Nape, Mnyika, Mtatiro: Wapi Itikadi Zenu? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nape, Mnyika, Mtatiro: Wapi Itikadi Zenu?

Discussion in 'Great Thinkers' started by Mchambuzi, Jan 25, 2012.

 1. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #1
  Jan 25, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Pamoja na ukweli kwamba vyama vingi vya siasa Tanzania vinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, na Taratibu, pia kuna ukweli kwamba vyama vyote vikubwa – CCM, Chadema na CUF, vina udhaifu mkubwa katika itikadi zao. Kama tutakavyobaini katika mjadala huu, itikadi ndio moyo wa chama ambao unasukuma damu katika viungo vingine vya chama kama vile katiba, kanuni, taratibu, mwongozo, sera na ilani. Mjadala huu utalenga zaidi kwenye vyama vikubwa vitatu vya siasa Tanzania: CCM, Chadema na CUF.

  Ina maana gani kusema Idara za Itikadi, Siasa na Uenezi za CCM, Chadema na CUF zinapwaya?

  1. Tanzania, tuna vyama visivyokuwa na itikadi inayoeleweka na ya vitendo. Mfano, CCM; CCM ilifanikiwa ki-itikadi chini ya mfumo wa chama kimoja kutokana, iliyolenga ukombozi wa nchi na Utaifa (chini ya TANU); baadae siasa ya Ujamaa na kujitegemea ililenga kumwinua mtanzania/mtanganyika. Lakini tangia kifo cha azimio la Arusha mwaka 1992, CCM imekuwa inahubiri itikadi ya Ujamaa, lakini upande mwingine, inatekeleza itikadi ya soko huru, tena bila ya mchujo. Ukosefu wa msimamo kiitikadi ndio tiketi ya Kifo kwa CCM, na wala sio Ufisadi. Tutalijadili hili kwa undani baadae.

  2. Pia tuna vyama vilivyo jizolea umaarufu kutokana na sababu ambazo hazihusiani na UMMA kubaini ubora wa itikadi ya chama baada ya kufananisha na itikadi za chama/vyama vingine vilivyopo. Badala yake, umaarufu wa vyama hivi unatokana na UMMA kuvikubali kwa sababu nyingine nje kabisa ya ubora wa itikadi zao. Mfano mzuri ni umaarufu wa NCCR miaka ya 1990, na ule wa Chadema miaka ya 2000 – hadi sasa. Nimetumia neno ‘jizolea umaarufu’ badala ya ‘jipatia mafanikio’, Kwa sababu, tofauti na ‘mafanikio’ ambayo hutokana na itikadi, mara nyingi ‘umaarufu’ hutokana na vitu vya mpito, na huwa haudumu kwa muda mrefu. Wengi tunakumbuka umaarufu NCCR miaka ya 1990; umaarufu wa Chadema hauna tofauti kubwa sana kwa sababu mafanikio tunayoyaona hayatokani na ubora wake wa itikadi, bali kwa vitu vya msimu tu, ambavyo vinaweza meguka kirahisi. Hili pia tutalijadili zaidi baadae.

  3. Lakini pia, Tanzania tuna vyama vilivyopata mafanikio kisiasa (sio umaarufu) kutokana na itikadi zao. Lakini vyama hivi vina udhaifu mmoja mkubwa juu ya itikadi zao: Itikadi hizi zinaendana na hali halisi ya upande mmoja tu wa jamii badala ya jamii nzima. Mfano, CUF na mafanikio yake visiwani ambayo imekuwa vigumu kuyarudia Bara. Tutalitazama hili pia baadae lakini kwa sasa ni muhimu tu kusema kwamba - mafanikio ya sasa ya CUF visiwani hayana tofauti kubwa na mafanikio ya TANU bara miaka 1960. Kama ilivyokuwa TANU miaka ya 1960, mafanikio ya CUF yanatokana na itikadi inayolenga Utaifa /Ukombozi dhidi ya Utawala wa Bara. Pamoja na mafanikio yake visiwani, itikadi ya CUF haina mashiko upande wa bara, na pia haitachukua miaka mingi kabla ya itikadi hii kuishiwa makali hata Zanzibar. Kama ilivyokuwa kwa CCM, CUF nayo itapitia hatua tatu za maisha: (1) Itikadi ya uhuru na Utaifa iliyozaa matunda hadi sasa (2) baada ya utaifa kupatikana, CUF itakumbwa na changamoto za kutekeleza ahadi ilizozitoa wakati wa mapambano ya kudai utaifa kutoka Bara. Hali itazidi kuwa ngumu zaidi iwapo patatokea vyama vingine vya upinzani upande wa Zanzibar (3) Iwapo vitajitokeza vyama vipya vyenye nguvu Zanzibar, itikadi ya CUF itazidi kuishiwa makali kwa kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi za ukombozi (kama ilivyotokea kwa CCM), na vyama vitabaki kukosoana huku CUF ikionekana sio lolote/dhaifu, huku vyama vya upinzani Zanzibar vikisahau kabisa kwamba adui yao ni mmoja – wawakilishi wa mataifa tajiri yani - WorldBank na IMF.Hili pia tutalijadili baadae.

  Udhaifu huu wa ki-itikadi ndani ya vyama vya siasa unawakosesha wananchi fursa ya kuunda muono na mtazamo wa kisiasa unaofuatana na imani (za kiitikadi) zinazotambulika, na nyepesi kueleweka au kutofautisha. Hii ndio sababu kubwa kwanini inakuwa rahisi kwa wananchi kuunga mkono vyama kishabiki zaidi kuliko kutokana na kushiba imani za vyama. Ndio maana, tofauti na nchi zilizokomaa kisiasa, kwa Tanzania, suala la wanachama kuhama hama vyama ni suala la kawaida. Vilevile kwa upande wa viongozi wa vyama, ni jambo la kawaida kuwasikia wanasiasa wa chama kimoja wakitetea wanasiasa wa vyama vingine hata kama wamepewa adhabu kwa kwenda kinyume na katiba na kanuni za vyama vyao (mfano Zitto kuwatetea kafulila na Hamad). Kama Chadema ingekuwa inaendesha siasa za ki-itikadi, jambo hili lisingetokea kwani itikadi ya Chadema na ile ya CUF ni tofauti kabisa. Katika demokrasia iliyokomaa na yenye kuendeshwa ki-itikadi, kitendo cha wanasiasa kuteteana kwa sababu binafsi, au wanasiasa kuhama hama vyama, ni kitendo cha kujimaliza kisiasa. Ni katika nchi kama Tanzania pekee ambapo leo mwanasiasa anaweza jitoa CHADEMA, CCM, au NCCR na kwenda chama kingine bila ya hofu yoyote. Hiki ni moja ya vielelezo vikubwa juu ya udhaifu wa vyama vyetu ki- itikadi. Katika mazingira ya kawaida, kitendo cha kiongozi kuhama chama ni sawa na kukana imani (itikadi) yake na kukumbatia imani (itikadi) nyingine. Kwa mwanachama kufanya hivi sio jambo la hatari sana, lakini ni la hatari sana kwa viongozi.

  Ni mapungufu haya ya ki-itikadi ndiyo hupelekea vyama vyetu kunadi ilani na sera zinazofanana, badala ya kuwa na ushindani mkali wa mtazamo unaotokana na itikadi. Katika siasa za sasa, vyama vyote vinashindana kwenda Ikulu, sio kuleta jambo jipya linalotokana na itikadi zao, bali kutekeleza sera zile zile za soko huria zilizojaa uholela, za WorldBank na IMF, kwa kasi na ufanisi zaidi. Vyama pia vinapoteza muda mwingi sana kushindania yasiyo na umuhimu sana yakiwa yametapakaa (not coherent), kama vile haki za raia, utawala wa sheria, na vita dhidi ya ufisadi. Siasa juu ya masuala haya zimekosa uthabiti (consistency) na kuungamana (coherence) kutokana na udhaifu wa ki-itikadi. Vile vile, kutokana na udhaifu wa ki-itikadi, umaarufu wa vyama mara nyingi (kama sio mara zote), unatokana zaidi na hulka (personalities) za viongozi waliopo katika vyama hivyo, hasa nguvu zao katika jamii wanazotoka, bila ya kujali vyama wanavyotoka au itikadi wanazoziamini.

  Mapungufu ya ki-itikadi yanapelekea vyama kushiriki katika ushindani wa siasa kama vile ni soko la kushindana ubora wa bidhaa. Vyama vinajikita zaidi katika ushindani wa nani ana bidhaa bora zaidi (sera na ilani), kuliko mwenzake, bila ya uwiano na itikadi zao. Vyama vinajali zaidi kuja na bidhaa zinazoendana na mahitaji ya soko kwa wakati huo. Idara za uenezi, siasa na itikadi hazijishughulishi kuzunguka nchi nzima kujenga chama na kusambaza imani (itikadi) zao ili kushawishi wananchi kuwa wafuasi wa kudumu, na pia wawe wapiganaji wa kutetea na kulinda itikadi zao katika maeneo wanayoishi. Nguvu ya chama cha siasa ipo kwenye matawi na mashina, huko ndiko watu wengi wanaishi. Lakini cha ajabu ni kwamba, Idara za itikadi, siasa na uenezi, zinatumia muda mwingi kwenye Redio, TV na magazeti kama vile nguvu ya chama ndio zipo huko. Huwa wanakumbuka umuhimu wa matawi na mashina wakati wa uchaguzi tu. Nia ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1960, ya kumwachia Kawawa uongozi wa nchi kwa muda na yeye kwenda vijijini ilikuwa ni kujenga chama akisaidiwa na idara ya itikadi na uenezi ya TANU. Aliporudia zoezi hili wakati anawaaga watanzania miaka ya mwisho ya 1990, alielezea kushtushwa kwake na jinsi gani imani ya chama ilivyokuwa ikishuka, kutokana na chama kuzembea kusambaza itikadi kwenye maeneo yanayostahili.

  Kwa Tanzania ya leo, udhaifu huu ndio unaozaa UMMA usiokuwa na msimamo wa kudumu wa kisiasa, na wengine wengi kutoona umuhimu wa kushiriki katika siasa. Wananchi wengi wamechoka na vyama vya siasa, kwani havitekelezi yanayohubiriwa. Isitoshe, mara nyingi, kauli na vitendo vya vyama vilivyopo hupishana, mfano suala la posho za wabunge n.k. Idara za uenezi, siasa na itikadi zimeshindwa kufanya kazi zake kwa ukamilifu, idara hizi mara nyingi uendesha siasa za leo kupinga hili, kesho kuunga mkono lile, ili mradi tu “kujiepusha wasipitwe na masuala ya kupita”. Suala la idara hizi kuja na pre – emptive strategies halipo, na badala yake ni pro-active strategies. Hiki ni kikwazo kikubwa sana kwa ustawi endelevu wa vyama vyetu vya siasa, na demokrasia kwa ujumla.

  Umuhimu wa Itikadi ya Chama

  Kama moyo ulivyokuwa na umuhimu kwa uhai wa binadamu, itikadi ni moyo wa chama cha siasa. Moyo wa chama (itikadi) ndio husukuma damu ili kuviwezesha viungo vingine vya chama (katiba, kanuni, taratibu, mwongozo, ilani na sera), vifanye kazi zake kwa uhakika na ukamilifu. Itikadi utengeneza mtazamo, msimamo, malengo na matarajio kuhusu masuala mbali mbali yanayozunguka maisha ya jamii. Na mitazamo, misimamo, malengo na matarajio haya uhathiri matendo na shughuli za kisiasa ndani ya jamii husika. Wananchi hutegema sana itikadi kama moja ya njia zao kuu za kuwasaidia kuelewa masuala mbalimbali ya kiulimwengu, kwani iItikadi hutoa mwongozo na kusaidia uwepo wa misingi ya kuratibu jinsi gani jamii iendeshe masuala yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, katika hali ya ufanisi, nidhamu na utulivu.

  Katika dunia ya leo, Itikadi zimegawanyika katika makundi makubwa sita kama ifuatavyo:

  1. Ukomunisti
  2. Ujamaa
  3. Ujamaa wa kidemokrasia/Deocratic Socialism/Social Democrats
  4. Uliberali/Liberal
  5. Conservative Liberals/mchanganyiko wa uhafidhiana na uliberali
  6. Uhafidhiana/Conservative

  Mpangilio huu wa itikadi hutokea kushoto kuelekea kulia (as a continuum) kama ifuatavyo:

  Communism=>Socialism=>Ujamaa wa Kidemokrasia=>Liberals=>Conservative Liberals=>Conservative

  Kwahiyo kwa mfano, itikadi ya kikomunist, na kijamaa zinatambulika kama itikadi za mrengo wa kushoto (leftist), wakati itikadi ya uhafidhiana (conservatism) inatambulika kama itikadi ya mrengo wa kulia (rightists). Katika miaka ya hivi karibuni, itikadi hizi kuu zimezaa itikadi nyingine tatu kubwa ambazo ni: (1) Centre/kati; (2) kati-kulia (centre-right); na (3) kati-kushoto (centre-left); Nitazijadili kwa undani baadae. Vinginevyo, kwa ujumla wake, ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia/democratic socialism zinazotambulika kama itikadi za mrengo wa kushoto, wakati uliberali, conservative liberals na conservative hujulikana kama itikadi za mrengo ya kulia.

  Tuzitazame itikadi hizi sita kubwa kwa undani, ili tuzidi elewa itikadi za vyama vya CCM, Chadema na CUF kwa undani zaidi. Ili kurahisisha zoezi hili, nitazigawanya itikadi hizi sita katika makundi makubwa mawili - kundi la kwanza ni lile la itikadi zote za mrengo wa kushoto yani ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia/social democrats; Na kundi la pili ni itikadi zote za mrengo wa kulia, yani uliberali, conservative liberals na conservatives. Tuanze na itikadi za mrengo wa kushoto – Ukomunisti, Ujamaa, na Ujamaa wa Kidemokrasia, kwa kufuatana na mpangilio tuliokwisha uona ambao ni:

  Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Conservative Liberals=>Uhafidhiana

  Itikadi za mrengo wa kushoto (Ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia), asili yake ni Karl Max ambae alidai kwamba Ubepari muundo wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wengi wetu tayari tunalielew vizuri suala hili.

  [TABLE]
  [TR]
  [TD]
  [/TD]
  [TD]UKOMUNISTI
  [/TD]
  [TD]UJAMAA
  [/TD]
  [TD]UJAMAA WA KIDEMOKRSIA
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]UTAWALA
  [/TD]
  [TD]Mamlaka yote ipo chini ya umma; kuna mwafaka katika jamii kuhusu michakato wa maamuzi mbalimbali.
  [/TD]
  [TD]Masuala ya umma yanaendeshwa kwa “power structure” iliyopo chini ya muundo wa halmashauri, kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa.
  [/TD]
  [TD]Masuala ya umma yanaendeshwa na viongozi waliochaguliwa kupitia muundo wa kidemokrasia.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]CHAGUZI
  [/TD]
  [TD]Hakuna chaguzi kwani serikali ya kikomunisti inakubalika na wote.
  [/TD]
  [TD]Ingawa mara nyingi huwa na chama kimoja cha siasa, huwa kunakuwepo na chaguzi za mara kwa mara, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka juu hutokana na watu.
  [/TD]
  [TD]Viongozi wa umma hutokana na chaguzi za mara kwa mara zenye uwazi na uhuru kwa wapiga kura;
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]SERIKALI
  [/TD]
  [TD]Maisha yote ya jamii, kuanzia utawala, uchumi na maisha binafsi, yapo chini ya serikali.
  [/TD]
  [TD]Kuna za makusudi za kuunganisha serikali na jamii nzima.
  [/TD]
  [TD]Serikali thabiti huitajika ili kuendesha mipango na sera za kugawanya keki ya taifa.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]UCHUMI
  [/TD]
  [TD]Hakuna soko wala ubadilishanaji (exchange) wa aina yoyote; hakuna umiliki binafsi wa mali; bidhaa na huduma zote zinagawanywa sawa katika jamii bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
  [/TD]
  [TD]Uwepo wa mishahara isiyotofautiana sana; Pia huduma na bidhaa nyingi kwa umma hutolewa na serikali.
  [/TD]
  [TD]Ubepari unakubalika, na unashamiri kupitia muundo thabiti wa kugawana keki ya taifa na upatikanaji wa huduma bora za kijamii.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]KAZI/AJIRA
  [/TD]
  [TD]Hakuna matabaka ya aina yoyote miongozi mwa wafanyakazi.
  [/TD]
  [TD]Kuna muungano wa tabaka la wafanyakazi; uwepo wa fursa sawa kwa watu wote bila kujali matabaka.
  [/TD]
  [TD]Kuna umoja wa kitabaka miongozi mwa wafanyakazi kupitia taasisi zinazounganisha tabaka hili.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]MAPINDUZI
  [/TD]
  [TD]Kuna mapinduzi yanayolenga kufuta uhaba (scarcity) na pia umiliki binafsi wa mali.
  [/TD]
  [TD]Kuna mapinduzi ya kuangamiza ubwanyenye.
  [/TD]
  [TD]Mapinduzi hayahitajiki kwani ubepari unakubalika hivyo kuendelea kushamiri.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]PROGRAMU ZA KIJAMII
  [/TD]
  [TD]Wananchi hupatiwa huduma zote za msingi na serikali bure, kwa mfano elimu, afya, n.k.
  [/TD]
  [TD]Umiliki wa umma wa njia kuu za uchumi, na matumizi ya rasilimali ya taifa kwa manufaa ya umma pamoja na upatikanaji wa huduma zote za msingi kwa watu wote.
  [/TD]
  [TD]Msisitizo mkubwa ni uwepo wa a “Welfare State”, yenye Social security programs zinazolenga kutoa msaada kwa wote wanaostahili - kama vile huduma ya afya, elimu, makazi, n.k; Pia serikali hugawanya mapato (redistribute income) kwa kutoza kodi za aina mbali mbali kwa lengo la kupunguza tofauti za kiuchumi baina ya matabaka mbalimbali, huku pia ikiweka kinga thabiti kwa watu wasio na ajira, wagonjwa, na wastaafu.
  [/TD]
  [/TR]
  [/TABLE]


  Na sasa tuziangalie itikadi za mrengo wa kulia –Uliberali, Liberal Conservatives, na Conservativesm/uhafidhiana.

  1. Uliberali
  Asili ya itikadi hii ilikuwa ni kupigania haki za watu katika jamii za mataifa ya magharibi yaliyokuwa chini ya tawala za kifalme; tawala hizi hazikutoa haki na fursa sawa za kiuchumi kisiasa na kijamii kwa wananchi. John Locke ndiye (mwanzilishi), na wenzake walidai kwamba – binadamu huru ndio msingi wa jamii imara yenye amani na utulivu; pia walihimiza umuhimu wa kuwepo kwa serikali yenye wajibu wa kulinda haki za msingi za wananchi; harakati hizi ndiyo zilizokuja kuzaa dhana nzima ya demokrasia ya uwakilishi (representative democracy); Baadae harakati hizi ziilichochea kuzaliwa kwa uliberali katika eneo la uchumi, muasisi wake akiwa Adam Smith, ambae alihimiza umuhimu wa serikali kutoingilia shughuli za kiuchumi, kwa mtazamo kwamba, serikali ikiachia shughuli za uchumi zijiendeshe na kujisahisha zenyewe itapelekea ufanisi zaidi katika uchumi. Katika dunia ya leo, Itikadi hii bado ina nguvu kubwa. Kuna jamii nyingi duniani zinazo himiza umuhimu wa serikali kutojiingiza katika shughuli za kiuchumi na kijamii, kwa mfano, serikali kukaa mbali na na utoaji wa huduma za kijamii – afya, elimu n.k; na pia serikali kutoshiriki katika uchumi kupitia mashirika ya umma, na badala yake, mashirika binafsi pekee ndiyo yatawale shughuli za kiuchumi.

  2. Conservative Liberals
  Itikadi hii ni mchanganyiko wa mawazo, sera na imani za uliberali (liberalism) na uhafidhiana (conservatism). Itikadi hii inaunga mkono ulegezaji wa masharti mbalimbali ya kiuchumi na utandawazi (globalization), Pia inaunga mkono sera kali zinazozuia uhamiaji (strict immigration policies). Kiuchumi – itikadi hii inaunga mkono uwepo wa uhuru wa kiuchumi miongoni mwa wananchi, hasa kuwapatia wananchi uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Itikadi hii haijihusishi sana na masuala ya kijamii lakini kila inapobidi kufanya hivyo, huwa na msimamo wa kijamii ulio sawa na ule wa kiliberali (rejea mjadala wa uliberali hapo juu).

  3. Conservatives/wahafidhiana
  Asili ya itikadi hii ni harakati za kupinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa Ufaransa katika karne ya kumi na nane. To conserve maana yake ni ‘kuhifadhi’, hivyo conservatives hawaamini katika mabadiliko au uharibifu wa desturi/utamaduni. Edward Burke ni muasisi wa itikadi hii; yeye alipinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa ufaransa kwa mtazamo kwamba kitendo hicho kitaharibu desturi, imani na taasisi zilizojengwa kwenye jamii kwa muda mrefu ambazo ni muhimu katika maisha ya watu. Katika siasa za leo, wahafidhiana wanapinga ushiriki wa serikali katika uchumi kwa madai kwamba, umaskini ndani ya jamii ni matokeo ya serikali kuingilia maisha ya wananchi kwani kitendo hiki hulea watu wavivu, na kuua dhana ya uchapa kazi na uwajibikaji katika jamii. Badala yake, wahafidhiana wanahimiza kila mtu kujipatia riziki yake kwa jasho lake, na sio kusubiri serikali kupitia huduma za kijamii, social security, n.k. wahafidhiana pia wanapinga uwepo wa mashirika ya umma katika uchumi, na badala yake wanahimiza uchumi uendeshwe na mashirika binafsi.

  Kama tulivyoona awali, itikadi hizi sita zkubwa baadae zilizaa itikadi nyingine tatu: Centre/kati; kati-kulia (centre-right); na kati-kushoto (centre-left). Tuzitazame na hizi:

  Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Conservative Liberals=>Uhafidhiana

  1. Itikadi ya Mrengo wa Kati (Centre) – Huu ni mrengo kati ya Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia. Chadema inatamka hii kama itikadi yake kama chama. Kwa kawaida, Itikadi ya mrengo wa kati (centre) inaamini na kuunga mkono mambo makuu yafuatayo:
  · Ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato vitokanavyo na shughuli za uchumi (progressive taxation); Umiliki binafsi wa mali; Uhuru na haki ya wananchi mbele ya sheria; Uliberali wa kiuchumi na uliberali wa kijamii.

  Uliberali wa kiuchumi kwa maana ipi:
  · Kuwapatia wananchi uhuru wa kujiendeshea shughuli zao bila ya kuingiliwa na serikali; Umiliki wa mali binafsi; Serikali kuratibu/rekebisha (regulate) uchumi, lakini wanapinga serikali kukwaza uhuru wa biashara na ushindani katika soko; wanaunga mkono sera za serikali za kuondoa ukiritimba binafsi (private competition) kwa imani kwamba ukiritimba huu unaumiza wananchi maskini;

  Uliberali wa jamii kwa maana ipi?
  · Haki ya kijamii na uhuru kwa watu wote; Wajibu wa serikali kuinua hali za maisha ya wananchi kwa njia kama vile – ajira, afya, elimu, huku haki za wananchi zikizidi kuimarishwa.

  2. Mrengo wa Kati - Kulia (centre-right) – huu ni mrengo uliopo katikati ya Uliberali na Conservative Liberals.
  · Kwa ujumla, itikadi hii inaunga mkono kanuni nyingi za soko huru; lakini vilevile inapinga serikali kujiingiza kupita kiasi kwenye shughuli za kiuchumi (kupitia mashirika ya umma); inapinga serikali kujingiza kupita kiasi kwenye utoaji wa huduma za kijamii (kama vile afya na elimu); na inaunga mkono umiliki wa mali binafsi;

  3. Mrengo wa Kati – Kushoto – huu ni mrengo uliopo kati ya Ujamaa wa Kidemokrasia na Ujamaa.
  Mrengo huu unaamini katika yafuatayo:
  · Jamii endelevu na serikali endelevu; Uliberali wa kijamii (rejea hapo juu), na siasa za kijani (green politics); pia ina amini katika mchanganyiko wa sekta ya umma na sekta binafsi kuendesha huduma za kijamii kama vile elimu, afya n.k; Uwepo wa social security ya kutosha kwa wananchi wanaostahili tu (sio katika kiwango cha Ujamaa na Ukomunisti) ili kupunguza kasi ya umaskini na kulinda ‘vipato’ vya wananchi wanaioshi katika mazingira ya uzee (wastaafu), wagonjwa, walemavu na wasio na ajira; mrengo huu pia una amini katika haki na fursa sawa kwa wote; inaunga mkono uwepo na umuhimu wa taasisi za serikali zinazoratibu sekta binafsi kwa nia ya kutetea wafanyakazi na walaji (consumers), kwa kuhakikisha uwepo wa vyama vya imara vya wafanyakazi, na pia ushindani wa haki (fair competition) katika soko; pia wanaunga mkono ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato katika uchumi, lengo kuu likiwa kukusanya kodi ya kutosha ili isaidie kutoa huduma muhimu za kijamii kwa wale wanaostahili.

  Kwa leo naomba niishie hapa ili kupunguza urefu wa uzi huu ambao tayari umepitiliza. Ila ningependa kumalizia kwa kusema kwamba - ni muhimu kwa vyama vyetu vya siasa kuamka na kuchagua itikadi zilizokuwa ‘relevant’ na mazingira ya nchi na kuondokana na siasa za kubahatisha. Siaza za ki-itikadi zitavipatia vyama vyetu vya siasa mafanikio ya kudumu, na maisha marefu, badala ya umaarufu wa muda mfupi kama ule uliotokea kwenye chama cha NCCR, mzimu ambao pia unaviwinda vyama vya Chadema na CUF hivi sasa, huku CCM ikiwa imeshafikia katika hatua ya mwisho kabisa ya maisha yake. Ni muhimu wananchi kushiba itikadi za vyama. Ni muhimu kuanza kuwavutia wananchi kwa sababu nje ya personalities za viongozi wa vyama, au kelele za ufisadi ambazo hazina mashiko ya ki-tikadi. Pa ni muhimu nitamke kwamba kwa hali ya sasa ya udhaifu ki-itikadi ndani ya vyama vyetu vikubwa, sio CCM, CHADEMA, CUF, au NCCR, ambavyo vina majibu ya kumnyanyua mtanzania kutoka katika umaskini. Kinachoendelea sana sana ni mbio za vyama hivi kukimbilia Ikulu ili kuwa watekelezaji wazuri zaidi kuliko wenzao, wa sera za soko holela zinazolazimishwa kwetu na WorldBank na IMF.

  Lakini vyama vya siasa Tanzania bado vina nafasi nzuri ya kurekebisha mapungufu yote haya. Kwa CCM ambayo ndio chama tawala, ni lazima sasa itambue kwamba Ujamaa wa Marxist – Lenin ulishaanguka zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini haina maana kwamba Ujamaa umefeli. Ujamaa wa Kidemokrasia kama ule uliopo katika nchi za Sweden na nyinginezo ndio njia sahihi ya CCM kuifuata ki-itikadi. Nje ya kufanya haya, CCM haina mbadala mwingine zaidi ya KUFA, kwani kitaendelea kushindana na vyama kama Chadema katika sera zile zile, tofauti kubwa ikiwa, mmoja yupo madarakani, mwingine ni mpinzania. Kwa Chadema na CUF, ingawa wana declare itikadi zao kuwa ni mrengo wa kati (Chadema) na Uliberali (CUF), vyama hivi bado vina mapungufu makubwa ki-itikadi, ambazo nitazijadili siku ningine. Poleni na pia samahanini kwa uzi mdefu.
   
 2. Kimbunga

  Kimbunga Platinum Member

  #2
  Jan 25, 2012
  Joined: Oct 4, 2007
  Messages: 13,012
  Likes Received: 1,817
  Trophy Points: 280
  Mkuu mada nzuri na elimu yake mujarabu lakini yatizo huwa huna summary! Uchambuzi mzuri. kwa maaana nyingine unasema vyama ni vingi tunavyovishabikia ni vya msimu?
   
 3. M

  Molemo JF-Expert Member

  #3
  Jan 25, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Wewe mtu wa CCM tangu lini ukawa na nia njema na Chadema?
   
 4. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #4
  Jan 25, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Upo sahihi. Hakuna Chama chenye itikadi thabiti ya kuweza kukitofautisha na chama kingine 'black and white'; pia hakuna chama chenye itikadi yenye majibu ya kumwokoa mtanzania maskini zaidi ya kuwa na shopping list isiyotekelezeka, na isiyo na mwelekeo wa kupambana na changamoto za WorldBank na IMF, kwani hawa ndio wadau wakubwa wa umaskini wetu.
   
 5. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #5
  Jan 25, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Ndiyo hayo nayozungumzia. Pangekuwa na elimu tosha juu ya umuhimu wa itikadi katika ushindani wa siasa za vyama vingi, ungeenda mbali zaidi na kujibu hoja.
   
 6. M

  Molemo JF-Expert Member

  #6
  Jan 25, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Mchambuzi,
  Nakushauri hangaika na namna ya kuwaondoa mafisadi ndani ya chama chako.Pili kwa vile wewe ni mwanachama mwaaminifu wa CCM kakae na Nape mzungumze mambo ya Itikadi ya Ujamaa ya chama chenu.Mambo ya Chadema waachie wenyewe.Hapo huna lengo lolote zaidi ya kuipiga vita Chadema kitu ambacho naamini hutafanikiwa.
   
 7. Suzie

  Suzie JF-Expert Member

  #7
  Jan 25, 2012
  Joined: May 7, 2010
  Messages: 1,264
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  Tatizo unataka tukufanyie Research paper yako humu JF fine hatujakataa put in summery form basi highlite possible angles umesoma wapi wewe???? Hujui humu JF sio ofisini kwetu tunamashughuli yetu yanatuumiza kichwa unatuletea kizunguzungu tena jamani
   
 8. RaiaMbishi

  RaiaMbishi JF-Expert Member

  #8
  Jan 25, 2012
  Joined: Jan 18, 2012
  Messages: 252
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Wadau, mnashindwaje kumwelewa Mchambuzi jamani, hivi tupo makini katika kufikiri kweli? Amekuwa very neutal na straight to the point. Tatizo letu watanzania tunapenda sana kusikia maneno matamu peke yake. Hivi tukija kamata nchi 2015 baada ya kuyatoa magamba, na ikatokea magamba yanachukua tena nchi mwaka 2020, je haitakuwa kwa sababu kama hizi? tujifunze kufikiria kwa mapana. Kama tunawatakia watanzania mema, na kama tunakitakia Chadema mafanikio na ustawi wa kudumu, tujifunze kwa hoja kama hizi, na kama hatukubaliani na mchambuzi, tumjibu kwa hoja. Jamani, sio kila kitu kuhusu Chadema ni fitina, mengine ni ya kweli kabisa. kama kina Mnyika ni viongozi makini, watashughulikia vacuum hii aidha kimya kimya au hata huko majukwaani. Pia nimependa hoja yako kuhusu Zitto na kimbelembele cha Kafulila na Hamad. Huyu mtu ni wa ovyo sana. Tunasubiria hoja zako zaidi kuhusu udhaifu wa Chadema na CUF katika itikadi zao za sasa, kama ulivyo ahidi. Usife moyo kwani haubomoi, bali unajenga. Jukwaa la Siasa linalalamika hakuna msisimko, lakini kila wakati mada nzuri kama hizi zikija, zinapigwa vita.
  Na je, una maana kuna pengo katika siasa za Zanzibar ambalo Hamad akija na chama chake kipya anaweza kuliziba? Kazi nzuri sana mchambuzi. Pamoja na kwamba wewe ni Gamba, wapo wa kuelewa vyema hoja zako. Ila nakushauri uondoke huko kwenye chama maiti, kasaidie vijana wenzako katika mapambano chini ya vyama vingine. Karibu Chadema.
   
 9. Nun

  Nun New Member

  #9
  Jan 25, 2012
  Joined: Jan 3, 2012
  Messages: 2
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Jamani eeeh, mkilemewa na hoja au mkiona zinawapa kizungu zungu kutokana na maandishi marefu, ziacheni, wapo wenye muda huo.
   
 10. M

  Molemo JF-Expert Member

  #10
  Jan 25, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Mkuu RaiaMbishi
  Nimeisoma makala ya Mchambuzi na kuirudia mara mbilimbili.Na pia nimesoma andishi la mwandishi wa Raia Mwema Mayage S Mayage siku chache zilizopita.Utadhani watu hawa walijifungia mahali wakaandika wanachodai ni utafiti.Mchambuzi anajifanya kuwa neutral kuzungumzia vyama vitatu lakini hakika halengi vyama vyote vitatu.Lengo lake analenga chama cha Demokrasia na Maendeleo.Mwandishi Mayage S Mayage katika maandishi yake alijifanya yuko neutral mwanzoni lakini baadaye alivyoteka akili za watu akaanza kutoa hitimisho za makala zake kwa kuishambulia Chadema na kudai watanzania kuunda chama kipya kwa madai kwamba Chadema haina Itikadi inayotambulika.Nashukuru upotoshaji ule ulikuja kujibiwa vilivyo na Katibu Mkuu Dr Wilbrod Slaa.
  Sasa wenye ufahamu tukisoma between the lines tunanusa harufu kama ya Mayage ya kuishambulia Chadema kwa mlango wa nyuma.Mchambuzi si mjinga kwani anafahamu Chadema kwa sasa ndicho chama maarufu zaidi na kinachopendwa na vijana na wasomi wengi,kwa hiyo anaanza kupandikiza hayo aliyopandikiza ili kupotosha watu.Ili asisakamwe sana anataja vyama vitatu katika mjadala wake lakini lengo lake mwishoni itakuwa ni kuishambulia Chadema.Na tusubiri tuone.
  Mcha,buzi anafahamika.Ni kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi.Swali dogo tu-Ni tangu lini kada huyu maarufu na mkereketwa wa CCM akawa mwema sana kuishauri Chadema.Mchambuzi anafahamu mpinzani mkuu wa Chama chake ni Chadema,Je kweli ana nia njema ya kuishauri Chadema ili isonge mbele iking'oe chama chake CCM madarakani ?
  Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kwamba Mchambuzi anaweza kutoa ushauri au hoja yeyote kwa maslahi ya Chadema.Bali nina hakika chochote akisemacho kitakuwa na maslahi ya chama chake CCM na kukiangamiza Chadema.
  Hatujasahau-ni wiki mbili tu zilizopita pale wabunge wa Dar es Salaam walipolalamikia ongezeko la nauli kwenye Kivuko cha Kigamboni.Ni Mchambuzi huyu huyu aliyetoa makala ndefu ya kumshambulia John Mnyika mbunge wa Ubungo-Chadema kana kwamba ni Mnyika mwenyewe aliyetoa lile tamko,huku akijua fika mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam ni Zuberi Mtemvu mbunge wa Temeke.Wenye akili tulijiuliza mbona ashambulie mbunge wa Chadema pekee? Kwa hiyo haya tunayoyasoma hapa tunaamini ni mwendelezo uleule.
  Mchambuzi kwanini tukuamini??
   
 11. M

  Molemo JF-Expert Member

  #11
  Jan 25, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Mkuu fmpiganaji-Hakika umemaliza kila kitu.Hata mimi tangu mwanzo niliona kitu kama hicho.Nimeamini JF ni home of great thinkers.Asante sana umetufumbua macho wengi.
   
 12. tembeleh2

  tembeleh2 JF-Expert Member

  #12
  Jan 25, 2012
  Joined: Jul 27, 2010
  Messages: 768
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Mchambuzi hii habari ni nzuri lakini ingefaa zaidi kuwekwa kwenye gazeti. humu tunaweka habari kwa kifupi. angalia wenzako wanavyopost habari zao.
   
 13. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #13
  Jan 25, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Asante kwa mchango wako mzuri,

  Tukianza na suala la Mnyika na nauli za Feli - nilitoa mawazo yangu kwa hoja ambazo zilikuwa zinajadilika kabisa. Pia niliweka bayana kabisa kwamba msimamo ule ulistahili kutolewa na wabunge wa CCM ambao wengi wao, tumewazoea na siasa zao ni za 'butua ili mradi kiende'. Lakini kwa jinsi ninavyomheshimu na kumkubali Mnyika, ambae kwa maoni yangu ni mmoja ya wabunge tano bora katika bunge la Tanzania (wengine wakiwa Zitto, Lissu, Mnyaa na January), sikutegemea kama Mnyika angeingia katika sakata lile, kwani busara ingekuwa aidha kulinyamazia kwani lisingemletea madhara makubwa kisiasa, lakini kama aliona kuna umuhimu kulitolea maelezo kwa nafasi yake, angetulia kwanza. Vinginevyo suala hili litakuja kumuuma baadae, kwa maelezo niliyokwisha yatoa. Kina Nape, Mtatiro, kwa nafasi zao waliliacha suala hili lipite, na je, wameathirika vipi? Na je, Mnyika kanufaika vipi? Msimamo kuhusu nauli angewaachia wabunge walio karibu zaidi na eneo lile kikazi na kimakazi. Isitoshe, tumewazoea wabunge wengi wa CCM na kauli na misimamo holela iliyojaa siasa kuliko mantiki. Lakini sio J.J Mnyika.


  Kuhusu hii mada ya itikadi ya vyama mbalimbali, kwanza mimi sio kada maarufu wa chama na mkereketwa kama unavyoelezea, ingawa shati hili la chama linaweza kukufanya uamini hivyo. Mimi ni mwanachama wa CCM, kama alivyokuwa mwanachama mwingine yoyote aliyelipia ada zake zote. Na pia naomba utambue kwamba sina uongozi wowote ndani ya Chama, na sitarajii kutafuta uongozi huo katika siku za hivi karibuni. Vinginevyo nabakia kama mwanachama wa CCM mwenye mawazo huru, kama ilivyo kwa manachama mwingine wa CCM, Chadema, CUF, NCCR, n.k. Katika mazingira hayo, naamini kabisa nina haki ya kutoa maoni yangu juu ya miendendo ya vyama vyetu vya siasa, kama ilivyokuwa haki kwa Mtanzania yoyote. Suala muhimu linakuja kwamba - iwapo kuna yoyote anayepingana na mawazo yangu, ana uhuru wa kufanya hivyo ilimradi anajibu kwa hoja, sio kwa matusi, shutuma, au hisia kwamba nimetumwa na CCM, nina nia mbaya na Chadema, n.k. Nilishatamka tangia miaka ya mwanzo ya 2000 kwamba, iwapo itatokea ntaacha kuwa mwanachama wa CCM kwa kukata tamaa kwamba kimeshindwa kumwokoa mtanzania, kutokana na arrogance tu miongoni mwa viongozi wake, basi chama changu kingine kitakuwa Chadema, ilimradi kifanye mabadiliko kidogo katika itikadi yake ili ilenge zaidi siasa za demokrasia ya kijamaa, na sio soko huria kama linavyopigiwa debe hivi sasa na wahisani kwa niaba yao na WorldBank na IMF. Niliyatamka haya kwa wengi tu, tena kabla ya Chadema kupata umaarufu huu wa sasa.

  Kwa mtazamo wangu, hiyo hiyo ndiyo njia pekee ya kumwokoa Mtanzania maskini. Vinginevyo kwa hali ya sasa, siasa zilizopo ni za kukimbilia tu Ikulu - wote CCM, Chadema, CUF, NCCR, n.k, sio siasa za kumwokoa mtanzania aliyepo kijijini (70% of the population).
  Naombeni mniwie radhi iwapo nimeagusa wengi pabaya. Mada yangu ilikuwa na nia njema tu from a neutral ground, na inajadilika kabisa. Tatizo pengine ni kwamba imetolewa na mtu aliyevaa shati la CCM. Vinginevyo nia yangu ililenga kuleta mada ya kuamsha majadiliano katika platform hii ya siasa, hasa kwa kuzingatia hoja za kina Mkandara na wengine kwamba jukwaa linapwaya, hivyo kuleta mada ambayo inagusa masuala yanayotuzunguka kila siku. Nadhani sijafanikiwa katika hilo. Nadhani ili kuondoa kero hii miongoni mwa wengi, itakuwa ni busara nikisitisha uchambuzi wangu kuhusu mapungufu ya itikadi za CCM, Chadema, na CUF. Nielezeni tu hilo, nami nitatekeleza.
   
 14. Ringo Edmund

  Ringo Edmund JF-Expert Member

  #14
  Jan 25, 2012
  Joined: May 10, 2010
  Messages: 4,895
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 0
  huyu mchambuzi ni mnafiki na ambaye ni wakuogopwa kidogo.
  anasema mnyika yupo tano bora za bunge sijui kwa utafiti upi?wengine ni zito,lisu,mnyaa na makamba,tumwulize chama kilichoongoza nchi miaka 50 na wabunge 250 kwenye tano bora kina 1,chenye 80 kina 3 ndani ya 5 bora,chenye mbunge 1 tz bara kina 1 tano bora.
  ccm chini ya mafisadi 249 ukiongeza epa,meremeta,iptl,ndege ya rais(tumeshindwa hata kuitoa gereji),mikataba mibovu ya madini,uuzaji wa nyumba za serikali,mfumuko wa bei,ulaghai kwa wananchi(tumetengeneza ajira milioni),posho za wabunge,uuzaji wa wanyama hai,upitishaji wa wahamiaji haramu,viongozi wa chama kujimilikisha mali za uma,kushindwa kulipa mishahara watumishi,rada,ubalozi wa tz italia,kashfa za mafuta,reli,atcl nk.
  hapo bado unajiita mwanachama mwaminifu wa ccm eti mpaka hapo ccm itakaposhinda kumwokoa mwananchi ndipo utahamia chadema.
  swali unataka uone nini ndipo uamini ccm sio tu imeshindwa kumwokoa mwananchi bali inauwa wananchi?
  2.unasubiri mpaka ccm ikose mbunge hata mmoja kwenye 5 bora ndipo uamini kuwa kimekwisha?
  3.unataka mpaka tunze kuuza magereza,jwtz,polisi na uhamiaji(kwa sababu ndipo tunaelekea).
  5.unataka kikataliwe miji yote ya tz na kubaki na kura za bibi zetu kule vijijini ndipo uhamie cdm na kuacha propaganda zilizoshindwa?
  6.unataka kura za wapiga kura tz zifikie laki 5 uchaguzi mkuu ndipo uvue hilo shati?
  7.unataka makada wa ccm waanze kupigwa mayai viza badala ya kuzomea ndipo uamini mwisho wa ccm umefika?
  8.unataka kila kura moja ya ubunge inunuliwe na ccm kwa laki3 ndipo ujue kiama kimewadia?
  9.unasubiri makada wangapi wapewe sumu ndipo utundike shati la kijani?
  10.unasubiria katibu mwenezi anyimwe kwenda kukieneza chama kwenye chaguzi ndogo ngapi ili ujue jahazi linaenda pemba ila limefika mtwara?

  ukijibu haya maswali nipm ukanipe kadi ya ccm.
   
 15. A

  Akili Kichwani JF-Expert Member

  #15
  Jan 25, 2012
  Joined: Jan 7, 2010
  Messages: 1,504
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  mchambuzi = mcha mbuzi (source: Mwita 25).................. hahaa, wakati wengine wanamcha Mungu, we jamaa unamcha mbuzi ............. teh teh (joke)..............

  nimependa uchambuzi wako mkuu.................. keep it up, hao wanaokulaumu............. aidha hawajasoma hadi mwisho, au wamesoma hawakukuelewa................... mimi nimekluelewa na uchambuzi wako umetulia sana mkuu..................... nimeukubali...............
   
 16. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #16
  Jan 25, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Huu ni mtazamo wangu tu ambao sio lazima ukubaliwe na wengine kwani hautokani na utafiti bali ufuatiliaji wangu wa vikao vya bunge, kwa kuangalai wabunge wanaojenga hoja kwa kusukumwa na maslahi ya taifa letu. Ni hicho tu, na ni dhahiri kwamba hii listi yangu inaweza kabisa kubadilika, lakini muhimu zaidi, kuwa challenged, kwani kuna uwezekano ikawa subjective zaidi ya kuwa objective, depending kwa wanaonipinga kwa hili wanatoa hoja gani. Nisititize tu kwamba huu ni mtazamo wangu binafsi, usio na utafiti bali utokanao na ufuatiliaji wangu wa karibu wa vikao vya bungeni. Na niliamua tu kuwataja hao ili kufikisha ujumbe, lakini haikuwa sehemu kuu ya mada husika na sidhani kama ina mashiko yoyote ya maana kama ikigeuzwa kuwa mada ya kujitegemea.

  Pia naomba usigeuze mambo, sikusema nitahamia Chadema CCM ikishindwa kuwaokoa maskini. Nilichosema ni kwamba niliwahi kutamka mwaka 2000 kwamba iwapo nitahama CCM kutokana na kushindwa kuwaokoa maskini kwa sababu za arrogance tu ya viongozi na pia uzembe, basi chama changu kingine kitakuwa ni Chadema, ilimradi kirekebishe itikadi yake ili iwe na mwelekeo wa demokrasia ya kijamaa, kwani kwa itikadi yake ya sasa, kama ilivyokuwa ya CCM, haitafanikiwa kumwokoa maskini wa kijijini. Kuna utofauti mkubwa sana wa sentensi hizi mbili. Vinginevyo naendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM kwani nina imani kubwa bado kwamba mabadiliko ndani ya CCM yatakuja tu, kwani tuna viongozi wengi sana ambao wana nia ya dhati ya kuliokoa taifa hili. Viongozi wa aina hii pia wapo Chadema (baadhi, sio viongozi wote wa Chadema). kwa mfano, nina imani kubwa sana na Mnyika, huyu ni kiongozi wa kipekee, na bado ana umri mdogo sana - ni mdogo wangu pengine wa pili lakini anatosha sana katika siasa za nchi yetu, pengine kuliko viongozi wengine karibia wote wa rika lake.

  Tatizo langu kubwa ni itikadi za vyama.
   
 17. Lucas

  Lucas JF-Expert Member

  #17
  Jan 25, 2012
  Joined: Dec 3, 2011
  Messages: 2,452
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  He might be a ccm but SIKILIZA hoja

  Kwanza nakushukuru kaka Mchambuzi, hili ni jamboambalo ni la msingi sana, kuliongelea maana kwa sasa mimi naona ilivyo ni kama vile, pamoja na serikali kuongozwa na ilani ya chama tawala, lakini ukweli ni kuwa sehemu kubwa inaongozwa na priority za aliyeko madarakani, i mena raisi, ina maana regardless ni nani atakuwa raisi, ila akishika nchi vipaumbele vyake ndivyo vitakavyofanya kazi, that is why leo tumefika point nchi hii haieleweki ni ya kijamaa au ya kibepari ama ni mixed economy??!! (kama unajua unisaidie)

  pia habari ya kuongelea ufisadi as hoja ni sawa, lakini huwezi sema kuwa itikadi yako ni kupinga ufisadi, assume leo Tanzania ufisadi umeisha, je ina maana harakati zitaishia hapo? maana kwa system iliyopo bila mabadiliko ya kiitkadi, twaweza ondoa ufisadi lakini tukabaki napengo kubwa sana kati ya walio nacho na wasio nacho!! ambayo mimi nadhani ni hatari kuliko unavyoweza kudhani!!

  point yangu ni kuwa,hapa kuna point nzuri na ya nsingi sana ambayo sote nivyema tuijadili. nitafurahi nikiwaona hapa kwa ID zao watu kama Zitto, Mnyika, Nape, Kigwangala, Mtatiro, Waberoya. Kiranga, Mwita, na wadaue mbalimbali wa siasa tuwasikie pia majibu yao.

  by the way, thanks Mchambuzi for free lecturer, haya ndio masomo ya uraia yanahitajika kwa Watanzania walio wengi. ningependa vyomo vya habari vilichukue hili kwa umuhimu sana, badala ya kutupa habari za fulani kamwambia fulani, fulani kasema hivi, fulani kajisafisha... hizi zaweza kuwa craps tu, now we need to hear things like these ones
   
 18. M

  Molemo JF-Expert Member

  #18
  Jan 25, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mchambuzi ni vigezo gani umetumia kumpa mtu kama Habib Mnyaa wa cuf eti yuko 5 bora ya wabunge? Huyu Mnyaa aliwakashifu sana wabunge wazalendo wa Chadema na Nccr waliokuwa wamesimama kidete kupinga mswada wa katiba ulioletwa bungeni.Tangu siku ile nilimpuuza huyu Mbunge.Kamwe kwake yeye hajui utaifa ni nini anachojua ni maslahi ya Zanzibar.Mnyaa yuko Tayari kutukana yeyote kama alivyofanya anapodhania kitumbua chake kinaguswa.Kwa msimgi huu ni kituko kusema Mnyaa wa Cuf naye ni mbunge bora
   
 19. mgt software

  mgt software JF-Expert Member

  #19
  Jan 25, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 10,728
  Likes Received: 1,636
  Trophy Points: 280
  kaka mchamcha-kuku fupisha kidogo mada ni nyingi nakushauri uombe ukurasa kwenye gazeti lolote ila lisiwe la CCM ndipo tutaweza kusoma tukiwa tumetulia tunakuelewa lakini yaitaji muda kujibu hoja
   
 20. Kimbunga

  Kimbunga Platinum Member

  #20
  Jan 25, 2012
  Joined: Oct 4, 2007
  Messages: 13,012
  Likes Received: 1,817
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mchambuzi hebu naomba unichambulie vyama vya siasa katika dunia ya tatu; ni chama gani cha siasa chenye itikadi inayoeleweka. Tuachane na hivyo vya ulaya na marekani nipe mifano ya vyama hapa Afrika.
   
Loading...