SoC01 Namna Bora ya kukabiliana na Uvuvi Haramu

Stories of Change - 2021 Competition

Mwadilifu Mdhulumiwa

JF-Expert Member
Jul 22, 2021
418
630
Utangulizi

Kwa muda mrefu kumekuwapo na changamoto ya wananchi wengi waishio katika maeneo yanayozunguka bahari, maziwa na mito kufanya shughuli za uvuvi bila kufuata sheria na taratibu zinazowekwa na serikali na hivyo kufanya serikali kukosa mapato huku samaki na viumbe wengine waishio majini wakitoweka kutokana na kuvunwa bila mpangilio.

Uvuvi wa aina hii unavuruga pia mipango ya serikali inayokuwa imewekwa katika kuendeleza ustawi wa samaki na viumbe wengine wa majini kwani wavuvi wa aina hii huenda kuvua samaki hata katika maeneo ambayo yanakuwa yametengwa au kusitishwa shughuli za uvuvi kwa muda ili kuwezesha samaki kukuwa na kuzaliana kwa wingi.

Pamoja na hatua mbalimbali ambazo serikali imekuwa ikichukua ili kupambana na uvuvi haramu, Ikiwemo kukamata wahusika na kutaifisha au kuchoma moto vifaa vyao wanavyotumia kufanya uharamia huo. Hata hivyo tatizo hili limekuwa sugu, hivyo zinahitajika jitihada na mbinu mbadala katika kulishughulikia suala hili.

Katika makala haya nitajadili changamoto zinazosababisha wavuvi kujikuta wakiendelea kufanya uvuvi haramu na njia bora na endelevu za kukabiliana na tatizo hili.

Changamoto zinazochangia uvuvi haramu katika maeneo ya maziwa, bahari na mito ni kama zifuatazo;

  • Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi wengi wa maeneo hayo juu ya umuhimu wa kuzilinda na kuzitunza maliasili zetu. Uchunguzi unaonyesha wananchi wengi waishio maeneo ya kuzunguka bahari, mito na maziwa hawana uelewa mkubwa kuhusu dhana nzima ya maliasili za taifa letu na umuhimu wa kuzitunza kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
  • Gharama kubwa za vibali na leseni za uvuvi. Uchunguzi unaonyesha serikali imeweka gharama kubwa za vibali na leseni za uvuvi kiasi ambacho baadhi ya wananchi wanashindwa kufikia uwezo wa kulipia, huku pia wakiwa hawana shughuli nyingine za kiuchumi wanazoweza kuzifanya na kujiingizia fedha za kuhudumia familia zao.
  • Katika mazingira haya wananchi hulazimika kutumia njia zisizo halali kuvua samaki ili kuendesha maisha.
  • Umasikini wa wananchi wengi wanaoishi maeneo ya kuzunguka bahari, mito na maziwa.
  • Hali hii inawafanya washindwe kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi na kubaki wakitegemea shughuli za uvuvi tu ambazo wamerithi kutoka kwa vizazi vya huko nyuma.
  • Ukosefu wa uaminifu miongoi mwa watendaji wa serikali hususai wanaopewa jukumu la kusimamia suala uvuvi katika bahari mito na maziwa. Baadhi ya watendaji hawa wamekuwa wakijiuhusisha na vitendo vya rushwa kutoka kwa baadhi ya wavuvi na hivyo kuruhusu uvuvi haramu. Hali hii inarudisha nyuma jitihada za serikali katika kukabiliana na janga hili.
  • Kukosekana kwa teknolojia rahisi itakayowezesha uvumbuzi wa miradi mbadala kimkakati itakayozalisha ajira nyingi katika maeneo ya bahari, mito na maziwa. Hali hii itakayosaidia kuwaondoa wavuvi wengi kutoka kutegemea shughuli za uvuvi na kujiajiri au kuajiriwa katika sekta nyingine zitakazowawezesha kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji ya kila siku katika kuzihudumia familia zao.
  • Kukosekana kwa mpango wa ulinzi shirikishi katika maeneo mengi ya bahari mito na maziwa. Hali hii inafanya wananchi wanaoyazunguka maeneo hayo kujiona kanakwamba wao si sehemu ya wadau wa kupambana na uvuvi haramu na kuona kuwa jukumu hilo ni serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama pekee.
  • Mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo yanayozunguka mito, maziwa na bahari. Kukua kwa shughuli nyingi za kiuchumi na viwanda kumechangia kuathiri hali ya hewa katika maeneo mengi yanayozunguka mito, maziwa na bahari. Hali hii imesababisha baadhi ya mazao ya kilimo katika maeneo hayo kushindwa kuhimili mazingira hayo na hivyo kutoa mavuno kidogo yasiyotosheleza mahitaji ya kibinadamu. Pia baadhi ya viumbe na wanyama wa majini wamekuwa wakiharibu mazao ya mashamba ya wananchi wanaojaribu kujishughulisha na kilimo , na kuwalazimisha kuendelea kutegemea zaidi shghuli za uvuvi badala ya kuhamia kwenye kilimo.

    Nini Kifanyike Kupata Suluhisho la Kudumu?
  • Serikali izidishe jitihada za mikakati ya kuwaelimisha wananchi katika maeneo ya mito,maziwa na bahari juu ya umuhimu wa utunzaji wa maliasili zetu ikiwemo samaki na viumbe wa majini.
  • Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo iwekekeze katika kutoa mitaji kwa wananchi na kutengeneneza mazingira ya kuwawezesha wananchi hao kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi badala ya kutegemea uvuvi wa samaki pekee.
  • Serikali kupitia maofisa uvuvi ianzishe bwawadarasa la ufugaji wa samaki kwenye kila kata katika maeneo ya mito,maziwa na bahari ili kutoa elimu ya ufugaji wa samaki kwa kila kaya zinazozunguka maeneo hayo na iunde sheria kali itayoilazimisha kila kaya kuwa na bwawa la kufugia samaki ili kupunguza uvuvi katika maeneo ya umma.
  • Serikali iongeze usimamizi wa karibu na uthibiti mkali dhidi ya maofisa uvuvi wasiokuwa waaminifu. Wale wote wanaopokea rushwa na kuruhusu uvuvi haramu waadhibiwe vikali ili iwe fundisho kwa wengine.
  • Serikali iweke mfumo wezeshi wa utowaji wa vibali vya uvuvi. Ikibidi yafanyike makubaliano kati ya serikali na wavuvi ili wavuvi wa eneo husika wasajiliwe na kuruhusiwa kuvua samaki, kisha serikali ichukuwe sehemu ya samaki hao ili kufidia gharama za vibali vyao.
  • Serikali iweke mpango wa ulinzi shirikishi katika maeneo yote yanayozunguka maito,maziwa na bahari ili kumfanya kila mwananchi kujiona ni mdau muhimu katika ulinzi wa maliasili hizo, na kuwa balozi wa kueneza mapambano dhidi ya uvuvi haramu.
  • Serikali ifanye tafiti zitakazosaidia kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kupunguza athari za tabia nchi na kuwaandaa wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika mazingira yao, ikiwemo kubadili shughuli za kiuchumi au mazao ya kilimo yatakayohimili mabadiliko hayo.
  • Serikali iwekeze katika kuanzisha miradi ya aina nyingine ili kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mito,maziwa na bahari ili kupunguza mashambulizi ya uvuvi haramu na kuwezesha ongezeko na ukuwaji wa samaki utakaoongeza thamani ya samaki wetu katika soko la ndani na nje ya nchi.
  • Serikali izipitie upya sera na sheria za uvuvi ili kuziboresha kukabiliana na wimbi la uvuvi haramu na kuongeza thamani ya samamiki wetu katika kuchangia pato la serikali na kuwezesha uwekezaji wa vitegauchumi mbadala katika maeneo ya mito,maziwa na bahari.

    Hitimisho

    Shughuli za uvuvi ni moja kati ya shughuli muhimu za kiuchumi zinazochangia katika kuongeza pato la taifa letu, hivyo ni wakati sasa kwa serikali kuboresha mazingira na uthibiti wa shughuli hizi. Aidha serikali pia iboreshe mitaala yake ya elimu hasa kwa shule na vyuo vinavyozunguka mito, maziwa na bahari ili wanafunzi wa shule na vyuo hivi wafundishwe madarasani mbinu bora za utunzaji wa maliasili pamoja na njia za kisasa za ufugaji wa samaki na viumbe wengine wa majini. Wito kwa serikali na wadau wote kuboresha sera na sheria zinazotawala sekta ya uvuvi ili kukomesha kabisa uvuvi haramu na kuiwezesha sekta hii kuongeza tija katika uchumi wa wavuvi na taifa zima kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom