekani kwa urahisi. Wahalifu hujitahidi sana kuficha matendo yao, wakiwaacha watoto – hasa wale ambao hawana uwezo wa kuripoti au hata kuelewa wanachopitia – katika hatari ya kutendewa maovu zaidi.

Ukatili huathiri watoto wote. Hata hivyo, watoto wanaoishi na ulemavu, wale wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri na walio katika uangalizi wa kitaasisi, pamoja na waliotenganishwa na familia zao au wanaohama (k.m vile wahamiaji, wakimbizi au wanaotafuta hifadhi) – wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi.

Haijalishi ni aina gani ya ukatili ambao mtoto anakumbana nao, uzoefu wake unaweza kusababisha athari kubwa katika maisha yake kama vile majeraha ya kimwili, magonjwa ya zinaa, wasiwasi, huzuni, mawazo ya kujiua, mimba zisizopangwa na hata kifo. Athari za kitabia za muda mrefu kwa watoto zinaweza kuwa ni pamoja na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, tabia hatarishi za kingono na uhalifu.

UKATILI DHIDI YA WATOTO DUNIANI.png

Licha ya madhara haya mabaya ya afya ya kimwili na kiakili, idadi kubwa ya watoto walioathiriwa huwa hawatafuti au kupewa msaada wa kupona. Wasichana na wavulana wengi wanaokabiliwa na ukatili huishi kwa kutengwa, upweke, na hofu na hawajui wapi pa kupata msaada, hasa pale mhalifu anapokuwa ni mtu wa karibu na ambaye wanamtegemea kwa ulinzi na ustawi wao.

Waathiriwa wanaokabiliana na athari za kisaikolojia na kimwili za unyanyasaji pia wanakabiliwa na vikwazo vya kushiriki katika maisha ya kijamii na kutumia uwezo wao kufikia malengo katika maisha. Lakini pia, ukatili unapotokea shuleni hudhoofisha uwezo wa watoto kujifunza na kuathiri matokeo na matarajio yao ya kielimu na ajira.

Katika Mkataba wa Haki za Mtoto na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), nchi zimejitolea kukomesha ukatili dhidi ya watoto, na kutoa wito wa kukomesha unyanyasaji, unyonyaji na aina zote za ukatili na mateso dhidi ya watoto ifikapo mwaka 2030.

Watoto wote wana haki ya kulindwa dhidi ya ukatili, bila kujali aina au kiasi cha ukatili. Aina zote za ukatili zinaweza kusababisha madhara kwa watoto, kupunguza hisia zao za kujithamini, kudhalilisha utu wao na kuzuia maendeleo yao.

Marufuku ya adhabu zote za viboko ni hatua muhimu kuelekea kufikiwa kwa lengo hilo na malengo mengine, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusiana na afya na ustawi, na elimu bora.

Marufuku za kisheria za ukatili dhidi ya watoto zinapaswa pia kelekezwa katika maeneo yanayoibuka kama vile matumizi mabaya ya teknolojia mpya ya habari na mawasiliano. Ni muhimu serikali ziwekeze katika katika mifumo na huduma imara za ulinzi wa watoto.

Lakini pia, kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kunahitaji mabadiliko katika mitazamo na tabia zisizofaa ambazo zimekita mizizi. Wadau wote wakiwemo viongozi wa kijamii na kidini wanapaswa kushirikiana kujenga jamii ambazo zinakataa vitendo vyote vinavyowanyang’anya watoto haki zao.

Familia lazima ziungwe mkono ili ziweze kuwatunza watoto wao ipasavyo. Hii itasaidia kuzuia utelekezwaji wa watoto na kukomesha uwekaji wa watoto katika uangalizi wa kitaasisi ambapo wanaweza kuwa katika hatari kubwa ya ukatili. Uwekezaji katika malezi chanya, mifumo ya ulinzi wa kijamii na maendeleo ya utotoni yanapaswa kupewa kipaumbele na ufadhili.
 
Back
Top Bottom