Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,021
- 2,478
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Pombe Joseph Magufuli
I. UTANGULIZI
- Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020 umekwisha, ukiwa unasindikizwa na ukosoaji mkali kutoka kwa vyama vikuu vya upinzani vya Chadema, ACT Wazalendo na CUF. CCM imepata wabunge 261 kati ya wabunge 264 wa majimbo, sawa na 98.86% Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ametangazwa na NEC kama mshindi halali, na tayari ameunda serikali itakayotafsiri na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
- Sera zote zilizo katika ilani za vyama vyote vya siasa, zinaweza kugawanywa, bila kubaki, katika makundi matano. Makundi hayo ni: Afya, Elimu, Ikolojia, Ofisi za uongozi, na Uchumi. Nakumbuka maeneo haya matano kwa msaada wa vokali tano za Kiswahili, yaani “A, E, I, O, U.”
- Kwa kuzingatia haya, katika aya zifuatazo nafupisha ahadi zote 90 nilizoziona kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ili kuweka rejea murua itakayotusaidia kufanya ufuatiliaji na tathmini ya kazi za serikali kuanzia 01 Januari 2021.
- Kuna ahadi kuhusu ujenzi na ukarabati wa vituo vya huduma za afya, ushirikishwaji wa sekta binafsi katika huduma za afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, upatikanaji wa watumishi na mabingwa wa kada ya afya, na sera ya mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
- Pia, kuna ahadi kuhusu mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, mapambano dhidi ya magonjwa yanayotokana na virusi kama vile VVU, upatikanaji wa mlo kamili na bora, na sera ya uduma za ustawi wa wazee.
- Aidha, kuna ahadi kuhusu huduma za ustawi wa watoto na familia, huduma za watu wenye ulemavu, kusimamia upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, kusimamia mipango miji na mipango vijiji, sera ya ujenzi wa nyumba na makazi bora, sera ya bima ya afya kwa wote, na sera ya afya ya mama na mtoto. Lakini, katika ilani hii, haikutajwa ahadi ya “bima ya afya kwa watu wote.” Hii ni ahadi ya jukwaani.
- Kuna ahadi kuhusu elimu ya msingi, elimu ya sekondari , elimu ya ufundi stadi, na sera ya elimu ya Juu.
- Pia kuna sera za kuanzisha makampuni ya katika sekta mbalimbali ili kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu; kujenga mfumo wa Taifa wa ubunifu (national innovation system); na sera ya kuendeleza vituo atamizi kwa ajili ya kukuza na kuendeleza ubunifu wa kisayansi na kitejinolojia.
- Kadhalika, kuna ahadi kuhusu kuhamasisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika uzalishaji, usambazaji, na utawala kwa kutumia tekinolojia ya kidijitali; kuanzisha vituo vya umahiri wa sayansi na teknolojia (centres of excellence) katika taasisi za elimu ya juu; na sera ya kuimarisha mafunzo ya walimu wa sayansi, teknolojia na ufundi katika ngazi za shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vikuu.
- Kuna ahadi juu ya kuhimiza watu kuepuka kadiri inavyowezekana kutumia nishati zinazozalisha hewa ya ukaa ambayo ni chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabia nchi; kuwekeza katika miradi ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi (climate adaptation strategies); na kuwekeza katika miradi ya kupunguza ukubwa wa vyanzo vya mabadiliko ya tabia nchi (climate mitigation strategies).
- Aidha kuna ahadi juu ya kuhifadhi uoto wa asili ulioko juu ya nchi, kuhifadhi uoto wa asili ulioko majini, kuhifadhi wanyama wa porini, kuhifadhi wanyama wa majini, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, na kunzisha mfuko maalum kwa ajili ya utafiti, usimamizi na tathmini juu ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.
- Kadhalika kuna ahadi juu ya kuzuia uchafuzi wa mazingira unaofanyika kupitia uzalishaji wa takangumu; uzuia uchafuzi wa mazingira unaofanyika kupitia uzalishaji wa takamaji; na uzuia uchafuzi wa mazingira unaofanyika kupitia uzalishaji wa takahewa.
- Kuna ahadi juu ya kuheshimu haki ya kujitawala katika ngazi za chini za serikali kwa kugatua madaraka, kusimamia maadili katika utumishi wa umma, kufanya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kuheshimu misingio ya demokrasia na haki za binadamu, kuheshimu katiba na kuzingatia utawala wa matakwa ya sheria, na sera ya kuhuisha usawa wa jinsia katika sekta ya umma na sekta binafsi.
- Pia, kuna ahadi juu ya kuhami uhuru wa vyombo vya habari, kuheshimu uhuru wa raia kujieleza na kuwasiliana, kuhesimu uhuru wa asasi za kiraia, kulinda uhuru wa kuabudu, kulinda haki za wafanyakazi na uhuru wa vyama vya wafanyakazi, na sera ya kukabiliana na majanga ya asili kwa kuzingatia kanuni ya utawala auni (principle of subsidiarity).
- Kadhalika, kuna ahadi juu ya kupambana na dawa za kulevya, menejimenti ya mahusiano ya kisiasa na kiuchumi katika ngazi ya kimataifa, menejimenti ya kidemokrasia ya vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi, na sera ya kuzuia utekaji, utesaji na uteketezaji wa uhai wa raia wasio na hatia.
- Kuna ahadi juu ya ushirikishaji wa sekta binafsi katika uwekezaji, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, na kuzalisha ajira kwa vijana, kusimamia vyama vya ushirika, kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara na mfumo wa kodi, vituo atamizi kwa ajili ya kuzalisha wajasiriamali, na kubuni sera za kifedha zinazoruhusu mzunguko wa fedha wenye kasi kubwa ya kuhakikisha kwamba fedha inapita katika mfuko wa kila raia anayejishughulisha.
- Pia, kuna ahadi juu ya barabara za chini, madaraja, makalvati, mizani ya kupima magari, vivuko, bandari, reli, viwanja vya ndege, na mawasiliano ya simu.
- Aidha, kuna ahadi juu ya ujenzi wa barabara za juu (Flyovers) zifuatayo ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, kwenye makutano ya barabara katika maeneo yafuatayo: Chang’ombe, Uhasibu, Kamata, Morocco, Mwenge, Magomeni, Tabata, Fire, Makutano ya Ally Hassan Mwinyi na United Nation, na Makutano ya Ally Hassan Mwinyi na Kinondoni. (Ilani ya CCM 2020-2025, ib. 55(e)(i)).
- Kadhalika, kuna ahadi juu ya nishati ya umeme, nishati ya mafuta, nishati ya gesi asilia, madini, utalii, maliasili, matumizi bora ya ardhi, na kuendesha sekta ya utamaduni, sanaa na michezo kibiashara.
- Muhtasari: Ahadi zote zilizo katika ilani ya CCM, zinaweza kugawanywa, bila kubaki, katika makundi matano. yaani: Afya, Elimu, Ikolojia, Ofisi za uongozi, na Uchumi (A-E-I-O-U). Nimefupisha Ilani yenye kurasa 303 za maneno 103,640 katika kurasa 3 za maneno 1,507; maneno ambayo ni sawa na 1.5% ya maneno ya awali.
- Hitimisho: Napenda kuhitimisha kwa kusema kwamba muhtasari huu wa ahadi katika sekta za afya, elimu, ikolojia, ofisi za utawala na uchumi, utaweza kutoa fursa kwa wadau wa maendeleo kufuatilia yanayojiri katika korido za serikali kuu na serikali za mitaa kuanzia Januari mosi 2021.
- Mapendekezo: Ahadi ni deni na muungwana ni vitendo. Kwa hiyo, naikumbusha serikali mpya kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaid na kazi zaidi, ili siku moja Tanzania Mpya izaliwe ikiwa inafanana na Mji wa "California," kama tulivyoahidiwa wakati wa kampeni. Lakini, kusudi ndoto hiyo itimie, nashauri kwamba yafanyike marekebisho kadhaa kwa ajili ya kuboresha kasi na ufanisi wa muundo wa utawala wa nchi (pichani chini). Kwa mfano, naona kwamba, Wizara ya TAMISEMI ni dude kubwa linalopaswa kuwa na Manaibu Waziri watatu wenye majukumu tofauti yanayokamilishana. Hao ni: Naibu Waziri wa TAMISEMI CITIES, Naibu Waziri wa TAMISEMI MUNICIPALITIES na Naibu Waziri wa TAMISEMI RURAL kwa ajili ya maeneo baki. Kwa sasa, sekta za " Halmashauri, Miji na Manispaa" zinayumba sana.
Chanzo:Henry A. Mollel (2010), Participation for local development: The reality of decentralization in Tanzania (Leiden: African Studies Centre, African Studies Collection, vol. 29), uk. 18. (NB: Natambua kwamba tangu 2015 majukumu ya PMO-RALG yako chini ya PO-RALG)
Kwa leo sina la ziada.
Nawatakia Mwaka Mpya wa 2021.
Karibuni Sumbawanga!
Kwetu kuchele!