Nguvu ya Kila Mmoja Bado Inahitajika ili Kufikia Lengo la Ustawi Usiobagua Jinsia Katika Kila Nyanja

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
USAWA WA KIJINSIA 2.png

Mazungumzo yanayohusu ukosefu wa usawa wa kijinsia katika sehemu kubwa ya dunia ni ngumu kuepukika. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni wanawake wamekuwa wakipambana zaidi kuliko hapo awali ili haki yao ya kuonekana na kutendewa kwa usawa izingatiwe na kutekelezwa.

Ukosefu wa usawa wa kijinsia unafafanuliwa kama mfumo wa kijamii ambao watu wanatendewa tofauti kwa msingi wa jinsia. Hili limedhihirika katika jamii nyingi kote duniani, na linatokea katika namna nyingi na tofauti.

Baadhi ya mifano ya ukosefu wa usawa wa kijinsia dhidi ya wanawake ni: Malipo yasiyo sawa, Unyanyasaji wa kijinsia, Ukosefu wa elimu, Ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji, Utegemezi wa kiuchumi, Ukosefu wa uwakilishi serikalini, kutofikia/kutopata huduma za afya n.k

Katika nchi zilioendelea, angalau wanawake wana uhuru wa kujieleza, wanaweza kuingia barabarani kwa maandamano na wanaweza kuelezea changamoto zao kwa serikali. Lakini pia, katika nchi hizo wanawake wengi wamebahatika kupata elimu, kujiamini na kuungwa mkono na wanaume katika maisha yao ili kukabiliana na masuala ya ukosefu wa usawa wa kijinsia uliopo katika jamii.

Katika nchi zinazoendelea – hususan za Afrika – kumekuwa na hatua ndogo kuelekea katika usawa huu na nguvu ya ziada bado inahitajika kuhakikisha pengo kati ya wanawake na wanaume katika nyanja zote linapungua zaidi na hatimaye kuondoka kabisa.

Hali Ilivyo Duniani

Kwa mujibu wa ripoti ya Global Gender Gap Report (2021) inayotolewa na World Economic Forum, pengo la jumla la kijinsia katika bara la Afrika, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara ni 32.7%. Yaani ni kama 67.2% tu ya pengo limezibwa hadi sasa, na itachukua miaka 121.7 ili kuzibwa kabisa.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa kati ya nchi 35 katika ukanda huo, ni Namibia na Rwanda pekee ambazo zimeziba angalau asilimia 80 ya mapengo yao.

Katika suala la ufikiaji wa elimu, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiyo ukanda ulio nyuma zaidi ya kanda zingine, ikiwa ni 84.5% tu ya pengo hili limezibwa hadi sasa. Ingawa nchi sita (Botswana, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Mauritius na Eswatini) wameziba 99% ya pengo hili, nchi 8 bado hazijafunga zaidi ya 20% ya hili pengo.

Hata katika ngazi za elimu ya msingi, pengo la usawa wa kijinsia bado linaendelea katika nchi kadhaa. Katika nchi 18 kati ya 35 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, bado kuna mapungufu ya zaidi ya 20% katika viwango vya kusoma na kuandika kati ya wanaume watu wazima na wanawake. Wenye viwango vya chini sana ni Chad ambapo ni 44.5% tu ya pengo la kusoma na kuandika limezibwa hadi sasa, na 14% tu ya wanawake wanaweza kusoma.

Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa wastani ni 20.8% ya pengo lake la kijinsia katika Uwezeshaji wa Kisiasa limezibwa; nchi nne ni miongoni mwa 20 bora duniani na zaidi ya 46% ya pengo hili limezibwa hadi sasa, wakati nchi 7 zimefunga chini ya 10% ya pengo hilo, jambao ambalo linaziweka nchi hizo katika 20 ya mwisho kidunia.

Miongoni mwa mataifa yaliyofanya vizuri ni pamoja na Rwanda (ya 6), ambayo imefunga 56.3% ya yake Pengo la Uwezeshaji wa Kisiasa, Msumbiji (ya 13, 49.3%), Afrika Kusini (ya 14, 49.3%) na Namibia (ya 19, 46.3%).

Ulaya Magharibi inaendelea kufanya vizuri zaidi na imeimarika zaidi mwaka 2021 ambapo imeziba 77.6% ya pengo lake la jumla la kijinsia, kutoka 76.7% mwaka 2020. Ripoti ya Global Gender Gap Report (2021) inaeleza kuwa ikiwa maendeleo yataendelea kwenye kiwango hicho, itachukua miaka 52.1 kuziba kabisa pengo hilo la kijinsia. Nchi sita kati ya 10 bora kidunia ni kutoka eneo hili: Iceland (89.2%), Finland (86.1%), Norway (84.9%), Sweden (82.3%), Ireland (80.0%) na Uswisi (79.8%).

Usawa wa Kijinsia.png

Nini Kifanyike

Katika nchi nyingi ambazo zinachelewa kupiga hatua, vikwazo vilivyo wazi ni vya kimila na kitamaduni ambavyo vimekita mizizi pamoja na mitazamo ya kijamii dhidi ya wanawake kama viongozi na watoa maamuzi.

Hivyo basi, ni muhimu kwa wanawake kupatiwa usaidizi unaohitajika wa kijamii na kifamilia ili kuondokana na hili. Ni muhimu kuangazia faida za kuwa na wanawake katika kufanya maamuzi na kuwa na mifano ya kuigwa. Ili kukuza vyama vya siasa, ni muhimu kuwa na viwango vya lazima (asilimia fulani) ya wanawake katika miundo ya uongozi.

Katika suala la vikwazo vya kiuchumi, hili linaweza kupunguzwa kwa kukuza fursa na kutoa usaidizi wa kuwakwamua wanawake katika biashara na kuwapa uwezo wa kupata rasilimali sawa na wanaume. Mila na taratibu – za kijamii na zilizo katika maandishi – zinazomnyima mwanamke haki ya kumiliki ardhi na rasilimali nyingine zinahitaji kupingwa kwa nguvu kubwa ya pamoja katika ngazi zote za kijamii na kiserikali.

Kwa mujibu wa Umoja wa Matataifa ni kuwa ingawa ushirikishwaji wa kiuchumi unaongezeka duniani kote, pengo la kijinsia bado lipo: asilimia 80 ya biashara zinazomilikiwa na wanawake na mahitaji ya mikopo hazijafikiwa, na wanawake katika nchi zinazoendelea wana uwezekano mdogo kuliko wanaume kuwa na akaunti ya benki. Hivyo, upatikanaji sawa wa huduma za kifedha sio tu kufungua uwezo wa kiuchumi, lakini pia kuwapa wanawake nguvu katika maamuzi yao ya kifedha.

Inahitajika pia kuhimiza ushiriki wa wanawake katika kazi na shughuli zinazohusu digitali/TEHAMA na kuhakikisha uwepo wa mafunzo ya mbinu za maisha katika zama za digitali kwa wanawake. Shirika la Plan International linasema wasichana na wanawake mara nyingi wana ufikiaji mdogo wa teknolojia na mtandao ikilinganishwa na wavulana na wanaume.

Hasa katika nchi zinazoendelea, wasichana na wanawake wanatatizika kumudu teknolojia na ufikiaji wa mtandao. Isitoshe, dhana potofu kuhusu teknolojia kuwa ‘ya wavulana’ na hofu ya kubaguliwa huzuia wasichana kutumia zana za kidijitali.

Hata hivyo, kuna maeneo mengi yanayopaswa kutazamwa. Uwezeshaji unaweza kuhakikishwa wakati hakuna ubaguzi unaopatikana katika taasisi; kuna elimu ya bora kwa wanawake; hakuna miiko ya kijamii kwa wanawake n.k.

Usawa wa kijinsia unasalia kuwa “operesheni” ambayo haijakamilika katika kila nchi duniani. Mageuzi ya kisheria, kuimarisha ulinzi wa kijamii unaozingatia jinsia na utoaji wa huduma sawia kwa umma, nafasi za uwakilishi wa wanawake, na usaidizi/ uungaji mkono wa harakati za wanawake ni mikakati ambayo imeendelea kuleta mabadiliko na inapaswa kuongezwa.

Serikali, Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia, na sekta ya kibinafsi zikifanya kazi pamoja, zina uwezo wa kubadilisha maisha ya wanawake na wasichana kwa manufaa ya jamii nzima.
 
Suala si Wanaume vs Wanawake. Tukibakia kwenye mabishano hayo hatufiki popote. Baadhi ya mifano ya ukosefu wa usawa wa kijinsia dhidi ya wanawake ni: malipo yasiyo sawa, unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa elimu, kutopata au kufikia teknolojia/ huduma za kidigitali, ukatili, utegemezi wa kiuchumi, ukosefu wa uwakilishi serikalini, kutofikia/kutopata huduma za afya n.k

Usingependa bintiyo, dada au rafiki ajitegemee kiuchumi? Usingependa alipwe kiwango stahiki kutokana na ujuzi wake? Usingependa apate elimu? Ni sawa tu akitendewa maovu?

Mbona huwa hamtaki haki sawa kwenye kutoa matumizi?
 
Back
Top Bottom