Lakini, kwanini upoteze muda wako kuchangia mawazo kuhusu 'kitu' ambacho wewe unaamini kuwa hakipo?
Swali hili ni zuri sana.
Sipotezi muda, tunaelezana, tunajadiliana, tunaelimishana.
Ngoja niongee kwa mfano, labda utanielewa vizuri zaidi.
Tuchukulie kuna ugonjwa, mbaya sana , unaua. Hauna dawa wala kinga.
Ugonjwa huu unaenezwa kirahisi sana. Tuseme kwa kujamiiana bila kinga.
Halafu, wakaja watu wawili, mmoja tapeli, mwingine mjinga tu.
Yule tapeli anasema anayo dawa ya huo ugonjwa. Anawauzia watu miti tu ambayo si dawa, anapiga pesa ndefu.
Yule mjinga, yeye hapendi tu kuishi kwa hofu, anafuata upepo kusema ugonjwa una dawa, dawa ni ule mtishamba anaouza yule tapeli.
Sasa wewe daktari, umehakikisha kabisa ule mtishamba hautibu ugonjwa.
Na katika maadili yako ya kidaktari, una wajibu wa kuwaelimisha watu, kwamba jamani eeh, hiyo inayoitwa dawa si dawa, ni utapeli tu.
Sasa, katika habari hii, mimi ni kama huyo daktari, Mungu - dawa ya uongo- ni kama huo mtishamba, na hapa kuna matapeli wenye makanisa yao, viongozi wa kisiasa, mashehe etc, wanaouza hiyo dawa ya mtishamba kwa utapeli. Na kuna waumini wanaoamini tu kama bendera kufuata upepo, kwa ujinga.
Sasa, swali uliloniuliza ni sawa na umuulize yule daktari.
Wewe daktari, huamini hii dawa, unasema dawa haipo, sasa kwa nini unapoteza muda wako kupinga dawa ambayo haipo?
Ukweli ni kwamba, daktari huyu asipoelimisha wenzake, ile dawa feki itaua watu. Kutokuwepo kwa dawa maana yake si kwamba hakuna madhara.Watu watafanya ngono zembe, wakijua kuna dawa, tukiumwa tutapata dawa. Watu watapoteza hela zao nyingi kununua dawa isiyoponya kitu.
Hii habari ya dawa ya uongo, ni vizuri imulikwe ili watu wasipoteze maisha, wasipoteze mali zao, wasiishi maisha ya kufuata habari za uongo.
Kutokuwepo kwa Mungu kunaweza kuleta madhara kama watu wataaminishwa Mungu yupo, watafanywa waishi kwa kufuatisha imani ya uongo, watachukuliwa mali zao kwenye imani hiyo ya uongo. Wataishi kwa hofu ya kwenda motoni maisha yao yote, kwa kufuata imani hiyo ya uongo, watashindwa kujiamini wenyewe na kuchukua majukumu ya maisha yao wenyewe, kwa sababu ya imani ya uongo.
Sipingi Mungu ambaye hayupo.
Napinga imani potofu ya kuamini Mungu yupo, ambayo inaweza kuwa na madhara kama imani ya kuwa dawa ya uongo isiyoponya inaponya.