Mwisho wa Azra Malama

Mwisho wa Azra Malama

SEHEMU YA 16

“Sikiliza Azra,” Mzungu mwingine aliyekuwa amekaa aitwaye Smith, alizungumza akisimama, akaendelea;

“Sisi kuwa weupe na wewe kuwa mweusi haimaanishi hatuwezi kuwa mtu na kaka zake, sisi ni ndugu na ili kudumisha undugu wetu imetupasa tukupe kazi ya kufanya itakayokupa uhuru.”
“Simwagi damu ya binadamu tena!” Azra alijibu kwa mkazo.

“Ha! Ha! Haaa!” Wale Wazungu walicheka.
“Inashangaza kuona binadamu anakimbia kivuli chake.

Hata hivyo miguu hii haijakufuata hapa kwa kazi ya kumwaga damu ya ndugu zako, tunahitaji kukusaidia kurudi kwenu Swadege ya Rwadege ukatawale na kuwa mfalme, bila shaka umefurahi kusikia taarifa hii!” Smith alimwambia Azra.

Azra alibaki ametoa macho akitafakari maneno yale ya huyo Mzungu aliyekuwa amesimama mbele yake.

Kauli hiyo ilimkumbusha azma yake ya muda mrefu ya kurudi kwao Swadege ya Rwadege, ambako marehemu baba yake mzazi aliwahi kumwambia kwamba ni sehemu nzuri kuliko mahali popote pale duniani.

“Jua la nyumbani ni zawadi nzuri na ya kujivunia ambayo Mungu alitubariki, Swadege ya Rwadege ni mfano wa gadeni ya Hedeni, nyumbani hakuna ugonjwa wala uzee, kuna maisha yenye uhai usio na kikomo kwani hata wafu huishi pamoja nasi,” Azra alikumbuka maneno ya baba yake.

Lakini akiwatazama Wazungu wale alipata swali kwamba nini watu hao walikuwa wanahitaji kupata ndani ya Swadege mpaka watafute mtu akatawale. Azra aliwafahamu Wamarekani, wasingeweza kufanya jambo lisilo na manufaa kwao.

Hata hivyo alipokubali kukaa chini na kusikiliza nini hasa aliitiwa mahali hapo, Smith alimwelewesha lengo lao la kumsaidia kurudi kwao Afrika na kwenda kuwa Mfalme wa Swadege ya Rwadege.

Smith aliongeza kumwambia kwamba walifikia uamzi huo wakiwa wamelenga kuyapata mazao ya uhai yanayopatikana kwenye kisiwa hicho hata kuyasaidia mataifa mbalimbali duniani, kutibu wagonjwa, kuboresha teknolojia, lakini zaidi kutoa msaada kwenye mambo tofautitofauti.

Azra Malama baada ya kusikiliza kwa makini na kutafakari hicho alichokuwa ameambiwa, alikubali kuifanya kazi hiyo lakini kwa sharti moja tu. Jaji Steven Kessy atolewe gerezani pia, jambo ambalo lilitekelezwa mara moja!

“Siamini Azra!” Mzee Kessy alimwambia Azra siku aliyotolewa gerezani.
 
SEHEMU YA 17

“Lakini ninakumbuka uliwahi kuniambia ipo siku utatoka kwa mujibu wa mazungumzo na Mungu wako!” “Ni kweli.

Lakini sikuwahi kuwaza siku niliyokuwa ninaisubiri kwa hamu, siku ya kupata uhuru wangu ingekuwa namna hii.”
“Yametimia.”
“Asante sana.”
“Mshukuru Mungu wako.”
“Hakika sitakusahau Azra maishani mwangu.”

Baada ya maneno hayo Azra alitabasamu, kisha akamwambia; “Jaji Kessy tufurahie kufahamiana.”
Walipomaliza maongezi wawili hao waliagana kwa kukumbatiana, kisha mzee Kessy alielekea Manhattan nyumbani kwake na Azra alielekea Queens, kabla ya kuanza safari ya kwenda Swadege ya Rwadege.

Antananarivo, Madagaska
Saa 6…, mchana

Baridi kali lilikuwa limetanda siku hiyo kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha na jiji zima la Antananarivo lilikuwa limetulia tuli.

Hadi kufikia majira hayo ya mchana bado jua lilikuwa halijachomoza na kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ivata, wasafiri wengi walionekana wamepigilia masweta, majaketi au nguo nzito za baridi lakini pia ndege zilikuwa zikitoka kwenda mataifa mbalimbali na nyingine zikingia.

Yapata dakika kumi toka ndege kubwa ya abiria Boeing 790 Dash 9 Dreamliner, iegeshe uwanjani hapo.

Nje ya uwanja miongoni mwa watu waliyokuwa wanatoka alionekana mwanaume mweusi, mrefu na mwenye misuri mingi mwilini mwake aliyetundika miwani mieusi juu ya paji lake la uso akiburuza begi lililokua likimfuata nyuma yake.

Mwanaume huyo alisonga mbele kuelekea upande wa kushoto kwa watu waliyokuwa wanatoka uwanjani hapo zilipokuwa zimeegeshwa gari za abiria ‘taxi’.

“Karibu…” mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama mbele ya taxi alimkaribisha kwa Lugha ya Malagasy, inayozungumzwa nchini hapo.

“Mh!” Azra Malama aliguna baada ya kusikia lugha hiyo. “Nataka kwenda kwenye hoteli ya karibu,” alisema kwa Lugha ya Kiingereza.

“Mmarekani?” Yule dereva taxi badala ya kujibu alichoelezwa alitamka kwa mshangao.

Azra naye akashangaa na kujiuliza moyoni, “huyu mtu vipi?” Kisha akamuuliza tena;

“Inawezekana au haiwezekani?” Mara hii alimkazia macho huyo dereva.
“Nipe kwanza malipo yangu.”

Yule mwanaume bado alizungumza kwa Lugha ya Malagasy ambayo Azra Malama alikuwa haielewi.
“Kingereza tafadhali,” Azra alimwambia yule dereva
 
SEHEMU YA 18

Lakini alionekana ni mtu ambaye haelewi kwani alizungumza kwa lugha hiyo tena akisisitiza Azra amlipe ujira wake ndiyo ampeleke kule anakotaka.

Ndipo Azra alipoona ni kama mwanaume huyo alikuwa anamchezea kwa lugha ambayo hakuwa anaielewa na zaidi alikuwa akimpotezea muda.

Hasira zikampanda, kwa kutumia mkono wa kulia ambao haukuwa umeshika begi alimkunja kwenye shati kooni mwanaume yule, kisha akamvutia kwake na kumpiga kichwa cha nguvu ‘PUU’, yule mwanaume alidondoka chini kama mzigo.

Baadhi ya madereva taxi waliyokuwa eneo hilo walishangazwa na kitendo kilichokuwa kimetokea. Walijiuliza kulikuwa na sababu gani ya mwanaume huyo mweusi kumpiga dereva mwenzao lakini hakuna aliyepata jibu.

Wakaona hicho ni kitendo cha ukorofi na uonewaji kwa mwenzao,haraka walisogea kujaribu kumsaidia mwenzao lakini na wenyewe waliambulia kichapo. Ikawa vurugu uwanjani hapo, kila aliyemsogelea Azra Malama aliambulia mkong’oto wa maana.

Hata hivyo vurugu zilipozidi, king’ora cha hatari uwanjani hapo kilianza kugonga na punde askari polisi kama mvua walimwagika kwenye eneo hilowakamzunguka Azra Malama na kumnyooshea bunduki, alinyoosha mikono juu, kuonyesha kwamba alitii amri, akakamatwa na kupelekwa kituoni.

Alipofika kwenye Kituo cha Polisi cha Maleki, kwanza paspoti yake ilichukuliwa ma kugundulika kwamba alikuwa ni Mmarekani, kisha akawekwa kwenye chumba maalumu kwa ajili ya mahojiano.

“Kwa nini umefanya fujo uwanjani?” Askari aliyekuwa ameketi mbele yake wakitenganishwa na meza kubwa alimuuliza kwa Kiingereza.

Azra Malama kabla ya kujibu aliinua miguu yake na kuipandisha juu ya meza. Yule askari alitoa macho zaidi kumtazama akionyesha kushangazwa na kitendo kile kilichofanyika.

“Kwa sababu hamna jambo la kunifanya nyie wote ni wapumbavu!” mara hii Azra aalizungumza kwa Kifaransa.
“Oh Kifaransa?”

Yule askari aliuliza akiiinuka na kumsogezea uso karibu zaidi. “Babu yangu aliwahi kuniambia kila azungumzaye Kifaransa anafahamu Kingereza, naomba unijibu kwa nini unafanya fujo kabla sijakuharibu pua yako hii nyeusi!” Yule askari alimkazia uso Azra.

“Ninahisi njaa ninaweza kupata chakula?” Azra, wakati huu aliuliza kwa Kingereza tena kwa dharau.
“Mmarekani…!” Yule askari
 
SEHEMU YA 19

“Mmarekani…!” Yule askari alizungumza kwa hasira. “Unataka nikuonyeshe kwamba hii ni Afrika?” Aliongeza.

“Wote asili yetu ni hapa,” Azra Malama aliendelea kujibu kwa dharau.
Yule askari hakuongeza neno zaidi ya kuiinuka na kutoka ndani ya chumba hicho Azra akimsindikiza kwa macho.

Baada ya dakika mbili alirudi na askari wengine wanne waliofura utadhani chura wenye mimba, walikuwa na miili iliyojazia na mikononi walikuwa wameshika mijeredi.

Baada ya kufika karibu na Azra, walimkamata kwa nguvu kisha wakamfunga pingu na kumuweka sehemu ya wazi.

Mfano wa mchwa wanavyoshambulia mbao ndiyo walivyomrukia Azra na kuanza kumshughulikia kwa kichapo cha maana. Walimpiga kwelikweli kiasi kwamba wakamchania nguo zake.

Damu ikawa inaruka juu na kutapakaa kwenye chumba hicho, Azra alilia kwa maumivu makali, lakini kichapo hakikukoma, aliendelea kusurubishwa mpaka akaishiwa nguvu na kulegea kabisa akawa amening’inia kwenye pingu katikati ya dimbwi la damu. *** Gereza la Koba,

Kaskazini ya Madagaska “Niongeze…” mfungwa mmoja alilalama kwenye foleni ya chakula.
“Pisha mbele.” Aliyekuwa anagawa chakula alimfokea.

Mfungwa yule alipita kuwapisha wenzake wapate mgao wao wa mlo huku akilalamika kupewa chakula kidogo.
Malalamiko yalikuwa ni mengi kwenye gereza hilo la Koba lililopo kaskazini ya Madagaska ambapo walipelekwa watu watukutu na wenye kesi nzito zaidi.

Ambapo mbali na chakula kidogo, hali ya usafi haikuwa inaridhisha hata kidogo.
Maeneo mengi yalikuwa ni machafu, panya walitawala kila kona na kunguni ndiyo usiseme.

Zaidi magonjwa ya mlipuko yalikuwa yanalipuka mara kwa mara utadhani mabomu ya kutegwa huko Iran, katika gereza hilo wafungwa wengi walionekana kukondeana na kubaki mifupa mitupu, kiufupi waliishi bila matumaini!

Hata hivyo, katika jioni hiyo huku wafungwa wengine wakipata chakula, katika chumba kilichotengwa kwa ajili ya huduma ya hospitali gerezani humo, wagonjwa waliendelea kutibiwa na mama Cecilia, ambaye aliambatana na binti yake Jemima, aliyekuwa akimsaidia kila mara alipokwenda gerezani hapo.

“Aah…” mgonjwa alilalamika kuumia na kuushika mkono wa mtu aliyekuwa anamfungua bandeji mwilini mwake. Mgonjwa huyo alikuwa anavidonda vingi mwilini
 
SEHEMU YA 20

Alipoushika mkono wa mtu huyo aliyekuwa anampaka dawa, mgonjwa aliinua uso na macho yake yakakutana ana kwa ana na macho ya msichana kigori, mwenye uzuri wa asili, aliyevaa sketi ya asili iliyotengenezwa kwa ngozi ya simba na kunakishiwa kwa urembo.

Kifuani msichana huyo hakuwa amevaa kitu chochote kile, kwa hiyo matiti yake yaliyosimama mfano wa vipapai vilivyoanza kukomaa yalikuwa yakionekana sawia, shingoni msichana huyo alikuwa amevaa kingozi kingine cha simba kilichonakishiwa kwa shanga za rangi tofautitofauti, kichwani alikuwa amevaa kacha iliyopendezeshwa kwa shanga za rangi mbalimbali kama ilivyokuwa singoni kwake vivyo hivyo na mikononi mwake, msichana huyo alivaa vikacha kama alichovaa kichwani.

“Pole.” msichana huyo alimwambia.
“Asa…nte…aah...” Mgonjwa alijibu kwa shida akikunja uso kutokana na mauamivu aliyokuwa anahisi.

Baada ya kujibu mgonjwa huyo alijitahidi kuinuka kitandani hapo kisha akaketi na kuegemea ukutani. Akashusha pumzi na kuanza kupepesa macho katika chumba kile.

Hakuweza kuamini macho yake kwa hali aliyoiona ndani ya chumba hicho. Wagonjwa walikuwa wamelala hohehahe wakiwa wamejitapikia na harufu kali ilikuwa inasikika katika chumba hicho chote.

Baada ya kutazama huku na huko, yule mgonjwa alirudisha macho kwa Jemima aliyekuwa anampaka dawa kwenye vidonda vyake.

“Nimefikaje hapa?” Aliuliza. Jemina alimtolea macho bila kumjibu.
“Dada naomba unijibu nimefikaje hapa?” Aliongea kwa msisitizo zaidi na sauti ya juu kiasi kwamba wagonjwa wenzake na watu wengine waligeuka kumtazama.
“Sifahamu.” Jemima alijibu.

“Anasemaje huyo?” ilisikika sauti ya mama mmoja aliyekuwa mita chache kutoka wawili hao walipokuwa.

Yule mgonjwa taratibu aligeuza macho kumtazama huyo aliyezungumza, alimuona mwanamke mnene na mfupi, aliyevaa sawa na dada aliyekuwa mbele yake, tofauti kati yao mwanamke yule alikuwa amevaa vikoi alivyojitanda mwili mzima kwa mtindo wa rubega, kwa hiyo hakuwa matiti wazi lakini kichwani, shingoni na mikononi alikuwa amevaa kacha kama binti yake.

Mgonjwa huyo akiwa anaendelea kumtazama huyo mama, alimshuhudia akisogea kitandani pale alipokuwa amelazwa.

“Anauliza amefikaje hapa?” aliuliza tena.
“Ndiyo.”Jemima alimjibu.
 
SEHEMU YA 21

Mama Cecilia aliachia tabasamu hafifu. “Pole baba,” alimwambia mgonjwa akimtazama machoni. “Inaonekana ulipata ajari mbaya, masikini hata hukumbuki umefikaje hapa, lakini tutakufanya upone, tunayo mazao ya uhai!”

Baada ya mama Cecilia kumwambia mgonjwa huyo hivyo huku akimtazama machoni alipeleka mkono ili kumpaka dawa kwenye vidonda vyake.

Yule mgonjwa aliushika mkono wa mama Cecilia huku akimtazama kwa makini. “Mazao ya uhai…” Kauli hiyo iliyojirudia kichwani kwa huyo mgonjwa.

Kisha akamruhusu mama Cecilia kumpaka dawa hizo, jambo la kushangaza baada ya kumpaka tu mwili mzima vidonda vyote vilikauka na kupona. Mama Cecilia na Jemima walitabasamu huku wakitazama namna kijana huyo alivyokuwa akijishangaa.

“Haya ni maajabu…”Yule kijana alisema akiwatazama kwa chati. “Hakuna uwezekano wa vidonda kupona ndani ya sekunde kadhaa!”

“Kwetu Swadege ya Rwadege hili ni jambo la kawaida.” Mama Cecilia alimwambia akitabasamu.
“Hapa ni Swadege?” Yule kijana aliuliza kwa shahuku.

“Hapana, ni jirani na hapa. Umewahi kupasikia?” Mama Cecilia alimuuliza. Yule kijana alishusha pumzi; ‘Huuuu!’ kisha alijibu kwa kichwa akimaanisha aliwahi kupasikia.

“Lakini unavyosikika haina shaka wewe ni Mmarekani, unaitwa nani?” Mama Cecilia aliuliza.

“Azra Malama.” Kijana yule alijibu.
“Ooh! Jina la Malama hata sisi tunalo. Hongera kwa kupona.”

Baada ya kutamka maneno hayo, mama Cecilia na binti yake Jemima, walibeba dawa zao na kusogea kwa wagonjwa wengine kuendelea kutoa huduma, Azra Malama aliwasindikiza kwa macho akitazama namna walivyokuwa wakiponyesha wagonjwa wengine.

Kwa mbali Azra malama aliachia tabasamu hafifu, kuwafahamu wawili hao na siri waliyomwambia kwamba wanatoka Swadege ya Rwadege ilikuwa ni hatua kubwa aliyopiga kwenye azma yake ya kuingia kwenye kisiwa hicho.

Suala la kufanya fujo mpaka kufika katika gereza hilo ilikuwa ni mipango ambayo walipanga akiwa Marekani na kina Smith, kwani kwa mujibu wa ramani hakukuwa na namna ya kuingia Swadege ya Rwadege, bila kupitia katika gereza hilo ambalo lilikuwa ni makazi ya wafungwa watukutu zaidi!
 
SEHEMU YA 22

Mama Cecilia alikuwa ni mjane na mzaliwa kutoka kisiwa kisichokaukiwa maajabu miaka nenda rudi na walikoishi watu wenye busara zaidi duniani cha Swadege ya Rwadege na alikuwa ni mkazi wa kusini mwa kisiwa hicho.

Alikuwa ni mama wa watoto wawili, Jemima na Kalega, sifa zake kubwa zilikuwa ni kwamba, alikuwa mwanamke mwenye huruma na aliyependa kuwasaidia watu wengine.

Mama Cecilia akifahamu uwezo wa ajabu wa mazao yaliyopatikana katika Kisiwa cha Swadege ya Rwadege, aliamua kuyatumia kwa kutengeneza dawa kwa ajili ya kutibu watu hasa wafungwa kwenye Gereza la Koba, lililokuwa jirani na kisiwa chao hicho, lenye sifa ya kuwa na wagonjwa wengi watokanao na magonjwa ya mlipuko.

Mwanzoni alipoanza kazi hii wenzake katika kisiwa cha Swadege walimuita na kumpiga marufuku. Hawakutaka siri ya nguvu zao itoke nje hata watu wengine waipate na kuwa sawa na wao.

Lakini baada ya mama huyu kuwahakikishia kwamba asingeruhusu kitu kama hicho kitokee, ambapo yeye alitengeneza tu dawa za kuwatibia watu ambazo zisingeweza kuwapa nguvu zaidi ya kuwaponyesha, walimruhusu aendelee na azma yake.

Kila Jumatatu ya kila wiki, mama huyo alikuwa anasafiri kwa boti kwa mwendo wa robo saa kwenda kwenye gereza la Koba kutibu wagonjwa,akisaidiana na binti yake Jemima.

Wagonjwa wengi walipona kutokana na huduma yao, lakini hawakuisha kutokana na hali duni ya usafi iliyokuwa katika gereza hilo iliyopelekea magonjwa ya mlipuko kuwatesa wafungwa wengi na kila siku wagonjwa wapya walizaliwa.

Ilikuwa ni jumatatu nyingine, mama Cecilia na binti yake Jemima walikuwa gerezani hapo wakiendelea na huduma yao ya matibabu. Wakiwa wanaendelea kutibu wagonjwa mara Jemima alimuona Azra Malama na vijana wengine watatu wakileta chakula kwenye chumba hicho cha wagonjwa.

“Mama,” Jemima aliita. Mama Cecilia alimtazama binti yake. “Yule Mmarekani umemuona?” Jemina aliuliza, mama Cecilia alitupa macho mbele ya mahali walipokuwa, akamuona Azra Malama, aliyekuwa amebeba sinia kubwa lenye chakula kisha akatabasamu.
“Mmarekani?” mama Cecilia aliita.
 
SEHEMU YA 23

“Mama.” Azra aliitika akiupamba uso wake kwa tabasamu.
“Bila shaka mgao wetu upo pia kwenye hiyo sinia,” Mama Cecilia alitania.

“Chakula ni kwa ajili ya kila mmoja wetu.”
Baada ya kujibu, watu wote, yaani Azra, mama Cecilia na Jemima, kwa sekunde kadhaa walibakia wakitabasamu mpaka midomo yao ilipofunga mfano wa mwanga wa jua unavyopotea majira ya jioni huko magharibi.

Baada ya hapo, wawili hao, mama na mwana waliendelea kumsindikiza kwa macho Azra, aliyeanza kugawa chakula kwa wagonjwa.

Toka siku hiyo Azra alianza kujenga ukaribu na wawili hao, ambapo kila siku ya jumatatu mama Cecilia na Jemima walipokuwa wakifika gerezani hapo Azra alifanya juu chini kuonana na Jemima kwa siri na kuzungumza naye mawili matatu.

Baada ya mazungumzo ya mara kwa mara, siku moja Azra aliamua kuvunja yai kwa kumwambia Jemima kwamba alikuwa na asili ya Swadege ya Rwadege na Marekani, jambo ambalo Jemima hakulitegemea na kuliamini.

Hata hivyo, baada ya Azra kumuonesha Jemima, alama kifuani kwake ya tobo lililochongwa kwa mfano wa ndege aina ya tai, ambayo ndiyo ilikuwa alama ya utambulisho wa Waswadege wote kama ilivyo alama ya chanjo ya ndui kwa ‘Wabongo’, msichana huyo alimuamini.

Machozi yakambubujika hasa aliposikiliza historia ya Azra aliyomsimulia juu ya mababu zake kupelekwa Marekani kama watumwa.

Zaidi, Azra alimsimulia mambo mengi, mengine ya uongo ilimradi kuikamilisha simulizi iliyoleta maana kwa Jemima, kwamba ndiyo ilikuwa sababu ya kumfikisha kwenye gereza hilo.
“Pole sana kaka,” Jemima alimwambia Azra huku akifuta machozi.

“Asante.” Azra alijibu. “Natamani niikanyage ardhi ya nyumbani, nifahamu kuhusu hali ya hewa na uoto wa asili.
“Baba yangu aliwahi kuniambia jua la

nyumbani ni zawadi nzuri ya kujivunia ambayo Mungu alitubariki, kwamba Swadege ni mfano wa gadeni ya Hedeni, nyumbani hakuna ugonjwa wala uzee, kuna maisha yenye uhai usio na kikomo kwani hata wafu huishi pamoja na walio hai.” “Ni kweli kabisa, lakini yakupasa kuwa mvumilivu kidogo.” Jemima alimwambia.
 
Sehemu ya 24

“Uvumilivu si chaguo sahihi, fanya jambo kwa ajili yangu Jemima.” Azra alizungumza huku amekaza macho.

Jemima alibaki kimya akimtazama Azra kwa huruma. Kisha akamwambia;
“Usijali nyumbani umefika.”

“Naiona bado ni safari ndefu mdogo wangu.” Azra alizungumza kwa upole. “Ikiwa mpaka nimalize haya matatizo yaliyonifikisha gerezani ndiyo nianze tena kuhangaikia kufika nyumbani!” aliongeza.

“Usisafiri kimawazo mpaka huko, umeniomba nifanye jambo kwa ajili yako. Kuwa na amani nitafanya kama ulivyoniomba,” Jemima alimwambia Azra.
“Utafanyaje?” Azra alitia hoja.

“Nitazungumza na mama na tutajua tukusaidie vipi.” Jemima alibandika kifuniko kwenye kauli yake aliyoizungumza juu ya kumsaidia Azra.
Ukweli ni kwamba Azra alihisi mpaka mwili wake wote ukisisimka.

Hakuamini kama ni kweli alikuwa amefikia hatua kubwa kiasi hicho kwenye safari yake ya kwenda Swadege, kwani taratibu njia alikuwa ameanza kuiona.

Baada ya kuachana na Jemima usiku wa siku hiyo Azra hakuweza kulala ingawa akiwa kwenye kitanda cha chuma, ndani ya gereza hilo alikuwa amefumba macho.

Kufumba kwake macho ilikuwa ni namna ya kuyasafirisha mawazo yake mbali. Akiwa amefumba macho Azra aliona namna ambavyo alikuwa akiwagawa watu wa Swadege ya Rwadege na kisha kutawala.

Kama haitoshi, aliwaza ambavyo atawaingiza Wamarekani, kisiwani hapo kama sisimizi wanavyovamia uchafu na kuanza kusafirisha mazao yao kwenda mataifa mbalimbali makontena kwa matani kusaidia kukuza teknolojia, kutibu watu na kufanya matumizi mengine.

Akiwa amefumba macho akielea katika dimbwi la mawazo yake hayo Azra alikuwa mpaka akitabasamu.

Kuna muda alisema kwa nguvu; ‘yes’ mpaka wafungwa aliokuwa nao kwenye kichumba hicho cha gereza walishangazwa naye. Lakini Azra hakujali kushangaa kwao! ***

Kwa upande wa Jemima, kama ambavyo alimuahidi Azra kuwa atazungumza na mama yake namna ya kumsaidia, kweli alimweleza mama Cecilia kwamba Azra alikuwa ni ndugu yao ingawa alikuwa amezaliwa Marekani.

Mama Cecilia alishangazwa mno na taarifa hizo. Alimhojia mara mbili binti yake juu ya uhakika wa habari hizo, Jemima alimhakikishia juu ya alichosema kama ambavyo alisimuliwa na Azra.
 
SEHEMU YA 25

“Anafafana na sisi?” Ndilo jambo lingine aliulizwa haraka Jemima.
“Ndiyo nimeiona alama yake kifuani kwa macho yangu.” alijibu.

“Ooh! Basi inawezekana ni kweli.” Mama Cecilia alisema na kumeza mate. “Jina la Malama nimewahi kulisikia pia Swadege.
“Kweli ni ndugu yetu tumsaidie,” Jemima alizungumza kwa upole.
“Kivipi?” Mama yake alimhoji.

“Atoke gerezani.” Jemima alijibu. “Mama,” akaita. “Hivi kweli tunaweza kumuacha ndugu yetu ateseke katika hali kama hiyo iliyopo kwenye gereza la Koba?” Jemima aliuliza. Kabla hajajibiwa aliendelea;

“Itakuwa ni roho mbaya na ubinafsi. Inamaana tutakuwa tunajifikiria sisi wenyewe tu. Kwa sababu hatupati shida haina haja ya kuwasahau wenzetu wenye shida.” Jemima aliweka kituo.

Mama yake hakuzungumza neno baada ya hapo na alionekana amezama kwenye mawazo, kisha baada ya sekunde chache za tafakuri alimwambia Jemima atawaza juu ya hilo.

Hatimaye siku tano zilikatika toka Jemima azungumze na mama yake juu ya kumsaidia Azra na mama Cecilia tayari alikuwa amekwisha pata jibu la nini afanye ili Azra afike nyumbani kwao Swadege ya Rwadege.

Hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kumtorosha. Zoezi ambalo kwao lilikuwa ni rahisi mno maana walijivunia mazao ya uhai.

Siku hii ya jumatatu, ambapo mama Cecilia na Jemima walikuwa katika gereza la Koba, tayari walikuwa wamekwisha jipanga kwa ajili ya kukamilisha zoezi la kumtorosha Azra na tayari walikuwa wamekwisha mtonya juu ya suala hilo.

Azra alijiandaa pia. Ambapo baada ya mama Cecilia na binti yake kumaliza kazi ya kutibu wagonja siku hiyo, alimpa Azra dawa ya ungaunga na kumwambia ajipake mwilini mwake, baada ya kupaka wakaanza kutembea pamoja kutoka ndani ya gereza hilo.

Azra Malama alishangaa namna ambavyo alikuwa anakatiza katikati ya walinzi bila kuguswa wala kuulizwa lolote lile.

Aliendelea kushangaa mpaka walipotoka ndani ya gereza hilo kabisa, wakasonga mbele mpaka ufukweni na kupanda boti. Safari ya kuelekea Swadege ya Rwadege ikaanza na moyoni mwake Azra alikuwa na furaha isiyopimika.
 
SEHEMU YA 26

Swadege
ya Rwadege

Hali ya hewa ilikuwa ni freshi, mandhari yalikuwa ni safi na mimea ilikuwa imestawi vyema.

Kwa upande wa majengo mengi yalikuwa ni ya kifahari, wanyama wafugwao pamoja na watu walionekana wenye afya, umri na furaha tele.

Azra, aliendelea kupepesa macho kufurahia fahari za kisiwa hicho baada ya kukanyaga kwenye ardhi ya Swadege ya Rwadege na hakika kila kitu kilionekana tofauti machoni kwake.
Swadege ilikuwa inastaajabisha.

Barabara za juu zilikuwa ni zaidi ya barabara zilizopo jijini Cairo na zile za Paris, Ufaransa. Maghorofa aliyoyaona ni zaidi ya yale ya Washington, DC au yaliyopo Hong Kong, China.

Mazingira yalikuwa ni ya kupendeza. Swadege ilikuwa ni zaidi ya Jiji la Nice na hata fukwe zake zilikuwa zinavutia zaidi ya fukwe za Zanzbar na Miami, Marekani.

Wakiendelea kupiga hatua kutoka ufukweni, akiongozwa na mama Cecilia na binti yake Jemima, kuna mahali walifika Azra akapiga hatua tatu mbele zaidi ya wenyeji wake na kusimama.

Akanyoosha mikono juu na uso wake akauinua kutazama juu mawinginu. Mama Cecilia na Jemima, walisimama na kumtazama alitaka kufanya nini.

Walimshuhudia kijana huyo akipiga kelele za nguvu; “YAAAAAAAAAAAA!” Kisha alibaki kimya na kuganda hivyohivyo bila kushusha mikono chini.

Mama Cecilia alipiga hatua mpaka mahali alipokuwa Azra na kusimama mbele yake.
“Karibu nyumbani,” alimwambia akitabasamu.

“Unajisikiaje?” Azra alishusha mikono na kukaa sawa, akamtazama mama huyo huku tabasamu hafifu likichanua usoni kwake, kisha akamjibu;

“Najiona mtu mwenye furaha zaidi kuliko wakati wowote ule maishani mwangu.” Alimeza mate na kuendelea; “ Ilikuwa ni nusu kifo nusu uhai, lakini hatimaye nimetimiza ndoto zangu za muda mrefu.”

“Unamaanisha nini?” Mama Cecilia alimuuliza. Wakati huo Jemima pia alikuwa amesogea mpaka mahali hapo walipokuwa wawili hao.

“Kuhusu nini?” Azra alihoji kana kwamba hakulielewa swali.
“Unavyosema nusu kifo nusu uhai!” Mama Cecilia alifafanua.

“Namaanisha nimepitia mengi mpaka leo ninakanyaga ardhi hii,” Azra alijibu. “Ninaonekanaje, siye mtu mwenye furaha?” Alihoji akitupa mikono na kupitisha macho mwilini mwake kana kwamba anajikagua.

ITAENDELEA…
 
SEHEMU YA 27

“Namaanisha nimepitia mengi mpaka leo ninakanyaga ardhi hii,” Azra alijibu. “Ninaonekanaje, siye mtu mwenye furaha?”

Alihoji akitupa mikono na kupitisha macho mwilini mwake kana kwamba anajikagua.
“Ha! Ha! Haaa!” Mama Cecilia alicheka.

“Furaha unaitafuta mwilini?” Alimuuliza. Lakini kabla hajajibu, Jemima alidakia;
“Hakika umefanana mpaka na sisi, ninaiona furaha isiyopimika kwenye mboni za macho yako.”

Mazungumzo yalikuwa yamenoga. Huyu alitupa hili na yule akatupa lile, lakini wakiendelea kucheza na maneno mara walishitukia kundi la vijana waliyokuwa kwenye farasi likitinga mahali hapo.

Vijana hao weusi walikuwa ni wenye miili iliyoshiba, walivaa nguo za asili zilizoundwa kwa ngozi za simba kama ilivyokuwa kwa Jemima pamoja na kacha zingine za kiutamaduni na viatu vilivyoundwa kwa maganda ya miti.

Mikononi walikuwa wameshika mapanga na mikuki, podo zenye mishale zilipamba kona ya viuno vyao, walishuka kwenye farasi na kusogea zaidi pale waliposimama watu wale watatu.

Kundi hilo la vijana walikuwa ni walinzi wa mpaka na waliongozana kwa zamu, wakati huo zamu ilikuwa ni ya Kanyara Shebo.

“Salamu kwako mama uliyejaliwa hekima na busara, afya iendelee kustawi kwa binti yako mpole anayependezesha uso wa Swadege ya Rwadege,” Shebo alisalimia. Mama Cecilia na Jemima waliinamisha vichwa chini wakimaanisha walijibu salamu yake.

“Ni nani huyu?” Shebo alihoji.
“Naitwa Azra Malama,” Azra alijibu mwenyewe.

Hakutaka kujibiwa na mtu kisha alisogea mbele alipokuwa amesimama Shebo, wakawa wanatazamana usoni utadhani majogoo yaliyotaka kupigana. Vijana wale walinzi wa mpaka waliyokuwa nyuma ya Shebo walivuta mishale yao kumuelekezea Azra.

Mama Cecilia aliwafahamu ndugu zake. Hawakuwa watu wa mchezo linapokuja suala la mtu kuvamia kwenye ardhi yao, waliua mara moja. Haraka alipiga hatua mbele mpaka walipokuwa Shebo na Azra kisha akamwambia Shebo, kijana huyo mbele yao hakuwa adui, bali ndugu yao.

Shebo, alihoji alikuwa ndugu yao kivipi na kundi zima lilisimuliwa na mama Cecilia historia ya babu zake Azra, waliyochukuliwa kisiwani hapo kama watumwa na kupelekwa huko Marekani alikozaliwa yeye.

“Kwa hiyo umefuata nini hapa?” Shebo alimuuliza Azra.
 
SEHEMU YA 28

“Baada ya babu zetu kuondoshwa na volcano kwenye ardhi yao, nyie mlipohamia hapa mliulizwa na nani mmefuata nini?”

Azra alihoji pia.
“Uhakika ni upi kama wewe ni mmoja wetu?” Shebo alizidi kuhoji. Azra alivua tisheti aliyokuwa amevaa na wote wakaona alama kifuani kwake.

“Bado si jambo la kutushawishi moja kwa moja. Wamarekani si watu wazuri, wanatumia kila namna kutufikia, ni lazima akaonane na wazae,” Shebo alimwambia mama Cecilia.

Kisha, yeye na kundi lake walimchukua Azra Malama, wakampandisha kwenye farasi na kumpeleka moja kwa moja mpaka kwenye kilima cha Bunja, eneo walipokusanyika wazee wote wa kisiwa hicho na kutengeneza makazi.

Wazee hawa wote walikuwa na busara, maono, wenye umri mkubwa na siku zote walionekana kama vijana, ngozi zao ziling’aa utafikiri ngozi ya mtoto mchanga.

Walikuwa na uwezo wa kutumia akili zao vilivyo, walikuwa na uwezo wa kupunguza na kuongeza kasi ya mapigo ya mioyo yao na pia walikuwa na uwezo wa kukaa wiki kadhaa bila kupata usingizi. Kiufupi walikuwa ni wazee wa ajabu.

Uwezo wao wote huo mbali na mazao ya uhai ulitokana na kupendelea kula mboga za majani na walikuwa na mlo wao maalumu waliouita ‘sasa’, hapa kisamvu kilichanganywa na karanga, lakini pia walikuwa imara kutokana na shughuli walizokuwa wanafanya pamoja na mazoezi, wazee hawa ndiyo walikuwa injini ya Swadege ya Rwadege.

Baada ya kufika kwenye eneo hilo Azra alishangazwa na uwepo wa maua ya jua mengi ambayo yalikuwa yanapeperushwa na upepo mwanana kulia na kushoto, uliovuma kutoka kwenye miti mbalimbali iliyozunguka eneo zima la Milima wa Bunja.

Mbali na maua hayo yenye kupendeza machoni kutokana na rangi yake, Azra aliweza kuona pia mashamba makubwa yenye mazao ya rangi kama ya machungwa, katika mashamba hayo kulikuwa na ulinzi usiyo wa kawaida.

Azra aliendelea kukaa kimya akiyasoma mazingira hayo yote na hatimaye walifika kwenye makazi waliyokuwa wanaishi wazee hao.

ITAENDELEA…
 
SEHEMU YA 29

Yalikuwa ni makazi ya tofauti pia. Kutokana na utajiri pamoja na mazao ya uhai ambayo walikuwa nayo watu wa Swadege, Azra alitegemea angekuta mahali hapo nyumba kubwa za kushitua, lakini jambo la ajabu alikuta nyumba za kawaida, lakini zilikuwa zimejengwa kwa ubunifu wa hali ya juu huku zikinakishiwa kwa sanaa na ustadi mkubwa.

Nje katika makazi hayo, walimkuta mzee mmoja aliyevaa kofia ya mkeka, mkakamavu na mwenye uso uliojaa uhai zaidi. Mzee huyo alipowaona wageni hao aliachana na kile alichokuwa anakifanya, kisha akasimama pamoja nao uwanjani hapo na kuwakaribisha.

Baada ya kuwakaribisha pamoja na salamu, Shebo alimueleza mzee huyo kila kitu kuhusu Azra kama ambavyo mama Cecilia aliwasimulia, hakuficha wasiwasi wao jambo ambalo ndiyo lilisababisha mpaka wampeleke Azra mahali hapo kwa wazee.

Mzee huyo alivua kofia yake ya mkeka aliyokuwa amevaa kichwani akaacha upala wake nje, kisha akamsogelea zaidi Azra.

Jambo la kwanza baada ya kumsogelea alimuuliza kuhusu utambulisho wake.
Azra alivua shati na mzee huyo akaona alama yake kifuani.

Alipoiona alama hiyo mzee huyo aliwatazama wenzake kwa chati kisha akamwambia Shebo na kundi lake waondoke wamuache kijana huyo ili aweze kumdadisi zaidi. Kundi la Shebo lilifuata kama ambavyo lilielekezwa. ***

Taarifa za Azra Malama, Mmarekani aliyedai ni Mswadege kuingia kisiwani hapo na kuanza kuishi kwenye milima ya Bunja zilisambaa utadhani ugonjwa wa surua unapoingia kwenye kijiji fulani.
Watu walikaa makundimakundi kumjadili.

Wapo waliyoona ni sawa juu ya uamuzi alioufanya. Kwamba kama alikuwa na asili ya Swadege na alihitaji kurudi kwenye ardhi ya babu zake hakukuwa na namna ya kumkataza kuishi, kwani alikuwa nyumbani.

Lakini wapo wengine ambao hawakuwa wanaamini kwamba kijana huyo kweli alikuwa na asili ya Swadege ingawa alikuwa na alama kama yao. Walichofikiri ni kwamba alipandikizwa na Wamarekani, kwa ajili ya mpango wao wa muda mrefu wa kuchukua mazao ya uhai.
 
SEHEMU YA 30

Hata hivyo kwa kuwa watu wa Swadege waligawanyika kimtazamo, ilikuwa ni nafuu kwa Azra Malama, kwani uamuzi wa moja kwa moja juu yake kwamba aondoke ulishindwa kufikiwa, safari yake mpya ya maisha ndani ya Swadege ya Rwadege ikawa imeanzia hapo, akifurahia kuishi na wazee kwenye milima ya Bunja.

*** Akiwa kwenye milima hiyo, Azra hakupenda kupoteza muda. Alianza kuyasoma mazingira na namna ambavyo watu wa Swadege ya Rwadege walikuwa wanaishi.

Mambo mengi yalikuwa ni tofauti na alivyozoea lakini pia ya kumshangaza na kumuacha mdomo wazi. Kuanzia kwenye chakula, ingawa wazee hao aliokuwa anaishi nao walikuwa ni matajiri na wenye kila kitu wanachohitaji, ulaji wao ulikuwa ni wa kawaida.

Walijali sana kila kinachopita mdomoni kwao. Hawakula ilimradi kula na vyakula vyao vikuu vilikuwa vya asili, yaani mihogo, viazi, ndizi na magimbi. Mboga zao kuu zilikuwa ni za majani, nyama angalau walizokula kwa uchache zilikuwa za wanyama pori tu pamoja na matunda.

Chumvi waliyotumia kwenye mboga ilikuwa ni ya mawe, kwenye chai waliweka asali na si sukari. Maji waliyokunywa walihakikisha ni maji safi na salama tena kutoka kisimani.

“Kwa nini mnazingatia sana suala la kula?” Azra alimuuliza siku moja mzee Makimbi, ambaye alimpokea. Ilikuwa ni sehemu ya udadisi wake.

“Unavyokula ndivyo jinsi ulivyo.” mzee Makimbi alimjibu. “Sisi tuna afya njema, sura zetu zinavutia na hazina mikunjo ya uzee.

Ngozi zetu unaziona zilivyo ni kama za mtoto mdogo.
“Kuzingatia chakula ndiyo siri pekee ambayo inatufanya sisi tuishi umri mrefu zaidi duniani.”

“Inavutia kusikia hivyo.” Azra alimwambia mzee Makimbi. “Lakini lingine lipi la ziada kutoka kwenye chakula mnachokula, unauhakika ni kwa sababu ya afya tu?”
“Sababu kuu ni afya, lakini chakula cha asili kinasaidia pia kwenye kuimarisha kufikiri na utendaji wa jumla wa akili.”

Azra aliendelea kujifunza mambo mbalimbali ingawa mwanzoni maisha ya eneo hilo yalionekana magumu sana kwake.

Kila kitu alichojifunza alikuwa akiandika kwenye kitabu chake cha kumbukumbu alichokuwa nacho kwa siri.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom