Mkuu naomba usome haya maelezo kwa kina.... Nimeyatoa mahali...
UFAHAMU KUHUSU NDOA
Ndoa ni nini?
Ndoa inaweza kutafsiriwa kwa namna nyingi kulingana na kusudi la mhusika na lengo la tafsiri hiyo. Katika tafsiri za kisheria Ndoa inatambulika kama mkataba wa kisheria ambao unaweza kuvunjwa wakati wowote. Kwa sheria za Tanzania Ndoa ni mkataba unaofungwa kwa hiari baina ya Mwanamume na Mwanamke ambao wanakusudia kuambatana na kuishi pamoja kama mke na mume.
Kwa kuwa si kusudi letu kutafakari sheria za nchi zinasema nini kuhusu Ndoa, tungependa kujikita zaidi katika maana ya Ndoa kwa imani ya kikristo ambayo msingi wake unajengwa katika neno la Mungu. Hata hivyo tunapenda kuweka wazi kwamba Ndoa ni suala la kisheria, na ni muhimu sana kwa wanandoa kutambua kwamba zipo taratibu za kisheria zilizowekwa na serikali zinazosimamia masuala ya Ndoa. Kwa kuwa tumefanyika wana wa Mungu, mwenendo wetu na maisha yetu ya Ndoa yanaongozwa na imani yetu kwa Mungu na si sheria za kibinadamu.
Katika imani ya kikristo, Ndoa inaweza kutafsiriwa kama AGANO KATI YA MWANAMKE NA MWANAMUME AMBAO WAMEKUSUDIA KWA HIARI KUAMBATANA NA KUISHI PAMOJA KAMA MKE NA MUME KWA SIKU ZOTE ZA MAISHA YAO. Jambo la msingi kulitambua hapa ni kwamba Ndoa ya kikristo ni AGANO. Kuna tofauti kubwa kati ya kile kinachoitwa AGANO na MKATABA kimsingi agano ni zaidi ya mkataba kwa namna nyingi. Zifuatazo ni baadhi ya tofauti za msingi kati ya agano na mkataba;
AGANO
Hufungwa katika msingi wa kuaminiana, kuheshimiana na kuthamini uhusiano uliopo baina ya pande mbili. Wanaoingia agano wanaaminiana kuamua kwa dhati kujitoa kuishi katika agano siku zote za maisha yao.
Agano linaunganisha utu wa ndani wa mtu katika mahusiano, hupelekea kuunganisha watu katika mahusiano yenye uwajibikaji usio na kikomo.
Agano hushuhudiwa na Mungu ambaye pia ndiye mdhamini wa agano la Ndoa. Hii ndiyo sababu baadhi ya watu katika tamaduni zao wanapoingia agano huapa kwa jina la Mungu wanayemwamini. (Mfano agano la urafiki wa damu katika mila za kiafrika na tamaduni nyingine)
Agano hudhihirisha, kuweka wazi na kuimarisha mambo ya msingi yanayojenga uhusiano wa kudumu/usiovunjika mpaka kifo kiwatenganishe.
MKATABA
Mkataba hufungwa katika hali ya kutokuaminiana, na hivyo wanaoingia mkataba huweka bayana taratibu zitakazoongoza na kusimamia mahusiano yao ikiwemo majukumu ya kila upande unaoingia katika mkataba.
Mkataba unaunganisha huduma inayotolewa na mtu na si utu wake wa ndani. Kwa lugha nyingine, mkataba huainisha na kuweka wazi mipaka ya uwajibikaji baina ya watu wanaohusika.
Mkataba hushuhudiwa na wanadamu na ndio wanaokuwa mashahidi wa mkataba uliofungwa.
Mkataba huainisha na kuweka wazi njia halali za kuvunja uhusiano baina ya watu wanaohusika na mkataba huo.